heshima yangu tu, msikilize Colins. Tafadhali kubali kuonana naye
mzungumze. Hali yake mbaya. Amedhoofu, hali kabisa.” “Nikwambie ukweli shem,
mimi mwenyewe nina hamu na Colins wangu. Hivi hapa nilipanga kesho niende
nikamuone. Nimejuta kuongea vile. Nahisi bado nilikuwa na hasira nikihisi
hanitaki. Ila nikajiambia nitajitahidi kumuonyesha nampenda mpaka aje
anipende.” James akacheka kwa aghuheni.
“Kweli
nimegundua nampenda Colins. Siwezi kuishi bila yeye. Akiniambia ananipenda hata
kwa kunidanganya, nakubali.” “Hakudanganyi. Colins anakupenda
sana. Ila kuna alikopita kwenye mahusiano ya nyuma, ndio maana unamuona vile.
Mimi namfahamu Colins. Ukimuonyesha unampenda, na unataka kuwa naye kama hivi
ulivyoniambia, atapata ujasiri, naamini atakuwa kile unachotamani.”
“Nashukuru
shem. Mimi naona yeye ndio aje kesho. Nimpikie vitu vizuri, ale, kisha alale
ndio aende kwake. Safari hii nitamsikiliza anachosema na kumkubalia bila
kumpinga ili atulie. Nampenda Colins wangu. Ujue aliniambia kama mapigo yake ya
moyo bado yanadunda, nijue mimi ndio mwanamke wake tu, hatakuwa na mwingine?” James akacheka. “Kweli Shem. Sasa nitake nini kingine?” “Na mimi ameniambia
hivyohivyo. Atatoka hapa duniani akiwa anakupenda wewe tu.” Jelini
akafurahi. “Mwambie namsubiria.” “Nashukuru shem.”
Wakaagana Jelini akaanza kurukaruka kwa furaha. “Kazi ipo!” “Si kidogo.”
Akajibu Jelini akicheka.
Jumamosi.
Jelini akadamka
kwenda sokoni akimjua Colins anaweza kufika hapo wakati wowote. Akataka awahi
ili akifika hapo asimkose. Akarudi na kuacha geti wazi, akiwa amerudishia tu.
Kazi ya kupika ikaanza. Jelini cha uvivu alipika mpaka basi. Kila alichopika
akaona hakitatosha. “Kingine nitamfungashia akale kwake.” Akawaza moyoni. “Na
akija, nitamwambia nashukuru kwa heshima ya kunisubiria mpaka ndoa.” Hayo
anazungumza na cheko huko jikoni, mama yake alishaondoka kwenda kwenye biashara
zake.
Akafanya yote huko
jikoni mpaka akasafisha jiko, Colins hajafika. Akaenda kuoga ili akija
amkute msafi. Akajitengeneza vizuri na nguo ya heshima tu si kimtego. Colins hakutokea.
“Labda atakuja jioni.” Akajipa moyo. Mpaka saa nne na nusu usiku mama yake
anaingia hapo na kukuta vyakula mezani, Colins hakuwa ametokezea.
Akafunga milango yote akimuhurumia mwanae. Jelini alishakuwa amerudi chumbani
kwake. Akaona hata asimuulize. Ni kawaida ya Colins kutotokea, ila kurudi na
sababu. Kazi ya kuweka vyakula kwenye friji ikaanza mpaka mwisho. Akaona aingie
tu chumbani kwake bila kutafuta ya undani.
Jumapili.
Hakuna Msiba Usiokuwa Na Mwenziwe.
Siku ya jumapili
Jelini akiwa bado chumbani, anaona hata shida kutoka asije akaulizwa na mama
yake juu ya Colins, kwenye mida kama ya saa nne asubuhi. Mama yake alikuwa na
yeye chumbani kwake akijiandaa atoke, wakasikia hodi getini. Wakapata ugeni
mzito. Babu, bibi, na wazazi wa Colins wakawatembelea. Ikawa kama hali ya
kushitusha kidogo, ila Jelini akadhani sababu ya kumkataa Colins, basi wameamua
kuja kutoa posa. Ikawa hali ya sintofahamu. Ila kwa jinsi walivyoingia
na kukaa hapo sebuleni, hata mama yake akaanza kuingiwa wasiwasi.
“Kwema jamani?!”
Akaanza mama Jema baada ya kufunga mlango na kukaa. “Labda uturuhusu tuanze kwa
maombi kwanza ili kumuharibu mkuu wa anga wa mahali hapa. Ili kila
tunachozungumza, kieleweke.” Akaongea bibi mtu, Jelini na mama yake wasielewe.
“Maana zipo nguvu za giza, zinaweza kuteka watu ufahamu, wakafanya mambo bila
kujijua. Ila sisi tunasimama kinyume cha kila aina ya nguvu za giza…” Bibi
akajawa jazba na nguvu ya ajabu. Akasimama kabisa na kuanza kukemea.
Anazunguka hapo
aking’oa na kuharibu kila falme za giza. Akimtenga Colins na kila alicholishwa.
Hapo mama Jema akamwangalia Jelini, na yeye akawa haelewi. Akapiga simu kwa
James na kumuacha asikilize. Bibi aliomba huyo bila kuchoka, akilia na kumsihi
Mungu amtete Colins. Hiyo kelele ikamfanya hata Jeremy atoke chumbani kwake
aende akaangalie. Ikawa hali ya sintofahamu, maombi yakiendelea.
“Hodi ya mlangoni,
Jema, mumewe na mtoto ndio iliyomfanya bibi apoe maana alikuwa akisaidiwa kwa
sauti za uombaji za kawaida za waliokuja nao. James na familia yake wakaenda
kukaa hapohapo sebuleni, ndipo bibi akaanza kupoa.
“Kwema jamani?” Akauliza
James akimtizama baba yake Colins kisha mama yake na wengineo. “Sisi tumekuja
kuwekana sawa.” Wote kimya baba Colins akizungumza. “Colins ni kijana wetu na
tumemlea katika mazingira, tamaduni na imani yetu. Hata fikiria yake na penda
yake, inaendana na kile alichokuzwa na sisi.” Babu akawa akitingisha kichwa
kukubaliana na anachozungumza baba Colins.
“Kitendo cha Colins,
kuanza mahusiano na mtu kama Jelini, kimekua cha kushitua na kushangaza sana.”
“Mtu kama Jelini?!” Mama Jema akauliza. “Samahani mama. Naomba waache wamalize
tu. Tafadhali sana.” James akataka kusikia.
“Mbona jibu ni rahisi
tu. Baba yake anapozungumzia Mtu kama Jelini, anamaanisha asiwe mwenye haiba
kama ya Jelini.” Babu akaongeza kwa haraka na kuendelea. “Colins amelelewa kuwa
kiongozi wa familia. Akizingatia uchumi wa familia nzima. Sio wake tu, ukoo
mzima. Na hiyo sio kwake tu. Ni kwa vijana wetu wote wanaozaliwa kwenye ukoo
wangu. Na ndio maana wote utakuta wanaoa wanawake wenye maadili. Wacha Mungu,
wanaojua na kuelewa jinsi ya kubeba familia kwenye maombi kama hivi
mlivyomsikia bibi yake akiomba. Waliosoma, nikimaanisha wenye kipato
chakusaidia uchumi wa familia.” Babu mwenyewe amekaa hapo anaonekana bado salio
benki linasoma. Mzee mwenye neema.
“Endelea.” Akamtaka
baba Colins aendelee. “Kwa hiyo chochote mlichotegemea kitokee kati ya Jelini
na Colins,” “Kwanza mtambue kabisa, tumeshatengua katika ulimwengu wa roho.
Hakuna silaha itanyanyuka kinyume ya Colins ikafanikiwa. Kila ulimi
utakaotamka jina la Colins kwa ubaya wa kutaka kumfanya mateka,
tumeshauhukumu mkosa. Tunatengua kila laana.” Bibi alimkatiza mtoto wake na kuendelea
kwa muda mpaka wenyeji wao wakabaki wametoa macho.
Mama Jema hajui
kanisa, wala mganga. Hanaga vita na shetani wala Mungu. Hajawahi kukemea
pepo, wala haombi Mungu. Maisha yake yanajiendeaga tu. Sasa akakutana na wakristo
wenye imani ya namna yake. Kulisemwa ya
kimungu hapo, akabaki amepigwa na mshituko. Hiyo fujo ya kimungu ikaendela hapo
mwishoe wakahitimisha kuwa Jelini aachane kabisa na kijana wao. Hawataki
kumuona tena hata nyumbani kwa Colins.
“Bora mmeongea hivyo,
maana mlikuwa mnanichanganya. Sijui mnaomba au mnaongea! Ila mimi niwaambie
ukweli kabisa, mwenzenu nampenda Colins.” Jelini kama kawaida yake akaongea
kirahisi tu. “Na angenioa mimi, ningekuwa nampenda, namuheshimu na kuwa
naye katika kila hali kwa kuwa nampenda Colins wangu.” Wote wakabaki wamepigwa
nabutwaa kama ambao hawakutegemea.
“Ila bora hivi
mlivyokuja nimejua nyinyi sio wazazi wazuri kwa watoto wenu. Mnalazimishia
watoto wenu mambo wasiyoyapenda. Kwahiyo hata mimi pia sitaki
tena kuwa karibu na nyinyi mtakuwa watu wakulazimishia mambo yenu tu kila
wakati na watoto wangu sitaki wawe kama nyinyi. Kwa hiyo wala msiombe Mungu,
eti sijui nisije kwenu! Hata mimi japokuwa nampenda sana Colins, lakini sitaki
tena. Hatuji tena kwenu. Hatutaki tena. Na nyinyi hapa kwetu pia hatutaki
mje tena. Mnaleta fujo na kelele ambazo kwanza sisi hatuwaelewi! Mkiondoka
hapa, msirudi tena.” Jelini akaongea bila shida na akamaliza.
“Mimi sijui nyinyi
mnaongelea nini, lakini Colins niliyezungumza naye mimi siku ya ijumaa, siye
huyu mnayemuwakilisha hapa.” James akaongeza kwa Jelini. “Si kwa sababu sio
akili zake!?” “Mimi si mshirikika wala mcha Mungu sana kusema najua kila kitu.
Ila wazazi wangu, hiki mnachokifanya kwa Colins si sawa, na
kinaniashiria kabisa hamjaweza kumsikiliza Colins mwenyewe mkajua
kinachoendelea kwenye maisha yake. Mimi nafanya kazi na Colins na nipo naye
karibu sana. Namjua…” “Sema ulikuwa ukifanya naye kazi.” Baba mtu akamkatiza
James na kumchanganya James kidogo.
“Colins ni mtawala wa
mali nyingi sana ambazo sisi tumezitafuta kwa jasho letu. Kuanzia jumatatu
anaanza kazi kwenye mali za familia kama mtawala na kiongozi sio hicho
anachokifanya huko ambacho hakiongezi chochote kwenye maisha yake ila kumpa
pesa ya kula tu. Colins anauwezo mkubwa sana lakini kwa muda mrefu sana
amejifunga kwenye vichache, ndio anaanza kuchukua hatua sasa kama mtawala.
Tafadhali acha kumfuata nyuma na kumchanganya.” “Nahisi mimi nitakuwa
kama Jelini tu, msiwe na wasiwasi juu yangu. Wala sitamsumbua ili awe kile mnachokitaka
awe.” James na yeye akajiweka pembeni.
“Naona mpaka hapo
tupo sawa. Hapatakuwa na lawama baadaye.” Akaongeza baba Colins akisimama
kuashiria kikao kimeisha. “Sio kutoka kwa familia hii.” Akaongeza James na yeye
akisimama kama wageni wao. “Ila mama Colins, tafadhali mwangalie Colins. Hali
kwa muda mrefu sababu ya kuchanganywa na hayo mambo ya kwenu.” “Wala si kwetu.”
Akadakia bibi mtu. “Sawa. Naomba nirudi kwa mama Colins. Mimi nimemshuhudia
Colins akitaka kuanguka mara kadhaa kwa njaa. Hali na halali. Hayupo sawa. Kwa
hiyo wakati mkiendelea kumuombea, tafadhali mama, kumbuka na swala la
chakula.” “Atafunguliwa na atakuwa huru tu.” Bibi akaongeza kibabe,
chakushangaza mama Colins hakujibu wala kuongea, ila na yeye walimuona
akichangia kwa nguvu zote kwenye maombi. James akaenda kufungua mlango kuwaashiria
waondoke. Na wenyewe bila shida, wakaondoka bila ya kuaga.
Kwa Kina Jelini.
“MmmmH! Lakini mimi nahisi kuna kitu hakijakaa
sawa. Kwa nini waje wao bila Colins?” Jema akawaza kwa sauti. “Unakumbuka hali
niliyokwambia anayo Colins? Hana nguvu hiyo ya kufanya fujo zote hizi. Colins
amedhoofu mpaka ikabidi kumuombea azungumze na Jelini. Na nilivyompa majibu
kuwa Jelini alishakuwa na hamu naye, atamuandalia chakula aje, akataka kuja
usiku uleule.” “Kweli shem?” Jelini akauliza kwa kunyongea.
“Hakika. Mimi ndiye
niliyemkataza na kumsihi alale mpaka kesho yake. Aje kwako akiwa ametulia na
akili inaweza kufikiria, maana alikuwa hoi. Nikamtisha nikamwambia akikujia
tena vile alivyo, ataharibu zaidi maana atakuwa hana uwezo wa kufikiria vizuri.
Ndio akakubali kulala ila akaniambia asubuhi na mapema sana atakuwa hapa. Sasa
kutotokea hapa siku ya jumamosi halafu leo wanatokea hawa! Na mimi nipo
kama Jema, nahisi kuna kitu hakipo sawasawa.” Pakazuka ukimya wa muda.
Wakamsikia mama Jema
akiguna. “Nini mama?” Jema akauliza. “Nahisi, sitaki kukuza, ni kama wanahisi
pengine Jelini amemloga kijana wao!! Au niwe sijaelewa!” “Eti hata mimi
nilihisi kama wanatuona sisi wachawi!” Jelini naye akawa kama hajaelewa.
“Sitaki kuongeza
ubaya kwenye ubaya, lakini kwa jinsi walivyokuwa wakiomba, ni kama kuharibu
hapa nguvu zilizotumwa kwa Colins, ambazo zinamshikilia. Kwamba wanajua
amelogwa na nyinyi au Jelini. Kwa hiyo kuwa hapa nyumbani kwa kina Jelini ndio
wamekuja kung’oa mzizi wote wa uchawi.” Maelezo ya Jema yakawatoa macho wawili
hao, mama na mwana. Wote hawajui uchawi wala nguvu za Mungu.
“Makubwa! Haya
nashukuru kwa kuja kwa haraka. Mimi natoka kwenda kutafuta pesa.” “Na mimi
nakuja mama. Sitaki kuendelea kuonekana mvivu na kila mtu. Kwanza kichwa
chenyewe hata hakisumbui kama nikiwahi kunywa dawa. Kama Jema hutajali kwenda
na Jeremy naomba muende naye nitakuja kumchukua.” “Hapana Jelini. Wewe unataka
kuniharibia ratiba yake huyu. Nataka saa mbili na nusu awe ashalala. Ukianza
kumzungusha kwenye majumba ya watu, utamchelewesha. Mwache abaki hapa. Chakula
kipo. Anajua muda wake wakula, kuoga na kulala. Utaratibu uleule. Kugusa kitasa
cha mlango ni mpaka…” “Kuwake moto.” James akacheka vile Jeremy alivyomalizia
kwa haraka.
“Kumbe ndio maana
Colins alikuwa anasema alikuwa akija hapa, anagonga mpaka anachoka!” “Kabisa.
Huna funguo za humu ndani, mimi au Jelini tusipokuwepo, huwezi kuingia.”
“Utaratibu huo sisi tumekua nao tokea wadogo. Huyu Jelini ndio alikuwa
matatizoni kila siku, maana ndani hawezi kutulia, mpaka aende mtaani. Sasa mama
akirudi kwa kushitukiza halafu asimkute, anaenda kumfuata mtaani anakoenda
kucheza. Utamsikia anarudi naye kamshika mkono, analia. Anakuja
kufungiwa tena.” Wakaanza kucheka. Angalau wakajisahau machungu ya kina Colins.
James na familia yake wakaondoka, Jelini na mama yake wakaingia mtaani. Jeremy
akarudi chumbani. Maisha yakaendelea.
Kwa Kina Colins.
Kilichotokea Siku Ya Jumamosi.
Huku kwa Colins kumbe
asubuhi aliyokuwa amepanga aende kwa kina Jelini, Love alifika hapo kwake akiwa
na wazazi wa Colins, Kemi Kasa na baba wa makamu tu. Kemi alisema ndiye
atakayewasaidia kumkomboa Colins. Wakawa wamejiandaa haswa kumkabili kwa
siku hiyo. Sasa walipofika hapo, Colins akabisha kuwakaribisha wakae,
akiwaambia safari hiyo hataki kabisa kupotezewa muda kwa vikao visivyo isha. Hapo
ndipo aliharibu.
“Mnanipotezea muda na
maneno mengi yasiyoisha. Nishasikiliza mnachotaka, niacheni na mimi niamue.
Hamuwezi kuniburuza mimi kama mtoto mdogo, kiasi cha kunijia nyumbani kwangu
muda na wakati mnaotaka nyinyi! Hapana kwakweli. Leo iwe mwisho na naomba tuheshimiane.
Naombeni tokeni. Halafu hichi mnachotaka kiendelee, tukipangie muda
mwingine.” Colins akaweka msisitizo tena akiwa amesimama.
“Yaani wewe Colins
kweli unakataa hata maombi kweli!” Love akashangaa sana kwa sauti kama
anayetaka kuhamasisha wengine. “Hayupo sawa huyu. Na hizi si akili zake. Colins
siwakukataa maombi.” Akaweka msisitizo. “Lazima umpe nafasi mtumishi wa Mungu
kuomba. Ameacha shuguli zake zote na kuamkia kwako halafu unataka umfukuze bila
maombi!? Hapana. Mama Colins zungumza naye.”
“Ni maombi tu Colins,
mwanangu. Haitachukua muda mrefu.” “Umepatwa na nini mama wewe! Kwa nini
umekuwa mtu wa hivyo na unaelewa kila kitu? Kweli wewe niliyekuamini na
mambo yangu ya ndani hivyo ndio leo unakuwa mgeni wa kila kitu na kumkumbatia Love
na kumuacha aendeshe mambo vile anavyotaka!?” “Ni kwa kuwa nakutakiwa mema
Colins. Hata kama kulikuwa na tofauti zetu, lakini siwezi kukuacha ukapotea
hivihivi. Nakupenda, nimejirudi lakini bado tu huoni!” “Si akili zake. Mimi
nashauri mtumishi aanze kuomba.” Kemi akaweka msisitizo.
Wakati Colins
anakataa, wakaanza kusema ni mapepo. Huyo muombaji akafanikiwa kumuangusha
chini, Colins ambaye hakuwa na chakula mwilini, ukimlinganisha na mtumishi
aliyelipwa na kupambwa na Kemi pamoja na Love, na ahadi kemkem endapo
atafanikisha shoo nzima. Kwa hiyo alijawa mukari wa kazi kufanikisha.
Kusukumana kukaendelea, akimuombea akiwa amemminya sakafuni akimpaka mafuta.
Yale mafuta yakamchefua Colins, akaanza kutapika.
Hilo nalo likawa jambo la
kufurahisha, akasema anatapika vitu alivyolishwa na Jelini. Akahangaika
hapo sakafuni akiwa amekabwa vilivyo mpaka akawa amejichafua kila mahali. Hatua
ya mwisho akasema anamuwekea kitambaa cha upako, hicho ndicho kilichommaliza
kabisa. Colins akanyamaza kimya. Mtumishi akasema sasa ametulia, akaoshwe,
apumzike.
Love akajitolea
kwenda na mtumishi ndani akamuogeshe, apumzike na akasema atakuwa naye mpaka
atakapoamka. Hilo zoezi lilichukua muda wa kutosha tu asubuhi hiyo. Lakini
wazazi wakaondoka wakiwa wamepewa tumaini kuwa, yote mabaya aliyokuwa
amelishwa, basi yametolewa. Colins yupo huru ila anahitajika kuendelea
kuombewa. Kwamba mtumishi bado analo zoezi endelevu. Na wenyewe
wakamlipa, ila iliitwa sadaka ya shukurani, Colins akaachwa mikononi mwa Love,
shoga mpya Kemi, na mtumishi.
Jumapili.
Sasa walipotokea kwa
kina Jelini, maneno ya Jelini, vile walivyokuwa wakiwashangaa pale na kile
wanachokifanya, bibi kuomba akikemea, na James kumalizia kuzungumza naye ramsi,
kitu kikaanza kumsumbua mama Colins. Akawa hajui sawasawa nini hakipo
sawa, lakini hajui aseme nini. “Kuanguka kwa Colins, inaweza kuwa kweli ni
njaa!” Akawaza mama Colins na kushindwa kuongea kwa wenzie waliokuwa
wameongozana, zaidi wakwe. Mama mkwe wake anajulikana kama mama mwenye hekima,
mcha Mungu na anatembea na roho ya uonaji. Leo aje aseme vinginevyo, wakati
asubuhi hiyo pia walitoka nyumbani kwa Colins akaomba sana!
Akazidi kuwaza kwa
hofu ila asiseme. Hao wakwe sio wakwe njaa. Wasomi, wanapesa na hata mumewe na
nduguze, wanawaogopa mbali na heshima. Kikubwa, anamuunga mkono mumewe
anayetaka jasho lao lisipotee, akimtaka kijana wao awe mtawala wa mali zote.
Sababu ikawa nzito, iliyoungwa mkono mpaka na wakweze, leo yeye peke yake
anapingaje? Akalinyamazia kimya, ila akili kumkichwa.
Palipotulia, akaenda
kununua dripu ya maji ya sukari, akaenda nyumbani kwa Colins. Akamkuta mama Simba
na binti zake hapo, wamejaa sebuleni wakiongea yao na kucheka. Alipouliza juu
ya Colins, akaambiwa na Love amerudi kulala muda si mrefu, alikuwa hapo
akizungumza nao. Haikuwa kweli, alimdanganya tu mama Colins. Huyo Colins
hakutoka kitandani tokea wamuweke hapo akiwa na mtumishi.
Akaomba kwenda
kumuona, akamkuta amelala. Na wenyewe wakaingia hapo chumbani. Wakamuona
anampima pressure. “Atakuwa tu sawa. Na
hivi hayo majini aliyokuwa ametupiwa yameondoka, hapo tu nikukazana maombi na
apumzike kwa muda wakutosha.” Akaongeza mama Simba. Mama Colins akabaki kimya
akimtizama kijana wake. Walipoona hajibu, wakatoka. Alipoachwa tu peke yake na
mwanae, akamuwekea maji yale ya kuongeza nguvu mwilini, kwani pressure ilikuwa
chini sana. Na walitoka hapo hata hawakutaka kujua majibu ya pressure
aliyoyapata kwa Colins. Hilo huyo mama likamshangaza.
Nesi huyo hakuchukua
muda kupata mshipa wa kijana wake, akamuwekea mwanae drip. Akalifungulia kwa
haraka ili limpe nguvu. Akabaki amekaa hapo chumbani peke yake. Hawakurudi.
Akakaa mpaka likaisha, Colins akawa bado amelala. Akatoka. Kuzungumza na Love.
“Naona bado amelala.
Sasa kama kuna msaada wowote unaotaka, nijulishe ili usaidiwe, ibakiwe kazi
yake tu huyo. Hata nguo nitamtuma kijana aje achukue, afue. Na chakula
nitawaletea.” Love akashukuru, mama Colins akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nini kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment