Aliporudi ofisini akakuta barua ya James kuanza likizo kwa siku 7. Akampigia. “Nilisahau kukupa hongera James. Am so proud of you, man!” “Nashukuru aisee. Siamini. Mtoto mtamu kuliko pesa, aisee!” Colins akacheka. “Kama wewe unasema hivyo, naamini. Hongera sana. Na mpe Jema pongezi na pole. Pakitulia nitakuja kumuona mjomba.” “Jema atasikia na karibu sana.” “Kabla hujakata simu, utajali nikiwa nikimtumia yule kijana wako aliyekuwa akiwasaidia wewe na Jema hapo nyumbani kwenu? Au sasahivi mtakuwa mkimuhitaji zaidi? Maana ulimsifia ni mwaminifu sana.”
“Bila
shaka. Maana kwa sasa hapa ndani kumejaa mno. Tunamsaada kila kona. Na najaribu
kumshawishi Jema akubali tuletewe msichana wa kazi kwa ajili ya mtoto. Unajua
kwao wamekua bila msichana wa kazi. Sasa namchukulia taratibu sana. Hataki
msichana wa kazi kabisa humu ndani. Ila najua tutahitaji atakapokuwa anarudi
kazini. Ninachotaka kusema, wewe zungumza na Chaz mwenyewe. Na kwa kuwa
alishafika kwako, mpange naye muda na siku. Hapa nyumbani atabakiwa na kazi za
nje tu, ambayo najua kwa jinsi alivyo, haitamtosha. Atahitaji pesa zaidi.” James asijue jinsi
anavyomsaidia.
“Basi acha
nizungumze naye. Tuwekane sawa. Nakushukuru, ila naomba nikuombe msaada James.
Najua sasahivi unamtoto, akili zipo kwa mkeo na JJ.” James akacheka. “Au umebadili jina?” “Hilo lilishapitishwa, naona na mwenyewe
analijua.” Colins akacheka. “Sawa baba JJ.
Lakini naomba niangalizie Jelini wangu.” James akanyamaza.
“Kuhakikisha
anapata dawa sahihi kichwa kitulie. Na tafadhali zungumza na mama yake, atulie
swala la kazi kwanza mpaka apone kabisa. Kwa jinsi nilivyomsikia yule daktari
akizungumza na sisi tulipomrudisha hospitalini na mama, Jelini bado ni mgonjwa,
James. Aliona kabisa ndani hajapona. Na yeye alimwambia. Hata mwanga wa nje
alimwambia atumie miwani ya jua wakati wote ili kufanya mishipa ya kichwa
itulie. Tafadhali naomba ulisisitize hilo. Ni kwa muda tu wakati
nikijipanga. Nikiweka mambo sawa, nitakuwepo mwenyewe. Lakini kwa sasa,
naona upo sahihi. Nitamuumiza yeye zaidi. Acha nitengeneze mazingira yetu. Ni
hilo tu. Nisaidie tafadhali. Na kama kuna uhitaji wa pesa, niambie, utakuwa
ukichangia kupitia mfuko wangu.” “Sawa, Colins.” Hakuamini jinsi James alivyokubali.
Akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Zilipita siku tatu
tu, ramani ya nyumbani kwa Colins ikawa imekamilika. Kazi ikawa inaanza rasmi
siku ya jumatatu. Katika siku zote hizo tatu alishatuma ujumbe kwa wazazi kuwa
James amepata mtoto, yupo likizo. Kwa hiyo kazi zake zote anafanya yeye.
Atakuwa busy, akitoka alfajiri kurudi usiku, hakutani na watu wa nyumbani kwao.
Siku ya jumamosi
akiwa saluni akijisafi kichwa, simu ya mama yake ikaingia. Akapokea na
kumsalimia. “Mbona huji kula nyumbani.” “Kwa sababu
napika kwangu.” Mama yake akatulia. “Kama hakuna
jingine, naingia saluni mama, nitawaona kesho asubuhi kabla ya kwenda
kanisani.” “Sawa.” Mama yake akakata, akijua wazi hajafurahia ila
hakujali tena. Yupo kwenye kutengeneza kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati anatoka saluni,
simu ya baba yake ikaingia. Na yeye akamsalimia. “Usiku
tumekubaliana kukutana nyumbani kwa mzee Simba.” “Sawa.” Colins
akakubali kirahisi mpaka baba yake akashangaa. Ila akaamua kumuaga. Colins
akarudisha simu mfukoni, alikuwa na mpango wa kurudi kwake, akaamua kurudi
kazini akiwa na mawazo haswa. Akili yote inamuwaza Jelini.
Jumapili Ya Mapinduzi Mazito.
Asubuhi akasikia mtu akimgongea, akaamka
usingizini akaenda kufungua mlango akiwa na usingizi maana alikesha akiwa
anacheza game, akishindwa kulala. “Baba anakuita. Amesema sasahivi.” Alikuwa
Jose. Colins akatoka baada ya kuvaa suruali.
Akawakuta mezani
wakipata kifungua kinywa, na Connie alikuwepo. Akasimama na kumkumbatia kaka
yake, Colins akampa busu la kiusingizi, Connie akarudi kukaa mezani na wazazi
wake. “Kwa nini jana hukutokea kwa Simba?” Colins akakunja uso kama ambaye
hajamuelewa baba yake lakini alijua wazi ni nini anazungumzia. “Colins?” “Sijui
unazungumzia nini!” “Usijifanye hujaelewa Colins! Sikukupigia simu kukutaarifu
kwamba tumekubaliana usiku ule tunakutana kwenye familia ya Simba? Tena ukasema
sawa!” “Kabisa.” Colins akakubali.
“Sasa kwa nini
hukutokea?” “Wapi tena baba? Mbona unanichanganya!? Wewe ulinipigia simu na
kuniambia mmekubaliana mnakutana kwa Simba. Sasa!?” “Swali ni kwa nini hukuja,
na simu ulifunga?” “Labda kama unataka kugomba tu na mimi, baba. Kama
mmekubaliana kukutana kwa Simba, hapo mimi nahusikaje!?” Mama yake alitegemea
tu. Connie kimya.
“Mimi sikuwa na
ratiba ya kwenda huko. Sasa kwa nini nivunje mambo yangu kuungana kwenye
makubaliano yenu?” “Kwa…” “Subiri kwanza baba. Nahisi kuna jambo unalipuuza
hapa. Simba ni rafiki yako wewe. Au yeye na mkewe ni marafiki zenu nyinyi, mlio
wachagua nyinyi tokea zamani. Mkalea familia zenu, mkizijenga kwa
makubaliano yenu nyinyi. Ikafaa wakati ule sisi ni wadogo. Lakini si
sasahivi. Usitake mimi nijenge familia yangu kwa misingi yenu, wewe na mzee
Simba! Hapana baba.” Colins akaongea kwa ujasiri maana alimjua mzee
wake.
“Nyinyi ndio
marafiki. Lakini mimi nafahamiana nao kukupitia nyinyi!” “Na mimi ni mzazi
wako.” “Sawasawa. Lakini haimaanishi ulichochagua wewe ndio nitakachochagua
mimi! Marafiki zangu, sio marafiki zako. Au marafiki wa mama sio
marafiki wa Connie. Tafadhali hilo naomba uzingatie baba. Wakati ule
nilikuwa niko na nyinyi kwenye ile familia kila wakati kwa sababu kulikuwa na
mahusiano mengine kati yangu na Love. Yale mahusiano yameisha.” “Lakini
ameomba msamaha na anakiri ana…” Colins akacheka akitingisha kichwa akikataa.
“Nilisema, simtaki
tena Love, na NILIMAANISHA. Sitarudiana tena na Love, baba. Hilo naomba
ulipokee.” “Na nisipolipokea?” “Hilo tena litakuwa nje ya uwezo wangu.” Colins
akajibu akionyesha hajali tena. “Colins!?” “Nini mama? Nini? Yaani gafla
mnataka eti mimi nijenge familia yangu kwa kupitia misingi yenu!? Hapana.
Kuna faida gani basi ya kunilea na kunifundisha kufikiria na kufanya maamuzi
mimi kama mtoto wa kiume? Si kila wakati mtapenda nilichopenda, na mimi
hivyohivyo. Sio wakati wote nimekuwa nikiyafurahia maamuzi yenu!” “Kama yapi?”
Baba yake akamuuliza.
“Moja wapo ni hilo na
mengine ambayo sitayataja hapa kwa sababu siyo pointi ya sasahivi. Ila
ninachotaka kusema, nimeamua kuwa na maisha yangu ya kujitegemea kama
vile nilivyokuwa nikiishi nje ya nchi. Nitaishi kwangu nikijitegemea.
Nitafanya maamuzi yangu kama mimi Colins. Mimi ni mmoja wa familia hii,
si kina Simba na marafiki zenu wengine. Ikitokea mna jambo lenu ambalo
linaangukia kwenye ratiba zangu, sitahudhuria. Ila ikitokea kwenye siku
ambazo nina nafasi na najisikia kuhudhuria, nitahudhuria. Lakini msiniburuze
mimi kama Colins wa miaka 10. Nimekua. Na hilo naomba mkumbuke na
kuliheshimu.” Colins akaweka msisitizo.
“Kingine ambacho
nilipanga kuwataarifu baadaye mkitoka kanisani, ila kwa kuwa mmeniita sasahivi,
acha tu niwaambie.” “Kwamba wewe hutaenda pia kanisani?” “Nitatafuta kanisa
ninalopenda mimi. Ambalo ndipo na familia yangu itakapokwenda huko.”
“Umechanganyikiwa Colins?” “Labda tumpigie simu babu, tumuulize kama yeye ndiye
aliyekuchagulia mke, rafiki na akakupangia sehemu ya kwenda kuabudu.”
“Colins mwanangu
wewe!” “Hapana mama. Naona mnataka kuyaendesha maisha yenu na yangu pia! Nimekataa
na nashauri hilo mliheshimu. Maana mnanijua. Katika hili sitayumba kama
nilivyobaki na msimamo nikiwa na Love, huku akinitesa moyo wangu mchana na
usiku bila huruma, lakini nikabaki kuwa mwaminifu kwa ajili mahusiano yenu.
Lakini sitafanya hivyo TENA. Sitaendelea kuishi maisha yako baba. Na
wewe naomba usiendelee kuishi maisha yako na yangu. Mwishoe utajikuta
ukitaka kuendesha familia yako na yangu pia.”
“Toka Colins. Unanivunjia
heshima.” “Mimi naondoka, ila mjue kuanzia kesho kampuni ya ujenzi inakuja
kuzungushia nyumba yangu uzio. Ujenzi utaendelea, na wameahidi ndani ya majuma
matatu watakuwa wamekamilisha. Kwa hiyo mkiona watu pale, msishituke.” Akamgeukia
mama yake. “Mama, wamesema upande ule unaopakana na kwangu wanaweza kukuharibia
ukoka wako kidogo, ila wamesema watapatengeneza vizuri, kiasi kwamba mpaka
panakamilika, na wewe ukoka wako utakuwa sawa. Ni hilo tu.”
“Na mimi pia sitaki
tena kwenda nyumbani kwa kina Simba.” Connie naye akadakia kwa haraka kabla
kaka yake hajaondoka. “Nyinyi watoto mmepatwa na nini!?” “Mimi nilikuwa sijui
jinsi ya kuwaambia mama. Lakini mimi pia nipo kama Colins. Wale watoto wa Simba
ni marafiki mnaotuchagulia kwa lazima, lakini mama wewe unajua wazi sio
watoto wazuri. Loreta anamsumbua Reji mpaka Reji ameshindwa. Anasema amevumilia
na amemuonya Loreta, lakini hakomi. Anamtumia mpenzi wangu mpaka picha za
uchi!” Mama yao akashituka sana.
“Haiwezekani Connie!”
“Hakika dad. Nimevumilia lakini nimeshindwa. Reji anasema yupo kama amepagawa.
Wakati mwingine anampigia simu mpaka usiku kabisa anamwambia halali anamuwaza
yeye na kuanza kumtumia picha zake akiwa uchi kabisa.” “Anauthibitisho?” Hilo
swali lilimfanya mpaka Colins akacheka kwa masikitiko.
“Yaani wewe baba
unafikiri Connie au Reji wanadanganya ili iweje?” “Acha kunihoji mimi kama
mtoto mdogo, Colins!” “Maana unachukua upande wa watoto wa Simba bila kutaka
kutufikiria sisi! Tangia lini mimi na Connie tumekupa sababu kuwa sisi ni
watoto wakaidi kiasi hiki? Ni kwakuwa tumevumilia, tumeshindwa baba.
Wale watoto ni shida, na najua mama alishakwambia ila unalifumbia macho ili tu
wewe undeleze urafiki na baba yao.”
“Colins unavuka
mipaka na sitakuruhusu.” “Unataka kunimalizia mimi hasira bure sababu
safari hii ameongea Connie kipenzi cha kila mtu humu ndani na wote tunajua
Connie anaishi maneno yake si muongo. Huna jinsi yakutoka ndio..”
“Nyamaza Colins.” Mama yake akakaripa. “Sawa.” Akajibu na kunyamaza akicheka
kwa masikitiko.
“Ninazo picha
alizomtumia Reji. Tena sikutaka anitumie yeye kwenye simu yangu, nimepiga picha
kabisa simu ya Reji, sehemu ambayo Loreta anachati naye mpaka muda utaona mama.
Sikutaka kumuuliza, lakini kumbe ndio sababu Reji alikataa kuja kabisa siku ya
mwaka mpya baada ya kujua Loreta atakuwepo. Anasema ni mbaya mno, tena anasema
akijikuta wapo wawili tu sehemu, yupo physical kabisa.” “Haiwezekani
Connie!” “Kweli mama. Reji anasema anatakaga kumshika kwa nguvu. Anasema
imebidi aniambie isije tokea siku namkuta amemshika sehemu, nikadhani ni tabia
yake.” Connie akaendelea taratibu kama mama yake.
“Wote mnamjua Reji
ananipenda na ndiye mwanaume pekee aliyekubali kuniunga mkono kwenye ndoto
zangu. Ananisubiria bila kuchoka. Halafu Reji ni mwaminifu. Sitaki
amjaribu mpaka amshinde nguvu. Hapana dad. Nakwambia ramsi kwa
sababu nataka leo jioni mama anisindikize kwa mama yake, tuzungumze na Loreta.
Kuanzia hapo mimi wale watoto siwataki tena.” “Sasa hapo Love
anahusikaje?” Mzee akaendelea kuhoji na kuendelea kumshangaza Colins.
“Love na Loreta ni
wale ndugu wa kufichiana siri za wanaume. Kabla hujauliza nimejuaje, kumbuka
nimekua nao. Inamaana kama Loreta amekua akimfuatilia Reji, basi ujue anazo
baraka kutoka kwa dada yake. Au dada yake anajua. Wale watoto ni wabaya dad. Ni
hivyo Colins hawezi kukwambia kila kitu kwa undani, lakini hata huyo Love unayempenda
pia ana mambo ya wanaume. Hatuliagi na mwanaume mmoja. Hatosheki, mkorofi
halafu mbabe. Anapenda mambo yaende kama anavyotaka yeye. Anapenda
kutupelekesha mimi na Colins tokea tupo wadogo. Yaani eti kwa sababu alizaliwa
miezi miwili kabla ya Colins, alikuwa anatuambia yeye ni mkubwa kwetu, anajua
mambo mengi kuliko sisi, ndio anatupelekesha! Mimi sitaki tena, dad. Na
naomba uelewe.”
“Na kingine kabla
sijasahau.” Colins akamuwahi mzee akiwa kwenye utulivi akimsikiliza binti yake,
maana kwake huwa ni mtulivu. Wote wakamwangalia. “Nawapa tu taarifa. Maamuzi
yangu yote, nimezungumza na babu kwanza.” “Unasemaje Colins!?” “Kwa nini!?”
Mama yake akaongeza kwenye swali la mumewe kwa mshangao mkubwa sana.
“Kwa sababu kama
hizi. Hakuna mtu ananielewa kwenye hii familia kwa urahisi kama babu.
Nimezungumza naye kwa urefu na mapana. Tofauti na nyinyi, babu amenielewa na
kunipongeza sana.” “Kwa kuwa hajui kwa undani..” “Baba, wewe
unalazimishia mambo na babu nimemwambia. Amesema anakuja uzungumze naye kwa
kuwa mimi huwezi kunisikiliza na ameomba rasmi, marekebisho au ujenzi
unaoendelea pale kwangu, nimwachie asilimia fulani ya garama, anataka
kulipia.” “HAIWEZEKANI.” Mzee akahamaki.
“Wewe mpigie simu
mwenyewe, mkatalie kuwekeza urithi kwa vitukuu vyake. Maana yeye
mwenyewe amesema nisifanye marekebisho ya kimasikini, yeye anayo pesa.
Anamalizia kuuza kahawa yake ya msimu huu, anitumie pesa.” “Sasa mimi sitaki
kusaidiwa majukumu yangu. Hiyo ni dharau na baba anafanya makusudi.” “Pengine
anaona kwa kuwa uko kinyume na mimi ndio maana.” “Colins!” “Wewe
usinikasirikie mimi. Mpigie simu babu wewe mwenyewe uzungumze naye. Au msubiri
anakuja yeye mwenyewe, naona yeye akizungumza na wewe ndio utamuelewa
zaidi.”
“Kweli Colins unakuwa
mkaidi kiasi ya kwamba upo radhi kuona jasho langu na Simba linapotea bure
hivihivi!?” “Kwani nilazima mimi nirithi baba jamani!?” “Unafikiria kweli wewe
Colins!?” Mama yake pia akazidi kumshangaa.
“Kwa nini mnanilazimishia
mim? Mpeni Love na mwanaume atakayemuoa! Sio lazima mimi! Kwani mtoto nimekua
mimi tu kwenye hizi familia?” “Mtoto wa kiume kwenye familia zetu hizi mbili ni
wewe peke yako! Kweli hilo unashindwa kulithamini Colins, na kuweka tofauti
zako na Love pembeni ukafanya maamuzi magumu ya kiume?”
“Nimeyafanya hayo
maamuzi magumu na kuweka hizo tofauti zetu pembeni kwa muda mrefu sana, tena
kwa machungu makubwa sana baba. Nimeweka kikomo, sitaendelea
kujitesa sababu ya ndoto zenu. Kwanza Love ndiye anayejitambua kuwa ni mkubwa
kwenye hizi familia zetu. Anasema anahaki ya kutuongoza mimi, Connie na Loreta.
Na nyinyi wote mnamsifia ni kiongozi mzuri na anaakili sana. Sasa kwa
nini msimpe hizo mali yeye kiongozi mzuri akaongoza mkiwa na uhakika zitakuwa
salama!?”
“Sisi tunachotaka mali zetu zote ziendelee kwa
kizazi hadi kizazi chetu. Kwamba wewe na Love ndio mngeendeleza mali zetu na zibaki
kwetu tu na vijuu mpaka vitukuu. Ili hangaika yetu isiwe bure! Lakini ikitokea
Love anakuja kuolewa na mwanaume mwingine, inamaana mali zote zinakuwa chini ya
huyo mwanaume na ukoo wake. Kweli kwa ukaidi wako tu unashindwa kuliona hilo!?”
“Sio ukaidi baba. Siwezi
nikawa kwenye ndoa na mwanamke asiyeniheshimu, hakubali mawazo yangu
hata kwa mchango mdogo tu, yupo tayari kunibishia hata kwenye mambo ya msingi, ilimradi
yeye ndio aonekane ana uwezo mkubwa wa kufikiria kuliko mimi! Love hanipendi,
ananidharau. Sasa eti mnataka mimi nibaki kwenye aina hiyo ya mahusiano eti
sababu ya mali zenu! HAPANA kwakweli baba.”
“Mimi pamoja na mke
wangu tutatafuta zetu na watoto wetu. Na naumia sana kuona mnachotaka nyinyi ni
mali tu bila ya kunifikiria mimi! Hakika unaniumiza zaidi. Na kuanzia
sasa, mimi binafsi naomba babu ndio azungumze na wewe kwa niaba yangu. Ukiwa na
swali lolote juu yangu, wewe muulize babu.” Colins akaondoka kwa hasira. Mzee
akanyanyuka ili aondoke kwa hasira.
Connie na sauti yake
ya upole akamuwahi. “Ila kanisani nitakuwa nikienda na nyinyi, dad. Mimi bado
nitasali na nyinyi ili tuwe tunapata muda mbali na wodini. Ila tafadhali isiwe
kwa kina Simba.” Huyo mzee anampenda Connie, roho yake! Akamwangalia tu, na
kupotelea chumbani kwake, mkewe akamfuata.
~~~~~~~~~~~~~~~
Colins aliondoka kwa ujasiri akijua mzee
atakuja tu kuwekwa sawa na babu. Hao baba zao, vichwa ngumu na baba yao, yaani
babu yao kina Colins ndio anawawezea. Babu yake Colins alikuwa mkoloni haswa,
lakini mwenye pesa ambayo akiongea mbele ya hao wanae aliosomesha kwa elimu ya
juu mpaka baba yake Colins huyo daktari, wanamsikiliza. Mkali kwa watoto wake
kama pilipili kichaa, lakini kwa wajukuu, ni mtu mwingine tofauti. Akisema
anakupa pesa, si pesa chache. Hapo Colins alikuwa akifanya ukarabati kwa jeuri,
akijua mamilioni ya babu yanakuja, na mzee atawekwa sawa tu.
Kama Penzi Lipo, Lipo tu.
Katikati ya likizo
yake ya siku saba ya uzazi, James akapokea ujumbe mwingine tena kutoka
kwa Colins. Akafikiria, siku hiyo ya jumamosi akaona amfuate mama Jema
aliyekuwa amefika hapo mapema na kuchukua nguo zote za mtoto kwenda kufua nje.
“Samahani mama yangu. Naomba tukae hapa kidogo.” “Hata nisisuuze kwanza!?”
“Mimi nitasuuza. Naomba nisaidie maana nipo kwenye wakati mgumu kweli.” Mama
Jema akaosha mikono na kukausha akiwa na wasiwasi. Wakatafuta sehemu wakaa hapo
nje.
“Naomba soma hizi
jumbe kuanzia hapa.” James akamfungulia simu yake na kumkabidhi. Mama Jema
akaanza kusoma. Akashangaa sana. “Huyu ni nani!?” James akamuonyesha jina kwa
juu ya zile jumbe. Akasoma. “Colins!?” James akatingisha kichwa kukubali.
“Mbona sasa anachoandika hapa si alivyoniambia Jelini? Jelini aliniambia ni
kama amerudi kwa mwanamke wake wa kwanza.” “Ndiyo na hapana. Ndiyo kwa sababu
siku miahadi yake na Jelini ilipovunjika, alilazimishwa na familia
kwenda kumuona hospitalini. Si peke yake, ila kama familia. Na ukweli baba zao
wanatamani sana waoane.”
“Lakini mama Jema,
Colins anampenda Jelini, anakaribia kurukwa na akili.” “Nimesoma hapa!
Sasa ni nini kinaendelea James!? Maana mimi aliniumiza sana Colins. Sikutegemea
jinsi alivyofanya kwa Jelini alipokuwa matatizoni, halafu na kuja kumgeuka!”
“Kwa kuwa namfahamu Colins, acha mimi nimsemee na nimuombee msamaha. Si muongo,
na wala si muhuni. Ni mtu wa maneno yake. Anajisikia vibaya hata
kukuona. Anahisi kukusaliti vibaya sana.” “Mimi?!” James akacheka.
“Unakumbuka juzi
usiku kuniona natoka, wewe ukiwa na Jema pale chumbani. Nikamwambia Jema asome
ujumbe kisha nikatoka?” “Ukarudi na dawa za Jelini pamoja na juisi sijui na
vitu gani?” “Ewaaah! Basi Colins ndiye aliyevileta. Aliishia getini baada ya
kujua wewe upo ndani. Akaniomba nikupe umpelekee Jelini, ila niseme vimetoka
kwangu. Sasa nimezungumza na Jema, nikamwambia lazima nizungumze tu na wewe.
Colins amelelewa…” James akamsimulia historia ya familia ya Colins na kina Love
kwa mapana na marefu mpaka mama Jema akapoa.
“Sijui kama
umenielewa?” “Lakini tuwe tu wawazi James. Ile familia yao na mimi niliiona.
Aina ya watu wao, wote tuliwaona. Mimi sijasoma, sipo kwenye mazingira kama
yale yao ya kisomi. Jelini wangu ndiye huyo shule hataki hata kusikia.
Kweli unataka mwanangu akajiingize kwenye hiyo familia, wanayotaka mahusiano ya
wao kwa wao! Si mnanitafutia matatizo kweli mimi? Maana sitaweza
kunyamaza nikiona wanamuonea mwanangu au wanamnyanyasa.”
“Kwa alivyoniambia
Colins, anaandaa mazingira ya Jelini kwanza kabla hajarudi kwa Jelini na
kumchanganya zaidi. Maana mimi nilimkemea kwanza. Nikimuonya asimchanganye
Jelini. Nikimpa wasiwasi wangu kama huo. Baadaye ndio akakiri kuwa, anafanyia
kazi udhaifu wote na kuziba mianya yote. Amekiri amekua akiishi kwenye misingi
ya baba yake, na amesema ameshazungumza na wazazi kuwa, anaanzisha maisha yake
sio yale aliyokuwa akiishi akizungukwa na chaguzi za baba yake.” James
alishaaminika kwenye moyo wa huyo mama, hakuchukua muda mrefu sana kumuweka
upande wake.
“Kwa hiyo ndio
hivyo.” “Mmmh!” “Na kutomuona mpaka sasa ujue ni kwa sababu ya kukuheshimu sana
wewe. Colins asingeacha kuingia ndani. Anaishia nje getini akisema hataki
kuharibu zaidi. Tafadhali mpe nafasi. Nina uhakika kama Jelini akiishia na mtu
kama Colins, hatajuta. Ni miongoni mwa watu waadilifu sana.”
“Sasa mlitaka mimi
nifanyaje?” “Cha kwanza nakuomba nisaidie haya mawasiliano kati yake na Jelini unipokee
ili nimfurahie mwanangu.” Wakacheka wakimjua Colins. “Sihemi mama yangu! Nakua
utafikiri naishi na Jelini humu ndani. Na akianza kuulizia hali yake, inakua
ugomvi kabisa. Mwishoe ndio unasikia nina mgeni getini. Na hapo atataka
nimpigie simu Jelini, niweke spika, asikie majibu ya anavyoendelea. Mpaka
nikamwambia Jema, Jelini atakuwa hanielewi. Maana hata kama ni kujali, vimezidi
mama yangu.” “Juzi Jelini aliniambia Chaz ametumwa na shemeji apeleke chakula
na kusaidia kazi pale ndani. Kufua na
kupiga pasi nguo zote. Mimi nikamwambia pengine umeona mimi nipo nikisadia sana
kazi za hapa kwako, ndio maana ukaamua kutupa Chaz.” James akacheka na
kutingisha kichwa kwa masikitiko akimuhurumia Colins.
“Ni yeye Colins, wala
si mimi. Tafadhali nisaidie mama yangu. Mwisho nitajivunjia heshima kwa Jelini,
bure! Ataona navuka mipaka. Kujali gani huko mpaka usiku mwingi kumpigia simu
kumjulia hali! Msamehe tu Colins, na naomba umuelewe.” “Acha nikwambie
ukweli James, ni vile umesema wewe. Lakini alishaniumiza sana na nikaona
ametudharau akitufananisha sisi na zile familia zinazo wazunguka. Ila
nimemuelewa. Na mwambie namshukuru kwa kumjali Jelini. Naona zile dawa
alizoleta, zinamsaidia. Jana ameshinda bila kulalamika.”
“Kuna jambo jingine.”
“Nini tena!?” James akacheka kama anayesita. “Niambie tu.” “Anavyosema Colins,
siku waliyompeleka Jelini hospitalini, daktari alieleza wazi kuwa pale
alipoumia Jelini, kwa ndani hapajapona.” “Hata nje hapajakauka kabisa.” “Basi
anasema daktari alitoa ushauri mkubwa wa Jelini kutulia ili kutofanya mishipa
ya kichwa kuuma. Kwamba Jelini anatakiwa kupumzika. Hata mwanga wa nje
anatakiwa kuvaa miwani ya jua.” Mama Jema akabaki kusikiliza akijua silo
analotaka kuwakilisha.
James akacheka. “Sasa
hili ndilo ombi lake Colins. Kwamba, Jelini asianze kitu kipya sasahivi.”
“Kwamba asifanye kazi?” James akacheka na kuendelea. “Amesema yeye anaweza
ajiri mtu, afanye kazi za Jelini, atamlipa yeye mwenyewe. Na wewe akupe pesa
uwe unampa Jelini kila mwisho wa mwezi ili atulie. Amesema unaweza mwambia
Jelini ni pesa yake ya matumizi unampa mpaka apone. Ili kumfanya atulie mpaka
apone kabisa.”
“Jelini mwenyewe
anataka kufanya kazi, James! Wala si mimi.” “Tukikubaliana, tunaweza kuzungumza
naye kwa pamoja na kumsisitiza kwa sasa anatakiwa atulie mpaka apone kabisa. Na
kwa sababu anamwangalia sana Jema, tunaweza kumwambia Jema azungumze naye.”
“Hapo atakubali. Maana anaona Jema alijikana sana. Yeye kuacha ni kama kukimbia
kuwajibika. Ila kwa kuwa kwenye saa nne watakuja hapa yeye na Jeremy, acha
tumpange kwanza Jema azungumze naye.” “Nashukuru mama yangu. Nampigia simu
Colins, namwambia namuhamishia kwako.” James akalifurahia hilo ila akakumbuka.
“Ila ujiandae. Maana
simu zake na jumbe si moja.” “Mbona mimi namjua! Wewe mpe tu.” “Basi acha
nimalizie hizi nguo.” “Hapana James. Wewe rudi ndani kwa mkeo na mtoto. Mimi
namalizia sasahivi nakuja ndani. Kwanza ni nguo chache tu. Nafua kila siku ili
zisilundikane, na sitaki mama James aje akutane na nguo chafu. Iwe chakula tu.”
“Nashukuru sana.” James akaondoka na kumuacha huyo mama moyo umetulia kuona
kuna mtu anamjali na Jelini kwa kiasi hicho.
Atafutaye Asiyechoka.
Baada ya muda mfupi
sana akiwa anasuuza nguo ujumbe ukaingia. Akaangalia simu kwa haraka akidhani
ni Jelini, kichwa kimeanza tena. Akakutana na huu ujumbe. ‘Nashukuru sana mama yangu kunielewa. Sikukusudia kumuumiza
Jelini.’ Amemaliza tu kusoma, ukaingia mwingine. ‘Nilisahau kukusalimia. Shikamoo.’ Ukawa wa pili. Kabla hajajibu
salamu, ukaingia na wa tatu. ‘Sijui hali ya Jelini leo.
Ameamkaje?’ Mama Jema akabaki akiitizama simu maana hajui ajibu nini.
James akatoka.
“Nimemuhamishia
Colins kwako. Nahisi atakutafuta tu.” Mama Jema akaanza kucheka akitingisha
kichwa. “Tayari nini!?” “Hapa nina jumbe tatu tayari, sijui nijibu ipi. Na
nyingine ya nne hii. Sijui ameandika nini!” James akacheka na yeye kwa
masikitiko akimsogelea.
‘Inabidi
kuongeza umakini kwa Jelini anayeonekana mzima akitembea, kumbe kichwa kina
matatizo. Matukio kama yale ya mahakamani ndio yanayoweza kuonyesha kuwa si
mzima.’
“Hakika kazi ipo! Hivi mimi sitaweza James. Sina muda wa kukaa chini na
kuandika jumbe, hata wanangu wananijua. Ni bora kupiga tuzungumze, tuyamalize.”
“Sasa fikiria ndio mimi. Nimelala na mke wangu, jumbe za kumzungumzia Jelini
zinaingia na anataka ajibiwe. Lasivyo ugomvi au unashitukia yupo
mlangoni.” “Hivi sitaweza, James. Bora uendelee naye.” James akashituka
sana.
“Hapana mama.
Tafadhali sana. Mwisho Jema atajikuta alibeba mwenyewe, na kulea
mwenyewe, wote tunakwama kwenye jambo moja tu, Jelini. Acha hii likizo
ya siku saba isiishie kwangu na Colins ambaye nitarudi ofisini, tuendelee naye.
Wewe nipokee tu kwa muda. Tafadhali sana.” “Sasa nafanyaje?” “Wewe usiwe na
wasiwasi. Usipomjibu, atakupigia. Na kwa kuwa anajua upo hapa, ndani ya nusu
saa atakuwa amefika hapa. Wewe endelea na yako.” Wakacheka. Ila akamjibu.
‘Marahaba
Colins. Jelini ameamka vizuri. Na mida ya saa nne atakuja kumuona dada yake na
mtoto.’
Hapohapo simu ikaingia. Colins tena. “Usione kama
nakusumbua mama yangu.” James akacheka kimyakmya huku akiondoka kwa
kunyata. “Bila shida.” “Nilikuwa nikifikiria swala lake
yeye Jelini. Kwa mfano wewe upo hapo kwa Jema. Sasa sijui yeye kule inakuaje?
Maana bado ni mgonjwa hata kama ataonekana ni mzima, lakini bado Jelini
anahitaji msaada.” “Wewe ulikuwa una wazo gani Colins mwanangu?” “Nashukuru
mama. Au labda nije kabisa hapo, tuweke mipango vizuri.” “Hilo naona litakuwa
la msingi.” “Basi sitakawia.” Simu ikakatwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaanika nguo na
kurudi ndani, Jema akampokea na cheko. “Nasikia umekabidhiwa Colins.” “Mbona
ninaye! Hapa yupo njiani anakuja tuweke mipango ya jinsi ya kumjali Jelini.”
James akasikia akaingia akicheka. “Acha masihara mama!” “Anakuja. Amesema baada
ya muda mfupi sana atakua hapa. Maana anavyoona yeye, inaweza kuwa rahisi sana
kumsahau Jelini, tukidhani ni mzima, kumbe ndani ni mgonjwa. Kwa mfano asubuhi
hii mimi nipo hapa, kule amebaki peke yake.” Wakaanza kucheka.
“Jamani Colins! Sasa sijui anataka kuweka
mipango gani?” Jema akaongea akifikiria. “Ndio anakuja tumsikie.” “Na ujue yule
hana asubuhi wala usiku.” “Mwambie mama. Colins hana asubuhi ya kawaida wala
usiku ule wa giza zito. Alfajiri mnaweza kuamshwa na ujumbe wa kujuliwa hali ya
Jelini. Saa 11 asubuhi!” “Haiwezekani James!” “Muulize Jema huyu. Mpaka wakati
mwingine Jema yeye ndio alikuwa akimjibu nakumwambia bado nimelala, labda nilikuwa na
mtoto usiku ndio mtoto amelala, na mimi nimeweza kulala. Na hatujawapigia
nyinyi simu bado, kuulizia hali ya Jelini.” “Na usifikiri hapo ataridhika.
Ataniambia nimwambie James ampigie mara atakapoamka.” Jema akaongeza. Wakazidi
kucheka. Mara kengele mlangoni.
“Haiwezekani!” Mama
Jema hakuamini kama ndio ameshafika. “Wewe usicheze na Colins. Hapo hajalala.”
“Bora wapatane, wengine wapumzike.” Kengele tena. “Nenda kamfungulie bwana
James, atamuamsha mtoto.” James akatoka akicheka.
0 Comments:
Post a Comment