Kwa Jelini.
Jelini akarudi kwa
dada yake akamkuta amebaki peke yake. “James ameondoka na yeye sasahivi. Mama
yeye naona ni kama mliongozana. Hakukaa sana baada ya wewe kuondoka. Ila amefurahia
pesa ulizompa huyo! Anasema imekua kama ameokota alumasi!” Jelini
akacheka tu akikaa. “Vipi lakini kichwa?” “Naendelea vizuri. Hapa
nimekurudishia gari nimfuate mama. Nataka nijifunze anavyofanya kazi. Mama
anajuhudi Jema! Mpaka nahisi mimi nimechukua uvivu kutoka kwa huyo
mwanaume aliyempa mimba yangu.” Jema alicheka sana.
“Haki tena Jema. Mimi
mpaka nasema pengine ndio maana mama aliachana naye, labda alikuwa mvivu sana!”
“Na baba yangu mimi naye?” Wakaanza kucheka wakifikiria baba zao na sababu za
kutokua na aina ile ya mama kama mke. “Ila bwana umejua kumfuta mama machozi!”
“Mwenzio mimi amekuwa akinifuta machozi maisha yangu yote. Na mwanangu.”
Akamuona amepoa.
“Unafikiria nini?”
“Unakumbuka vile nilivyokuwa na mimba ya Jeremy?” “Halafu ulikuwa mdogo Jelini,
halafu mkali haswa!” “Ni hofu na uchungu Jema. Ukumbuke nilikuwa nikibakwa
kikatili mno. Kwa hiyo nilikuwa na maumivu ya roho na mwili muda wote mpaka
niliposhika mimba akaniacha, ndio mwili ukapona ila si maumivu ya roho! Halafu
nilikuwa silali sababu ya hofu ya kuja kumtoa mtoto kulekule kwenye maumivu,
halafu nilikuwa sijui nakuja kufanya naye nini!”
“Sasa kitendo cha
chupa kupasuka, nalia, mama akanisaidia mpaka kunipeleka hospitalini,
nikadhani ataondoka, lakini akabaki na mimi! Halafu kujifungua tu, akamtawala
mtoto kama wake! Pale ndipo nikarudisha tumaini, na hofu kupungua.” “Na mama
alihangaika na Jeremy jamani! Kuanzia
mpo hospitalini mpaka mnatoka, kama yeye ndiye kazaa!” “Kumbe unakumbuka Jema?”
“Kabisa.”
“Ile ilinisadia sana
kutulia, na ndio kumpenda mama kukazidi. Hakujua tu alichonifanyia, ila
nikikubwa zaidi ya hizo pesa anazohangaika nazo sasahivi. Mama hajawahi
kunichoka mimi na mwanangu hata mara moja Jema. Akimuongelea Jeremy ni kama
mwanae wakuzaa!” “Mimi nafikiri ndivyo anavyomuhesabu.” “Kabisa. Mimi sikuwa
nikijua umwa ya huyu mtoto wala vaa yake. Ni mama. Nilikuwa nikiishi naye, nina
uhakika wa maisha yangu na mwanangu na sijui bwana alikuwa akifanyaje! Wakati
wote Jeremy alikuwa msafi na anachakula bila kuzembea!” “Si kama sisi tu! Mama
hajawahi kutulaza njaa aisee yule mwanamke! Muhangaikaji hivyohivyo, siku zote!”
Wakatulia kidogo wakimfikiria mama yao.
“Ila ninachotaka
kusema Jema, hiyo pesa ilipotea njia ili imfikie mama wala si yangu. Mimi
nikiishika tu, itaisha yote kwa matumizi yasiyo maana. Lakini sasahivi mimi na
Jeremy tunakula vizuri kweli pale nyumbani. Mama anafanya manunuzi ya pale
ndani na kulipa bili zote bila kuwapigia simu kina mama mdogo kuwakopa! Hilo
linanifariji, hujui tu Jema.” “Hata yeye mwenyewe anasema anapambana msirudi
tena kule kwenye kuombaomba. Na naona wanajipanga hapa na James, atafanikiwa
sana tu. Mungu atasaidia.” “Na mimi nitaongeza nguvu.” Akaongeza akiwaza.
“Lakini isiwe
sasa, Jelini.” Hakutegemea. “Nataka kuwa kama wewe Jema!” “Mimi nilifanya kazi
kwa bidii kwa kuwa sikuwa mgonjwa. Wewe ni mgonjwa Jelini. Hizo dawa za
kupunguza maumivu zisikudanganye, ukajisahau, baada ya muda ukarudia
hali mbaya zaidi ya hiyo. Jiuguze mpaka upone kabisa, ndipo uhamishe akili
kazini.” “Jema wewe! Mwenzio nipo nyuma sana!” “Najua na mimi nakuunga mkono
kwenye kutoka hapo. Ukipona tu, hata mimi nitakuhimiza.”
“Ni kwambie ukweli
Jema?” “Nini?” “Ukweli hiki kichwa si chakupona hivi karibuni. Sitaki tu
kusema. Nilimsikia yule daktari akimwambia Kasa siku moja hospitalini wakidhani
nimelala, alisema ndani nimeumia sana, mbaya ni kichwa. Mpasuko ulikaribia
ubongo kwamba hata fuvu la kichwa lilipasuka ndio kufikia karibu na ubongo.
Alisema itachukua muda mrefu sana kupona. Sikutaka tu kumwambia mama.”
“Basi mama amejua
kupitia Colins.” Jelini akakunja uso kwa mshangao. “Colins halali kwa ajili
yako Jelini. Anahangaika sana.” Hakuamini. “Na mimi!?” “Kabisa, mpaka
utamuhurumia. Alimwambia James, hakumbuki kulala usingizi mzuri tokea usiku wa
kwanza ametoka hospitalini kumuona Love, akiwa amevunja miahadi yenu,
kisha kukukosa kwa simu. Anasema hakumbuki kulala tena.” “Lakini nilimpigia simu
siku inayofuata Jema! Hakupokea simu yangu wala kurudisha ujumbe. Mimi nikaona
nimuache tu.” “Mimi sijui nini kilitokea Jelini, lakini yule kaka ni majibu
ya maombi yako.”
“Colins hawezi Jema.
Ana Love. Na ikifika kwenye swala la Love, yupo radhi kufanya lolote ilimradi
iwe Love KWANZA. Mimi hivyo siwezi Jema. Na mimi nataka mtu wangu wa
peke yangu kama hivyo wewe. James anakupenda Jema. Kweli unataka mimi niishie
na mtu kama Colins!?” “Mimi nahisi bado hujamjua Colins kama ambavyo mimi
nimeweza kumfahamu sasa hivi. Hivi unajua simu zote anazokupigia James, anakua
amesimamiwa na Colins, akitaka.., au acha niseme akilazimisha akupigie,
ajue jinsi unavyoendelea?” “Colins!?”
“Hakika tena.
Wanagombana hapa na James, mpaka nawafukuza ndani nawaambia wakamalizie
malumbano yao huko nje. Maana James analalamika mambo anayotaka akufanyie
mwishoe wewe utakuja kumuona anavuka mipaka.” “Wala nisikudanganye. Mpaka
nilimgusia mama ila kwa mipaka kidogo. Nikajiuliza, kujali kwa shemeji, ndio
kujali gani huko!?” “Basi ni Colins huyo. Hata Chaz ujue anatumwa na yeye huyohuyo
Colins kwa jina la James.” “Jema!” “Sikudanganyi Jelini. Haya, dawa pia ni yeye
mwenyewe Colins.” Jelini akabaki ametoa macho.
“Colins!?” “Hakika
Jelini. Yaani umemkuta hapa leo, sababu aliombewa msamaha kwa mama, alipoambiwa
tu amesamehewa na akajieleza hakukusudia kukuumiza ni shindikizo la
wazazi, hapohapo akaja kuanza kuweka mashariti ya jinsi gani uhudumiwe.”
Jema akamueleza yote.
“Colins anakupenda
Jelini!” “Ila mimi sitaweza Jema. Japokuwa nampenda sana, lakini siwezi.
Kwao wana mambo yakizungu na umoja ambao huo sitaweza. Mimi nataka mtu
atakayenipenda na kunijali kama hivyo yeye anavyomfanyia Love. Sasa leo aje
anioe halafu aniache ndani aniambie nakwenda kwa Love sijui familia imesema
hiki au kile! Hakika sitaweza Jema. Mshauri tu aache.”
“Natamani kama haya
ungekuwa ukizungumza na James. Maana yote hayo James ashamkaripia nayo. Tena
sio kama hivyo wewe. Ni kwa kugombana kabisa.” “Sasa anasemaje?” “Hata leo amemwambia
na mama. Kuwa huo utaratibu wa kwao yupo kwenye kuweka kikomo. Hivi hapa hata
nyumba ametuambia anarekebisha kwa ajili yako na watoto wenu. Amemwambia mama
amemuita hata babu yao ili aje awaweke wazee wake sawa. Ili aheshimiwe, abaki
kuwa na wewe tu na mjenge familia yenu.” “Jema!?”
“Kama huamini muulize
mama. Amejieleza leo hapa, mpaka utamuhurumia. Mwenzio anamipango na wewe,
tena mikubwa. Na anajua amekuumiza sana tu. Ila anasema anataka aweke mambo
sawa ndipo akurudie. Hataki kurudi kisha kukuumiza tena na mambo ya kwao.
Anachotaka arekebishe kwanza kwao ndipo akurudie.” Jelini akabaki kimya
akifikiria.
Penzi Lisilo Changanywa Na Pesa.
La Dhati.
Ilipofika mida ya
jioni Jelini na mwanae wakaondoka kurudi nyumbani. Bado mama yake hakuwa
amerudi nyumbani. Kwa kuwa walishakula nyumbani kwa Jema, Jeremy akapitiliza
chumbani kwake kufanya yake, mama mtu chumbani kwake kubadili nguo. Lakini
akiwa anamfikiria sana Colins. Moyo wote upo kwa Colins. Hakujua kama
anamuhangaikia kwa kiasi hicho. Moyo ukajawa penzi, akashindwa kujua
chakufanya. Tatizo akabaki Love. Akamtumia ujumbe.
‘Nashukuru
sana kwa msaada unaonipa hapa nyumbani na dawa. Asante.’ Colins alipopata tu
huo ujumbe, akili ikaruka na kujua moja kwa moja ni Jelini. Akamjibu. ‘Nakufikiria Jelini wangu. Nakufikiria sana. Nipe tu muda.’
Jelini akafikiria, akaona amjibu. ‘Naomba wewe endelea
tu na maisha yako, Colins. Mimi sitaweza, kwanza sitaki. Na mimi nataka mtu
wangu kama hivyo Love alivyokupata wewe.’ Wakati anatuma huo ujumbe, akamsikia mwanae analia chumbani.
Akashituka sana. Akarusha simu kitandani na kukimbilia chumbani kwake.
Akakuta analia,
amekaa chini, vitu vyake vimezaa sakafuni. “Kuna nini!?” “Nimeteleza na kuangukia treni yangu, imevunjika yote.”
Akazidi kulia. “Umeumia?” “Nimeharibu treni yangu
yote!” “Usilie, njoo tujenge wote. Nitakusaidia.” “Wewe hujui.” “Jeremy naye, si utanifundisha!” Akazidi
kulia. “Nakuahidi nitakaa hapa chini nijenge na wewe.” “Wewe
hujui. Na nikianza kukufundisha ujue ndio nazidi kuchelewa.” “Basi kama
hutaki kunifundisha, uwe unanituma vitu nakuletea.” “Nimejenga
muda mrefu sana. Mimi sitaki tena.” “Jeremy wewe unakata tamaa! Ujue
ukirudia tena hutachukua muda mrefu kama mwanzo kwa kuwa sasahivi unajua sio
kama mwanzo. Njoo mtoto mzuri. Njoo tuanze.” Akaendelea kulia amekaa chini.
Jelini akaanza
kukusanya. Vilikuwa vimesambaa chumba kizima. Sakafu hiyo mtelezo. Marumaru
inang’aa, kitu kikianguka hakuna ukinzani. Kazi ya kuvikusanya ikaanza
akimbembeleza. “Ujue wewe Jeremy ni mtoto mzuri sana? Halafu mimi nakupenda,
unaakili. Na nina kuaminia. Ukianza sasahivi, mpaka muda wako wa kulala
ukifika, utakuwa umefika mbali sana.” Akampamba hapo kwa maneno mengi,
akanyanyuka kumsaidia mama yake kukusanya huku akilia taratibu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda wakiwa
wameshakusanya vyote hapo chumbani, Jelini ndio amekaa chini kabisa
kumuaminisha atamsaidia, wakasikia kengele mlangoni. “Narudi kuja kukusaidia.
Usidhani nakimbia.” Jeremy akamwangalia bila kujibu akaendelea huku akifuta
machozi na kamasi.
Kufungua mlango
Colins. Akashituka sana. “Kwanini unapenda kunitesa bila sababu Jelini?” “Mimi
nimefanya nini!?” “Kwa nini hujibu jumbe zangu na hupokei simu?” “Nikikwambia
kwa maneno, hutaamini. Twende nikuonyeshe. Kwanza hata simu yenyewe sijui ilipo!
Nifuate chumbani kwa Jeremy. Kule anakojenga vitu vyake.” Hapo akapunguza sauti kama anamnong’oneza.
Akashangaa kidogo ila akamfuata nyuma.
Kuingia, wakamkuta
ameanza kulia tena huku anaanza kujenga. “Treni ya kaka imeparanganyika.
Aliidondokea.” Hapo Jeremy akaongeza kilio. “Usilie Jeremy. Acha nikusaidie.
Sasahivi nakurudishia iwe kama ulivyoijenga mwenyewe. Na nitakapofika
ilipokuwa, niambie ili nisikumalizie.” “Nilikuwa
nakaribia kumaliza! Reli yote ilikuwa tayari. Nimeharibu bahati mbaya.”
“Usilie. Acha tuanze pamoja. Muda si mrefu itarudi kuwa kama mwanzo.” Colins
akaanza kazi ya ujenzi wa treni ya Jeremy.
“Basi hata nitumeni
kitu jamani! Mbona mnanitenga?” “Wewe hujui. Utaharibu zaidi.” “Mwaya Jeremy!
Basi bwana kama hutaki msaada wangu.” Jelini akatoka kwenda kufuata simu akijua
yapo majibu ya Colins.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi chumbani
kwake alipokumbuka alipokuwepo nayo mara ya mwisho. Akaikuta kitandani. Akakuta
missed calls 5. Akashangaa sana. Akakimbilia ujumbe. ‘kwa
jinsi ninavyokupenda, mimi nisingekukatia tamaa Jelini. Na wala nisingekususa
kwa kumuachia mwanaume mwingine. Hujui ni kwa kiasi gani nilikuwa nikikusubiri.
Hata nilipopigwa marufuku, nilibaki nikikusubiria tu, bila kukata tamaa.’
Mpaka Jelini akakaa kitandani. Akajifikiria, akaona atoke.
Kurudi chumbani kwa
Jeremy akakuta Colins amekaribia kumaliza, Jeremy anafuraha huyo, cheko nje
nje. “Muone!” “Anko anajua sana.” “Lakini hapa palipobaki nakuachia Jeremy.
Malizia mwenyewe.” “Asante. Ila wewe unajua sana. Mbona unafanya harakaharaka
hivyo! Mimi nimechukua siku nyingi kufika hapo ndio maana nilikasirika.” “Sasa
nisikilize Jeremy. Hii spidi inakuja kwa kurudia kujenga zaidi ya mara moja.
Hiki unachokifanya wewe unakumbuka nilikwambia nilifanya mara nyingi kwa miaka
mingi zaidi ya umri wako?” “Nambuka.”
“Sasa ujue ajali kama
hizi huwa zinatokea sana. Hata mimi nilikuwa nikiharibikiwa au kuweka LEGO
moja au mbili sehemu isiyo sahihi. Kwa hiyo wakati mwingine nilikuwa nikibomoa
ili nichomoe hiyo LEGO nyuma kuja kuweka mbele. Cha kwanza na muhimu,
huu mchezo unafundisha kutokata tamaa. Kuna mambo mengine utakuja kupitia ukiwa
mkubwa, yapo kama hivi vitu/LEGOs zikiwa hazijajengwa. Lazima kukaa chini na
kuanza hatua ya chini kabisa mpaka kufika mwisho na uwezo wa kutatua tatizo
kubwa kabisa. Kukata tamaa isiwe sehemu yako. Umeelewa?” “Sirudii tena
anko. Ikiharibika, nitaanza tena.” “Hapo umenifurahisha. Haya endelea.”
Wakatoka na Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Umekula?” “Hapana.” “Kuna
chakula, acha nikupashie moto ule.” Akaongea hivyo na kuondoka akimuogopa
kumuangalia. Colins akamfuata jikoni. “Katika mahusiano niliyokuwa nayo na
Love, wakati wote alinionyesha hanitaki ni kama namghasi. Nikaishi naye
nikijibidisha kumuonyesha naweza kuwa kile anachotaka bila mafanikio.” Jelini
akabaki akimsikiliza ila kushindwa kumtizama kabisa akiwa ameshajua
anachomaanisha.
“Ulipokuja wewe, na
kuonyesha kunijali na kunihitaji mimi kama Colins, ikanitia moyo Jelini. Lakini
umenibadilikia vibaya sana. Uliniacha nimesimama nje ya geti!” Jelini akaumia
sana. “Leo unaniandikia ujumbe wa kunikataa!” “Ila siku ile nilikuaga Colins na
nikakwambia kichwa kinaniuma naenda kulala.” “Hakika mimi siwezi
kukufanyia hivyo Jelini! Eti uje kwangu, nikuache nje ya geti! Hata nisingeweza
kulala.” Jelini akazidi kuumia.
“Nahisi
nachanganyikiwa Colins. Sijui chakufanya, sijui nafasi yangu ni ipi! Najihisi
ni kama nakulazimisha tu, ndio maana ikitokea Love anakuhitaji, inakuwa rahisi
kuniacha mimi.” “Si kweli. Si rahisi hata kidogo, Jelini. Mwenzio nimeshindwa
kulala usingizi mzuri tokea usiku ule. Sikuwa na jinsi Jelini. Ila nipo kwenye
kutengeneza. Tafadhali usinichukie kiasi cha…” “Sijakuchukia Colins. Ila sielewi!
Sijui hata nafasi yangu itakuja kuwa wapi kwenye maisha yako! Naishia kuumia tu
kila wakati!”
Jelini akamuona
anafungua vifungo vya shati kwa juu. Akakunja uso. “Unataka kujua nafasi yako?”
Jelini akabaki ametulia. “Au ni kweli umenikatia tamaa kabisa?” akapandisha
mabega juu kukataa kama kawaida yake. “Basi nipe mkono wako wa kulia.” Jelini
akiwa haelewi akanyoosha mkono.
Akasogea mpaka karibu
yake na kuuweka moyoni mwake. Jelini alikuwa akitetemeka mwili mzima. Amemshika
Colins kifua! “Maadamu hayo mapigo ya moyo
yanaendelea kudunda kwenye huu mwili, ujue hakuna mwanamke mwingine kwangu ila
wewe tu Jelini. Itabaki hivyo mpaka uje uhakikishe hakuna unachosikia kwenye huu
moyo wangu, ndio ujue umepoteza mtu wako wa peke yako.” “Kweli Colins? Maana
na Kasa alisema maneno yanayo fanana kama hayo, lakini nikaja kumfumania na
mwanamke wake. Kama hivyo wewe na Love.”
“Mimi sio yule mzee.
Na swala la kuachana na Love sio nita, ni nimeshaachana naye.
Hayupo kwenye maisha yangu na wala hatawahi akarudi. Umebaki peke yako na
itabaki hivyo mpaka kifo changu.” Jelini alifurahi, akabaki hajui chakufanya.
Ila akatoa mkono hapo kifuani. “Naomba amini mimi ni wako mpaka kifo, na anza
kuishi na mimi hivyo.” “Nilikata tamaa Colins.” “Isiwahi kutokea. Si kwangu.
Ujue nitabaki na wewe mpaka unichoke.” “Mimi siwezi kukuchoka. Mwenzio
nakupenda Colins.” Kisha akaongeza.
“Safari hii jishike
na wewe mapigo yako ya moyo.” Colins akacheka akijishika ila nje ya kifua.
“Mmmh!” Akataka kujua anataka kusema nini baada ya kujishika. “Basi, kila unapoyasikia hayo mapigo yako ya moyo. Popote
ulipo. Muda wowote, hata kama mimi hunioni, ujue yupo Jelini anayekupenda kwa
moyo wake wote, mpaka niondoke hapa duniani. Hakuna ulimwengu utakaokuwepo
wewe, nisikupende Colins. Ujue nitakupenda mpaka kifo chako.” Colins
akataka kumuwahi ambusu.
“Bado sijapima, Colins!
Tafadhali naomba tusubiri.” “Siwezi. Bora uniue wewe kuliko kuja kufa na kitu
kingine. Siwezi kuishi bila wewe Jelini. Niruhusu angalau kukukumbatia na
kukubusu tu. Mengine naweza kusubiri.” Jelini akafurahi huyo. Alipomuona
amelainika, akamsogelea. Colins alipoipata midomo ya Jelini tu, na yeye hali
ikabadilika. Jelini akajiachia hoi hajiwezi mikononi kwa Colins. Alikuwa
haamini. Amepata midomo ya Colins! Akajisogeza
zaidi. Wakalemewa kabisa, Colins akajikaza kiume, akamuachia taratibu, wote
wakihema.
“Nimefurahi Colins!
Nimefurahi sana.” “Sasa umefurahia nini?” “Wewe kunikiss hivyo! Nimepatwa na
hisia za ajabu! Sijawahi jua kama zipo ndani yangu hisia za namna hiyo!
Asante.” “Nakupenda Jelini. Nakupenda sana. Usije wahi sahau hata siku moja.”
Akatigisha kichwa kukubali akicheka. “Sasa unacheka nini!?” “Nimefurahi sana.
Hujui tu.” “Kweli Jelini?!” “Mimi sijui bwana! Lakini ninavyojisikia
kwako Colins, aisee ni hisia za tofauti! Acha nikupashie chakule ule,
nikubembeleze ulale.” Colins akacheka asiamini.
“Nakaribishwa tena
chumbani?” “Si umesema hujalala vizuri tokea siku ile?” “Nimechoka Jelini.
Nikilala sitaweza kuamka mpaka kesho. Acha tu nikalale kwangu. Nahisi leo
nitalala. Na hivi nimekukiss. Nitalala.” “Nimekumiss Colins. Ndio maana.” “Hata
mimi nimekumiss Jelini wangu. Acha nile nikukumbatie.” Ikawa kama ameahidiwa
ulimwengu. Akamuwekea chakula mezani. “Ukimaliza kula, njoo chumbani kwangu.”
Kisha akakimbilia kuoga wakati akila.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipomaliza kuoga
akavaa nguo za kulalia kabisa. Ila za stara. Akamtumia ujumbe mama yake. ‘Colins yupo nyumbani. Amechoka sana.’ Mama yake
hakujibu. Akampigia. “Sasa mbona hujibu!?” “Nina mambo
mengi Jelini. Na ninajua kuna unalolitaka tu. Sasa hata nikikushauri kitu
utanisikiliza?” “Sasa ushauri gani mama jamani! Mimi nataka abaki na mimi.”
“Kwamba ahamie hapo?!” “Kuna ubaya gani? Si analala tu, kesho anaondoka? Tena ni
kama akipitiwa na usingizi. Sio kwamba anahamia!” “Nyinyi wawili mnajuana
wenyewe Jelini. Hakuna mnayemsikiliza. Nyinyi endeleeni.” Jelini
akaanza.
“Ameniambia
ananipenda mimi, mpaka kifo chake.” Mama Jema akacheka akimfikiria Jelini.
“Weza kuta na mimi nimepata mtu wangu mama. Nampenda
sana Colins.” “Basi taratibu mama yangu mzazi. Taratibu ili uone ndoa.”
Jelini akatulia akifikiria. “Unanisikia?” “Ameomba
nimpe muda.” “Hata mimi ameniambia. Lakini asije akabweteka tu.” “Sasa
nitafanyaje mama? Nampenda Colins, sitaki nianze kumwambia mambo akanikimbia
tena. Naomba nimchukulie taratibu. Kama nimeandikiwa basi atakuwa wangu, kama
si riziki basi mama yangu.” “Na kweli. Haya, acha mimi niendelee. Nitarudi
kwenye saa nne.” “Jeremy yupo chumbani kwake, bado anajenga vitu vyake.” “Leo
ameniomba achelewe kulala. Nitakuja kumtoa huko mimi mwenyewe, wewe muache tu.”
“Nashukuru mama yangu.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akasikia mlango
unagongwa taratibu. Akajua tu ni Colins. Moyo ukajawa furaha. “Ingia tu.”
Akaingia. “Umeshiba?” “Nakuridhika pia. Sitaki sisi tukosane Jelini. Inaninyima
raha, kila kitu kinakosa ladha.” “Kwa kuwa nilikuwa sijakuelewa Colins.” “Kwa
hiyo sasahivi umenielewa?” “Ndiyo, na nakushukuru kunijali.” “Utaendelea
kutafuta mtu mwingine?” “Hapana Colins! Mimi nakutaka wewe.” Colins
akacheka kwa furaha akimsogelea.
“Na mimi nakutaka
zaidi Jelini wangu. Natamani ungeenda kunibembelezea kwangu sio hapa.” Jelini
akacheka akifikiria akiwa amemuelewa. “Siwezi kumuacha Jeremy. Halafu bado nina
hofu. Acha nikapime kwanza. Panda kitandani ulale.” “Nimechoka Jelini! Naweza
kupitiwa na usingizi mpaka kesho bure.” “Ndio itakuwa vizuri.” “Nilale hapa!?”
“Usiwe na wasiwasi.” Colins akafikiria, akasita. “Hata hivyo siwezi kulala bila
ya kuoga. Acha tukae wote, kisha nirudi tu nyumbani.” “Si uoge hapa?
Nitakupisha.” “Siwezi Jelini. Utanisamehe. Hii ni nyumba ya mama, haitakuwa
heshima. Ingekuwa kwako hapo sawa.” Jelini akamuelewa.
“Basi kwa kuwa
sasahivi umetulia. Rudi nyumbani ukapumzike. Tupange kuonana tena kesho.”
“Utakuja nyumbani?” “Ukinikaribisha, nitakuja.” “Pale napaandaa kwa ajili yetu.
Mimi, wewe na watoto wetu. Huitaji kukaribishwa. Muda na wakati wowote njoo tu.”
Jelini akafikiria mawazoni na kucheka.
“Nini?” “Nimefurahi
Colins! Ila usije badilika tu.” “Mimi si kigeugeu Jelini. Na nimekupata wewe
mwenye kila kitu, nitafute nini tena? Sina sababu. Nakupenda na nakuahidi
nitabaki na wewe tu. Nipe tu muda niweke mambo sawa. Nakuahidi tutafunga ndoa
kabisa.” “Kweli Colins!?” “Jelini wewe ni mke wangu. Moyo wangu ndivyo
unavyokuhesabu. Nakupenda, hata James anajua. Na naomba na mimi unihesabu
hivyo. Usije tafuta mtu mwingine. Utaniua Jelini.” “Wakati mimi ndio
nilikupenda kwanza, Colins wewe! Wewe ndio usije tafuta mtu mwingine.”
“Siwezi.” Yaakanza mabusu tena.
Hapo yanaendelea,
Jelini ananguo za kulalia. Colins akajitahidi kutovuka mipaka. Wakahamia
kitandani. Wamelala huku romance inaendelea. “Nikuombe kitu Jelini?” “Nini?”
“Kesho uje tushinde kwangu mpaka usiku. Au unawasiwasi na mtoto?” “Umesahau
nilikuwa nikishinda baa?” Colins akaanza kucheka. “Usicheke bwana! Ninachotaka
kukwambia, nilikuwa nikizurula, nikitoka hapa naweza nikaondoka hata siku tatu
au nne. Mpaka wakawa wameshazoea ni kama sikuwa nikiishi hapa. Kwa hiyo mama
amemfundisha huyo Jeremy, anajua kujitegemea mwenyewe. Hapo alipo, anamaagizo
ya mpaka anakwenda kulala. Wewe mjaribishe tu muulize pengine saa tatu
unatakiwa kufanya nini. Atakwambia.” “Haiwezekani Jelini!”
“Mama hakuwa na jinsi
Colins. Nilikuwa naishi na pombe kichwani muda mwingi sana. Hakuwa akiniamini
naye. Na yeye mama muhangaikaji. Ikabidi amlee hivyo. Ila hata mimi na Jema
tumekua hivyohivyo. Alikuwa akitufungia ndani ili akahangaike kutafuta pesa. Na
kama unavyopaona hapa, tumekua hapakuwa na majirani wengi. Hayo majumba
yamekuja kujengwa miaka ya karibuni tu. Kwa hiyo alivyotulea mimi na Jema, ndio
hivyohivyo na Jeremy. Anakua na maagizo yake ya mpaka usiku.” “Hasahau?” “Si
mama atampiga mpaka achanganyikiwe! Hathubutu kusahau. Halafu Jeremy yupo kama
Jema. Hataki matatizo. Mimi ndio alikuwa akinipiga sana.” Colins akazidi
kucheka.
“Nikuulize kitu
kingine. Wakati ulipokuwa ukiondoka hapa nyumbani kwa hizo siku tatu au nne,
ulikuwa ukienda wapi?” Akamjaribisha tena kuona kama kuna jibu la tofauti na
mwanzoni. “Kwa dada Doro. Anamihela huyo! Kwake pazuri kweli halafu chumbani
kwake amefunga A/C, basi nilikuwa nalala mchana na usiku kwa raha ya upepo
mwanana. Akienda kazini, ananiacha nimelala, jioni tunakwenda baa. Alikuwa
kampani yangu kubwa sana. Ndiye aliyekuwa akinipa pombe za bure na nguo nzuri
na za maana. Maana dada Doro anapenda kuvaa bwana! Na hapendi kurudia sana
nguo. Basi huko ndio nilikuwa nikiishi. Nikimkumbuka mwanangu ndio nilikuwa
nakuja hapa kidogo, narudi kwa dada Doro.”
“Kwa hiyo mpaka sasa
hivi mnamawasiliano?” “Kasa alihakikisha anamtoa kabisa kwenye maisha yangu. Kwanza
wivu, halafu alikuwa akisema haniongozi vizuri. Halafu naye Kasa alitukuta tupo
kwenye kutoelewana vizuri, kwahiyo kwa kifupi sijawasiliana naye muda
mrefu sana.” Colins akabaki akifikiria.
“Kuna jambo nataka
kukuuliza, ila ni kama nasita. Sitaki kukuumiza.” “Juu ya nini!?” “Natamani
kujua kilichotokea kati yako na baba yake Jeremy.” “Naomba usiwahi kumtambua
kama ni baba yake. Inaniuma sana. Wewe muite tu mwalimu. Mwanangu ni
mtoto mzuri sana, hawezi yule kuwa baba yake.” “Akija kutaka kumfahamu?”
“Hakika hatamfahamu. Mbona mimi na Jema mpaka leo hatujui baba zetu! Hakika sitaki.”
Akatoka kabisa hapo kitandani.
“Naomba usikarike
Jelini. Njoo. Nikatika kutaka kufahamiana na kuweka msingi wetu. Ujue kwangu
Jeremy atabaki kuwa kama watoto tutakao kuja kuzaa pamoja? Pale nyumbani kwa
James, sikuwa nikiongea tu. Namuhesabu ni kama mtoto wetu wa kwanza, watakao
zaliwa baada yake ni wadogo zake. Na tukioana tu, nataka nimuombe mama
tumchukue tuishi naye.” Jelini hakutegemea.
“Colins!?” “Kabisa.
Sasa wewe ulifikiria tutakuwa tukiishi bila yeye?!” “Pale kwa Kasa hakuwahi
kukaribishwa hata mara moja ila mimi tu! Na wala hakuwahi kutaka kukutana naye
watoke kama hivyo wewe ulivyotaka kutoka naye mkaogelee!” “Sasa hiyo itakuwa
familia ya namna gani? Nataka tumu adopt kabisa awe wetu moja kwa moja
na tuwe na dhamana naye. Wote tunatumia ubini mmoja.” Jelini akatulia kabisa.
Colins amekuja na gia kubwa. Akakusudia kumfunga kabisa Jelini. Atake
nini tena!
“Mwenzio nimejifunga
kwako Jelini. Nimejifunga mazima kabisa. Labda uniambie kama unawazo jingine.”
“Sina Colins. Ila siamini! Ujue wewe unaonekana kijana wa kileo, mtoto wa
mjini, hufananii na mipango uliyo nayo!” Colins alicheka sana.
“Kweli! Unaonekana
kama wale vijana ambao bado wanajirusha. Starehe kwa sana. Mambo ya club
na totoz. Ila ukiongea hivi, unasikika kama mtu mzima! Mawazo ya kikubwa si ya kitoto!
Mwenzio sijategemea!” “Nakupenda Jelini. Umekuja kunifuta majonzi nikiwa
sijatarajia. Ukanionyesha upendo wa kipekee. Halafu yale maneno uliyoniambia
siku ya harusi ya Jema na James, ambayo uliniambia hukumbuki,
yalinibadilisha sana moyo wangu.”
“Hivi nilisema nini!?”
“Hakika sitakwambia mpaka uje uyarudie tena mwenyewe. Maana niliuliza,
nikaambiwa, mlevi hazungumzi kitu ambacho hakipo ndani yake. Ila pombe
inamsaidia kukitoa tu. Mwenzio nasubiri tu, naamini ipo siku utakuja kuniambia
tena. Maana ulimaanisha Jelini.” Jelini akatulia akijaribu kukumbuka bila
kufanikiwa, huku Colins akiwa amejilaza hapo kitandani akimwangalia, yeye
amekaa.
“Hakika sikumbuki
Colins. Ila najua nakupenda wewe kuliko mtu mwingine yeyote yule
niliyekwisha kuwa naye. Nikikwambia hata nilivyokuwa na Kasa nilikuwa
nikikuwaza wewe, utaamini?” Colins hakujibu, kitu kilichomshangaza
Jelini. Akatulia kabisa.
“Nakupenda Colins.”
“Lakini mimi yule mzee ananiumiza kichwa Jelini! Sijui nifanyaje?” “Huko
sirudi tena Colins. Tafadhali usiwe na wasiwasi.” “Lazima na siwezi kuzujia. Japokuwa
uliniahidi kutorudi kwake, na nikakuomba ukiwa unarudi huko mimi niwe wa
kwanza kujua, lakini leo ulikuwa ukirudi kwake Jelini! Hilo linanitisha, wala sitakudanganya.
Najiambia kama nisingekuwepo kwa James leo asubuhi, inamaana pengine sasahivi
ungekuwa uko kwake, mimi tena basi.”
“Nisingefanya kitu
Colins! Nikuchukua tu vitu vyangu!” “Ambavyo uliniahidi unaachana navyo
Jelini! Lakini bado umeendelea kuvifuatilia. Hivyo vitu vimekua na nguvu
kubwa sana kwako kuliko ahadi na makubaliano yetu. Inanifanya
najuta kuzaliwa masiki. Najuta kuwa sina hela kama za yule mzee. Maana na mimi
kama ningekuwa na uwezo kama wake, inamaana pengine…” Akaona anyamaze tu.
Jelini akatulia akikumbuka alivyomtuma Sheha. Akafikiria. Akamuona anasimama
kufuata simu yake. Jelini ni mzuri bwana! Hata hapo tu Colins alikuwa akila kwa
macho.
Mtaka Chauvunguni, sharti ainame.
Ni Colins.
Akamuona anapiga simu.
“Ndosi?” “Kwema?” “Samahani nimekupigia muda mbaya.”
“Bila shaka. Kwema? Mbona umenyongea?” “Nilifanya kosa. Sikuwa nimefikiria
vizuri kwenye swala la kufuata vitu vyangu kwa Kasa. Tafadhali mwambie sivitaki
tena. Anaweza kumpa yeyote amtakaye.” “Jelini!?” Haikuwa ikiingia
akilini hata kwake. Na kwa kiasi alichomfahamu Jelini, alijua anamsimamo mkali.
Anapelekaje taarifa kama hizo kwa mzee!
“Hakika
tena Ndosi. Acha tu iishie hivyo. Na wewe nakushukuru kwa kila kitu. Hutanipata
tena kwa hii namba. Na tafadhali usijaribu kunitafuta tena. Nimemalizana rasmi na
Kasa, inamaana hata wewe tumemaliza. Sina nililobakiza kwako. Mambo yote
umenifanikishia vizuri tu, nashukuru. Nakutakia kila la kheri.” Akamaliza na kukata
simu bila ya kusubiri jibu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akamuona anampigia
tena mtu mwingine. Colins akimtizama tu. “Anti langu?”
“Niambie mtoto mzuri.” “Usiende tena kunidaia vile vitu.” “Jelini! Kwahiyo
unanitosa anti?” Sheha akaishiwa nguvu kabisa. “Hapana
anti. Miahadi yetu ipo vilevile. Ila usije kwenda kule, ukanitaja. Nishamwambia
wakili wake, vitu vyote sivitaki tena.” “Sasa mimi nitaenda kwake nimwambie
nini?” “Nitakuelekeza anga zake. Anapoendaga kwa chakula cha jioni, na maeneo
yake anayopenda kuwepo. Anti wewe mjanja. Hutamshindwa malaya yule.” Hilo
likamfurahisha sana Sheha mpaka acheka.
“Kama hivyo
sawa. Tena naona hiyo ndio itakuwa nzuri zaidi. Maana nikikutumia wewe, anaweza
akakataa akidhani nitakwambia. Acha nikamtege kivyangu.” “Na wala ukifanikiwa
huko huna haja ya kuniambia. Wewe endelea naye tu.” Sheha akafurahi kama
kapewa limwengu. “Nakushukuru mnooo.” “Wala usijali.
Kila la kheri.” Akaaga.
“Sasa usije
nisahau Jelini.” “Nakutumia sasahivi. Na tusije mzungumzia tena mimi na
wewe. Wako kabisaaa. Ufanikiwe, usifanikiwe, ni juu yako. Sitaki tena.
Ukimtaja kwangu ujue tutakosana anti.” “Hilo tena! Ndio raha yangu. Maana
nilikuwa nikihofia usije nitangaza nikifanikiwa.” “Sio mimi, na wala
hutanisikia nikimwambia mtu. Labda uropoke mwenyewe. Wewe mawindo mema.” “Mungu
akupe heri.”
Jelini akacheka na kukata.
Akamuona anaanza
kuandika ujumbe huku akifikiria mpaka akamaliza na kutuma. Akamuona tena
anaizima simu kabisa. Colins akimtizama tu. Kisha akatoa line nyuma.
Simu akaiweka mezani, akamuona ile line ameingia nayo chooni kwake.
Baada ya muda akasikia choo kikimwaga maji. Akajua ameitupia chooni. Akatoka na
kumuona anaingia chumba kidogo cha nguo, akatoka amevaa koti linalofanana na
kigauni kizuri sana chakulalia alichokuwa amevaa. Silk safi nyeusi. Na vile
alivyokuwa mweupe, ikatoa uzuri wa aina yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi kukaa
kitandani. “Nimemalizana ramsi na Kasa. Safari hii nakuahidi hutakaa
ukamsikia tena. Na samahani, nilikosea. Vile vitu vilikuwa vikiniuma roho
Colins, nikakosa uvumilivu. Lakini sivitaki tena. Huko sirudi, naomba
uniamini.” Colins akazidi kumpenda Jelini wake. Love hakuwa akikosea. Mara zote
hakuwahi kukiri kosa, na hata alipokosa basi amekoseshwa na huyohuyo
Colins. Akafurahi na kumsogelea na kumlalia hapo mapajani. Jelini akaona raha!
Akamshika kichwa vizuri.
“Naomba nikubali hivi
nilivyo Jelini. Naweza nisiwe na mali nyingi, lakini mimi tajiri wa mapenzi.”
Jelini akacheka. “Sitakusaliti. Utabaki wewe tu.” “Umenisamehe sasa?” “Naamini
tutakuwa sawa. Kwanza niambie ni nini umefanya? Sijaelewa mazungumzo ya simu ya
pili.” “Kuna dada namuunganisha na Kasa.” Colins akakunja uso. “Huyo dada
anatafuta watu kama Kasa, na yeye Kasa anapenda watu kama huyo dada. Sasa kwa
kuwa mimi simtaki tena, akaniomba nimpe yeye. Ndio nimemuachia.”
“Jelini!”
“Kasa ni malaya yule.
Hataishi bila mwanamke mmoja. Sasa kwa nini shoga yangu asinufaike naye,
akatulia. Maana yeye shida yake ni pesa. Hana shida na umalaya wa mtu kama Kasa.
Hivi kipindi hiki cha bunge, ametoka Dodoma kutafuta pesa, hana neno. Kwanza
mwenyewe anasema hataki mwanaume wa peke yake ili asimgande, aendelee na maisha
yake. Anapenda sana starehe anti Sheha. Alishazaa watoto wake wawili,
wanasomeshwa na baba yao, yeye starehe tu. Hataki kuolewa au kuwekwa ndani na
mwanaume. Kwa hiyo nimewaunganisha na naachana nao. Na wewe naomba tuache
kumzungumzia. Usinirudishe tena huko. Nishatoka. Inatosha.” Wakatulia kidogo.
Ukawa kama umezuka ukimya fulani. Jelini akimpapasa kichwani.
Akawa kama amekumbuka
kitu. “Lakini bado hujanijibu Colins. Najua nilikukosea. Nilivunja ahadi.
Umenisamehe?” “Yameisha na nimesamehe. Ila tafadhali naomba turudie maagano
yetu Jelini. Kuna vishawishi vingi na vitaendelea kuja. Yule mzee ni jaribu la
kwanza. Mengine yanakuja. Tusiposimama sisi wenyewe, tukateteana kwa hao
wanaojaribu kutuingilia, tutashindwa haraka sana. Mwenzio nataka niishie kwako
tu.” “Nashukuru Colins. Na ujue mimi sitakusaliti. Na mimi nitabaki na
wewe tu. Na si kwamba najitetea, hata ningeenda kwa Kasa, na ningemkuta, japo
nilimuomba mwanasheria wake amwambie amtaarifu kwamba nitaenda kuchukua vitu
vyangu, nikijua anaweza asiwepo awe kazini, lakini Colins, hata ningemkuta,
nisingefanya naye kitu.” “Huwezi kujua Jelini!” “Najua na ninajiamini.”
“Wanaume kama Kasa,
ndio ilikuwa kampani yangu. Na sikuwahi kushawishika. Mimi si limbukeni na wala
si dhaifu wa ngono. Kwangu nakiona ni kitendo kikubwa sana ndio maana yule
mwalimu aliniuma Colins.”
“Alikuwa akinifanyia
kama mnyama! Halafu hata baada ya pale hakuwa na shukurani kwa kutumia mwili
wangu. Anaweza maliza haja zake na kuanza kunipiga.” “Kwa nini tena!?”
“Kunitisha tu kwamba nisije sema. Yaani ilimradi tu. Mara ya mwisho
nilipomwambia nimeshika mimba. Jamani alinipiga, mpaka nikazimia.” “Jelini!?”
“Kweli
Colins. Alikuwa akinipiga eti nimtaje aliyenipa mimba. Mimi mzembe, najiachia
tu kwa wanaume. Yeye hausiki na huo ujauzito. Nikija mtaja atamuua mama yangu
na Jema. Bwana alinipiga siku ile!” “Naomba usilie Jelini wangu. Natamani
kama ningejua tokea mwanzo. Na ningekuwepo na wewe mahakamani. Niliumia sana.
Na sikujua kama ndio sababu iliyokuwa ikikufanya uishi na pombe kichwani kila
wakati!” Akajinyanyua pale alipokuwa amemlalia mapajani akimsikiliza na kuanza
mabusu kama kumtuliza.
Yakaendelea mabusu ya
muda, Colins akamuachia. “Acha niondoke nisije nikashindwa kuwa na kiasi, nikaishia
kulala kwa mama mkwe bure.” Jelini akacheka akimwangalia anavyonyanyuka. “Kesho
umekubali kuja tushinde wote?” “Nataka asubuhi nianzie hospitalini. Anti Sheha
ameniambia siku hizi kuna vipimo vyakupima UKIMWI hata kama vijidudu vimeingia
muda mfupi.” “Unataka nikusindikize?” “Ningeshukuru Colins. Maana naogopa kweli!”
“Basi usiende, unisubiri nitakuja kukuchukua twende wote mida ya saa nne
asubuhi bila kukosa. Na acha woga. Uwe umeathirika au la, zipo njia nzuri tu
tutashauriwa na kujua jinsi ya kuishi kuanzia sasa. Na usiulize swali jingine
mpaka kesho tutakapojua matokea.” Ikabidi tu acheke.
“Ulijuaje?!” “Najua
upo kwenye wakati wa kutaka kupata majibu yote sasahivi. Na najua utakaribisha
hofu isiyo na sababu. Leo ulale ukijua kila kitu kitakuwa sawa.” “Nashukuru
Colins.” Akamsindikiza, kijana huyo akaondoka bila mengi mpaka akamshangaza
Jelini na kumuacha na maswali yasiyo majibu yakueleweka.
Siku Ya Miahadi Mingine Tena, Na Jelini
Kesho yake akiwa
anajiandaa kwa furaha kubwa sana, akijua siku hiyo Jelini atakuwa nyumbani
kwake, akasikia hodi mlangoni. Akatoka na kubaki na mshituko mkubwa sana.
Hakutegemea aliowakuta hapo mlangoni. Babu yake, bibi pamoja na wazazi wake.
Akawasalimia na kuwakaribisha ndani akiwa bado na mshituko. Alitegemea babu
yake afike mjini ili azungumze naye yeye kwanza, ndipo akamrekebishie kwa baba
yake, lakini ujio wake ukawa kama wakushitukiza! Na sura aliyoingia nayo hapo,
si kama yupo upande wake, yupo na aliokuja nao!
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni Usiku Uliopita Tu, Ametoka Kutoa Ahadi Nzito Kwa Jelini, Na
Makubaliano Ya Kuanza Upya.
Je, Safari Hii Colins Atafanikiwa Kwa Jelini Aliyetupa Kila Kitu
Kwa Ajili Yake, Au Ndio ‘Sikio
Halizidi Kichwa’?
USIPITWE NA
MUENDELEZO.
0 Comments:
Post a Comment