Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 13 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 13

 Mtaka Cha Mvunguni, Shariti Uiname. Siku ya jumapili baada ya ibada, na kupata muda na familia wa chakula cha pamoja, wachaga hao akili zikahamia kwenye kusaka pesa, kasoro Jema na watoto ndio wakarudi nyumbani. Sasa Jelini akiwa kwenye duka lake akashitukia mama Colins amesimama dukani. Akamsalimia, akaitika na kuanza kuagiza vitu. Jelini akamuacha Fiona ndio amuhudumie, yeye kimya anaendelea na mambo mengine. Mara Ezra akafika hapo na yeye.

Akampungia mkono. Jelini alifurahi! Kwa hakika hakutegemea kuja kumuona tena hapo dukani kwao kwa jinsi ilivyoishia vibaya mara ya mwisho alipomletea chakula. Maana hata kanisani siku hiyo hawakusalimiana. Akajikuta akicheka na kutoka kabisa getini kumfuata nje ambako na mama Colins alikuwepo upande huohuo ila wakajivuta karibu na alikoegesha gari yake.

“Kwamba umeshabadilisha nguo kabisa!” “Nilisharudi nyumbani, nikapumzika, ndio nikaona nikuletee hii CD. Nakumbuka jana pale ukumbini, ulisema ulipenda sana nyimbo zake.” Jelini akashangaa sana. “Ezra! Kwamba ulikuwa ukinisikiliza na ukakumbuka!?” “Kabisa. Siwezi kukupuuza.” Ikamgusa Jelini, hakutegemea. Akamwangalia kwa mshangao usoni lakini uliojaa shukurani. “Nashukuru kujali. Naanza kuziweka hapahapa dukani. Iwe ikiimba kila wakati.” Akabaki akiangalia ile CD, akamuona anacheka.

“Jelini bwana! Sasa unacheka nini?” “Nimefurahi, asante.” “Karibu. Na leo utakaa kazini mpaka usiku sana?” “Hapana. Jumapili huwa tunafunga mapema. Kwa nini?” Akamuona anasita. “Niambie tu Ezra!” Akamsihi kwa kubembeleza kidogo. “Ungependa baada ya kazi twende tukapate icecream?” Mpaka akasisimkwa. Akajikuta akijibu. “Ningependa Ezra. Nimekua busy, sijapata muda wa kukaa chini hata kufanya mambo madogo kama hayo. Nashukuru pia kwa ofa.” Ezra alifurahi, asiamini.

Ukweli Jelini alionekana kufunguka kwake tofauti na mwanzoni. Akajipongeza kwa juhudi zake za kuinama, afikie cha uvunguni. “Usijali. Jiandae kupumzika na kupata icecream nzuri.” “Nashukuru.” Hakutaka kumpotezea muda zaidi, akaaga na kuingia kwenye usafiri wake wa haja! Gari nzuri sana ya kisasa, ikatangaza ipo neema kwa Ezra. Akaondoka akamuacha Jelini hapo nje baada ya kumpungia mkono. Wote wakionekana na furaha.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati anarudi ndani, mama Colins naye akaondoka bila ya kusema kitu ila kwa hakika alifanya manunuzi ya haja. Alitoka hapo na mifuko kibao! Jelini akajiuliza bila yakupata jibu. “Hawa watu vipi!?” Akazidi kuwaza ila safari hii hakumwambia mama yake. Ile huzuni ya kuona wamemkataa asiwe na kijana wao, siku hiyo ikapoozwa na furaha ya kutolewa na Ezra.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kadiri masaa yalipokuwa yakisogea, wasiwasi ukaanza kumwingia na kumuibia furaha yote ya kutoka. Alitamani arudi nyumbani aoge, ajitengeneza kama alivyokuwa akijiandaa alipokuwa akiambiwa na Colins watatoka. Lakini! “Historia isije jirudia.” Akawaza na kupoa kabisa. Furaha ikamuisha kabisa, akabaki na wasiwasi wa Ezra asije aka mcollins. Akanyongea kabisa.

Ilipofika majira ya saa moja, akimalizia mahesabu, wanakaribia kufunga na Fiona alishaondoka tangia saa 11 jioni, alibakiwa na Chalii tu, akamuona Ezra. Hakutegemea. “Umekuja?!” Ezra akawa kama hajaelewa lile swali la mshangao. “Nimewahi sana nini?” “Hapana. Sikutegemea kama ungerudi! Nisubiri, nakuja sasahivi.” Kwa hakika akawa amemchanganya Ezra mpaka kutoelewa kama ni amewahi au amekuja siku isiyo yenyewe. Ila kule kuambia anatoka baada ya muda mfupi, kukamtuliza.

Baada ya muda Jelini akatoka na pochi yake, akamkuta akimsubiria nje ya gari. “Sehemu niliyofikiria twende, sio mbali na hapa. Ni sawa tukiondoka na gari yangu, kisha nitakurudisha hapa uchukue gari yako ndipo urudi nyumbani?” “Sawa.” Akamfungulia mlango, akaingia, akamfungia mlango na kurudi upande wa dereva.

Alionekana alijiandaa na hiyo safari. Maana alibadili nguo kabisa. Akavaa mavazi ya kutoka, ila casual simple. Alionekana ni kijana anayejijali. Aliweza kupata harufu nzuri, marashi ya kiume. Jelini akajishuku. “Na mimi nilitamani kurudi nyumbani angalau nioge na kubadili, lakini sikuwa na uhakika kama ungerudi.” Ezra akawa bado hajampata vizuri.

“Kwamba ningevunja miahadi yetu, au sijaelewa vizuri?” “Mipango hubadilika!” Ezra akaguna na kumtizama maana hata ile zungumza yake ilibeba simanzi kidogo. “Labda isiwe na mimi, Jelini. Siwezi kupanga kitu na wewe nikagairisha tu. Na huwa sipangi kitu ambacho sina uhakika kama nitafanya.” Jelini akatulia tu.

“Au nimekupa dalili zozote za kukuonyesha mimi ni mbambaishaji?” “Hapana Ezra. Imekua kinyume na ndio maana umeona nimekubali kutoka na wewe. Nafikiria ni kujishuku tu. Nilihofia unaweza pata dharula ukashindwa kurudi.” “Nafikiri kama kungetokea dharula ingine, basi wewe ndio ungekuwa dharula yangu ya kwanza.” Jelini akacheka kwa kuridhika, na kunyamaza. Ila hilo lilibeba maana kubwa sana masikioni kwa Jelini, yeye asijue tu. Akalitunza moyoni na kuzidi kuvutiwa naye. Ezra akawa muungwana, mara yake ya kwanza kutoka naye, hakutaka kumkera na maswali mengi.

“Sasa wewe siku yako ya kupumzika ni lini kama unafanya kazi mpaka jumapili?” Jelini akacheka akijifikiria. “Maisha yangu yote kutoa miezi inayokaribia na nane sasa, yalikuwa ni kupumzika tu. Kula, kunywa na kulala tu. Haya maisha ya kazi hivi, nimeanza hata mwaka haujaisha.” Ezra akacheka na kumtizama huku akiendesha. “Usiniambie ndio ulikuwa ukila bata kwa kiasi hicho!” “Sio kitu kizuri bwana! Nimebadilika. Kwa hiyo sasahivi nimejikuta sina chakufanya. Nimebadili ratiba. Badala ya starehe, nafanya kazi. Ili nisijikute nimekaa tu, nikaanza kufikiria ujinga.” “Safi sana.” Akampongeza akicheka kama aliye na maswali mengi, ila kukusudia muda uje ujibu.

“Na wewe?” “Kwa sasa mimi ni mtu wa mshahara. Jumatatu mpaka ijumaa. Asubuhi mpaka jioni, basi. Baada ya mida hiyo nipo tu huru kufanya yangu, ndio utanikuta kanisani. Sina ratiba ngumu.” Jelini akatulia mpaka wakafika hiyo sehemu. Kweli hapakuwa mbali.

Wakaingia ndani kuagiza icecream wanazotaka, wakapewa na kurudi kutafuta sehemu ya kukaa.  Jelini akajisikia vizuri. Ezra akamuona akivuta pumzi mara kadhaa kama ambaye anajaribu kutulia, na kweli akatulia. Akawa akimwangalia kwa makini tu, huku akiendelea kula.

Akawa kama amekumbuka kitu. “Ezra!” Akamuita na kumuangalia, asijue huyo Ezra macho yako kwake muda wote. “Asante kurudi kunichukua, na kunitoa.” “Itabidi unisaidie Jelini. Nahisi kuna kitu hapo sielewi!” “Nilitamani kutoka kwa muda mrefu. Nikafanya majaribio mara kadhaa, ikashindikana. Tena nikiwa nimeshajiandaa kabisa. Nafikiri ikanitia hofu ya kutoka hivi na mtu mwingine, ikawa ni mpaka iwe na mama pamoja na Jema. Hata leo nilitaka nirudi nyumbani nikajiandae, lakini nikaogopa nisije nikajitia tena nuksi. Nikajiandaa halafu ukapatwa dharula, ukashindwa kutoka.” Ezra akakunja sura kidogo.

“Kwamba nikwambie tutoke, kisha nisitokee?!” Jelini akatulia kama anayefikiria. Kisha akaona afupishe. “Nilitaka kukwambia nimefurahi umekua mwaminifu, umesimamia hii miahadi, na tumetoka. Asante.” Ezra akawa haamini kusikia hivyo kutoka kwa mrembo Jelini. Ila akaanza kumsoma tofauti na muonekano wake. ‘Amejawa shukurani.’ Hilo ndilo likabaki kwa Ezra.

“Nafikiri mimi ndio natakiwa kukushukuru zaidi Jelini. Umekubali kutoka tena baada ya siku ndefu ya kazi. Mwenzio nilirudi nyumbani, nikapata mpaka muda wa mapumziko. Kwa hiyo nimefurahi umekubali kutoka. Naona mimi ndio natakiwa kukushukuru.” Jelini akacheka taratibu na kuendelea kula hiyo icecream.

“Nikuulize kitu Jelini?” Akamwangalia. “Huwa unapenda kutoka na kwenda kula wapi?” Jelini akacheka akifikiria. “Au nikurahisishie. Huwa unapenda vyakula gani?” “Nafikiri si vyakula pekee, ila ule wakati wakutoka na kufurahia kwa pamoja ndio huwa napenda zaidi. Nimekuona wewe sio mkorofi, mtu mzuri, ndio maana nimekubali kutoka na wewe. Mimi huwa sizoei mtu hovyo.” Ezra akacheka kama anayejaribu kuelewa.

“Hunifahamu kabisa Jelini! Na ulikataa ukaribu na mimi. Umejuaje kama si mkorofi na ni mtu mzuri? Maana nyakati nyingi tumekuwa tukikutana sehemu zinazolazimisha kuwa na haiba nzuri. Nikimaanisha ni rahisi nikaigiza.” Jelini akamkumbuka maneno ya shemeji yake yaliyofanana na hayo. Akacheka.

“Ni kweli Jelini.” “Unafikiri nakataa basi. Ila katika vitu nimeamini hapa duniani,  ni tabia huwa haijifichi. Popote anakofahamika mtu. Utakapomuulizia huyo mtu, utatambulishwa kwake kwa tabia zake. Na ikitokea kama ni mbaya. Au uliishi hilo eneo ukiwa na tabia hizo mbaya, kisha mtu akaenda kukuulizia hapo, atatambulishwa Jelini mwenye zile sifa. Utasikia, ‘unamzungumzia Jelini yule,…’ hapo zinatajwa zile sifa zako zote mbaya. Ila kwako imekua tofauti Ezra. Watu wanakusifia kuwa ni muungwana na unajua kujishusha.” Ezra akacheka akifikiria.

“Nimeambiwa pia huwa hupendi kumuudhi mtu.” “Jelini!” “Wewe umeniambia nijichanganye pale kanisani. Biashara matangazo. Sasa?” Ezra akacheka sana. “Watu wanaongea.” “Ni kweli.” “Sasa unatakiwa kushukuru. Upoje Ezra?” “Si kwa kiburi, lakini sikutegemea! Najua nabii hana heshima nyumbani kwao. Na mimi pale kanisani ni kama nyumbani. Sikutegemea kusikia mtu akinisema vizuri!” “Na hilo ndilo limenipelekea kukuamini. Nilijua si taarifa za uongo. Kwa sababu zingekuwa mbaya, wangesema tu. Hawakuwa na sababu ya kukusema vizuri kama ni mbaya.” Ezra akacheka na kutulia.

Kisha akamchokoza. “Sasa kwa sababu umeshasikia mimi ni mtoto mzuri, kwa hiyo hata nikikuomba tutoke tena kwa chakula cha usiku si utakubali?” Jelini alicheka sana. Hakutegemea. “Ezra!” “Nitafanyaje na mimi nishasifiwa? Au nimewahi sana?” “Ulitaka tutoke lini na twende wapi?” “Hii nitataka uchague wewe, na nataka upate muda wa kujiandaa kabisa, ukijua wewe utakuwa dharula ya kwanza kwangu. Nilazima nitakuja kukuchukua. Kwa hiyo upendeze kwa kadiri ya upendavyo, tutoke.” Jelini akajikuta akifurahia.

“Kweli Ezra?” “Sina sababu ya kukudanganya. Na mimi napenda muda na wewe.” Hivyo alivyozungumza vizuri, Jelini akamtizama na kuangalia chini, akabaki akifikiria. Ezra akabaki na maswali. Jelini aliyemfuata mwanzo, alikuwa mgumu sana kwake. Lakini Jelini huyu anaonyesha ni kama ni bahati kuwa naye! Hilo likamshangaza kidogo na kubaki akimtafakari akimwangalia vile alivyoinamia icecream yake.

Akajikuta amejisahau. Akimwangalia kiumbe cha ajabu mbele yake. Kwa hakika moyo wake ulifurahia kupokea macho yanachochukua. Akavuta pumzi kwa nguvu akimtizama. Yaani pale amekaa tu mbele yake, alivutia. Ezra alitamani azungumze kitu, akazuia maneno yake asije haribu.

Ila akamuita taratibu. “Jelini!” “Abee!” Akamtizama kike haswa, kiasi chakumlainisha Ezra vilivyo. “Tunakwenda wapi kwa chakula cha pamoja?” “Ni sawa nikifikiria kisha nikujulishe kabla ya siku yenyewe?” “Ambayo ni lini?” “Najua mpo mwishoni kwenye maandalizi ya harusi. Sitaki kukuingilia.” “Tafadhali niingilie tu.” “Ezra!” “Mimi nakupa ruksa. Panga, kisha nijulishe. Kama itashindikana, nitakwambia, tubadili muda pamoja. Ila tafadhali hii harusi isitufanye tushindwe kutoka. Kwanza harusi si yetu, ni ya upande wa bwana harusi. Sisi ni kama tulimaliza yetu siku ya jumamosi. Kwa hiyo muda nilio nao, unaweza kuupangia utakavyo.” Jelini akamtizama vile alivyokuwa akizungumza naye kwa upendo! Akajisikia kutulia kabisa.

“Ulifikiria lini?” Akamuuliza kama kumrahisishia. “Ijumaa kwangu sio siku ngumu kama jumamosi.” “Muda gani mzuri?” Ezra akauliza bila ya kulazia damu. “Nilikuwa nikifikiria kuanzia saa moja usiku. Lakini na wewe pendekeza muda.” “Ijumaa, saa moja usiku.” Ndio akawa na yeye amependekeza hivyo. Jelini hakuamini. Akabaki akimtizama.

“Ujiandae, nitakuja kukuchukua popote utakapotaka.” “Ila tafadhali sana Ezra. Ikitokea unapatwa na dharula, nijulishe kabla ya huo muda. Ikiwa mapema zaidi nitashukuru ili nisi…” “Jelini, naitizamia hiyo ijumaa kwa hamu sana. Hakuna jinsi nikagairi. Labda uzima wangu.” Jelini akatulia.

“Sawa?” “Acha muda uje ujibu Ezra. Ahadi za maneno naona moyo umeingiwa hofu, ngumu kuamini mpaka vitendo. Ila jua na mimi naitizamia sana hiyo siku. Na ujue nitapendeza.” Ezra akacheka. “Zaidi ya hivyo!?” “Acha masihara Ezra. Mwenzio napenda kupendeza. Nivae vizuri, nijitengeneza ndio naona raha.” “Ndio maana sijawahi kukuona hovyo hata mara moja!” “Nawekeza kwenye muonekano wangu, na sina uvivu. Hivi leo ni kwakuwa sikuwa na uhakika tu. Ila ingekuwa ni wakati ule, ningesharudi nyumbani, nikaoga na kujitengeneza kwa ajili ya kuja tu kula icecream. Nilimiss kutoka!” Hapo akaongea kinyonge kidogo.

“Basi itabidi tufanye juhudi za makusudi tuwe tunatoka mara kwa mara.” Jelini akacheka na kutulia. “Mbona hujajibu?” “Nimekwambia nimeingiwa hofu na ahadi, Ezra. Acha tufanye moja baada ya jingine.” “Nini kilikuogopesha?” “Nitakuja kukwambia wakati mwingine kama tutafanikiwa. Kwa sasa naomba tufurahie hii icecream tu.” Ezra akawa muungwana, akatulia.

Hawakuwa wamezoeana sana, na hawakutaka kuvuka mipaka. Kila mmoja akawa anajiwinda na neno lake. Ila utulivu wa aina yake. Baadaye wakaanza kuzungumzia mambo ya pale kanisani. Watu wanao wafahamu. Kidogo wakapata kitu cha kuzungumza mpaka wakamaliza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati wapo njiani akimrudisha kwenye gari yake, Ezra akaanza. “Nikiomba namba ya simu kwa mawasiliano, nitaharibu?” “Hapana Ezra. Ni sawa.” Hapohapo akamtolea simu yake na kumkabidhi. Jelini akajua ndio anatakiwa kuandika namba. Akaweka namba yake na kuandika, ‘Jelini’. Kisha akamrudishia. Akashukuru na kuweka pembeni, akiendelea kuendesha mpaka akamfikisha nje ya duka lake.

“Nashukuru Ezra. Nimepata wakati mzuri. Nimefurahi.” Ezra akacheka akimtizama. Jelini akainama akiwa bado amekaa kitini. “Naona unashukuru kwa kitu kidogo sana Jelini! Mbona ulishashukuru. Au umesahau?” “Nakumbuka.” “Na unakumbuka kukwambia mimi ndio nimefurahia zaidi?” Akatingisha kichwa kukubali na tabasamu. Ezra alijaa vizuri ndani ya hilo gari, kiume. Akavutia. Kadiri Jelini alivyojishusha, ikamuongezea ujasiri yeye kama mtoto wa kiume, maana Jelini anatisha. Ni wa viwango, inahitaji moyo kumtongoza. Ila usiku huo baada ya kuwa naye, ikamfanya Ezra amfikirie tofauti.

“Kwa hakika nimefurahia muda wetu, na ninatizamia siku yetu ya ijumaa. Na mimi ujue nitapendeza.” Jelini akaanza kucheka. “Sitaki kukuangusha.” “Huwezi. Wewe wakati wote ni msafi, Ezra. Sijawahi kukuona ukijikosea.” Ezra akacheka sana. “Kweli. Unajijulia. Halafu mtulivu mpaka usoni. Unazungumza taratibu, huna haraka. Pale kanisani wanakuigilizia unavyozungumza.” Ezra alicheka sana, asiamini.

“Haiwezekani Jelini! Nani huyo?” “Wewe usiulize sana. Ila ujue watu wanakuangalia sana. Na wanakusifia.” “Basi itabidi niongeze nidhamu.” Wakazungumza kidogo, Jelini akashuka asiamini baada ya muda mrefu sana wa upweke, usiku huo hatimaye amepata muda mzuri hivyo na Ezra.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

  Wakati anakaribia kulala, ujumbe ukaingia. ‘Uwe na usiku mwema. Ezra.’ Akacheka akirudia kusoma, kisha akajibu. ‘Asante. Na wewe ulale unono.’ Akatuma huo ujumbe na kuongeza. ‘Na asante kwa namba pia. Niliogopa kujichukulia.’ ‘Karibu. Lakini nijisingejali kama ungechukua. Ingenifurahisha zaidi kuona na wewe unataka mawasiliano na mimi, kuliko kulazimishia.’ Ezra akamjibu kwa haraka tu. ‘Tafadhali usione kama unalazimishia.’ ‘Sitaki kuharibu kama mwanzo.’ Akamchokonoa kidogo kujua anaposimama.

‘Sikuwa nikikufahamu Ezra. Niliogopa nisiharakishe nikajiumiza tena. Nimezungukwa na mianzo mizuri, lakini hakunaga muendelezo. Nabakia kuumia na kusubiria bila kikomo. Moyo wangu umechoka, nafikiri nikaongeza kujiwinda.’ ‘Pole. Lakini mimi nina mwanzo na mwisho wangu hautakuwa wa maumivu.’ Jelini akasoma, na kushindwa kujibu. Akajihisi machozi kumtoka. Akamkumbuka Colins.

‘Nakuahidi Jelini.’ Ezra akaongeza. ‘Tafadhali acha muda ujibu Ezra. Tutembee hatua kwa hatua. Ahadi zinaniogopesha kwa sasa.’ ‘Sawa.’ Akajibu hivyo na kuongeza. We are equal, but not same. Nikimaanisha wanaume wote tunaweza kufanana, lakini haina maana tunatenda sawasawa. Tunatofautiana. Tafadhali usituweke wote kwenye kikapu kimoja. Utanipunja nafasi ya kutenda yale ninayotamani kwako, nikihofia utanifananisha na waliotangulia. Au kuhofia hutaniamini. Nataka ujue, nina maanisha kila neno nitakalokwambia. Na nakuahidi, nitasimamia maneno yangu kwako, kwa garama yeyote ile.’ Jelini aliposoma, akajibu kwa haraka.

‘Na hiyo nimesikia ni moja ya sifa zako. Kwamba ukiahidi jambo, unatenda hata kama itakugarimu wewe. Na hiyo nimesikia akisema mama mchungaji wakati wakikusema kwenye kamati ya kitchen party. Walikuwa wakisema yule msimamizi wa ule ukumbi ni mkorofi sana. Mmoja wao akawa na wasiwasi unaweza ukakimbia jukumu la kusimamia ule ukumbi siku ya kitchen Party ukijitoa kwa ukorofi wake na kusema kwanza ni ya wanawake. Ndio mama mchungaji akasema, hata iweje, maadamu uliahidi kufanya, eti utafanya kwa garama yeyote ile mpaka ikamilike. Akasema anakufahamu upo hivyo tokea kijana mdogo sana na mpaka sasa katika hilo hujabadilika. Akawa anawaambia katika hilo lisiwasumbue kabisa, wakuachie tu.’ Hilo likamshangaza sana Ezra, hakutegemea.

‘Waw! Ametukuza mimi na Junior yule kijana wake mkubwa.’ ‘Alisema yeye ni kama mama yako wa pili. Ndio maana nimepata ujasiri kwako Ezra. Isingekuwa hivyo, ingekuwa ngumu.’ ‘Nashukuru kwa kuchukua hiyo hatua ya kwanza, naomba nikuombe hatua ya pili.’ ‘Ipi?’ Jelini akauliza.

‘Ni sawa nikipiga?’ Jelini akajawa furaha, mpaka akajishangaa. ‘Ni sawa tu.’ Alipotuma tu huo ujumbe, Ezra akapiga. “Nashukuru kwa ruhusa ya kupiga. Sikujua masharti ya namba.” “Muda na wakati wowote ule. Nisipojibu ujue nina majukumu tu, ila nitarudisha simu yako.” “Kama ndio hivyo, nashukuru.” Wakatulia kidogo. Kisha akaendelea.

“Nilitaka kuomba hatua ya pili.” Jelini akacheka taratibu. “Naruhusiwa?” “Nakusikiliza.” “Basi ndio hicho ninachotaka kukuomba. Hatua ya pili, ni unisikie. Mimi kama Ezra, nisikie ninachokwambia mimi. Sio kile kilichozoeleka kusikika kwenye masikio yako. Inaweza ikawa ngumu, lakini tafadhali naomba na mimi unipe nafasi ya kunisikia.” Ikamgusa Jelini. “Nitajitahidi Ezra. Na wewe univumilie. Inaweza isiwe rahisi, au kwa haraka, lakini nakuahidi nitajitahidi.” “Nashukuru.” Wakatulia kama wanaoona uzito kuagana.

“Jelini?” Akavunja ukimya. “Nipo.” “Leo ni jumapili. Inamaana kuja kuonana tena ni mpaka ijumaa?” Ikawa kama anayelalamikia muda. Mbali. “Nilifikiria ndivyo tulivyokubaliana.” Akajibu Jelini kwa kubembeleza kama na yeye ameshapatwa hamu naye. “Naruhusiwa hata kupita kazini kukuona? Nakuahidi sitakuchukulia muda mrefu sana. Ni salamu tu. Au nitakuwa nikikubugudhi?” “Hapana Ezra. Ningependa kukuona. Tuwasiliane tu. Ili usije kuja pale nikawa nipo sehemu nyingine. Maana nakuwa nikizunguka sehemu zingine pia. Sikai tu pale.” “Uzuri nimepata baraka zako juu ya mawasiliano, basi tutakuwa tukiwasiliana ili tuwe tunapata muda wetu.” Jelini akacheka baada ya kusikia hivyo.

“Angalau niwe najua siku yako iliendaje. Si kwa simu. Nikuone kabisa. Maana kwa simu unaweza ukaniambia tu, upo sawa. Kumbe siku imekua na changamoto, ilikunyima raha.” “Si nitakusimulia kwa simu tu! Usihangaike.” Akajibu kwa deko. Ila asiamini. Maisha yalishamfanya ajione si kitu, hapo anaona bahati ya mtende. “Hapana. Simu itanipunja. Tukiwa pamoja hata kama kwa muda mfupi tu, ni tofauti na simu. Acha simu iwe ikilazimu. Au nazidisha? Ninawahi sana?” “Mimi nataka uzidishe.” Ezra alicheka sana, asiamini. “Jelini!” “Wewe zidisha tu. Ndio nitafurahi.” Ezra akaamini maneno ya Jema.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Maana ukimya wa Ezra, kumbe alikuwa akizungumza na Jema. Alimtafuta na kuzungumza naye kwa mapana juu ya Jelini. Ezra alimwambia jinsi alivyompenda Jelini. Na akamwambia anajiona yeye ndio mume bora kwake, wengine watamsumbua tu. Jema alicheka sana.

Kwa kuwa alishampenda Ezra, akamuibia siri nyingi sana juu ya Jelini. Akamwambia jinsi anavyopenda kupendwa, kubembelezwa na kufuatilizwa yeye tu. Hapo Ezra anamfahamu Colins vizuri tu. Hata mahusiano ya Colins na James, Jema alishamwambia. Na Jema ndiye aliyemwambia amchukulie taratibu sana mpaka amfungulie yeye mwenyewe mlango. Ila akamwambia akishafungua tu mlango mmoja, aingie kwa nguvu zote bila ya kuzembea. Full swing!

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Acha nikuache upumzike, Ezra. Najua kesho kazini.” “Basi chakula cha usiku, nitaleta, tuje tule wote kwenye gari ndipo urudi kazini.” Jelini akabaki kama na kigugumizi. “Muda gani huwa unakula, nije tule wote. Nitaleta mimi. Usihangaike.” “Si nitakuwa nikikusumbua sana!” “Kumbuka mwenzio ni mwajiriwa. Nikimaliza kumpa mwajiri muda wake, kesho sina kipindi kanisani, nakuwa sina lakufanya. Sasa kwa kuwa wewe upo na majukumu mpaka usiku mwingi, naomba nikupunguzie la chakula. Akili ifikirie tu kazi. Niambie muda unaotaka kula, nije tule wote.” “Asante kujali.” Ikamgusa Jelini, akajikuta akicheka.

“Eti nimefurahi!” “Kweli Jelini?” “Sana. Nashukuru kujali. Wewe ukipatwa njaa, njoo uje tule. Mimi sina muda maalumu.” “Muda gani unakuwa na wateja wengi sana?” “Kuanzia saa 11 jioni mpaka saa 1 usiku. Hapo panakuwa pamejaa sana pale dukani.” “Kumbe bora nimeuliza! Basi muda wetu wa chakula utakuwa saa mbili usiku. Au tutakuwa tunachelewa sana kula?” “Nimefurahi! Sasahivi siwezi kufikiria tena. Wewe njoo tu.” Ezra akacheka. “Nitakuona kesho Jelini. Ulale vizuri, na uamke na furaha hiyohiyo.” “Na wewe Ezra. Bye.” Ndipo wakafanikiwa kukata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ukweli Ezra Ameingia Full Swing! Mzima Mzima Bila Kulazia Damu.

Nini Kitaendelea Kati Ya Jelini & Ezra, Wanaoanzisha Jipya Huku

 Colins Akimsaka?

Usipitwe Na Muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment