Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 15 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 15

Kwa hakika Jelini alipania. Alitoka kazini mapema, akaenda saluni. Akatengenezwa vizuri na kurudi nyumbani. Saa moja kasoro Ezra akawa amewasili. Akamtumia ujumbe yupo nje getini.
‘Natoka.’ Hakutaka Ezra aingie, na kwa kuwa na yeye hakukaribishwa ndani, akabaki ndani ya gari akisubiri mpaka alipomuona Jelini dirishani. Akafungua kabisa mlango na kutoka.

Wakajikuta wakicheka. “Ndio unapendeza hivyo!” “Mimi napenda kupendeza. Na wewe umependeza sana Ezra. Unanukia vizuri!” “Asante. Ila kweli umependeza sana, mpaka naanza kufikiria ni wapi nikupeleke.” “Wewe wala usijali. Mwenzio kupendeza ndio kawaida yangu.” Ezra alicheka sana.

“Sikutanii. Mimi naweza kupendeza hata sehemu ambayo unaweza dhania hapahitaji kupendeza. Napendeza tu kwa ajili yangu, ndio najisikia raha. Sijali mazingira wala walionizunguka.” “Ilimradi wewe upendeze?” “Kabisa. Na kama nipo na Jeremy, nataka na yeye pia apendeze sanaaa.” “Ndio maana kila wakati ni msafi?” “Kabisa. Napenda sana awe nadhifu. Naona ndio starehe yangu.” “Hongera. Basi tuondoke hapa.” Safari ikaanza, wakifikiria pakwenda.

“Usiogope garama, nitakusaidia. Leo nilitamani kutoka, niende sehemu nzuri sana. Nipumzike.” “Sijali garama, ila sehemu utakayoifurahia. Na mimi nataka usiku mzuri.” “Mwenzio nataka usiku mzuri ambao naona nishaanza kuupata, ila na wa hadhi.” “Umeshaupata!?” “Kabisa! Umekuja kunichukua Ezra! Nimefurahi.” Mwishoe wakakubaliana sehemu ya kwenda. Wote walipafurahia, na wakajua watapata huduma nzuri zitakazofanana na wao kwa usiku huo. Ezra akaelekea huko.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walifika na kutafuta sehemu nzuri wakakaa kwenye kona yao. Wakiangaliana. Muhudumu akafika kwa haraka, wakaagiza vinywaji, na kutulia. “Wewe huwa unapenda nini?” Ezra akaanza kwa swali. “Kupendwa.” Ezra alicheka mpaka machozi, maana Jelini alijibu kwa haraka bila kufikiria. “Usicheke sasa nikwambie.” “Nakusikiliza Jelini. Ila sikutegemea! Wenzio huwa hawasemi hivyo.” “Mimi vingine vyote sitaki. Naweza kujitafutia mwenyewe. Kwanza sasahivi ni kama nina kila kitu.” Hapo Erza akakubaliana naye. Jelini alikuwa mambo safi.

“Ehee!” Akataka aendelee. “Nataka mtu anipende kwa dhati. Mimi tu, na anifuatilize. Anipe mimi kipaumbe. Katika watu wote, mimi ndio niwe mtu wake wa kwanza. Anibembeleze mimi tu kila wakati.” Ezra akaanza kucheka tena maana Jelini alikuwa akijieleza kama aliyekuwa amejiandaa kwa hilo swali.

“Sitajali kama akinipenda sanaaa. Ndio nitafurahi. Umeelewa sasa?” “Nimeelewa Jelini.” Akakubali akicheka huku akimtizama, mara kinywaji kikaletwa, akainamia glasi yake na kuanza kunywa bila wazo la pili.

“Labda niulize swali jingine.” “Karibu.” Ezra akaanza kucheka akimwangalia. “Usicheke sasa!” “Sawa Jelini. Itakuaje sasa ikija kutokea mtu akakupenda hivyo na wewe usimpende?” “Wala sitampa mtu bahati ya kunipenda kabla mimi mwenyewe sijampenda kwanza.” “Waw!” Ezra akajiweka sawa.

“Sasa wewe utapata wapi muda wa kunipenda wakati haupo na mimi? Huna namba yangu ya simu wala hukai karibu yangu! Utanipendaje sasa? Si mpaka nikupe nafasi ya kuwa karibu na mimi ndio utaweza kunipenda!” “Lakini kweli!” “Umeona sasa?” Ezra akatulia akifikiria.

“Swali jingine.” Jelini akaanza kucheka. “Bora niulize nijue vizuri.” “Wewe uliza.” “Hudhani huyo mtu akipata hiyo nafasi atakua akihofia kukosea. Atabaki akibabaika mpaka atakosea kweli kwa hofu?” “Ujue huyo mtu atakuwa hajanipenda kwa dhati. Mtu anayekupenda kwa dhati hajitahidi kukufurahisha. Na wewe utamuona tu. Inakuja so natural. Anakuwazia furaha yako kuanzia asubuhi mpaka usiku. Anafikiria kula yako. Hata kama anakua amechoka, anatoa muda wake anakuja kula na wewe. Anahakikisha umeshiba. Anataka kujua siku yako iliendaje. Na si kwamba anakuuliza tu, anakua anakusikiliza kila neno. Halafu ukimwambia kitu, hasau.” Hapo Ezra akatulia kwa furaha maana alisema yote anayomfanyia yeye.

“Jelini wewe umejawa shukurani mpaka unanifanya nianze kujichunguza mimi mwenyewe.” “Kwa nini tena?” “Aaah! Sijui bwana! Ila sijawahi kukutana na mtu anayeweza kugeuza jambo dogo, akalikuza kwa shukurani kama wewe. Na hufananii hivyo kabisa! Unafurahishwa na vitu vidogovidogo sana!”

“Acha nikuulize Ezra, kisha uniambie tu ukweli. Wewe unapata mtu. Sio kwamba ni wa kijiweni. Hapana. Anashuguli zake. Nyingi tu tena za maana. Kumbuka huyu mtu anaamka saa 11 asubuhi. Anaratiba nyingine za kifamilia pia. Kanisani. Lakini bado akiona jua kali, hata kama yupo njiani akiwa na shuguli zake, lakini anachepuka hata kukuletea maji, anahakikisha unayanywa hayo maji, ndipo anaondoka.” Ezra alicheka sana. Maana alimfanyia hivyo Jelini akimwambia anaweza kuwa busy akasahau kunywa maji. Alimletea chupa ya maji akiwa anawahi kanisani. Akasubiria mpaka alipoimaliza, ndipo akaondoka.

“Halafu mchana. Muda wake wa chakula, anakuletea wewe matunda na maji pia. Na jioni. Mtu huyohuyo mwenye majukumu yake, eti anakufuata kazini. Anakusubiria kwenye gari mpaka mle naye. Kana kwamba haitoshi, anakutafuta tena usiku. Kukusikia kama ulirudi nyumbani salama. Nakutaka kusikia siku yako iliishaje. Na hasau wafanyakazi wako wote na vituko vyao.” Hapo Ezra alicheka sana. Maana alianza kuwa akiwaulizia wafanyakazi wa Jelini kwa majina na vituko vyao. Basi watazungumza wakicheka viroja vya siku mpaka kuagana.

“Acha kucheka bwana! Sasa wewe niambie, hivyo ni vijikiti vidogovidogo?” “Hapana Jelini.” Ikabidi tu akubaliane naye tena. Maana alishakuza tena aliyomfanyia. “Umeona eeh! Sasa utafananisha na kuhongwa nyumba au gari halafu mtu hakujali? Anakua na mambo mengi na wanawake wengine akikunyanyasia mamali aliyokupa! Akuu! Mimi hivyo sitaki. Sasahivi hata mimi nikitaka gari ingine naweza kujinunulia mwenyewe bila hongo.” “Hapo nimekuelewa Jelini. Nimeelewa sana.” Wakatulia na muhudumu alikuwa amefika.

Jelini mzoea kula nje na alishaishi na Kasa, anajua majina yote kwenye menu. Akachagua kwa urahisi tu mpaka Ezra akamshangaa wepesi wake. “Naona mwenzangu wewe mwenyeji kwenye maeneo haya!” “Sitakudanganya. Mimi sinaga shida kucheza kwenye viwanja vya ugenini.” Ezra alicheka sana.

“Ujue Jelini wewe ni mtundu sana!” “Acha nikusaidie Ezra. Mimi sina neno.” Akaongea kwa urahisi tu, na kuanza kumtajia vile vyakula mpaka Ezra akapata anachotaka. Wakamuagiza muhudumu, akaandika na kuondoka baada ya kuwaongezea vinywaji.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Jelini?” Jelini akamwangalia maana aliomba abakie na menu, asome kitu atakachoweza kuagiza chakula cha kuondoka nacho. Jeremy alimwambia hatalala anasubiria chakula cha hotelini.

“Abee!” Akaitika akifunga menu. “Eti unafikiri naweza kufaa nikawa mtu wako?” “Yaani hapo ndio unanitongoza!?” Ezra hakutegemea, ilibidi acheke yu. Maana alianza kwa hofu sana akikusanya nguvu. “Nyie jamani Ezra! Sasa hivyo ndio unanitongozaje jamani! Huna swaga kabisa! Mimi sijavutiwa.” Jinsi alivyolalamika na kupandisha mabega kabisa, Ezra akashindwa hata kumtizama. Alicheka sana.

“Bwana nitongoze vizuri na maneno mazuri sio hayo maneno ya jumla hivyo!” “Jelini!” “Kweli hivyo mimi sitaki. Wenzako wanasemaga yale maneno mazuri. Mpaka wengine wakinywa maji eti wananiona kwenye glasi.” Ezra hana mbavu.

“Sasa hii ndio kali Ezra. Mwingine anasema yeye halali, usiku ananiota.” Ezra akazidi kukaukiwa ila yeye Jelini analalamika. “Sasa anakuotaje hajalala?” “Ndio ushangae sasa. Lakini wewe huoni hizo ngonjera zinavutia? Wewe umekuja kirahisi sana bwana! Mimi hivyo sitaki.” “Basi nisamehe Jelini. Naanza upya.” “Sasa sio sasahivi na wewe Ezra! Tusubiri kidogo mshituko uishe! Maana umenishitua sana. Hujanitendea haki.”

“Kipengele cha kunisamehe je?” “Nitakufikiria Ezra. Umecheza sana chini ya kiwango. Na nitakuja kusimulia na wanao, jinsi ulivyoanza vibaya.” Ezra alishituka nafsini mwake, hakutegema Jelini kuzungumza hivyo. Ila mwenyewe aliongea kama kitu cha kawaida sana, akarudisha macho kwenye menu. “Inamaana ameshaona uzee wangu na yeye!” Ezra hakuamini. Akapoa kabisa mpaka kuhisi kutetemeka.

“Huyu Jeremy ananinyima raha bwana! Nakuwa nawaza chakumpelekea mpaka mimi mwenyewe sifaidi! Naomba uniwie radhi. Nimpigie simu, nimuulize anataka kula nini, asinipe mimi kazi ya kumchagulia.” “Usijali.” Akatoa simu kuzungumza na mwanae.

Akawa akimwangalia kwa kujiiba akiwa anazungumza na mwanae. Anacheka na mwanae hana mbavu. “Sasa kumbe unajua unachokitaka, kwa nini hukuniambia tokea mwanzo?!” Akamsikiliza akicheka, mwishoe akamuaga. “Kweli Jeremy maneno mengi kama mama yake!” Akaongea hivyo akirudisha simu kwenye pochi. Ila akagundua Ezra amepoa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa mbona umepoa tena?” “Nilikuwa nikikupa nafasi ya kuzungumza na Jeremy.” “Hanaga kumaliza kama mama yake. Mama kila siku anatuambia. Tuna maneno mengi. Tukianza kuongea, hatumalizi.” “Yeye si mzungumzaji?” “Mama Jema!?” Akamuuliza kwa mshangao na kuanza kucheka. “Kwa nini?” “Labda awe na lililomfurahisha. Hanaga muda wa maneno mengi, kwanza hanaga mazoea ya kijinga. Ila mimi na Jeremy tunamjualia. Tunaweza kumkalisha kwa muda atusikilize. Lakini si hivihivi. Na nahisi Jema yupo kama mama au yeye kazidi. Jema mkimya na mpole sana.” Wakaletewa chakula, wakaanza kula.

Ya Ezra.

“Zamu yangu ya maswali.” Ezra akamtizama. “Wewe mchumba wako ilikuaje?” Ezra akaanza kucheka tena. “Kwa nini udhani kulikuwa na mchumba?” “Hivyo ulivyo na unazungukwa na warembo hivyo! Kweli usiwe na mchumba?” “Hukukosea. Ila aliniacha alipokwenda masomoni.” Jelini akatoa macho. Ezra akacheka na kunyamaza.

“Tuanze taratibu. Kwamba mlikosana au mlikuwa na matatizo kwenye mahusiano yenu?” “Hapana Jelini! Nilimvisha mpaka pete ya uchumba nikawa nataka kumuoa kabisa ndipo ikaja hiyo nafasi ya kwenda masomoni. Kwa mujibu wake, hiyo nafasi ya masomo ni kitu alikuwa akikisubiria kwa muda mrefu sana, na ndio yalikuwa maombi yake. Akasema lazima aende. Junior alipomwambia tufunge ndoa kwanza, ndipo aende, akasema akirudi likizo ndipo tutafunga ndoa. Basi, vikao vikaanza. Huku tukiwasiliana. Ilipobakia kama miezi miwili arudi nchini, ndio tufunge hiyo ndoa, mawasiliano yakaanza kusuasua.”

“Kumpata ni kwa shida, na kila ukimpata analalamika yupo busy. Zilipobakia siku kama 20, akamtafuta Junior, akamwambia yeye haoni maisha yake tena huku nchini, ameamua kuishi huko.” “Sasa na wewe?” “Naona na wewe ulikuwa kama Junior. Alimuuliza hivyohivyo. Akasema…” “Umfuate?” Jelini akamalizia kwa swali. Ezra akacheka kwa masikitiko.

“Bora ingekua hivyo. Alimwambia aniambie niendelee tu na maisha yangu. Yeye ameanza kule upya.” “Jamani!” “Na hakutania. Nafikiri ndani ya mwaka uleule tulisikia ameolewa, tena ana mtoto.” Jelini akabaki ametoa macho.

“Yeap. Hiyo ndio historia yangu. Sio ndefu sana, ila imekamilika. Mbaya zaidi familia yake ipo palepale kanisani. Dada zake utakuwa unawajua na kaka yake. Na wenyewe walikwenda harusini. Mmoja nafikiri kama hakumsaidia yeye, basi alimfuata huko, anaishi naye.” “Ezra!” “Kabisa. Na ukumbuke na vikao vya harusi hapa nchini, pale kanisani, vilikuwa vikiendelea, na ndugu zake walikuwa bega kwa bega na mimi kuhakikisha nafanikisha kila jambo. Lakini waliponigeuka, ikawa ni kama mimi tena natakiwa nisiwe mbinafsi. Nielewe nafasi aliyokuwa nayo huko. Inawezekana halikuwa andiko langu, na mengine mengi. Ikabidi niwe mpole. Nikubali yaishe. Kuwe na amani.”

