Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 48. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 48.

“Itabidi tukupe funguo za milango.” Wakamsikia James akimwambia wakati akimfungulia. “Jelini anaendeleaje?” “Twende ukamuulize mama yake, yupo hapo ndani.” “Kwamba wewe hujui!?” “Sijui Colins. Ila mama yeye kwakuwa ametokea huko alikokuwepo Jelini, atakuwa na majibu mazuri. Ila Jema na JJ wao wameamka salama.” Wakamsikia akicheka. “Ni kwa kuwa Jelini ni mgonjwa, bwana. Lakini si kwamba simjali Jema. Jema wangu wa karibu sana, na yeye analijua hilo.” “Basi matendo yako hayaonyeshi kabisa Colins. Njoo huku.” Jema akadakia akimuiga yeye mwenyewe anavyopenda kusema hivyo akimshutumu James.

Colins akacheka akifuata sauti ya Jema chumba cha uzazi. Anachoshida Jema na mwanae mpaka usiku ndipo anarudi chumbani kwake. “Kwanza anko wangu yuko wapi?” “Umemuamsha na kengele.” Jema akamshutumu, akacheka na kusogelea kitanda. “JJ mwenyewe hana neno. Amelala hana habari. Mama wewe tumeshasalimiana.” “Mapema sana, Colins mwanangu. Ulilala salama lakini?” “Nina wasiwasi juu ya Jelini mama yangu. Nahisi ni kama rahisi kumpuuza kwa vile anavyoonekana!” “Ulikuwa na wazo gani? Na kabla hutajaanza haya mzungumzo ya muhimu, acha nimuwekee mzazi supu, halafu ndio na sisi tuzungumze.” “Ila na mimi nina njaa, mama yangu. Sijala tangia jana.” James akabaki akimwangalia Colins, haamini.

“Sasa nini?” “Kwamba na wewe unataka supu ya mzazi!?” “Si lazima nipewe hiyohiyo! Hata nyingine mimi sina neno.” Jema na mama yake hawana mbavu. “Mimi njaa inauma James, wewe vipi bwana!? Nishazoea nikija hapa, Jema ananipa chakula kwa haraka.” “Uwe na aibu Colins, bwana!” “Hivi wewe vipi James!? Unajua wazi mimi siwezi kufikiria bila kula.” “Mama James anajua kupika chakula kingi. Acha nikupashie na wewe Colins.” “Changu nitakuja kupasha mwenyewe mama Jema. Nisikusumbue. Mimi huko jikoni mwenyeji sana. Najua mpaka vijiko na mabakuli yalipo. Nilitaka tu uhakika wa ukaribisho wako.” Akaongozana na mama Jema jikoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati mama Jema anampangia hiyo supu Jema, Colins akaingia na bakuli lake ameshika mkononi. “Hukai mezani?” “Acha tuzungumze tu hapahapa. Maana nishakubaliana na Jema, atazungumza na Jelini, apumzike kazi mpaka apone kabisa.” “Hujakubaliana na mke wangu, ila kumpa maagizo.” “Haya mazungumzo hayakuhusu kabisa James. Maana kama sijakosea, leo asubuhi umenipiga marufu kabisa nisikuhusishe tena juu ya mambo ya Jelini. Ndio naweka mipango na mama Jema.” “Basi mwambie ukweli ajue kuwa na yeye hatakuwa na chaguzi ila kupokea maagizo tu.”

“Kumbe ndio hivyo!” “Tafadhali usimsikilize James.” “Sawa. Mimi nanyamaza, tuone mtakapofika. Kama utapokea ushauri wa mtu au kutaka ulichokifikiria wewe ndio kikubaliwe hapa.” “Kwani eti mama Jema, kuna ubaya gani pale kwako kuwekwa msichana wa kazi ili asaidie kazi za Jelini pia? Na kabla hujakataa, naomba nikutoe hofu. Malipo yote ni juu yangu.” Wakaanza kucheka.

“Sikusema mimi?” “Hivi wewe James ujue sikuelewi kabisa?” James akacheka na kutingisha kichwa akimtizama. “Colins, mimi sina wasichana wa kazi si kwa sababu ya uwezo, ni kwa kuwa sina uwezo wa kuishi nao. Sijawahi, sitaki, kwa kuwa siwezi kuishi na mtoto wa mtu ila wangu.” “Unaweza pata mzuri kama yule wa mama. Ameishi pale zaidi ya miaka 7.” “Hapana Colins. Labda tuendelee tu na Chaz. Anakuja, akimaliza kazi zake anaondoka. Hapo sawa.” “Si umeona jinsi mimi na mama Jema tunavyopanga yetu na kuelewana bila shida? James mgumu!” “Sawa mzee. Mimi nishakua mbaya wako. Sasa nikuone unarudi kinyumenyume.” “James wewe wangu mkuu.” Wakataniana kidogo, wakasikia mlango unafunguliwa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wote wakamtizama Colins, mpaka akasimama kwa kusikia tu Jelini anaingia. “Bibi!” Wakasikia sauti ya Jeremy. “Niko huku, njoo.” Akaingia akiwa amependeza kweli. “Jeremy umependeza!” “Mama alinipeleka kunyoa nywele.” “Lakini pia nguo zako nzuri na safi.” “Asante anti. Shikamoo anti. Shikamoo anko James, na anko Colins. Halafu na bibi wewe pia shikamoo.” Wakacheka. “Kwani nyinyi mnao lala pamoja hamjaonana?” “Aliamka wakati najitayarisha, nikamwambia arudi kulala bado mapema.” “Mama yako yuko wapi?” “Anamlipa mwenye bajaji. Naweza kumshika mtoto?” “Amelala bwana.” “Basi akiamka nitamshika.” “Umekula?” James akamuuliza. “Mimi na mama tumekula.” Akatoka hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakasikia Jelini akiingia. Akashituka sana kumuona Colins. “Vipi Jelini?” “Safi tu.” Akamjibu nakusita kama ambaye hakutegemea. “Umependeza sana.” Akamsifia kwa upendo. Jelini akamwangalia na kujibu. “Asante.” Kisha akapitiliza kwa Jema. “Pole na hongera.” “Nishapoa, hapa nina kazi ya kula nahisi nikitoka hapa nitakua kama dubu.” Jelini akacheka. “Na usivyopenda unene!” “Sasa kwa mama James amechemka. Anamwambia amnyonyeshee mjukuu, usichana baadaye.” Mama Jema akaongeza na kufanya wacheke kidogo, Jelini akasogelea kitanda cha mtoto akabaki akimwangalia.

“Jeremy alizaliwa mweupe, ila huyu kazini! Ana rangi kali kama kwa kina shem. Hongereni shem. Mtoto mzuri, mkubwa na afya nzuri.” “Asante, aisee. Mtoto mtamu aisee! Ni mpaka uwe naye ndio utaelewa.” James akaongea kwa hisia. Colins akamsogelea pale alipokuwa amesimama akimtizama mtoto. Jelini akamwangalia, mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi, ni Colins! Mwili mzima msisimko, akakwepesha macho.

“Na sisi tutakuwa na watoto wa ngapi?” Akamuuliza taratibu, chumba kizima wakaangaliana. Jelini alishituka, akamtizama akiwa amekunja uso. “Au unataka kuzaa na mtu mwingine?” Uliza hiyo ya kubembeleza, Jelini akapandisha mabega kukataa, kwamba hataki kuzaa na mtu mwingine, ila macho alisharudisha kwa mtoto. Chumba kizima kimya Jema akaendelea kunywa supu yake.

“Mimi napenda familia kubwa zaidi ya kwetu au hii yenu. Angalau watoto wanne.” Jelini akamwangalia akimshangaa. “Kwamba Jeremy apate mdogo wake mwingine wa kiume, halafu na dada zao wawili. Au unaona watakuwa wengi sana?” Jelini akabaki hajui azungumze nini. Wapo kwenye kujenga familia hata hajamwambia kama anampenda! Akabaki kimya macho kwa mtoto, anashindwa hata kusogea.

“Jelini, au unaonaje?” “Mimi sijui Colins.” Jelini akajibu na kuondoka hapo akarudi kwa Jema. “Naomba uniazime gari yako, au unampango wa kutoka?” “Sina niendako mimi. Wewe chukua tu.” Akamgeukia mama yao.  “Mama, nitarudi baadaye.” “Umekumbuka dawa lakini?” “Nimemeza na nyingine zipo kwenye pochi.” “Sasa usije ukajisahau huko, ukaacha kunywa dawa kwa wakati, kichwa kikaanza tena.” “Nitakunywa.” Akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakamuona Colins anacheka. “Siku nikipata mtu mwenye kichwa kama chako!” Colins akazidi kucheka. “Bwana Jelini hataki kuzaa na mtu mwingine. Nishajua sina mpinzani.” Mpaka Jema akapaliwa na supu kwa kucheka. Wakasikia gari inaondoka huko nje. “Amesema mwenyewe. Sasa hivi amenikasirikia tu. Hasira zikiisha, tunaweka mambo yetu sawa.” “Wewe mbambaishaji bwana.” “James amekosa imani na mimi! Sasa si natengeneza mazingira ya nyumbani kwetu kwanza? Maana tulianza na msingi wa watu wengi mno. Nishakata mizizi yote. Nikikamilisha jambo langu la mwisho, ndio narudi kuanza…” Akawa kama amekumbuka kitu.

“Jelini anakwenda wapi?” Akauliza na kumtimza mama Jema. “Sijui.” “Haa! Hatuwezi kutojua Jelini alipo, na yeye ni mgonjwa.” Akaanza hivyo taratibu lakini kila sekunde ilipozidi kwenda ndio paniki ikamzidia. “Sasa wewe si umesikia akiaga hapa. Kwa nini hukumuuliza, unataka kutukera sisi?” James akambadilikia. “Nashauri mama Jema ampigie, amuulize.” Hapo amebadilika kabisa.

“Labda tumsubirie arudi.” “Nashukuru kwa hilo wazo  mama, lakini sidhani kama ni sawa. Lazima tujue alipo ili…” “Mimi namjua Colins, mama. Hutameza mate, mpaka upige hiyo simu. Sasa kuliko uwaache walumbane hapa na James kama watoto walionyang’anyana ziwa, piga wote tuheme.” “Asante Jema.” Bila aibu akashukuru na kurudisha macho kwa mama Jema. Kwamba apige.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mama Jema akaona bora tu apige. Ikaita mpaka ikakatika. Tayari Colins akabadilika rangi na sura. “Tafadhali jaribu tena.” Akapiga tena, haikupokelewa. Kisha wakaona Jelini mwenyewe anapiga. “Simu ilikuwa kwenye pochi mama. Kwema?” “Nilisahau kukuuliza, unakwenda wapi?” Jelini akashangaa kidogo. “Nimesema narudi! Kwema?” Colins akaanza kutingisha kichwa akikataa kama anayetaka Jelini ajibu anapokwenda. Mama Jema akaelewa. “Nataka kujua ulipo mama yangu. Sitaki kichwa kianze  huko halafu ujikute upo peke yako.” “Asante mama Jema.” Colins akanong’ona. James akatingisha kichwa kwa masikitiko.

“Jelini?” “Naenda kuchukua vitu vyangu vyote kwa Kasa, sitakaw..” “HAPANA.” Akasikika Colins kwa mshituko mkubwa sana, na kupokonya simu ya mama Jema. “Hapo hapana Jelini.” “Sasa hapana ya nini wakati hata wewe nilikwambia niliacha vitu vyangu kwake.” “Tukakubaliana vipi?” “Mimi sikumbuki tena.” Jelini akajibu.

Hapana. Hapana Jelini. Huwezi kwenda.” “Sasa kwa nini wakati ni…” “Hapana Jelini. Unataka kunichanganya bila sababu. Huwezi kurudi kwa yule mzee. Hapo nimekataa. Na sivyo tulivyokubaliana hivyo na najua unakumbuka.” “Sasa unakasirika nini wakati nimesema naenda kuchukua vitu vyangu tu, nakurudi! Kwani nimesema…” “Jelini. HAPANA. Hivi unafikiri sisi tutakuwa wazazi wa namna gani? Watoto wetu watakua kwenye makuzi ya namna gani? Wazazi ambao wanapanga…” “Colins. Tafadhali toka nje kazungumze mipango ya watoto wenu nje ya hapa, mimi mwanangu amelala. Unaongea kwa sauti, utaniamshia mtoto.”  Akamgeukia mtoto.

“Toka bwana.” Akasogea hatua chache akakumbuka ni simu ya mama Jema, akasimama. “Jelini?” “Mimi naenda kuchukua vitu vyangu tu.” “Tulizungumza nini mimi na wewe na kukubaliana nini juu ya kabla yakurudiana na yule mzee au hata kabla hujaanza jambo jingine, na mtu mwingine? Kimya. “Najua unakumbuka ila nakukumbusha, tulikubaliana tuambizane. Na tukakubaliana vizuri sana. Sasa leo unataka kufanya nini tena?” “Sasa nani amesema naenda kurudiana na Kasa?! Mimi nimeomba kwenda kuchukua vitu vyangu.” “Hapana Jelini. Huwezi kufanya hivyo. Nimekataa. Tafadhali usiende. Huwezi kuwa unasema humtaki mtu, halafu unachukua vitu vyake. Kama kweli humtaki Kasa, muonyeshe kwa vitendo na mali zake hutaki.” Kimya.

“Jelini?” “Mimi naomba nikuage Colins, nisimame sehemu nilie kwanza.” Pale chumbani wote wakaangaliana. “Sasa unalia nini na wewe mtu humtaki? Au humaanishi?” “Naomba nikuage Colins. Sasahivi nataka kulia mwenyewe.” “Unalia wapi na mimi nije?” “Nataka kulia peke yangu.” “Sasa kwa nini unalia?” “Toka Colins. Toka na simu ya mama Jema tunakupa. Toka nayo, usiniamshie mwanangu.” James akamfukuza. Akatoka.

“Jelini tafadhali usilie, kichwa kitakuuma. Niambie ulipo nije.” “Sitaki. Wewe unanichanganya tu. Mara urudi kwa mwanamke wako, mara ukimbilie alipo halafu mimi ndiye unayechagua kuniumiza. Sasahivi mimi naenda kuchukua vitu vyangu, unanikatalia! Acha nilie peke yangu.” “Lakini bora mimi nilikuaga kabla sijaenda. Japokuwa nilikuwa naumia, lakini nilikuaga Jelini. Nilikuaga nikiumia sana moyoni, lakini sikuwa na jinsi, ilikuwa ni shindikizo kutoka kwa wazazi na nilikwenda hospitalini kama mmoja wa familia si mpenzi.” “Sasa nani amesema nakwenda kwa Kasa kama mpenzi?” Jelini akauliza.

“Kwa nini sasa mimi nisijue kama unaenda kwake, na kwa nini uende peke yako? Halafu inaleta picha gani, eti unamwambia mtu humtaki, lakini bado unamfuata kwake? Tena sehemu mliyokuwa mkikutania! Hapana Jelini. Hatutakuwa na maisha hayo. Tafadhali turidhike na tulicho nacho. Na wewe mwenyewe umeniambia nisijifananishe naye.” “Sasa kwa nini ujifananishe naye?” “Wewe ndio unaanza kunifanya nianze kujifananisha naye na nione amenipita. Maana ningekua na pesa kama zake, ningesema nikununulie hivyo vitu vyote, ilimradi tu usirudi tena kwake. Lakini mimi sina hela. Tafadhali naomba usirudi kwa yule mzee sababu ya mali Jelini. Utaniumiza mpaka kifo changu.” Jelini akapoa.

“Unanisikia?” “Siendi.” “Nashukuru. Kwa hiyo unarudi?” Akauliza kwa kubembeleza. “Napitia saluni, kumuona dada mmoja hivi, kisha narudi.” Colins akapoa. “Siendi kwa Kasa, Colins! Nishakwambia siendi, ujue sitarudi tena huko. Ila ujue sio vitu vyote vilivyopo huko kwake vinatokana na pesa yake. Vingine ni vitu vyangu.” “Jelini!” “Nimesema siendi Colins! Mbona wewe unashindwa kuniamini, wakati wewe huwa unarudi kwa Love na sija…” Akasita kisha akakubali yaishe. “Sirudi kwa Kasa.”

“Sasa bado utalia?” “Sasa naliaje na mazungumzo yote hayo mpaka tena hamu ya kulia imeisha!” “Afadhali. Maana itakua kama unalilia vitu vya Kasa, na ujue mimi ndio nitaumia zaidi.” Jelini akatulia. “Uwe mwangalifu huko. Na usisahu dawa.” “Sawa. Asante.” Wakakata.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hapo nyumba nzima walikuwa wakiwasikiliza wao. Maana mwanzoni alimwambia mama Jema aweke kwenye spika na yeye asikie, sasa wivu ulivyompanda, akasahau kutoa kwenye sauti, akafukuzwa chumbani, akatoka bado sauti ipo juu. Wanamsikia Jelini na yeye mwenyewe. “Kazi ipo. Hapa!” Mama Jema akaongea kwa sauti ya chini. “Na si kidogo.” Jema akamalizia, wakacheka taratibu.

Akarudi ndani. “Nashukuru mama Jema kwa simu.” “Sasa si mazungumzo unahamisha kwa Jelini mwenyewe au bado tu?” “Nivumilie mama yangu. Nataka safari hii nikirudi kwake, iwe kama James alivyosema. Asinione mbambaishaji. Naweka sawa mambo ya nyumbani. Pakikaa sawa, sio tena longolongo, nafanya kama hivi alivyofanya James. Nakamilisha kabisa, akiwa anauhakika tunayo mazingira yakuweka watoto wetu bila fujo na mipango ya wazazi.” Mama Jema hoi. Huyo Colins anamipango mizito, si yeye mama Jema anayejua, wala Jelini mwenyewe hajui ndio anasikia hapo kama kuna kuanzisha familia na huyo Colins.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“We Colins hebu rudi kwanza hapa ndani, acha kutuchanganya.” Colins akarudi tena pale chumbani macho kwenye simu. “Sijui sasahivi atakua….” “Subiri kwanza Colins. Mbona unazungumzia familia na Jelini wakati sijasikia mipango ya hatua za mwanzoni za msingi!?” “Siruki hatua hata moja. Na mama naomba uniamini. Ila jamani hapa tunamzungumzia Jelini. Yaani wewe ukijidai upo kwenye hatua ya kwanza ya kutongoza, wenzio wanakuwa wameshamfikisha kanisani, wanapewa viapo vya mpaka kifo.          Unabaki kuitwa shemeji.” Wote hoi.

“Wewe acha aone mwisho tokea mwanzo, ili akitokea mpuuzi huko mbeleni na uongo wake, yeye Jelini anabaki na msimamo akijua anayo familia yake kabisa. Anatulia hakuna wa kumshawishi.” “Bado sikusikii kabisa, Colins!” “James! Mbona imani yako ipo hivyo na unakua kama hatujazungumzia hili?” “Wewe ongea mama akusikie.” “Sawa.” Akamgeukia mama Jema.

“Kuna vijitabia vilikuwepo kwenye familia yetu. Ndio nipo kwenye marekebisho. Kama uliangalia vizuri, utagundua hata geti la nyumbani kwangu lilikuwa likiingiliana na wazazi. Sijui kama uliona?” Akauliza akimwangalia mama Jema. “Sikuwa hata nikiangalia mazingira.” “Basi mambo kama hayo nipo narekebisha na mengine mengi, ambayo yanahitaji mpaka babu aje amuweke sawa baba. Wajue nimekua na waelewe mimi ni mtu mzima naweza kufanya maamuzi yangu, ili tukianza maisha yetu na Jelini, kusiwe na muingiliano tena. Sitaki anione mbambaishaji. Kwahiyo mipango ninayo. Nikimaliza hapo nafanya kama James, kila hatua. Sitaruka hata moja mama yangu. Mimi si muhuni. Si mbambaishaji.” “Sawa.” Mama Jema akiwa anaitika, wakasikia mama James naye anaingia. Baada ya salamu yeye Colins akaondoka lakini akamuacha mama Jema na furaha.

Mtu Chake.

Huku kwa Jelini akafikiria bado roho haikutulia. Akaenda saluni anayopenda kwenda kucheka na kuongea na mashangingi wa jijini. Wanawake waliopenda jiji na kulijulia, ndipo alipokuwa akiwakuta hapo. Stori zikianza, Jelini na yeye mtoto wa mjini, basi atashinda hapo siku nzima, kisha baa, enzi hizo. Kashazoeleka hapo, akifika anaanza porojo kisha kurembwa. Akajua hapo atampata mtu wa kumsaidia.

Akaenda mpaka hapo, akamkuta Sheha. “Niambie anti langu.” “Nina dili hilo anti Sheha, utanipenda bure.” “Zaidi ya hivi?” “Njoo nje tuzungumze.” Wakatoka. “Nipe dili za mjini.” “Panda kwenye gari tutete yetu kwa kituo.” “Mbona gari hii sio ile ya ukweli? Au ushapokonywa?” “Habari yake ndefu. Ila ipo, sijapokonywa.” Akaingia garini.

“Sasa mimi nina jambo langu nataka msaada. Ila ujue na wewe utanufaika sana. Unisikilize kwa makini usije kosea.” “Mie tena?” “Nakuaminia ndio maana nimekufuata wewe. Sasa mimi yule mzee nimeachana naye, simtaki tena.” “Yule aliyekupa gari!?”  Sheha akashituka haswa. “Sasa na wewe unafikiri yupi?” “Unawazimu wewe!?” Akawa kama ameona mzimu kwa mshituko. Unaanzaje kumuacha mwanaume kama Kasa! Hilo likashindwa kuingia akilini kabisa.

“Sasa nataka kukupa wewe.” Hapo Sheha akakaa sawa. “Kwa nini!?” “Nimekwambia mimi napenda mtu wangu wa peke yangu.” Sheha alicheka mpaka machozi. “Bado huo utoto unao tu?” “Wala sikati tamaa.” “Basi hama kabisa ulimwengu huu wa wanaadamu.” “Wewe unamtaka au humtaki?” “Mie tena! Kwa baraka zako walahi silazii damu. Ila nataka uhakika Jelini. Usije ukaona kwangu vimenoga, ukarudi kinyumenyume!” “Hutanisiki anti wangu. Ila tu, nataka vitu vyangu nimeacha kwake. Roho inauma!”

“Kwamba wewe hutaki hata kumuona!?” “Ewaaa!” “Kwa nini!?” “Unataka nikwambie ukweli?” “Ndio maana yake! Nijue tatizo lake.” “Nilimfumania na mwanamke wake.” Sheha akabaki akimsikiliza kujua tatizo. “Ndio hivyo.” “Wewe mtoto si mzima! Au mimi sijaelewa kwamba umemkuta na mwanamke wake!” “Aliniambia anamuacha kwa ajili yangu.” Sheha alicheka tena, mpaka machozi.

“Kama ndio hivyo naondoka.” “Basi anti. Nipe mimi nisiyetaka wangu wa peke yangu. Sitaki kufuatana mimi. Wakati yeye anagongesha kwingine, na mimi nagongwa na wengine. Tukikutana, tunaendelea.” “Sasa hapo ndio pagumu. Kwa jinsi ulivyo hivyo, ndio udhaifu wake, na atakuwekea wivu sana.” Hapo akafikiria kidogo, lakini akaona bado hamna tatizo. “Mjini hapa, nitampiga chenga za kiutu uzima tu. Wewe usijali. Sema jingine.” Jelini akacheka.

“Nini?” “Anataka kavukavu.” “Kwa mihela ile, nampa.” “Hujaelewa. Anataka kavukavu lakini kabla ya mchezo lazima akupime.” Akatoa macho. “HAIWEZEKANI!” “Kweli. Ana kipimo chake hapohapo kwake.” “Mmmh! Hapo mtihani. Maana hapa kati nimecheza rafu! Asikwambie mtu. Nimepiga chenga za Ronado.” “Bila kinga!?” “Wala sitakudanganya, kwingine nimetoa kavu, sababu ya pesa. Nataka kufungua saluni nyingine, kubwa zaidi ya hii.” “Sasa huyu atakufaa, ila kupima nilazima.” Akabaki akifikiria.

“Kwa hivyo ulivyo anti langu, hakika nakwambia ukifuata ninachokwambia, ukafanikiwa kuingia kwake, hutahitaji mwanaume mwingine. Bwana yule mwanaume anayo pesa!” “Acha kunipagawisha bwana!” “Kwani mimi huwa nakuongopea? Ukimpata yule, umepona. Na hivyo huna shida akiendelea na wanawake zake!” “Namtaka wangu wa peke yangu kwani yeye roho? Akuu! Sitaki kugandwa kama luba mimi.” “Sasa yule atakuganda.” “Wewe hilo niachie mimi. Nitampiga chenga hizo, namfunga kasimama.” Jelini hana mbavu.

“Ila atanikubali? Maana wewe dogodogo.” “Kwa jinsi nilivyomfahamu, anapenda rangi kama hiyo yako na hilo tako. Hivyo utamchanganya wala hatajali umri. Maana mwanamke niliyemkuta naye na ndiye huyo nimemfumania naye wala si msichana mdogo, mkubwa tu tena anaweza hata kukupita wewe. Ila umbo lake lipo kama hili langu na wewe, ila sema yeye mweusi. Sasa hivyo wewe anti ulivyo kama shombe! Utamvuruga kabisa.”

“Tatizo huko kupima!” “Yaani ndio umecheza rafu mbaya hivyo anti Sheha?!”  “Umechelewa tu hapo saluni. Nilikuwa nawapa michapo ya Dodoma. Nimechanganya wabunge kwa mawaziri mpaka nikatimiza lengo, ndio nikaondoka. Sasa kwingine nilikuwa nakwenda na wengine wabishi, hawataki kondomu, halafu pesa yao ndefu! Nikajitoa muhanga, ila nilikuwa nikijitahidi kujilainisha ili wasinichubue. Ila nimewaza kitu.” Akawa kama amekumbuka.

“Wewe nipe siku ya leo, nikajipime mwenyewe kabla sijaenda huko na kuingia aibu.” “Sasa kwani miezi mitatu ishapita tokea ucheze hizo rafu zako?” “Jelini naye? Mbona unaniangusha anti langu? Siku hizi wana vipimo hata kama vijidudu ndio vimeingia jana, wataviona. Sema sikuwa nataka kupima. Ila kwa jinsi ninavyomtaka huyo mwanaume, acha niende leo, kesho nipe mipango.” Jelini akabaki akifikiria. “Kumbe na mimi sina haja yakusubiri muda wote huo! Nabaki kujitesa bure kwa hofu nikisubiri muda ufike, nipime! Nakwenda kupima.” Akawaza.

“Mbona umepotea?” “Yule mzee yupo busy. Ukitaka kumpata kwenye 18 zako, iwe leo.” “Jelini wewe unataka nisifanikiwe bwana! Nahitaji muda na niende kwake nikiwa nimetulia. Sio na paniki. Kumbuka ndio umenipa taarifa zakupima. Hapa roho mbio. Sijajitengeneza! Nisaidie anti langu nicheze mchezo kwa utulivu.” Jelini akafikiria. Na kwa jinsi anavyomjua Kasa, hataki pupa. Akafikiria kwa haraka akajua chakufanya.

“Basi sawa. Juma hili zima wewe jiweke sawa. Kapime. Ila jumamosi jioni lazima kwenda ukiwa umetulia. Sasa sio ufanikiwe, usahau mizigo yangu.” “Siwezi. Lazima nikulipe fadhila.” “Na kingine, usije fika pale ukaanza kwa ushangingi. Unakwenda pale ukiwa nimekutuma kuchukua mizigo yangu tu. Weka mazingira ya akutamani. Malaya yule, atakutaka tu. Vaa kitu kitakachoonyesha tako lako na…” “Jelini naye? Sasa mimi ndio wakuniambia chakuvaa!” “Usiende kishangingi dada. Yule mzee msomi. Muendee taratibu. Maswala ya shanga 90, acha.” “Usiniambie huyu ni wale wa cheni moja?” “Basi naona umeshanielewa. Mpe ya kikubwa, kiustarabu mpaka abaki anakuwaza.” Wakacheka hapo muda tu, Jelini akimpanga mpaka wakaelewana.

Jelini akaondoka akiwa amefurahia atapata vitu vyake na taarifa kwamba anaweza kupimwa hata siku hiyo, hana haja ya kusubiri kwa muda mrefu, hilo likamfurahisha na kuliweka moyoni. Safari ya kurudi kwa dada yake ikaanza.

~~~~~~~~~~~~~~~

Njiani akampigia simu Ndosi. “Vipi Jelini mtoto mzuri?” “Naomba mwambie Kasa awaambie walinzi wake nawafanyakazi wa ndani, sitakwenda leo, mpaka jumamosi ijayo ndio nitamtuma mtu.” Ndosi akapoa. “Ndosi?” “Nipo. Kwa nini tena!?” “Hee! Mbona unaongea kana kwamba nimevunja miahadi na mtu!? Mimi ndiye niliyekupigia simu na kukuomba umwambie Kasa awaambie walinzi wake na wafanyakazi kwamba nitakwenda kuchukua vitu vyangu leo.” “Sasa kwa nini huendi tena leo?” “Wewe Ndosi vipi?! Unataka kunipangia kitu gani chakufanya?! Vitu ni vyangu na muda ni wangu. Nimesema siendi leo mpaka jumamosi ijayo ndio nitamtuma mtu. Fikisha ujumbe.” Akakata simu.

~~~~~~~~~~~~~~~

Huku kwa Kasa siku hiyo aliahirisha kila kitu baada ya kuambiwa na Ndosi kwamba Jelini ameomba kwenda kufuata mizigo yake. Akajua msamaha alioomba hospitalini, ndio anakwenda kujibiwa. Alifurahi kupita maelezo. Ikaanza kazi ya kumpikia na kujiandaa kwa maneno mazuri atakayomwabia pindi atakapofika hapo, mpaka Jelini asamehe na warudiane kabisa.

Matayarisho yakaendelea kwa nguvu zote. “Hata akitaka ndoa nampa. Akitaka watoto?” Kasa akabaki akiliwaza hilo muda wote akifanya matayarisho ya Jelini huku akijishauri. “Vichanga sasa hivi!” Akabaki njia panda. “Ila nitamuhakikishia Koku si tatizo tena. Atakaa jela mpaka ajute kunidhalilisha mbele ya Jelini. Hakika atalipa kwa uchungu.”

~~~~~~~~~~~~~~~

 Mzee alitoa vijana wake tu, na mume wa Kemi ila si Koku. Alikuwa na uchungu naye kama aliyebakwa! Lakini kwa hakika aliwapa adhabu. Kule alipokuwa akifanya kazi mume wa Kemi, alishaziba hilo pengo. Akaweka mfanyakazi mwingine. Noah anatoka jela akiwa amekusudia kuvunja ndoa kabisa, kuwa Kemi amemponza. Talaka ndio kinachofuata, anarudi Shinyanga na kutafuta makazi ya kudumu, anagundua hana kazi. Na hakujua Kasa alifanya nini ila alitoka rumande mali zake zote zimekuwa frozen. Kwamba mali zake zimeshikiliwa mpaka uchunguzi ukamilike. Hiyo ikawa adhabu ya Kemi kupitia mumewe. Wakajikuta wote wawili huru bila kazi na mali zimeshikiliwa.

Kwa upande wa Kasa Kevin, yeye akakuta magari ya mzee yote yamefungiwa. Na vitu vyake vyote yaani nguo, zimewekwa kwenye masanduku, vipo nyumbani kwa dada yake. Nyumba zote za mzee zimefungwa, haruhusiwi kufika huko. Ukawa mshituko wa aina yake, ila angalau anayo kazi. Wote watatu hati zao zakusafiria pia zikawa zimeshikiliwa, hawaruhusiwi kutoka nchini, eti mpaka uchunguzi ukamilike. Lakini Koku, akawa bado ndani. Ikawa ni hali ngumu kupita kiasi.

Ila wote wakamlaumu sana Jelini. Kwamba kama sio yeye kuwepo kwenye maisha ya baba yao, yote hayo yasingewapata. Jelini akawa mbaya wao wa kupita maelezo wanataka kumuumiza aumie kama wao wanavyoumia.

~~~~~~~~~~~~~~~

Ø  Watamlipaje kisasi Jelini Ambaye Naye Anawakwepa Kwa Kukaa Mbali Na Baba Yao?

Ø  Sheha Atafanikiwa Kwa Kasa? Litatimia La ‘Ukisema Cha Nini, Wenzio Wanalia Watakipata Lini’?

Ø  Habari Ya Kutokwenda Kwa Jelini Siku Hiyo, Akiwa Anajiandaa Vilivyo Mpaka Ndoa, Kasa Ataichukuliaje?

Ø  Colins Atafanikiwa Kumshinda Baba Yake Au Ndio,  ‘Sikio Halizidi Kichwa’?

Usipitwe Na Muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment