Jini Likujualo Halikuli Likakwisha.
Bado ilikuwa mapema
tu, ndio wanafunzi wengine wakijiandaa kwa siku ya shule. Akamkuta Belinda na
Fei ni kama wanamsubiria chumbani kwake. Alikuwa ameshika mizigo aliyotoka nayo
hotelini. Roho ikazidi kumuuma Belinda akijua hiyo yote ni pesa ya Victor maana
ingeingia mfukoni kwake na si kwa Vai. Akawasalimia akiweka mizigo yake kwenye
kabati lake huku akiwatizama vile walivyojawa jazba.
“Kwema?” Akawauliza. “Malaya
wewe! Umeona mimi nafaidi sana kurudi na vitu hosteli, ukaona umchukue mwanaume
wangu. Yule boya wako alikuwa akikurudisha hapa mikono mitupu, ukaona
ujitongozeshe kwa Victor, mpaka akulale wewe, aniache mimi!” “Belinda
umekasirika, unatukana bila sababu.” “Kwani uongo?” Akadakia Fei. “Tafadhali
sana Belinda. Usimuite Bale boya. Hausiki katika hili. Na Victor si mtoto mdogo
wa kushawishika na mtu mgeni kama mimi. Nafikiri anajua analolifanya.” Vile Vai
alivyomalizia tu kusema hivyo, wakamvamia na kuanza kumpiga.
Matusi huku wakimpiga
sana. “Na tutakukomesha na hiyo sura inayokupa wazimu.” Vibao na ngumi
za usoni vikaanza, ndipo ikabidi Vai asalimu amri, apige magoti na kuficha sura.
Akashindwa kujibu mashambulizi. Aliyekuwa akilala naye aliporudi na kukuta hiyo
hali na kushindwa kuamualia, akakimbilia nyumbani kwa matron maana wengine
walikuwa wakishangilia nje ya mlango. Mpaka matron anafika pale, Vai alikuwa
amepokea kipigo cha paka mwizi.
Alikuwa akilia na
kutema damu. Na vile alivyokuwa mweupe, basi uso ulishavilia damu wala si kuwa
mwekundu. Alikuwa akilia matron akashindwa kujua damu zinapotokea, ila akaamuru
achukuliwe apelekwe hapohapo hospitali ya Muhimbili kwa madaktari
wakamuangalie. Vai akatolewa hapo akilia kwa uchungu wa maumivu na
kudhalilishwa. Ilibidi wamvalishe nguo maana alizokuwa nazo walimchania kwa
makusudi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Hapohapo matron
akampigia simu mwalimu wa nidhamu kuripoti tukio zima. Akaambiwa kitaitishwa
kikao cha dharula. Belinda machozi. Akajua mpaka hapo hana chuo. Maana katika
moja ya sheria za chuo chao ilikuwa kupigana au kumpiga mtu ni kosa la nidhamu.
Moja kwa moja akajua hakuna msamaha, ila kuadhibiwa. Zaidi kusimamishwa chuo.
Anarudije kwao,
nakusema amefukuzwa chuo sababu ya kupigania mwanaume wakati nyumbani anaye
mchumba aliyekwisha toa mpaka mahari inasubiriwa tu ndoa! Fei naye machozi.
Ushabiki na kupenda kula vya bure vimemponza. Nia yao ilikuwa kumpiga Vai, kama
kumtia adabu, basi. Hawakujua kama atalia vile na mwenzie kwenda kumuita
matron. Maji yakawa yameshamwagika.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa Vai yeye
akasubiria kumuona daktari. Wakamuangalia vizuri tu, hapakuwa na madhara ya
ndani isipokuwa hayo ya nje yaliyokuwa yakionekana. Akapewa mapumziko ya siku
saba. Akarudi nayo kwa matron ndipo akaambiwa asubiri atatakiwa kwenye kikao
cha walimu hapo chuoni.
Baada ya muda wote
wakaitwa kikaoni. Vai akiwa na ushahidi wake wakutosha, muonekano wake wa
kipigo. Hakuongea sana ila tu kusema walimvamia na kumpiga. Uso ulikuwa
umevilia damu. Kina Belinda walikuwa wakilia sana na kuomba msamaha.
Wakasimamishwa chuo kwa miezi 6 na kutakiwa wakirudi, warudi na wazazi. Kwa
maana nyingine, huo muhula mzima watakosa shule. Ni kama wanarudia mwaka tu.
Ukawa uchungu wa kupitiliza. Wakatakiwa kuondoka chuoni.
Usitukane Wakunga, Na uzazi ungalipo.
Vai akaruhusiwa
kurudi bwenini, lakini akaogopa hao waliofukuzwa chuo wasije mfanyia kitu
kibaya cha kumuaga, na aibu. Akarudi chumbani kwake akachukua vitu vyake muhimu
na kutoka hapo na kwenda kutafuta sehemu, akakaa akiwaza. Anakwenda wapi? Kwao
asingethubutu kurudi. Maana aliahidi kubadilika ndio akarudishwa chuo. Sasa
anarudije na majeraha ya ugomvi wa mwanaume! Hathubutu.
