Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 12 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 12

Huku kwa Jelini maisha ya upweke yaliendelea, kwa muda wote huo kimya, ila akitizamia kurudi kwa Colins. Alishamtafutia sababu zote ambazo atarudi nazo. Mpaka nzito zaidi, lakini alishajiambia akirudi, atamsamehe tu. Ikawa asubuhi, ikawa jioni. Siku, mwezi wa kwanza, wa pili, watatu, wanne, kufika wa tano akaanza kukata tamaa. Kadiri siku zilivyozidi kwenda, ukweli ukaendelea nafsini mwake kuwa Colins ameondoka, na ni wa Love, yeye anaendelea kujichelewesha tu.

Wakati huo ukweli ukiendelea kwenda ndipo na masikio yakazidi kusikia habari za vijana hao wawili. Ezra na Junior ambaye ni mtoto wa mchungaji wa hapo kanisani. Vijana waliojituma hapo kanisani bila kuchoka. Akiwa ndugu mtazamaji tu, mwenda kanisani siku za jumapili tu, akagundua ni kweli hao vijana wapo hapo na mabinti wanawahangaikia. Ikawa popote alipo hapo kanisani, hata akiwa chooni tu, basi atasikia wasichana wa hapo wakimsema Ezra kwa kuvutiwa naye.

Hata akiwa amesimama nje ya kanisa wakisubiriana au Jema akisalimia kina mama wa hapo kanisani, basi masikio yalisikia habari za Ezra hata kwa kina mama watu wazima wakimsifia amefanya hiki au kile, ilimradi akasikilizishwa. Au wakitumana kwake kuwa wakitaka jambo liende bila maswali na lisiharibike, basi iwe Ezra au Junior. Akaanza kumfikiria Ezra aliyekwisha mkataa na kumkwepa.

Ila akagundua warembo wanamsema zaidi yeye, sababu ni kama Junior alikuwa na mchumba anayejulikana mpaka kwa wazazi. Kwa hiyo akagundua anayewindwa zaidi na yupo ndotoni mwa warembo wa hapo, ni Ezra. Halafu sasa, kanisa lenyewe lilikuwa na warembo wanao jielewa, si wachovu au useme wamekosa soko. Kwa hiyo wanapomzungumzia mwanaume mmoja kwa kurudia rudia, lazima uweke umakini.

Kadiri siku zilivyozidi kwenda na majuma kukatika, upweke umeongezeka, akaanza sasa kama kijiwivu kwa Ezra huku akimnung’unikia nafsi mwake, hana wakumwambia. “Kwa hiyo alikuwa akinijaribisha tu!” Akajilalamisha kadiri siku zilivyozidi kwenda na Ezra kujifanya kana kwamba hawaoni kabisa. Hakukosea hata kuwasogelea.

Akabaki akitamani  hata wapishane hapo kanisani ili amsalimie, akumbuke na yeye bado yupo, lakini ikawa kama aliyejiapia, hatakosea kukutana nao hata kwenye kikapu cha kutoa sadaka. Hapakuhitaji maswali, hata wao wakaamini Ezra ameweka juhudi za makusudi kuwakwepa. Akiwaona mahali, basi hatapita hapo kabisa. Na hakurudi tena sehemu anayofanyia kazi Jelini.

Naye Jelini ikawa kama amepata mkosi, hapakutokea tena mwanaume wa kumtongoza kwa mahusiano ya maana. Si wa wazee kama kina Kasa wala vijana aina ya Ezra. Akapoa, na kuanza kujidharau maana waliobaki ni wale vijana waliokuwa wakivutiwa tu na umbile lake, wanataka tu kumtoa nguo, waone na kuonja vya ndani. Akapoa. Akijiona ashazeeka, si binti mdogo tena. Akakumbuka sababu za kukataliwa kwa kina Colins. Akaumia. Akabaki kujiambia, “Kwanza nishazeeka, nina mtoto. Vijana kama kina Ezra wanataka vibinti vidogo.” Akajikatia tamaa. Akaamua kutuliza akili kwenye biashara zake na mama yake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ikawa mchungaji anaozesha binti yake. Mdogo wake Junior waliyefuatana naye. Likawa jambo la wengi pale kanisani na watu kulibebea umaana. Maandalizi yakifahari yalishakuwa yakiendelea. Maana kanisa lenyewe kwenye ibada ya asubuhi ni ya wale waliosoma, halafu waswahili wanaoishi Bongo, lakini lugha yao na familia ni ya umombo. Basi hao walikuwa na ibada yao maalumu. Saa tatu asubuhi, mpaka saa nne na nusu. Hiyo iliendeshwa kwa wakati bila kupitisha hata dakika. Mchungaji aliwatengezezea muda wao na watoto wao. Wakitoka hao mida hiyo ndio wanakuja wenzetu na sisi wakina mama Jema.

Wao ibada yao ya kiswahili. Napo walitunziwa muda. Ila si kama hawa wa asubuhi. Na hawa wa ibada ya kwanza, wao ndio wale mchungaji akisema kuna mchango, wanataka kujua kiwango. Kikishatajwa, basi hiyo hela inakusanywa bila kutafutana. Kila mtu anatamka kiwango chake, ifikapo mwisho wa juma pesa hiyo inakua ilishafika kwenye akaunti za kanisa bila kigugumizi.

Sasa iliposikika harusi ya binti wa mchungaji, tena binti wa pekee, kila mtu alijitolea bila shida kufanikisha shuguli nzima. Na Jelini akapata tenda ya kukodisha kiti kikubwa cha kukalia maharusi pamoja na vitambaa. Ikawa anatakiwa nusu ya hiyo seti nzima kupeleka ukumbini siku ya kupamba kitchen party. Halafu kwenye sendoff akawa amekodishwa seti nzima ili sasa, wakae maharusi na wasimamizi wao pia. Jelini mpenda vizuri, alinunua hiyo seti kwa pesa nyingi sana, halafu nzuri mno. Akiiweka na rembo zake hapo jukwaani, hata kabla ya maua, panapendeza. Wenye uwezo huwa hukodisha vitu vyake.

Jumamosi.

Siku hiyo ilikuwa siku ya kitchen party. Ilikuwa ikifuatiwa na sendoff. Mida aliyokubaliana na mpambaji kufikisha vitambaa, hilo kochi na marembo yake hiyo sehemu ya kukalia, ukafika. Jelini akafika hapo ukumbini na kijana wake mmoja. Wakaanza kushusha vitu taratibu. Maana vingine vikishafika kwenye jukwaa ndipo unajengea sehemu ya kicho kiti ambacho kipo kama kochi hivi. Wakati wamebeba na huyo kijana, wanaingia ukumbini, akamuona Ezra ndani ya huo ukumbi kama na yeye anaweka sawa mambo fulani upande wa vinywaji.

Aliwaona wakati wakiingia, maana aliyekuwa naye, alikwenda walipokuwepo kina Jelini kutoa maelekezo. Akaelekeza sehemu waliyotaka bibi harusi na mpambe wake wakae. Jelini akauliza maswali wakati kijana wake akiendelea kuleta baadhi ya vitu vya kuunganisha kwenye hicho kiti/kochi. Kisha Jelini na yeye akatoka kama kusaidiana na kijana wake.

Wakati wakiendelea, kuingia na kutoka wakibebelezea vitu ndani Ezra akawasogelea karibu ya gari waliyokuja nayo. “Nashawishika kusaidia, lakini nahofia isije ikaleta picha ingine.” Jelini akamwangalia, moyo ukabadili mapigo yake. Amemuongelesha! Hakuamini, lakini alikuwa amemuelewa anachomaanisha. “Hamna shida. Kuwa tu na amani. Hata hivyo tunamalizia.” Japokuwa alitamani aseme ‘ndiyo’ kwa haraka sana, maana alishakua na majuto ya kumkataa kwa haraka wakati ule wa mwanzoni mwanzoni, akijua Colins atarudi. Lakini akaona amuwekee pozi. Ni Jelini! Na pia alimuigiliza usemi wake Ezra mwenyewe wa ‘kuwa tu na amani’. Akacheka taratibu na kuondoka kurudi ndani bila nyongeza. Jelini na kijana wake wakaendelea kusombelea mpaka wakamaliza.

Ikaanza sasa kazi ya kutengeneza hiyo sehemu ya kukalia hapo jukwaani. Ukumbi una joto, makubaliano ya A/C ni kuwashwa muda wa shuguli. Ulikuwa ukumbi mzuri sana, madirisha vioo tupu sababu ya A/C kitu kilichopelekea joto endapo A/C hiyo haijawashwa. Jelini mwenyewe alikuwa akitokwa na jasho anajifuta na mtandio. Kazi ikaendelea hapo ukumbini kila mtu akifanya lake ilimradi kumaliza kwa wakati. Halafu sasa na yeye Jelini wa mengi, biashara mtaani bado zinamsubiri. Akawa amekazana, awafungie kila kitu, awapishe wapambaji wamalizie, na yeye ahamie kwenye kusaka pesa kwengine.

Ezra akawasogelea tena pale jukwaani. “Mimi nipo upande wa vinywaji. Nagawa maji kwa kila mtu hapa ukumbini. Kama ukiangalia, utagundua kila mtu anachupa ya maji ya kunywa, niliyowagawia mimi. Sasa sijui na nyinyi hapa mngependa maji? Sitaki ilete picha ya hongo.” Jelini akajua bado anamanung’uniko juu yake. Hilo likamfurahisha kidogo kuwa bado hajamsahau. Maana angemsahau, asingekumbuka alichomwambia.

Ezra mwenyewe zungumza yake ya utulivu kweli. Hana papara. Hapo yupo kazini, lakini jinsi yeye Jelini alivyomuona, alimuona yupo vizuri. Akavutiwa naye. “Tunashukuru kutukumbuka na sisi. Naona Chalii ndio amelemewa zaidi.” “Bila shaka.” Akamkabidhi huyo kijana wake maji. “Na wewe?” “Kama yapo mengi na mimi ningeshukuru kama ningepata.” Akazungumza kwa sauti ya kujishusha, kama aliyejirudi. Akamkabidhi na kushukuru. Ezra akaondoka bila ya nyongeza. Akayanywa karibu yote, akaendelea na kazi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usiku kwenye mida ya saa tano Jelini akawa amerudi tena hapo ukumbini na gari ya mama yake aina ya pickup, kuchukua vitu vyake. Akamkuta Ezra na yeye amekaa nje pamoja na watu wengine kama ambao na wao wanasubiria kuisha kwa hiyo shuguli. Jelini alijua shuguli ingekuwa inakaribia kuisha. Hakutaka mtu ashike hivyo vitu vyake, kuhofia kuharibiwa. Kwa hiyo aliwahi kidogo kuhakikisha hachelewi kuhofia asije kuta amesaidiwa kutolewa hapo alipoviweka.

Akawasogelea pale walipokuwepo. Kama kawaida yake, hajikosei. Kutoka mida anaweka vile vitu hapo ukumbini mpaka mida hiyo, alisharudi nyumbani kuoga na ndipo kuendelea na shuguli nyingine. Kwa hiyo hata hapo alijiwakilisha vizuri kama kawaida yake.

“Nilijua na wewe ungekuwepo katika wahudhuriaji humo ndani?” Ezra akamdaka kwa hayo maneno. Jelini alifurahi huyo, akajisogeza karibu. Maana alikuwa hajui asimamie upande upi kwa hao aliowakuta hapo. “Bado hatujafahamiana hata na mama wa bibi harusi. Bado sisi ni wageni. Tenda yenyewe imekua kama bahati tu, nilimuomba Jema akamuonyeshe mama mchungaji picha, na kuomba kama watataka niwakodishe kwa bei nzuri, ndio naona kamati ikapenda, nikapewa kazi ya hicho kiti na vitambaa.” “Ila umeshakaa sana pale kanisani Jelini. Inabidi uanze kujichanganya. Wewe mfanyabiashara bwana. Na biashara matangazo.” Jelini akacheka. “Au kuna watu maalumu unawalenga?” “Hapana. Hilo lipo kwenye kulifanyia kazi.” Angalau usiku huo, wakazungumza kidogo.

Ikamtuliza Jelini kuona sio kwamba amemfungia vioo moja kwa moja. Na akajua wazi kujishusha kwake mchana, na kupokea maji kwa shukurani ndio kumemfanya azungumze naye tena usiku huo. Akafurahi na kuomba bahati kama hiyo ije ijurudie tena au hata arudi tena kazini kwake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lakini ikawa kimya. Hakumuona wala kumsikia tena. Hata siku ya jumapili, hakumuona kwa karibu ila kumuona kwa mbali akizungumza na kucheka na watu wengine. Akanyongea. “Mimi nilidhani ndio yameisha, jumapili angenitafuta hata anisalimie tu!” Akajilalamisha kwa uchungu nafsi mwake. Akasikia kunyongea na upweke kumzidia. Ikawa jumatatu, ikawa jumanne, kimya.

Jumatano.

Akiwa dukani kwake, ni kama akamuona baba Colins. Akashituka sana akihisi pengine amemfananisha, kisha akawa amepotea gafla. “Nilitaka kushangaa! Yule baba awe anatafuta nini kwangu!” Akawaza akiwa anaangaza macho kuhakiki kama sio yeye. Maana duka lao lilikuwa limetengwa na vyuma vya urembo lakini kama ulinzi kwamba wezi washindwe kuwaingilia ndani. Kwa hiyo mteja unaona kila kitu ndani. Ukichagua, unaonyeshwa au kupewa kwa kupitia dirisha ambalo si dogo sana, lakini si rahisi mtu kuingia.

Ijumaa.

Ikawa hivyohivyo siku ya ijumaa. Safari hii akamuona kabisa baba Colins. Ila safari hii ni kama akasogea kabisa karibu na duka, akasimama kwa muda kama anayejishauri. Akaangalia simu yake kidogo, Jelini akamuona anaondoka bila salamu. Hilo likamshangaza, asielewe.

Jumamosi.

Siku ya jumamosi ambayo alikuwa akiandaa hilo kochi au kiti kikubwa cha maharusi kwenye tafrija ya sendoff, akiwa anaweka kwenye gari na marembo yake, akamuona tena baba Colins ameegesha gari yake mbele yake. Akashuka garini kabisa, Jelini akajidai kama hajamuona. Akaendelea kusombelea vitu akiweka garini. Akasimama nje ya gari yake kama anayemsubiria kisha akamuona anaondoka tena bila salamu. Hakumsemesha ila Jelini akaogopa sana.

Akiwa njiani, akampigia simu mama yake. Akamuelezea kuanzia kumuona mara ya kwanza mpaka siku hiyo. “Nilivyomuona leo si kama anayekuja kwa shari!” “Sasa anataka nini kama si kutaka kunitibua tu?” Mama Jema akaanza kulipuka. Hataki na wanae! “Labda tuache tuone.” “Hakika iwe heri, lakini si kukubugudhi. Hapo tutaonana wabaya.” Akamtuliza mama yake kwa maneno mengi, wakacheka na kuagana.

Subira Yavuta Kheri.

Safari hii akakuta kama Ezra anamsubiria amsaidie. Akamchokoza. “Huogopi nitaona kama ni hongo?” Wakaanzia hapo utani, kila kitu wakawa wakitaniana ni ‘hongo’. Angalau ukaribu ukaanza. “Jambo haliishi Ezra jamani!?” “Ulinipiga stop mbaya! Mpaka wema ukaoza!” Wakataniana, mpaka wakamaliza, Jelini akazidi kuvutiwa na haiba ya Ezra. Alikuwa na furaha huyo. Ezra yupo naye akimsaidia! Kila mtu akawa wakiwaangalia wao jinsi wanavyocheka. Halafu ule ukaribu, wakusaidiwa na Ezra, kila mtu akaona jinsi anavyojituma hapo kwa Jelini. Mara maji ya kunywa, mara amsogozee hiki, ikawa ilimradi tu mpaka wakamaliza. Jelini mwenyewe alijua amejaliwa kwa namna yake.

Alipomaliza, akiwa anamsindikiza kurudi garini, Jelini akaanza. “Sasa leo na wewe si ni mualikwa?” “Sema mimi ni mualika.” “Acha masihara Ezra!” “Esta ni kadada kangu. Kama ungekuwa umepazoea kanisani na watu wake, ungegundua, yule mtoto mkubwa wa mchungaji ni rafiki yangu sana.” “Kumbe!” Akajifanya hafahamu sana mambo yake wakati alikuwa akimfuatilia sana tu. “Basi hongereni. Sasa mbona mimi sijaalikwa?” “Niliogopa isije ikaleta picha ya hongo.” Jelini alicheka sana.

“Nakutania bwana! Ila niliambiwa siku za jamamosi kwako ndio kazi inakuwa imepamba moto. Hushikiki.”  Jelini akajua kumbe na yeye alikuwa akimfuatilia! Hakumsusa moja kwa moja. Akafurahi na kujibu, “Wala aliyekwambia hajakosea. Leo ndio nakusanya pesa ya jijini. Wenye kufunga ndoa, najitahidi na mimi nipate kidogo. Kama sio viti kama hivi, basi kukodisha vitambaa vya meza na maua yake. Mapambo ya bibi harusi, ilimradi tu kuwe na neema na kwetu.” “Hongera sana.” Akacheka, kama ambaye hajui azungumze nini tena.

“Ila harusi ni juma lijalo, tena ni jumapili. Nakukaribisha tuwe wote.” Kwa mshituko, akahisi kama hajamsikia vizuri. Akaogopa asijichanganye. Gafla akajihisi kufa ganzi, hajui ajibu nini! Ilishapita muda mrefu, karibia mwaka, hajatongwazwa na wanaume kama Ezra. Ikampa ububu wa sekunde.

“Ishakuwa hongo tena, nini?” Akauliza kwa utani kidogo ila hata na yeye akiwa na wasiwasi asije kataliwa kwa mara ya pili. “Hapana! Nilikuwa najaribu kufikiria kama nina kitu nilishakipanga siku hiyo ya jumapili. Nisije kukubali halafu nikashindwa.” Akajaribu kuzungusha. “Kama kuna mipango mingine, uwe tu na amani. Tusiharibu mipango ya muhimu.” Ikawa kama anahitimisha, aachane naye.

Jelini akajua bahati haitarudi mara ya tatu. Akawahi. “Nafikiri sina kitu kinachonishikilia, na mimi naweza hudhuria.” Akakubali kike. Mpaka Ezra mwenyewe hakuamini kama amekubali. “Sasa mbona kama huamini!” “Sikutegemea ukubali hivyo kirahisi! Basi kesho nitakupa kadi.” “Sawa.” Kama walioogopa wasije haribu, wakaagana hapohapo. Akaondoka akicheka huku akimfikiria Ezra. “Acha na mimi nitoke kidogo, nipumzishe mawazo.” Akajiwazia moyoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jelini Akiwa Amekata Tamaa Ya Kumsubiria Colins, Kijana Ezra Anafanikiwa

Kupenya Akilini Kwa Jelini.

Baba CJ naye?

Chelewachelewa, Utakuta Mwana Si Wako.

Nini Kitaendelea?

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment