Akamjibu kwanza Ezra,
‘Nakuombea na tutazungumza vizuri kesho.’ Kisha
kwa Jelini. ‘Ezra ni mtu mzuri sana. Na uzuri, anahofu
ya Mungu. Nina uhakika hatakuumiza. Mpe nafasi. Na nakuombea.’ Akatuma
huo ujumbe wa pili kwa haraka, akazima kabisa simu na kuiweka pembeni
akimsubiria mumewe. Jelini aliposoma ujumbe kutoka kwa dada yake, wakabaki
akimtafakari Ezra. Kwa hakika alipata wakati mzuri mpaka akajishangaa. Kwa mara
ya kwanza akalala bila hata kumuwaza Colins.
Kesho Yake.
‘Nimeamka
salama, na ninafuraha nikitizamia jioni yangu na wewe.’ Jelini alipoamka,
akakutana na huo ujumbe. Ulitumwa saa 11 asubuhi. Akaangalia muda, ilikuwa saa
12:30 asubuhi. Akaamua kumjibu, ‘Na mimi nimeamka
salama, Ezra. Uwe na siku njema. Kazi njema. Naamini kukuona tena usiku.’ ‘Bila
kukosa.’ Jelini akacheka akilamba midomo yake kwa furaha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika mida ya saa
1:30 usiku, Ezra alikuwa akiegesha gari kazini kwa Jelini. Akamtumia ujumbe. ‘Sina nia ya kukuharakisha, ila nataka kukutaarifu kuwa
nimeshafika. Ukimaliza, muda wowote ule njoo garini. Nitakusubiria tu.’
Jelini aliposoma, mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi. Akashindwa kutulia
kabisa wakati alikuwa na wateja wengi. Akaaga na kutoka. Ezra hakutegemea
alipomuona akija garini, na yeye akatoka kumpokea.
“Vipi!? Naona
unawateja wengi bado! Hutakula vizuri.” “Leo naona kumevuta. Mpaka sasahivi
bado wanakuja. Nilitaka kukusalimia tu, kisha nirudi.” Ezra akacheka
akimwangalia. “Nimefurahi umekuja Ezra.” “Ninafuraha ya kukuona. Umependeza
sana.” “Nilikuwa busy sana leo. Nikizunguka mtaani. Nimemaliza mizunguko kwenye
mida ya saa nane. Nikarudi nyumbani kuoga na kubadili, kutoa jasho. Ili hata
tukikaa wakati wa kula nisikunukishe.” Ezra akacheka.
“Nisingejali. Ila
nimefurahi kukuona unafuraha. Basi nenda kaendelee na kazi, ukimaliza tuje
tuzungumze vizuri.” “Wewe ulikuwa na siku nzuri leo?” Na Jelini akauliza
kuonyesha kujali. “Sana.” Jelini akacheka. “Mbona ‘sana’ yako inanitia wivu?”
“Kwa kuwa wewe ndio umeisababisha. Nimefurahi umezungumza na mimi jana pamoja
na ujumbe wa asubuhi.” “Kweli Ezra?” “Kabisa. Yaani mpaka Junior amenigundua
kwenye simu, na kuniuliza kulikoni. Akaniambia hajanisikia na furaha kama ya leo
kwa muda mrefu. Nikamwambia Mungu amenipa kicheko. Sikutegemea kama ungenipokea
baada ya kuwa ukinikimbia.” Jelini alicheka sana, ila kwa aibu.
“Nilijua ulikuwa
ukinikimbia Jelini.” “Nilikuwa na wakati mbaya! Nilihitaji muda wa kupokea taarifa
fulani hivi, ambazo nilikuwa nikizikataa kwa muda mrefu. Sikutaka kujichanganya.
Nilitaka muda wa peke yangu ili nikifikia maamuzi fulani, niwe nina uhakika
nayo.” “Sasa umeshafikia hayo maamuzi?” Akatulia kidogo akifikiria, akamuona
amepoa.
“Tuingie kwenye gari
nikwambie kitu.” “Na kazini?” “Watakuwa sawa. Usiwe na wasiwasi.” “Sitaki
waharibu, unichukie!” “Hapana. Ni watu wazuri, sema nakuwepo tu kama kuvutia
wateja. Wengi wanapenda wakifika, wanikute mimi mwenyewe.” Wakaingia garini.
Jelini Ajifunua Kwa Ezra.
Alipokaa kitini
akaanza. “Acha nikwambie ukweli.” Akaanza Jelini. “Kwa mara ya kwanza kwenye
maisha yangu, nafikiri nilipenda. Nilishindwa kujizuia wala kujisaidia.
Mimi sikuwa mtoto wa nyumbani au kanisani, ila mshinda baa. Nikinywa na
washikaji, na klabu kwa sana tu.” Ezra akacheka akimsikiliza.
“Nakwambia ukweli.”
“Nakusikiliza.” “Lakini katika hangaika yangu yote, sikuwahi penda kama
nilivyompenda Colins, lakini tayari alikuwa kwenye mahusiano na msichana
mwingine ambaye ni kama mchana na usiku na mimi. Na uzuri wao wao,
huyo msichana alipendwa sana na wazazi wake Colins.”
“Nilimwambia Colins
kuwa nampenda, akanikataa akiniambia yupo kwenye mahusiano na huyo msichana.”
Ezra akabaki kimya, asiamini mtu kama Jelini anaweza kweli kutongoza mwanaume!
“Nikaumia sana, nikaja kupata mtu mwingine, nikaanza
naye mahusiano, lakini tukiwa katikati ya hayo mahusiano, Colins akarudi,
akanipa sababu za kunikataa kwa wakati ule, nikashindwa kumkubali tena, japo
nilikuwa nikimpenda, ila nilishakuwa na mwanaume mwingine, sikutaka kuwa
msaliti. Colins hakukata tamaa, akabaki akinisubiria mpaka iliposhindikana kule
nilikokuwa.” “Kwa nini kulishindikana huko ulikokuwa?” Akauliza akihofia
isijekuwa Jelini alimtafutia huyo jamaa sababu ili arudi kwa Colins. Jelini
akamsimulia mkasa wa mzee Kasa kwa kifupi tu. Ezra akashangaa sana.
“Katika kipindi hicho
kigumu cha maumivu ya usaliti, ndipo tukaanzana na Colins kwa kuwa alisimama na
mimi kunifariji. Lakini Ezra, hakuna tulilowahi panga na Colins, likafanikiwa hata
mara moja. Hata kutoka kwenda kula kitu pamoja au kunisindikiza hata
hospitalini! Hatukuwahi kufanikiwa. Ilikuwa ni kupanga na kuvunjika na mimi
nikiishia kuwa muhanga na yeye kurudi na sababu nzuri tu zenye mashiko.
Nilibaki nikisubiri pengine itakuja kuwa bora kwa sababu katikati ya
hayo mahusiano ambayo ni kama hatukuwa nayo, lakini kama yapo, yule
msichana akarudi kwa kupitia wazazi akitaka warudiane na Collins. Kwa hiyo
kukawa na shindikizo la wazazi. Hawanitaki mimi kabisa, wanataka Collins amuoe
huyo msichana.”
“Collins nilimpenda sana.
Hilo sitakudanganya. Ilikuwa ni ngumu, lakini kwa sababu moyoni nilimpenda
sana, nilikuwa na tumaini nikijua siku moja patatulia tu. Vurugu ikaongezeka,
maana ndio kipindi hichohicho yule msichana wake akapata taarifa za tabia zangu
mbaya au maisha mabaya niliyoishi nyuma na kuwaambia wazazi wa Colins.”
“Haiwezekani Jelini!” “Oooh yeah. Ilikuwa mbaya sana. Alinianika kwa
kadiri ya uwezo wake mpaka wazazi wenyewe wakakinahiwa.” Akamsimulia
mpaka kufuatwa na bibi, babu pamoja na wazazi wake nyumbani, na Colins kuishia
kuishi na Love.
“Lakini Ezra, moyo
wangu ulishindwa kabisa kumuachilia.” “Kwamba ulikuwa ukisubiri pengine
atarudi?!” “Kabisa. Yeye nilishajiandaa na kumsamehe kabisa. Miezi yote
hiyo nilikuwa nikimsubiri tu arudi, aniombe msamaha, huku akinipa sababu
nzuri, zenye mashiko kama kawaida yake, tuendelee. Ndio maana sikutaka
kujichanganya na mtu yeyote yule. Nilijiweka kwenye mkao wa kumpokea.
Nikabaki nikisubiri tu kama mjinga vile!” “Hapo nimekuelewa.” “Kweli?” “Kabisa.
Wala si ujinga. Najua nguvu ya kupenda kwa dhati na kwa uaminifu. Si ujinga.”
“Basi mimi nilijiona
mjinga. Maana kwa Kasa, nilishindwa kabisa kusamehe, ila Collins ambaye ninajua
anaishi na huyo mwanamke kama mke wake kabisa, eti nilibaki nikimsubiria.”
“Sasa ni nini kimebadilika?” “Nafikiri nimekubaliana na ukweli. Kwamba
ameondoka. Amemchagua Love. Na kwa ukimya huu karibia mwaka sasa, inamaana yake
yanakwenda sawa. Sina changu tena.” Ezra akawa kama anaswali, lakini
hajui aliulizaje.
Wakabaki garini
wametulia kimya, kila mmoja akiwaza lake. Akamgeukia Ezra kama aliyekumbuka
kitu. “Kwa hiyo sikuwa nikikukimbia wewe kama Ezra, nilikuwa nikijitenga na
kila mwanaume. Ili isitokee anarudi akanikuta katikati ya mahusiano
yeyote yale. Sijui kama umenielewa?” “Nafikiri nimeelewa.” Akajibu hivyo na
kutulia kama ambaye anatafuta jinsi ya kuzungumza jambo lake, ila anakwama.
“Kuna swali nataka
kukuuliza. Lakini sijui niliulizaje!” “Juu ya nini?” “Juu yako.” “Wewe uliza
tu. Maana mimi nafahamika sana. Hata nikikataa kukwambia ukweli, ukiamua,
haitakuchukua hata siku nyingi kupata habari zangu huko mtaani. Najulikana kwa
mengi mno. Kwa hiyo kuwa huru tu.” Ezra akamtizama na kusita.
“Naona tule tu.” “Ni
nini hicho unachokihofia kuniuliza? Nakuahidi hutaniudhi Ezra. Mwenzio sio
mwepesi wa hasira na sioni shida na maisha yangu. Yapo ambayo najua nilikosea,
lakini nafikiri ndiyo yamenifanya niwe hivi nilivyo leo, na siwezi
kubadili nyuma. Nilishaishi, basi. Atakayeweza kuwa na mimi kwa jumla yangu,
sawa. Atakayeshindwa, pia naelewa kabisa. Hainisumbui. Kwa hiyo kuwa tu na
amani. Niulize.” Ezra akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha.
“Kwa jinsi
ulivyompenda Colins, unafikiri utakuja kumfungulia moyo wako mwanaume
mwingine?” Jelini akafikiria na kutulia kabisa. “Naona kweli tule tu.” “Swali
limekua gumu?” Ezra akauliza. “Sikujua kama utaniuliza hivyo! Nilifikiri
utaniuliza juu ya maisha yangu.” “Hayo ni maisha yako ya baadaye pia, Jelini. Huwezi
kukwepa. Nyuma nipo kama wewe tu. Huwezi kubadili. Najua Mungu husamehe
na husahau. Wewe ndio upo kuvuna madhara ya makosa uliyokwisha samehewa.
Hapo huwezi kuepuka.” Jelini akatulia.
“Asante kwa chakula.
Napata harufu nzuri!” Akabadili mazungumzo kabisa. Ezra akajua, ila akawa
muugwana. Akatoa vyakula na vinywaji, wakaanza kula kimyakimya.
Shauku Ya Jelini Bado Ipo Japo Mazingira Yote Bado Yanamkatisha
Tamaa.
Wakati wakila kimya
kimya, mwenyewe akavunja ukimya. “Acha niwe mkweli Ezra. Maadamu tunazungumza,
acha tu nikwambie. Nina shauku ambayo siwezi nikaipuuza. Na sitaki
kukata tamaa.” “Shauku gani?” Ezra akauliza taratibu tu kama kawaida yake, akila.
“Kuja kupata mtu wangu. Mtu ambaye atakuwa radhi kunilipia garama kama
Colins alivyofanya kwa huyo mwanamke wake. Anipende mimi kama Jelini niliyebeba
historia mbaya. Lakini bado anibebe. Awe wangu tu. Anioe. Tuzae watoto. Najiona
naweza kuwa mke wa mtu atakayenipenda kama vile Jema. Sitaki kukata tamaa, japo
ni ngumu. Nimezungukwa na wanaume malaya, hawawezi kuishi na mwanamke mmoja tu.
Lakini sitaki kukata tamaa.”
“Na haitakiwi ukate
tamaa. Na si wanaume wote ni malaya. Niliomba usituweke kwenye kapu moja.
Inawezekana kujizungumzia mwenyewe naweza kusikika najitetea, lakini
naishi karibu sana na Junior. Na yeye anakazi nzuri tu, inayompa maisha mazuri.
Anazungukwa na warembo wazuri wakila namna. Kazini na kanisani. Lakini wote
tumekubali kusubiri mpaka ndoa. Japo Junior anaye mchumba wake, lakini
hamgusi mpaka ndoa. Si kwamba hana tamaa za mwili, lakini tumekubali
kusubiri, tukimuamini Mungu kwa wake bora.” Ezra akaendelea.
“Ni nini nataka
kukwambia, unachotamani si kitu cha ajabu sana. Mungu hana mtu mmoja au
mwanaume mmoja tu mwaminifu. Mungu ana watu wengi sana. Hata kama mimi
na Junior tukaanguka kesho, hatutafilisi mbingu. Kwa hiyo usikate tamaa.
Omba Mungu, subiri, weka malengo yasiyoyumbishwa na matukio, utapata
unachokitaka.” Jelini akavuta pumzi kwa nguvu, akiingiza ule ushauri moyoni kwa
upya, akaendelea kula.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakala mpaka
wakamaliza. “Acha nirudi kazini. Nikamalizie siku, nirudi nyumbani. Nashukuru
kwa chakula. Nimefurahia nyama choma.” “Karibu.” Akaitika hivyo na kubaki
akimtizama. Jelini akajikusanya, akafungua mlango, na kutoka. Ezra akabaki
amekaa kitini. Akamfuata.
“Ipo siku nitakujibu
swali lako.” “Nilijua umeamua kulikwepa.” “Hapana Ezra. Ila kwa sasa sina
jibu. Sikupanga kumpenda Colins kwa kiasi hiki. Ilitokea tu. Najipa uhuru wa
kuja kupenda tena. Sitaki kujifunga au kukata tamaa kama nilivyokwambia.
Inawezekana hakuwa andiko langu.” “Anaweza akaja andiko lako na usimpende!”
“Mimi si muhuni na wala si muongo, Ezra. Ninaweza nisiwe kama wasichana wa pale
kanisani. Ambao hawajapitia maisha kama yangu, lakini linapofika swala la mahusiano
ya kimapenzi, hapo nakuwa makini.” Akaendelea taratibu tu Ezra akimtizama
kupitia dirisha, akiwa amekaa ndani ya gari yake, yeye amesimama nje.
“Nina msururu wa
wanaume wananitongoza kila leo. Hata leo nimepata. Lakini siwezi kuwa karibu na
mtu ambaye sijamkubali na najua nia yake ni kunichezea tu. Na kwa
jinsi nilivyo, nikishampa mtu nafasi ya kuwa wangu, ujue moyo wangu umempenda.
Na nitampenda yeye tu, bila ya kumchanganya na yeyote yule au
kuruhusu hisia ambazo hubadilika, kuingilia mahusiano yetu. Nitasimama
naye katika kila hali, kwa kuwa atakuwa wangu.” Hapo kidogo Ezra
akaridhika.
“Ukiwa kitandani,
unataka kulala, nipigie ili nikutakie usiku mwema.” Jelini akaanza kucheka.
“Jana nililala vizuri.” “Hata mimi Ezra. Nilifurahia muda na wewe. Unautulivu
wa namna yako, hata sauti yako imetulia, ikanifanya nitulie kabisa.” Ezra
akaanza kucheka. “Kweli! Unamfanya mtu anatulia kabisa. Hata kama kuna uchungu,
mawazo mabaya, mtu akikusikiliza, anatulia.” “Sipigii kila msichana simu usiku,
bwana Jelini! Sizungumzi hivi na wasichana wengine! Ni wewe tu.” Jelini
akainama tu hapo mbele yake.
“Na ni kwa kuwa
nataka wewe utulie, uwe na furaha, ndio maana nakupa muda wangu.” Ezra
akaendelea akibembeleza asijue jinsi anavyomfariji Jelini. Akatoa tabasamu akanyanyua
uso na kumtizama. Macho yakagongana. “Nashukuru Ezra. Nitakupigia.” Wakaagana,
Jelini akarudi kwenye majukumu yake akiwa na hisia tofauti kabisa juu ya Ezra.
Msimamo wa Mama Jema.
Alipofika nyumbani,
akamsimulia mama yake yote, asijue na Jema alishamsimulia mama yao juu yake na
Ezra. Mama Jema alishampenda Ezra kwa mengi aliyoyasikia kupitia Jema. Jinsi anavyompenda
Jelini na kumtaka vile alivyo. Maana Jema alimwambia mama yake, ilimbidi
amsimulie Ezra ukweli juu ya Jelini, ili asije mfuata kisha baadaye kukiwa
kumenoga, kuja kujua ukweli halafu akamuumiza tena mdogo wake. Jema alimwambia
mama yake, alishamueleza kwa kifupi ila ukweli wote juu ya Jelini, na bado Ezra
kumuhakikishia Jema, kuwa yeye anajiona ndiye mume wa Jelini. Hilo likamfurahisha
sana mama Jema.
“Sasa hao ndio wanaume. Wanakuacha na kicheko
sio unalala na huzuni muda wote! Mipango mingi. Maneno mengi
ambayo hayajawahi timia! Hekaheka mchana mpaka usiku! Mwishoe kuja kuitwa wachawi
nyumbani kwetu.” Hilo mama Jema alishindwa samehe kabisa. Kuitwa mchawi! Tena
nyumbani kwake, mbele ya wanae na mjukuu! Hakutaka hata kuwasikia hao wazazi wa
Colins, na Colins mwenyewe. Na James alijua jinsi alivyoumia. Na yeye akaacha
kuzungumzia mambo ya Colins kabisa mbele ya familia hiyo, japo alikuwa
akimkumbuka sana Colins. Akazungumza kidogo na mama yake, akawahi kitandani
akijua Ezra anamsubiria.
Aluta Kontinua.
Alipojiweka tu kitandani, akampigia. “Nilidhani ungenisahau!” “Sina mtu wakumfikiria sasahivi,
mbali na familia yangu, ndio umeongezeka na wewe, Ezra. Siwezi kukusahau.”
Ezra alijisikia vizuri sana. “Halafu umenijali.
Umeniletea chakula kizuri, tumekaa wote. Nimefurahi, asante.” “Nimefurahi kama na wewe umefurahia. Ila unajijua kama wewe
ni rahisi sana kukufurahisha, Jelini?” Jelini akacheka.
“Ni tofauti
na muonekano wako kabisa. Mtu akikuangalia kwa haraka, anaweza dhania matunzo
yako ni ya kufilisi benki.” Jelini alicheka sana. “Kabisa. Lakini
unatukuza vikitu vidogo sana, unavyopewa.” “Basi mimi siangalii thamani ya kitu, ila kunifikiria na
kunitendea. Kama kukumbuka swala la mziki niliopenda. Kisha kuacha shuguli zako
zote na kunitafutia hizo nyimbo na kuniletea! Kwangu si jambo dogo Ezra. Au
kuacha shuguli zako na kuja kula na mimi, tena garini tu! Ukiwa umetoka kazini,
pengine ungependa kupumzika. Kwangu si jambo dogo hata kidogo. Ndio maana
nimeona ile asante ya pale haitoshi, nikuandikie ujumbe kabisa.” Ezra
akacheka akimfikiria. Maana baada ya kushuka garini kwake baada ya kula pamoja,
akiwa nyumbani kwake, ujumbe wa shukurani ukaingia kwenye simu yake, kutoka kwa
Jelini.
“Pumzika
Ezra. Tutazungumza kesho.” “Naomba na kesho tufanye kama leo. Tule pamoja.”
“Utanichoka bure! Wewe kula tu, Ezra. Mwenzio naagiza chakula palepale,
nakula.” “Nahisi mimi ndio nahitaji muda na wewe, Jelini. Nafurahia tukiwa
wote.” “Kweli Ezra?” “Sina sababu ya kukufuata kwa kiasi hicho kama si kutaka
kwangu. Ningekuwa sehemu nyingine au hata kwa Junior, mpaka muda wangu wa
kulala ufike.” “Lakini kweli!” Ikawa kama imemu hit Jelini akilini. Akakubaliana naye.
“Ndio ujue nataka kuwa
karibu na wewe.” Jelini akatulia akifikiria. “Mbona
kimya?” “Nina maswali mengi juu yako, Ezra.” “Kama hayana haraka, nakuahidi
kukujibu ijumaa. Naamini tutapata wakati mzuri. Katikati ya juma nataka
tukikutana, iwe kupumzika baada ya majukumu yetu ya siku, basi. Labda iwe
unataka majibu kwa haraka.” “Nitasubiri.” “Basi
lala, nitakuona kesho.” “Nashukuru Ezra. Usiku mwema.” “Na wewe.”
Wakacheka na kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hiyo kukutana kwa
chakula cha usiku ikaendelea kama jumbe za asubuhi za kutakiana siku njema,
kisha usiku wakati wa kulala pia walikuwa kwenye simu pamoja. Ezra alijitahidi
kuleta vyakula tofauti tofauti, ilimradi tu kumfurahisha Jelini. Wanaingia
kwenye gari, wanakula wakielezana siku zao zilivyokuwa. Vituko vya siku hiyo.
Basi watacheka, kisha Jelini kurudi kuendelea na kazi, na yeye Ezra kuondoka
akienda kusubiria simu ya usiku mwema kutoka kwa Jelini.
Na akaongeza safari
ya mchana pia. Yaani muda wa chakula cha mchana kazini, yeye hali, anawahi kumpelekea
Jelini popote alipo muda huo, maji na matunda. Ilimradi kuonyesha kumjali huyo
Jelini.
Siku Moja Kabla ya Kutoka kwao.
Siku ya alhamisi
wakati wakilala, kabla hawajaagana, Jelini akaita. “Ezra?”
“Nipo.” “Naomba nikuombe na uniahidi utafanya.” “Sawa. Niambie.” “Ikitokea
dharula yeyote ile kesho. Ukashindwa kuja au itakayosababishia tusitoke,
tafadhali kabla ya saa 11 jioni, nijulishe.” Ezra akawa haamini kama
bado Jelini haamini jinsi anavyojisikia ni kama ameokota alumasi kuwa naye.
“Dharula
itakayonipelekea nikose kuwa na wewe kesho, ni kifo.” “Acha kusema hivyo,
bwana! Mambo yanatokea.” “Kesho usiku nitakua na wewe, Jelini. Kama si
kwenye chakula cha usiku, basi tutakuwa pamoja huko kutakaponilazimu
tusiende kwa chakula cha usiku. Nikimaanisha itabadilika mazingira tu. Ila tutakuwa
pamoja.”
Jelini akacheka akifikiria.
“Ikitokea
unapata mgonjwa wa gafla?” Jelini akauliza akitaka uhakika. “Nitakuja
kukuchukua twende wote kwa huyo mgonjwa, kisha tuendelee na yetu.”
Jelini akafurahi huyo, akabaki akicheka. “Kesho usiku
ni usiku wetu. Tuombe Mungu iwe sehemu ya chakula, vinginevyo tutakuwa wote
popote itakapotulazimu.” “Asante Ezra. Nashukuru.” “Na mimi nakushukuru
kukubali kuwa na mimi. Pumzika, tutazungumza kesho.” Ezra akaomba kwa
kifupi. Akamuombea Jelini usingizi mzuri, ulinzi wa kiMungu juu yake, biashara
zake. Akaomba kila anachofanya afanikiwe na kuombea siku yao ya kesho. Wakaagana
Jelini asiamini kilichomtokea. “Hapa kama ni karata, basi Jelini safari hii
umelamba dume.” Akajiambia akicheka mwenyewe hapo kitandani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa Jelini&Ezra Vinazidi Kunoga.
Ni Nini Kitaendelea KWAO! Je,
wao watafanikiwa kutoka.
USIPITWE.
0 Comments:
Post a Comment