Kwa Bale, aibu.
Aliondoka kwa nguvu zote, asijue Belinda alishamwambia yupo na mwanaume
hotelini. Akabaki amekaa nje tu hapohapo Muhimbili, hajui pakwenda.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa upande wa Belinda
yeye akajifariji, akijua Felix yupo tu. Yeye mtakuja wake. Hata amfanye
nini, alishamdhibiti, hana pakwenda. Japokuwa ni kama hawakuwa kwenye maelewano
naye tokea walipotoka kwenye chakula cha mwisho cha usiku walichokaribishwa na
Victor. Walitoka hapo hotelini na Felix akimfanyia atitude za aina yake.
Huwa wakati wote Felix humbembeleza sana. Si ni nyumba ndogo yake! Basi hupewa mapenzi
zaidi ya mkewe. Basi humfanyia Felix vitimbwi vya namna yake.
Belinda ni mzuri.
Anajiamini. Hata Victor kumkataa alimshangaza kidogo. Ila akajua ni kuongeza tu
nguvu. Na akajua tatizo ni Felix. Akiachana naye, Victor anaweza
mfikiria. Ndio akawa anamfanyia Felix visa, ilimradi tu amuache lakini
naye Felix akawa mtulivu kwake. Hata usiku ule walipotoka hotelini baada ya
kushindwa kula na kina Victor na Vai, bado Felix alimtaka arudi naye kwenye
chumba walichokuwa wamepangisha, wakazungumze, lakini Belinda akamkatalia, tena
kwa kumtusi haswa, akarudi zake hosteli. Hakupokea simu zake wala kujibu jumbe
zake tena. Ndio ukawa mpango wa kumuacha moja kwa moja ili Victor asijemkataa
kwa sababu ya kusema ni shemeji.
Kwa hiyo hapo
wamefukuzwa chuo, akamtuliza Fei. “Usijali. Twende kwangu. Tukajipange vizuri.
Tunaweza kuishi wote hapo kwenye hicho kijinyumba. Si pakubwa. Maana ni chumba
kimoja na sebule, jiko, choo na bafu vipo humohumo ndani. Tena unaweza hata
usirudi kwenu mpaka baada ya hiyo miezi 6, tukaishi wote. Muda ukifika wakurudi
chuo tutatafuta wazazi wa bandia, tutawaleta.” Wakaanza kutiana moyo na
kupambana. Hofu ikaisha.
Ukaanza ushabiki na kushangilia. Wenzao
wanarudi kwa mapumziko, wakawakuta wamejawa furaha, mabingwa wao. Hawajali tena.
Na neno lao ni, “Hatucheki na kima sisi. Ukileta ujinga, tunakuchapa mpaka
unakimbia chuo wewe mwenyewe.” Wakazidi kumsema Vai ambaye ndiye aliyetakiwa
kuwepo hapo, lakini ameondoka kwa kuwaogopa wao.
Fujo zilipozidi,
matron akafika hapo kuwaambia waondoke. Wakakusanya vilivyo vyao. Wakaita
taksii, wakapandisha mizigo yao wakishangilia kwelikweli. Wanachuo wengine
wakiwaangalia tu na wapambe wengine kuwashabikia.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Safari ya Mkwajuni
ikaanza. Mipango mingi. Fei na Belinda wakipokezana maneno kwelikweli humo
ndani ya gari. Cheko limewajaa mpaka wakafikishwa. Wakashushiwa mizigo yao,
wakamlipa mwenye taksii, akaondoka.
Belinda akatoa funguo
zake za nyumba. Kila alipojaribu kufungua, ikawa hapafunguki. Akahangaika wee, mwishoe
akaamua sasa kumpigia simu Felix. “Umenikumbuka
mrembo?” Felix akaanza kwa kebehi. “Mbona
milango haifunguki!?” “Milango gani tena!?” “Acha
ufala Victor! Si hapa Mkwajuni?” Akamsikia anaanza kucheka. “Wewe vipi Victor?!” “Fala kaishiwa. Fala mwanaume suruali,
kashindwa kumiliki nyumba mbili. Kaachia wenye visu vikali wale nyama. Fala
karudi kwa mkewe bwege.” Hayo yote yalikuwa matusi ya Belinda kwa Felix
kila wanapokwaruzana. Lakini huwa hujishusha. Anabembeleza nyumba ndogo.
Anapewa penzi, anatulia. Lakini safari hii bubu kasema!
“Umeelewa
mrembo?” “Sasa kwa nini unaparudisha bila kuniambia? Pengine ningelipia mimi
mwenyewe kwa pesa yangu!” “Wala usianze matusi yako ya nguoni. Bado mwenye nyumba hajapata mtu. Hiyo nyumba nimeirudisha juzi tu
nilipokuwa nikikupigia simu, hupokei.” “Sasa si nilikuwa naumwa!” “Basi maadamu
sasahivi ni mzima, na pesa unayo, nenda kamlipe mwenye nyumba, muandikishane
mkataba mpya.” Akaendelea taratibu tu bila jazba.
“Na hapa kwangu
usipige tena. Maana sasahivi nitakuwa na yule bwege wangu. Na kama unavyomjua,
kanishika masikio, na simu nitampa kabisaa. Sasa sitaki fujo kwa mke wangu.
Hana matusi kama wewe, usimvuruge mama watoto wangu. Ukijichanganya tu na
kunipigia, ujue na mimi nampigia yule mwanamme wako uliyenidanganya ulimuacha,
kumbe maandalizi ya harusi yanaendelea. Nitajitambulisha kwa kina na picha zetu
zote namtumia yeye na baba yako mzazi aliyekula mahari yake.” Belinda akashituka
sana.
“Wanakudanganya
Felix. Mimi yule mwanaume nilisha…” “Hayo hayanihusu tena. Ukimya wako na jeuri
yako ndio vilinifanya kukuchunguza kwa kina. Ndio nikajua wewe tapeli tu.
Unanibana mimi kwa mke wangu, kumbe wewe unafaidi kotekote! Sasa nakuonya.
Ukinianza, ujue nakumaliza Belinda. Habari zako zote ninazo. Na kama ulikuwa
ukimpigia mahesabu Victor, andika maumivu. Hutampata Victor. Labda iwe sio mimi
niliye kutambulisha kwake. Sasa usinijaribu. Ukimtibua tu mke wangu, au
kumtafuta ili kumjaza maneno ya kipuuzi kama kawaida yako, jua mjini na kijijini
kwenu, utapaona pachungu. NISIKUSIKIE. Tafuta soko kwengine. Ila si kwa wanaume
wa hapa Bandari ninakofanya kazi mimi.” Simu ikakatwa. Huo ukawa mwisho wa
Felix. Cha mtu mavi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Vai akabaki akiwaza
bila jibu. Joto la nje na maumivu, vikamshinda. Akamtumia ujumbe Bale. ‘Nimekwama. Nina shida. Naomba msaada wako.’ Akatuma
huo ujumbe na kusubiria. Ilikuwa tayari mida ya saa saba mchana. Akasubiri bila
jibu. Akakata tamaa akijua Bale amemkasirikia. Akabaki akichungulia simu kuona
kama hata amesoma!
Ilipofika saa 8
akaona Bale anampigia. “Kwema?” “Uliniruhusu muda na
wakati wowote nikiwa na shida nikutafute, Bale. Hiyo ahadi bado ipo?” Bale
hakujibu, kukawa na ukimya kidogo. Wasiwasi ukazidi kumuingia. Akajua
ameshanyea kambi. Bale hambabaikii tena kama zamani.
“Kama upo na mambo mengi basi. Lakini nilikuwa nimekwama. Naomba msaada wako.”
“Hamna shida. Kuna ujumbe umeingia sasahivi ndio nilikuwa nikiusoma wakati
ukizungumza. Ulitaka nini?” “Unihifadhi kwa muda wakati nikijiuguza. Siwezi
kurudi nyumbani.” Bale akashituka kidogo.
“Unaumwa
nini?!” “Ni maumivu tu. Nimepewa mapumziko ya siku saba ndipo nirudi chuo. Sina
pakwenda Bale. Vinginevyo nisingekusumbua.” “Hunisumbui hata kidogo. Unajua
kama ingekuwa amri yangu, au kupenda kwangu, ungekuwepo hapa kila siku Vai.” Vai akatulia. “Upo wapi nikufuate?” “Sitaki kukusumbua. Wewe ukiniruhusu,
mimi nitakuja tu mwenyewe.” “Tokea lini imeanza kuwa usumbufu?!” Kimya,
lakini hilo swali likamfariji.
“Eti Vai?
Kuna ishara yeyote nimeshawahi kukuonyesha kuwa unanisumbua?” “Hapana Bale.
Nahisi ni kujishuku tu. Na kuona sistahili tena.” “Si kwangu. Na
nilishakwambia, kidogo nilicho nacho, sitakuwa na shida kugawana na wewe. Hiyo
ni mpaka muda wangu. Usijali. Niambie ulipo nitakufuata.” “Nipo hosteli. Lakini
sio pale. Nimekaa upande wa huku kwenye daladala.” “Basi nakuja. Sitachelewa.”
“Nakushukuru Bale. Asante.” “Usijali.” Bale akatoka kwa haraka kumuwahi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Alishituka sana
kumuona vile alivyo. Ila akajua ni kipigo, hakutaka kumuuliza sana. Maana ni
kweli Vai alijawa fedheha. “Pole sana.” “Asante.” Bale akasubiri alipokaa sawa
kitini na kufunga mkanda, akaondoa gari. “Umekunywa dawa ya maumivu?” “Ndiyo.”
Bale akabaki akijiuliza huku akiumia moyoni. Moja kwa moja akajua ni Victor
ndiye aliyempiga.
Baada ya muda
akamwangalia, akagundua ametulia tu, hajalala. “Nimefurahi umenipigia Vai.
Nilishakuwa na hamu na wewe!” Akashindwa kujibu hata kumtizama, akanyamaza tu.
Bale akaamua kumuacha. Akaendesha mpaka kwake. Akafungua mlango, akamkaribisha.
Akaingia, Bale
akafunga mlango. “Sijaweza kula wala kupika tokea uondoke. Niambie unahamu ya
kula nini, nipike tule.” Vai alishangaa, akamwangalia na kushindwa kujibu.
Alitisha usoni. Akaweka mkoba wake kwenye kochi na kuelekea chooni. Bale
akaelekea jikoni na kuanza kutayarisha nyama ya mifupa kwa ajili ya supu.
Vai akamfuata. “Nikusaidie
nini?” Bale akamtizama akiendelea kukatia kitunguu kwenye yale mafupa na minofu
baadhi. “Natengeneza supu ya harakaharaka. Nachanganya kila kitu humohumo.
Hamna chakusaidia.” Bale akamjibu akiendelea kukatia na kitunguu swaumu vipande
vidogovidogo bila kutwanga. Kimya kwa muda.
Bale akamtizama pale
alipokuwa amesimama kama mgeni na kuendelea na hoho. Kimya. Taratibu kama
anayejiiba, akatafuta mahali pakukaa hapo jikoni. Ni jiko la ndani. Pasafi
sana. Na wawili hao kukaa jikoni pamoja ni kawaida yao. Na mpishi wakati wote
ni Bale. Pakazuka ukimya kwa muda, Bale akifanya yake mpaka akabandika kwenye
jiko la gesi la sahani 4.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Zamani jumbe zangu
ulikuwa ukinijibu kwa haraka, Bale! Leo mpaka nikaingiwa na wasiwasi!
Umenichukia?” Ikawa kama analalamika. “Kwa nini ufikiri hivyo?” “Pengine vile
nilivyoondoka!” “Na kwenda kwa Victor?” Vai alishituka, mpaka mate yakapitia
njia ya hewa. Akaanza kukohoa mfululizo. Akampa maji. Baada ya muda akatulia.
Bale kimya akimtizama.
“Alikuwa na mke na
watoto wawili. Ila wametengana na mkewe.” Ikawa kama anayejitetea. “Kwa hiyo ni
kama vile ulivyokuwa ukitamani? Kupata mwanaume mwenye watoto tayari?” Bale
akamuuliza. Akashindwa kujibu kwa muda kama ambaye anafikiria.
“Ila nafikiri
sikufikiria vizuri. Niliharakisha.” Bale akamtizama akiendelea kusafisha pale
alipokuwa akitumia. “Sidhani kama nitaendelea naye.” Akaongeza. Bale kimya,
hakumjibu.
“Kwa hiyo kumbe ni
kweli umenikasirikia Bale!?” “Kukasirika? Hapana. Kuumia? Ndiyo.
Najiambia kama na mimi pengine ningekuwa na uwezo kama wake, pengine
usingeniacha Vai!” Akaumia sana.
“Mungu wangu ni
shahidi sijamfuata Victor kwa sababu ya hela. Nilimfahamu kupitia Belinda.
Akaniambia alikuwa akinifuatilia muda mrefu ila Belinda alikuwa akimzungusha
akimwambia nipo kwako. Lakini yeye hakukata tamaa maana alijua ni kama Belinda
alikuwa akimbania. Belinda alikuwa akimtaka yeye, mimi sijui. Kwa hiyo ndio akanipiga.”
“Huko hotelini ulipokuwa naye muda wote?” Vai aliishiwa nguvu, hakutegemea.
“Aliyenipiga sio
Victor! Ni Belinda na Fei ndio walinipiga. Belinda akidai nimemchukulia
mwanaume wake. Victor hajanipiga.” “Pole.” “Sasa wewe umejuaje!?” “Alinitaarifu
Belinda.” Vai hakutegemea. “Kwamba Belinda ndiye aliyekutafuta mwenyewe!?”
“Nakuniambia umejifungia hotelini na mume wa mtu.” Vai alitamani kugeuka upepo.
“Kwanza sikuamini! Kwa sababu wewe mwenyewe uliniambia maisha anayoishi Belinda
huyapendi. Hutaki kuwa na mahusiano na mume wa mtu. Sasa kuja
kusikia upo hotelini na mume wa mtu! Nikahisi kuna kudanganywa. Ila sasa ndio
nimeamini uliponiambia wewe mwenyewe.” Vai akawa kama hajamuelewa.
“Si umesema ni kweli ni
mume wa mtu na ana watoto naye wawili?” “Lakini wametengana!” Bale akamtizama
kwa kumsuta. “Mimi ndivyo alivyoniambia.” “Vai! Kwamba wewe unafikiri kuna ndoa
isiyo na matatizo?” Kimya. “Kwamba watu wakitengana kwa matatizo yao ya ndoa
ndio tuseme wameachana? Ruksa kutembea nje ya ndoa!” Kimya. “Wewe unajua ni kwa
muda gani Victor ametengana na mkewe?” “Ameniambia muda mrefu.” “Sasa kama
amekusudia kuendelea na maisha yake, ni kwa nini hajamuacha mkewe ramsi kwa
talaka?” “Amesema sababu ya watoto.” “Kwa hiyo unakubaliana na mimi kuwa bado ipo
ndoa?” Kimya.
Bale akaondoka hapo
jikoni kuelekea chumbani kwake. Akiwa chumbani akamsikia Vai nje ya mlango.
“Unakumbuka nilisema nahisi niliharakisha?” Bale akafungua mlango kumchungulia
akiwa ametoa shati. “Ulikuwa na haraka ya wapi?” “Hata sijui Bale! Sijui
nilipatwa na nini!” “Ulitumia kinga?” Kimya. Bale akashangaa sana. “Kwamba wewe
ulimuamini tu kwa maneno yake, ukalala naye bila hata kinga!?” “Hapo
ndipo nilipokosea Bale. Mimi ni mtu wako, naomba usini…” “Mimi ndivyo
nilivyodhani, mpaka ulipoondoka hapa, ukiniacha bila huruma. Ukijua mimi ni
mpweke Vai! Nakutegemea wewe kwenye kila kitu! Ukaondoka, na kukimbilia kwa
Victor. Inamaana kama isingekuwa kina Belinda kukuumiza inamaana leo
nisingekusikia Vai!”
“Ila ujue niliondoka
kwa sababu nakufikiria wewe Bale.” “Nilikwambia unizalie mtoto?” Kimya. “Eti
Vai?” “Hata nikikwambia hutanielewa Bale. Bora ubakie ukinichukia tu kama itasaidia.”
“Mimi sikuchukii hata kidogo.” Bale akarudi ndani na kufunga mlango. “Ila ni
nini?” “Nimekwambia nimeumia.” Akajibu akiwa ndani. Kisha akafungua mlango.
“Nimeumia kwa kudhani
mimi ni mtu wako, kama ulivyosema. Kumbe sivyo. Unaweza kuondoka hapa
muda na wakati wowote na nisiwe na chakufanya. Na kingine, nimeumia
nikidhani nakufahamu Vai, kumbe sikufahamu. Unaweza ukafanya kinyume na
ulichopinga na ukawa sawa tu. Maana Vai niliyemfahamu mimi, asingeweza
kujifungia na mume wa mtu kwa siku zote hizo na akawa sawa, kiasi cha kutetea.
Vai niliyemfahamu mimi asingeniacha mpweke, hata iweje.” “Niliondoka kwa ajili
yako Bale! Mbona hilo unakataa kuamini?!” “Lipi? Maana mpaka sasa sijui niamini
nini Vai! Sijui.” Akaegemea mlango, Bale akarudi ndani kumalizia kubadili nguo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akatoka akiwa
amebadili nguo. Akiwa na Vai huwa huru kuvaa pensi, mguu wake nusu akiuacha
wazi tu bila shida. Akampita hapo mlangoni na kuelekea jikoni kuongeza sasa
maji yakutoshea supu. “Sasa kama ulitaka nibakie mbona hata hukuning’ang’aniza
nibaki?” Bale akatulia. “Maana kama kweli unayosema ni kweli, mimi ningekuwa
wewe kwanza nisingekuruhusu uondoke, Bale. Lakini wewe mpaka
ulinisindikiza! Na wala hata hukunipigia simu au hata ujumbe kama kawaida yako
ukitaka nilale salama na kujua niliamkaje! Mimi nikajua hunitaki tena hapa
kwako.” “Vai unataka kunitupia lawama mimi bure tu.” Hapo akaanza kulia.
“Ningekua
hapa kwako, nikijua wewe upo sasa ningeendaje kwa Victor?” Bale kimya. “Ulinirudisha chuo na kuniacha Bale, mimi nikiwa
nimekwambia hofu yangu na sababu ya kuondoka. Ila wewe ukasema huko
ninapokwenda mimi ni zaidi ya kumpa mtu watoto na mambo yako mengine
uliyoniambia. Ila hukutaka hata kunibembeleza nibaki! Nikaenda nilikojua
natakiwa.” Akaendela kulia.
“Victor
alinipokea na kuniambia hana neno hata kama sitazaa. Akawa kama amejibu
hofu yangu. Ndio ikawa kila analoniambia mimi naamini tu, nikijua pengine Mungu
amenijibu. Na yeye nilimwambia nimeondoka kwako nikiumia sana, kwa kuwa sizai!” “Naomba utulie Vai.
Utazidi kujiumiza.” Akaondoka hapo kurudi bafuni.
Ikawa zamu ya Bale
kumfuata. Vai ndani chooni, Bale nje ya mlango. “Nahisi siku ile nilipaniki
Vai. Hata Joshua nilimwambia. Nikajua ni katika muendelezo wa Mungu kuniadhibu
ndio maana anakutoa kwangu. Ndio maana nikabakia mnyonge, nisijue chakufanya.”
Kimya. “Njoo nikwambie habari njema.” Baada ya muda kidogo Vai akatoka.
Akamshika mkono mpaka sebuleni, akamfanya akae pembeni yake.
“Unakumbuka
ulinisaidia kumuomba Mungu nipate kazi na kunihimiza kuchukua hatua ya kutafuta?”
Akatingisha kukubali. “Joshua amenitafutia kazi benki. Nilipomuamba awaambie
wasubiri mpaka nipate mguu, akaniambia huo mguu utakutana na baraka
zangu mbele ya safari. Natakiwa nijiandae kwa usahili, sio kusubiria
mguu. Akaniandaa kiakili. Sasa jana nilikwenda kwa hatua ya kwanza ya mtihani
wa kuandika. Ila kwenye kompyuta. Haikuwa mbaya sana. Jioni wakanipigia kunipa
majibu, na kuniambia natakiwa kwa hatua ya pili. Usahili wa mahojiano.”
“Ndio leo asubuhi
nikaenda. Aisee wale watu wanauliza maswali! Uzuri Joshua aliniambia nisiogope
kutumia biashara zangu za nyuma kama kigezo. Akaniambia na Naya alitumia
biashara alizofanya nyuma mpaka alipokuwa kazini, ikamuongezea sana sifa.
Nisiache kuwaambia changamato na jinsi nilivyoweza kupambana nazo nakubakia
kwenye soko kwa muda mrefu. Aisee ilinisaidia sana. Kila swali
walilokuwa wakiniuliza, ilinisaidia kujibu kwa ufasaha. Mwishoe wakaniambia
wanamtu mwingine wanamfanyia usahili, wakimaliza, watanijulisha kujua kama
nimepata nafasi au nijaribu wakati mwingine.”
“Sasa uliponitumia
ujumbe, sikuona. Nilikuwa katikati ya mawasiliano, nikisoma email au barua pepe
zao za ukaribisho na hatua zinayofuata.” “Hongera Bale. Subira imevuta
heri.” “Mambo mawili nataka kukwambia. Moja, sikukujibu kwa haraka kwa
sababu nilikuwa nikisoma jumbe zao na pia nilikuwa katikati ya mawasiliano na
Joshua. Kumjulisha kupata hiyo nafasi ya kazi. Kumbe Joshua alishataarifiwa
kabla yangu kuwa ningepewa ile nafasi. Walivutiwa na mimi tokea kwenye usahili.
Lakini kisheria au kwa kanuni za kampuni ilikuwa lazima na yule mwingine apewe
nafasi ya usahili. Ndio maana sikufikia ujumbe wako kwa wakati. Umeridhika?”
Vai akatabasamu na kunyamaza. Akamuona, akajua ameridhika.
“Chapili. Hiki
alichonifanyia Joshua, angenifanyia muda mrefu sana, lakini nilikosa subira.
Kama wakati ule ningesubiri kama nilivyofanya safari hii, nakwambia
ukweli Vai, si Malon, baba, mdogo wangu wala wale wengineo
niliosababisha vifo vyao wangekuwa wamekufa. Haraka zangu zimenifikisha
hapa nilipo nikiwa mpweke na mlemavu.” Vai akaumia sana.
“Na Naya aliniambia
na kunisihi sana niwe mvumilivu. Nimpe nafasi Joshua. Huwa hafanyi mambo
yake kwa pupa. Lakini sikutaka kumsubiri Joshua. Nilikuwa na haraka.
Nafikiri pia kutaka kushindana na baba, kulishanipa laana tokea yupo hai.
Nikakimbilia kwa Malon, mengine yote ni historia.”
“Ndio maana wakati
ule uliponishauri nijaribu kutafuta kazi, nilikuwa nikisita sana.”
“Nilikuona. Na ni kama uliingiwa hofu sana, mimi nikashangaa, ndio maana ukaona
niliacha kukuhimiza kutafuta kazi. Ulikuwa ukibadilika mpaka sura!” “Joshua ni
mtu mkubwa sana. Anafahamiana au kuzungukwa na watu waliofanikiwa sana hapa
nchini. Ni kiasi cha kunyanyua simu tu kama hivi, nikapewa
nafasi. Sasa ule ukimya wote huku akinilisha kama mtoto mdogo, nikajua Naya
yupo sahihi. Anataka kunichunguza, ili akiniweka mahali, nisiharibu,
akalaumiwa yeye. Na nakwambia ukweli Vai, angemtafutia kazi Bale
wa wakati ule, ningeharibu vibaya sana.”
“Nilijawa kiburi mno.
Lakini sasahivi maisha yamenifundisha, hata yeye leo ameniambia nipo tayari kwa
ofisi yeyote. Ameniambia anashuhudiwa moyoni, hakuna ofisi nitapewa,
nitashindwa kuitumia ipasavyo.” “Kweli Bale!?” “Hakika Vai. Mpaka machozi
yalinitoka kumsikia Joshua akisema hivyo. Na usifikiri amenitafutia nafasi
ndogo au hizi benki za kawaida! Kubwa na pesa yao ni kubwa mno. Marupurupu
kibao. Ukipona macho nitakupa usome uone Mungu alivyotujibu.” “Hongera Bale.”
“Asante. Acha nikaangalie supu.” Akasimama, na yeye akamfuata.
Akamuona anaongeza
maji na kuchukua simu yake. “Unaanza lini kazi?” Akamuangalia na kumuona
anaandika. Akatulia akimsubiria. Akamaliza na kuweka simu pembeni. “Nilikuwa
nikimtaarifu Joshua kuwa umerudi.” Vai alishituka. “Bale!” “Sina mtu mwingine
mbali na wewe na yeye, Vai. Uliniacha. Ukaondoka. Nilikuwa siwezi
hata kutoka kitandani.” “Bale!” “Sikudanganyi Vai. Hii nyama kama
ningekuonyesha kabla sijaiweka jikoni, ungekumbuka tulinunua wote. Sijapika
wala kula tokea uondoke. Yaani jana na leo imenibidi ninywe chai ya rangi ili
niweze kufikiria.”
“Uliondoka gafla
tukiwa na wakati mzuri mno Vai. Amani na utulivu wa namna yake.
Hatukuwahi kugombana hata mara moja! Halafu ukaondoka gafla tu!Nilikuwa sijui
chakufanya! Kutoka kwenye kuniokota, ukawa mtu wangu. Mchana hadi mchana tupo
wote. Gafla unaondoka, halafu naambiwa yupo Victor amefanikiwa kukufungia
hotelini. Na wewe umetulia naye! Kweli wewe unafikiri ningejisikiaje?”
Vai akatulia.
Ukweli Mchungu.
“Nenda akajipumzishe
kwenye kochi. Supu ikiwa tayari nitakuletea.” “Nataka tukae wote.” Bale
akacheka akimtizama. “Na mimi nilikumisi Bale. Usifikiri ndio nilikuwa
nafurahia kuwa mbali na wewe. Mpaka
nilikuwa nikitamani Victor ndio angekuwa wewe!” Bale akanyamaza.
“Mimi sio muongo
Bale. Ila ni binadamu. Nimekosea. Sijakudanganya. Ila nimekosa.
Nikiomba tuanze tena urafiki wetu utakubali?” “Kwa makubaliano yepi?” “Yeyote
yale. Ila safari hii sitakimbilia tena mume wa mtu. Nitatulia kabisa.” “Na ukajiangalie
afya yako.” Hapo Vai akapoa.
“Mwenzio haraka
zimenipa kilema cha maisha. Ila wewe nakuombea usipate gonjwa la kudumu.”
“Nimeingiwa hofu Bale!” “Lazima. Huyu Victor humfahamu. Umesikia na kuelewa kile
ulichotaka kukisikia wewe. Ukapime. Na kama hujaathirika, iwe fundisho
Vai. Tafadhali jifunze. Na hapa nitakwambia ukweli.” “Sio usubiri nipone kwanza!”
“Ukiondoka kabla hujapona! Maana wewe hutabiriki.” “Bale! Si nimesema siondoki
tena?”
“Hapana Vai.
Tafadhali nisikilize. Unaonekana wewe swala la kinga unapuuzia sana Vai.
Kwa hapo ulipo, ningetegemea ungekuwa makini sana na kinga. Umekuwa ukishika
mimba hovyo tokea mdogo.” Vai hakutegemea! Akamtizama kwa kumshangaa kwa
uchungu, na kunyamaza akiangalia chini. “Mimi nakwambia ukweli Vai, na usichukie.
Madhara ya kutokutumia kinga, ukapata mimba ambazo hukuwa ukipanga,
kasoro moja nafikiri! Ambayo kama nitakumbuka sawasawa ilikuwa ya yule
aliyekuwa mume wa mtu.” “Sikuwa nimejua! Yeye alinidanganya.” Akajitetea.
“Sawasawa. Lakini
ukiwa hata humfahamu vizuri! Si mchumba wala mume! Kama tu huyu Victor
uliyekuwa ukimtetea hapa. Ukajiachia mpaka kushika mimba iliyokuachia
majuto mpaka leo. Hofu na huzuni inayokutesa mpaka sasa. Sikutarajia
kama na kwa Victor naye ungekimbilia kitandani bila KINGA!” Vai akamwangalia
kwa kuumia sana.
“Acha mimi niwe
Joshua wako. Usipokubali makosa. Ukajifunza kwayo. Hakika hutatoka hapo Vai, na
madhara yatakayozidi kukupata mbeleni ni makubwa zaidi ya unavyofikiria
hata sasa nikizungumza hapa na wewe. Mwenzio Joshua alikuwa akinipa ukweli
uliokuwa msaada kwangu japo ulikuwa ukiniuma sana. Nilikubali makosa, nikatubia
mbele ya Mungu na kwa niliyeweza kumfikia. Joshua. Ndipo nikaanza kujifunza
jinsi yakusubiri. Wewe ni shahidi. Sijakimbia japo kwangu ilikuwa ngumu
mno mwanzoni. Mpaka baadaye na wewe ukaja. Ukaongeza tabia nyingene ambazo hata
sikuwa nazo! Ikafanyika rahisi KUSUBIRI. Nimesimama hapahapa mpaka majibu yangu
yamenikuta. Barua yangu aliyotumwa malaika na Mungu aniletee, imenikuta
pale nilipokuwa nikimsubiria Mungu wangu. Leo Mungu amenipa kazi nzuri
sana. Na amenirudishia WEWE. Na yote hayo ni Joshua.”
“Alinipigia simu
nikiwa siwezi hata kutoka kitandani, kwa uchungu wa kuniacha.
Akazungumza sana na mimi na kuniambia sina chakupoteza kwenye maombi. Nikiwa
nina hofu. Maana ni kama Belinda aliniambia Victor anayo pesa. Aina ya hoteli
mliyokuwepo, hata mimi na wewe hatujawahi kufika huko! Nikajihisi kipanzi
mbele yake. Lakini nikawa kama alichonifundisha Joshua. Nikamwambia Mungu mpaka
hofu yangu. Na nikamwambia sijui chakufanya. Naogopa. Nimebaki peke
yangu. Nahisi akanihurumia. Ndio amenipa kazi na kukurudisha na wewe.” “Sasa unajuaje kama Mungu ndiye amenirudisha na si
shetani?”
“Kwenye bibilia kitabu
cha Yakobo 1:17 inasema hivi, ‘Kila kitolewacho kilicho
chema na kilicho kamili, hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga,
ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka.’ Shetani
hawezi kutoa kitu kizuri kama wewe Vai. Akipate wapi!?” Vai akaumia
sana. Akaondoka hapo kurudi sebuleni, akilia. Bale akabaki jikoni akimalizia
kupika. Vai akalia mpaka akapitiwa na usingizi kwenye kochi.
Atafutaye Hachoki.
Ilikuwa mida ya
jioni, Jelini akiwa dukani, simu ikaingia. Akaitizama, alikuwa mwanasheria wa
Kasa, akajua tu ametumwa na mzee. Akapokea. “Halo.”
Akaitika Jelini. “Mbona umepotea Jelini bwana! Nakusaka
kama shilingi ya mkoloni!” “Nipo. Kichwa kilikuwa kikiniuma sana, nikaamua
kupumzika kwanza. Kwema?” “Pole sana. Unaendeleaje lakini?” “Sio mbaya sana.
Nashukuru.” “Nimekwama mambo kama mawili matatu, nahitaji kukuona ili tuweke
muongozo.” “Hatuwezi kuzungumza tu kwenye simu? Mimi siku hizi nina kazi. Ndio
nimeanza tu, sitaki kuanza kumangamanga mida ya kazi.” Akasikia kimya.
“Ndosi?”
“Nipo Jelini. Unanafasi muda gani naweza kutuma dereva akaja kukuchukua, na
kukurudisha.”
Akajua wazi anayezungumza hapo ni Kasa, ila hakujua kama yupo kwenye simu au
yupo naye hapo. “Shida si usafiri, ila muda. Niambie ni
nini unanitafutia kwanza ili nipime kama ni jambo naweza kuahirisha mambo
mengine ili nije.” “Muda wa ile kesi ya yule mwalimu umefika. Ndio maana
nilikuwa nikikutafuta sana.” Moyo wa Jelini ukashituka kama kumeanguka
chuma sakafuni.
“Jelini?”
“Nipo. Natakiwa kufanya nini?” “Ni maandalizi tu ya jinsi ya kujieleza
mahakamani.” “Lini?” “Ijumaa hii, ndio maana nilikuwa nikikutafuta sana.
Lasivyo kesi itaahirishwa tena au kufutwa kabisa endapo hutatokea siku ya
mahakamani.” “Kesho ni siku nzuri kwako?” Jelini akauliza. “Ulitaka uje saa ngapi? Asubuhi nina kesi mahakamani mpaka
mchana ndio nitakuwa nimerudi ofisini.” “Basi nitakuwepo hapo mida ya saa nane
mchana.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usiku alipotoka na
kurudi nyumbani akamfuata mama yake na kumueleza. “Nenda, mshenzi yule
akahukumiwe kihalali.” Mama yake akamtia moyo. Jelini akarudi chumbani kwake
kujiandaa na kesho yake akijua anakwenda ofisi za maana. Akatafuta nguo za
kujiwakilisha ipasavyo, ndipo akalala.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wapi Mizani Italemea?
Jelini na yeye mlango mwingine umefunguka kama Vai. Wakati Colins analemewa na familia, Kasa anarudi kwa mlango wa nyuma.
Huku kwa Vai naye, ni Victor au Bale ambaye hajasema chochote juu ya mapenzi, wakati Victor yeye hana shida ya familia. Tayari yupo na familia yake anachohitaji starehe tu.
Nini kitaendelea?
Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment