Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 4. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 3 - SEHEMU YA 4.

Baada ya siku tatu mama Colins akamkuta yupo sebuleni mida ya jioni. Love hakuwepo, alikuwa kazini. Akamsalimia, akashangaa ameitika na kutulia kabisa. Si mkorofi wala hana fujo. “Unajisikiaje?” “Najisikia vizuri.” Akajibu Colins na kutulia. Akakuta sahani pembeni yake. Akajua chakula alichokuwa ameletewa na Jose, kijana wa kazi wa mama Colins, na kumwambia ahakikishe anamuwekea kabisa kwenye sahani, amekila. Hilo likamridhisha. Akakaa naye hapo kidogo, tv ilikuwa ikiendelea na yake, na Colins ametulia tu hapo kochini. Kimya mpaka mama yake akaaga.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mzee Simba na mkewe wakaomba kikao na wazazi wa Colins. Jumosi ikawa siku nzuri. Kikaandaliwa chakula hapo kwao, mzee Simba na familia yake akiwepo na Colins wakaenda hapo. Ikawa hali tulivu tu, na Colins ametulia haswa. Wakala na kunywa ndipo wakapata muda wa mazungumzo.

“Kwa kuwa sasahivi tupo ukurasa mmoja, nafikiri ni wakati muafaka wa Colins kuchukua nafasi yake, yeye kama kiongozi. Maadamu ofisi yake ipo tayari na kila kitu kimekamilika, naonelea jumatatu aanze majukumu yake.” Hilo likawa zuri na la kheri. “Na kwa sasa alipo, na wadhifa alio nao, lazima abadili hata aina ya usafiri na nyumba. Atakuwa mtu mkubwa sana. Au unasemaje Colins?” Pakatokea utani hapo kidogo, basi mzee Simba akaonelea kampuni yao, impe gari nzuri, na yeye na Love sasa, wahamie kwenye jumba la Kigamboni.

Huko nako wazee hao wawili na wake zao walinunua si kiwanja tu, ni kiwanja cha MAANA, karibu kabisa na baharini kama hoteli! Waliwekeza nguvu kwenye ujenzi wa hilo jumba, hata wao wenyewe hawakuwa wakiishi kwenye jumba zuri la kiasi hicho. Yote hiyo walikubaliana ni kwa ajili ya vizazi vyao. Basi likawa jambo la furaha kubwa. Wazazi wa Colins wakafurahia kuona tena wazo linatoka kwa mzee Simba mwenyewe wala si wao, upendo ukazidi kuongezeka katikati yao, wasijue yote hiyo ni shindikizo la Love kwa wazazi wake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jumapili kazi ya kuwahamisha wawili hao ikaanza. Kwa furaha zote wazazi hao kama hawamjui Mungu, na hawajui wanachokwenda kufanya vijana wao ni kwenda kinyume na amri ya sita. Kuishi bila ndoa. Wakatoa baraka zao. Mpaka siku inaisha, nyumba ikachukua sura ya wawili hao. Love na Colins. Wakaachwa hapo, Colins habishi kwa chochote, ila kuitikia kila jambo. Maisha yao yakaanza tena, wakiishi kama walivyokuwa wakiishi nchini Marekani. Wawili tu, ila hapo wakitumikiwa na wafanyakazi wa ndani na nje.

Penzi Linalosubiriwa.

Mwezi ulishapita tokea amsikie Victor. Na chuoni alisharudi kikamilifu akipambana tokea tukio la kina Belinda. Akabaki akijiuliza nakushindwa kuuliza, kulikoni Victor waliyetumia naye vilivyo kwenye hoteli ya maana vile! Alionekana kumkubali sana Vai. Vai akazidi kunyongea moyoni asijue wa kuzungumza naye.

Akabaki kukumbuka hili na lile alilozungumza Victor juu yake alipokuwa naye. Alimshusha hapo chuoni kwa ahadi ya kurudi jioni yake watoke kwa chakula. “Hata kama alirudi na kunikosa, ndio ashindwe hata kunipigia simu au hata ujumbe!” Ikashindwa kuingia akilini kwa Vai na kubaki akiumia sana jinsi alivyotumika kikamilifu na kuja kupigwa na kina Belinda kwa mwanaume aliyemuacha vibaya vile! “Hata ujumbe!” Akazidi kushangaa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hata hazikupita siku mbili tangia akijiuliza hivyo. Akiwa kitengo cha mifupa MOI, alipangiwa juma hilo na wenzie wawili, akiwa anapita nje ya vyumba vya madaktari akamuona Victor akiwa na watu aliohisi wazi ni familia yake kutokana na mazungumzo walipokuwa hotelini. Kijana mdogo aliyekuwa amefungwa POP mkononi. Akajua ni mmoja wa mtoto wake. Mwanamke, aliyeonekana mtanashati tu. Kikazi. Safi. Nadhifu. Macho kwenye simu kama mtoto wao. Moja kwa moja alijua ni Vera mkewe Victor. Na Victor mwenyewe ambaye macho yaligongana moja kwa moja na Vai. Akawa kama ameshituka kumuona Vai, akapigwa na butwaa kwa muda.

Vai alibaki akiwatizama kadiri alipokuwa akiwasogelea maana walikuwa wamekaa nje tu kama waliokuwa wakisubiria zamu yao ya kuingia chumba cha daktari. Ila hakuna aliyekuwa akimuongelesha mwenzie kati ya watatu hao, wanafamilia. Vai akashangaa alipowakaribia karibu kabisa, Victor akainamisha kichwa kana kwamba hamfahamu kabisa! Akahamia kwenye simu yake kama mkewe na kijana wake.

Vai akiwa amevaa sare yake ya kiuuguzi, akawapita bila hata salamu. Lakini kile kitendo kilimuuma sana, kwani Victor alijifanya ni kama amemuona mtu asiyemfahamu kabisa. “Kwamba kweli Victor ameshindwa kunigundua kwa ajili ya sare niliyovaa au ndio ameamua kujidai hanifahamu!” Akajiuliza Vai akishindwa kuamini vile alivyodharaulika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku ikaanza kuwa nzito. Wenzake walimuona kabisa hayupo sawa. Na kweli akili ilikuwa imevurugika vilivyo. “Isijekuwa lengo lake ilikuwa ni kuniambukiza tu gonjwa!” Akaingiwa hofu ya ajabu. Akijiambia pengine lengo lake lilikuwa nikusambaza tu vijidudu vya UKIMWI, ndio akamfikia na yeye. Hapo ndio akashindwa kabisa kufanya kazi. Akadanganya kichwa kinamuuma sana, akaruhusiwa kurudi hosteli kupumzika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walishatengeneza kautaratibu kao. Bale akitoka kazini siku ya jumamosi mchana, basi atampitia hosteli, anarudi naye kwake. Watalala hapo, kisha kesho yake wanakwenda kanisani pamoja. Kujaliwa na Bale kuliendelea ila kukazidi kitu kilichomchanganya Vai. Swala lake la kujifungia na Victor hotelini hakulizungumzia tena. Wala hakumkumbusha swala la kupima. Akaendelea kuishi naye kana kwamba hakukosea, kitu kilichovuta hisia za Vai zaidi kwa Bale.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akarudi chumbani kwake na kujikuta akilia sana. Akalia mpaka akamkumbuka Bale jinsi anavyomjali. Akajikuta akimtumia ujumbe. ‘Nalia mwenzio.’ Hapohapo Bale akiwa kazini akampigia. “Nini tena!?” Akamuuliza kwa kumjali. “Najilaumu Bale! Najilaumu sana.” “Ni nini?” Vai akaendelea kulia. “Unataka nije?” “Hapana. Wewe endelea tu na kazi.” “Siwezi kufikiria kama wewe haupo sawa Vai. Niambie nini tatizo. Zungumza na mimi, pengine itasaidia.” Akazidi kumbembeleza.

“Mwanaume wa mwisho ameniacha mgumba. Lakini nahisi huyu wa safari hii ameniacha na gonjwa la kufisha.” Akaendelea akilia kwa wasiwasi. “Nimekutana naye leo. Akiwa na mke wake na mtoto. Nimekumbuka maneno yako Bale. Huyu mtu nilijiingiza kwake akiwa hana mpango wa kumuacha mkewe. Nikajiachia. Sasahivi ananiona kama takataka!” “Nikuulize swali? Lakini usikasirike.” “Nini?” Vai akataka kujua kilichopo moyoni kwa Bale.

“Ulimpenda Victor?” Vai akashangaa sana. “Hapana Bale! Ila nimejidharau na kuona nilijidhalilisha. Ni kama aliyekuwa na agenda fulani kwangu. Kama kuniua tu.” “Au alikuona kwenye picha kama ulivyoniambia. Akakutamani na kutaka kukutumia tu. Usiogope.” Akajaribu kumtuliza. “Hilo ndio tatizo. Naogopa na siwezi kwenda kupima hapa Muhimbili ninakofahamiana na watu wa maabara. Kama nimeathirika kila mtu atajua.” “Basi nikitoka kazini nakuja kukuchukua twende ukapime kwengine, halafu tutaenda kula. Nitakununulia na icecream.” Ikabidi tu Vai acheke.

“Unanifanya mimi kama mtoto mdogo! Unanidanganyishia icecream!” “Sio icecream peke yake. Nitakupeleka na kula sehemu nzuri utakayochagua wewe.” “Mimi nataka kuwa na wewe popote pale. Sitajali sehemu. Ilimradi uwe na mimi. Wewe unanijali Bale, mpaka napatwa wivu siku ukipata mwanamke wa kumuoa.” Bale akajisikia vizuri huyo! “Usipatwe wivu. Tutakuwa sawa tu.” “Wewe ndio utakuwa sawa. Mimi nitabaki mpweke Bale. Sijapata mwanaume wa kunipenda na kunijali hivi, kama wewe. Wengine wote niliokuwa nao wanapenda kunitumia tu na kunitupa kama takataka!” Bale akatulia.

“Najichukia Bale! Najiona mjinga. Narudia kosa kila wakati.” “Si tumekubaliana hutarudia tena?” “Nimekoma.” Bale akaanza kucheka vile jinsi alivyosema. “Unanicheka Bele?” “Kidogo tu. Ila wewe sio mjinga. Sema inakuchukua muda mrefu kujifunza jambo.” “Sasa si ndio ujinga huo?” “Sio ujinga. Na naamini kwa kuwa safari hii umejifunza kiukweli na kuelewa hila za wanaume kwako, hutarudia tena. Nitakuja tukapime. Na ujue nina zawadi yako nzuri sana.” Vai akacheka.

“Umeninunulia nini?” “Kitu kizuri. Nimeenda kulipia leo baada ya kulipwa mshahara wangu wa kwanza, jana. Nilipanga tokea naanza kazi, nikilipwa, mshahara wangu wa kwanza, nikununulie kitu kizuri.” Vai akajikuta akitokwa na machozi. “Nakufikiria Vai. Nakufikiria sana. Ni hivyo tu uwezo mkubwa sina.” “Nakupenda Bale. Nakupenda hivyo ulivyo. Na kwangu wewe ni tajiri wa kila kitu. Mimi sikuoni kama ni masikini. Kwa Victor nilikosea Bale. Nilikosa. Na si kwa kuamua kwangu moja kwa moja kwenda kulala naye. Niliamka pembeni yake siku inayofuata.” Kwa mara ya kwanza akamsimulia ilivyokuwa. Kunywa wine na kulewa.

“Nakiri baada ya kuamka ile asubuhi, pengine ningeondoka pale hotelini. Ila nafikiri…” Akasita. “Nilikosea Bale.” “Ila hata kabla ya hapo ulishaamua kuniacha Vai! Uliondoka nyumbani nikiwa nakuhitaji!” “Ni kwa kuwa nakupenda Bale. Nakutakia mema. Hata nikikuomba unioe mimi, pengine ukakubali, sina uwezo wa kukupa unachotamani.” “Na mimi siku ile niliongea si kutaka kukuumiza. Nilikwambia kile nilichokuwa nakifikiria kufanya maishani kutokana na kosa nililofanya kwenye familia ya baba yangu. Kwamba nilijipa deni. Lakini nikiwa sina nia ya kukupoteza. Maisha hayana furaha bila wewe Vai. Nimeshakuzoea, na sijui itakuaje bila wewe.” Ikamgusa zaidi.

“Nimeahidi kutulia na kutoondoka Bale. Sitabadilika, mpaka uwe tayari kuendelea na kipengele kingine. Sitakuacha peke yako tena, hata iweje. Tafadhali niamini.” “Nimeona umejirudi na kwa vitendo. Na mimi nakushukuru. Acha nirudi kazini, na wewe usijifungie muda huu wa kazi, ukilia kwa ajili ya kosa la nyuma. Huko ni kumpa nguvu Victor.”

“Rudi kujifunza, tupate hicho cheti cha unesi. Punguza hofu. Jioni tutakuwa na wakati mzuri.” “Kama nimeathirika?” “Tutatumia dawa. Na maadamu utakuwa umewahi, naamini tutakuwa sawa tu. Wala usiogope. Tutabadili maisha yetu kutokana na hayo matokeo.” “Kwamba na wewe utasimama na mimi?” Mtoto wa kike akataka uhakika. Maana alishahangaika na wanaume mpaka akachoka. Na hivi tatizo alilo nalo ni gumu kupokelewa na mwanaume yeyote anayefikiria kuanzisha familia! Akataka kusikia zaidi ili kujihakikishia.

 “Nikasimamie wapi tena? Sina mwingine, ila wewe Vai. Katika yote, tutasimama tu. Na Joshua anausemi wake, anasema katika kila dhoruba itakayopiga, tuhakikishe ikishapita, sisi ndio tubakie tumesimama. Na nilimshuhudia akiishi hivyo, aisee. Hakuna urefu atakao takiwa aruke, yule mtu asiruke ili kufikia lake. Hakuna dharuba iliyowahi mpiga yule kiumbe, asibakie yeye ndio amesimama. Na sisi itakuwa hivyohivyo. Si kwa maradhi, si kwa uzima wetu. Sisi ndio tutabaki tumesimama.” Vai alifurahi huyo, asiamini masikio yake!

“Nimefurahi. Nimefurahi sana. Asante Bale. Hivi niliruhusiwa kurudi nipumzike lakini umenipa nguvu mpya. Narudi tena wodini.” “Kabisa. Nitakuona baadaye.” Wakaagana wakiwa wamejawa hisia za ajabu. Ikawa mapenzi ya ajabu yasiyoweza kutamkika. “Sijui ndio Bale atanioa mimi!” Akaanza kuwaza Vai akirudisha sare zake mwilini.

Mara ujumbe ukaingia. Ulikuwa ukitoka kwa Victor. Akafungua kwa haraka akitaka kujua amemwambia nini. ‘Nashukuru kutoniharibia mbele ya mke wangu. Asante. Maana tupo kwenye kipindi tete. Mwanaume niliyedhani anamahusiano naye haikuwa hivyo. Kumbe bado Vera ananipenda. Ameomba tujaribishe tena mahusiano. Nimerudi nyumbani kwetu. Tunalea watoto wetu. Hali siyo mbaya. Ukweli Vera amejirudi na hata yupo tayari kuongeza mtoto mwingine, anaamini safari hii tunaweza pata wa kike. Na mimi nimeamua kutulia kwenye ndoa yangu.” Hapo akamuumiza roho Vai. Akajuta kumwambia hazai. Kwamba mkewe anampa kitu yeye hataweza mpa. Ila akaendelea kusoma.

‘Naamini umeelewa. Ungekuwa ni wakati mwingine, mazingira mengine, wewe ndio ungekuwa mwanamke wa kuwa na mimi. Lakini kwa sasa naona tuache iwe kama ilivyo, nijenge kwangu. Nisiwe mwanaume wa kukimbia familia. Najua hata wewe usingetaka mwanaume wa namna hiyo. Samahani kwa maumivu yeyote nitakayo kusababishia, ila naomba uwe muelewa. Nakutakia kila la kheri.’ Vai akabaki amepigwa na butwaa, asiamini alichokisoma.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ujasiri ukampungua. Furaha yote aliyoacha Bale moyoni ikapotea. Akajiona si bora kuliko wanawake wote duniani. Hana uwezo wa kuzaa. Hilo likampunguza ujasiri vilivyo. Hata uzuri wake ukaanza kufifia kwenye kioo. Asijione bora.

Jioni ilipofika akaanza matayarisho ya kutoka na Bale. Kujishuku kukawa kwingi. Anajiona hafai tena. Ujumbe wa Victor ukaendelea kujirudia kichwani mwake na kuendelea kumpunguzia ujasiri hata kwa Bale aliyemwaga moyo wake vilivyo. Ukweli Vai alipendeza ila sivyo alivyojiona yeye.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bale alipompigia simu kuwa amefika, akatoka. Akamkuta akimsubiria nje ya gari. Msafi, kiofisi, kama kweli mfanyakazi wa benki. Vai akacheka lakini Bale akagundua hayupo kama walivyoagana mara ya mwisho kwenye simu. “Umependeza kweli Vai. Naamini umeshajua pakwenda kula. Maana hivyo ulivyo, hatuwezi kwenda kula chips vumbi.” Akacheka akijiangalia kwa kujishuku. “Asante. Lakini naomba tuanzie hospitalini kwanza.” “Huna njaa wewe?” “Hapana. Nisindikize kwanza kupima ili nijue hatima yangu.”

Bale akauvuta mkono wake na kuushikilia. “Subiri kwanza.” Akabaki ameshikilia mkono wake kwa mkono mmoja, mwingine akatoa cheni mfukoni. Vai hakutegemea. “Bale! Hii si dhahabu!?” “Na mimehakikisha nimenunua nzuri na uzito wa kueleweka. Ikupendeze.” Akamvalisha cha mkononi. “Hii ni ya shingoni. Na naona shingoni unayo cheni tayari.” “Hii ni bati tu. Naweza kutoa.” Hapo hapo Vai akatoa ile cheni aliyokuwa amevaa.

“Naomba mimi ndio nikuvalishe.” Vai akacheka asiamini. “Mwezio sijawahi vaa dhahabu!” “Geuka.” Akamgeuzia mgongo. Bado ilikuwa mapema tu, hata giza halijaingia. Mishale ya saa 11 jioni. Akamvalisha na kumfanya ageuke. Cheni ilikuwa nzuri sana. Mnyororo wa rembo za kopa, virembo vya moyo vilivyosukwa vizuri sana kuzunguka kote. Hapakuwa na kidani. Ila ule uzito hata Vai mwenyewe aliuhisi. Alifurahi Vai, akabaki amejishikilia shingo, ameinama mbele ya Bale hajui aseme nini. Bale akacheka.

“Imekua kama vile nilivyotaka iwe mwilini mwako. Umependeza sana Vai. Unamwili mzuri sana wa dhahabu. Imekaa vizuri mkononi na shingoni.” Vai akajitizama mkononi. Akajihisi machozi kumtoka. “Nashukuru kunifikiria Bale. Asante.” “Karibu. Twende.” Akamfungulia mlango, akaingia.

Wazo la zawadi aina hiyo alipata kwa besti yake, Malon. Alimuona ndio zawadi alikuwa amemnunulia Naya siku ya graduation yake. Bale mwenyewe alipenda. Na kipindi hicho marehemu Malon alikuwa ameishiwa kabisa. Amerudia umasikini baada ya kutoka jela. Lakini alifanya kazi ya ulinzi, akakusanya pesa mpaka akampatia Naya zawadi na kuja kuikamilisha seti nzima baadaye. Cheni ya mkononi, shingoni na hereni. Aina hiyo ya zawadi ndio alijichanga mpaka akamnunulia Naya.

Sasa na yeye alipokuwa akifikiria kitu cha kumnunulia Vai, hilo wazo likamjia kwa haraka sana. Vai hakuwa msichana wa shida sana. Alimuona bado anatunzwa vizuri kwao. Hakuwahi kumsikia akilia shida. Mara nyingi alikuwa akimsikia akisema kaka yake amemtumia muda wa maongezi au pesa. Na bado baba yake alikuwa akimtunza kwa kumlipia ada na malazi hapo hosteli. Kwa hiyo akataka kitu cha tofauti kitakachoweka kumbukumbu kwake. Na kweli akawa amepatia. Vai amemwambia hajawahi vaa dhahabu.  Wakatoka hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walikwenda hospitalini. Vai akatolewa damu. Walipotaka kumpa ushauri nasaa akakataa kwa haraka sana. “Mimi mwenyewe ni nesi. Najua kila kitu. Ninachotaka ni kupima tu, nijue moja.” Akawa mkali kidogo, Bale kimya. Hakutaka hata kujibu maswali yale ya ushauri nasaa ya awali. Akang’ang’ania vipimo tu, bila risala. Aliye muhudumia akawa muungwana. Akampongeza kwa kwenda kupima, akatolewa damu, wakatoka nje kusubiri majibu.

Walikuwa wamekaa upande wa peke yao. Bale akamuona amepotelea mawazoni, ila anazungusha cheni yake ya mkononi. Akamsukuma kidogo kama amtizame. Akavuta pumzi kwa nguvu, kisha akamwangalia. “Nikuonyeshe kitu?” “Nionyeshe.” Bale akakubali bila maswali mengi.

Akamtolea simu na kumuonyesha ujumbe kutoka kwa Victor, akamuacha asome. Bale akasoma mpaka mwisho. Akamtizama. Akamuona anaendelea kuzungusha cheni yake mkononi. Akarudia kuangalia muda ule ujumbe ulipotumwa. Kisha akatizama muda waliozungumza kwenye simu. Akagundua aliupata huo ujumbe baada ya kuzungumza naye. Akagundua ndio maana amekosa raha. Wivu ukaanza kumsumbua.

“Ndio maana umekosa raha?” Akauliza swali la jumla tu kujua aliposimamia Vai. “Yeye kama Victor hajaniumiza, kwa kuwa nilishaamua kuachana naye. Lakini huwezi amini katika ujumbe wote huo mrefu, mimi nimekwama kwenye mkewe kuzaa. Imenirudisha mbali! Huwezi amini Bale. Nimerudi kule nilikokuwa nikihangaika na yule mwanaume wa mwisho kutafuta mtoto ili asiniache. Ulikuwa wakati wa kunyanyasika sana kihisia.” “Kwani Victor yeye anajua kama huna uwezo wa kuzaa!?”

“Anajua.” Bale akashangaa sana. “Yaani huo muda mfupi tu mliokuwa wote hotelini ndio amekufahamu kwa undani hivyo!?” “Kuna kitu nilimwambia juu yetu, ndio maana. Lakini sio kwamba tulizoeana kwa kiasi hicho!” Bale akawa bado hajaelewa. Kabla hajauliza swali lingine, Vai akaitwa jina lake. Wakaenda kuchukua majibu. Aliposikia tu hajaathirika, hakutaka mengi. Akashukuru na kusimama. Ikabidi Bale naye ashukuru, watoke.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ila Vai akamuona amepoa haswa. “Tunakwenda kula wapi?” Bale akauliza. “Victor aliambiwa habari zako na Belinda. Akaambiwa kwako ndio ninakokuaga mara nyingi. Alipotaka kujua mahusiano yetu, ikabidi mimi niwe mkweli.” Akamuona anainama kama anashindwa kusema. Bale akakunja uso.

“Vai?” “Nilimwambia kile ninachojisikia kwako.” Hayo maelezo yakawa hayajatosha kwa Bale ambaye wivu ulishakuwa ukimtesa. “Tafadhali niambie kile ulichomwambia Victor, juu yetu au yangu.” “Nilimwambia tulianza kama marafiki. Lakini baadaye mimi mwenyewe, wala si wewe, mimi. Hisia zilianza kubadilika. Nikajisahau uwezo wangu, nikatamani niwe na wewe tu, mpaka uliponikumbusha shauku yako yakuja kuwa na familia. Ndio nikagundua mimi sitaweza kuja kukuzalia watoto hata kama nikikuomba unioe mimi. Ndio ikabidi niondoke kwako japo moyo ulikuwa ukiniuma. Ndio akajua mimi sizai.” Akamalizia hivyo.

Bale akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Ila akapata aghueni ya ajabu rohoni. Kwamba Vai na yeye anampenda! Wakatulia hapo nje ya viwanja vya hospitalini kwa muda kama waliopoteza dira.

Baadaye akavunja ukimya kwa swali. “Lakini ulielewa vile nilivyokwambia juu ya mpango wangu?” Vai akamwangalia akiwa amekunja uso kuashiria hajaelewa anachomaanisha. Maana alikuwa mbali kimawazo. “Kwamba sikuwa na maana ya kukuumiza au kukupoteza. Nilishajiwekea deni. Na kwa kuwa wewe ni mtu wangu wa karibu. Tunazungumza kila kitu. Zamani sikuwa nikihitaji kuchuja jambo kukwambia ukweli, ndipo nikakwambia bila kufikiria.” “Mimi sitaki uchuje mambo kwangu.” “Lakini hilo liliniponza Vai. Uliniacha.”

“Nimeahidi nitabadilika Bale. Na wewe niahidi hutabadilika.” “Hata kama jambo litakuumiza?” “Acha niumie, ila niambie ukweli wote.” “Sawa. Twende tukale.” Wakaondoa gari hapo hospitalini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Hongera kwa afya njema.” Vai akacheka. “Nimefurahi. Na nimekoma.” “Ila mimi sijafurahia wewe kuumizwa na huo ujumbe wa Victor.” Vai akashituka. “Wewe si umetaka kujua ukweli wote? Ndio hivyo. Wewe tuliagana ukiwa na furaha na umerudisha morali wa kazi. Amerudi Victor na ujumbe wa kukukataa, eti unakosa raha!” “Nimekwambia ni swala la kutozaa!” “Kwani wakati tukiagana mimi na wewe hukuwa ukijua huzai mpaka alipokwambia Victor?” Vai akashindwa ajibu nini.

“Mimi nahisi ni kama ulishampenda na kumpigia mahesabu.” “Mwanzoni, ndiyo. Wala nisikatae. Nilimpigia mahesabu. Kwa sababu alishaniambia ana watoto na anaachana na mkewe. Nikamuamini. Ila ujue ni kipindi kile cha ujinga cha kutofikiria mpaka wewe uliponifanya nifikirie. Lakini sio kwamba nilimpenda, ila niliona ni kama kimbilio. Kwake isingekuwa kuna maswala ya watoto, kitu ambacho ni kama na yeye aliniambia pale nilipokuwa nikilalamika kuondoka kwako kwa kuwa sina uwezo wa kuzaa. Akaniambia nisikose raha kwa wakati ule, hatupo pale kutafuta mtoto. Ndio nikabweteka. Ila mimi nakupenda wewe. Hii ni aibu tu ya kuachwa vibaya vile, tena nikiwa nimepigwa vibaya vile na kina Belinda.” Bale akatulia.

“Tafadhali nifikirie hata kidogo Bale. Kipigo chote kile! Tena baada ya kutumiwa muda wote ule na Victor, halafu aje anikatae kwa namna hii, tena akijieleza mkewe atamzalia! Kulikuwa na ulazima gani wakuniambia yote hayo kama si kunifikishia ujumbe wa kuwa mkewe anampa kitu ambacho mimi sina uwezo wa kumpa? Si angesema tu nimeamua kurudiana na mke wangu?” Bale kimya akiendelea kuendesha. Muda huo ndio walikuwa wakijenga msingi wao mpya. Ni kama wote walikusudia kuanza upya.

“Tafadhali usinifikirie vinginevyo Bale. Mimi nimeridhika na wewe.” Bale akamtizama. “Na Mungu wangu atakuwa shahidi wangu katika hili.” Vai akaongeza akibembeleza. “Na najua sasahivi huamini, lakini muda utajibu. Mimi mtu wako Bale.” “Nakuamini Vai.” Hakutegemea. “Kweli Bale!?” “Kabisa. Huna sababu ya kuwa na mimi kipindi chote kile. Nikiwa mlemavu, sina kitu, natunzwa na shemeji, kama si kunipenda. Najua unanipenda.” Hayo maneno ndio yalimmaliza kabisa Vai. Hakutegemea.

“Ndio maana ulinishangaza ulipoondoka! Nikajihisi kweli mimi nimjinga! Niliwezaje kukusoma sivyo! Ikaniuma sana, na nikajilaumu kwa mengi. Lakini nimeshukuru umerudi Vai. Naomba tuachane na ya nyuma.” “Naomba tuachane hata na la Victor basi. Huo ukurasa niwe niliukosea, tuufunge. Naomba tuanze upya, iwe kama zamani.” “Sawa.” Bale akakubali bila mengi mpaka Vai akashangaa. Bale huyu anajua kukosea, kusamehewa na machungu ya kutosamehewa. Amefikishwa sehemu mpaka akawa mwepesi sana wa kusamehe. Na asichokijua Vai, kuwepo kwake hapo, yeye Bale anahisi ni kama Mungu anamtangazia msamaha. Akampokea kwa furaha zote.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walienda kula sehemu ngeni kwao wote wawili. Lakini sehemu ya hadhi. Wakawa wanajicheka. “Tumepanda chati.” Vai alimfanya Bale acheke sana. “Ila sasa sio tusahau vijiwe vyetu vya zamani.” “Tena!?” “Wewe Bale vipi? Sasa tukiendelea kula hapa, tutajenga kweli?” Bale akazidi kucheka ila akafurahia sana hilo wazo. “Hapa tunakuja mara moja moja, sanaaaa! Lakini hatuachi kwenda kwenye vijiwe vyetu. Au unasemaje?” “Mimi nimekukubali. Kwamba unakula ila unawaza na kesho!” “Kabisa baba yangu.” Bale alicheka mpaka machozi maana hapo Vai aliongea kwa lafudhi ya kichaga kabisa.

Stori zikaendelea wakichekana kula kwa kisu na uma. “Sasa hapa tena sio tutie aibu na wewe Bale! Tujidai ni mambo ya kawaida kabisa.” “Wewe ndio unatetemeka mikono. Mwenzio nimeshazoea.” Vikaendelea vicheko mpaka wakamaliza. Kesho yake wote majukumu yanawasubiri. Wakaamua kufunga siku. “Natamani turudi wote nyumbani, Vai.” “Ujue kesho itabidi udamke alfajiri na mapeme ili uniwahishe hosteli.” “Hamna shida. Twende.” Safari ya kwa Bale ikaanza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bale hulala kwenye kochi, Vai chumbani kwa Bale. Bale akawahi chumbani kwenda kuoga wakati Vai yupo sebuleni akimsubiri atoke amiliki chumba. Ni utaratibu wao, walishazoea wala si kupanga. Bale akatoka akiwa ameshavaa mavazi ya kulalia, na mto pamoja na mashuka. Akachechemea mpaka kwenye kochi kubwa. Wakazungumza hapo, wakaomba pamoja, wakaagana kwenda kulala.

“Ulale unono.” “Bila hata kuniambia, leo nitalala unono. Na dhahabu hizi mwilini! Aisee lazima.” Bale akaanza kucheka. “Usifanye mchezo na nguvu ya dhahabu mwilini. Inaleta usingizi.” “Sawa Vai.” Vai akaelekea chumbani kisha baada ya muda Bale akamsikia akifungua mlango.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Bale alishafunga milango ya nyumba na kuzima taa. Akanyanyua kichwa pale alipokuwa amelala, na kumuangalia pale mlangoni alipokuwa akitoka. “Nimeshindwa kulala.” “Umetoa dhahabu?” Akamuuliza kwa utani lakini akashangaa anajibu kwa unyonge. “Hapana Bale. Nilikwambia nakupenda mara kadhaa. Hujanijibu hata mara moja!” Akaongea kwa kulalamika akiwa amesimama palepale mlangoni. Bale hakutegemea. Akarudisha kichwa kwenye mto vile alivyokuwa amejilaza kabla hajatoka. Vai akabaki amesimama palepale akimtizama ila na yeye akahisi kukataliwa kimapenzi, amepewa nafasi ya urafiki tu. Akajisikia kuumia vibaya sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kemi Ametimiza Azma Yake. Na Jelini Na Yeye Amekosa. Colins Maisha Mapya Na Love. Vai&Bale?

Usipitwe Na Muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment