Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 50. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 50.

 “Unajiandaa kwenda kanisani?” Baba mtu akamuuliza. “Hapana.” Akamjibu. “Unamaanisha nini!?” “Na maanisha leo siendi kuabudu, nina ratiba nyingine, hivi hapa nilikuwa nikijiandaa nitoke.” Akamuona baba yake akitingisha kichwa kwa masikitiko makubwa sana, Colins asielewe. “Kuna nini!?” “Kweli hii sio akili yake. Kweli siku ya kumuabudu Mungu, unaacha kwenda kanisani, unasema unaratiba ingine! Tokea lini siku ya kuabudu unakuwa na mipango yako na si Mungu?”

 “Baba wewe unataka kujiudhi bure, na kutengeneza kesi yako mbele ya babu na bibi. Tafadhali acha mazungumzo yanayotuweka sisi mbali zaidi na tulipo. Nilishakwambia swala la kanisani nitalifanyia kazi. Nikishapata sehemu itakayoendana na mimi na mke wangu, nitaanza kwenda huko. Kwanini kutaka kugombana na mimi kila wakati? Kwa nini hutaki kuniacha ukaangalia ninachofanya?”

“Kwa sababu unapotea, Colins! Huyo mwanamke uliyempata safari hii anakupotosha. Hauongozi vizuri. Unakuwa kama umeharibiwa ufahamu kabisa!” Hapo Colins akashindwa chakujibu kabisa. Akabaki kimya akimtizama. “Unanisikia Colins?” Akacheka kwa masikitiko. “Unanidharau mimi Colins!?” “Nasikitika jinsi unavyojiandaa kumchukia mke wangu. Maana ulishasema hutamkubali. Hilo halikuwa tatizo. Maana si lazima wewe umkubali, ni mke wangu mimi. Sasa kukuona unajiandaa na kumchukia pia! Ndio nasikitika. Na tafadhali naomba niwaombe kwa heshima baba, mama, bibi pamoja na babu. Nina ratiba imebana kidogo, nataka nitoke sasahivi halafu hichi kilichowaleta hapa, tafadhalini sana, kwa heshima zote, naomba tukifanye wakati mwingine hata jioni.” Hilo ombi likawa baya zaidi. Likathibitisha kulogwa kwake.

Mambo yakazidi kuwa mabaya, hayaishi. Bila kutarajia, Love na wazazi wake na wao akashangaa wanaingia hapo kwake. Mashitaka yakaendelea. Love akitoa mazito na makubwa haswa juu ya Jelini mpaka kumshangaza Colins, maana alizungumza kwa kumfahamu haswa. Mambo yakazidi kuwa makubwa na mabaya zaidi, Jelini akimsubiria waende hospitalini.

Kwa Jelini.

Huku kwa Jelini alipoona Colins hafiki mpaka mida ya saa 6 mchana, na yeye wasiwasi umemzidia, alishajiandaa tangia saa nne asubuhi. Hana simu ya jinsi yakuwasiliana naye, akajua tayari mambo ya familia yake yameanza. Hakutaka mengi. Alishakusudia siku hiyo akapime afya yake. Akamuaga mama yake. “Si ulisema unakwenda na Colins?” “Mimi hata sijui kinachoendelea mama. Colins aliniambia angekuwa hapa saa 4 asubuhi bila yakukosa. Simuoni! Na mimi nazidi kuingiwa hofu. Maadamu nimekusudia kwenda, acha tu niende nikajue moja kwenye maisha yangu.”

“Nikisema nimsubirie Colins, mpaka lini mama yangu? Anamaisha yake na vipaumbele vyake. Mpaka aje anikumbuke mimi, si leo. Na ni mimi ndio naendelea kutesema, maisha yake na watu wa nyumbani kwao yanaendelea vizuri tu.” Akaongea kwa kusononeka kweli. Mpaka hapo hata mama Jema akashindwa chakusema. Kwa kumsikia Colins alisikika anamipango mizuri. Ila utendaji wake, kila mara anamuumiza mwanae. Akabaki na yeye akiwaza.

“Ila naomba simu nimpigie dada Doro yeye anajua mambo hayo. Anielekeze vituo hivyo vinavyoweza kuona hata kama vijidudu vimeingia hivi karibuni. Na kama nimeathirika, yeye pia anielekeze wapi pakupata dawa. Yeye anayajua yote hayo.” Hapo mama yake akamsifu. “Kweli umeamua!” “Nakaa kwa hofu sana. Sitaki kuendelea kuishi na sintofahamu hii.”  Akachukua simu ya mama yake na kuingia nayo chumbani.

Old is Gold

Kwa mara nyingine, akampata Doro. “Ulinisusa mdogo wangu.” “Mambo mengi dada. Ila kuna nilikopita hapa katikati, kunanitia wasiwasi, nataka nikapime, nijue afya yangu. Nisaidie kunielekeza sehemu wanayoweza kuona hata kama vijidudu vya UKIMWI ndio vimeingia karibuni.” Akamuelekeza. “Acha niende dada japo naogopa!” “Nani anakusindikiza?” “Naenda peke yangu. Mama anaenda kwenye biashara zake.” “Acha basi nikupeleke mimi. Ulinifaa sana kipindi nahitaji mtu. Au hutaki, bado umenikasirikia?” “Yaliisha bwana dada. Nashukuru. Ila sina gari na hii simu ya mama.” Wakajipanga pakukutania ikawa nyumbani kwa Doro, Doro akiwa amefurahi sana. Jelini alikuwa mtu wake haswa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akamrudishia simu mama yake, na kutoka hapo akiwa amependeza haswa, maana alijiandaa akijua anakuja kuchukuliwa na Colins, kwahiyo akatoka hapo akiwa ameumia roho, akijua ni mambo yake tu na Love ndio yanayomfanya azidi kumpa Love kipaumbele na si yeye. Akanyongea haswa. “Nitaweza kweli!?” Akajiuliza bila jibu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mtoto wa jiji akaunganisha usafiri mpaka nyumbani kwa Doro. Mpaka Doro akalia kwa furaha ya kumuona Jelini. “Ulinitupa mdogo wangu.” “Wewe ndiye uliyeanza kunisimanga dada. Nikaona unachoongea kweli, nikarudi kwetu.” “Najuta mpaka leo. Ni bora vile tulivyokuwa tukiishi wote akilala siku nzima kuliko kubakiwa na mimali yote hii halafu sina mtu wa kweli. Naomba yaishe.” Zikaanza stori kuanzia walipoachana mpaka hapo.

Safari ya hospitalini ikaanza. Vicheko wakipeana habari za watu wanaofahamiana. Jelini muoga wa hospitali, sie huyo. Kajawa cheko. Anatolewa damu hana habari. Yeye na Doro kazi yao kumaliziana sentesi. Ikaendelea mpaka anapewa majibu anajulikana hana maambukizi yeyote ya UKIMWI, likawa tena si jambo la furaha kama kukutana na Doro, shoga yake kipenzi. Simu kwa washikaji wa kijiweni kwamba Jelini ameonekanika zikaanza. Wakapanga kukutana mahali. Cheko.

Ikawa imeshafika jioni ya siku hiyo ya jumapili, kwa mara nyingine tena Jelini akarudi baa. Zikaanza kuagizwa nyama choma. Stori, cheko. Jelini akaanza kwa kusema, “Mimi siku hizi sinywi.” Lisaa la kwanza na la pili, vishawishi vikamzidia. “Basi nakunywa tu moja.” Haikuishia moja. Wala haikuhitaji ushawishi mkubwa kuongeza ya tatu na ya nne mpaka akapoteza mahesabu. Stori, anacheka kama anatekenywa! Pombe ikaendelezwa.

Ubaya, Ubaya tu.

Huku kwa Colins, jumapili aliyokuwa akiitegemea iwe nzuri, ikageuka kuwa mbaya haswa. Kesi ikawa kubwa. Mzee yupo akidai anamuokoa mwanae kwa mwanamke aliyepata mashitaka yake kuwa ni malaya tu wa baa. Anatembea na wazee kama kina Kasa. Alishazaa. Hayo yote yaliletwa na Love akiwa amesindikizwa na wazazi wake siku uliopita, ya jumamosi. Wazazi wa Colins wakaelezwa kwa mapana na marefu juu ya Jelini, mpaka mama CJ akajuta kumfungulia mlango Jelini.

Jumamosi.

“Hakika sikujua kile kilio cha yule binti ni kumlilia mzee kama yule!” “Sio binti yule anti. Ni mwanamke kabisa ambaye ana mtoto mkubwa tu. Na nasikia ni muharibifu. Kila akiingia kwenye familia ya watu ni kuharibu kama hivi mnavyomuona Colins ameharibika. Huko kwa Kasa nasikia ameharibu kwelikweli. Kafarakanisha watoto na baba yao. Unaambiwa huyo mzee alikuwa akipenda vijana wake, lakini baada tu ya kuingia Jelini, mzee amewafukuzisha kazi binti yake na mumewe. Kijana wake ambaye ndiye kama mrithi wa huyo baba, ambaye huyohuyo Jelini nasikia alimtongoza yeye kwanza, kijana akamkataa, akamfuata baba mtu, naye amewafarakanisha kabisa kwa maneno ya uongo na kiuchonganishi. Huyo mzee Kasa amemfukuza kijana wake kabisa sababu ya huyohuyo Jelini.”  Love aliendelea mbele ya wazee hao usiku huo wa jumamosi.

“Tena hapo ni baada ya kumfukuzisha kazi binti yake huyo mzee Kasa kwenye kampuni ya baba yake. Inavyosemekana huyo binti ndiye aliyekuwa akimkaimu baba yake kwa miaka mingi sana. Na mumewe hivyohivyo huko Shinyanga. Lakini unaambiwa kwa muda mfupi tu huyu Jelini alipoingia kwenye maisha yao, amefanikiwa kumtenga huyo baba na kila mtu akabaki yeye tu mwenyewe akimtawala. Wanavyohisi huyu Jelini anatumia nguvu za giza.” Love akazidi kuwaogopesha sana wazazi wa Colins.

“Nasikia akianza na mwanaume, anakuwa kama hivyo Colins. Kila mtu anamuona mbaya. Wanasema anakuwa kama anawateka ufahamu kabisa. Akisharidhika hapo, ndipo sasa anaanza kumtenga huyo mwanaume na kila mtu ili abaki peke yake azidi kumtawala na kumfilisi kabisa.” Love akaeleza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ndipo sasa ikabidi mzee ampigie simu baba yake ambaye ndiye babu yake Colins ambaye Colins alimshitakia huko. Mzee akaeleza kwa masikitiko makubwa, na hofu kubwa sana. Akimuomba baba yake amsaidie kumuokoa kijana wake wa pekee. Ndipo sasa babu akaacha kila kitu na kukimbilia jijini, kufanya hicho kikao kilichochukua karibu siku nzima.

Siku Ya Kufa Nyani, Miti Yote Huteleza.

Colins alifika nyumbani kwa kina Jelini mida ya saa 11 jioni. Akakuta nyumba imefungwa. Huna jinsi ya kumfanya Jeremy akufungulie mlango, kama hajaambiwa na bibi yake. Atanyamaza ndani kimya kama hayupo. Baada ya kubisha hodi na kuchoka, akaamua kumpigia simu mama Jema.

“Samahani mama yangu. Namtafuta Jelini.” “Atakuwa nyumbani.” Jinsi alivyojibu, Colins akajua si kwema. “Nimegonga, hakuna aliyefungua.” “Basi atakuwa hajarudi.” Colins akatulia kidogo kisha akaendelea kabla hajakatiwa simu. “Samahani kwa usumbufu. Sijui unajua alipokwenda?” “Kwani nyinyi mlikubaliana leo mnakwenda wapi na saa ngapi?” Colins akajua amekasirika, asijue na yeye anahali mbaya kuliko yake.

Hapo ametoka kwa lazima nyumbani kwake, akiwaacha wazee bado wanataka kikao na yeye. Akawaambia lazima aondoke, kikao kiendelee wakati mwingine. “Ilikuwa nije kumchukua asubuhi ya saa nne, lakini nikapata wageni wa gafla. Babu na bibi wakisindikizwa na wazazi walikuja kwangu. Hivi nimelazimishia tu kuondoka.” “Basi yeye alichoka kukusubiri. Akijua mambo yako ya familia yatakuwa na maelezo kama hivyo, halafu yeye ndio aje akumbukwe kama hivi. Akaona amtafute Doro, amsindikize.” Moyo wa Colins ukapasuka kama kumeangushwa chuma.

“Doro tena!?” “Ndiye aliyekuwepo na kuweza kumsaidia! Jelini muoga wa hospitalini. Hajiwezi mbele ya sindano bila mtu. Wewe upo na familia yako. Mimi natafuta pesa ya chakula kwa ajili yake na mwanae. Sasa ulitaka akwame akiwa anakusubiria wewe ambaye kila leo kunakuwa na sababu ya msingi ya kutokumpa yeye kipaumbele? Ulitarajia kweli akwame akikusubiri wewe mpaka lini?” Colins akaanza kumuelewa James juu ya mama Jema na wanae. “Jelini hana simu mama yangu. Nitampataje huko aliko?” “Sijui.” Akamjibu hivyo na kuagwa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ikabidi akae nje ya nyumba mpaka giza likamkuta. Saa moja, mbili, tatu, Jelini hajarudi. Saa nne usiku mama Jema akawa anaingia, akashuka kwenye gari yake na kumsogelea mama Jema aliyekuwa ameshushwa na pikipiki. “Bado tu upo!?” “Najua nimekosa mama yangu. Nisaidie jinsi ya kumpata Doro. Simuamini Doro akiwa na Jelini. Nisaidie kunielekeza anapoishi au namba yake ya simu.” Mama Jema akafikiria.

“Wewe utamchanga Jelini, Colins. Kwa nini usiweke sawa mambo ya nyumbani kwenu kama ulivyosema, kisha kumtafuta? Jelini alikusudia kutulia kabisa. Lakini kwa jinsi unavyo mchanganya, nirahisi sana kurudi kule kwenye pombe zilizokuwa zikimsaidia kuficha kinachoendelea moyoni. Asubuhi unakuwepo, jioni unapotea na kumuacha akisononeka hapa kwa uchungu sana. Utaendelea hivyo mpaka lini?”

Nimeamua kumuoa Jelini, mama yangu. Na hata babu na wazazi nimewaambia leo. Aidha wapende wasipende, mimi nitamuoa Jelini. Love amepewa maneno machafu sana juu ya Jelini, naye ameyabeba kama yalivyo amewaambia wazazi, wazazi nao wameyabeba kama yalivyo na kuwamwagia bibi na babu ambaye alikuwa upande wangu. Sasahivi wote wapo kinyume, hawamtaki Jelini kwenye ukoo.” Mama Jema akashituka sana.

  “Amesema nini?” “Mambo mengi wala hayatasaidia. Na mimi mengine ndio nimeyasikia leo.” “Juu ya huyo Jelini?” “Unataka nikwambie ukweli wote?” “Hata ukificha itasaidia nini? Bora niambie tu.” “Tabia zote za Jelini kushinda baa, na zaidi mzee Kasa. Hapo ndio parefu na papana.” Colins akamueleza mpaka yule mama akakaa chini kwenye kibambaza.

“Colins!?” “Yaani ni mengi na marefu. Hapa nimelazimishia kuondoka. Wamejaa hapo nyumbani kwangu, wote wananihurumia kwamba akili sio zangu, nimelogwa. Ila hitimisho la babu, ameniambia nisimwingize Jelini kwenye ukoo wake.” “Sasa utafanyaje?” “Kama nilivyowaambia wazazi na kina babu pamoja na familia ya Simba, Jelini ndio mwanamke nitakayezeeka naye. Ndiye mwanamke pekee atakaye pokea kiapo changu kanisani, kwamba, mpaka kifo. Na nitasimamia hapo. Tafadhali nisaidie kumpata Jelini. Nina hisia mbaya sana. Asije kuwa amerudia pombe kitu ambacho amesema ameamua kuacha kwa ajili ya mtoto. Sasa kitendo cha kutokuwepo hapa na mtoto mpaka muda huu, hisia zangu zinaniambia vinginevyo.”

“Sasa anakoishi Doro mimi sipafahamu. Labda tutafute namba aliyompigia Doro asubuhi wakaenda kuzungumzia chumbani. Walichozungumza huko sijui.” Akamkabidhi simu. Colins akapekua hiyo simu mpaka akafika namba zilizopigwa asubuhi. Akamuonyesha kama hiyo anaitambua, hakuwa akiitambua. Akaichukua.

“Nikuulize kitu kabla hujaondoka?” Colins akatoa macho kwenye simu akiwa anaelekea kwenye gari yake. “Utafanyaje kweli ukimkuta baa na amelewa? Maana mimi Jelini namjua. Muoga wa matatizo. Nina uhakika kwa asilimia 100 sasahivi atakuwa amelewa huko. Na hivi yupo na Doro!” “Nitamchukua mama yangu. Siwezi kumuacha huko na siwezi kumleta hapa akiwa amelewa. Najua atajisikia vibaya sana asubuhi pombe ikiisha.” “Sasa unataka kumpeleka huko wanakomsema na tabia zake hizihizi!? Maana itakuwa kama unakwenda kuwathibitishia huko kwenu.”

“Ninauhakika kwa asilimia kubwa, watakuwa wameshaondoka. Na pia nitampigia simu mlinzi kuhakikisha hamna mtu hapo kwangu ambako naishi peke yangu. Tafadhali usiwe nawasiwasi. Mimi ndiye nimeharibu leo na kumfikisha hapo, na mimi nakuahidi kumlinda Jelini. Wakati wote nitamlinda. Akiwa mikononi mwangu, nakuhakikishia atakuwa salama. Ila sasahivi lazima niende kumtafuta. Siwezi kulala wala kufikiria nikiwa sijui alipo.” “Mmmh!” Mama Jema akaguna akiumia moyoni. Maana yeye alikuwa akimuacha tu. Hata akipotea siku tatu, alikuwa akijiambia atarudi, leo Colins anakwenda kumsaka! Akapoa kabisa.

“Nakushukuru Colins. Na tafadhali nijulishe pindi utakapompata. Na sijui utampataje, maana na Doro mwenyewe ni mlevi haswa. Anaweza asipokee simu mida hii ambayo atakuwa ameshalewa.” “Usiwe nawasiwasi.” Akaondoka kama akimbie na kumuacha mama Jema na hukumu pamoja na mawazo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kazi ya kumsaka Jelini ikaanza. Akaanza kwa kumpigia simu Doro. Ikaita bila mafanikio. Akajaribu kukumbuka jina la baa aliyosikia Love akisema ndiko anakoishi Jelini akibadilisha waume za watu. Akiwatumia mpaka vyooni. Akafika hapo, akauliza. Kweli walikuwa wakimfahamu Jelini na Doro, ila wakaambiwa siku hiyo hawajaonekana hapo. Wazo la kwenda kwa mzee Kasa likamjia usiku huo.

Kwa tajiri hupotei. Akampigia simu mwanae akitaka kujua baba yake anapoishi. Kwa mshangao sana, Kevin akamuelekeza. “Ila mida hii mzee anakuwa ameshalala. Hawezi kukuona. Kwema?” “Nashukuru sana. Kwaheri.” Hakutaka mengi, akamkatia simu, safari ya kwa baba yake ikaanza.

Mafahari Wawili.

Akafika getini akaambiwa hivyohivyo. Mzee amelala, haamshwi isipokuwa ni dharula. “Sasa hii ni dharula. Mwambieni Colins amesema ni dharula. Lasivyo mimi naondoka, na nikiondoka hapa, kesho hamtaelewana naye, na kibarua hapa kitakuwa kimeisha.” Akawatisha kwa mengi mpaka wakaona bora kwenda kumuamsha. Baada ya muda akaona anafunguliwa geti, akaingiza gari yake mpaka ndani, akamuona kwa mbali amesimama kwenye ngazi.

Akashuka garini na kumsogelea akimtizama tu. “Nimekuja kumfuata Jelini.” Akamwambia hivyohivyo. Mzee akabaki akimtizama kwa muda kisha akaweka mikono mfukoni. “Jelini yuko wapi?” “Umechanganyikiwa au unakitafuta kifo kwa nguvu.” “Hakika sasahivi huna utakaloniambia na kunitisha. Namtaka Jelini, bila hivyo hapa siondoki.” “Sema utaondoka maiti. Kwa sababu umebakiza dakika chake sana nakupiga bastola, Colins.” “Mimi sijakufuata wewe, nimemfuata Jelini. Na kwa taarifa yako, ni mke wangu. Tutazaa watoto wanne.” Kasa akamcheka na kumuudhi zaidi Colins.

“Acha dharau.” “Sasa kama hayo unayoongea unayaamini, kwa nini upo hapa kwangu usiku huu?” “Namtafuta Jelini wangu.” “Kama kweli ni wako, hajakuzalia hata mtoto mmoja bado, tayari umeshampoteza! Wewe utakuwa baba au mume wa namna gani?!” “Usizidi kunichanganya.” “Nakwambia ukweli. Wewe ulishasikia Jelini kupotea kipindi yupo kwangu?” Kimya kwa muda.

“Wewe ni mzembe. Unang’ang’ania mambo usiyoyaweza.” “Namuweza Jelini.” “Yuko wapi sasa?” “Mbali na ile baa ya Tegeta, wapi kwengine unafikiri anaweza kuwepo?” “Yaani mara hii tu umeshamrudisha baa!?” “Acha kuniuliza maswali ya kunidhihaki.” “Mimi nilipokuwa na Jelini, alitulia na kuacha pombe kabisa. Huko alikokuwa akijifichia huzuni zake, ALIONDOKA. Nikaweza kumtuliza, akatulia. Wewe umekua naye hata…” “Acha kabisa kunilaumu mimi. Wewe ndiye uliyemrudisha Jelini huko sababu ya kupenda hovyo wanawake. Jelini anawasiwasi akihofia umemuambukiza UKIMWI.” Kasa akakunja uso.

“Acha kujidai huelewi. Sio wewe uliyekufumania hapa kwenye dangulo lako? Na anakujua huwa hutumii kinga. Tokea akufumanie mpaka leo, Jelini halali vizuri sababu ya wasiwasi pengine umemuambukiza vijidudu vya Ukimwi. Wewe ndiye uliyemuharibu. Na nipo hapa kwa kuwa wewe unahusika kwa kumpoteza mke wangu. Na nakuonya acha mtindo wa kunitisha. Sitishiki kirahisi. Niambie maeneo unayodhani anaweza kuwepo, nikamtafute.” “Nini kinakupelekea kufikiri nitakwambia alipo?” Colins akamtizama kwa muda akawa kama na yeye amegundua kitu kwa Kasa.

“Unanipotezea tu muda, hata wewe hujui alipo kama mimi tu.” “Nipe masaa mawili tu kama hujasikia Jelini ameamkia hapa nyumbani kwangu.” “Nakuonya. Kaa mbali na Jelini.” “Wewe si unataka kujifananisha na mimi? Sasa kaa pembeni uone baada ya masaa mawili kama hutasikia Jelini ametulia humu ndani. Na ndipo utakapojua kama hili ni dangulo au sehemu pekee iliyokuwa ikimtuliza Jelini na kumfanya asizurule tena mtaani.” Kidogo akatishika.

“Nakwenda kumtafuta mimi mwenyewe. Acha ujuaji kwenye mambo yasiyokuhusu. Na nikikuona karibu na Jelini, nakuchoma kisu.” Akamtisha Kasa. “Nakupa mpaka asubuhi. Nisipopata simu yako ya kuwa umempata Jelini, ujue mimi nitamtafuta. Na nikimpata mimi, hakika nisikuone tena Colins. Nitakuadhibu mpaka ujute kumfahamu Jelini. Kama unadhani nakutania au nakutisha, muulize Kevin linapofika swala la Jelini kama huwa natania. Nitakuweka mbali na dunia aliyopo Jelini, hutakaa ukamuona tena. Haya toka haraka kaanze kumtafuta. Na asubuhi nipate majibu ya kueleweka si ujinga na uzembe. Unapotezaje mwanamke kama Jelini?!” “Wewe…” “Toka na usirudie tena kunijibu. Ondoka haraka kabla sijabadili mawazo na kuamuru ufungiwe jela, na usitoke mapaka uje ukutane na hao watoto wa nne wa Jelini lakini ni wa Kasa. Potea.” Colins akatoka hapo kwa haraka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jelini!

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment