Maisha lazima yaendelee. Huku kazini kwa kuwa
Colins alikuwa mtu wa watu, wakamvumilia mpaka wakachoka. Amepotea kazini.
Viongozi wanamtafuta kwa simu mpaka wakajaribu kwenda kwake, hawakumpata. Baada
ya mwezi ikabidi nafasi yake ijazwe. Alipotaka kupewa James, mchaga akaikataa.
“Mimi sina muda wa vikao zaidi ya huu ambao nishaupa kampuni. Nina mambo mengi,
na ninafamilia changa. Haya mambo ya vikao vya
mpaka usiku, yangu yatakwama.
Ila nashukuru kwa kunifikiria.” Wakajaribu kumbembeleza James ambaye tayari
anajua hiyo kazi. James akapiga mahesabu ya muda atakao takiwa kuongeza
hapo kazini akipunja muda kwenye biashara zake, akaona kiasi cha pesa wanachopanga
kumlipa hakiwezi kutosha kufidia pesa anayotengeneza nje ya kazi. Akakataa
kabisa, ila akaahidi akiletwa mgeni, japo atakuwa kiongozi wake, atamfundisha
kazi.
Nafasi ya kazi
ikatangazwa, baada ya majuma matatu, nafasi ikajazwa na kijana mdogo tu. Hakuna
aliyemuona wala kumsikia Colins. Maisha yakaendelea.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa Jelini yeye
akabakiwa na sababu moja tu. Amekataliwa na wakwe sababu hana kazi. Akajiona
mvivu. Wala la uchawi halikumuingia akili. Kwanza ni kama aliliacha
palepale. Akakazana kazi yeye na mama yake. Mama Jema alijawa na furaha, Jelini
akawa mtu ambaye hakumtegemea. Akili imechangamka, biashara akaijua vizuri na
kujiongeza. Tabia kama za Kasa, akaiga. Kuamka alfajiri, kulala usiku ulioshiba,
tena bila malalamiko.
Mashoga zake wote
wenye masaluni yeye ndio akachukua kazi ya kuwapelekea kila bidhaa ambayo
wangetaka kununua. Basi anakusanya oda kwa simu, anatuma kijana kushusha kwenye
masaluni. Mama Jema hakuamini hiyo akili. Akawa anaingiza pesa kwa kujituma, na
maneno yake mengi kwa wateja. Kila mteja yeye ni besti yake. Ukimkuta dukani,
maneno mengi akikusifia kwa hili na lile na cheko, mpaka utanunua. Wakawa
wanampenda. Kila anayefika dukani, anataka kumkuta cha maneno. Naye kuongea
alijaliwa, hachoki na hakosi neno kwa kila mtu. Na hivi hakujaliwa
dharau japo ni mzuri wa kuvutia, basi utapenda kumsikiliza maana hutahisi hila
nyuma ya cheko lake.
Ataongea hapo na
kutoa ushauri akikusifia, basi lazima umsikilize. Kwanza yeye mwenyewe alijaliwa
ngozi laini kama mtoto mchanga. Akikwambia tumia kitu fulani, lazima ukubali
ili uwe kama yeye, kumbe yeye ngozi na uzuri ni vya kuzaliwa. Akianza kusifia
nywele alizonazo hapo, utanunua hata kama bei kubwa, ilimradi ukasuke ili
upendeze kama yeye. Maisha yake yakaendelea akihangaika, na yeye hakumsikia
wala kumuona Colins hata kwa bahati mbaya.
Ila habari za
masaluni zilizokuwa zimeenea ni Kemi na Love kuwa wamemkomoa. Alitaka kuiba
mwanaume wa Love, wakamuwahi. Wakajaribu kumchafua, lakini Jelini mtu wa
watu, hayakwenda mbali. Ila akajua kwamba Colins anaishi na Love, kwenye jumba
la kifahari, Kigamboni. Akabaki akimsononekea Colins wake, akawa hana jinsi. “Colins
amemchagua Love kwa kuwa yeye amesoma ana mihela.” Ndicho kilichobaki
moyoni mwake.
Maisha yakaendelea
ila hakuacha kumkumbuka Colins. Hakupata mwanaume kama yeye. Mwenyewe alimuona
mzuri kuliko kila mtu, halafu moyo wake ulimpenda sana Colins. Akabaki
akisubiria aje atokee Colins mwingine.
Kila mwanaume
anayemjia, sio mweupe. Akija mweupe, basi si mweupe sana kama Colins. Sauti
yake na midomo pia vitakuwa na tatizo, havifanani na Colins. Hawaongei vizuri,
ilimradi tu. Ila hakukata tamaa ya kuja kuwa na mtu wake. Biashara ikapanuka na
yeye akawa wakusafiri kwenda kufuata bidhaa nje ya nchi. Sehemu mbalimbali
ilimradi alete vitu vya tofauti nchini. Ikawa kweli biashara ndio kipaji chake.
Alifanya kwa moyo na ikamkubali.
Kwa Kasa hakutaka
hata kuhisi tena. Kwanza mwanae ndio alitibua kabisa. Hata kama kungekuwa na
kimwanya, Kemi akasaidia kabisa kufunga, Kasa asijue ya mtaani. Kuwa mwanae
ndiye anamnyima penzi la Jelini. Akajibakia peke yake na wala hakutaka kujua
kilichoendelea kati ya Kasa na anti yake aliyemuunganishia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jema hakuacha
kuwaombea na kuwasisitiza wawili hao mambo ya kanisani. Akawakaba, ikawa hakuna
jingine analozungumza nao hao wawili isipokuwa kuanza kuishi ukristo. Uzuri
Jema mwenyewe alionyesha ukristo wa vitendo wakaanza kumsikiliza.
Shuguli ikawa mama Jema. Umwambie awe mkrito wa kukaa kanisani na nyumbani siku
nzima ya jumapili asifanye kazi! Hapo pakawa pagumu.
“Ndio ujinga huo
ninao uzungumzia mimi. Mnafundishwa nini humo kanisani siku nzima?” “Sio lazima
mama. Tunaenda ibada moja tu. Masaa mawili, hayazidi matatu. Ukitoka, unaenda
kutafuta pesa. Halafu mara moja tu kwa juma! Kweli ushindwe mama jamani! Mimi
na watoto wangu wote tutakuwa tukienda kanisani. Mwenzio James kakubali.” Mama
Jema akamtizama James, James akacheka. “Na usinigeuke James.” “Mimi mbona
nimekubali!” “Sasa mwambie mama. Wewe anakusikiliza.” Wote wakamgeukia James.
“Mimi na familia
yangu ni dini ya Jema.” “Acha bwana kusema hivyo James, wakati
tulikubaliana vizuri!” “Haya basi. Sisi, familia yetu, ni watu wa Mungu.
Jumapili, siku moja tu, hatutashindwa kumpa Mungu masaa mawili tu. Yeye ametulinda,
amekua na sisi. Hata hizo biashara tunazohangaikia, ni Mungu ametupa.”
Jelini hana mbavu maana ongea yake kama anayemnukuhu Jema, mkewe anamtizama tu.
“Au nimekosea mama
JJ?” “Wewe mshawishi mama bwana, acha kuwa na wasiwasi na mimi.” “Uangaliaji
wako ndio unanitia wasiwasi. Kwa hiyo mama Jema. Mimi na familia yangu.
Tukiamka siku ya jumapili, sio kuwaza biashara. Tunaenda kumuabudu Mungu
aliyetupa vyote, ndio ratiba nyingine zinaanza. Hata JJ anabarikiwa siku
si nyingi.” “Makubwa! Haya huko kanisani ni wapi? Ndio huko wanakolia?” “Ni…”
“Sasa hapo kazi yako imeisha, naendelea mwenyewe.” James akanyanyua
mikono juu kama anayemuachia ukumbi mkewe.
Jema akazungumza nao
hao watatu siku hiyo ya jumamosi asubuhi wote walijikuta kwa Jema akiwa ndio
anamalizia likizo yake ya uzazi. Akazungumza nao mpaka watatu hao wakakubali
kuanza kwenda kanisani siku ya jumapili, ila wakimpa Jema mashariti mengi juu
ya huko kanisani, kama sio wakristo! Lakini Jema akawachukulia taratibu tu
akiwang’ang’aniza na kuwatia moyo kwamba hawatakaa huko siku nzima. Akawaambia
kanisa lao linazingatia muda. Akafanya ushawishi mpaka wakafika muafaka. Jema
alifurahia sana. Kumuingiza mama yake kanisani! Kwake ukawa muujiza wa kama
kumuombea kipofu na kuona.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakristo hao wakaanza
maisha ya kanisani mara moja kwa juma. Angalau wakajitahidi. Mpaka Jeremy akawa
akienda kanisani. Wakitoka wanakaa kula wote kwa pamoja, kisha James, Jelini na
mama Jema wanaelekea kwenye biashara zao. Jema na mwanae pamoja na mama wa kazi
ambaye aliletewa kumsaidia mtoto, wanarudi nyumbani na Jeremy. Akisha kula
usiku na kuoga, Jelini anakwenda kumfuata kwenda kulala. Jumapili walikuwa
hawafanyi kazi mpaka usiku mwingi. Maisha yakaendelea.
Kila Jambo Na Wakati Wake.
Mguu wa Bale ulikuwa
umefika na alitakiwa kwenda kuwekewa na kujaribisha kutembea. Alishafanyia
mazoezi hata kabla mguu wenyewe haujafika, kwani hakuacha kwenda mazoezini
tokea apone kidonda. Huyo Bale alifanya mazoezi ya huo mwili wake kwa kujituma bila ya kuchoka.
Ukimwangalia tu, utajua ni mtu wa mazoezi. Aliweza kuishi na mguu mmoja
akitumia gongo moja bila shida. Akajua kugeuka na kufanya yake kwa wepesi
sababu ya kuzingatia mazoezi na wataalamu waliokuwa wakilipwa na Joshua
hapohapo kitengo cha MOI.
Alipopata taarifa
kuwa mguu wake umefika, anaweza kwenda kuwekewa, akamtumia ujumbe Joshua. ‘Mguu umefika. Nina mpango wa kwenda huko siku ya jumatano asubuhi
mida ya saa nne baada ya kikao cha ofisini. Nakushukuru Joshua. Asante.’ ‘Anytime.
Hongera.’ Akamjibu tu hivyo. Akajua yupo busy siku hiyo ya jumatatu,
akamuacha.
Akaona amtaarifu na
Vai. Ilikuwa bado mapema tu siku hiyo ya jumatatu. Hapohapo akampigia. Bale
akashangaa anampigia simu mida hiyo, ila akapokea. “Sasa
kwa nini usubirie mpaka jumatano na wewe ulikuwa ukisubiria huo mguu kwa hamu!?”
Vai akaenda moja kwa moja kwenye lake bila hata kupoteza muda. “Si umesema upo unafanya round wodini wewe, mbona umepiga!?”
Akaanza kucheka mwenyewe. “Madaktari wawili walikuwa
wakibishana hapa, wamekutana wote wajuaji, naona wameamua kurudi ofisini
kuwekana sawa, ndio warudi tumalizie roundi. Kwa hiyo tumekaa tu hapa
tukiwasubiria. Sasa kwa nini unasubiri mpaka jumatano?” Akarudi kwenye
lake.
“Jumatatu
na jumanne panakuwa busy sana na vikao vingi hapa makao makuu. Ila jumatano
baada ya kikao cha kitengo asubuhi, panakuwa pametulia, ndio naona niende.”
“Kwamba ukiwaomba ruhusa kesho kwa jambo la muhimu hivi unaona watakukatalia?” Bado haikuwa
ikimuingia akilini. “Hapana. Mimi bado ni mgeni Vai. Na
najiona nitakaa sana hapa. Nataka kujifunza mengi bado nikiwa mgeni, ili
isichukue muda mrefu kuweza kuaminiwa kwa makubwa. Kwa hiyo ni uamuzi
wangu, hakuna wakunikatalia.”
“Au
nikazungumze na mtu wa MOI akusubirie jioni ukitoka kazini?” Bado akasisitiza iwe
mapema. “Usiwe na wasiwasi Vai. Mguu ni wangu mpaka
kifo changu. Acha unisubirie tu.” “Eti nakuonea huruma, umesubiria muda mrefu
hivyo! Nataka ufurahi.” Bale akacheka. “Mimi
ninafuraha hata bila huo mguu.” “Utaongeza kitu.” “Najua. Lakini acha iwe siku
ya jumatano, hata Joshua nimeshamwambia itakuwa siku ya jumatano. Sitaki niwe
myumbishaji.” Hapo akaharibu kwa Vai. Akanyamaza, maneno yote
yakaisha.
“Mbona
kimya tena?” “Hata nikiongea chochote najua haitasaidia tena. Unamuheshimu
sana Joshua, Bale! Chochote kinachomuhusu yeye hutaki kiharibike!” Bale akanyamaza. “Kwamba upo tayari usiweke mguu leo, ambapo mimi nakushauri,
na nakuahidi kwenda kuzungumza nao wakusubirie mpaka uje, uondoke na mguu wako
leo hii, eti mpaka jumatano ilimradi tu, usibadili kwa Joshua! Hudhani kuwa
ataelewa!?”
“Nafikiri
si yeye moja kwa moja. Nataka kubakia mtu wa maneno yangu, Vai. Nisiyumbe
yumbe. Nikiamua kufanya jambo, nilisimamie kwa garama yeyote ile. Nipo kwenye
kujifunza uadilifu, kufikiri kabla sijaahidi au kupanga. Ili ikitokea nakosea,
basi nilipe garama mpaka nijifunze kufikiri vizuri kabla
sijatenda nikiwa nimepima madhara ya mpaka mbeleni. Tafadhali naomba unielewe.
Nimeshafanya haraka, na kuyumbayumba bila kuwa wa msimamo, nimeharibu mpaka baadaye
zangu. Inanigarimu sana mpaka hata sasa. Acha nijufunze kuwa mtu wa maneno
yangu.”
Alianza vizuri, lakini hapo katikati akampoteza tena. “Sawa.”
Vai akajibu akisikika anakubali ili yaishe tu hivyo.
Bale akajua. “Mbona kama umekosa raha?” Akataka kukataa, lakini
akaona aseme tu kwa njia ya swali. “Katika huko kufikiria
kwako kabla ya kupanga mambo, na mimi nitakuwa nikihusishwa?”
Bale akatulia akijua lazima kuongeza umakini akizungumza na Vai. “Maana kama ukibakia na aina hiyo ya msimamo kwenya maamuzi
yako ambayo unakuwa umeshapanga na kuamua kuyasimamia, na mimi nakuwa labda
nina wazo la tofauti, itakuaje sasa? Au huoni tena maisha yetu ya pamoja?”
“Naona Vai.
Basi niseme kuanzia leo, nitajifunza kukushirikisha mambo. Ili tuwe tunaamua
pamoja. Si ni sawa mke wa Bale?” Ikawa kama sabuni moyoni kwa Vai.
Ikaosha takataka zote. Akajisikia kupendwa haswa. Akacheka taratibu kwa
furaha. Bale huyo, anajua kujishusha bwana. Anayo nafasi nzuri kimaisha. Kazi
inayolipa vizuri kwamba kuna uhakika wa maisha ya kueleweka baadaye. Vai atake
nini tena! Akabaki akijichekesha.
“Unacheka
nini sasa?” “Nimefurahi kuitwa ‘mke wa Bale’.” “Si kushirikishwa kwenye
maamuzi?” “Mimi nataka niwe mke wako kwanza. Mengine naona tutawekana tu sawa.
Wewe sio mbishi.”
Bale akacheka akifikiria. Naya angemsikia huyu! Bale si mbishi! Hata Bale
mwenyewe akashindwa chakujibu, akabaki kimya tu, mwishoe madaktari waliokuwa wakiongoza
roundi hapo wodini wakarudi, Vai akaaga kwa haraka na kurudisha simu mfukoni,
akarudi kundini.
Siku Iliyokuwa Ikisubiriwa Kwa Hamu.
Bale alifika
hospitali ya Muhimbili majira ya 3:30 asubuhi na kwenda mpaka kitengo cha MOI,
akakuta Vai akimsubiria. “Sasa wewe nesi wangu, mida hii unasubiria mpenzi
huku, cheti tutapata kweli?” Alikuwa amevaa sare zake za kiuuguzi. Akapendeza
mwenyewe! Akacheka. “Nisingeweza kukosa. Nimeomba ruhusa. Usiwe na wasiwasi. Sasa
mbona umependeza hivyo!” “Mbona unaongea kama si kitu kizuri?” “Mimi naona wivu
bwana! Ndio kila mtu anakuona hivyo?” Bale akazidi kucheka. “Usijali.
Nakuwakilisha vizuri.” Akajua kumpatia Vai, akawa akiishiwa manung’uniko.
“Kama hivyo sawa.
Nishaingia ndani. Nishampanga kila mtu, hapa unasubiriwa wewe tu.” Bale akavuta
pumzi kwa nguvu na kuzishusha tararibu. “Mbona hufurahii tena?! Ujue kuanzia
leo hutahitaji tena gongo. Unarudi kutembea kama kawaida. Yaani ukitoka kwenye
ule mlango pale, unatoka bila gongo kwa kuwa umeshafanyiwa mazoezi yote na wote
wanakusifia unafanya vizuri.” “Najua. Lakini naomba usiingie na mimi ndani.
Nisubirie nje mpaka nitoke.” Vai hakuelewa. “Kwa nini?!” “Naomba tu usiwepo
Vai.” “Kwa nini?” Bale akasita. Vai akaumia sana.
Akaona bora tu
amwambie hofu yake. “Sitaki kukuvunja moyo Vai. Ili kama ikitokea sijafanikiwa
kutoka na huo mguu, isikuumize. Najua na wewe ulikuwa ukiusubiria huo mguu kwa
hamu.” Vai akaumia sana. “Nafanya kwa ajili yako Bale. Uwe na mguu, usiwe na
mguu, mimi nitabaki kukupenda hivyohivyo. Sitajali. Nitasimama na wewe
katika kila hali, na si kwa hili tu. Ni katika kila jambo. Mimi ni wako Bale.”
“Basi twende wote ili nipate pakuegemea endapo chochote kisipokwenda kama
tunavyo tarajia. Huu mguu ni wa garama sana, Vai. Kila mtu anausubiria kwa
hamu, hata hao waliokuwa wakinifanyia mazoezi wanausubiria kama kitu cha ajabu
sana. Nahofia kusije haribika jambo. Ukawa ni mguu sahihi lakini mguu wangu mimi
ukashindwa kuupokea. Itakuaje?”
“Naomba tusiazime matatizo ya baadaye
Bale. Sasahivi, tuliposimama hapa, mimi nimefurahi kukuona wewe, na wewe
umefurahi kuniona. Tupo salama. Si wagonjwa. Maisha yetu yanaendelea kama
kawaida. Ukiwa na mguu, usiwe nao, sisi tupo sawa. Hakuna
kitakachoharibika. Naomba matatizo ya baadaye, tuyaache yabakie hukohuko
baadaye.” Hilo ndilo alilompendea Vai. “Ni sawa?” “Naona upo sahihi. Twende. Na
asante kunifariji.” Wakaongozana mpaka ndani.
Haikuchukua muda
mrefu. Mguu wenyewe ulikuwa laini kiasi ya kwamba haukuleta maumivu yeyote kwa
Bale. Akatembea nao bila shida. Baada ya muda mfupi sana, wakaruhusiwa. Bale
akatoka akitembea asiamini Mungu amemrudisha kwenye kusimama wima kama zamani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakatoka, na kumkuta
Joshua na Jema wamesimama nje, pembeni kidogo kama waliokuwa wakiwasubiria.
Walishituka, hawakutegemea. Yeye Bale kashituka kumuona Joshua pale. Maana
tokea siku ya jumatatu alipomrudishia majibu ya, ‘Anytime.
Hongera.’ Hakumsikia tena. Ndio anamuona ametokezea hapo, muda na
siku ileile aliyomwambia angekwenda kuwekewa huo mguu. Hamjui Jema. Kwa
upande wa Vai yeye akashituka kumuona wifie pale na mtu mgeni kwake, hamjui
Joshua. Wote wakabaki na mshangao wasijue wanashangaa watu wawili tofauti, waliopo
pamoja. Bosi na msaidizi wake.
“Tulikuwa na kikao
maeneo ya Posta mpya, kilipoisha tu, nikamuomba Jema muda mfupi, tupitie hapa
ili nihakikishe kila kitu kimeenda sawa.” Muda wote huo Bale macho kwa Joshua,
asiamini. Bwana Joshua akiwepo mahali huwa uwepo wake unatoshea.
Alivyonyooka! Kisha kusimama kimamlaka kama anayejua yeye ni nani! Safi.
Kuanzia utosi mpaka kiatu alichovaa. Hapo amesimama tu, amejiwakilisha vilivyo.
Nadhifu haswa.
Vai akazidi
kuchanganywa. Jema amemjuaje Joshua! Kwa nini Joshua amuombe Jema muda?! Na
Jema naye akabaki amepigwa na butwaa kuona wawili hao bado wako pamoja! Hakujua
kama baada ya mumewe kuwasha ule moto,
bado wawili hao wangebaki kwa ukaribu ule tena wa kushikana mikono! Akabaki
kimya akiwatizama.
“Usinge hangaika
Joshua!” “Sio usumbufu hata kidogo. Nimefurahi kukuona unatembea vizuri aisee.
Kumbe kweli mazoezi yanasaidia! Hongera.” “Halafu mguu wenyewe mzuri kila mtu
alikuwa akiushangaa pale. Wenyewe wanasema hawajawahi ona mguu kama huu kwa
macho ila tu mitandaoni. Imekuwa ndio kwa mara ya kwanza kuingia hapo kwao. Unanisapoti
vizuri, sihisi maumivu hata kidogo. Nakushukuru Joshua.” “Nimefurahi kama
umefaa.”
Akamgeukia Vai. “Kwa
ushikwaji huo mkono, naamini wewe ndiye Vai.” Wakacheka na kujiangalia vile
walivyoshikana mikono, wakaachiana kwa haraka. Hawakuwa hata wanajua kuwa
wametoka wakiwa wameshikana mikono. “Ndio.” Vai akajibu akicheka kwa hofu
kidogo, akijua Joshua anajua alimuacha Bale na kujifungia hotelini na Victor.
“Bale, huyu ni Jema,
msaidizi wangu. Bila yeye, huwa kazi haziendi. Hapo alipo ananihesabia dakika,
nitoke hapa. Kuanzia naingia kazini mpaka natoka, kila dakika yangu yeye ndiye
anayeipanga nini chakufanya. Na pia ni mke wa James. Yaani wifi yake Vai.” Bale
alishituka, mpaka akapaliwa na mate. Akaanza kukohoa mfululizo baada ya kusikia
ni mke wa James. Joshua akajua.
“Aisee pole sana.
Jema ana maji kwenye gari.” Jema ndio akajua anatumwa maji. Akatoka hapo kwa
haraka. Wakawa wakimfuata nyuma. “Naamini kila kitu kitakuwa sawa.” Wakatoka
nje wakakutana na Jema naye anarudi na chupa ya maji. Akamkabidhi Bale.
“Nashukuru. Ila nataka ujue, sipo kumchezea Vai. Nampenda Vai. Na najua
simstahili kwa jinsi nilivyoishi nyuma, lakini Jema, nilikosa, na nimekusudia
kubadilika.” Wote kimya, Jema hakutegemea.
“Kwamba kumbe huyu
Bale ndiye anayevunja ratiba za Joshua, asubuhi hii muhuimu hivi, ili aje
kumuona yeye!”
Hakutegemea kama Joshua ndio yupo karibu hivyo na Bale. Joshua bosi wake. Naya
besti wake lakini hakutaka kabisa kuzungumzia Bale, ila na yeye alishajua
hawana mahusino mazuri kwani Naya alishamueleza ubaya aliotendewa na kaka yake.
Akaingiwa hofu fulani hivi. Akajikaza na kumgeukia Joshua. “Zimebaki dakika 5
tu. Tafadhali nakuomba usizidishe. Sitakuwa na muda mwingine tena. Natangulia
garini.” Akaondoka Jema. Hapo alipo alikuwa amependeza haswa. Kiatu cha juu
kama kawaida yake, usingejua kama ni mama JJ. Akaacha hapo harufu nzuri ya
manukato.
Joshua na yeye akaona
aage. Hawakuwa mbali na gari. Wakati anakaribia gari, Vai akamuita. Bale
hakutegemea. Akamkimbilia akimuacha Bale nyuma. Joshua akageuka akiwa
amekaribia gari. “Nampenda Bale. Sipo kumtapeli. Najua ulijua nili nili..” Akasita
mbele ya Joshua akiwa anatetemeka. “Nimemuomba msamaha. Na nimebadilika.”
“Labda nikuulize Vai. Maana sitaki ucheze na hisia za Bale.
Unaweza kuwa umesikia mabaya mengi sana juu yake, ikakufanya ubweteke.” Akaanza
Joshua kimamlaka na kuzidi kumtisha.
Jema akiwasikiliza tu
ndani ya gari maana alikaa kiti cha mbele na dereva, Joshua hukaa nyuma, wao
wasijue kama wanasikilizwa na Jema. Maana wakati wote hawazimi gari. Inamaana
vioo vimefungwa kwa ajili ya A/C. Joshua akajua dereva na Jema hawatasikia
mazungumzo yao, akawa huru kuzungumza na Vai. Kumbe Jema kwa makusudi alishusha
kidogo kioo ili kusikiliza anachotaka kumwambia bosi wake. Vai naye hakuwa
akimuona kwakuwa alikuwa amezibwa na Joshua mbele yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Vai
Mbele Ya Joshua. Joshua Anataka Kumuuliza Nini Vai ? Atafanikiwa
Kujibu Maswali Ya Joshua na kumshawishi?
Jema Naye Amegundua Umuhimu Wa Bale Kwa Joshua. Itabadili
Kitu?
Itaendelea.
0 Comments:
Post a Comment