“Maana habari zake za harusi, mtoto wa kizungu aliyezaa na…” “Kwamba ameolewa na mzungu?” “Sasa unafikiri wazazi wake wangetoa baraka zao hivihivi? Wanasema huyo mzungu ndiye atamsaidia kuishi kule kwa utulivu. Maana na yeye atakuwa raia huko, sababu huku harudi na mengine mengi. Sasa kashazaa na mtoto wa kizungu tena, mimi nina faida gani? Basi habari zangu zikafukiwa uvunguni, zikawa sasa ni zake na za mume mpya wakizungu.”

“Jamani Ezra!” “Ilikuwa mbaya Jelini! Nilikaribia kuchanganyikiwa, nisiamini. Nilikuwa nikijiuliza nilipokosea mpaka kuachwa vile! Halafu sasa hakuna pakuhuzunikia, ikawa ni kama yeye amebahatika. Nikabaki kujiuliza, kwamba kweli hawa watu wamesahau kabisa kama mimi ndiye niliyekuwa mchumba halali! Lakini ikawa ni kama machozi ya samaki.”

“Nikabaki kusimama na baba yake Junior, ambaye ndiye mchungaji pale, Junior na mama yake. Ukweli hawakuacha kunifariji. Alipoona akili haijatulia, alinitoa kabisa hapa mjini. Akanichukua mimi na Junior, tukaenda Milimani kuhubiri injili.” Jelini akaanza kucheka. “Na nikikwambia Milimani, ujue ni kwenye kusubiri giza liingie ndio mkaoge mtoni. Hamna umeme. Ila hali ya hewa nzuri.” “Na yule mchungaji hashindwi.” Akasadiki.

“Siku saba! Tunahubiri injili. Mpaka anatuambia tunarudi mjini, moyo umepoa, zimebaki stori za Milimani tu. Ukikaa na sisi watatu, utakuja kugundua ni neno tumelizoea sana. Tunamtania mchungaji. Mtu akisumbua tu, tunamwambia ampeleke Milimani.” Jelini alicheka sana. “Hata Junior naye yupo hivyohivyo. Ukishamsikia tu akikwambia huyu ni wa Milimani, ujue huyo mtu hayupo sawa.” “Pole Ezra jamani! Pole sana.” “Asante. Ila ikawa kama imenitia hofu ya mahusiano kabisa. Sikurudia kutongoza tena.” “Hapo nakuamini kabisa.” Ezra alicheka sana.

“Kwa utongozaji ule! Unaonekana uliondoka kwenye game muda mrefu sana. Lakini usijali. Taratibu.” “Sijaharibu?” “Matendo yako yamenivutia Ezra, kuliko maneno.” “Kweli?” “Kabisa. Mimi ni muwazi, nisingekudanganya. Kwanza wala usingekuwa hapa na mimi. Si unakumbuka hata nilikukatalia chakula mara ya kwanza?” “Usinikumbushe.” Jelini akaanza kucheka.

“Mimi sihongeki kwa urahisi Ezra. Kwanza sitaki. Ila wewe mtu mzuri. Mkweli. Unasimamia maneno yako. Hayo mashairi ya kudanganywa kupendwa, nayasikia mpaka masikio yamezoea.”

 “Kwa hiyo bora nisijayasema tu?” “Usijitoe kirahisi hivyo Ezra, bwana! Lazima wewe uniambie. Wewe nataka kukusikia. Na sio useme mara moja halafu eti tukiwa wazee husemi tena!” Ezra akazidi kucheka kwa furaha. “Mpaka uzeeni?” “Yaani uwe unarudia rudia tu.” “Hutachoka?” “Usijali, nitakuwa sikumbuki. Kila ukisema nitakua naona mpya.” Ezra akacheka akimtizama. Asiamini kama anazungumza na Jelini kirahisi hivyo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walikula mpaka wakamaliza. Akaletewa chakula cha Jeremy, akamchukulia na mama yake. “Naomba nilipie Ezra. Tafadhali. Jeremy kuna chakula chake anapendaga. Ni garama. Na nimemchukulia mama nyama choma. Bei ni kubwa. Nimejiandaa.” “Usijali. Na mimi nilijiandaa.” “Lakini kwa ajili yetu tu. Sio ukoo mzima! Siku nyingine utalipia, ila leo acha iwe sisi tu.” “Jelini, acha nilipie. Kwanza nimefurahi jinsi unavyojali watu wa nyumbani kwako. Sijali kulipia.” “Najua. Ila hawa ni jukumu langu. Tafadhali acha nilipie.” “Na mimi ni jukumu langu.” “Hata kutongoza hujatongoza bado! Inakuaje jukumu lako?” Ezra akaanza kucheka.

“Nimesema najiandaa. Nitakutongoza Jelini. Mbona pressure?” “Sasa unajuaje kama nitakukubali?” Ezra akamtizama kwa makini kama anayejaribu kumsoma. “Maana naweza kukataa.” “Jelini! Wewe unayeona mpaka uzee wetu pamoja, kweli unikatae.” Jelini alicheka sana, kama mazuri.

“Basi mama pia amenigundua. Nimekua na furaha. Moyo umekua mwepesi. Anasema mpaka usoni naonyesha.” “Sasa ukamwambia sababu ni nini?” “Nikamwambia nahisi Ezra atakua ananipenda.” Ezra alicheka mpaka akapaliwa. Jinsi alivyoongea, eti kama kwa soni vile. Kisha akajificha.

    “Jelini! Sijakupatia mwenzako.” “Mimi nataka ibakie hivyohivyo.” “Hutaki mwenzio?” “Sitaki.” Akakataa na kupandisha mabega kabisa. “Unataka ujaliwe wewe tu?” “Peke yangu.” “Na sitakutafutia mwenzio. Kama utabaki kwangu. Ukaamua kuwa na mimi. Ukaniahidi katika yote, hutabadilika. Maisha yako ni yangu. Utasimama na mimi katika yote, ujue utabaki peke yako. Nitakupenda Jelini, mpaka na wewe utajua nakupenda. Nitatunza furaha yako kwa kadiri ya uwezo wangu. Na kama mimi nikishindwa, basi nitamuomba Mungu wangu. Sitakuacha ulale na uchungu moyoni. Utakalobeba litakuwa langu. Na sitabadilika.” Mpaka machozi yakamtoka Jelini.

    “Ila hizo ahadi zangu, ni pale utakapoamua kubaki na mimi. Usilie sasa!” “Mimi nimefurahi.” “Kweli?” “Sana.” “Kwa hiyo?” “Acha kwanza nifurahie bwana Ezra! Mbona kama unakua mtu wa wivu?” Haya anaongea na machozi kibao. Ezra hana mbavu. “Mwenzio napendwa!” “Na kweli unapendwa na Ezra.” Akajifuta machozi akatulia.

Akamuona ananyanyuka anamfuata muhudumu. Akamuona anazungumza naye kitu. Akamkabidhi kikaratasi. Akaenda kulipia na kurudi na bili yao akamkabidhi Ezra. “Mbona kidogo hivi?” “Nimelipa chakula cha mama na Jeremy.” “Jelini! Kwa nini umefanya hivyo?” “Ili wapate hamu ya wao siku nyingine ukiwakaribisha, waje. Wasidandie bahati yangu.” Japokuwa alizungumza kwa utani, lakini Ezra alipoa kabisa. Akamuita muhudumu kwa ishara, akafika hapo, akamlipa. Jelini akamuona jinsi alivyopoa.

Usiku wa Ahadi.

    “Asante kwa chakula Ezra. Nimefurahia.” Jelini akavunja ukimya mara walipoingia garini, kabla Ezra hajatoa gari. “Karibu. Na mimi nimefurahia.” Akalazimishia tabasamu. “Ila sasahivi huna furaha. Naomba nisamehe na unielewe Ezra. Nimeingiwa hofu, kila kitu nachukua tahadhari.” Ezra akamwangalia.

    “Usiondoke kwanza. Acha nikwambie. Katika siku chache nilizokuwa na Colins, ni kama alimzoea sana Jeremy. Jeremy akampenda sana. Hakuacha kumuulizia akitaka kuja kumuona tena. Nilikuwa sijui jinsi ya kumwambia maana ni kama alimuamini sana Colins. Sasa kitendo cha wazazi wake kuja kunivamia nyumbani na maneno mabaya sana kwangu na mama, mbele ya kila mtu mpaka Jeremy, kilimchanganya sana, mpaka ikabidi mama azungumze na mimi na kuniapisha.” “Juu ya nini?”

    Jelini akafikiria akaona amwambie tu. “Jeremy nilimzaa nikiwa mdogo sana. Mama akamchukua kama mwanae. Anamlinda kwa kila namna na Jeremy ni mtoto mzuri sana. Mama anasema hataki nimchanganye. Aje aige tabia za wanaume wa ajabu ajabu. Sasa alichoniapisha ni kwamba, nilichokifanya kwa Colins, nisiwahi kurudia tena.” Ezra akatulia kama kujaribu kuelewa.

    “Colins alikuwa akija nyumbani anaingia mpaka chumbani kwangu na kwa Jeremy. Nilimuweka kwa haraka karibu ya Jeremy. Wakazoeana sana, kisha akaondoka na asigeuke nyuma ila maneno mabaya ya wazazi wake. Kwa hiyo amenionya nisilete tena mwanaume mle ndani, isipokuwa nina uhakika naye kwa asilimia 100. Na afike pale akiwa na wazazi wake, ameenda kutoa mahari, na sivinginevyo.” Ezra akaelewa ndio maana hakukaribishwa hata ndani.

    “Na ukiangalia ni kweli Ezra. Mama anahaki. Pale ni kwake. Ametutunza mimi na mtoto wangu mpaka sasa. Hata mara moja, hajawahi leta mwanaume pale ndani. Tafadhali nipe muda nirekebishe makosa. Nimeishi maisha ya ajabuajabu sana. Yaani sasahivi ndio kama nahisi nitatulia, kwa sababu nimekuchunguza, nimeamini wewe umetulia Ezra. Ndio maana napata moyo, najiambia pengine safari yangu ya kuhangaika imefika mwisho. Kwa maneno tu, hakuna atakayeniamini. Maana nishawaahidi sana, na kurudia makosa sana. Naomba muda uje uwaaminishe. Tafadhali nivumilie.”

     “Nimeelewa Jelini. Ila kama kweli umeamini mimi si myumbishaji. Nitabaki na wewe, kwa nini usinipe nafasi tukaanza wote?” “Sikujua kama unataka Ezra.” “Kweli nisitake nafasi ya kuweka msingi pamoja na wewe! Hudhani kwamba itatusaidia? Na si lazima ikawa matangazo. Ni maisha yetu mimi na wewe. Hakuna sababu ya wengine kujua. Tufanye kimyakimya ila kwa makini tukijua watu wanatuangalia, na Mungu pia anatuangalia.” “Sawa Ezra. Basi katika hilo naomba msaada wako. Na univumilie. Taratibu. Mabadiliko yote hayatakuja kwa haraka.” “Naelewa.” Akamuona akicheka.

    “Nini?” “Kwahiyo tunaanza msingi wetu?” “Mimi sina kipingamizi Ezra. Wewe unanipenda na unatabia nzuri. Hata mama anakusifia. Tuanze taratibu, tuone tutakapofikia.” Hilo likamfurahisha sana Ezra. Kakubaliwa na Jelini! Hakuamini. Akajinyanyua kutoka kitini, akambusu shavuni. Bwana Jelini alifurahi! Akabaki amejishika shavu akicheka. Ndipo akaondoka gari.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

    Ukawa usiku wa namna yake. Kwa mara ingine tena, Jelini akajikuta anatoa kiapo kwa mwanaume mwingine tena. Tena kwa furaha tu wala asijilazimishe. Alikusudia kweli kutafuta ndoa, kwa udi na uvumba bila kuchoka. Palishindikana kwa Colins. Akasubiria kwa muda  wote huo akiamini kama kawaida yake, atarudi tu. Lakini ikawa kimya, asijue jinsi Colins anavyomtafuta.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

    Usiku huo alipofika tu nyumbani, akampigia Jema akiwa na mama yake. Wanazungumza na Jema kwenye simu, wao wapo chumbani kwa Jelini. Akawasimulia jinsi hilo juma lilivyokwenda mpaka usiku huo wa ahadi.

“Ila wanamsifia kweli pale kanisani.” Mama Jema akaongeza. “Na mimi hizo sifa ndio zikanifanya nimpe nafasi. Lakini mpaka sasa sijajuta. Aisee Ezra anajali jamani! Anaweza nifuata, eti kunipa tu maji ya kunywa! Matunda na maji ya kunywa ni kila siku mchana ananiletea popote nilipo. Anakula na mimi chakula cha usiku. Ananijali sana.” “Na Jelini unavyopenda kupendwa wewe!” Jema akaongeza. “Nakubembelezwa.” Akaongeza yeye mwenyewe mama yake akimtizama yu. Wakazungumza mengi watatu hao wakicheka, ila Jema akagundua Colins hajatajwa usiku huo hata mara moja. Na yeye akaona amuache tu.

Jumamosi Ya Mazito&Maamuzi Magumu.

    Mida ya saa nne asubuhi, siku hiyo ya jumamosi Ezra akamfuata tena kazini. Alipomuona kwa mbali, akatoka kwa haraka akiwa amejawa furaha. Ezra akamshika mkono na kumvutia upande aliokuwa ameegesha gari lake. Kisha wakasimama nje ya gari. “Nimekuwahi kabla hujaanza kuwa busy.” Jelini akafurahi. “Ulilala vizuri?” “Sana. Na wewe?” “Na mimi, nikijua nina Jelini kwenye maisha yangu.” “Sasa sio uwe busy, uanze kusahau hilo.” Ezra akaanza kucheka. “Si mpaka uzeeni?” “Mimi naona nibadilishe. Iwe mpaka kifo.” Ezra hana mbavu, furaha imemjaa.

    “Nimekuletea hii cooler. Ndogo tu. Inaweza kukaa hata kwenye gari yako bila kukubugudhi. Yakutunzia maji ya kunywa.” Jelini akaanza kucheka, huku akichungulia ndani ya gari, akiitizama. “Asante kujali Ezra. Ila mimi sijatoka, nitatoka baadaye. Nitakunun…” “Sio mashindano Jelini! Nimefikiria jinsi unavyozunguka mchana kutwa, joto, jua kali, na hapa dukani mnatumia feni tu. Unatokwa jasho, unahitaji maji ya kunywa wakati wote.” “Wewe unanifikiria sana Ezra! Ila ujue na mimi nakufikiria bwana. Nitakununulia zawadi.” Ezra hana mbavu.

    “Tena nitakunununulia zawadi nzuri sana mpaka ushangae.” “Kuna zawadi moja kubwa ninayotaka kutoka kwako Jelini. Unataka kuijua?” Jelini akatingisha kichwa akicheka kwa deko, huku akimtizama.

    Akamshika mikono yake yote miwili kwa upendo sana akimtizama. Kisha akamwambia. “Niahidi hutaniacha mimi. Niahidi utabaki kuwa wangu tu. Na nakuahidi hutajuta Jelini. Nikubali tuwe wote, tufunge huu ukurasa wa kutafuta, tuanze kujenga kwetu. Nilikwambia hutajuta?” Jelini akacheka. “Mpaka sasa sijajuta.” “Basi haitakuwa ni mwanzo tu. Kama ulivyoona uzee wetu, ujue tutabakia hivihivi tukipendana.” “Na mimi nataka tubakie hivihivi, tena wawili tu. Hatutaki mtu mwingine.” Ezra akacheka akimwangalia kama anayesubiria jambo, lakini Jelini akawa amemalizia hapo.

    Ezra akagundua hajawahi kumwambia kama na yeye anampenda. Akajisikia kuumia kidogo, ila akaona amchukulie taratibu. Pengine bado hofu ya kukataliwa baada ya kumwambia  Colins anapenda, ilikuwepo. Ila akashangaa anamwachia mikono. Hapohapo nje. Hadharani. Akamkumbatia. Kisha akatulia kabisa mikononi kwa Ezra. Ilibidi amshike tu vizuri, maana alikuwa ameegemea kwenye gari. Akatulia hapo kwa muda kama ambaye hana majukumu. Ezra naye akamuacha tu, ila akiwa amemshikilia vizuri, kisha akamuachia yeye mwenyewe kama aliyetosheka.

    “Nimefurahi Ezra. Asante kwa muda wako na zawadi.” “Karibu. Usiku baada ya kikao, nitakupigia. Kama utakuwa na nafasi, nitakuja tule wote.” “Si ulisema kikao cha mwisho kinaweza kikachukua muda mrefu sana?” “Ndiyo na hapana. Maana leo tunahitimisha kila kitu. Kinaweza kuvuta. Lakini pia ukumbuke harusi si yetu. Na sisi ni waalikwa. Ila tunajipanga kinyumbani tu. Ila tutawasiliana.” Akambusu juu ya kipanda uso, Ezra akaondoka Jelini akimwangalia anavyoondoa gari. Kisha wakapungiana mkono, ndipo akageuka kurudi dukani kwake.

Mama ni mama tu.

Wakati amegeuka akirudi ndani, uso kwa uso na mama Colins kama aliyekuwa akimsubiria hapo pembeni ya duka, muda wote. Akashituka sana. Akabaki ameduaa akishindwa kusogea. “Colins anaumwa.” Jelini akakunja uso wa mshangao. “Kama ungependa kumuona, yupo nyumbani.” “Unataka nije halafu jambo litokee, mnisingizie mie mchawi ndio nimemloga! Akuu! Mimi sitaki. Nyinyi mna imani za ajabu! Mimi sitaki ukaribu na nyinyi.” Jelini akaingia ndani.

Mama Colins akaondoka akiwa amekata tamaa kabisa. Mbali na maneno aliyoyasema, amekutana na kijana Ezra anayeonekana mambo safi, halafu anamjali Jelini, wakati kijana wake hata hatizamiki! Akaondoka hapo njia nzima akilia kwa uchungu na majuto. Akafika kwake, akakuta Colins amelala. Ndipo akaweza kueleza yote aliyoyakuta hapo, akiwepo kijana Ezra, jinsi alivyowaona wawili hao. Na majibu ya Jelini. Connie na baba yake wakabaki kimya kila mtu akiwaza lake.

Mchana wa Siku Ya Jumamosi.

Alipokuwa kwenye mizunguko yake. Alikuwa ameenda kupeleka vitambaa na maua ya urembo kwenye ukumbi, vikiwa vimekodishwa, na yeye amevurugikiwa kabisa, akaona ampigie simu Jema. Alishatoka kazini tokea saa sita mchana. Akawa nyumbani tu na JJ, James kama kawaida yake akili ilishahamia kwenye biashara. Akamuelezea akiwa njiani kurudi dukani kwake.

Jema akasikiliza mpaka mwisho. “Wewe unataka kufanya nini?” Akamuuliza akitaka kujua moyo wake ulipo, katikati ya wanaume hao wawili. “Nimeshindwa hata kuweka kitu mdomoni tokea yule mama aniambie Colins ni mgonjwa! Nashindwa hata kufikiria Jema! Na leo ni siku yangu nakua busy sana. Lakini nimekua kama nimepoteza dira kabisa! Ni Colins! Huwezi jua yule mzee alikuwa akija pale kumbe kutaka kuniambia lakini anashindwa! Pengine hali yake sio nzuri! Nina wasiwasi mpaka tumbo la hedhi limenianza.”

“Pole. Sasa unakumbuka nilikwambia lazima uanze kuomba?” “Hata sijui naanzia wapi, Jema!” “Mwambie Mungu upo njia panda. Kwanza ukiwa ndio umekubali tu kuwa na Ezra. Yaani ndio kwa mara yako ya kwanza umemfungulia mlango mtu mwingine, halafu ndio unapata taarifa za Colins aliyekuwa amepotea karibu mwaka sasa.” “Hivyo tu!?”  Jelini hakuamini kama ni rahisi hivyo.

“Wala huhitaji maneno mengi kwa Mungu anayeijua mpaka kesho yako. Anachotaka usemezane naye tu, ili apate njia ya kuzungumza na wewe. Hata akikujibu, akileta majibu yake, uwe kwenye mkao wakupokea. Anza. Na uombee hata hiyo hali unayojisikia. Weka gari pembeni, pata muda wa kuomba. Mwenzio huwa naomba mpaka chooni. Pata muda sasahivi, omba kabla hujatingwa na kitu kingine, ukashindwa kuomba.” Jelini akajicheka ila kweli akaegesha gari, akaanza kuomba. Kuomba kwenyewe akawa anaongea kama alivyoambiwa na dada yake mpaka akamaliza ndipo akaondoa gari kurudi sasa dukani kwake.

Watafutaji Wasio Choka.

Connie akafikiria, akashindwa kuvumilia. Akatoka moja kwa moja mpaka anakofanyia biashara zake Jelini. Jelini hakutegemea, akabaki akimwangalia hapo dirishani. “Naomba tuzungumze Jelini. Tafadhali, na samahani kwa kukupotezea muda.” Alivyopoa huyo Connie, huwezi kumjibu vibaya, ni mpaka uwe mwehu.

Jelini akatoka. Wakasogea pembeni. “Najua wazazi wamekuudhi. Na mimi mama amenisimulia. Kwa hakika binafsi nimeumia, pole sana.” Jelini akabaki kimya akimtizama tu. “Unapofuatwa na baba, daktari, akisema Colins anaumwa, ujue ni kweli anaumwa.” “Mimi hajaniambia kama Colins anaumwa! Amekuwa akija hapa, hasemi kitu, kisha anaondoka bila hata salamu!” Connie akawa kama hajaelewa ila akaona aendelee.

 Anyways, pengine itakuwa anasumbuliwa na dhamira. Lakini Jelini, Coly nimgonjwa. Na kama ulishawahi kumpenda kama yeye anavyokupenda…” “Colins hanipendi mimi. Amemchagua Love, ndiye anayeishi naye. Labda kama na hilo hujaambiwa.”

“Mimi sijui kilichoendelea hapo kati. Maana kulikuwa na mvutano mkali, mimi nikaamua kuacha kabisa kwenda nyumbani, nitulize akili kwenye shule. Mara ya mwisho kuwasiliana na Colins, ni aliponipigia simu na kuniambia haya maneno.” Akamtolea simu yake na kumpa asome. Baada ya kusoma maneno yake mwenyewe aliyokuwa amemwambia Colins, kama ahadi au kiapo, akamuona amepoa kabisa. Akamrudishia simu.

“Sasa hayo maneno aliyarudia kwangu, kisha akaenda kuyaandika yeye mwenyewe, tena kwa mkono wake. Kama utagundua hapo hiyo ni picha. Alipiga picha pale alipokuwa ameandika. Mbaya zaidi, japokuwa pengine wewe hayo maneno yamepoteza maana kwako, lakini yamebaki moyoni kwa Colins. Hakika anakutafuta. Mpaka wakati mwingine inabidi kufungwa kamba asitoke. Maana anatoroka kwenda kukutafuta na yeye nguvu hana na akili yake ni kama haipo sawa!” Jelini alilia sana.

“Colins unayemfahamu wewe, si huyu anayekutafuta sasahivi. Ameisha kila kitu mpaka akili, lakini amebakiwa na hayo maneno yako tu. Anaishi kwa madawa ya usingizi ili asitoke nje kukutafuta ndio maana umeona mpaka baba ilibidi akutafute. Aliposhindwa ndio nafikiri mama akaja. Amerudi nyumbani akilia anasema tumeshachelewa. Wewe umeendelea na maisha yako.”

“Mimi nimekuja tu, japo wazazi wamekata tamaa. Nakusihi, kama ulimaanisha chochote ulichomwambia hii siku, basi tafadhali Jelini, hata kama umepata mwanaume mwingine, nakuomba, nipo chini ya miguu yako, nenda ukamuone Coly. Pengine itamtuliza, nakumfanya apoe. Sasahivi anafungiwa kama mgonjwa wa kichaa. Anaishi kwa madawa kitu ambacho akiendelea hivyo kwake si nzuri. Amedhoofu, hali, anaishi kwa dripu tu! Ana madonda ya miguu, kwa kutembea akikutafuta wewe. Hataki yaguswe hayo madonda mpaka awe amelala.” Jelini akazidi kulia. “Hata kama sisi umetukasirikia, basi muhurumie Coly. Ni hilo tu.”

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

MAMBO YANAENDELEA…

Ezra Naye Akiwa Ndio Amepata Tu Kiapo Cha Jelini Na Asubuhi Hiyo Kuweka Ombi Maalumu Akitaka Ndio Iwe Zawadi Pekee Kutoka Kwa Jelini Kwenye Maisha Yake, Na Connie Naye Amekuja Kudai KIAPO Cha Kaka Yake.

Je, Jelini Atasimamia Wapi?

Kwa Ezra Ambaye Hata Hajabahatika Kuambiwa Neno Nakupenda Au Colins Aliyelowa Mvua Ya Neno Hilo, Na Ndiye Aliyekuwa Akisubiriwa Na Msamaha Wake Mkononi.

USIPITWE NA MAZITO YA SIKU Hii Ya JUMAMOSI.

Ya Maamuzi Magumu.

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment