Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 2. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 2.

Mwishoe akaamua kumpigia simu mama yake. “Samahani nakusumbua. Nilikuwa na Jelini. Ameondoka bila maelewano. Sijui kama upo naye?” “Mimi bado nipo kwenye biashara zangu. Na kama ameondoka kwako, usiwe na wasiwasi, atafika tu anakotaka leo awepo.” Colins hakuridhika. “Usiku huu!” “Hawezi akapotea hapa mjini na wala hakuna litakalompata. Mimi namjua Jelini. Sasa hivi kwake ni mapema sana. Kama wewe kutembea mchana, ndio Jelini kutembea kwenye hili jiji usiku. Hapotei kwenye hili jiji. Wewe jipumzikie tu.” “Ni sawa nikienda kumtizama nyumbani?” “Hata nikikwambia hapana, utanisikiliza Colins?” “Si kwa ubaya mama yangu. Nikutaka tu kujua kama amefika salama.” “Sawa. Usiku mwema.” Mama Jema akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kazi ya kwenda kwa kina Jelini kumsaka bila mafanikio ikaendelea. Mchana wakati wa chakula, anatoka kazini anakwenda kwa kina Jelini. Atagonga mpaka achoke. Muda ukiisha anarudi kazini. Akitoka jioni kazini, anarudi tena kwa kina Jelini. Atakaa hapo mpaka anachoka na mbu, anaondoka. Jelini hakuwa na simu. Alimsikia akitupa chooni line ili kumridhisha. Walinzi nyumbani kwao walishaondolewa na mama Jema. Hakuna wa kufungua geti aingie ndani ni mpaka wenye nyumba watake wao. Colins akagonga mwamba.

Siku alipomtuma kijana wa kazi, Chaz, kwenda kufua na kusaidia usafi, hakufunguliwa mlango. Akampigia simu Colins. “Hakuna mtu. Nimegonga kwa muda mrefu hakuna aliyefungua.” “Umejaribu kumpigia simu mama yao?”Colins akauliza. “Labda nijaribu. Ila naye kupokea simu ni shida! Mara nyingi siku na muda ambao huwa nakwenda, walikuwa wakiniachia geti dogo wazi, naingia kwenda kugonga mlango tu ndani.” “Mjaribishe mama yao, kujua kama kuna mtu ndani.” Chaz akakubali bila shida. Na yeye anataka pesa.

Baada ya kupiga sana simu bila kupokelewa, akaonelea atume tu ujumbe. ‘Ni mimi Chaz, nipo hapa nje ya geti, nimekuja kufua na kufanya usafi.’ Baada ya kama dakika 20 hivi akajibiwa. ‘Wala usihangaike kurudi tena hapo. Naona uhitaji hakuna tena. Tunashukuru sana kwa msaada wako. Siku njema.’ Ikabidi ampigie simu Colins kumpa taarifa. Hilo likazidi kumtesa Colins.

Nyongo Mkalia Ini.

Akaanza kunyongea, utengano na Jelini ukazidi kumla ndani kwa ndani, hana wa kuzungumza naye. Anamwambiaje James? Amsimulie nini na aache kipi? Amwambie ukweli juu ya kuogopa kwake kulala na Jelini? Maana kwa Jelini yeye amechukua ni kukataliwa, na akajua ndivyo atakavyomwambia mama yake na Jema, na Jema naye kumwambia James. Watajua bado anamshikilia Love, kumbe ni zaidi ya hivyo. Ni ndani zaidi ya watakavyomuhukumu. James anamjua Colins si mcha Mungu wa kiasi chakushindwa kuparanganyisha amri ya 6. Si tatizo hata kidogo, kwa hiyo hata yeye alijua James atamuona ni mbambaishaji tu.

Akabaki akiwaza. Nyumbani hapakaliki sababu ya tuhuma kali sana juu ya Jelini ambaye hata hawawasiliani! Chakula kwa Colins asiyeweza kupitisha mlo, kikaanza kukosa ladha. Cha asubuhi kikapelekwa mchana, cha usiku kikapuuzwa. Ikawa asubuhi, ikawa usiku, Jelini hapatikaniki. Sauti ya mzee Kasa akimtisha kuwa hao watoto anaopanga kuwa nao na Jelini wataishia kuwa na wao kina Kasa kama Kelvin, ikazidi kumla ndani kwa ndani. Usingizi ukaanza kukosekanika. Usiku badala ya kulala, anacheza game.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

James akamaliza likizo yake, kurudi ofisini, anakutana na Colins ambaye hakumtarajia. Alijua ukimya wake kwake, ni kwakuwa yake na Jelini yanamuendea sawa, kumbe aibu ya kumshirikisha ukweli wa kile kinachoendelea. Na Jelini naye safari hii akakosa cha kumlalamikia mama yake akijua mama yake akijua ndio Jema naye atajua. Sasa Jema ajue amemnunia Colins kwa kukataa kulala naye akimwambia wasubiri mpaka ndao!? Jelini akalibeba moyoni, hata mama yake asijue kama Colins hayupo kwenye picha.

Na mama Jema naye biashara zimechanganya, akili na muda wake wote kwenye biashara zake, Jelini yupo nyumbani akilea kichwa na mwanae, kuanzia mambo ya shule mpaka nyumbani. Hilo mama Jema akalifurahia, angalau amepokelewa mtoto, akili zinabaki kwenye pesa tu. Akitoka hapo asubuhi ni mpaka usiku mwingi tu. Maisha yakaendelea wasijue moto unawaka ndani ya Colins.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Kwema wewe!?” “Kwema kaka. Vipi JJ?” “Anakimbia sasahivi. Anaita mpaka baba!” Colins akacheka maana huyo JJ hata mwezi alikuwa hajatimiza! “Sasa akili imerudi kazini au bado unawaza ulezi?” “Lazima. Maana sasahivi atahitaji ada ya shule. Lazima kuongeza nguvu kwenye utafutaji.” Colins akatingisha kichwa.

“Usifanye masihara! Lakini mbona kama upo hovyo? Kwema?” “Kwema tu.” James alimjua Colins. Hawezi kujificha kwake. Akamuacha akijua akiwa tayari atayasema mwenyewe. Kazi zikaendelea, siku tatu zikapita akimuona kabisa hayupo sawa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku na hiyo akiwa anasimama, ametoka kwenye meza yake, maana zinaangaliana na ya James, akataka kuanguka. Hapakuwa na chakumfanya aanguke. James akaacha kila kitu, akamtizama. “Vipi wewe!?” “Naona giza.” James akashituka na kusimama haraka, akamsogelea. “Kwa nini?!” “Nahisi sukari ipo chini sana.” “Kwamba hujala?” Akanyamaza. “Sasa hapa utakufa, kama huniambii jambo linaloeleweka.” “Unataka nini tena? Nishakwambia sukari ipo chini. Nenda kaniletee hata Fanta.” James akatoka hapo mbio. Akaenda kwenye fridge yao, akachukua soda, akarudi nayo, akamkuta amesimama palepale ila ameegemea meza. Akamshikisha.

Akainywa yote kwa haraka na kurudi kukaa. “Naenda kuleta soda ya pili.” “Sasa nitajaza tumbo kwa soda tu?” Ikabidi James asimame. “Sijui unataka nini!” Akanyamaza. “Labda nikuulize, mara ya mwisho kula wewe ilikuwa lini?” “Sikumbuki.” “Haya tutoke tukatafute chakula.” Akamuona habishi. Wakatoka.

Akamuendesha mpaka kwenye mgahawa ambao wanapenda kwenda kula. Akaagiza wakati James akizungumza na mkewe. Akagundua ameagiza supu tu. “Acha kunitania na kunipotezea muda wangu. Ndio chakula gani hicho?” “Nimepoteza hamu ya kula kabisa. Yaani hii nitakunywa kama dawa?” “Kwa nini? Unaumwa?” Akanyamaza. “Jelini anajua?” Ikabidi aanzie tu karibu, akimjua Colins.

“Jelini hanitaki tena.” “Umefanyaje safari hii!?” “Mbona kama unanishutumu mimi moja kwa moja!?” “Haya samahani. Kwa nini hakutaki?” “Wewe vipi James?” “Kwa upotezaji huo wa muda, ukinizungusha kwa kutaka kunilaumu, narudia swali la kwanza, safari hii umefanya nini?” Colins akabaki akijishauri huku akijitahidi kunywa supu yake. James naye akaona aagize supu. Kimya kwa muda.

Ukweli.

“Unakumbuka nilikwambia niliishi na Love?” James akamtizama. “Kama mke na mume kabisa.” “Nakumbuka.” “Sasa katika moja au mengi ya malalamishi yake ni ufanyaji wangu wa mapenzi. Alikuwa akilalamika wakati mwingine ni kama namchafua tu.” “Kwamba hujui au?” “Aisee mpaka aibu!” James akafikiria kwa haraka na kuongeza swali zito zaidi. “Alikuwa akilalamikia maumbile?” “Aisee mpaka ikanimaliza kabisa na kushindwa kabisa hata kufanya naye mapenzi.” Colins akaendelea bila ya jibu la ‘ndiyo’ au ‘hapana’ ikawa kama James amenena.

“Nikaja kugundua ameanzisha mahusiano nje. Nikamuuliza kwa nini na wakati tunaishi nyumba moja! Akasema mimi ndiye nimemsababishia. Sijui chochote kitandani, halafu nina…” Akasita na kubaki kama asiyejua azungumze nini ili asijidhalilishe zaidi. “Kwa ujumla wake ni kwamba haridhiki. Si ndivyo?” James akaona amrahisishie.

“Ndiyo. Kwa hiyo akasema amekaa hivyo kwa muda mrefu akinivumilia ila akiteseka sana. Na yeye ni binadamu, ikabidi kutafuta mwenye mashine ya kiume kweli, ili apunguze haja zake. Lakini yeye si malaya. Kwamba kama mimi ningeweza kutumia vizuri hata kidogo nilicho nacho, yeye angeridhika.”

“Subiri kwanza Colins. Wanawake zako wengine kabla yake  walikuwa wakisemaje? Maana isijekuwa hicho ni kisingizio chake tu!” “Sikuwahi kuwa na mwanamke kabla James! Yeye ndio mwanamke wangu wa kwanza. Na kama unavyomjua mama. Katika hilo, alihakikisha ananiweka sawa tokea mdogo sana. Kwa hiyo ikaniingia akilini. Kwamba si kitendo unafanya tu hovyo. Kwa hiyo katika maswala ya ngono, mimi si kwamba nimekubuhu. Yeye ndio mwanamke wangu wa kwanza, na akaishia kunitia kilema.”

“Sasa inahusianaje na Jelini?” “Imeniathiri James! Nikiwa na Jelini, naweza nikasisimkwa kabisa. Tena napatwa na hisia ambazo naweza sema sijawahi pata maishani. Nikiwa kwenye hiyo hali, gafla hofu ya ajabu inaniingia kiasi ya kwamba nashuka kama ‘joka la Kibisa’. Sasa siku ile uliponisaidia kumsaka Jelini, si nilienda naye kwangu?” “Nakumbuka.”

“Aisee tulipata wakati mzuri! Mzuri sana, wa ajabu. Mimi mwenyewe siku ile nilitamani sana kufanya naye mapenzi. Tukiwa kwenye ile hali, si hofu ikanijia tena mpaka nikaanza kutetemeka!” “Haiwezekani! Mbele yake!?” “Kitandani kaka. Sasa akajua kabisa. Maana nilikuwa juu haswa, nakaribia kumtoa nguo, ndio nikanywea kama mtoto wa kiume aliyezaliwa leo. Akatoka kitandani.”

“Sasa kwa kupaniki, maana na yeye nilikuwa nimemuandaa, yupo juu haswa. Ikawa kama nimemkatili, nikamwambia naona tusubiri mpaka ndoa. Si na yeye akajua kama niliishi na Love kama mke! Akaniambia bado namuwaza Love ndio maana nimeshindwa kulala naye. Akaondoka usiku huohuo, sijamsikia tena mpaka leo.” “Duuuuh!” James akakwama.

“Sasa hapo ndio nini? Mimi nakwambia yote hayo, wewe unaishia kusema ‘duuuh!’” “Acha kunikasirikia bila sababu. Nafikiria.” “Sasa unafikiria nini? Maana mimi nakutegemea wewe unisaidie. Na wewe unakwama!” James akabaki ametulia. “Na wakati ukifikiria, acha nikuongezee upande wa Kasa.” “Kasa, yule mzee tena?!” “Aisee bado hajakata tamaa kwa Jelini, mpaka napagawa!” Akamsimulia mazungumzo yote kati yake na mzee. James akabaki hoi.

“Nahisi dunia si yangu kabisa. Nimkose Jelini!” “Itabidi urudi kwa gia kubwa.” James akawaza kwa sauti. “Ndio nafanyaje?” “Hivi ulivyonielezea mimi, ndio na yeye umwambie.” Alishituka Colins, mpaka akapaliwa. “Sasa nini?” “Hakika nataka kujua upande uliopo James! Upo kama hunitakii mema vile! Maana mimi nilipanga chochote kilema nilichonacho, nikinyamazie mpaka ndoa. Aje akutane nayo ndani ya ndoa.” “Kwamba ujifiche kwake, ukidhani mkiwa ndani ya ndoa ndio itakuaje?” “Si hataweza kuniacha tena!? Wewe vipi James? Unakuwa kama hunifikirii!” “Akija kufanya kama Love?” Hapo Colins akapoa.

“Wewe hutamani kuja kuwa na mwanamke atakayekupenda hivyo ulivyo mpaka kifo chako?” “James! Tunamzungumzia Jelini, kaka! Mimi sio mwanamme wake wa kwanza. Jelini hazinguliwi na pesa, kwa kumsikia mwenyewe anapenda mikono. Unakumbuka kilio alichomlilia yule mzee? Unafikiri ilikuwa bure? Halafu unataka nijitoe mwenyewe? Aniache mapema hivi hata sija..” “Sasa bora vipi? Ajue, akuache ujue moja kabla hujamuingiza kanisani, au ajue ndani ya ndoa kisha akuache na kanisani mlishafungishwa mpaka kifo?” Kimya Colins akifikiria.

“Ni bora umwambie ukweli ujue kama ni wako au si wako. Akibaki na bado akakupenda si ndio utajua unafunga ndoa ya mpaka kifo! Acha kucheza mchezo wa ajabu Colins! Ndoa si kama hivi anavyojifungia kwa mama yake, wewe upo kwako. Ndoa ni mpo naye nyumba moja. Kikitibuka huko ndani ya ndoa, halafu kina Kasa wakajirudi?” Colins akatulia. Akajua kimemuingia ila hofu.

“Nisikilize Colins. Mimi nimeishi na wewe, nakufahamu. Ni mtu mzuri sana. Mwanamke yeyote atakaye bahatika kuolewa na wewe, na akaridhika, mtakuwa na ndoa nzuri sana.” “Unafikiri hivyo?” “Ila uanze vizuri sasa. Sio kuweka msingi mbaya. Ungekuwa ukimuoa mwanamke kama aina ya kina Jema, ni rahisi kumwambia mpaka ndoa. Ameokoka. Anaogopa kumtenda Mungu dhambi. Lakini wewe umeenda kuchagua mwanamke wa viwango vingine kabisa, halafu anakujua na wewe upo katika ulimwengu wake. Huna sababu ya kumwambia mnasubiri. Kwa nini?” “Namuheshimu.” “Kwamba mwanamke mliyekuwa mkiishi naye mwanzo, tena kwa muda mrefu huo hukuwa ukimuheshimu?” Kimya.

“Hizo ndio sababu zinazokufanya ukataliwe. Uongo wa waziwazi.” “Sasa hata nikitaka kumwmabia, nampataje? Jelini alitupa chooni namba yake ya simu kwa ajili ya kuniridhisha. Akitaka aniaminishe hatakaa akarudi tena kwa yule mzee. Nisaidie.” James akashituka na kutoa macho. “Sikutumi ukamwambie maswala ya mapenzi! Acha kupaniki hovyo. Nataka tu umwambie tukutane tuzungumze.” “Hapo sawa. Nilifikiri unataka uanze yale mambo yako!” “Mimi sio mjinga.” James akamwangalia kwa kumsuta na kuendelea kula.

“Ni mjinga kidogo tu kwa Jelini.” Akajirudi nakumfanya James amtizame tena. “Acha ushabiki James!” “Labda nikusaidie, sio ujinga, ni unakuwa unachanganyikiwa.” “Naona unaanza matusi, huna msaada.” “Nitazungumza naye. Ila sitoi ahadi.” “Hata hilo tu nashukuru. Ila iwe leo sasa.” “Umeanza Colins!” “Kwa hiyo unataka mpaka nije kufa? Utamwambia nini mama yangu?” “Daaah! Colins ukianza jambo lako! Basi nitakwenda kwao leo.” “Hapo sawa. Sio sasa tena uende usiku ambao unajua wazi wamelala!” “Unataka nikazungumze na Jelini au hutaki?” “Basi. Ila ujue sitalala nitakuwa nikisubiria simu yako.” “Hata bila simu yangu, hulali. Acha kutaka kuja kunibebesha lawama.”

Kwa Jelini.

Jioni baada tu yakutoka kazini akapitia kwa kina Jelini. Akamkuta ametulia kimya nyumbani kwao, mtoto wake anafanya yake. “Karibu shem!” “Nashukuru japo najua umeshajua ni kwa nini nipo hapa.” “Kama ni juu ya Colins, acha nikwambie ukweli shem.” Hofu ikamuingia. Asije anza kuzungumzia mapenzi naye! James mtu wa maadili sana na mipaka.

“Mimi Colins simtaki tena.” “Jelini!” “Mimi sina hela wala si kwamba ni tajiri nitegemee starehe kwenye hilo. Raha yangu ni moyo wangu. Sasa kuwa na Colins kwangu ni adhabu shem! Inakua ni kumbembeleza yeye kila wakati kwa kila jambo, wakati mimi ndio…” “Unataka ubembelezwe.” “Hapo umemaliza. Nataka mimi ndio nibembelezwe na nipendwe mimi tu. Sio kama hivi mimi na Colins. Hivyo SIWEZI na SITAKI.” “Colins anakupenda Jelini.” “Upendo wa hivyo mimi shem siutaki. Ujue kwa nini nilimlilia sana Kasa?” James akajiweka sawa.

“Unataka kujua au na wewe hutaki?” “Ni kwa nini?” “Mwenzio alikuwa akinibembeleza kama yai! Ananifikiria mimi mchana na usiku, na kutafuta jinsi ya kunifurahisha kila wakati. Alivyogundua mizawadi yake hainifurahishi, akatafuta kujua ninachokipenda. Huwezi amini shem, yule mzee na biashara zake na utajiri wake wote, akiwa na mimi ni mimi tu. Akili, mawazo na mikono yake ni mimi tu.”

“Atakaa na mimi kama vile kijana wa kijiweni asiye na mipango mizito. Na simu ya kazi anazima inabaki simu ya familia tu, tena ya dharula. Na tena kama sio dharula, akipigiwa na wanae mimi nipo naye, anawaambia kabisa, atazunguza nao kesho yake akiwa kazini, ndio maana wanae wakaanza kunichukia.” “Sikujua hivyo!”

Ubaya Ubaya Tu.

Ubaya Bayana.

“Mimi nimeambiwa na mashoga zangu wa saluni. Aliyempa habari zangu za uongo Love, ni mwanae Kasa. Anaitwa Kemi. Maana mimi aliponiambia Colins eti Love ameongea habari zangu kwa wazazi wake, akiwa na uhakika kuwa ameambiwa na mtu wa karibu sana na Kasa, ikabidi nianze uchunguzi. Nikaanza kujua anakoenda saluni Kemi na Love. Nikapajua.” “Jelini! Umejuaje yote hayo!” “Umesahau mimi mtoto wa mtaani shem? Shule niliyonayo ni ya mtaani. Mashoga zangu ni wa mtaani. Saluni ndio mitaa yangu ya kujidai. Huna utakaponisema saluni, maanti zangu wasinifikishie ujumbe.” James akachoka.

“Sasa ndio nikaambiwa Kemi amemuahidi Love atamsaidia kunitoa kwenye familia, sijui ‘umoja wao wa familia’ kama walivyofanikiwa kunitoa kwenye familia yao.” “Kwao walikutoaje?” “Hata sijui shem! Mimi ninachojua ni kwa Kasa niliondoka mimi mwenyewe. Na yule mzee ananitaka mpaka kesho. Sema tu mimi simtaki tena. Naona nitulie mpaka nije mpata mwanaume kama yeye ila anioe ndoa.”

“Sasa si ndio Colins!” “Shem wewe hujaelewa. Mwenzio simtaki tena Colins. Ananiumiza roho bila sababu. Kwanza kwao wana mambo mengi. Wataninyima raha bure. Mimi simtaki tena.” Akaongea kama jambo la kawaida.

“Mimi nilifikiri ulimpenda Colins!?” “Wala nisikudanganye shem. Kwa mara ya kwanza nahisi nilipenda. Ila kama mapenzi ni vile, mimi sitaki tena. Bora nije niolewe na mtu nisiyempenda kama Colins, ila niwe na raha.” “Jelini!” “Kweli shem. Mbona Kasa sikuwa nikimpenda au niseme sijawahi kujisikia kwake kama vile nilivyokuwa nikijisikia kwa Colins, lakini tulikuwa tuna raha shem! Asikwambie mtu. Tulikuwa tukianza stori zetu, tunacheka mpaka machozi, tena ujinga tu. Na si unamuona yule baba alivyo na maakili na hela, lakini tulikuwa tukiongea ujinga, tunacheka bila kuchoka.”

“Anaweza akanipigia simu katikati ya kazi, mchana kweupe, ananiambia amekumbuka hiki na kile tulichokuwa tumezungumza labda siku iliyopita, akaanza kucheka peke yake, tena saa ingine katikati ya mkutano mpaka watu wanamshangaa. Basi hapo tena tunaanza stori. Hakuna chakuumizana roho, wala sijui ujinga kama huu unaoendelea kati yangu na Colins. Mimi hivyo sitaki.” James akachoka kabisa.

“Sasa nikamwambiaje?” “Mwambie mimi simtaki tena.” “Jelini!” “Basi tafuta jinsi ya kuzungumza naye, ila ukijua mimi simtaki tena.” “Hutapata mwanaume kama Colins, Jelini. Ame…” “Mimi mwenyewe sitaki mwanaume kama yeye.” James hoi. “Wakuninyima raha! Hapana shem. Nyinyi mna mambo mengi yakuwafurahisha. Kweli mimi kidogo nilicho nacho pia nikigawe! Leo ni yeye. Halafu nasikia tena ndugu zake wapo kinyume na mimi! Akuuu! Kwa nini! Kwanza hayo ndio yatakuwa maisha gani? Yaani yeye aninyime raha, na ndugu zake pia! Akuu.”

“Na kwa Kasa mbona kama watoto wake walikuwa kinyume na wewe?” “Bwana yule mwanaume pale nilimuheshimu, shem. Alisimama kama simba akinilinda, mpaka wanae walikuwa wakiniogopa. Wewe unafikiri kwa nini Kemi alinichukia?” “Ulichukua nafasi yake.” “Basi umemaliza. Alikuwa akimwambia kabisa, azungumze naye akiwa ofisini maana akiwa nyumbani yupo na Jelini.” “Jelini!?” “Muulize Kelvin atakwambia maana na yeye kilimpata kitu. Alijidai kunidharau, eti mimi mtoto wa mtaani tu, malaya, nashinda baa. Maneno kama hayo anayosambaza Love huko kwa kina Colins. Acha baba yake ambadilikie. Muulize, atakwambia. Mimi ndio maana nikabaki naye. Maana Kasa alinijua ndani na nje, lakini bado akaniheshimu. Nikiongea, ananisikiliza. Nikiwa naye, utafikiri dunia nzima tupo peke yetu! Huwezi mfananisha na Colins kwangu hata kidogo. Ndio maana mimi nililia sana nilivyomfumania.” James akabaki ameinama. KAKWAMA.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Shem wewe ungeenda tu kumpumzika.” “Basi nikuombe jambo la mwisho.” “Juu ya nini?” “Naomba ukutane na Colins mzungumze.” “Basi kumbe wewe shem hujui! Nilikuwa kwake, tukazungumza kila kitu. Akanieleza kwa mapana na marefu ndio nikaja kufikiria, nikajua yeye hatakuwa mume wangu. Ananinyima raha.” Jelini akawa amemaliza, akabaki akimwangalia shemeji yake. Kimya.

“Yaani kama hujaelewa shem, mimi na Colins hatuna chakuzungumza tena. Sitaki tena.” “Nimekuelewa Jelini. Ila naona kama unatupa bahati.” “Acha tu ipotee. Nitajua mbele ya safari. Kwanza mimi mwenzio sipo kama Jema. Maswala ya kuolewa hivi na kutulia nyumbani! Sio kabisa. Sasa hapa katikati nikataka kujaribu, ndio nimeona kumbe ndio vigumu hivyo! Sitaki tena. Nikupe chakula shem?”

“Naona Jema ananisubiria nyumbani.” “Ameniambi. Ujue Jema anakupenda sana?” “Najua Jelini. Hata mimi nampenda mke wangu. Ananivumilia kwa mengi.” “Nikwambie shem, uvumilivu unakuja kama mpo na mtu upande mmoja. Jema ameshajua upo naye katika kila upande, ndio maana anakuvumilia. Huwezi kuvumilia usilolijua!” Hapo James akakubaliana naye.

“Au uongo shem? Utamvumilia mtu mwenye vifichovificho?” “Huwezi.” “Basi umemaliza. Mimi mwenzio si mbaguzi wa watu. Kila mtu ninayemfahamu mtaani mshikaji wangu. Mpaka mateja mimi wangu. Ndio maana mimi nazurura mpaka usiku, nasindikizwa na vibaka, mpaka utashangaa. Kila kona hapa mtaani napajua na watu wake. Napenda na kuheshimu watu wote. Nawajua. Na kuna maeneo japo wanaudhaifu wao, hata hao mateja nawavumilia. Huko saluni naweza nikaenda, nikatoka nimependeza lakini sijalipa hata shilingi. Kwa sababu sisi wenyewe tunajuana na kufaana nyakati ZOTE. Nikichoka au mambo sio mazuri, nakwenda mtaani kucheka. Sasa leo niolewe, niwe na mawazo, halafu eti nifungiwe ndani sina hata wakuzungumza naye! Akuu!” Hapo akapandisha mabega kabisa na kunyanyuka kochini.

“Acha nikupe mzigo wa Jema. Tena mama alinituma kwake leo, nimeona uvivu kutoka. Najua atampigia kumuulizia kama nimepeleka.” “Sawa.” James akapewa huo mzigo tena Jelini akiwa amesimama kumuashiria ndio waagane. Na yeye akawa muungwana, akaondoka.

Mjumbe Hauwawi.

Akiwa njiani akampigia simu Colins. Akatafuta hekima ya kuzungumza naye. “Kwa jinsi nilivyomsikia Jelini, si kwamba hakupendi, ila anawasiwasi na aina ya mahusino yenu. Anachoona yatamfanya aendelee kuishi bila furaha. Ndio maana anaona asitishe.” Hapo akajisahau. “Kwamba hanitaki tena, sio kwamba anasubiria mpaka ndoa!?” “Acha nikwambie ukweli Colins, anavyosema mazungumzo yenu ya mwisho au ulichomwambia mwishoni, kilimfanya arudi kwao afikirie zaidi.” James akaendelea kwa makini tu ila kwa uwazi.

“Yeye binafsi anasema anakupenda sana. Lakini imekua adhabu. Ni bora vile alivyokuwa na yule mzee, hampendi kama wewe, lakini alikuwa na furaha. Anasema kwako wewe anakupenda sana, lakini imekuwa ni adhabu, na yeye hataki. Wewe unamjua Jelini alivyo.” “Daah! Sasa kwa nini hukumwambia tukutane tuzungumze?” Lawama kwa James. “Nimemwambia Colins. Ila anasema mara ya mwisho mlikuwa nyumbani kwako. Mkapata muda mzuri tu wa kuzungumza na wewe ukaongea vizuri tu. Sasa hicho ulichomwambia eti ndio kimemfanya akafikirie na kugundua, hataki tena. Ila habari njema, harudi tena kwa yule mzee. Amesema anajua yule mzee bado anamtaka, lakini amekusudia hatarudi tena.” Akamueleza kwa kifupi ila kwa makini mazungumzo yake na Jelini, mwishoe akasikia akimuaga bila ya nyongeza. “Nashukuru kaka. Salimia familia huko.” Siku zikaendelea ila taratibu isivyo kawaida kwa Colins. Mchana mrefu, usiku mrefu zaidi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kemi Anaendeleza Mashambulizi. Amefanikiwa Kuingia Mpaka Kwenye Ukoo Wa Kina Colins Kupitia Love. Mwisho Wake Ni Nini?

Jelini Na Colins Huo Ndio Mwisho?

Usipitwe.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment