Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 17 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 17

Akapokea kabla haijakatika na kuongeza idadi kwenye missed calls alizoacha huyo Ezra kwenye simu yake. “Kwema!? Naona simu zangu hazipokelewi tena! Na wala jumbe hazijibiwi! Halafu dukani nimeambiwa umetoka tokea mchana, hujarudi na huna sherehe popote! Upo salama!? Nimeingiwa na wasiwasi, maana si kawaida yako!” “Samahani sana Ezra. Pole. Simu ilikuwa kwenye pochi muda wote, na haikuwa na sauti.” Jelini ni mfanyabiashara. Simu kwake ni kitu cha muhimu sana. Hawezi akaishi bila simu. Hilo likashindwa kuingia akilini.

“Tokea mchana nakutafuta Jelini! Hujapata hata wazo lakunitumia ujumbe hata kujua kinachoendelea na wakati tulikubaliana tunakula pamoja!? Kwamba hukunikumbuka kabisa na kuhisi pengine nipo nakusubiria?!” Jelini akajisikia kuumia. Ni Ezra. Mwanaume anayemjali kwa kumfikiria masaa 24.

 “Samahani Ezra. Nilipata mgonjwa, ndio nikaondoka kuja kumuona. Umekula?” Dharula aliyokuwa na wasiwasi Ezra asije mpa kama Colins alivyokuwa akimfanyia yeye, akimsubirisha bila kikomo, siku hiyo, kwa mara ya kwanza, na yeye akampa Ezra. Kumbe hutokea!

Wakamsikia akimuuliza. “Sijala Jelini! Njaa inaniuma, ndio nilikuwa nikikujaribisha kwa mara ya mwisho, nirudi tu nyumbani, nikalale.” “Hapana. Usilale na njaa. Nakuja sasahivi na samahani sana.” “Ni nani mgonjwa?” Jelini akasita. “Jelini?” “Acha niage hapa. Nakuja. Tutazungumza vizuri wakati tukila. Hata mimi nina njaa. Sijala tokea asubuhi.” “Jelini, ni nani mgonjwa?” Chumba kizima kimya, Colins akimtizama tu pale kitandani alipokuwa amejilaza.

Kimya. “Ni nani huyo ambaye unashindwa kumtaja!?” “Ni Colins, anaumwa.” “Oooh! Sasa naelewa. Usiku mwema Jelini. Kuwa tu na amani.” “Tafadhali usikasirike Ezra. Nakuja tuzungumze. Sijakusahau ila nilitingwa.” Akatoka hapo chumbani. Ila wakamsikia akimbembeleza kwa sauti iliyojaa hofu.

“Naomba usiende kulala ukiwa na uchungu. Na kumbuka uliniahidi hutaniacha nilale na uchungu.” “Mimi sijui kama unauchungu Jelini! Upo na Colins, uchungu unatoka wapi?” “Usiponiona leo. Ukaamua kwenda kwako bila ya kuzungumza na mimi, nitaumia sana.” Ezra akapoa.

“Unanisubiri?” Akamuuliza kwa kumbembeleza. “Kama unataka nikusubirie, nitakusubiri.” “Nataka kukuona Ezra.” “Basi nakusubiri.” Jelini akakata na kurudi ndani. Akakuta kama alivyowaacha. Kimya, Colins akimtizama.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaanza kulia. “Natamani mngeniambia siku 8 kabla.” Akaendelea kulia kwa uchungu sana. “Muda wote kabla ya hili juma, nilikuwa nikimsubiria Colins, nikidhania atarudi na kunipa sababu yeyote ile kama kawaida yake, ili turudiane. Nilikataa kila mtu kwa muda wote huo, nikimsubiria Colins.”

“Ni siku chache tu, ndipo nimemkubalia Ezra, nikiwa nimekata tamaa nikijua Colins wangu hatarudi tena! Mmenikatili! Mmenikatili vibaya sana. Bora mngeniambia kama Colins wangu yupo na ananitafuta. Nisingejali usaliti wa kwenda kuishi na Love, nilikuwa nipo tayari kusamehe, tuanze tena kuahidiana ahadi zetu ambazo hazijawahi tokea.”

“Ni jana tu, nimetoka kumuahidi Ezra nitakuwa naye mpaka kifo. Ezra ni mtu mzuri sana na ametokea kunipenda kwa dhati. Na ni mcha Mungu. Mwaminifu na ameningojea kwa muda wote niliokuwa nikimsubiria Colins. Na Colins ananijua. Nikishamkubali mtu, siwezi kuwa msaliti. Siwezi kumuumiza Ezra. Nitasimamia maneno yangu kwake, kwa sababu nyinyi mlimtoa Colins kwenye maisha yangu.” Hasira zikapanda.

“Na wakati nikiahidi hapa nitakuwa hapa na Colins, msitafute mtu mwingine wa kumuuguza, nilimsahau kabisa Ezra ambaye yeye ananijali sana. Ananifikiria masaa 24 bila kuchoka, akitafuta vitu vya kunifurahisha. Mimi ni dharula yake ya kwanza na amenipokea kama nilivyo. Madhaifu yote mliyokuja kunitukania nyumbani kwetu mbele ya ndugu zangu, na mtoto wangu, bila kujali hisia zangu, Ezra amenipokea nayo akinipa moyo ni maisha ya nyuma. Leo siwezi kumgeuka.”

“Kabla sijaendelea na chochote hapa, nahitaji muda wa kwenda kuzungumza na Ezra juu ya Colins. Kile ataridhia, nitafanya. Japokuwa nampenda sana Colins, lakini sitamuumiza Ezra, kama Colins alivyokuwa akiniumiza mimi na nyinyi mkichangia. Sitatoa ahadi hewa ambazo atakuwa akizisubiria tu, kama Colins alivyokuwa akinifanyia mimi. Sitamsababishia Ezra maumivu kama nyinyi wote mliyo nisababishia.”

Mmenikatili sana. Na nyinyi wote, mpaka Connie, sio watu wazuri. Mmefanya juhudi za makusudi kunitoa kwenye maisha ya Colins mpaka mmefanikiwa. Mungu anawaona.”

“Jelini umekasirika, naomba…” “Hapana Connie. Kukasirika ni jambo dogo sana. Nina maumivu yakupita maelezo na wewe ukiwa unajua moyo wangu na wa Colins! Umechangia bila kutufikiria.” “Nilikwambia mambo yalivyozidi kuwa na msuguano hapa, niliamua kujitenga kabisa. Nikawa siji kabisa hapa nyumbani.” “Ili kunusuru nafsi yako na si kutupigania mimi na Colins. Si ndiyo?” Kimya.

“Achilia mbali hilo. Wewe ulijua lini kama Colins wangu ni mgonjwa?” Kimya. “Kwa nini mumchome sindano za usingizi, asinitafute?  Au kwa nini hamkunitafuta tokea mwanzo mkabaki mkimfunga kamba na kumpa madawa ya usingizi ilimradi tu asinifikie mimi!? Kwa nini Connie, kama si chuki mliyonayo juu yangu?” Jelini akaanza kulia tena kwa uchungu sana.

“Sio chuki mama. Tafadhali tusamehe. Mimi nilijaribu kuja kwako mara kadhaa, ila nilishindwa na dhamira.” “Kweli baba yangu wewe uliweza kuja kwetu. Mbele ya ndugu zangu, na mtoto wangu aliyekuwa akimuheshimu Colins kwa kiasi kile, ututusi kwa muda wote ule, kweli leo eti Colins ni mgonjwa, ananitaka mimi. Eti mshindwe kuja kuniambia jambo zito kama hilo, mnamchoma madawa ya usingizi ilimradi tu asinifikie mimi, huku mlitoa baraka zenu aende kuishi na Love!” Jelini akaendelea kwa machozi.

“Kweli jamani?! Nina uhakika kama angekuwa akimtaka Love, nina uhakika kwa asilimia zote, msingefikiria mara mbili, mngempeleka. Ila kwa kuwa ni mimi ambaye mnaniona mbaya, mkaona shida kunisogeza karibu ya kijana wenu. Lakini wazazi wangu, narudia tena kama nilivyowaambia siku ile mlipokuja kunitusi mimi na mama yangu. Inawezekana mimi sijasoma, lakini nina mapenzi ya dhati na Colins.” Akaendelea.

“Inawezekana mimi sijakulia kanisani kama Connie na Love, nimekua nikishinda baa, lakini sijawahi kumsaliti Colins hata mara moja. Sijui uchawi wala mlango wa mganga wa kienyeji ulivyo. Sijaishi ulaya, lakini mimi nilimpenda Colins kwa moyo wangu wote bila maigizo ya kizungu. Nilisema na narudia tena, ningempenda Colins, na kumuheshimu mpaka kifo changu. Lakini kwa kuwa mimi sio Love, sijasoma, mmenitoa kwenye maisha ya Colins.”

“Naondoka na kuwaacha na amani yenu. Nikikubaliana na Ezra, na kama bado mtanikaribisha kwenu, nitarudi kumuona Colins. Vinginevyo endeleeni tu na maisha yenu. Mkitaka kumtafutia mtu baki wa kumuuguza, hiyo ni juu yenu. Sitaingilia tena, maana nyinyi kwa makusudi, mmenipokonya hiyo nafasi.” Akaokota pochi yake, na kukusanya vitu vyake vyote, akatoka akijifuta machozi.

Kimeumana.

Colins akavuta pumzi kwa nguvu, akajivuta mpaka akakaa. Alikuwa kimya akimsikiliza Jelini, ila hakuwa ameelewa mengi. “Naombeni mkae, tuanze taratibu. Na msiniambie nilale mpaka nipate nguvu, wakati yupo Ezra kwenye maisha ya Jelini, na si Colins.” Akaanza taratibu tu.

“Mimi nishalala na kula, sina ninapokwenda leo wala kesho. Ninao muda wakutosha tu kurudi kulala. Naanza na wewe Connie. Bila kunificha, leo ni tarehe ngapi, mwezi na mwaka?” Akamtajia. “Ni kwamba sijasikia na kuelewa, au!? Umesema leo ni tarehe ngapi!?” Connie akarudia. Colins akanyamaza kama anayejaribu kufikiria. Wakamuona anatingisha kichwa kukataa. Akamwangalia tena dada yake. “Umesema leo ni tarehe ngapi?” Akarudia tena ila safari hii na machozi zaidi.

Haiwezekani! Kwani nimeugua kwa muda gani?!” Akazidi kushangaa. Kimya. Akamtizama mama yake kama anayetaka yeye ndio ajibu. “Kwa muda mrefu.” “Mama please!” Akamsihi kama vile anayemuomba asimzungushe. “Tokea tukutoe kule kwa Love, itakuwa imefika miezi miwili sasa, si ndio baba CJ?” Akamrushia mumewe mpira akitetemeka mpaka midomo kwa hofu.

Colins akarudia kuhesabu. Akatoa hiyo miezi miwili. Akabakiwa na miezi kama nane ambayo hana kumbukumbu nayo nzuri. Akakunja uso na kujivuta kujiegemeza kwenye kitanda vizuri. “Labda ungepumzika kwa leo, tuta…” “Connie pls.” Akamuonya dada yake. Kimya.

“Nina miezi 8 hapa, achilia hiyo miwili ambayo tutakuja kuzungumza vizuri baadaye. Sina kumbukumbu nzuri ya hii miezi nane. Najiwa kama ndoto halafu uhalisia hivi! Ila Jelini ndio amenifanya nifikirie zaidi na kuchanganyikiwa! Labda niende kwenye swali jingine,  kwani mimi niliishi na Love!?” “Ndiyo.” Mzee akajibu na kuendelea.

“Ulikuwa ukiishi naye Kigamboni na ukawa ukifanya kazi kwenye kampuni zetu.” “Hapo sasa umenisaidia, maana nilifikiri ni kuweweseka au ndoto!” Akaongea hivyo kisha akatulia kwa muda akifikiria. Wote kimya wakijua anajaribu kuvuta kumbukumbu. Kisha akaona aulize zaidi.

“Ilikuaje nikaishi na Love na si Jelini!? Hapo ndio nachanganyikiwa kabisa! Maana kumbukumbu zangu zinanirudisha mpaka kwenye makubaliano yetu mimi na Jelini kuanza upya. Huku nikiweka mipango ya kumuoa, nikitayarisha sehemu ya kuja kuishi naye!” Akawa kama amekumbuka zaidi.

“Tena nilishazungumza na James, anisaidie nimuoe, ili nitulie, nikijua ni wangu. Na nilikuwa nikipanga nimtengenezee pete ya uchumba kabisa, nimuombe tuone! Sasa hapo ndio nachanganyikiwa! Ikawaje tena nikaishia kuishi na Love mwanamke anayenichukia kupita kitu chochote hapa duniani!? Ananidharau kuliko takataka yeyote ile ya mwisho ambayo unaweza kuifikiria. Hakuwa hata akitaka nimguse kimapenzi, akisema ananionea kinyaa, na akilalamika hata mapenzi yenyewe sijui!” Akafikiria tena kidogo, wakamuona anatingisha kichwa kama anayekataliana na uhalisia.

Haiwezekani kabisa nikawa nilirudi kuishi na Love kama wapenzi wakati alikuwa akinitukana waziwazi na kunitusi hata maumbile yangu! Alikuwa akiyatoa kasoro kwa kunitusi vibaya sana! Au mimi ndio sijaelewa baba ulivyosema nilikuwa nikiishi na Love Kigamboni!?”  Kilisikika kilio cha mama yao hapo, kama aliyefiwa.

“Hili sio geni kwako mama! Inaweza nisiwe nimekwambia kwa undani hivi, lakini kwa hakika, nisingethubutu kuja kurudi kuishi na Love! Alikuwa akinifedhehesha kwa matusi mabaya sana! Tena bila hata huruma au kunifikiria mimi ni binadamu! Sijajiumba mwenyewe, na ninaumia! Sasa ndio najiuliza, niliwezaje mimi kwenda kuishi na Love na kumuacha mwanamke kama Jelini aliyerudisha hali yangu ya uwanaume!” Akawa kama anawaza kwa sauti, anahisi pengine yeye ndio haelewi anachoambiwa.

“Hapana! Nahisi kuna kitu hakijakaa sawa. Tafadhali naomba urudie tena baba. Unasema niliishi Kigamboni na Love!?” “Ndiyo.” “Kwa muda gani?!” “Takribani hiyo miezi nane.” Colins akakunja uso. Akatingisha kichwa kabisa akikataa. Kisha akawatizama. “Nyinyi mnajua kilichonipelekea kuwa na Love na si Jelini?” Kimya. Akaanza kumtizama mmoja baada ya mwingine. Kimya. Akazidi kushangaa.

“Ni nini kinaendelea!? Na kama nilikuwa nikiishi na Love, yuko wapi sasa? Au kwa nini nipo hapa na si huko Kigamboni ambako mnasema nilikuwa nikiishia naye!? Na ninaumwa na nini?” Kimya.

Hapo wakazidi kumshangaza. “Ni kwamba mnamajibu ya maswali yangu ila hamtaki kunijibu?!” Kimya.

Akamgeukia mama yake. “Wewe mama, unafahamu chochote juu ya kinachoendelea kwenye maisha yangu au nikatafute haya majibu kwengine?” Mama Colins akazidi kulia na kuanza kusema. “Nisamehe Colins mwanangu. Nisamehe baba. Nisamehe.” Colins akabaki akimtizama, haelewi. “Nisamehe.” “Nisamehe nini mama?! Mbona unanichanganya na kunifanya niongeze maswali mengi zaidi? Ni msamaha wa nini unao omba?”

Maji Yalishamwagika, Hayatazoleka Tena.

“Ilikuwa hivi.” Mzee akaona amuokoe mkewe. Colins akamgeukia. “Siku moja ya jumamosi, alikuja Love na wazazi wake hapa. Wakaeleza mengi juu ya Jelini.” “Mbali na shutuma za kuwa ni malaya na anashinda baa, ambazo niliwaambia najua?” Colins akauliza na kuendelea. “Kama ndio hizo mbona wote tulikuwa tukijua na niliwaambia nafahamu hayo yote kutokana na kuelezwa na Jelini mwenyewe! Tena baadaye nilikuja kugundua alikuwa akishinda na pombe kichwani ili kufunika kumbukumbu ya alivyokuwa akibakwa shuleni!” Hapo akawasimulia mpaka kufungwa kwa huyo mwalimu.

“Hayo hukutuambia Colins!” “Sikufika kwa umbali huo, kwa sababu mlishaniita mkiwa na Love na wazazi wake. Nikawaambia yaliyokuwa yakiwahusu kwa wakati ule, kuwa hizo shutuma anazotoa Love kwangu si ngeni, namfahamu kwa undani mwanamke niliyemchagua, na nitamuoa yeye. Nilisema, pengine hamkuwa mkiniamini!” “Yeye Love alirudi na kusema zile sio akili zako, Jelini pia ni mshirikina.” Colins akashangaa sana asielewe pointi ya baba yake.

“Kwa hiyo!? Maana hata hilo la ushirikina halikuwa geni!” “Alirudi na kusisitiza hata kule kumkubali Jelini sio akili zako. Ni uchawi uliofanyiwa na Jelini. Ndio akasema amepata mtu wa kukuombea, atakuja naye siku inayofuata, akuombee. Alimleta hapa siku inayofuata asubuhi, ndio tukaja kwako. Yule mtumishi aka…” Hapo Colins akakumbuka.

 Akawa kama amefunguliwa macho yote. Akakumbuka kitambaa cheupe alichofunikwa nacho puani, baada ya kuvuta hewa, akapoteza fahamu. Yaani hapo ndipo akili inamrudia na kukumbuka kila kitu.

“Nimekumbuka! Mlinivamia nikiwa nakwenda kutengeneza na Jelini!”  Akaongea kwa kuhamaki na kuongeza. “Inamaana, kabla sijatengeneza na Jelini, ndio na nyinyi mkanivamia kwa nguvu, tena nikiwa nimewasihi tufanye yale maombi wakati mwingine!”

Akamgeukia mama yake akiwa ameanza kupaniki mpaka sauti ikaweza kutoka. “Mama. Tena mama akanilazimisha!” Akakumbuka. Adrenaline yote ikawa imepanda. Akajawa na nguvu ya ajabu, akiwa amehamaki haswa.

“Sasa, ikawaje yale maombi yanifanye nipoteze fahamu na si…” Akawa ni kama tena ameshachanganywa. Akashindwa tena kuelewa. Kumbukumbu ikagomea hapo. Akaona aulize tu. “Sasa ilikuaje baba!?” “Hakuwa mtumishi wa Mungu, kumbe yalikuwa mambo ya kishirikina!” Colins akatoa macho na machozi. “Kwamba nyinyi ndio mlisababisha mimi kuwekewa yale mapepo yaliyotolewa hapa!?” Hilo swali likawa gumu hakuna aliyejibu.

“Tafadhali malizia baba, ili nijue ilikuaje nikaishia kurudi mikanoni kwa Love.” Ndipo mzee akafunguka. “Acha nikwambie yote bila kukutesa zaidi Colins. Hapo ulipo, unavuna malipo ya ukaidi na makosa yangu. Si mama yako wala Connie. Tafadhali usiwachukie wao. Mimi nahusika.” Akamueleza bila ya kumficha. Kuanzia anapokumbuka mpaka kwenda kumchukua Kigamboni kumleta hapo.

Colins alilia. Akalia SANA. Akalia kwa uchungu. Akalia sana. Alijikunja hapo kitandani akilia kwa kuumia na kusononeka kwa uchungu mno. Mama yake alishindwa kuangalia, akaondoka na yeye akilia. Connie naye akaondoka akilia.

Colins alilia bila kuweza kuongeza neno jingine. Alilia kama anayechinjwa na kisu butu. Mzee yeye alishindwa hata kusogea, akaishia kukaa kwenye kochi la pembeni yake, hajui aseme nini tena. Maji alisha mwaga, hawezi tena kuyazoa.

Akabaki hapo kitini kama asiyejua chakufanya tena. Baadaye alikuja kugutuka pale chumbani pako kimya, Colins alishanyamaza na kupitiwa na usingizi, hata asijue alipotea hapo kimawazo kwa muda gani! Akamsogelea pale kitandani kwa kunyata kama asimuamshe. Akamnyoosha vizuri, akamfunika, na kubaki amesimama, ameduaa.

Kwa Jelini.

Huku kwa Jelini aliendesha kama apae. Akafika dukani kwake, akaegesha gari yake, akashuka kama akimbie. Ezra alikuwa ametulia kwenye gari yake, kimya. Akagonga kioo, akamwangalia. Alionekana alikuwa mbali hata hajui alipo. Akamuona anatoa lock. Akaelewa amekaribishwa garini.

Akaingia mbele upande wa abiria. Kulikuwa na ubaridi mzuri tu. Gari haikuwa imezimwa. Akamwangalia Ezra. Akamuona jinsi alivyopoa usoni. Bila kutarajia akajikuta machozi yakimtoka. Akajifuta kwa haraka. “Nisamehe Ezra. Tafadhali nisamehe mpenzi wangu.” Ezra kusikia mpenzi wangu, akajiweka sawa. Alijua ndio anaachwa. Gafla mpenzi! Akataka kusikia zaidi.

“Nimekosa Ezra. Simu ilikuwa haina sauti. Na nikapaniki, kwa sababu nilimkuta…” “Kwanza naomba utulie, tuzungumze. Sijakasirika Jelini, ila nimekuelewa. Pengine mimi ndio niombe radhi kwa kukupigia simu hovyo. Natamani ningejua tokea mwanzo kuwa upo na Colins, kwa hakika nisingekusumbua.” “Hujanisumbua Ezra!” “Hapana. Ule si uungwana. Mimi si mtu wa kufanya hivyo. Ni mtu ninayeamini ukipiga simu mara moja, kama mtu hajapokea, inamaana kwa wakati huo hayupo kwenye nafasi ya kuzungumza. Atarudisha simu baadaye.” Akaendelea Ezra, taratibu tu kama kawaida yake.

“Nakiri niliingiwa hofu ya ajabu, nikashindwa kufikiria, nikidhani historia inajirudia. Kuachwa bila kosa. Kumbe ni kweli!” “Sio na mimi. Nilikuahidi sitakusaliti Ezra, niamini sitakusaliti.” “Colins amerudi Jelini! Na kuonyesha ana nguvu kwenye moyo wako, ulinisahau kabisa! Tafadhali usiniahidi tena. Tuache tu.” “Hapana. Najua ninachokizungumzia, na hata wao nimewaambia.” Jelini akamueleza kwa kifupi mpaka sehemu inayomuhusu yeye ya hapo mwisho.

    Kidogo Ezra akatulia kuona ametajwa huko kwa kina Colins kwamba na yeye anahusika kwenye maamuzi ya kumuuguza Colins. Ila kitendo cha kusahauliwa kabisa siku nzima, kikamuashiria, anashika kwenye makali wakati Colins yupo kwenye mpini. “Naomba zungumza na mimi Ezra! Na sijakudanganya. Na sitaki kukuumiza.” Akamuona anatingisha kichwa kukataa.Akatulia kwa muda, kisha akamuona anatingisha kichwa kana kwamba anapingana na kilichopo mawazoni.

     “Lakini Colins, mwanaume unayempenda, mwenye viapo vyako, uliyekuwa ukimsubiria muda wote, amerudi Jelini! Na si amerudi tu! Amejaa kwenye ulimwengu wako! Kwa vitendo, umeonyesha leo, linapofika swala la Colins, akili, mawazo na moyo wako vinakua ni vyake yeye tu. Huna nafasi ya mtu mwingine! Hilo siwezi kupuuza.” Jelini akazidi kuumia. Akafikiria akahisi ndivyo ilivyokuwa hata na kwa Colins linapofika swala la Love pamoja na familia yake. Hata yeye husahauliwa kabisa.

    “Nakuahidi sitafanya kama yeye alivyonifanyia mimi. Sitakuumiza Ezra. Leo nimekosa. Nitatoa simu kwenye silence, naweka sauti. Kabla sijafanya jambo, nitakujulisha japo kwa ujumbe. Sitakusaliti hata na Colins. Sasahivi ni mimi na wewe tu. Na Colins anajua mimi si msaliti.”

    Akafikiria, moyo wake ukagoma kabisa mpaka kichwa kupinga. “Tafadhali tule. Pata muda wa kutulia. Fikiria kwa upya. Mimi naelewa. Usiongee jambo jingine tena. Tule tu, ukapumzike. Pata muda wa kufikiria na kuingiza habari ya kuwa, Colins amerudi. Na nakuahidi sitakubugudhi tena kama nilivyofanya leo. Naomba usiku wa leo, tule tu, basi. Usiniahidi kitu kingine TENA. Tuache tu.” Jelini akapoa kabisa maana Ezra alizungumza kwa kumaanisha kabisa si kubembeleza tena, kama anaye msaidia kuhitimisha.

    Akatoa chakula. Bado kilikuwa na joto zuri kama aliyekuwa amehifadhi sehemu maalumu ili kisipoe. Aje akikute bado ni cha moto. Jelini akazidi kuumia jinsi Ezra alivyofika kiwango cha mwisho cha kumjali, wakati yeye alimsahau kabisa.

    Ukweli kwa masaa yakutosha kabisa, alimsahau huyo kiumbe. Akili yake haikupitisha hata jina lake kwa bahati mbaya! Akamsikia akiombea chakula. Akarudi pale garini kimawazo. Usiku huo wakala kimya kimya. Mpaka wakamaliza, Ezra akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kimechanganyikana!

Jelini Atasimamia Wapi?

Kwa Upande Wake Ezra Amekubali Yaishe. Ashajua Mwenye Kisu Kikali, Ni Colins Ndiye Anayekula Nyama. Bora Ajiweke Pembeni. Ameondoka Na Kumuacha Jelini Awe Huru.

Colins Analia Kupokonywa Tonge Mdomoni, Na Wazazi.

 Maji Yameshamwagika, Hana Uwezo Wa Kuyazoa.

 Ni Kilio & Maumivu Pande Zote.

Ni Nini Kitaendelea?

USIPITWE.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment