Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 1. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 1.

Akatoka hapo kwa Kasa akiwa amemchanganya zaidi. Akaegesha gari pembeni na kujaribu kumpigia tena simu Doro. Safari hii ikaita mara mbili na kukatwa. Akapiga tena. Ikapokelewa na matusi kwamba aache kusumbua watu kwenye starehe zao, kisha kukatwa.

Akufaaye Kwa Dhiki, Ndiye Rafiki Wa Kweli.

Akapiga tena na tena bila mafanikio. Akiwa katika kumsaka kwenye baa nyingine, simu ya James ikaingia. “Nina hali mbaya James, tafadhali naomba tuzungumze wakati mwingine.” “Nimepiga kutaka kujua jinsi ya kukusaidia! Jema ameambiwa na mama yake kinachoendelea. Nataka kukusaidia.” “Nashukuru. Huyo aliyekuwepo na Jelini, anaitwa Doro. Alikuwa akipokea na kukata. Alipopokea mara ya mwisho na kunitukana, amenikatia, na sasahivi simpati tena kwa simu.” “Umejaribu kumuuliza kama yupo na Jelini? Isijekuwa hayupo naye, unahangaika kumtafuta ambako hayupo.”

“Umenipigia ukisema unataka kunisaidia si kunichanganya zaidi James. Acha kuni…” “Basi Colins. Nilitaka kukusaidia ili ufikiri zaidi.” “Hivyo hunisaidii ila unataka kunichanganya zaidi. Maana ni kama unataka kuniambia pengine amerudi kwa yule mzee!” James akanyamaza ndipo Colins akajua ndicho alichokuwa akimaanisha.

“James?” “Mimi nilitaka ufikiri zaidi. Inaweza kuwa sivyo. Ila uwezekano upo. Maana anaweza hisi wote ni walewale tu. Alijaribu kwake ikawa ni swala hilohilo mwanamke aliyekuwepo kwenye mahusiano naye tokea mwanzo, na kwako ni yale yale. Ila tofauti yako na yake, mwenzio alikuwa akijitahidi kuwa naye. Na ndio maana nilikwambia Colins, weka mambo ya nyumbani kwenu kwanza sawa ndipo urudi kwa Jelini. Sasa ona tulipo sasahivi.”

“Yule mzee sio mwenzangu na kwa taarifa yako tu, Jelini aliachana naye ramsi jana. Na leo nimeenda kwake, Jelini hayupo huko.” James alishituka, hakutegemea. “Umechanganyikiwa wewe Colins!?” “Hakika nimechanganyikiwa na wewe unazidi kunichanganya, wala husaidii.” “Ujue yule mzee atakuja kukuua kweli!” “Sijali. Na kingine James, japokuwa unatamani sana kunilaumu, ila kwa sasa haitasaidia. Na kwakuwa sidhani kama mambo ya nyumbani kwetu yatakuja kuisha. Wamenyweshwa sumu mbaya sana juu ya Jelini. Hawamtaki kwenye ukoo. Sasa kwa kuwa wao wameshatamka wazi kabisa, hawatakaa wampokee, basi namuoa kwa haraka sana. Sina sababu ya kusubiri tena.” James hakutegemea.

“Colins!?” “Sasa nasubiria nini tena James? Familia nzima hawamtaki. Mimi ndio muoaji. Pesa ya kuoa ninayo. Sina chakusema namsubiria baba wala mama. Sasa kama hutaki kunisaidia nioe, uniambie sasahivi na wewe nikuweke kundi moja na familia yangu.” “Naona tuanzie kwenye kumtafuta kwanza Jelini.” “Jelini nitampata tu. Najua mimi ndiye niliyemrudisha kwa Doro, naenda kumfuata mwenyewe. Ukiweza kunisaidia sawa, kama huwezi basi.”

“Ulitaka nifanyaje?” “Nakutumia namba ya Doro, naomba uende ofisini, tumia mitandao ya kazini, niangalizie mara ya mwisho kuzungumza na simu yangu, alikuwa wapi. Na nipe taarifa zake kamili.” “Sawa.” James akaitika na kukata simu, safari ya ofisini kwao na yeye ikaanza, ili kusaidia kumsaka Doro.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mida ya saa saba usiku, mfanyakazi huyo wa kuajiriwa, na kesho yake saa mbili kamili asubuhi anahitajika kazini, ndio akawa amejua baa alipo Doro, akawasili hapo. Hapakuwa mahali pachini. Hoteli nzuri tu tena ya kitalii, akatafuta upande iliyopo baa ambako kuna live music. Bendi ilikuwa ikitumbuiza. Akaanza kusaka mpaka akafika kwenye meza aliyowakuta kina Doro, wanaume wengine ambao hata yeye alikubaliana na Jelini, ni wa maana hata kwa kuwatizama hapo na pombe zao. Walionyesha pesa ipo. Meza ilijaa vinywaji vikali na bia za kawaida pamoja na nyama choma. Kwao ilikuwa ni kama ndio panapambazuka. Kelele na cheko za kilevi.

Walikuwa wameunganisha meza, akamuona Jelini amekaa katikati yao. Akamsogelea mpaka pale  na kumgusa. Jelini alipogeuka na kukutana na Colins, alishituka sana. “Mimi sijafanya jambo baya.” Wazi alikuwa ameshalewa sana. Wote wakawageukia wao. Jelini mbabe kwa wanaume, anazungumza hivyo na mwanaume! Ikawatia hamasa yakumtizana huyo Colins.

 “Twende.” Akamuambia hivyo. “Mimi sijafanya jambo baya. Nilikuwa tu hapa. Na wala sijalewa. Nimekunywa kidogo tu kama kujituliza uchungu wa kukataliwa.” Akaanza Jelini. Kama kawaida yake akilewa na machozi hayapo mbali.

Akaanza kulia kuwa yeye hampendi. Anamtesa moyo wake bila sababu. Hamthamini. Anampenda tu Love, yeye hampendi. Hamjali. Akaongea mengi akilia walevi wenzie wakimpa pole na kumtuliza. “Mimi bora uniache tu, niendelee na maisha yangu, kuliko kuendelea kuteseka nikijua upo kwenye dunia ninayoishi mimi, halafu umemchagua mwanamke mwingine sio mimi.” Akaendelea kulia, hataki kuondoka na Colins. Akarudia tena yale maneno mazito anayopenda kuyasema kwa Colins akiwa amelewa, na yakaweza kuukamata moyo wa Colins. Jinsi Jelini alivyozungumza mpaka wenzake aliokuwa akinywa nao, wakashangaa. Alisema kwa kumaanisha kabisa tena bila hata aibu, akimtamkia Colins.

Lakini Colins akasisitiza nilazima waondoke. Mabesti zake wakaongeza nguvu kumwambia amuache. “Sisi wote tupo hapa leo kwa ajili ya Jelini. Tulimmisi ndio tumekuja kumkaribisha tena chamani.” Colins akawasikiliza na kurudisha macho kwa Jelini.

“Simama twende. Unaondoka na mimi Jelini. Sitakuacha hapa.” Akachukua pochi yake, wenzie wakimlaumu kwa nini anamchukua wakati bado ni mapema sana. Akamshika mkono, akasimama bila ubishi na kumuongoza njia mpaka nje kwenye gari yake. Wakati anamfungulia mlango, akaanza kutapika. Alitapika Jelini kama bomba. Akamshikilia kumsaidia asijichafue zaidi maana alishajitapikia. Simu ya mama yake Jelini ikawa inaingia, hawezi kupokea amemshikilia asikalie matapishi yake.

Baada ya hapo, akamfuta na shati lake alilokuwa amevaa akavua ili kumsafisha, akampandisha kwenye gari, yupo hoi kwa pombe na kutapika. Ikabidi afungue vioo vya dirisha kwa harufu kali.

Akarudisha simu ya mama yake. “Nashukuru Mungu nimempata. Lakini anahali mbaya sana. Tafadhali naomba nisimrudishe hivi nyumbani. Acha akalale, akimka na kujisikia vizuri, ndipo nimrudishe nyumbani.” “Unauhakika Colins? Naweza kuja kumchukua mimi mwenyewe.” “Hapa alipo amejawa matapishi, amelewa hajitambui. Kweli Jeremy amuone akiwa na hali hii? Maana ni wa kubeba kabisa.” “Na alimuahidi mwanae anaacha pombe!” “Tafadhali naomba mtaarifu na James. Acha nimpeleke akampumzike. Tutazungumza kesho.” Akaendelea kukanyaga mafuta mpaka kwake. Na akajiambia hatamwambia mzee Kasa.

Kwa Colins.

Alimfikisha kwake akiwa amelala, akamtoa garini mpaka bafuni. Ilibidi amtoe tu nguo, amuogeshe. Alikuwa akinuka vibaya sana. Matapishi ya pombe. Alikuwa hajitambui. Akamsafisha mpaka akaridhika, akamuweka chini. Akamkausha na kumvalisha tsheti yake na kumuweka kitandani, akamfunika vizuri, akapotelea usingizini kama mzigo.

Colins akabaki akisafisha na kufua nguo yake aliyotapikia. Akafanya yote ndipo akarudi kitandani na kubaki akimtizama. “Kweli Jelini ni mzuri. Anavutia kila mahali!” Ndipo akili ikaanza kumrudisha kwenye umbile la Jelini aliloliona likiwa tupu. Akabaki akiwaza mpaka akapitiwa na usingizi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alam ya kazini ikamuamsha akiwa tu ndio amelala. Akajivuta hapo, kisha akakumbuka na James hayupo ofisini. Akakurupuka. Akaandika ujumbe na kuuacha pembeni ya Jelini kwamba akiamka akutane nao. Akajiandaa, mpaka akamaliza, Jelini amelala kama mzoga. Akatoka kwenda kazini kuweka mambo sawa kisha arudi alete chakula, kisha arudi tena kazini.

Alirudi mida ya saa nne na nusu, akamkuta bado amelala vilevile kama ndio saa nne usiku. Akamtizama hapo, alikuwa amemletea supu. Akaiweka mezani, akatoa ujumbe wa asubuhi akaandika mwingine, akatoka. Kwenye mida ya saa nane ndipo Jelini akafungua macho nakuanza kufikiria alipo. Akakaa kwa haraka akiwa amejawa hofu. Alishituka sana alipojigundua hajavaa hata chupi na yupo na tisheti tu, hajui alipo, sehemu ngeni. Akaanza kulia akijua ameshabakwa.

Akiwa kwenye hali ya paniki, akaona karatasi pembeni yake. Akaichukua. ‘Jelini.’ Nje ilikuwa na jina lake akajua inamuhusu. ‘Nimeweka dawa za kichwa mezani pamoja na supu. Ukiingia bafuni utakuta mswaki wako nimekuwekea pembeni. Mataulo masafi yapo kabatini, chukua nguo yangu yeyote itakayokufaa uvae baada ya kuoga. Kisha kula na meza dawa kabla kichwa hakijaanza kuuma. Nimeenda kazini. Mida ya saa 12 jioni nitakuwa nimerudi. Tafadhali nikukute hapo nyumbani. Colins.’ Jelini akashituka kujua yupo kwa Colins. Akajaribu kuvuta kumbukumbu kujua alikuwa wapi, imekuaje yupo pale bila mafanikio.

Kichwa kikaanza kugonga kama kengele wakati kumbukumbu zikimrudisha alipokuwa akinywa na kina Doro, hofu ikazidi kumuingia na aibu. Hakufanya hatua zote alizoandikiwa. Ila kumeza dawa na kusafishwa kinywa. Akarudi kitandani, akazima kama mshumaa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alikuja kufungua macho, ilishakuwa usiku Colins anajikausha kama aliyetoka kuoga. Akajigeuza upande wa pili, Colins akajifunga taulo na kumsogelea upande aliogeukia. Akamkuta akilia taratibu. Alipomuona tu Colins akaingia ndani ya mto kama anayejificha. Colins akajipaka lotion na kuvaa nguo ya chini pamoja na kata mkono. Akaenda kukaa pale kitandani upande alipokuwa amegeukia.

“Vipi kichwa?” Akamuona anapandisha mabega kukataa. Akamtoa ule mto kichwani. “Naomba unisikilize sababu ya kuchelewa kuja kukuchukua nyumbani.” Jelini akabaki amelala kifudifudi ameficha uso. Colins akamueleza ujio wa wazazi, bibi na babu. “Nikidhani babu yupo upande wangu, kumbe Love alishawapa taarifa zako nyingi, za kutisha na kumuogopesha mpaka babu. Ndio ikabidi aje azungumze na mimi. Haikuishia hapo, akaja Love na wazazi wake kuongeza ushahidi wa kile kinachozungumziwa.” Jelini alishituka mpaka machozi yakakata.

“Ilikuwa ni kesi kubwa iliyoendelea kwa muda mrefu kwa sababu ni kama Love alionyesha anauhakika na anachozungumzia, kuwa ameelezwa na mtu wa karibu sana na mzee Kasa, ambaye na yeye ni muhanga wa mahusiano yako na mzee Kasa.” Jelini alitamani ageuke kuwa upepo, apotee duniani.

“Akaeleza baa zote ambazo huwa unashinda huko na waume za watu kama wale niliokukuta nao jana.” Hapo tumbo likaanza kumuuma. Hofu na aibu. “Iliendelea hiyo kesi mpaka ikabidi mimi niwaage. Na ukumbuke walikuwa hapa kwangu. Kesi ikiendelea hapa. Nikawaambia ni lazima niondoke, nikufuate. Tulikuwa na miahadi. Kama ungekuwa na simu, ningekupigia kukutaarifu kinachoendelea, lakini nikawaambia huna simu, na sina jinsi ya kuwasiliana na wewe, na nimeshakuchelewa, lazima niondoke. Hapo napo pakachukua muda mrefu sana.”

“Kufupisha habari, ndipo nikafanikiwa kuwatoa hapa nikaja kwenu. Nikakusubiri mpaka saa nne usiku, maana niliambiwa uliondoka na Doro. Ndipo nikaanza sasa kukusaka kwenye mabaa yote niliyosikia Love akishitakia kuwa ndiko unakoshinda huko. Kote waliniambia wanakufahamu, lakini hawajakuona muda mrefu. Ndipo nikakufuata mpaka nyumbani kwa mzee Kasa, nikijua ulirudi huko.” Jelini alishituka, nusura roho itoke.

“Nako huko nikagonga mwamba. Ndipo James akanisaidia kuitafuta simu ya Doro kujua alipo. Maana mara ya mwisho alipokea, akanitukana na kuikata.” Jelini akazidi kuingiwa hofu na aibu. “Mambo yamefika mpaka na kwa kina Shem! Najificha wapi mimi!” Akawaza akiwa bado ameinamisha uso kwenye godoro.

“Hatimaye nikakupata. Ulitapika sana na kujitapikia pia. Ikabidi kukuosha kabla sijakuweka kitandani. Kwa hiyo, sikuwa nimemchagua tena Love badala yako. Sitafanya hivyo kwa sababu nakupenda wewe Jelini. Narudia tena, na naomba hili usije wahi sahau. Wewe ni mke wangu, mama watoto wangu. Nilikwambia nikiamua kuwa na wewe, sitakuacha mpaka utanihurumia. Nakupenda Jelini, na mimi nitasimama na wewe. NIMEKUCHAGUA wewe, sitakusaliti. Kabla sijakuumiza wewe, jua mimi ndio nitaumia zaidi. Umenielewa?” Akatingisha kichwa kukubali akilia sana.

“Naomba utulie na uniambie kichwa kinaendeleaje.” Akalia hapo kwa muda, akamuona ananyanyuka kwenda bafuni. Akakaa huko akamsikia akioga. Akatoka kutayarisha chakula. Baada ya muda akamuona ametoka amevaa tisheti yake na kufunga taulo chini. “Hilo taulo litakuwa bichi. Njoo nikupe pensi ambayo nahisi itakuenea.” “Nilimuahidi mama na Jeremy nitaacha pombe. Na nilikusudia kuacha. Jana nilikosea. Naomba unisamehe, Colins. Najua nimekosa. Na narudia kukosea tena na tena. Sitarudi tena baa.” Colins akabaki akimtizama.

“Samahani nilikosea. Hutanisikia au kunikuta tena kwenye ile hali. Sirudii tena.” Kimya. Akajifuta machozi. “Na nashukuru hukunirudisha vile nyumbani. Ningemuumiza sana Jeremy. Huwa namuahidi hivyo, halafu narudia tena na tena. Mpaka akawa amechoka, haniamini tena.” “Kwa nini ulienda na Doro, mtu unayejua wazi huko ndiko anakokupeleka?” “Kwanza dada Doro anajua sana hayo mambo ya UKIMWI. Nilitaka aniambie ni wapi naweza kwenda nikapimwa na nikapata majibu ya uhakika hata kama vijidudu vimeingia muda mfupi na sehemu ya kupata dawa za waathirika. Sikutaka kusubiri tena Colins. Nimeishi kwa hofu kwa muda mrefu. Nikajua yeye ndiye angenisaidia kwa haraka.”

“Akanielekeza. Lakini nilikuwa naogopa kuwa mwenyewe hospitalini, Colins. Mimi muoga sana wa sindano. Naweza hata nikazimia kuona sindano inataka kuingia mwilini mwangu. Muulize mama.” “Ameniambia.” “Sasa dada Doro alipojitolea kuwa na mimi, nikakubali kwa haraka. Hata wakati ule nilipoenda kupima, nilikuwa na Kasa, ilibidi anifiche uso kifuani kwake ili waweze kunitoa damu. Nilikuwa naogopa sana, nusura kuzimia.” Wivu tayari kusikia mzee alifanikiwa kuwa naye hospitalini mpaka kumficha uso kifuani! Roho ikazidi kuuma.

“Na kwa nini hukunisubiria?” “Nilikata tamaa Colins! Nilifikiri ni mambo yaleyale ya Love kwanza, mimi ndio nakuwa mtu wa mwisho kunifikiria.” Colins akatulia. Kisha akauliza. “Uliweza kupima?” “Ndiyo. Nilipima.” Colins akabaki akimtizama kama anayemsubiria, Jelini akabaki ameinama mbele yake akifuta machozi. “Nakusikiliza.” Akamuona kama ambaye anajaribu kukumbuka kitu. “Sijui nimeacha wapi pochi yangu! Ilikuwa na majibu.” “Ipo chumbani. Twende ukatoe na hilo taulo.” Akaongoza njia, na yeye akamfuata kwa nyuma kama mtoto anayeogopa.

Wakaingia chumbani, akamtolea kwanza pensi yake nyeusi, kama ya mcheza mpira wa kikapu. Yaani hata hapo Jelini akapendeza! Colins akamtizama kwa kujiiba, akaenda kumtolea pochi yake. “Naomba mimi nirudi nyumbani Colins, nikuache upumzike tu.” Akamgeukia. “Huli?” “Hapana. Nashukuru. Lakini acha tu niondoke.” “Nilimuomba mama leo ubaki hapa, tupate muda wa mazungumzo kati yetu. Tuwekane sawa, kabla ya kuendelea.” “Unaona ni bora uniache tu?” Akauliza kwa upole na wasiwasi.

“Kwanza nataka kujua kama ni sawa tukabaki wote mpaka kesho ndio nikurudishe nyumbani?” Jelini akabaki akifikiria. “Jelini?” “Mimi naona bora niondoke tu.” “Kwa nini?” “Sijisikii vizuri.” “Unaumwa?” Akanyamaza. “Jelini?” “Sijisikii vizuri. Labda niende tu nyumbani. Tuje kuonana wakati mwingine.” Hapo anamjibu lakini hawezi hata kumtizama machoni. Akamsogelea na kumshika kipanda uso taratibu akiwa vilevile ameinama.

“Kichwa kinauma?” Akamuuliza tena. Akapandisha mabega kukataa. “Basi twende tukale kwanza. Mimi nataka kubaki na wewe. Twende.” Wakatoka hapo hata majibu ya vipimo alivyofanyiwa Jelini, hawakuangalia tena. Akakuta alishaandaa meza. Sahani mbili na umma zake, pamoja na bakuli na kijiko, kisha glasi pembeni. Mziki mtulivu, nyimbo kama kwenye gari yake ndio zilikuwa zikisikika na hapo kwake. Akaanza kusikia utulivu.

“Ulitapika sana jana. Kunywa kwanza supu.” Akammiminia kwenye bakuli. Akaanza kunywa taratibu. “Nzuri. Nashukuru.” “Karibu.” Akajiwekea na yeye chakula kwenye sahani, akakaa mbele yake akaanza kula akimwangalia. Kimya cha muda, Jelini haelewi ni kwa nini anataka kuwa naye. Akanywa supu mpaka akamaliza.

“Nimeharibu sana?” Akamuuliza Colins kwa sauti ya kumbembeleza. “Unamaanisha nini na kwa nani?” “Kwako. Wengine sijali. Wameshanizoea mimi ni mtu mbaya.” “Nilidhani uliniambia umebadilika Jelini!” “Jana sikupanga kabisa kunywa Colins. Na Mungu ni shahidi. Sijui ilikuaje!” “Kwa nini ulirudi baa?” “Dada Doro aliniambia niende naye nikasalimie washikaji tu. Ameshawaambia yupo na mimi, wamesema tukutane niwasalimie. Nikaona sio jambo baya. Na hata nilipofika pale niliwaambia mimi nimeacha pombe. Ndio dada Doro akaniambia moja tu. Sasa sijui ilikuaje, ila nakumbuka kukataa, sasa sijui ikawaje tena nikazidisha mpaka kulewa!”

“Doro si rafiki mzuri Jelini. Rafiki anatakiwa kuheshimu maamuzi yako. Ukisema hunywi, anaheshimu hilo na kukuacha si kukulazimisha.” “Nimekuumiza sana?” “Ndiyo Jelini. Kwa sababu tulikubaliana hapo hutarudi tena. Ni kwa nini umeruhusu Love kukuingia akilini kiasi cha kutoniamini mimi?” Akapandisha mabega kukataa.

“Huamini kama nakupenda Jelini. Niambie nifanye nini uamini nakupenda wewe, nimekuchagua wewe, na nitabaki kuwa na wewe. Maana bila hivyo hatutafika mbali. Tunavita mbele yetu. Haswa upande wangu, hawataki tuwe pamoja. Sasa kama mimi na wewe tukishindwa kuwa pamoja, ujue wakati tutakapojaribiwa kwa hakika, hatutasimama. Jana ilikuwa ni mimi kutotokea kwa wakati, ukapotelea kwenye marafiki wa zamani. Wakija kukuletea uongo mwingine juu yangu na uthibitisho wao, bila kutaka kunisikiliza na mimi, si ndio utakuwa mwisho wetu?” Jelini alilia sana.

“Nimekosa Colins. Tafadhali nisamehe. Nakuahidi nitabadilika. Na sitarudia tena kwenda baa, labda tuwe wote.” “Naomba utulie. Sitaki uendelee kulia. Kichwa kitaanza kuuma tena. Ila niambie kama angalau unaniamini Jelini. Maana nimerudia zaidi ya mara tatu, kukuhakikishia Love hatakaa akaingia katikati yetu. Ni mtu wa mwisho kabisa sasahivi namfikiria, ila wewe.” Jelini akaendelea kulia.

Akaenda kumnyanyua pale, wakahamia sebuleni. Akakaa na kumvuta akae pembeni yake, kisha akamkumbatia vizuri, Jelini akasikia upendo wa ajabu. Kumsafisha matapishi akiwa amelewa na bado kumkumbatia kwa namna ile, ikamgusa zaidi. Akalia hapo kifuani Colins akimpapasa mpaka akatulia.

“Nitabadilika.” Akamsikia akiongea taratibu. “Naomba kusikia umebadilika Jelini. Kuanzia kuniamini, kusimama na mimi bila kuchoka. Hata ukisikia kitu, kama hakijatoka kwenye mdomo wangu, baki na nilichokwambia. Nibebe kwenye udhaifu hata kwa mama yako nisitiri na kunitetea ukijua nakupenda, sina nia ya kukuumiza.” “Na nitakusubiri Colins. Hata ukichelewa, kuanzia sasa, nakusubiri wewe tu. Tukipanga jambo letu, nakuahidi kulisimamia. Sitafanya vinginevyo mpaka tukubaliane tena.” “Basi hapo ujue ndio kusimama kwetu. Na hakuna mtu atatuangusha kirahisi.” Wakatulia.

“Na mimi nikuombe radhi kutokuwa na wewe jana hospitalini. Nilishakuwa nimevaa kabisa, nakaribia kutoka ndipo wakanivamia. Nilipanga tutoke, twende tukapate kifungua kinywa pamoja ndio twende hospitalini. Lakini nikashindwa, na wewe hukuwa na simu angalau kukutumia ujumbe, kukutaarifu! Ila ujue sikukusudia.”

“Tutafanyaje kuhusu kwenu, Colins?” “Sijui. ila ninachojua sisi tuendelee na yetu, tutakuja kuungana nao watakapokuwa tayari.” Jelini akabaki amejilaza hapo kifuani kama kawaida yake, akifikiria.

“Colins?” Akaita taratibu, akiwa amemlalia, anapapaswa. Akaitika. “Hata iweje, niahidi hutaniacha mimi.” “Nimeshakuahidi Jelini. Tafadhali amini.” “Naingiwa hofu. Maana ni kama jana nimethibitisha walichonishitakia huko kwenu. Ila sikufanya jambo baya.” “Unajuaje Jelini? Hivi unajua hali unayokuwa nayo ukilewa?” Akaingiwa hofu.

“Au nikuulize, unakumbuka chochote kuanzia nimekufuata kule baa?” Kimya. “Yale maneno uliyoniambia siku ya harusi ya James na Jema, uliyarudia Jelini. Tena mbele ya wale niliokukuta nao, mpaka na wao wakawa wanashangaa. Hawaamini kama na wewe umepata mtu wa kumwambia hivyo. Sasa je, unakumbuka?” Jelini akatingisha kichwa kukataa.

“Sasa unajuaje kama hujafanya jambo baya.” Akaanza kuingiwa na hofu. “Maana wanaweza kukufanyia na kondomu, usijue hata kama kuna mtu alipita. Kwa hiyo kama hukumbuki chochote kilichoendelea baada ya kulewa, tafadhali usiseme hujafanya jambo baya, kwa kuwa hujui.” Jelini akajisikia vibaya sana. Akaficha uso hapo kifuani na kuanza kulia tena.

“Sina nia ya kukuhukumu, lakini nakwambia ukweli. Ndio maana mimi binafsi nachukia pombe, kwa kuwa inauwezo wakunifanya nisifikirie na kuzungumza kile ninachotaka kuzungumza kwa wakati ule. Ndio maana sinywi.” “Sirudii tena Colins. Nakuahidi sitarudia tena. Hata iweje, sirudi huko tena.” “Sawa. Mimi nitabeba maneno yako moyoni kwangu. Nakuamini.” Akaendelea kumbembeleza mpaka akatulia.

“Twende ukalale. Najua jana hukulala vizuri. Mimi nitakusubiria na kukubembeleza mpaka ulale. Twende.” Colins akacheka akimtizama. “Twende.” “Ujue hapa ndio nyumba tutakayolea watoto wetu?” Jelini akacheka akiangaza macho. “Au hujapapenda? Unaona padogo sana?” “Maadamu wewe utakuwepo hapa, mimi napapenda.” “Niahidi asije tokea mwenye mjengo, akakutoa hapa.” “Kasa hatanitoa hapa.” Colins alicheka sana.

“Najua Kasa anakutisha sana. Na sijui kwa nini!?” “Yule mzee anapesa nyingi sana bwana. Na ni kama hazina kazi!” “Mimi nakutaka wewe Colins. Nimeridhika na wewe. Wasiwasi wangu ni kuja kukupoteza tu, lakini si mali. Naomba yule mzee asikutishe. Kwanza nishamkabidhisha kwa anti Sheha, huo ukurasa nimefunga. Twende ukapumzike. Achana na mawazo ya Kasa.” Wakatoka hapo kwenye kochi, akamuona anazima taa zote.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Napenda hizo nyimbo zako! Zina maneno yakutuliza.” “Nitakuhamishia chumbani. Usijali.” Akamshika mkono akimuongoza njia mpaka chumbani. “Kesho unaondoka saa ngapi?” “Kwa nini?” “Nataka ukitoka, tutoke wote. Na mimi nirudi nyumbani.” Akabaki kama anawazo jambo, kisha akasita. Jelini akamgundua. “Ni nini?” “Natamani unisubirie mpaka jioni ndio nikurudishe.”

“Colins!? Nitakaa hapa mpaka lini?” “Akili yangu inatulia nikijua upo hapa. Hata naweza kufikiria vizuri. Niliingiwa na hofu jana! Hakika ungenihurumia. Sikujua kama nitakuja kukupata tena, na kama hata nikikupata bado ungeniambia unanitaka mimi. Nilijua nimekuumiza mpaka mwisho. Hutaki hata kuniona tena. Tafadhali nipe hata siku ya kesho tu. Nikirudi nakurudisha nyumbani. Hata hivyo mama na Jeremy hawatakuwepo. Utashinda peke yako. Sasa si heri ubakie hapa?” “Na wewe si unaenda kazini?” “Lakini naweza kurudi hata mchana kama leo, tukala wote.” “Kwani leo ulirudi?” “Ulikuwa umelala kama ndio usiku wa saa nne. Nikaona nikuache tu.” Jelini akatulia.

“Lakini kama hutaki kuwepo hapa, basi. Usijisikie nakulazimisha.” “Unajua ningetamani hata nisiondoke hapa, Colins.” “Sijajua. Maana hata hiki chumba na bafu vilivyopo humu havifanani na kwako.” “Acha kufanya hivyo bwana!” “Kweli Jelini. Unamiliki chumba na bafu vya hali ya juu sana. Ni rahisi kujishuku na nilivyonavyo.” Jelini akatulia akifikiria.

Colins akabadili nguo hapohapo mbele yake na kujiweka kitandani akimtizama kama alivyojilaza kwenye kitanda chake chumbani kwa Jelini. “Popote utakapokuwa wewe Colins, mimi nitafurahia kuwepo. Sitajali ni wapi.” “Unauhakika?” “Basi naomba muda uje ujibu hilo swali Colins. Mimi muaminifu sana. Hata nilipokuwa na Kasa, japokuwa nilikuwa na hamu na wewe, lakini nikajionya nafsi yangu kabisa, nikakuacha.” “Kweli Jelini!?” “Kama ungekuwa ukizungumza na Kasa mwenyewe angekwambia jinsi nilivyoumia kwa kitendo cha kukufuata, eti na kukuonya ukae mbali na mimi! Niliumia mpaka akajua. Lakini kwa kuwa nilikuwa naye, nikaona nitulie tu. Sitakusaliti Colins. Nitatulia na wewe.”

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akajinyanyua pale alipokuwa amejilaza kufikia midomo yake, mabusu yakaanza. Taratibu mkapa yakachanganya. Akiwa kwenye ile hali ya kuwa tayari kumvua nguo Jelini, gafla maneno ya Love aliyopenda kumkejeli nayo kitandani akimfananisha na wanaume wengine yakamrudia. Nayo picha ya Jelini akiwa mtupu, vile alivyo mzuri ikamjia kwa gafla. Kasa na maneno yake kuwa aliweza kumtuliza Jelini vikapita hapo kichwani mwake, Jelini akiwa amelegea, anamtaka tu yeye.

 Upinzani mwingi kwa Jelini. Nikizembea hapa, nisipotoa shoo ya kikabe, atabakiwa na kumbukumbu ya yule mzee.” Colins akaendelea kuwaza huku akimpapasa Jelini aliyekwisha muona akiwa kama alivyozaliwa siku iliyopita, na kumsafisha. Hali ilishakuwa mbaya. Yupo kwake, ndani ya chumba chake, Jelini anatoa miguno ya hatari.

Akaendelea kuwaza katikati ya romance ya kukata na shoka. Walikuwa wakinyonyana kama wenye uchu wa kupitiliza mpaka wakajikuta wamelala kitandani. Jelini naye amemng’ang’ania kama anayeomba asimuachie.

Hakuwa amevaa sidiria, kwa hiyo hata chuchu aliziona kupitia tisheti yake tokea wanakula. Picha ya mwili wa Jelini vikazidi kumsumbua Colins ila hofu. Anaogopa fedheha. Kuishi kwa muda mrefu na Love, akimwambia maneno hayohayo kwa muda mrefu vikamuingia akilini, mpaka akaamini. Gafla ikawa kama mtu amezima switch ya umeme au mshumaa uliopulizwa. Colins akazima gafla, asitarajie mpaka mwenyewe akashituka kwa hofu.  Jelini alipoona hivyo, akajitoa hapo kwa kuumia sana.

“Nakwenda kutumia choo.” Akatoka hapo bila yakusubiri jibu, Colins akajua ameharibu. Jelini amekasirika, asijue ni zaidi ya hivyo. Amehisi kukataliwa kwa hali ya juu. Colins akabaki hapo kitandani akihema. Kama kitu kikapita kichwani, akaruka hapo kitandani na kukimbilia upande wa bafuni alipoelekea Jelini. Akataka kumgusa, Jelini akamuona kupitia kioo, akamkwepa.

“Tafadhali acha kucheza na hisia zangu, Colins. Na mimi ni mwanadamu, nina hisia. Na ujue ipo siku zitafika mwisho.” Jelini akamgeuka asiamini. “Hujaelewa Jelini!” “Juu ya nini? Kwamba unaweza kuishi unyumba na Love, lakini huwezi kuwa na mimi?” Colins akashituka nafsini kwake, hakujua kama ingeleta picha ya namna hiyo.

“Ni vile nakuheshimu sana Jelini! Niliona si sawa kuendelea na chochote bila hata yakulipa mahari! Nilitamani ukiwa mke wangu ndio niwe huru na wewe. Sikutaka kuwa kama nakuvamia tu au nachukua kitu kisicho changu.” Akajitetea na kuzidi kuharibu.

“Sawa. Basi naomba nirudishe nyumbani. Ila kama unaona ni usiku sana kwako, mimi naweza kwenda peke yangu.” “Tafadhali usikasirike Jelini.” “Siwezi kukasirika kuheshimiwa! Nakusaidia kuishi matakwa yako. Bado mimi si mke wako, kwa nini kutaka nilale na wewe kitanda kimoja? Acha kama tutajaliwa hiyo ndoa, nitarudi tena hapa. Ila kwa sasa tafadhali tuishi ulichokisema. Na naomba usianze kuniyumbisha Colins. Simamia maamuzi yako, tafadhali.” Akatoa nguo palepale, akavaa gauni yake aliyokuwa amefuliwa na Colins, Colins akimtizama.

Akatoka akimtizama, akagutuka tena na kumkimbilia. “Acha nikurudishe. Ila huoni kama itakua usiku sana?” “Hamna neno.” “Utawasumbua wakiwa wamelala na mimi nilishakuombea ruhusa Jelini. Tafadhali naomba tulale mpaka kesho.” “Hapana. Ruhusa uliomba ya mazungumzo na kuniweka sawa. Ushaniweka sawa, nimekuelewa. Kuna sababu gani tena ya kulala hapa?” Colins akabaki kimya.

“Tafadhali acha kuwa njia panda hata katika hili. Kama kwako huu ni usiku sana, kwangu bado ni mapema sana. Tafadhali amua moja. Unanisindikiza au nitoke nikatafute usafiri hapo nje?” “Naomba kukupeleka.” Akachuka pochi yake na kutoka tena hapo chumbani.

Ikabidi Colins aanze kubadili nguo kwa haraka. Kutoka za kulalia, ili avae kitakacho mfaa kumsindikiza Jelini. Akamkuta mlangoni kabisa anajaribu kutoka. “Jelini umeshindwa kunielewa. Tafadhali tulia.” “Nimetulia na kufiria kwa karibu. Naona wewe utanichanganya Colins. Sijawahi pata mtu akaniumiza roho na akili kama wewe. Na hivi ninavyojisikia, sitaki kuendelea kuishi hivi. Mimi sitaki kuishi na hii hali.” “Jelini!”

“Hapana Colins. Nikijifikiria, naona kuwa na wewe kwenye aina yeyote ya mahusiano, napoteza na napotea. Nikijifikiria sababu ya kunifanya kumtafuta dada Doro na kuishia kunywa nikiwa najiambia ni kidogo tu, nilikuwa nataka nijitulize kile ninachojisikia juu yako na sikipati. Najihisi nimekwambia sana na kukuonyesha nakupenda mpaka kwako vimekosa maana. Colins, mimi sijawahi kubembeleza mtu hivi, aisee. Najiuliza nitaendelea hivi mpaka lini!? Jana sababu ya maumivu yako, nimevunja ahadi ya msingi sana kwangu mwenyewe na kwa mwanangu. Nilirudi baa na kufanya kitu ambacho sikuwa hata nampango wa kukifanya.”

“Nahisi na pengine ndivyo inavyoweza kuwa, pengine sisi hatukukusudiwa kuwa pamoja.” “Jelini…” “Subiri kwanza Colins. Wewe haupo tayari na mimi. Familia yako pia hainitaki. Kwa nini unataka kunichanganya bila sababu?” “Nakupenda Jelini.” “Pengine ndivyo unavyodhania. Lakini matendo yako sivyo. Na mimi sitaki mtu wa namna yako maishani. Utaniyumbisha kwa uchache nilio nao. Kwa heri Colins. Kila la kheri. Kama tuliandikiwa, basi acha muda utakuja jibu. Pengine hata wewe utakuja kujisikia utayari na mimi, kama bado na mimi nitakuwa bado nikijisikia hichi ninachojisikia kwako. Tafadhali nifungulie mlango nitoke.”

“Najua nimekuumiza Jelini. Lakini sikukusudia ni…” “Tafadhali usirudie rudie. Ulishaniambia. Mimi nataka kurudi kwetu nifungulie mlango.” Colins akafungua mlango, akashangaa Jelini anaongoza njia kutoka getini. “Tafadhali nisubiri nikurudishe nyumbani.” “Huna haja yakunirudisha, wewe siye uliyenitoa kwetu.” “Jelini?” “Basi labda nikwambie hivi, sipo tayari kupanda gari yako. Na mimi nimeona nisubiri kutumia vitu vyako mpaka au kama tukifanikiwa kuona. Mimi huwa sikubali vitu vya watu hovyo. Kama huamini, muulize Kasa.” Jelini akabadilika, Colins asiamini.

“Tafadhali naomba…” “Hapana Colins. Hakika nimekataa. Hutaendelea kunitesa kwa kiasi hichi. Heee! Kwa nini haswa!? Hapana. Utaninyima raha na kunifanya niishi na wewe kwa kukubembeleza mpaka lini!? Hapana kwakweli. Nimekataa. Siwezi kuwa mtumwa.” Jelini akaondoka, Colins asiamini. Ikabidi aache gari aanze kumfuata kwa miguu. Anatoka getini, kikampata kilichompata Kasa. Jelini mtoto wa jiji, hajazaliwa kwenye magari. Anajua kona na vichochoro vya jiji kama jina lake. Akikuponyoka dakika moja tu, humpati. Colins akakimbia mpaka kituoni, hakuwepo. Akaanza kumsaka akiamini atakuwepo tu hapo. Wapi!

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Vita Ya Ndani Na Ya Nje Inaendelea Kati Ya Wapenzi Hawa Wawili Walio Hakikishiana Wana Penzi La DHATI Kati Kati Yao.

Usipitwe Na Sababu Ya Kweli Ya Kushindwa Kumtoa Nguo Jelini Na KUMKATA Kiu Yake.

Love & Familia Ya Colins Wana Mipango KABAMBE Kuhakikisha Colins Anabaki Kubeba Mipango Ya Wazazi? Wakiwa Katikati Ya Kutoelewana Wao Wenyewe Wawili, Colins&Jelini. Je, Watafanikiwa Kumrudisha Colins Upande Wa Familia.

Kipi Kitaendelea?

USIPITWE.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment