Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 7 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 7

“Kwa nini uliondoka na kwa nini ulirudi?” Akamsikia Joshua akimuuliza kwa ukali kidogo. Jema akajiweka sawa kusikiliza. “Nilipaniki. Bale aliniambia ana deni anataka kulilipa. Au anasikia anawajibika kuendeleza jina la baba yake aliyemkatili. Kuwa na familia. Awe na watoto. Nikapaniki. Najua amekwambia kuwa mimi sina uwezo wa kuzaa.” Jema akashituka. Vai akasubiri kama Joshua atajibu, lakini akabaki akimtizama, mikono mfukoni.

Vai akaona aendelee. “Mimi sina uwezo wa kuzaa, Joshua.” “Nafahamu hilo.” Akajibu kama anayetaka aende moja kwa moja kwenye kujibu swali lake. Vai akazidi kutetemeka mpaka midomo. “Kwa hiyo aliposema vile nikapaniki na kuamua niondoke kwa kuwa nampenda Bale. Na nilijikuta tu nikimpenda. Nikaona kuwepo kwa ukaribu ule na pale tulipokuwa tumefikia kimahusiano, maana tulianza kama marafiki wa kawaida tu. Ila mimi ndio nikaanza kumpenda. Tukawa tupo karibu sana. Nikajua kuwepo vile kunaweza kumfanya akashindwa kupata mwanamke atakayempa anachokitaka. Ndio nikaondoka ili nisimkwamishe. Na ukweli Bale hakuonekana kujali sana kuondoka kwangu. Maana alinirudisha mpaka chuo, na kuniacha wala asinitafute tena hata kwa salamu. Nikajua kweli ameamua kutafuta msichana mwenye uwezo wa kuzaa ili amuoe.”

“Na uliposikia nipo hotelini na mwanamme mwingine ilikuwa…” Akameza mate ambayo ni kama yalisha kwisha kumkauka kabisa mdomoni. Mrembo akapata dry mouth ya hali ya juu.

Joshua kimya akimtizama. Akajikausha machozi fasta. Akaendelea asipoteze muda. “Ukweli si kwamba nilipanga. Mimi sinywi pombe. Sasa nilipotoka kwa Bale, nikiwa hosteli, siku moja rafiki yangu akanikaribisha chakula cha usiku akiwa na mwanaume wake na huyo rafiki yake. Tulipofika huko, wakanishawishi au nisema nikanywa sweet red wine, waliniambia ni tamu kama juisi. Nilipoonja kweli ilikuwa tamu, nikajua sitalewa. Nikaendelea kunywa mpaka nikalewa kabisa. Ndio nikaja kuamka chumbani na huyo mwanaume. Halafu huyo rafiki yangu niliyekuwa naye usiku uliopita na hao wanaume, aliniacha na huyo mwanaume hapo hotelini na kuja kumpigia Bale simu kunisemelezea.”

“Ila nirudi kwa upande wangu. Nilikosea tokea mwanzo, Joshua. Naomba msamaha kwako na nimeshamuomba msamaha Bale pia. Si kitu nilikuwa nimepanga.” Jema akazidi kushangazwa.

“Bado hujajibu ni kwa nini umerudi?” Joshua akazidi kumbana. “Niliugua. Na hapa mjini kwa muda mrefu sana, Bale ndio amekua akiniuguza. Hata nikiwa chuo, nikiugua, yeye ndio mtu pekee atahakikisha napata matibabu na kupona kabisa. Mama yetu yupo busy sana, na baba naye anaishi Moshi, anamaisha yake. Kaka James pia anamaisha yake. Na si mtu ambaye tumezoea kumtafuta kwa matatizo kama hayo. Au hatuna mazoea ya karibu na kaka ya kiasi hata chakutafutana kwa salamu tu, mpaka iwe kuna jambo muhimu sana. Sio kama anavyoishi na Nanaa. Kwangu na Viola ni tofauti kabisa. Hayupo karibu kabisa na sisi.” Jema akajisikia kuumia.

“Kwa hiyo nimejikuta nabakiwa na Bale tu. Nilipougua, sikuwa na jinsi. Ikabidi kumwambia. Bale alikuja kunichukua na kuniuguza kwake mpaka nikapona na kuhakikisha muda ule ambao nilishindwa kuwepo darasani, ananisaidia kusoma mpaka kufikia wenzangu. Ndipo kwa mara ya kwanza kipindi hicho nikamwambia ukweli kwamba mimi nampenda, na nilikosea. Na yeye akanieleza upande wake. Ninachotaka kukuhakikishia ni nampenda Bale. Amenipokea hivi nilivyo. Tuna maisha ya upendo na amani. Tunabebana katika kila hali, kitu ambacho sijawahi pata kutoka kwa mwanaume yeyote yule.”

“Nilikosea, nimetubu, nakuahidi hutasikia baya langu tena. Kwakuwa shida yangu ilikuwa mwanaume kama Bale, sina sababu ya kuhangaika tena. Nimetulia. Bale ndio sababu nipo chuo mpaka sasa. Anasoma na mimi. Ananielekeza. Ananitia moyo kwa sababu mimi sijajaliwa akili nyingi za darasani. Lakini Bale anasoma na mimi, na hachoki. Nafanya vizuri chuoni, kwa sababu yake. Najua najirudia rudia, na wewe unaharaka. Lakini nakuhakikishia nampenda sana Bale. Na nitatulia naye mpaka kifo.”

“Lakini kaka yako hamtaki! Utafanyaje?” Moyo wa Jema ulipasuka kusikia hivyo, kama kuliangushwa chuma sakafuni. “Kwamba huyu Joshua yupo kimya juu ya hili muda wote, kumbe anajua jinsi James alivyomfukuza Bale!” Jema aliingiwa hofu, asiamini muda wote huo Joshua anamchora tu yeye na James. Asiwaambie chochote ila kufanya kama kila kitu kipo sawa. “Inamaana na Naya anajua!” Akabaki kujiuliza bila jibu huku akisikiliza.

Vai akajifuta machozi akijaribu kutulia ili kuzungumza amuaminishe Joshua. “Tupo kwenye maombi. Mimi naamini kama Mungu aliweza kumsamehe Bale kwa makosa yote mabaya aliyo tenda. Halafu wewe mtu baki ukampokea na kumtunza kwa heshima kubwa hivi, naamini Mungu atagusa na wengine. Inaweza isiwe kwa haraka kwa sababu ukweli Bale alikosa sana. Tumekubaliana hatutafanya chochote, tutabaki tukimuomba na kumsubiria Mungu mpaka yeye mwenyewe Mungu atakapofungua mlango kwa wakati wake yeye. Ni hilo tu.” Hapo akaongea lugha ya Joshua. Akapa moyo wake.

Akamuona amevuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha. “Bale anakupenda sana Vai. Tafadhali usije wahi bweteka.” Vai akazidi kuumia nakushindwa kuzuia machozi. “Sithubutu, kwa sababu hakuna mwanaume atanipokea na kunipenda  hivi nilivyo, kama Bale. Mimi najua ninachozungumza. Sithubutu. Naomba na wewe unipe nafasi nyingine Joshua. Bale anakutizama sana wewe. Akipata baraka zako, najua atafurahi. Ni hilo tu.” “Nitazidi kuwaombea. Muwe na siku njema.” Jema aliposikia tu hivyo akapandisha kioo kwa haraka. Mpaka Joshua anageuka, akajifanya hakuwa hata akiwatizama. Wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Lakini Jema akabaki na maswali mengi sana mpaka kumtia hofu. Kwamba Joshua ndio yupo karibu hivyo na Bale! Halafu anajua kama Bale alifukuzwa vibaya vile nyumbani kwake na mumewe! Halafu hata asilizingumzie hilo hata na yeye au James, eti akabaki tu kimya! Kikamsumbua sana Jema asijue Joshua anawafikiria nini. Akapotea kabisa hapo garini. Lakini ni kawaida yao. Huwa mbali na kazi au vitu vya muhimu, hawanaga stori na Joshua. Ila James na Joshua wapo karibu sana. Wanazungumza sana tu. Kimya kikapita hapo garini, dereva akiendelea kukanyaga mafuta akitafuta barabara ya Cocacola.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bale akamsogelea pale alipokuwa akisindikiza gari ya Joshua kwa macho. “Tutakuwa sawa Vai. Usiwe na wasiwasi.” Vai akajifuta machozi. “Nenda tu kazini. Tutazungumza baadaye.” “Siwezi kuondoka nikakuacha huna raha. Nataka ufurahie pamoja na mimi. Tumepata mguu na umefaa. Usilie, nyamaza. Nisindikize kwenye gari.” Wakafuatana.

“Halafu ulikuwa sahihi, Bale. Inamaana ungebadilisha siku, inamaana Joshua angekuja hapa leo, akakukosa. Ningekuponza.” “Kama tungekubaliana kubadili, ningemtaarifu. Lakini sikutegemea kama angekuja aisee! Joshua yupo busy. Si umeona jinsi muda wake unavyobanwa na Jema? Hata dakika moja kwake ni muhimu mno. Eti imenigusa kiajabu sana. Sijatarajia kabisa kumuona hapa kwa hili, siku kama hii!” “Hata mimi nimeona jinsi anavyokuthamini aisee. Si kawaida.” Wakabaki wakizungumza mpaka Vai alipotulia ndipo wakaachana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

‘Usisahau nakupenda Vai. Na sitabadilika.’ Ujumbe ukaingia akiwa yupo na wenzake darasani. Akajisikia kupendwa, akabaki akifikiria ni lini Mungu atafungua hiyo milango, wapokelewe kwao, aolewe na Bale, nafsi yake itulie. Maana kila wakati alibaki akiota kuibiwa tu huyo Bale.

Kila Jambo Na Wakati Wake.

Ijumaa.

Naya alijua mumewe yupo kikaoni, akasubiri mpaka akamaliza kikao cha mwisho wa siku, akampigia. “Jema ameniambia ndio mmemaliza siku.” “Aisee namshukuru Mungu, juma lilikuwa na mengi, lakini nimehitimisha. Naona Jema amenikaba mpaka ameishiwa cha kunipa kesho, ameniambia kesho nipo huru.” Wakacheka. “Ameniambia jinsi alivyokubana hili juma zima.” “Hata muda wangu wa chakula cha mchana, alichukua yeye. Ikabidi tu nitangaze mfungo wa lazima. Akinipa hata dakika 5 nazungumza na Mungu wangu tu.” Naya akatulia kidogo.

“Mama Kumu, upo?” “Ulikuwa ukiwaombea kina Bale?” Naya akauliza kwa upole. “Usiwe na wasiwasi, wewe na wanao pia mlikuwa mkitajwatajwa hapo katikati.” Naya akamuhurumia mumewe ila akacheka. “Nakuja nyumbani muda si mrefu ili niwawahi kina Kumu kabla hawajalala.” “Kama ulikuwa umefunga, basi naona utangaze na mkesha pia. Leo wamelala mpaka jioni hii. Yaani mama G amepita ndio amewaamsha kwa lazima. Tumewaogesha, akaondoka na kunitakia mkesha mwema. Wamejaa hapo kwenye chumba chao cha kuchezea, wamechangamka kama ndio jua kali nje. Hivi nimetoka hapa mlangoni ili nizungumze na wewe.” Joshua akacheka lakini ndio akajua hiyo simu haikuwa ya salamu tu, kuna jambo.

“Niambie mama Kumu.” “Sijui niiwekaje hili!” Akaanza kama anayesita. “Hata ukianzia katikati, unajua mimi nitakuelewa tu. Niambie chochote kilichopo mawazoni mwako.” “Ni sawa kesho tuandae mazingira, tuwakaribishe kina Bale?” Joshua alishituka, akapatwa ububu wa gafla.

“Nimeumia kuona anafukuzwa kwenye majumba ya watu, Joshua. Watu wote tunamkimbia, umebaki peke yako ukimkumbatia bila kuchoka. Nimeshindwa kutulia na lile swali lako la kama baba Naya angekuwepo, angefanya nini juu ya Bale. Nikakumbuka baba alivyokuwa tayari kukosa harusi yangu ili akamtafute yeye. Mbaya zaidi baba hakumpata, akaishia mikononi kwa Malon aliyekuwa na hasira mbaya kwa wakati ule. Sijui alimwaminisha nini mpaka Bale akafikia vile. Lakini katika yote, nakumbuka baba hakuacha kufunga na kumuomba Mungu kwa ajili yake. Hakumkatia tamaa mpaka kifo chake.” Naya akaendelea kuzungumza kinachoendelea moyoni mwake.

“Halafu nikakumbushwa maneno ulizungumza na mimi siku moja ulikuja kunichukua kwenda kazini. Ilikuwa asubuhi sana. Tulikuwa tumekosana na Bale sababu ya huyohuyo Malon. Ukaniambia mimi ni mzaliwa wa kwanza kwa sababu na lazima niishi kama dada yake si mshindani wake. Maneno yanayofanana na hayo, mpaka nikampigia simu na kuzungumza naye, hakuamini maana aliondoka nyumbani na kwenda kwa Malon, Mbeya, tena baada ya kumuacha ile mara ya kwanza.” Naya akaendelea, Joshua kimya akijua Roho wa Mungu alikuwa akishugulika na nafsi yake mpaka amesalimu amri.

Anyways, ninachotaka kusema ni kwamba, mimi kama Naya au mama Kumu, nina hofu naye sana. Naogopa hata kumsogeza karibu na kina Kumu. Lakini nahisi na mimi nitakaa sana hapa, kama sitaamua kuchukua hatua. Sitatoka hapa na nitaendelea kumuadhibu kwa makosa ambayo alishasamehewa na Mungu. Nimeona na mimi nitembee na wewe kwa imani tu.” “Nakushukuru Naya. Asante sana.”

“Mimi ndio natakiwa kukushukuru Joshua. Bale ananihusu mimi zaidi kuliko wewe uliyekubali tu kutuchukua ukisimama kwenye nafasi ya baba Naya. Nashukuru Joshua. Naomba nivumilie. Nilihitaji muda. Bale alinitenda ukatili mbaya sana.”

 “Na mimi nilijua ndio maana sikukuharakisha. Naamini kwenye wakati wa Mungu. Na nakuahidi Naya, tutakuwa salama. Namuwekea dhamana Bale, amebadilika. Tafadhali niamini. Nimemuona kwa maneno na vitendo, mpaka utahisi amekua mtu mwingine kabisa. Sijawa kipofu katika hili kiasi cha kukubali kumleta karibu ya familia yangu, kama Mungu hajaruhusu. Nisingekubali kuhatarisha maisha yako na watoto hivihivi.” Naya kimya akiendelea kulia.

“Sasa hizi ni habari njema, mama Kumu. Usilie. Wanao watahisi haupo sawa, na mimi baba yao sijasimama kwenye nafasi yangu. Wataniona hovyo.” Naya akaanza kucheka. “Hivi wewe unajua wanao bado ni wadogo sana hawaelewi kitu.” “Hata kidogo. Wanahisia zote, wanaelewa kila kitu. Ndio maana wakiona unaimba na wao wanacheka na kupiga makofi. Wakikuona umepoa, na wenyewe wanapoa. Wanakuangalia sana usoni na wanafanya kila kitu kutokana na hisia zako. Tafadhali tubakie kwenye hili. Mwenzio nimefurahia sana. Mungu amefungua mlango ambao sikuwa nikijua utafungukaje! Na sikuwa nikijua hata nimuombe nini Mungu juu ya hili. Nikawa nikimuachia tu Roho wa Mungu, azungumze naye Mungu mwenyewe. Ila naona na huko mbinguni watapumzika.” Naya akaanza kucheka akilia.

“Jinsi walivyosumbuliwa?” “Si kidogo mama. Pakipoa kidogo tu, natuma maombi mengine. Hata nikiwa naoga, nikimkumbuka tu baba Naya, na maisha yenu niliyowakuta nayo pale kwenu Kiluvya siku ya kwanza mliponifungulia mlango nyumbani kwenu, na Bale akanipikia, basi namwambia Mungu, ‘tafadhali kumbuka rehema’. Naona akaona afupishe hili jambo, ahamie kwako. Sasa kabla hapajapoa, acha nimtafute Bale, niwakaribishe nyumbani kesho. Najua kwake itakuwa…” Akakosa neno. “Acha nimpigie.”

“Joshua?” Akamuwahi kabla ya kukata simu. “Nipo mama.” “Utafanyaje juu ya James? Kila nikifiria jinsi alivyowafukuza kwake, inaniuma, japo namuelewa.” “Sijui Naya. Kwa mara ya kwanza, nimekosa neno au maneno sahihi yakuzungumza na James. Ni kama wakili, aliyelipwa pesa nyingi kusimamia kesi ya mtu, halafu hana jinsi ya kushinda kwa sababu ushahidi wote unaonyesha mtu wake ni mkosaji, na adhabu ndio halali ya huyo mtuhumiwa. Hakuna ubishi, hakuna kupinga kwa sababu kweli huyo mtu amekosa. Ndipo nilipo mimi.”

“Lakini Naya, aisee acha huyu Mungu, abakie kuwa Mungu. Ndio maana naogopa sana kugusa utukufu wake. Ana njia zake za ajabu sana, ndipo nilipo mimi sasahivi. Na namshukuru Mungu, hata wao, wamekubali kumsubiria Mungu.”

“Juzi nilimpigia simu Bale, nilijua ni siku yake ya maombi. Akaniambia na Vai yupo hapo kwake walikubaliana waombe pamoja. Basi nikaungana nao kwa njia ya simu.” “Joshua?” “Kabisa Naya. Hakuna kinachoharibika mbele za Mungu, kwa kupitia maombi. Na hakuna aliyefilisi mbingu kwa kupewa na Mungu alichoomba. Kumejaa hazina isiyoisha.”

“Nilikuwa njiani kurudi nyumbani. Nikaomba nao, nikawapa neno moja tu kwa ufupi, nikawaacha wakiwa na amani kabisa. Hawa watu wawili wanapendana, Naya. Na wameamua kubebana vile walivyo mpaka utashangazwa na nguvu ya msalaba. Na hata ukiwaona kwa macho, uta…” “Subiri kwanza Joshua. Kwani wewe ulishakutana nao?” Joshua akajua amekamatwa. Asijue Naya anajilaumu kupitwa kwenye maisha ya kaka yake.

“Ndiyo, Naya. Kama juma moja hivi limepita, Bale alifanikiwa kuwekewa mguu wake. Ilikuwa siku ya jumatano, asubuhi, na mimi nikaenda huko MOI kushuhudia kile Mungu amemfanyia, ndipo nikakutana na Vai. Kumbe alikuwepo pale kumsindikiza. Ninachotaka kusema ni hawa watu wawili, ni binadamu walioamua kubebana vile walivyo. Hata wao ukiwatizama, utajua ipo amani katikati yao. Na wanamsubiria Mungu.”

“Kwa kujibu swali lako. Nitafanyaje kwa James, SIJUI. Ila ninachojua, huyu Mungu aliyeanzisha kazi yake kwa Bale, hatatulia mpaka ikamilike. Na kwa sababu alizungumza na mimi pia na kuniambia hajamalizana naye, basi namuachia yeye mwenyewe. Ila najua hao malaika wangu wa zamu, watakuwa wamesha choka. Nahisi na wenyewe wanamwambia Mungu, kubali kwa haraka, hili jambo liishe. Wote tupumzike.” Naya akacheka akilia.

“Asante Joshua wangu. Ujiandae kwa usiku mzuri sana.” Akamsikia akifurahia. “Sasa uache utoto.” “Acha nifurahie marupurupu yangu kutoka kwa Mungu, Naya. Acha wivu.” “Ujue ukianza kujisifu nitagairi.” “Huthubutu. Utashangaa hulali, unakesha. Mungu anakuadhibu kwa sababu….” “Nyie Joshua jamani! Kumbe ndivyo unavyo…” “Nakwambia sio mimi ni Baba yangu, anajua kunipa yaliyo mema. Na nilikwambia huwa malipo yake si madogo. Sasa wewe usimjaribu.” Naya alicheka mpaka machozi.

lingerie
“Ujue Joshua wewe hujatulia!” “Mimi nakushauri utende kazi pamoja naye, katika kunipatia yaliyo mema. Laza wanao haraka. Vaa lingerie nzuri, tena leo nataka nyekundu, nipe dozi inayofanana na mimi. Sio kunipunja. Utamuhuzunisha Baba yangu.” Naya alizidi kucheka. “Baba yako anataka nikulipe na lingerie?” “Mimi nafikiri anataka nipate ninachopenda mimi. Kwa hiyo ukamue kabisa, nikija nipate vitu vyangu vyote, na hayo matiti waliyonipokonya wanao, niyapate waziwazi.” Naya alicheka mpaka akakata simu, asijue Joshua ni zaidi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hatimaye Milango Ya Kwa Dada Yake Bale Imeanza Kufunguliwa.

Itakuaje Wakikutana Ndugu Hawa Waliobaki Wawili Tu, Tena Baada Ya Muda Mrefu Wakiwa Wameumizana Sana?

 Colins Yupo Wapi? Anafanya Nini Na Anaendeleaje Na Mpenzi Aliyepata Baraka Kutoka Kwa Wazazi?

Bado Jema Anataarifa Ya Umuhimu Wa Bale Kwa Joshua. Itakuaje?

Usikose Muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment