“Ni vile nilishindwa
kutamka Vai. Ila nahisi mimi hisia zilibadilika muda mrefu hata kabla yako.
Hayo mashaka uliyonayo sasahivi, yakutokuzaa, mwenzio nilishahesabu sio kitu.”
“Bale!” “Ukilinganisha na vile ninavyokupenda! Hakika mimi sitajali, hata Joshua
nilimwambia. Na ndio maana nilikwambia nilijilaumu ulivyoondoka. Nikajiambia
ningekwambia mapema, pengine,…” “Wala si pengine. Ni nisingeondoka Bale. Mimi
nakupenda sana.” Bale akacheka.
“Nakupenda Vai.” Vai
akacheka. “Sasa hivi nimefurahi. Nimekusikia.” “Nakupenda na ndio maana
nakujali wewe tu. Sijawahi jali mwanamke hivi, nafikiri ndio maana haikuchukua
muda mrefu kujua wewe nakupenda.” “Sasa utafanyaje swala la watoto?” “Hivi
umeshajua kuna yatima wangapi wanalelewa kwenye vituo vya Yatima hawana
wazazi?” Vai hakutegemea.
“Bale!” “Ni kiasi cha
kuamua jinsia, umri kisha kwenda kuomba. Hata ukitaka wakuanza kunyonyesha
mwenyewe, utapata. Ukitaka wakiume au wakike, utapata. Si lazima ubebe mimba
ndio uwe mama, Vai. Usifungwe hapo. Sisi tukipanga idadi ya watoto tunaotaka,
na jinsia zao, na muda, tunaanzisha tu familia bila shida.” Vai alihisi mwili
unatetemeka.
“Unanielewa? Kwamba
ukitaka baada ya ndoa tuanze na wakiume, mchanga kabisa. Ukataka uanze
kunyonyesha mwenyewe, tunaanzia hapo. Tunamchua huyo. Anakuwa wetu. Tukiwa
tayari na wapili, hivyohivyo kama tunao kwenda kupata leba, ila inakua Mungu
amewapitishia tumboni kwa mtu mwingine. Wote tunakua tunatumia ubini mmoja,
wanakua chini yetu. Tunawalea kwa kadiri Mungu atakavyotuwezesha. Wanakua wetu.
Basi.” Vai alipatwa na baridi iliyomfanya afe ganzi. Akabaki kimya.
“Unaona hapa
ninapolala?” Vai kimya. “Ukiwepo hapa nyumbani, mto nageuzia upande huu, macho
pale mlangoni unapolala. Hata kama sina usingizi, haichukui muda nalala,
nikijua Vai wangu yupo sehemu salama. Na hivi unalalaga wakati wote unaniacha
nacheka hapa, ndio inanifariji vilivyo Vai. Sikukuzwa sehemu yenye amani
hivi. Sio kila wakati niliona wazazi wangu wakicheka kama hivi sisi. Vai wewe
unaridhika kwa kila jambo, hata maji! Kweli watoto hawa wanakuja na kupita
mikononi kwetu ndio watutenganishe! Mimi nimekataa. Ni bora kuwa na wewe,
na haya maisha yetu. Acha mengine iwe ni baraka za nyongeza tu. Nimeridhika na
wewe hivyo ulivyo.” Vai hakutegemea.
“Kumbe ni afadhali
nimezungumza na wewe Bale! Sasa ulipanga haya yote uje uniambie lini!?”
“Ukimaliza chuo.” “Bale wewe! Hudhani kwamba nilitakiwa kusikia haya mapema?
Ili nitulie. Swala la kutokuzaa lilikuwa likininyima raha mpaka ujasiri mbele
za wenzangu! Lakini sasahivi umebadili mtazamo wangu kabisa. Nashukuru.” “Sasa
sio utoke hapa, uende kwa mwingine, umpe wazo langu, mkaanzishe naye
familia.” Vai alicheka sana.
“Maana wanadamu
hamkawii! Familia ni mimi na wewe Vai.” “Si rahisi hivyo Bale. Ni mpaka mtu
akubali na kupokea kama hivyo wewe. Kwani yatima wameanza leo? Wanaolilia
watoto si wapo tokea vizazi na vizazi? Lakini wengi wanateseka wakiingia kwenye
ndoa. Manyanyaso. Wanaume wakitaka watoto waliozaa wao wenyewe. Mimi nishahidi
Bale. Mwanaume huyu wa mwisho, nilikuwa siwezi hata kulala kwa raha. Hakuna
tunachozungumza isipokuwa kushika kwangu mimba. Mchana na usiku ndio swali.
Nilikonda kwa wasiwasi.”
“Basi huo ukurasa
tunafunga kabisa. Tushajua ni sisi tu. Wengine wataongezeka juu yetu. Tena
tutachagua sisi kwa muda na nafasi yetu.” “Umenitua mzigo! Ni vile tu hujui
Bale. Na milele nitakukumbuka kwa hili.” Bale akacheka akimwangalia.
Wakawa kama hawajui wafanye nini, mwishoe Vai akanyanyuka kwenda kulala.
Akaenda kujilaza
kitandani akitafakari. Akasikia Bale akichechemea kuelekea hapo chumbani.
Akagonga taratibu. “Umeshalala?” “Bado. Ingia.” Akafungua mlango. “Natamani
kama…” Akasita. Vai akatoka kitandani akitamani hata amkumbatie. Japokuwa
alikuwa amesimama kwa kusaidiwa na gongo, lakini Bale alilipa. Akajisogeza
mpaka mwishoni mwa kitanda na kukunja miguu akimtizama kwa upendo.
“Nakupenda Vai.”
Akajua hilo silo lililomleta. Vai akacheka taratibu na kuinamia magoti akaanza
kuchezea vidole vyake vya miguu taratibu Bale akibaki kumtizama kama
anayejishauri. Mwishoe akamsogelea. Akakaa pembeni yake.
“Haraka zimeniponza
kwenye mengi, na wewe ni shahidi.” Akaanza Bale taratibu. “Hapa nilipo hisia
zangu zinanituma mambo mengi, lakini naomba tusubiri Vai.” Hilo hakulitegemea.
Alijua kufunguliwa kule kwa mlango, hatimaye usiku huo atampata Bale ambaye
moyo wake ulishampenda kupita maelezo. “Tafadhali naomba unisubiri mpaka ndoa.”
Akamalizia hivyo na kukata hisia zote za Vai. Akabaki ameinamia magoti ila
akaitika kwa kichwa kukubali.
Bale akamuona vile
alivyo nyongea. “Umekasirika?” “Hapana. Ila najiuliza ni lini hiyo ndoa!” Vai
hakutaka kujivunga. “Ukimaliza tu chuo.” “Kwamba mpaka mwakani!?” Hilo swali
likamfanya Bale asielewe. Vai ni mwanafunzi. Ila akaona aulize. “Nilifikiri
unataka mpaka umalize chuo.” “Mimi naona ungemuuliza tu muolewaji.” Bale
alicheka sana. Hakutegemea.
“Sasa wewe unasema ulifikiri,
wakati mimi mwenyewe nipo hapahapa!” “Sawa Vai. Wewe ulitaka kuolewa lini.”
“Kama na wewe, hata kesho.” Bale akabaki ametoa macho. “Mimi kwako
sitajivunga.” “Na chuo!?” “Kwani mbona nipo hapa na bado chuo nakwenda?
Unanisaidia kusoma na mambo mengine mengi tu.” Vai akaendelea. “Nimeishi na
wewe hapa mbona hushangai hata likizo nilikuwa hapa na hakuna aliyenitafuta?” Hilo
likamfanya Bale afikirie.
“Nimeugua hapa
mara ngapi, na mbona usimuone mama yangu kunitafuta ili aniuguze ila wewe ndio
umehangaika na mimi mchana na usiku?” Hilo nalo likawa kweli. “Mimi nataka
unioe, nitulie na wewe, wajue Bale ana mke wake kihalali, waache kukuvizia.”
Bale hakutegemea. “Nani anivizie mimi?!” “Huko unakofanya kazi, unavaa vizuri
sana, unapendeza na kuvutia, kanisani pia. Na huko unapokwenda kufanya mazoezi
na kuacha misuli wazi, wadada wakikuangalia.” Bale akaanza kucheka, asitegemee
wivu wa Vai kwake.
“Mimi nataka unioe,
mimi, Bale. Katika hilo wala sitasubiri.” “Wazazi wakikataa?” “Kwani unawaoa
wao?” “Vai!” “Hakika sikusubiri Bale. Chelewachelewa nitakuja kukuta mwana
si wangu. Mimi nitakuja pata wapi mwanaume anayenipenda hivi kama wewe?”
“Nitakusubiri.” “Basi mimi sitaki unisubiri. Nataka unioe.” Ilibidi tu
Bale acheke akifikiria.
Ikabidi tu kuuliza.
“Tunaanzia wapi?” “Kwa kaka. Twende nikupeleke kwa kaka. Mfahamiane.
Akishakuona sio muhuni, na mimi nikamwambia nakupenda, kisha nikaomba unioe,
najua atakubali.” “Sasa mbona unazungumza juu ya kaka na si baba!?” “Wazazi
wetu wamempa dhamana kaka, anayo mamlaka naweza sema hata baba hafanyi kitu
bila kumuuliza yeye. Sasa bora tuanzie kwake. Akikubali yeye, ujue kwengine
huko ni taarifa tu.” “Sawa.” Bale akakubali bila shida.
“Lini sasa?” “Mama
unataka ndoa wewe!” “Hakika na wewe, Bale, NATAKA. Tafadhali nioe nipumzike.”
“Na mimi najua nitapumzika Vai. Namaanisha nikikwambia nakupenda.” “Basi sasa
si unioe tu?” “Mimi sina kipingamizi. Wewe ndio familia nzima niliyo nayo, na
Joshua. Na yeye anajua nakupenda wewe. Kwa hiyo mimi nakuachia wewe
uongoze mambo, niambie tu chakufanya mapema ili nisimshitukize Joshua.” “Sawa.
Basi ngoja nimtafute kaka kesho, nimuombe twende kwake.” “Sawa.” Acha Vai aanze
kushangilia hapo mbele ya Bale, Bale akicheka.
“Wewe cheka tu. Ni
mpaka upite nilikopita mimi, kisha umpate mtu kama Bale, ndio utanielewa.
Nilikuwa namwambia Victor, Bale wangu ananipikia kisha anakuja kunichukua chuo
nikale.” “Naona umeniuzauza huko kwa Victor!” “Mwenzio nilikuwa natamani ageuke
awe wewe, ndio niwe naye pale siku ile. Nakupenda Bale wangu, halafu kuna jinsi
umenizoeza, sina jinsi nikawa na mwanaume mwingine nikaridhika.” “Basi kweli
tuone tu.” Wakajipanga hapo ndipo wakaagana kulala.
Shemeji.
Dunia Duara.
Watu husema hujui
utakayekutana naye kesho. Dunia ni ndogo sana. Kuwa muungwana hata kwa mtu
unayepishana naye barabarani, maana huwezi jua hata dakika tano ya mbeleni.
Unaweza anguka hapo barabarani, yeye ndio akawa mtu wa pekee wa kukusaidia.
Ilikuwa majira ya saa
11 jioni wakati Bale na Vai wakigonga mlango wa nyumbani kwa aliyekuwa kaka
yake Vai. Maana walifunguliwa geti na mlinzi wa zamu, Bale akavuta gari mpaka
karibu na nyumba. Alikuta magari matatu hapo nje. Akahisi kuna wageni wengine
ndani. Akatembea vizuri tu na gongo lake mpaka mlangoni, Vai akamtengeneza
shati vizuri na kumkaribisha kabla hajagonga mlango.
“Mkewe mpole sana,
wala usiwe nawasiwasi.” Akajaribu kumtia moyo. Bale akavuta pumzi kwa nguvu na
kujipanga hapo mlangoni kuja kukutana na kaka mtu ambaye alipewa heshima na Vai
kuliko hata baba yake. “Wana mtoto mdogo, tusibonyeze kengele mara mbili,
tusije muamsha.” Vai akanong’ona.
Mara mlango
ukafunguliwa. Ila ikawa tofauti na matarajio ya Vai. Kaka yake alishituka kana
kwamba ameona jini mnyonya damu. “Unafanya nini hapa nyumbani kwangu wewe
Bale!?” Vai akakunja uso na kumtizama Bale ambaye alibaki ameduaa na yeye.
“Mimi sijataka ubaya
na wewe Bale, ndio maana uliniona nimekaa mbali na wewe tokea mwanzo kabisa.
Sina ubaya, na sitaki matatizo na wewe.” Vai akashangaa sana. “Kaka James, huyu
ndio mwanaume nilikwambia nitakuletea leo mfahamiane!” “Umechanganyikiwa wewe
Vai!?” James alishakuwa mwekundu na alionekana ameingiwa hofu haswa.
“Unamleta huyu
nyumbani kwangu kwa mke wangu na mtoto?! Kweli?” Wazi James alionekana
amepaniki. “Nimekufanyia nini mimi? Kwa nini unataka kuleta matatizo nyumbani
kwangu?” “James, sijaja kuleta matatizo.” “Mwanzo ndio kunakuaga hakuna
matatizo wakati lako likikuendea sawa. Lolote likikaa vibaya,
likaenda visivyoendana na wewe, huna ubinadamu Bale. Kila mtu
anakufahamu. Unageuka katili kuliko simba. Huwezi kujizuia. Huna mipaka. Si kwa
baba yako mzazi, wala ndugu mliozaliwa tumbo moja! Unaadhibu kwa kuangamiza.”
“Ndio maana mimi
umeona nilijitenga kabisa na wewe. Sikutaka matatizo kabisa na wewe. Sikutaka
kwa la kheri wala la shari. Kweli leo Vai unakuja kumleta huyu karibu na
familia yangu!?” Vai alibaki kimya akitetemeka kama kifaranga kilicholowa maji
kwenye baridi kali. Yeye na dada yake wanamuogopa sana James. Kuliko hata baba
yao mzazi.
“Uliahidi kubadilika
na kutulia Vai. Haya ndio mabadiliko yako?” “Tafadhali usimlaumu Vai, James.
Bale aliyekutana naye yeye, siye unayemfahamu wewe. Nimebadilika na nime…”
“Basi, kama kweli umebadilika, tafadhali ondoka kwangu. Na naomba
unapoondoka, iwe amani Bale. Mimi sitaki vita na wewe wala visasi. Sitaki
ugomvi tafadhali.” Ikawa kama anamsihi kwa hofu.
“Naomba amani kati
yetu ila isiwe kunifuata kwangu wala karibu na familia yangu. Hata katika haya
kama lipo limekukwaza, naomba nikuombe radhi. Ondoka kwangu kwa amani kabisa,
kaendelee na maisha yako.” “Nimebadilika James na nampenda Vai.” “Tafadhali
ondoka Bale. Hata kwa wazazi wangu naomba usifike. Nakuomba kwa heshima kabisa
bila ugomvi wala kisasi. Kaa mbali na familia yangu.” Kwa hakika hilo
alisisitiza.
“Waache wazazi wangu,
hata wao hawajakufanyia kitu. Tafadhali nakusihi Bale. Kuwe na amani. Uondoke
na usinitumie majambazi wala moto wa kutetekeza familia yangu. Mimi sitaki
ugomvi na wewe, na nimekuaga hapa kwa amani kabisa, na Vai nishahidi.” Bale aliumia
sana. “Tafadhali sana.” James akaendelea kusihi. Bale akaona aondoke tu.
Akachechemea kugeuka
aondoke. “Bale amebadilika kaka.” “Unamjua
alivyokuwa kabla?” Akasikia kaka yake akimuuliza Vai kwa ukali. “Nakuuliza Vai?
Unamjua Bale wewe?!” Bale akaendelea kushuka ngazi, Vai akimtizama machozi
yakimtoka. “Unaongea ujinga tu. Ulikuja hapa, ukazungumza hivihivi kuwa safari
hii unatulia mpaka umalize chuo. Hata hujafika nusu ya chuo, umerudia tabia
zako zilezile za wanaume. Unashida gani Vai wewe?!” Akaanza kumgombesha.
“Yaani chuo cha miaka
miwili tu, kinakushinda kutulia na kumaliza! Unataka nini kitokee maishani ili
utulie. Unajua alichofanya familia yake huyu?” “Amenisimulia,
na …” “Unajua alichomfanya mtu aliyekuwa rafiki yake kipenzi, mtu wake
wa karibu, pale walipopishana naye?” Vai akaendelea kulia.
“Huyu mtu ni mwema
jambo lake linapomuendea sawa. Hana msamaha kwa yeyote aliyekuwa kinyume naye.
Na ikifika kwenye hasira yake, hana anayemuangalia. Anateteketeza. Ndio
maana mimi nimeishi naye mbali kabisa. Nilijitenga naye. Lakini wewe umeenda
kuniletea matatizo nyumbani kwangu! Unaleta msiba kwenye ukoo wetu!” “Bale amebadilika kaka. Na yupo kanisani ana…”
“Kwani baba yake mzazi, rafiki yake na ndugu zake aliwachoma moto akiwa wapi?!”
James akamuuliza kwa ukali akimshangaa sana.
“Wewe vipi Vai? Unaongea
nini? Alikuwa kanisani akipiga kinanda na muimbaji kabisa! Akaua familia
yake yote, si kwa sumu! Aliwateketeza kwa moto kabisa. Yaani kuwaunguza
mpaka kifo, akabaki na mtu aliyekuwa aking’ang’ania ni mwema. Naye alipompinga
tu na kuwa kinyume naye, alimteketeza kwa moto. Kama nadanganya, muulize
mwenyewe.” Vai akazidi kulia akiwa nje ya mlango, kaka yake amesimama mlangoni
kama anayeulinda baya lisiingie.
“Kama huniamini,
muuulize ni lini aliijua dini unayodhani anayo sasahivi. Swala la kanisani si
jipya kwake. Amezaliwa na kukua kanisani. Acha upumbavu wako. Anaye dada yake.
Lakini hata yeye anamuogopa, muulize hata kama anafunguliwa milango ya kwa
familia ya dada yake na wanaishi hapahapa Dar. Bale ni tishio, kila mtu
anamfahamu. Kweli unakwenda kumzoa huko na kumleta kwangu! Hakika sitakusamehe
Vai. Ondoka, na wewe hapa usirudi. Tutakutana kwa wazazi. Ila, usiwahi
hata kumuonyesha mlango wa nyumba ya mama, au kwa baba. Unanielewa Vai?” Vai
alikuwa akilia sana maana kaka yake alikuwa akichemka haswa ila anagomba kwa
sauti ya chini kama anayeogopa Bale asimsikie ndani ya gari.
“Hakika hatika hili
nitataka uniahidi Vai. Maana wewe mtoto ni kama umekatwa masikio. Husikii la
yeyote. Umesikia?” Akamvuta kabisa, Vai akazidi kulia mpaka Jema akatoka.
“Naomba muachie. Tafadhali James. Mwache.” Akamwachia. “Sawa Jema. Lakini katika
hili naomba zungumza naye na akujibu kama amesikia na kunielewa. Sitaki
ampeleke huyu mtu kwa wazazi.” “Atakuwa amesikia. Eti Vai?” Akatingisha kichwa
kukubali.
“Haya ondoka. Na
ukahakikishe Bale hatufuati nyuma. Sina ugomvi naye. Ondoka Vai.” James
akamfukuza Vai kwa sauti ya chini ila ya kitisho haswa, huku akiangalia
lilipokuwa gari la Bale. Jema akamsaidia kumshusha ngazi kwani alikuwa akilia
haswa. “Taratibu usianguke.” Jema akawa akimwambia huku amemshika mkono.
Alipomfikisha chini ya ngazi akamuachia, Vai akarudi garini, wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kilisikika kilio cha
Vai tu garini. Bale akaendesha akiwa amepigwa na butwaa hajui aseme nini, mpaka
kwake. Vai akashuka garini moja kwa moja
akaingia chumbani na kujitupa kitandani. Bale akamfuata. “Naomba nisikilize
Vai.” Akageuka akilia sana. “Alichozungumza kaka yako, si uzushi. Ni
kweli kabisa. Na ndio maana hata yeye nimemwambia, yeye anamzungumzia Bale wa
zamani, wewe unamfahamu Bale wa sasahivi. Kaka yako anafanya yote hayo kulinda
familia yake au yenu, kitu ambacho mimi nilishindwa. Mtoto wa kiume wa kwanza,
kama yeye tu, lakini yeye yupo kwenye kujenga na kulinda, mimi niliangamiza
familia yangu.”
“Yupo sahihi na
katika hili, nimemuheshimu zaidi.” Vai hakutegemea. “Kwamba
unaniacha Bale!?” Bale akatulia akifikiria. “Hunitaki
tena?” Vai akarudia swali. “Hapana. Huko tulishapita Vai. Ila kuna kitu
Joshua aliniambia hata juu ya Naya. Mungu hana shida na kusamehe, endapo
ukitubu kwa dhati. Nimesamehewa na Mungu anayeona sirini. Lakini aliniambia, sitaacha
kulipa garama ya makosa yangu.”
“Kwa Naya nilielewa
na kuamua kumuacha kabisa kwa kuwa kwanza, hakuna jinsi nitakwambia, nafasi
alizonipa Naya kujirudi hata kipindi cha uhai wa baba yetu, nikashindwa
kujirudi kabisa. Naya anakumbuka hivyo vipindi vyote. Alifanya kwa hasira,
upendo mpaka kunibembeleza, nitulie na kusubiri, lakini ilishindikana.
Nikaharibu vibaya sana. Nimempokonya Naya, baba yetu ambaye hakuwa akijua
kuishi bila yeye. Na najua maisha yake hayatakuja kurudi kuwa sawa, hata
iweje bila baba. Labda katika ulimwengu ujao. Nimemkatili vibaya sana mpaka
wakati mwingine natamani ubaya niliomfanyia baba ndio angekuwa mama, useme
alizungumza kitu, akaniudhi. Baba yetu alikuwa mkimya sana, Vai. Nilimdhihaki
na kumdharau vile nilivyotaka, lakini alikuwa kimya kabisa.”
“Kingine
kinachonifanya nimuache Naya, ni ubaya niliomtendea yeye mwenyewe hata baada ya
kifo cha baba. Ilikuwa mbaya sana Vai. Mno. Mimi mwenyewe nilikuwa
nikikumbuka, siwezi kulala. Hayo yote, James kaka yako anayajua si kwa
kusimuliwa, ni kwa kuishi kwenye hayo maisha akishuhudia kupitia Geb ambaye ni
kama Joshua tu. Chochote kinachoendelea kwa Joshua ujue ni Geb, na Geb ni
rafiki wa James tokea shule ya sekondari na akaja kumuoa mdogo wa James.” “Ni Nanaa. Tumekua pamoja.” Vai akamsaidia.
“Ewaaa! Nanaa. Kwa
hiyo kwa kifupi, alichozungumza James, au ilipo hofu ya James, si kitu cha
kufikirika, amenishuhudia nikitenda ubaya wa kupita kiasi.”
“Cha mwisho
kinachonifanya niwe mbali na Naya, ni mumewe. Joshua katika hilo ameweka
msimamo wa waziwazi kabisa, ni mpaka Naya mwenyewe atakaponitafuta.
Hapa nilipo nazungumza na Joshua kila kitu, kasoro mambo yake na Naya. Hajawahi
hata kuropoka kumzungumzia Naya kwangu, mara chache nikitaka kujua hali yake,
jibu ni, ‘anaendelea vizuri’ au ‘Mungu anasaidia’, basi. Sijui alivyo, sijui chochote
juu yake. Mimi, Bale, nimesababisha kweli ukoo mzima hawatutaki.”
“Lakini kuhusu wewe,
wewe ni maisha yangu ya sasa na ya baadaye. Sitakaa mbali na James. Ninataka
kuomba anipe nafasi.” “Hatuwezi kurudi tena kwa
kaka wala kwenda nyumbani kwetu, Bale. Katika hilo siwezi kumkaidi kaka.”
“Mimi sitamtafuta, ila nitarudi kupitia Joshua.” Hapo Vai akakaa.
“Kama alivyo Roho
mtakatifu wangu mbele za Mungu, akinisaidia kuomba maana mimi sijui, ndivyo
atakavyokuwa Joshua kwao. Joshua anajua ni kiasi gani nakupenda Vai. Anajua
nimebadilika kwa kuishi na mimi, maana alinipa nafasi. Na uzuri yeye
anaheshimika sana kwao. Nitazungumza naye na kumueleza ilivyokuwa, kisha
nimuombe ushauri na kuomba akazungumze na James. Nitaheshimu kauli za
James. Sitarudi kwake mpaka Joshua atakaponiambia yupo tayari niende.” Hapo Vai
akafurahi sana maana japo hajawahi kukutanishwa na Joshua, lakini alishapata
habari zake, akajua hakuna kitakacho shindikana. Alishajua yupo upande wa Bale,
na Mungu ni baba yake, yupo upande wa Joshua, akajua mpaka hapo, huyo Mungu
wake hata katika lao, atawarekebishia tu.
Kwa Joshua.
Ilikuwa mida ya
usiku, simu ya Bale ilipoingia. Joshua alipoona namba ya Bale, alikuwa na Naya.
Walikuwa kwenye wakati mzuri sana. Wawili tu, watoto wamelala. “Naomba nitoke,
nipokee simu ya Bale. Si kawaida yake kupiga mida hii. Lazima ni kitu muhimu.”
“Acha mimi niwapishe.” “Huna haja yakufanya hivyo. Acha mimi ndio nitoke.”
“Hata hivyo ninataka kula kitu, njaa inaniuma. Naona wanao wamenyonya chakula
chote.” Naya akanyanyuka pale alipokuwa
amemlalia mumewe na kuelekea jikoni.
“Kwema?” Joshua akapokea simu
na hilo swali. “Nimegundua leo kuwa Vai wangu, ni mdogo
wake wa mwisho James.” Joshua akafunga macho. “Nilikwenda
kwake leo, aisee ilikuwa mbaya sana.” “Pole sana Bale. Natamani ningejua kabla
hujakwenda kwake.” “Sikujua Joshua.” “Aisee James anakuogopa sana, na
alishaniita kikao mimi na Geb, akiwa na wasiwasi wa Nanaa ambaye
alishakugombeza, sijui kitu kama hicho.” Bale akawa hakumbuki.
“Alivyosimulia
Geb, maana na mimi nilikuwa sielewi, wanasema ulikwenda ofisini kwake ukiwa na
madai ya mali za baba yenu, ndio ukaishia kwa mkewe, sasa kaka yake alipojua,
aisee ilikuwa mbaya. Alikuwa na wasiwasi wa waziwazi na akataka
akaandikishe polisi kabisa ili chochote kikimpata Nanaa, wajue ni wewe, isiwe
kama Naya. Yalikuwa ni mazungumza ya muda mrefu sana akitupinga akisema mimi
nilizembea kufikisha taarifa zako polisi, ndio maana ulipomteka nyara
Naya, polisi walishindwa kunisaidia. Akakataa kurudia kosa kwa dada yake.
Ilibidi Geb amuonyeshe ushahidi wa kubadili ulinzi na umakini kwa dada yake.
Ndio kidogo akatulia. Sasa ukiniambia leo ulikwenda kwake!”
“Aisee
ilikuwa mbaya sana.” “Naweza kupata picha.” Kilichomtia wasiwasi Bale ni ukimya wa
Joshua kama ambaye na yeye hajui chakufanya. “Joshua!?”
“Tafadhali nipe muda nifikirie chakufanya Bale. Mimi nipo na wewe na nakuamini,
na ni kwa sababu nilipata neema ya kukupa nafasi ingine baada ya kutambua na
kujutia makosa yako. Nimeona mabadiliko yako kwa vitendo ndio maana unaona nakuamini.
Naomba na wewe umuelewe James na umpe nafasi. Yeye anamfahamu Bale wa zamani.
Hajabahatika kukufahamu Bale wa sasahivi. Itahitaji neema ya Mungu hata kuweza
kuwa karibu na wewe. James anakuogopa si kwa kujisingizia, ni kweli
anakuogopa HASWA. Tafadhali mpe muda.”
“Namuelewa
Joshua. Namuelewa kabisa. Ila nampenda sana Vai.” “Naelewa. Ila ujue Vai
amempenda mtu ambaye yupo kwenye kulipa garama. Haitakuwa rahisi, na
yeye ajiandae. Na usimfiche kitu ili aweze kukusubiri. Na kwa upande wangu nipe
muda. Usimtafute tena James wala kukamkaribia kwa namna yeyote ile mpaka nitakapokwambia.
Lini! Sijui. Nitakapokuwa tayari juu ya hili, nitakujulisha.” “Nakushukuru
Joshua. Na samahani kukuingiza matatizoni.” “Hapana. Ni changamoto tu na lazima
tutakutana nazo. Usipokata tamaa, utafanikiwa.” “Nitasubiri. Nitakusubiri
Joshua. Na nitazungumza na Vai. Uzuri ananipenda na yupo tayari kuwa na mimi.
Najua na yeye atakuwa mvumilivu.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya alikuwa sehemu
akisikiliza, walipomaliza akaingia na kumuona mumewe amebaki ameshikilia simu,
kama anayewaza. Akamuhurumia. “Pole Joshua.” Naya akamtoa mawazoni. Akamtizama.
“Naamini kila kitu kitakuwa sawa. Ni muda tu.” “Hivi ni kwa nini unahangaika
hivyo na Bale!? Mimi mwenyewe nipo kama James tu. Namuogopa kuliko kawaida.
Huyu mtu ni mwema, yake yakimuendea vizuri. Huofii atakuja kukugeuka pale mambo
yake yasipoenda kama anavyotaka yeye?” Akajua alikuwa akisikiliza.
“Joshua, huyu mtu ni
mkatili kuliko nitakavyokwambia. Hana utu wala ubinadamu pale anapotaka jambo
lake liende anavyotaka yeye. Alinitesa vibaya sana akiwa na Malon, bila
yakujali kama mimi ni ndugu yake! Na si mara moja, Joshua. Aliishi akinitesa na
akijua nateseka, kisha kuendelea kunitesa. Kweli
unapanga kumsogeza kwenye familia ya James isiyokuwa na hatia? Unataka kuleta
misiba kwenye ukoo wa kina James wabakie ukiwa kama ukoo wetu?” “Naomba
usilie Naya. Tulia nikwambie kitu. Njoo ukae hapa.” Naya akakaa.
“Naomba nikuulize
swali. Na ufikirie kabla hujajibu.” Joshua akamtuliza. “Kama baba Naya angekuwa
hai. Yupo pale Kiluvya. Unafikiri angefanya nini na Bale?” Naya akalia sana
akikumbuka jinsi baba yake alivyohangaika na Bale mpaka kifo chake. “Lakini kumbuka mwisho wake na huyu Bale, Joshua. Kweli
unataka tuangamie hivihivi?” “Simtetei Bale, ila kama ungepata nafasi ya
kumsikiliza Bale yule aliyekuwa na bangi kichwani, haogopi mtu. Nia yake ni
kuumiza watu akitaka kufikia yake, ndio ungegundua hakuwa amekusudia kuua.
Hakutaka kumuua baba yenu ila kama kumkomoa. Malon yeye ndio alikuwa na agenda
ya kuua, akatumia hasira ya Bale kutekeleza azma yake.”
“Na kumbuka wakati
huo Bale alikuwa ameshaharibiwa hata fikra yake na bangi. Alifanya kile bangi
inamtuma afanye. Sitetei, ila nataka ujue nilipopita mimi mpaka nikapata neema
yakumpa nafasi ya pili. Na kingine, huwa kila wakati najiuliza swali kama
nililokuuliza wewe. Kama baba Naya angekuwepo mwenyewe, angefanya nini?
Hilo ndilo linanifanya nisizembee kwa Bale, na nafikiri ndipo nilipobeba roho
ya ubaba kwa baba yenu Naya. Alikuwa yupo radhi kufa, ili akamuokoe Bale. Hakuogopa
mauti. Alikuwa tayari kukabili kifo, ilimradi tu akamuokoe Bale. Na ndio
katika kipindi hicho, ndipo nikapata sababu ambayo nimebaki na Bale
mpaka sasahivi.” “Sababu gani?” Naya
akauliza.
“Baba Naya akiwa
kwenye mfungo, akimsihi Mungu rehema juu ya Bale, aliniapisha mbele za Mungu,
juu ya watoto wake. Aliniachia nyinyi wote. Naya, yule mzee alinisihi mbele za
Mungu, nakunitaka nimuahidi sitakuja kubadilika kwa watoto wake. Nyinyi wote, ni
kama aliyekwisha ona mwisho wake tokea zamani. Akajua yeye atakufa, atawaacha
nyinyi watatu. Na alinipa uhuru wa kukataa. Lakini nikakubali. Nikijua
Mungu atanisaidia. Na ukweli sijawahi kujuta hata kwa Bale.
Hajanipa sababu ya kutomuamini tena tokea nianze kutembea naye. Mungu wake
amenionyesha waziwazi, amemsamehe na anatembea naye, mpaka
nikaona wivu juu yake.”
“Siku moja tulikuwa
hapa, ile siku tuliwaalika wakina Magesa na James waje hapa tumshukuru Mungu
kwa sababu ya wewe kupata ujauzito, likatokea lakutokea, kina Jema wakaondoka
baada ya Magesa kuzungumza vile na Jema. Unakumbuka nilikuaga nikakwambia lazima
nitoke nje nizungumze na Bale?” Naya akakubali akilia.
“Naya, sikuwa nikijua
ni nini kilikuwa kikiendelea kwa wakati ule, lakini Roho wa Mungu aliniambia
nilazima, nimpigie simu Bale, nimwambie bado hajamalizana naye. Na anao
mpango juu yake.” “Joshua!?” “Hakika
Naya. Na jinsi nilivyokuwa nimesukumwa, halikuwa jambo la kumwambia baadaye,
ilikuwa ni haraka. Ilinibidi baadaye, nafikiri hata mwezi ulipita, nilimuuliza
Bale ni nini kilikuwa kikiendelea usiku ule. Maana ilikuwa ni kama Mungu
anaokoa kitu.”
“Ndipo anasema
alifika mahali, alijawa na majuto, hofu akijua ameharibu sana hapa duniani,
hana jinsi ya kuja kutengeneza tena, amepoteza kila mtu. Na neno samahani
pekee katika ulimwengu huu halitakaa likatosha, akakusudia kujiua. Pale nilipompigia
simu, alisema alishakuwa tayari kujiingiza kwenye kitanzi, ajiue.” Naya
alilia sana.
“Sasa najiuliza, kama
huyu Mungu mwenye enzi YOTE, amemsamehe, na bado anamipango naye,
mimi ni nani mpaka nizuie, au kupinga au kutokubali kutenda kazi na Mungu?
Kwangu ni heshima Naya. Nahesabu Mungu ameniamini naweza kuhusika na mtu kama
Bale, akaleta mabadiliko. Na hata leo mimi nikikataa kusimama na yeye,
nakwambia kabisa, Mungu atainua mtu mwingine kutimiza kusudi lake, kama
kwa Sauli aliyekuwa akiua watu wa Mungu, kanisa, mpaka Yesu akamtokea na kumuuliza,
‘kwa nini unanitesa?’ Kuna waliosimama na Sauli,
ambaye ni Paulo, mpaka akafanya kanisa kusimama imara mpaka leo na kuna waliompinga.
Lakini si kusudi la Mungu limesimama?” Joshua akaendelea taratibu tu
bila kutaka kumtibua mkewe.
“Mimi nilikataliwa na
watu wa nyumbani kwetu. Lakini kusudi la Mungu kwangu si liliweza kutimia.
Utukufu wa Mungu unajitangaza kupitia mimi, mpaka mwenyewe huwa naogopa na wewe
ni shahidi Naya. Lakini Mungu mwenyewe alikusudia KUSUDI lake litimie kupitia
mimi, hata wale walionifahamu walipokataa, alitumia hata misikiti kunilinda, na
kugeka nyumba yangu ya kulala, japo makanisa yalishindwa.”
“Nilijua misikiti
inayogawa sadaka na chakula siku za ijumaa. Nilijua muda gani wa swala, muda
gani na wapi pakujificha nikalala salama mpaka asubuhi. Ninachotaka kukwambia
ni hili, hakuna wakuzuia kusudi la Mungu. Akiamua kufanya jambo
lake, kwa hata vile visivyostahili, hakuna wakumzuia. Ni aidha ukubali
kutenda naye kazi, ili akiwa anapita kwa mlengwa na wewe uliyekuwepo
karibu na huyo mtu upate hata vimanyunyu vya baraka. Maana mimi namjua
Mungu. Hawezi kukutumia bure. Anakutumia haswa, ila ni mzuri sana kwenye
malipo. Ila kama ukishindwa, ni bora ukae pembeni kabisa, mwache kusudi lake
litimie.”
“Ninachokuhakikishia
Naya, Bale ni Mungu aliyepo kazini na ipo siku watu watashuhudia kwa macho,
wasiamini kama Mungu anaweza kufanya jambo jipya kwenye visivyostahili.
Historia tunayoisoma juu ya Sauli, nahisi, Mungu anataka kuirudia, watu
waishuhudie kwa macho. Bale amebadilika, Naya. Ni msikivu, mvumilivu na
anaweza kufikiria mtu mwingine mpaka huwa wakati mwingine namuhurumia.”
“Alitakiwa kupata
mguu mwezi mmoja uliopita. Ule mguu ukawa tayari kwa ajili yake kabisa. Ukamfaa.
Siku aliyotakiwa kwenda kuwekewa, akakutana na mtu ambaye yeye hana mguu hata
mmoja na ule mguu ungemfaa yeye. Bale akaomba apewe yule mtu, yeye akasema
atasubiri. Hilo nimekuja kujua siku nimempatia kazi, aliponiomba aanze kazi
akishapewa mguu. Bila kufikiria nikamwambia, lazima aanze kazi mguu utakutana
naye mbele ya safari.”
“Maana nafasi yenyewe
ilinijia kimaajabu, nikajua tu ni Mungu wake ameamua kumpa hiyo
nafasi ya kazi. Maana ni kama huyo kiongozi wao wakitengo cha HR mwenyewe katika
mazungumzo yetu akawa akinilalamikia hilo pengo na kuniambia bado hajaweza
kuliziba, linamcheleweshea kazi. Moja kwa moja akili ikanikumbusha Bale. Ikawa kweli
ni yake, kwenda tu, wakampenda. Sasa jinsi alivyojiuza vizuri, nafikiri na
Mungu wake alikuwa amekusudia kumpa yaliyo juu, hakika wamemuanzishia
malipo na marupurupu ya juu sana, Bale mwenyewe alinipigia akilia kwa hofu. Hata
hakutegemea, maana alitaka kuwatajia pesa ndogo endapo wangemuuliza. Sasa turudi
mwanzo alipotaka asubiri mguu na mimi kumwambia asisubiri mguu. Akakubali japo
nilijua hataki kuonekana kazini ambayo ni sehemu ngeni, kama ni mlemavu, ila
akakubali.”
“Ndipo sasa baada ya
kama siku tatu mbeleni nikakumbuka alitakiwa awe alishakuwa na mguu! Ikabidi sasa
kumuuliza, ndipo akanisimulia hicho kisa. Kwamba aliona bora ampe yule jamaa
mguu, ili angalau na yeye aweze kusimama kama yeye. Sikutegemea Naya, kwa
sababu Bale alikuwa akisubiria kwa hamu sana huo mguu. Na nilikwisha
lipia, lakini Bale yule tuliyemjua ni mbinafsi, anaye angalia
yake tu, aliugawa ule mguu kwa aliyeona anauhitaji zaidi yake!”
“Anatembea na mguu
mmoja mpaka leo, akisaidiwa na gongo, na anafanya kazi bila malalamiko. Na huko
kazini kwake nimeambiwa na bosi wake, anajituma kupita anavyotumwa. Na mwepesi
kuelewa. Ila na mimi nilivyojua amegawa mguu wa kwanza, nimeagiza mguu wa pili
uje bora, kuliko wa kwanza. Umegarimu sana, lakini nimetaka uwe
na uwezo mkubwa, akiwekewa uwe na uwezo kama mguu wake. Usimchukue muda mrefu
kuuzoea. Hata leo akitaka kuwa mwanariadha wa dunia, basi huo mguu usimzuie.
Na nimefanya hivyo makusudi ili tu kumtia moyo.” Naya akaondoka kabisa hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Vai alipoambiwa
majibu ya Joshua, kwa upande fulani akakata tamaa. Hazai! Lakini Bale
amempokea. Sasa leo kaka hamtaki tena! Hilo likamnyong’onyeza kabisa Vai
aliyepewa uzuri wa namna yake, lakini hofu ya kushindwa kuzalia wanaume watoto,
ikamfunga nakubaki akijidharau. Hapo kwa Bale aliona ndio mwisho kabisa,
ukizingatia alishajaribu kwa wanaume aliodhani ndio wangemkimbilia! Waliokwisha
kuwa na familia zao, wanatafuta tu starehe! Victor akamrudisha chini kabisa.
Akabaki
amenyong’onyea. “Tafadhali tuwe wavumilivu, kila kitu kitakuwa sawa.” “Usije
nibadilikia Bale. Ukaona kwangu haviwezekaniki, ukakimbilia kwenye urahisi.”
“Siwezi kubadilika kwa sababu kwako sipo kwenye majaribio. Sitafuti tena
kwa kuwa nimeshakupata wewe. Hilo zoezi la wanawake kwangu nimefunga na
Mungu wangu ni shahidi. Katika hilo tafadhali usitie shaka.” Akazidi
kumbembeleza na YEYE akihofia Vai asije tafuta mwingine mwenye historia
isiyo kama wake. Ukizingatia uzuri wa Vai! “Hakuna mwanaume atashindwa
kumpokea kwa mikono yote miwili. Mimi mlemavu, halafu jamii inanihesabu ni
muuaji! Ataishi na hiyo historia ngumu mpaka lini!” Wawili hao wakajikuta kila
mmoja amekwama kwenye insecurities kwa sababu ya maisha waliyoishi nyuma
na kusahau thamani yao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kitakacho Endelea?
0 Comments:
Post a Comment