Jelini akacheka tu.
“Au labda hujaelewa! Nazungumzia ile biashara ya mafuta!” “Nakuelewa Ndosi.
Kama na hilo ni moja ya mambo uliyoniitia, tumalize, twende kwenye jingine.”
“Sijaelewa Jelini! Kwamba unakataa ule mchakato wa kituo cha mafuta!?” “Ndiyo.”
Ndosi akabaki akimtizama. “Kwa kuwa tunaheshimiana na najua ulihangaika sana na
mimi kuanzia gari, labda niseme hivi. Wakati nikipokea pesa kutoka kwa mzee
Kasa, nilikuwa kwenye mahusiano naye. Sasa hivi hatuko kwenye mahusiano,
sitataka kupokea tena chochote kutoka kwake.”
“Jelini!” “Kabisa
Ndosi. Wala sijakurupuka. Mimi ndivyo nilivyo. Sipokeagi vitu kutoka kwa kila
mtu. Hata Kasa mwenyewe ananijua. Na kama ungezungumza naye hili, angekwambia usinitafute.”
“Yeye ndiye amesisitiza nikutafute.” “Basi mwambie Jelini hataki tena.
Tafadhali naomba twende kwenye ajenda nyingine, niwahi daladala kabla foleni
hazijaanza.”
“Kampuni ya mzee
inataka kukulipa kwa ajili ya madhara aliyokusababishia mtoto wake. Inakulipa
fidia na mnasainishana kabisa kisheria kwamba mliyamaliza hayo mambo.” Jelini
akashangaa sana. “Wewe unazungumzia nini?!” “Wanakulipa pesa ndefu Jelini!
Ndefu mno. Ilimradi tu mmalizane kwa amani. Na anayekulipa si mzee, ni Kemi
mwenyewe aliyekusababishia ajali.” “Hakika mimi sielewi wewe
unazungumzia nini!” “Wewe hukuanguka kwenye ofisi za Kasa na kupasuka?” “Sasa
kila aliyeanguka analipwa na Kemi!?” Jelini naye akamuuliza na kumuacha
Ndosi kwenye mshangao zaidi.
“Tafadhali twende
kwenye ajenda ingine usianze mambo ambayo mimi siyajui Ndosi. Unataka kuanzisha
kitu ambacho mimi sikijui!” “Kwa hiyo utakua tayari kusaini ili kukiri
kama haya mambo yameisha?” “Yalianza lini!? Mbona mnataka kunichanganya tu.
Tafadhali niache Ndosi. Lasivyo nitaondoka na hutakaa ukanipata tena kwa simu.
Usinianzishie mambo ya ajabu. Sina shida ya pesa za Kasa mimi. Na wala sijawahi
kuwa na shida ya pesa yake. Tafadhali nenda kwenye jambo jingine.” Jelini
akawa amekasirika kabisa mpaka akamshangaza Ndosi.
“Pesa yeyote
iliyokuwa ikiingia kwangu kutoka kwa Kasa ni kwa sababu tulikuwa kwenye
mahusiano naye. Sasahivi sipo kwenye mahusiano na Kasa, napokea pesa zake mimi
kama nani!? Malaya wake?” “Hapana Jelini. Tafadhali usiende mbali. Mimi ni
mjumbe.” “Hapana Ndosi. Inawezekana uliniona na yule mzee ukadhani mimi
nilimpendea pesa. Mimi nilimpenda yeye kama yeye. Sio pesa zake. Hilo
naomba uelewe na UAMINI. Maana baada ya leo, nakuonya uwe mwisho wa kutaka
kunihonga pesa mimi kama malaya. Mimi si malaya.”
“Niliishi naye
nikijua yeye ni mtu mwingine kabisa. Kumbe mzee Kasa hawezi kuwa mtu
niliyedhani ndiye, na ndiye niliyekuwa nikiishi naye, nikimpenda kwa dhati na
ndiye aliyenitambulisha kwako. Nilipomgundua huyo mtu sio yeye na hawezi
kuwa yeye, nikajiweka pembeni. Kwa hiyo kama unazo pesa za Kasa unatafuta mtu
wa kumpa, sio mimi. Mimi sio malaya. Sichuni watu. Sijui kama
umenielewa?” “Basi Jelini. Basi mama.” Jelini akaanza kutulia maana
alishapandisha hasira.
“Basi naomba twende
kwenye swala la mahakamani.” Wakajipanga vizuri, hapo Jelini alikuwa ametulia.
Akajaribu kuuliza maswali yote mpaka akaridhika. Wakakubaliana muda, Jelini
akasimama. “Naomba nikuombe kitu cha mwisho, Jelini.” Akageuka akinyanyua mkoba
wake. “Naomba nikusogeze.” “SITAKI.” “Kwa nini unakataa msaada wa kawaida
kabisa, na jua ni kali sana nje? Hukusema kichwa kinakuuma wewe?” “Ndosi, mimi
sikufahamu kabisa. Siwezi kupokea chochote kutoka kwako. Ila nashukuru kujali.
Asante. Tutakutana hiyo siku ya ijumaa.” “Kwa ajili ya kichwa, unatumia dawa
gani?” Akamuwahi kabla hajatoka.
“Kuna dawa walinipa
tena niliporudi hospitali. Kichwa kilikuwa kikiniuma sana. Zinakaribia kuisha,
ila zikiisha, sitatafuta tena kama hizo walizonipa. Zinanipa usingizi na mimi
nafanya kazi, nakua nachoka. Nafikiria kununua tu dawa za kawaida za maumivu.
Asante kujali Ndosi.” “Unauhakika hutaki kabisa nikusogeze?” “Kabisa. Uwe na
amani kabisa. Jioni njema, acha mimi niwahi.” Jelini akatoka na kurudi kwa
haraka.
“Samahani Ndosi.
Najua hii kesi inamgarimu mzee Kasa. Utakapo zungumza naye, tafadhali mwambie namshukuru
sana. Asante kwa huu msaada.” “Nitamwambia Jelini. Pole kwa matatizo.”
“Nashukuru.” Ndipo akatoka sasa, Ndosi akavuta pumzi kwa nguvu zote.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Nafikiri
umesikia kila kitu mzee wangu. Sina sababu ya kujirudia na kukupotezea muda.”
“Daah!”
Mzee Kasa upande wa pili kwenye simu akasikika kusikitika. Jelini alikuwa
akizungumza na Kasa kupitia Ndosi. Alikuwa kwenye simu muda wote kupitia bluetooth
ndogo alizokuwa amevaa Ndosi masikioni, Jelini asijue.
“Ila kwa
jinsi nilivyomsikiliza, sidhani kama atakuja tena kurudi kuwashitaki kwa ajali
iliyompata, maana amekataa kukiri kabisa kama imesababishwa na binti yako.”
“Lakini natamani hata angepokea hiyo pesa! Daktari aliyemtibu hilo jeraha,
aliniambia wazi kupona kwake haitachukua muda mfupi.” Akaongea Kasa kwa
kusikitika. “Tafadhali utakapomuona hiyo siku ya ijumaa
jaribu kumdodosa kujua ni wapi anafanya kazi.” “Nitajitahidi.” Mzee
akakata simu kwa masikitiko.
Ijumaa Siku Ya Mahakamani.
Japokuwa Naya alikuwa
amejifungua, hata mwezi haujaisha, ilibidi Joshua aliyekua yupo likizo ya
majuma matatu akisaidia mkewe na mama Magesa kulea mapacha ambao hata Naya
mwenyewe hakuwa amejua kama amebeba mapacha. Mmoja hakuonekana kabisa kwenye ultrasound
japo Joshua yeye alijua mkewe atazaa mapacha. Alimwambia mara moja tu,
alipombishia kwa hofu, akamuacha. Na ikawa kila sehemu anaonekana mtoto mmoja
tu, tena wakiume.
Siku Naya na Joshua
wapo chumba cha kujifungua, Naya akidhani amemaliza, anamfurahia mtoto wake wa
kwanza wa kiume, baadaya kama dakika 10 uchungu ukaanza upyaa. Ndipo akapata
kidume cha pili. Alimtizama Joshua kwa hofu, asiamini. “Nilikwambia umebeba mapacha
Naya.” “Mbona sasa hukusisitiza?” Joshua akacheka tu akifurahia double
blessing. Akachukua likizo yake ya mwaka kabisa, ili kulea.
Ila siku hiyo ikabidi
aende kazini mwenyewe ili Jema aende mahakamani kama kumsindikiza mdogo wake na
mama yao. James naye akasema lazima awepo kwa ajili ya hali ya mkewe, ila pia
kama mwanaume wa hiyo familia. Wakampitia Jelini na mama yake, safari ya
Kisutu, mahakamani ikaanza. Kwenye gari kimya, James ndiye dereva.
~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika wakakuta
Ndosi akiwasubiria. Akamsogeza Jelini pembeni. “Mbona unawasiwasi hivyo?”
“Sijui Ndosi! Na sikulala vizuri.” “Kwa nini?” Jelini akaanza kulia taratibu.
“Niambie Jelini.” “Nahisi ni hofu tu ya kukutana na
huyu mwalimu tena. Alikuwa akinifanyia ukatili sana. Sikuwahi kufikiria kama
naweza kuja kumuona tena.” “Sasa nisikilize. Kama tulivyozungumza wakati
ule, leo ndio siku ya kuhakikisha unasaidia kuhakikisha hatakaa akatoka tena
uraiani na kumdhuru mtu mwingine kwa kueleza mahakama yote bila kificho. Na
usiogope ukijua sasahivi hana mamlaka tena juu yako. Yupo kuhitaji rehema
zako.”
Wakati wakizungumza,
akawasogelea msichana mdogo tu, na ujauzito. Akamsalimia Ndosi na Jelini.
Wakamuona anapiga magoti na tumbo lake mbele ya Jelini. Jelini akarudi nyuma
akimshangaa. “Nihurumie mwanamke mwenzio dada.
Msamehe mume wangu. Shedy amebadilika
jamani. Siye yule wa zamani. Sasa hivi ni baba, na tunatarajia mtoto wa pili.
Tafadhali usimuhukumu kwa tabia zake chafu za zamani. Anajuta, na anaomba
msamaha.” Jelini alipigwa na butwaa ni kama alishindwa kupumua kwa muda.
Mama Jema akasogea
kama tembo aliyejeruhiwa. “Kama ulidhani hichi unachokifanya hapa ndio
kitamsaidia, sasa kamwambie Jelini yupo na mama yake. Lazima ataadhibiwa.
Kama si na mahakama, basi mimi mwenyewe, mama yake Jelini. Nitamuadhibu
mpaka paume ndipo nitamsamehe. Lazima aadhibiwe.” “Nihurumie mama, nina watoto wawili. Nitaishije bila
mume?” “Mimi mwenyewe nilikuwa na watoto wawili na nikalea mwenyewe.
Mmoja ndiye huyo mumeo alikuwa akimbaka, na wapili huyu hapa. Nililea
mwenyewe bila mume mpaka wakakua. Kwa hiyo badala ya kupiga hapa magoti, nenda
kaanze kufikiria na kujipanga jinsi ya kulea wanao. Maana mshenzi, mumeo,
hatakaa akatoka jela. Kama anataka msamaha wangu, ni pale
atakapohukumiwa kifungo cha maisha, tena sio kunyongwa, akae ndani kila siku
aamke jela, akumbuke mama Jema hakumzalia yeye mtoto wa kumbaka. Hapo
mwambie ndio nitamsamehe na si vinginevyo. Haya peleka ujumbe.” Akamshika mkono
Jelini na kuondoka naye wakiwa wamejaza watu hapo wakiwasikiliza. Wakamuacha
bado amepiga magoti.
Kila Kazi Na Malipo Yake.
Muda ukafika, wakaingia mahakamani. Shedy
akaletwa na pingu. Jelini alishindwa hata kumuangalia. Akajikuta akilia, Jema
naye akaanza kulia kwa uchungu sana. “Umeharibu maisha ya mwanangu. Na utalipa.”
Mama Jema akaongea kwa jazba. Kilio cha mkewe nacho kikasikika. Ikaanza fujo,
ndipo wakaamuriwa wasimame kwa sababu hakimu anaingia. Wakasimama wakati
akiingia. Kesi ikaanza. Shitaka likasomwa, Jelini akaitwa kizimbani, akaapishwa
na Ndosi akasimama kuanza kumuuliza taratibu.
Jelini akaeleza
mwanzo mpaka mwisho. Ukatili wote aliokuwa akimfanyia. Vile alivyokuwa akimbaka
kama mnyama, kisha kumfukuza kama paka mwizi. Jelini alikuwa akisimulia huku
akilia sana. Mama Jema naye akaanza kulia. Japo ndugu zake walikuja kwa
kuchelewa, wakaongeza nguvu. Wakili wa Jelini alivyomaliza, hakimu akampa
nafasi wakili wa Shedy.
Hakuonekana na
maswali magumu, ila kutaka kujua, kama anachosema ni kweli, ni kwanini
hakuwahi kumwambia mtu yeyote au hata rafiki? “Alisema
atanichinja mimi na mama yangu, pamoja na Jema. Alikuwa akinionea akijua hakuna
wakunitetea. Wakati mwingine alikuwa akinibaka kisha ananipiga hapohapo
chumbani kwake, tena bila kosa huku akinitisha nikitoka pale nikimwambia mtu,
atanipiga zaidi ya vile.”
“Huyu alikuwa
akiishi nyumba ya kupanga, kweli unataka kusema hakuna mpangaji hata mmoja
aliyeshuhudia hayo?” Akauliza wakili wa mshitakiwa Shedy. “Mimi sijui alikuwa akiwaambia nini wapangaji wenzie.
Kwanza alikuwa haniruhusu hata kusimama nje ya mlango wake au hata kusalimia
mtu wa pale ndani. Alikuwa akiniambia nikifika pale nipitilize ndani kwake moja
kwa moja. Nikifika nikikaa kidogo, na yeye anakuja. Akishamaliza kunibaka, ndio
ananifukuza, naondoka.” Vikasikika vilio hapo, kama msibani.
Akaletwa ushahidi wa
vipimo vya hospitalini alivyopimwa Jeremy, na yeye Shedy, vikasomwa na daktari
ambaye naye alilipwa na Kasa na kuomba atokee siku hiyo mahakamani.
Akasema kwa asilimia 100 Jeremy ni mtoto wa Shedy.
Hakuna Msiba Usiokuwa Na Mwenzie.
Lililokusudiwa Kuwa Baya, Mungu Akageuza Kuwa Jema.
Katikati ya kesi
Jelini akaanza kumlilia mama yake kichwa kinamuuma sana kinakaribia kupasuka.
Hapo mama Jema akapaniki hakimu bado akiwa anaendesha kesi. Jema anasimama
kwenda kumsaidia mdogo wake na yeye chupa ya uchungu ikapasuka. Ndio ukawa
mchanganyiko mara mbili. Mama Jema anataka yeye mwenyewe ndiye asaidie
wanae, mtu asiwaguse. Halafu sasa hawezi kujigawa.
James akamtuliza na
kumwambia wote waingie garini waelekee hospitalini. Akakubali kuwa na wanae
wote garini. Msafara wa mama zao nao nyuma Ikabidi Ndosi yeye abakie
mahakamani. Wote wawili wakapokelewa. James, mkewe na mama mkubwa wao upande wa
kujifungulia. Mama Jema na Mode wao wakawa wanasubiria daktari kumsaidia Jelini.
Jelini alipopewa
sehemu ya kujipumzisha, sehemu ya mapokezi, akiwa amepewa huduma ya kwanza
anasinzia, akabakia na shoga yake, mama yake mdogo Mode. Mama Jema akakimbilia
kwa Jema.
Baada ya masaa matatu
mbele, Jema na James na wao wakapata mtoto wao wakiume wa kwanza. “Mtoto
amefanana na baba yake huyu! James una damu kali sana.” James alikuwa na furaha
huyo. Wakwanza kumpigia simu ikawa mama yake kisha baba yake. Ndani ya muda
mfupi sana mama James akawa amefika hapo, hata biashara zake akaweka pembeni. Furaha
ya mjukuu. Ndipo baadaye akili ikamjia James kumwambia Joshua aliyekuwa
amemshikia kazi mkewe kwa siku hiyo.
Maji Yaliyomwagika Mchangani.
Akiwa amepumzika hapo
kitandani sehemu aliyopewa ya kupumzika kwa muda, ila amefunga macho akisinzia akaanza
kupata harufu nzuri sana manukato ya kitajiri. Akagundua ni manukato ya Kasa. Jelini
alishituka mpaka akafungua macho. Akamkuta amesimama pembeni ya kitanda chake. Alikuwa
amependeza. Msafi kama kawaida yake. Kiofisi.
“Pole sana.” Jelini
akabaki akimtizama. Mama yake mdogo alimuaga anakwenda kuangalia mtoto,
angerudi. Maana na yeye alipigiwa simu na dada yake kumtaarifu kuwa Jema
amejifungua na amesharudishwa wodini ambapo ni chumba cha mtu mmoja kama James alivyolipia.
Ndipo akamuacha Jelini apumzike, yeye akaondoka.
“Unajisikiaje?” Akamuuliza
tena kwa kumbembeleza lakini Jelini akafunga macho bila ya kumjibu. Pakatulia kwa
muda.
“Jelini?” Akamsikia akimuita
taratibu. “Nilikosa mpenzi wangu. Nilikosa vibaya sana. Naomba tafuta jinsi ya
kunisamehe. Nimebadili njia zangu zote. Nimebaki na wewe tu.” Jelini akajisikia
uchungu wa ajabu, akaanza kulia. “Tafadhali nipokee tena. Najuta. Sina jinsi
nikakueleza ninavyojuta ukaelewa. Na sikuwa nimepanga kabisa kulala naye siku
ile. Walinilevya, nikaamka pembeni yake, wote tukiwa uchi. Nakiri baada ya
kujikuta nimeamka pembeni yake, baada ya hapo nilifanya mengi kwa kupaniki tu
nikitaka kumridhisha aondoke asirudi tena. Ila sitetei nilichofanya. Nilikosea.
Nimekosa Jelini wangu. Tafadhali nisamehe.” Akaendelea taratibu.
“Nataka nibakie na
wewe tu. Na nakuahidi, ukinipokea tena, sitarudia tena kulala na mwanamke mwingine
yeyote mpaka kifo changu, ila WEWE tu. Na wewe ndio utanizika.” Jelini hakujibu
wala kufungua macho kumtizama tena.
“Na naomba uniamini. Vile
ulivyonikuta sio kwamba ndio maisha yangu. Sio kwamba ni kitu nilikuwa
nikifanya kwa siri au usifikiri ndio maisha niliyokuwa nikiishi nilipokuwa na
wewe. Hapana. Pale nilikosa. Na nasema ukweli, na Mungu ni shahidi. Tokea
tuanzane na wewe sikuwa nimelala na mwanamke mwingine ila wewe tu, mpaka siku
ile.” Akasikia simu yake imeingia, baada ya kuita tena na tena akamsikia akitoka.
Alipojiridhisha ametoka kabisa hapo alipopumzishwa, Jelini akatoka kitandani kama
akimbie. Akachukua vitu vyake vyote, akatoka mbio kwa mama yake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wote wakashangaa
anaingia hapo, ila mama Jema akaanza. “Si ulisema alikuwa amelala?” “Dada,
nilizungumza na Jelini, yeye mwenyewe akaniambia nije kuona mtoto, yeye
anapumzika.” “Sasa wewe unamuona amepumzika hapa? Kilichokushinda kutulia kule
mpaka mwenyewe nije ni nini?” “Hivi wewe Jelini mbona hunitetei shoga yangu,
unakuwa kama hatukukubaliana ulale mimi ndio nije kuona mtoto?” Jelini akaanza
kucheka.
“Mimi hajaniaga,
mwaya mama. Nimejikuta nipo peke yangu, nikasema bora niende kwa mama yangu
mzazi!” “Unapatwa dhambi Jelini wewe!” “Nakutania bwana mamdogo. Kichwa kimepoa
nataka niondoke. Jeremy atarudi shule asikute mtu pale nyumbani.” “Sasa umeruhusiwa?”
Mama yake mdogo akamuuliza. “Kwani walinileta wao?! Hee! Nimekuja kwa ridhaa yangu, naondoka kwa ridhaa
yangu. Mwishoe wataanza kuniongezea madawa yale ya usingizi.” “Haya ongoza njia
tunarudi. Usinitanie mimi.” “Mama jamani!” “Hakika twende. Nikazungumze na huyo
daktari ndio akili itatulia. Jema mama, nitarudi nikishazungumza na huyo daktari
aliyekuwa akimtibu huyu.”
Mama Jema akatoka
naye kurudi alipokuwa amelazwa huku Jelini akiogopa asije kumkuta mzee Kasa. Uzuri
hawakumkuta. Ila akaruhusiwa baada ya kusema anajisikia vizuri na anazo dawa,
hataki madawa mengine. Akasisitizwa mapumziko. Akakumbushwa tena, nje kunaweza
onekana kumepona, lakini ndani ikawa bado.
Ndipo wakarudi kwa
Jema na mtoto. Wakakaa hapo kwa muda, Jelini akarudishwa nyumbani na mama yake
mdogo. Jema akabakishwa hapo kwa ahadi ya pengine kesho yake ataruhusiwa kwa
kuwa yeye na mtoto walikuwa salama.
~~~~~~~~~~~~~~~
Jelini alirudi kwake,
na kulala moja kwa moja. Mama yake mdogo akamsubiria mwanae anaposhushwa na
gari ya shule. Akafanya yote aliyosisitizwa na dada yake juu ya huyo mjukuu.
Ndipo akampa simu apate maagizo kutoka kwa bibi yake. Jeremy aliyelelewa na
bibi, akapata maagizo yake. Simu alipochukua Mode, akaambiwa ruksa kuondoka,
kazi yake imeisha, huyo mtoto anajua chakufanya. Mode akaondoka akimuacha
Jelini amelala, Jeremy mezani akifanya homework zake. Kimya mtoto huyo
asiye na makuu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake alipomfikisha tu mkewe na mtoto
nyumbani akiwa na mama James, mama Jema na Viola, James akarudi ofisini
kuandika ruhusa ya uzazi. Alipofika ofisini akakutana na Colins alishafika
anafanya kazi. “Mbona ulipotea gafla na simu hupokei wewe!?” “Jana ilikuwa siku
ndefu hata sikukumbuka simu. Kuanzia mahakamani…” “Wooo, wooo! Mahakamani tena!”
“Jelini alikuwa na kesi ndio….” Mpaka James anamaliza kusimulia, Colins macho
mekundu kama nyanya.
“Kwamba yule mtoto
alimpata kwa kubakwa!?” Colins akamuuliza kwa kuumia sana. “Na ndio siri ya
unywaji ule wa pombe. Alikuja kusimulia, iliumiza sana. Maana kila mtu alijua
ni mtoto aliyeshindikana, kazi yake ulevi tu, hataki shule. Kumbe
kumbukumbu ya yale aliyokuwa akifanyiwa huku akiteswa, ilikuwa ikimsumbua.
Inabidi alewe ndipo alale. Na shuleni akawa hataki kurudi tena, anaogopa asije
pitia alipopitishwa na huyo mwalimu.” James akamueleza mengi, Colins akazidi
kuumia.
“Ninapokwambia Jelini
anahitaji mwanaume aliyekusudia kuwa naye yeye kama yeye Jelini, basi uelewe ni
kwa sababu hiyo. Ni mdogo, lakini amebeba historia ngumu sana.” “Nilielewa
James. Na nashukuru kwa kuwa naye hata huko mahakamani ambako ulishindwa
kuniambia na mimi.” “Unataka kunilaumu bila sababu. Si mimi niliyekuunganisha
naye tena safari hii ya mwisho lakini ukashindwa wewe mwenyewe?” Colins
akasimama na kuondoka kabisa hapo ofisini kwao.
Maamuzi Magumu.
Akijua wazazi wake
hawapo nyumbani, Colins alitoka hapo na kwenda kutafuta kampuni ya fundi
kabisa. Akarudi na kiongozi wake hapo kwake. Akamzungusha nje ya nyumba yake na
kuyatizama hayo mazingira. “Nataka ujenge ukuta kutenga hii nyumba yangu. Iwe
ndani ya ukuta wake kiasi ya kwamba, nipate geti lake, yenyewe. Isiingiliane na
nyumba nyingine. Utoe sehemu ya kuegesha magari na ijitegemee bustani yake.”
Akawa ameelewa. Akamwambia ampe muda.
“Hicho ndicho kitu
pekee ambacho sina. Ila pesa ipo. Sasa uniambie unaweza au huwezi.” Colins
akauliza kwa ukali. “Ulitaka ikamilike lini?” “Leo.” Akamjibu akimtizama
machoni kumuonyesha uzito wa kazi yake. “Nimeelewa. Ifikapo jioni nitakuwa na
taarifa kamili. Lazima nikamchukue muhandisi wetu, aje apaangalie na yeye,
atengeneze ramani yake. Ndipo nitawasiliana na wewe.” Akaondoka Colins akiwa
ameridhika hilo limekaa sawa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi nyumbani kwa
wazazi. Akamwambia msichana anayesaidia kazi hapo. “Nikusanyie nguo zangu zote.
Safi na chafu, ulete nyumbani, sasahivi.” “Sawa.” Akakubali akiwa na mshangao.
“Na huruhusiwi tena, kufika pale kufanya jambo lolote. Nashukuru kwa kila msaada
uliokuwa ukinipa wewe na Jose, lakini kuanzia sasa, nyinyi mtabaki mkisaidia
wazazi tu. Pale kwangu hamruhusiwi tena kufika. Mwenye shida na mimi atanipata
kwa simu. Na hata chakula ukiwa unapika, usinihesabie tena.” Fau akabaki na
mshangao ila akaondoka. Wakati msichana wa kazi akifanya hivyo na yeye akaanza
kukusanya vitu vyake vyote kama anayehama mji. Akahamishia kila kitu nyumbani
kwake, ndipo akarudi kazini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ni nini anapanga kufanya?
Je, Jelini ameweza kumtoroka Kasa?
Je, Kasa ndio amemalizana na Jelini?
0 Comments:
Post a Comment