Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 11 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 11

Baba CJ. Kwenye mida ya saa 10 jioni akawa amefika Kigamboni, mjengoni. Mlinzi akataka kumkatalia kuingia, mzee akawa mkali akisema yeye ndiye mwenye nyumba na mengine mengi kibabe mpaka akafunguliwa geti. “Ni dada ndiye amesema nisimfungulie mtu mlango.” “Sasa huyo dada yako anaishi kwangu. Acha ujinga.” Mzee akafunguliwa geti akaingiza gari mpaka ndani. Mlango wa kuingilia ndani ya nyumba ulikuwa umefungwa, akakaa nje.

Ilipofika mida ya saa 12 jioni, akaona ampigie simu Love. “Nipo kazini, nimebanwa na kazi.” “Colins yupo wapi? Maana hapatikaniki kwa simu.” “Yaani Colins amebadilika! Hapa najitahidi kumtunzia siri kwa baba. Hataki kazi. Kazi yake kuzurula tu.” Yakaanza mashitaka ya Colins kwa muda mrefu wakutosha. Akimlalamikia Colins.

“Labda nirudi kwenye swali la msingi. Yuko wapi au wewe unajua huwa ana kwenda kuzurula wapi?” “Sijui. Tena wakati mwingine inabidi kumuomba mtu akamtafute, ndioo..” “Huyo mtu anakwenda kumtafutia wapi?” Mzee hakutaka maneno mengi zaidi. “Sijui. Ila huwa mara nyingine anafanikiwa kumpata, ndio ana..” “Unaweza kunipa namba ya simu ya huyo unayemtuma kwenda kumtafuta?” “Ni kijana wangu wa kazi.” Hiyo sentensi ikamchanganya kidogo baba CJ.

“Ukimaanisha nini unaposema ni kijana wako wa kazi?” “Wa hapo nyumbani! Maana hapo ni kama pangu tu. Colins hana muda napo kabisa na ni mimi ndiye namlipa mshahara, maana sijui hata Colins anapeleka wapi pesa yote anayolipwa mshahara. Yaani…” “Love, shitaka lolote utakalonipa juu ya Colins, halitasaidia mpaka nimpate Colins mwenyewe. Sasa je, naweza kupata namba ya simu ya huyo kijana anayejua pakumpata?” Mzee akaweka msimamo. Maana Love ni mzuri sana wa maneno. Usipokuwa makini, anakupoteza lengo.

“Sio kwamba anajua sehemu yakumpata! Na yeye anakuwa kama anabahatisha.” “Sawa, naweza kupata namba yake?” “Nafikiri si ustaarabu kuanza kugawa tu namba ya mtu. Mimi nashauri nimpigie, akamtafute, kisha nimwambie unamtafuta. Atakaporudi hapo nyumbani, atawasha simu yake, atakupigia. Usiwe na wasiwasi. Colins atakupigia tu. Wewe nenda kapumzike. Na mimi mwenyewe nikimaliza kazi, nitarudi.” “Sawa. Nashukuru. Nisipomsikia leo, kesho itabidi nimuwahi kabla hajatoka.” “Usiwe na wasiwasi, usiku mwema.” Wakaagana.

Kila alipotaka kuondoka roho ikasita kama mkewe. Alishaingia kabisa kwenye gari, akawasha ili aondoke, lakini moyo ukasita kabisa. Mwishoe akaamua kubaki tu hapo garini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alikaa hapo mpaka mida ya saa tatu, akasikia watu wakiingia getini wakisukumana. Akatoka garini. Akaona vijana wawili. Mmoja anamvuta mwingine. Akashukuru Mungu yule anayevutwa hakuwa Colins. Maana alikuwa akivutwa si kwa heshima kabisa, kama mnyama! Kadiri walivyokuwa wakimsogelea, aliweza kumuona huyo kijana anayevutwa alivyo mwembamba, ndevu ndefu na nywele nyingi tu. Hakuwa akizungumza ila kupinga tu, kama ambaye hakuwa akitaka kurudi hapo. Baba CJ akasimama vizuri akiwatizama akijua watakapomsogelea, ndipo awaulize kama wanamjua Colins.

Hilo zoezi likaendelea mpaka wakampita na kuendelea kumburuza mpaka kupandisha ngazi zote mpaka juu kabisa, nje ya geti dogo la kuingilia mlango wa ndani. Akaona anamfunga na kamba aliyoitoa mfukoni kama aliyokuwa amejiandaa nayo. Mikono yote miwili na miguu. Akamfunga na kuikaza kabisa. Baba CJ akakunja uso. Kwamba kwa nini amfunge mwanadamu vile kama mnyama! Akabaki akiwatizama kwa juu, yeye yupo chini kabisa ya ngazi.

“Sasa hapo usiondoke mpaka dada mwenyewe aje. Na amesema akukute.” Baba CJ akashituka sana. Akapandisha ngazi akikimbia. “Huyo ni nani!?” Akauliza akijaribu kumtizama kwa karibu. “Mimi mwenyewe nilimkuta, lakini Eva yule aliyekuwa akifanya kazi humu ndani aliniambia, alikuaga mwanaume wa dada kabla hajachanganyikiwa. Ndio dada anakua akimtunza tu.” Nusura baba CJ aanguke kwa mshituko.

“Colins?!” Akamtizama. Weupe ule kama wa mkewe, uliisha wote. Akafifia kama aliyekuwa akiungua na jua. Hapo alipo hakuwa hata na viatu! Mchafu. Amekonda. Yupo kama takataka kweli. “Tafadhali mfungue?” “Ataondoka hapo, na dada amesema nimfunge mpaka arudi.” “Kabla sijakuua, tafadhali mfungue kijana wangu. Hichi ulichomfanya, naweza nikakufanyia na wewe. Nikakuacha hapa mpaka huyo dada yako akakukuta hapa ulipomfunga yeye.” “Samahani sikujua kama ni…” Akasita. “Mimi Eva aliniambia anahisi huyu ni yatima ndio maana dada amejitolea kumsaidia.” Baba CJ akaanza kumfungua mwenyewe kwa haraka.

Alipomfungua tu, akasimama na kutaka kuondoka. “Colins?” Akamgeukia baba yake. “Unataka kwenda wapi?” Akaonekana na yeye hajui. “Umekula?” Akanyamaza. “Funguo za kuingilia ndani zipo wapi?” Akawa hajui.

Kibao Kimegeuka.

Akutana Na Love Halisi.

Akampigia tena Love. “Nipo na Colins hapa kwenu.” Love alishituka sana. “Nilifikiri uliondoka!” Akaropoka. “Tunaingiaje ndani?” Baba CJ akauliza. “Atakuwa na funguo zake mwenyewe. Mimi nikitoka nafunga, nabakia na funguo zangu.” “Kwa jinsi alivyo hivi, kweli atakuwa na funguo za nyumba nzima kweli huyu!? Unajua mara ya mwisho atakuwa amekula lini!?” Hapo akaharibu.

Love akambadilikia mzee, asiamini. Akaanza kwa kulalamika kwamba anamsingizia yeye hamtunzi Colins wakati anayo majukumu mengine mbali na Colins! Kabla taarifa hazijafika kichwani sawasawa, binti akaanza kumlilia kwenye simu, mzee hajaweza hata kujibu, akasikia mzee Simba ameunganishwa kwenye simu, Love analia kwelikweli, anamshitakia baba CJ kwa baba yake kuwa anamgombesha kuwa anamtesa mwanae. Love aliongea mengi akilia. Mzee alipatwa na hali, hawezi hata kujibu kwa mshituko asiamini kama ni Love aliyekuwa akimtetea sana kwa Colins. Usiku huo akajifunua kwa wazi kabisa.

Sasa baba yake, mzee Simba akapokea. “Unawezaje kuzungumza na binti yangu bila mimi?! Yameanza lini sisi kuingilia mambo ya undani? Kweli ulitaka binti yangu aache kazi zake, ukijua garama aliyolipa kusoma, wakati Colins akikataa shule! Leo amefanikiwa ndio unataka abaki nyumbani akimlea Colins ambaye amechagua maisha yake ya ajabuajabu tu!?” Hizo shutuma zikaendelea wawili hao wamewaka kwelikweli na kumuacha baba Colins na mshituko mkubwa, haamini.

Mpaka hapo, ikawa kama Love ndiye aliyekuwa akimsaidia Colins kwenye maisha. Kukubali kuwa na mtu kama Colins ambaye hajasoma kama yeye Love. Mvivu. Hana uchu wa maendeleo. Love aliendelea kulia huku akisema madhaifu ya Colins, baba yake akimtuhumu baba Colins, mwishoe baba CJ akaona ahitimishe. Alilo nalo mbeleni ni zito kuliko hayo matusi yao. “Tutazungumza wakati mwingine.” Akawaambia hivyo tu, na kukata simu.

Mtu Chake.

Akamchukua Colins na kumuingiza ndani ya gari yake. Ikaanza safari ya kurudi kwake. Alifunga milango yote tena akaweka child lock ili asije akaruka garini. Akiwa njiani simu ya mkewe ikaingia. “Ulimpata Colins?” “Nipo naye hapa. Narudi naye nyumbani.” Mama Colins akawa hajui afurahi au ajiulize kwa nini usiku huo arudi naye nyumbani! Ila akauliza. “Kwema?” “Hali yake si nzuri. Anahitaji uangalizi wa karibu ambao pale anapoishi na Love, hawawezi kumsaidia.” “Unamaanisha nini!?” “Labda ukimuona, utajua ni nini nazungumzia. Ila naomba kuwepo na chakula laini. Anaonekana hajala muda mrefu.” Mama Colins akaingia jikoni yeye mwenyewe kuanza kupika uji.

Wana Kulitafuta, Wamelipata.

Aliposikia gari, akakimbilia nje. Akabaki akisubiria Colins ashuke. Maana aliyeshuka hapo hakuwa Colins aliyemtarajia. Akazunguka upande wa pili kuona kama yupo hapo. “Mbona sasa hujaja naye!? Umemshusha wapi!?” Baba CJ akabaki amesimama huku amemshika mkono akijaribu kumuongoza njia aingie ndani. Alikuwa akiyumba kama mlevi au mgonjwa wa kuhara na kutapika. Tena aliyesumbuka kwa muda mrefu mpaka akaishiwa nguvu.

“Baba CJ!?” “Huyu hapa ndiye Colins.” Akarudi kumtizama, kisha akamtizama tena. Mama ni mama. Katikati ya uchafu ule kuanzia wa mandefu na harufu mbaya, aliweza kumtambua mwanae. Mama CJ alipatwa hali mbaya, nusura aanguke. “Sasa katika hili, naomba ujikaze mama CJ, nisaidie ili tumsaidie huyu. Anakuhitaji sana.” Ikawa kama amemsaidia asianguke kwa mshituko, akamrudisha pale, ila akaanza kulia kwa kadiri alivyokuwa akimwangalia. “Umepatwa na nini Colins mwanangu!?” Akamuuliza na machozi. “Unaumwa baba?” Akamuuliza kwa kumuhurumia, Colins hakujibu. Alikuwa akitoa harufu mbaya sana. “Acha nimsaidie kuoga kwanza.” Baba yake akamvutia ndani maana alikuwa kama amezubaa tu.

Kazi ya kumsafisha ikaanzaa, mpaka akatakata na kumbadili nguo. Akamrudisha sebuleni. Akabaki amekaa, ameinamia chini, ameshikilia moyo kwa mkono wa kulia, ule mkono wa kushoto ameegemeza kichwa. “Unajisikiaje Colins?” Mama yake akamuuliza akimsogezea uji. Kimya. “Colins?” Kimya. Wazazi wake wakaangaliana. “Halafu mbona kama miguu ina madonda?!” Akamsimulia alichokutana nacho akiwa analetwa na huyo kijana wa Love. Akazidi kulia.

Baada ya muda wakamuona ananyanyuka, anataka kutoka nje. Baba yake akamuwahi. Akasimama kwa haraka na kukimbilia mlangoni. “Unakwenda wapi?” Akabaki kama na yeye hajui. Akataka ampite atoke, akamrudisha. Hilo zoezi likaendelea. Anamrudisha kukaa, anakaa kidogo. Anakuwa kama amekumbuka kitu, anasimama kutoka. Ila kila akirudi kukaa, anashikilia moyo kwa muda, kisha anasimama anakuwa anataka kutoka. Mwishoe wakaamua kumchoma sindano ya usingizi, wamuwekee maji ya sukari, apate nguvu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kazi ya kumuuguza hapo ndani ikaanza. Hawataki kumpeleka hospitalini kwa aibu. Lakini kila akiamka, anatafuta mwanya wa kutoka hapo ndani. Ila kichwani akawa hataki kabisa kuguswa. Ikabidi baba yake amnyoe upara kabisa ili iwe rahisi kumsafisha. Colins akawa kama kababu kalikokosa matunzo. Na muda wote huo, hakuna hata mmoja kwenye familia ya Simba aliyewatafuta hata kuulizia hali yake. Wao wakashika moja la kuuguza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Connie alipopata habari kuwa kaka yake hali sio nzuri na yupo nyumbani, akaenda kumuona. Maana ilikuwa kama siri hapo mwanzo. Wazee hao wakidhani wakimficha, akala vizuri, basi hali yake itarudia kama kawaida. Lakini ikawa ni mtu anayetakiwa ulinzi, lasivyo anatoroka. Mzee akapunguza shuguli za kikazi, akawekeza muda kwenye kumuuguza. Ndipo Connie alipotaka kujua mbona hamuoni sana huko hospitalini, na kila akipita ofisini kwake anaambiwa hayupo, ndipo ikabidi aseme ukweli. Ndipo akaenda kumuona kaka yake.

Alishituka sana kumkuta kaka yake kwenye ile hali. Hakutegemea kama ni yeye. “Ilikuaje!?” “Hakuna anayejua.” Akaelezewa mazingira waliyomkuta, akalia sana. Na mpaka hapo Love hakusikika tena. Siku hiyo ikabidi tu alale nyumbani kwani alikuwa kama amechanganyikiwa, akasema hataweza kufanya chochote hata akirudi chuoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake akaomba asifungiwe wala wasimpe dawa ya usingizi. Yeye atashida naye hata kutoka naye, ajue anapotaka kwenda. Kweli wakafanya hivyo. Alipomaliza tu kusafishwa na baba yake, mama yao akaanza kumlisha akiwa ameinamisha kichwa chake, kakishikilia na mkono wa shoto, wakulia kashilia moyo kama kawaida yake. Akimuita, ananyanyua kichwa, akimwambia afungue mdomo, anafungua, anamuwekea chakula. Anarudi kama alivyokuwa amekaa. Ameshikilia moyo wake. Connie akamwangalia kwa muda, kisha wakamuona ananyanyuka, anatoka kabisa pale. Hapo hajavaa hata viatu!

Connie akaanza kumfuata nyuma taratibu. Tembea yake yenyewe taratibu kama aliye mwenye vidonda vinavyomuuma kwenye nyayo. Akatembea, kufika getini akakaa chini kabisa. Akamuona anaanza kulia. Mama yao hakuwa mbali. Connie aliumia sana.

Na yeye akaenda kukaa naye hapohapo chini. Jua lilishakuwa kali. Chini bila viatu, panachoma. “Pole Colins. Niambie unataka nini.” Akajifuta machozi nakubaki amejishikilia.

Kitu kama kikapita akilini kwa Connie, akakumbuka mpaka akasimama kwa mshituko. “Nimekumbuka mama!” Mama yake akasogea, mzee alishatoka.

“Ni nini?” “Hivyo unavyomuona anashika moyo. Ni kiapo aliapiwa na Jelini. Colins aliniambia, aliambiwa na Jelini, tena mwenyewe anasema ilibidi aandike kwa kumnukuhu. Akapiga micha pale alipoandika alichoambiwa na Jelini, akanitumia na mimi kama kuthibitisha. Acha nikuonyeshe ujumbe wenyewe. Maana alinipigia akiwa na furaha huyo, ndipo akanitumia na huu ujumbe.” Akaanza kutafuta kwenye simu yake mpaka akaupata ujumbe.

Akamkabidhi simu mama yake. ‘Kila unapoyasikia mapigo yako ya moyo. Popote ulipo. Muda wowote hata kama mimi hunioni, ujue yupo Jelini anayekupenda kwa moyo wake wote, mpaka niondoke hapa duniani. Hakuna ulimwengu utakaokuwepo wewe, nisikupende Colins. Ujue nitakupenda mpaka kifo chako.’ Mama Colins alilia sana.

“Kumbe ndio maana anajishika moyo, kisha anaanza kutafuta!” “Usilie sasa! Yeye hapo alipo anaonekana bado hajajua anachokitafuta. Ndio maana anahangaika. Amebakia na hicho kiapo moyoni, hakumbuki.” Mama Colins akalia sana.

“Nitafanyaje Connie?” “Nikumtafuta Jelini, aje amuone labda atatulia.” Mama yao alishituka sana. “Hivi alivyo Colins ndio atataka mumuona kweli! Alipokuwa mzima tulimfuata na…” Akamsimulia jinsi walivyomuendea Jelini nyumbani kwao na kumuita mchawi, Connie akashangaa sana.

“Kweli mama na wewe ukaenda, wakati Colins alishakwambia ukweli wake wote juu yake na Love!?” “Sijui niliingiwa na nini!? Kulikuwa na shindikizo kila mahali nikawa kama nimezidiwa nguvu, na mimi nikabaki nikienda kama upepo, nikiomba hiyo fujo itulie. Mama Simba naye akawa kutwa kwenye simu akiomba nisimamie hilo jambo liwezekane! Akaja na bibi yenu naye. Kama unavyomjua akikazania jambo. Akalivalia njuga, nikabaki sijielewi! Ilikuwa mbaya mno.” “Mmmh!” Connie akaguna kwa kuchoka. Hajui hata aanzie wapi kulaumu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakamuona Colins anasimama, anataka kutoka nje kabisa. Connie akamuwahi. “Nisikilize Colins. Sasahivi jua ni kali sana. Utaanguka njiani. Kwanza umedhoofu. Hutaweza kufika mbali.” Akatulia kidogo,  kisha wakamuona anatoka. Akamfuata tena. “Turudi ndani. Ikifika jioni, nitakusindikiza tukamtafute wote Jelini.” Hapo akamuona kama amekumbuka kitu. Akarudia kwa sauti ya chini. “Jelini!” Wakamsikia kama aliyekumbuka vizuri sasa. “Ndiyo. Si ndiye unayemtafuta?” “Jelini!” Akarudia tena, ila safari hii na machozi. “Utakuwa sawa Coly. Twende ukapumzike ndani, halafu jioni tutoke tena. Sawa?” Akamshika mkono wakawa wanarudi ndani. Mama yao akilia sana.

Na kweli jioni akamvalisha sendozi nyepesi, wakatoka wakitembea akimsindikiza kumtafuta Jelini. Mwenyewe alikuwa dhaifu. Akitembea kidogo, anakaa. Wakafanya hilo zoezi mpaka giza lilipowakuta huko mtaani, mama yao akaja kuwachukua na gari kuwarudisha nyumbani. Kwenye gari akalala kwa kuchoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hayo ndio yakawa maisha yake huku baba yake akiwa anatumia madawa ya kila namna kumtibu bila kufanikiwa kurudisha akili yake. Asubuhi anatoka hata na mama yake, wanajidai wanakwenda kumtafuta Jelini. Wakitembea akichoka, wanarudi nyumbani. Jioni tena hivyohivyo, wanatoka naye kumdanganyishia kumtafuta Jelini mpaka achoke, wanafuatwa na gari popote wanapokuwa wamefikia, maana hapo anakua amemaliza nguvu zote na wazi anakuwa na maumivu ya nyayo zilizojaa madonda, hawezi tena kutembea kurudi nyumbani. Na mara zote anaishia kulala kwenye gari kwa kuchoka kutembea akimtafuta Jelini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ni Nini Kimempata Colins Katikati Ya Maombi Hayo Ya Mtumishi Aliyeletwa Na Kemi? Dawa Yake? 

Jelini Yuko Wapi?

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment