Wakati akifurahia
penzi hotelini, kwa Bale kulikuwa kunawaka moto tokea jana yake Belinda
alipomtumia ujumbe kuwa Vai amejifungia hotelini na mwanaume. Tena akaongezea
kuwa ni mume wa mtu, ametelekeza familia kwa ajili yake Vai. Kwamba Vai anatesa
familia ya Victor kwa makusudi. Zilikuwa taarifa nzito kuliko kipindi anaambiwa
kifo cha baba. Zikakaribia taarifa za kifo cha mama yake.
Kwamba Vai yupo na
mwanaume mwingine! Ikamtesa sana Bale. Tarehe 3 kuamkia 4 ukawa ni usiku wa
mkesha akijishangaa anavyoumia kana kwamba Vai ni mkewe, kumbe walishaagana na
akamrudisha chuoni kabisa. Ikamuua. Siku ya tarehe nne ilimkuta kitandani
amekosa hata sababu ya kutoka hapo. Akabaki ametulia tu hapo kitandani.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Kilichomkera Belinda
zaidi ni majibu ya Bale pale aliposoma ujumbe wake. ‘Vai ni mtu mzima, mwenye akili timamu. Yupo huru kuchagua
kama mimi na wewe. Nakushauri usiwe na wasiwasi naye, anajua anachokifanya.’
Hayo ndio yakawa majibu ya Bale kwa Belinda, baada ya kusoma ujumbe wake mrefu sana wakumchafua Vai.
Akabaki sasa
kumchafua Vai hapo hostelini kwao akilia kuibiwa mwanaume na Vai
aliyekaribishwa chakula cha usiku na kina Victor, tena kiungwana tu. Kwamba
hawakuwa hata na nia ya kutoka naye. Ila walifanya uungwana kama kumshukuru kwa
kumsaidia kubeba mizigo yake, yeye akakubali na kujitengeneza kwa kujipania
kama aliyetaka kumtaga mwanaume wake!
“Bwana Vai ni mshenzi yule mwanamke! Msiwahi
kumsogeza karibu ya mwanaume wako! Mambo aliyoyafanya huko baaada ya kulewa, hamuwezi amini kama ni yeye! Alimng’ang’ania Victor mpaka akaenda
kulala naye!” Akaendelea kumchafua.
“Sasa si na Felix
alikuwepo!?” Mmoja ya anayeyafahamu mahusiano yao akauliza. “Kwani nimeanza
kuwapanga leo, na wewe? Tokea mwezi wa 11, wote nilikuwa nao. Niliwapanga bila
shida mpaka Vai alipomchukua mwanaume wangu.” Akaendelea kulalamika mengi mpaka
akapata watu upande wake. Akaonyesha uthibitisho wa pesa alizokuwa akirushiwa
na Victor pamoja na Felix kwa muda mrefu tu. Mpaka wote wakaamini ni kweli Vai
ameingilia mipango yake. Alikuwa akivuna kotekote na yote kumuendea sawa.
Wakamuhurumia sana
Belinda. “Na tutamkomesha. Aache ushenzi wa kuibia watu mabwana zao.”
Likawa azimio la Belinda na shoga yake Fei, wanalala chumba kimoja. Hawa mshabiki akichochea maana Belinda alikuwa akileta chakula, anakula naye. Maana
wakati Belinda akiwa kwa Felix, Hawa anashinda na Fei chumbani kwao kwenye vitu
vizuri. Shoga.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Alibaki amejilaza
hapo mpaka majira ya saa nne asubuhi alipoona simu ya Joshua. Akaipokea kwa
swali, bila salamu. “Hivi wewe ulijuaje kama Naya ni
mkeo?” Joshua akatulia kidogo. “Joshua?” Akaita
na kuitizama simu kuhakikisha alipokea kabla hajazungumza. “Mzima lakini?” “Nataka kujua.” “Niliwasimulia ilivyokuwa
Bale. Na kwangu ilikuwa rahisi kupokea hisia kwake kwa sababu sikuwa
nimejizoeza au nisema sikuwa nafungua mlango wa mapenzi hovyo. Haikuwahi au
sikuwahi kuruhusu mambo ya wanawake kuwa udhaifu wangu na nahisi ndio maana
kwangu ilikuwa rahisi nilipoletewa Naya. Niliomba Mungu anipe mke.
Aliponionyesha ni yeye. Nikampokea kama zawadi iliyofungwa, na sikujua kilichokuwa
kimefungwa ndani.”
“Nikaanza
kufungua nikiwa nimeshapokea na kushukuru. Nikiamini kilichowekwa
ndani, Mungu wangu amepima uwezo wangu, ameniamini na Naya. Na kwa kuwa najua
Mungu anajua madhaifu yangu, nilijua hataniacha nikashindwa. Nina
uongozi wa Roho mtakatifu. Kwa hiyo kuanzia nimempokea, najua na wewe
unakumbuka mwanzo wetu. Haikuwa rahisi na nilimkuta yupo Malon, lakini kwa kuwa
nilijua ni WANGU. Mungu amenipa, nilijua hatakamilika bila mimi
na mimi hivyohivyo. Ndio maana sikutulia mpaka nilipohakikisha amekuwa wangu,
na yupo nyumbani kwetu.”
“Na ni
kwambie kabisa Bale, hangaika yangu yote, pesa yote na muda niliotumia,
nikimtafuta Naya awe wangu kama Mungu alivyonipa kwa imani tu, garama yake
nzima, hafikii hata chembe ya aina ya ndoa tuliyo nayo na Naya. Imekua yote
yale tuliyopitia ni kwa ajili ya kututengenezea maisha mazuri tuliyo nayo sasa.
Kila nikijifikiria na kujiuliza kama ningekata tu tamaa wakati ule, nikamuachia
Malon. Pengine kwa akili zangu ningeoa mwanamke mwingine. Lakini
nisingekuwa na aina hii ya ndoa au niseme maisha tuliyo nayo na Naya.” Wakatulia kidogo.
“Sijui kama
umenielewa?” “Nafikiri, japo nina maswali, sijui niulizaje?” Joshua akatulia
akimpa nafasi. “Unanafasi?” “Kidogo. Unaweza kuzungumza
tu.” “Na mimi katika mabaya yangu yote kwenye maisha. Mpaka najishangaa,
maswala ya wanawake shetani hakuwahi kabisa kupata nafasi kwangu. Linapofika
swala la mwanamke, hata kipindi navuta bangi, halijawahi kuwa tatizo nashindwa
kulishinda. Tamaa hovyo za wanawake sina. Na pia sijawahi kujiruhusu
kuwa mtumwa wa mapenzi. Nafikiri pia ilichangiwa na ndoa ya wazazi wangu. Ni
kama niliingiwa na hali ya kutotaka kurudia kosa. Sikutaka kuharakisha kwenye
mahusiano ya kimapenzi.”
“Lakini nilipata
msichana. Hatukuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi. Urafiki tu. Lakini Joshua,
yule msichana ni kinyume na mimi kabisa! Nikimaanisha, kila upungufu
unaouona kwangu, yeye ni kinyume. Anaridhika na SASAHIVI, wala si leo tu.
Anafurahia ule wakati mlio nao wakati ule bila kuruhusu hofu ya baadaye
iibe ile furaha ya wakati ule. Halafu mzuri sana.” Joshua akacheka.
“Yaani
ukimpa maji ya kunywa, inakuwa kama sijui umempa kinywaji cha namna gani vile! Halafu
mzuri haswa.”
Joshua akatulia akimsikiliza. “Wakati tunao kuwa nao
mimi na Vai, popote tunapokuwepo, hata kama ni pa hadhi ya chini sana,
utafikiri ni watu ambao mambo yetu yote yapo safi sana. Kumbe yeye ni
mwanafunzi tu, mimi natunzwa na wewe! Kwamba si kwamba hata tunajua kesho yetu
itakuaje! Lakini hatakagi tukose raha wakati huo kwa ajili ya kesho. Analeta
hali ya amani na utulivu mkubwa sana, kinyume hata na mazingira ya nilipokulia kwetu!
Kile kidogo kilichokuwa kikilalamikiwa nyumbani kwetu, yeye Vai atakipa
thamani mpaka unapatwa na hali ya kukitazama kitu kilekile kwa jicho la
tofauti! Halafu sasa Mungu akampa uzuri wa aina yake.” Joshua akagundua
swala la uzuri wake linarudiwa sana.
“Huwezi
kujificha kwake, kwa kuwa hana kuhukumu. Unajisikia upo salama hata kutubu
mambo mabaya unayoogopa hata mtu asifikiri nina uwezo wa kuyafanya! Na bado
atakusikiliza, halafu anabaki kukutizama kama mtu wa kawaida akikukumbusha
jinsi Mungu anavyosamehe. Anautulivu wa aina yake, uzuri uliochanganyika
na ucheshi. Mweupe mnoo. Mweupe haswa. Ule weupe wa uzuri. Ni mzuri.” Joshua akacheka na
kubaki kusikiliza kujua tatizo.
“Na mimi
nikamfahamu kwa undani, nikagundua hana uwezo wa kuzaa. Aliharibu mimba
nyingi sana akiwa anakua. Tukaendelea na mahusiano ya kawaida ila nafikiri kuna
tulipopitiliza, hisia zikawa tofauti lakini kwa sababu nilijua yupo tu,
sikutaka kuharakisha kumwambia ninachojisikia. Tukaendelea tu.”
“Sasa juzi
hapa aliniuliza swali lililonifanya kujibu bila kufikiria, akaondoka. Aisee
hapa panatisha bila Vai!” “Kwani mlikuwa mkiishi wote!?” Joshua akauliza. “Aisee ni kama nilikuwa nikiishi naye, ila si kimapenzi.
Aliondoa upweke wote. Kuna wakati mpaka nikajua Mungu amemleta kunifariji na
kuniambia amenisamehe! Maana jinsi nilivyokutana naye pia ingekuwa mtu mwingine
asingekuwa na mimi. Nilimfanyia ujeuri, nikiwa nimeanguka pale hospitali ya
MOI. Akaniokota na kunisaidia.” Akamsimulia mwanzo wake na Vai kwa ufupu
mpaka mazungumzo yao ya mwisho, kisha Vai kuondoka hapo na ujumbe aliopata
kutoka kwa Belinda shoga yake kipenzi Vai.
“Nashindwa
kulala, Joshua. Chakula ndio kimenishinda kabisa tokea aondoke hapa na rafiki
yake ndio amenichanganya zaidi. Vai amepata mwanaume ambaye amemwambia kile
nilichoshindwa kumwambia mimi, nikijua ninao muda zaidi au simstahili. Nipo
kama mgonjwa! Mpaka mazoezi naogopa kufanya nisije nikajiumiza, kwa njaa na
msongo wa mawazo! Nifanyaje?” Bale akauliza akisikika kukata tamaa kabisa.
“Wewe
unataka nini? Maana hilo ndilo la msingi.” “Bila kukupotezea muda zaidi, NAMTAKA
Vai. Sijawahi kujisikia hivi nilivyo kwa mwanamke yeyote yule hapa duniani, Vai
ndio wa kwanza. Sijali hata kama hatutapata watoto, ninachojua namtaka
yeye. Maana hata wazazi wangu walikuwa na watoto wajinsia zote, lakini sijawahi
hata kuwaona wakiwa na wakati mzuri kama niliokwisha kuwa nao mimi na Vai.
Hakuna kilicholeta maana kwao, kama Vai alivyoleta maana kwenye maisha yangu
yaliyokwisha kuwa makiwa. Namtaka Vai. Ila najihisi nimechelewa.”
“Hilo la watoto ndio lilikuwa
swali langu la pili. Maana ni bora wewe umejua mapema kuwa hazai. Mimi nilimuoa
Naya, nikampokea kama alivyo, nikajua mengine Mungu atayafanya kwa wakati wake.
Nilijiambia maadamu ni wangu, na kujithibitishia kuwa Mungu amenipa
mimi, hakuna kitu kitasimama katikati yetu. Nitapambana kwa nguvu zangu zote
bila kukata tamaa, na msaada wa Mungu, mpaka awe wangu. Mengine sikutaka kabisa
kujisumbua nayo. Maana huwa namjua Mungu wangu. Ana jinsi yake yakunipa vitu.
Si rahisi aisee, lakini hajawahi kunipa vitu vinyonge.” “Unamaanisha nini?”
“Wewe si
unajua kuna watu wanaomba tu, Mungu anawapa vitu vikamilifu? Kama ni mwanamke,
basi anakuwa binti mzuri, aliyetulia. Hata safari yao yakufunga ndoa ni kawaida
kabisa. Hamna shida. Wanafunga ndoa na maisha yanaendelea bila shida mpaka
watoto?” “Ndio!”
Bale akaitika na kutaka aendelee.
“Au wengine
wanaomba kazi. Unakuta anapewa kirahisi tu. Tena anapewa sehemu nzuri, ofisi
kabisa, kazi zinaanza bila shida na mshahara unaingia bila tatizo. Si ndivyo?”
“Ndio!” “Basi kwangu si wakati wote huwa inakuwa kama hivyo. Mungu huwa ananipa
vitu nakunijaribu haswa. Kama ambaye anayetaka kujua kama anaweza
kuniamini na hicho kitu! Ikishakuwa hivyo, najua anataka kunipa kitu kikubwa,
uwezo sina, ndio ananitengeneza. Aisee hapo hutanitoa Bale. Hata kwa risasi
hutanitisha. Ilimradi nijue ni changu na Mungu anataka kunipa mimi!
Aisee nitapambana mpaka Mungu wangu aridhike, anikabidhi sasa
kama wengine, ndio natulia, ila si kuzembea.”
“Nilikuona
kwa Naya! Kumbe ndio maana umefanikiwa sana Joshua!” “Hutaniyumbisha kwenye
ninalojua Mungu amekusudia kunipa mimi, Bale. Hutanitisha, hutaniogopesha.
Maana hapo najua Mungu, ambaye ni Baba yangu, yupo kazini. Kila silaha
itakayoinuka kinyume yangu najua kwa hakika haitafanikiwa, ni mimi tu
kusimama imara, anichonge mpaka nifae kuweza kuishi na hiyo baraka anayotala
kunipa. Najua natengenezwa tabia ambayo haipo ndani yangu. Nakwambia, hakuna
mwanadamu atasimama katikati yangu na kusudi la Mungu kwangu, endapo Mungu
mwenyewe akiamua kufanya kazi kupitia mimi. Kwa sababu wakati mwingine
anapigana huko kimyakimya, ananiletea tu ushindi mikononi. Hapo najua
anachonipa, anajua naweza kuishi nacho bila shida. Nipo tayari nacho.”
“Na kingine
Bale. Kama nikajua kwa hakika ni Mungu ndiye anayenipa hicho kitu. Hiyo zawadi.
Hata kama imefungwa vibaya, au imefungwa kwa ustadi wa hali ya juu na zile
karatasi za zawadi na riboni kabisa, maadamu inatoka kwa Mungu wangu, na
ananipa mimi, sinaga maswali na kuchunguzachunguza ndani nikitafuta kasoro.
Huwa napokea, na kujiambia mengine yoooote, nitajua mbele ya safari. Napokea,
na kutunza kwa uaminifu sana, kumuhakikishia Mungu, nimepokea kwa
shukurani na nitatunza. Basi. Mengine napambana nayo mbele ya safari.”
“Aisee kumbe
afadhali tumezungumza! Maana nilikuwa na hali mbaya!” “Usiache kunipigia kila
unaponihitaji. Nisipopokea, ujue nitarudisha nikipata nafasi. Na usiache
kumshirikisha Mungu.” “Nahisi bado ninahofu na Mungu. Nahisi bado sistahili
mambo fulanifulani ndio maana nilijiambia hata kuondoka kwa Vai hapa, ni yeye
Mungu alimtoa kwangu. Nikakubali aondoke nikijua ni adhabu yangu bado
inaendelea.”
“Sasa hapo sikuwa
nikijua kama ni kwa wema au ubaya!” “Mungu si wa visasi Bale. Kwanza hawezi.
Akikutizama wewe, anakumbuka kazi ya msalaba. Umesamehewa na kununuliwa
kwa damu ya thamani sana. Kuna garama utalipa, kwa uliyokosea nyuma, kama
ulivyoharibu mahusiano yako na Naya, pamoja na ndugu zenu. Ukiwa unao jisikia ni
kwa sababu ya makosa ya nyuma. Lakini haitokani na adhabu ya Mungu. Mungu
hakuadhibu. Lakini hata kama amekusamehe, hawezi kurudisha familia yako kama
ilivyokuwa zamani. Inamaana utabaki na madhara uliyosababisha nyuma, lakini
haimaanishi kila unapojisikia ukiwa ni kwa sababu Mungu anakuadhibu! Hapana. Ni
kwasababu familia yako haipo tena. Ni hilo tu. Usikubali huo uongo. Na katika
hiyo hali, lazima ujifunze kuishi kama uliye samehewa, ila unayewajibika na
kosa lako.”
“Sijui
jinsi ya kuishi hivyo Joshua! Ndio namuomba Mungu anisaidie kila siku. Naamini
siku moja Naya atakuja kunisamehe. Angalau niwe nimempata yeye.” “Hilo ndilo la
msingi. Hutapoteza kwenye maombi. Na hata yale unayoyaona sasahivi hayawezekaniki,
muombe Mungu. Omba hekima ya jinsi ya kuenenda. Maana hutaomba tu na kusubiri. Kwenye
kuwajibika, omba uongozi wa Mungu, kisha chukua hatua.” Akamuombea Bale na
Vai. Akaomba kusudi la Mungu litimie kwao. Wakaagana.
Tarehe 5.
Asubuhi hiyo Colins
akaamka mapema kuwahi kazini ila akapitia hospitalini kwanza kitu
kilichomfurahisha hata baba yake. Alimkuta mama yale akimsaidia kumsafisha. Kwa
hiyo hakukaa hata dakika 10, akaondoka. Akaingia kazini hata saa mbili haikuwa
imefika. James hakuwa ameingia. Akaanza kucheza game, James anaingia,
akamtizama tu na kurudisha macho kwenye kompyuta yake akiendelea kucheza.
James akamuwekea
kimfuko mezani. “Mzigo wako huu kutoka kwa Jelini, nimepewa na Jema. Sina
habari zake zaidi.” Colins akapokea, kufungua ndani, akakutana na simu yake
aliyokuwa amempa Jelini. Akabaki akiitizama. Chini kulikuwa na bahasha ndago,
imefungwa kabisa. Akaifungua.
Colins,
nashukuru sana kwa msaada wa simu. Ila nimeamua nisiuze tena ile simu yangu
nyingine. Kwa hiyo kwa sasa sina uhitaji tena wa simu. Naona ubakie nayo tu,
kunaweza tokea uhitaji kwengine, tena muhimu, ikapata matumizi kuliko kuweka tu
kitu cha thamani kama hicho. Pia nakushukuru sana kwa kuwa na mimi kipindi
nilichohitaji faraja. Mungu akulipe Colins. Umenisaidia kunijenga. Isingekuwa
wewe ningepoteza dira kabisa. Lakini umenikumbusha mimi ninaweza kuamua
kitu na nikafanya. Nisiyumbishwe na matukio. Nashukuru. Nitasimamia
hapo, na kupambana kwenda mbele, sio kurudi nyuma.
Asante.
Jelini.
Colins akavuta pumzi
kwa nguvu na kuzishusha. Akajua hiyo barua aliandika kabla hawajakutana.
Akabaki ametulia tu. “Kwema?” James akamjaribu. Akamuona ameumia haswa.
“Nisikilize Colins, mimi ni mtu wako, unaweza kuniambia chochote kile. Naweza
nikakushauri au angalau ukapata mtu wa kuzungumza naye, ukatoa uzito kifuani,
ukaweza kufikiria.”
“Nina wakati mgumu
James, sikuwahi kufikiria maishani kama naweza kupita hapa.” Colins akaanza.
“Tangia nazaliwa, sijawahi sikia kitu ninachojisikia kwa Jelini, na siwezi
kueleza, mtu akanielewa.” “Mimi nakuelewa. Kilinipata kwa mara ya kwanza
maishani, kwa Jema. Nilishindwa kuelewa mpaka ikabidi nizungumze na Geb.”
“Alikusaidiaje?” “Acha kudandia gari kwa mbele, Colins! Mambo hayafanani. Sasa
imekuaje?” “Love.” “Mbona kama uliniambia mlishamalizana?” “Aisee amerudi kwa
kasi akitumia wazee, wala si kina mama. Wazee kabisa akijua kabisa
anachokifanya, tena kwa makusudi! Mpaka ameniharibia kwa Jelini.”
“Hapo sasa si sawa
Colins!” James akambadilikia. “Jelini ametoka kuumizwa na yule mzee, na wewe
unaanza tena!?” “Si kuanza. Nahisi kwa mara nyingine tena, nimemuumiza Jelini.
Na sidhani kama nitampata tena. Imekua mbaya kweli.” Akamsimulia kila
kitu. Aina ya mahusiano ya familia walizo nazo. Jinsi walivyoishi wakikua
pamoja, wazee wao wakiwa wameapishana katika shida na raha.
“Aisee nasikia kuumwa
kabisa. Sikujua kama watu huwa wanaposema wanapenda, ndio hivi! Ni hisia za
tofauti!” “Kwani ilikuaje na Love!?” “Love ni kama tulijikuta, tukaona inabidi.
Lakini si kwamba kulianza mapenzi. Nimekua naye karibu mpaka tukajikuta
tunaanza mahusiano ya kimapenzi wakati tukikua. Lakini si kwa sababu ya
tulianza hisia. Na nafikiri ndio maana alikuwa akinidharau na kunitusi sana.
Kwa kuwa alijikuta ni kama inambidi kuwa na mimi sababu ya mahusiano ya wazazi.”
“Subiri kwanza
Colins. Matusi tena?!” “Acha James. Mpaka aibu kusema. Nina uhakika kwa
asilimia 100, matusi aliyokwisha nitukana yule msichana, sitakuja
kutukanwa na mwanadamu mwingine yeyote yule hapa duniani.” “Ndiyo mbaya hivyo!”
“Nakwambia, nilifika mahali mpaka mimi mwenyewe nikaanza kuamini maneno yake,
nikaanza kuishi kile anachonitukana. Nikaanza kuona ni kweli, ndio kama vile
nilivyokwambia, nikajua napotea, si sawa. Tukahitimisha vizuri sana, na yeye
akakubali vizuri, bila shida, nashangaa ananigeuka kwa kujirudi kupitia wazazi
tena kina baba!”
“Mimi sijui bwana
Colins! Lakini mimi namfahamu mwanadamu kwa kuishi naye. Ni kiumbe chenye nguvu
mno. Akiamua kufanya jambo lake!” James akacheka kwa masikitiko kama
aliyekumbuka mbali. “Aisee mimi ndio maana nilijitenga kabisa mpaka nilipompata
Jema wangu. Na ndio maana namng’ang’ania kwa moyo wangu wote bila
kuzembea. Siruhusu kitu wala mwanadamu mwingine katikati yetu, kwa sababu mimi
najua kwa kuona madhara ya kuzembea kwenye ndoa. Nimeshika haswa.”
Akakumbuka historia
ya Danny na Grace. Walivyokuwa na ndoa yenye heshima kwenye jamii. Bila ya
kutarajia Danny ni muathirika wa UKIMWI. Hana ndoa, kaua watoto
wawili kwa hasira. Amebaki peke yake! Mwanamke aliyemkimbilia, akimfananisha na
aliyekuwa mkewe, anaishi na wanaume wengine. Hana hata habari naye! Danny
amekua darasa lake James. Anaishi kwa kuona, anajifunza bila kupenda.
Kila akijisahau kidogo, anajirudi kwa haraka sana kwa mkewe.
“Daah!” Colins
akasikitika. “Ila kwa heshima kabisa Colins, tafadhali kaa mbali na Jelini
mpaka ujue ni nini unataka.” “Unafikiri mimi sijui nini ninataka!? Ni…” “Hapana
Colins. Tafadhali nisikilize. Wale binti wamelelewa na mama tu. Na cha kwanza,
nakwambia ukweli, chochote kibaya unachomfanyia Jelini, mama yake huwa anaumia
sana kuliko wale watoto wenyewe. Na Jema anasema huwa anasema watu wanadharau
binti zake wakijua hakuna mwanaume wa kuwatetea. Wanachagua kuonea
watoto wake, ili kukinga binti wenye baba zao.” “James!” Colins
akashangaa, asitarajie hilo.
“Hakika hujawahi
kuona yule mama akitetea wanae. Hutampenda. Mkali kuliko simba. Muulize Love
atakwambia jinsi alivyompandishia mbele ya mama zenu na Connie, pale alipoanza
kumsema Jelini akikumbushia siku aliyolewa kwenye harusi yetu. Ilikaribia kuwa mbaya
usiku ule, na mama Jema hanaga aibu na katika hilo hana utu wala staha. Akifika
kutetea wanae, Jema anasema anapandwa na hasira ya ajabu sana. Wanao mjua, huwa
wananyamaza ndipo na yeye anatulia. Sasa pona ya Love usiku ule, ilikuwa
kutulia, na kukubali kuondoka pale. Sasa nakutahadharisha. Hutaki kuona upande
mwingine wa mama Jema.”
“Hilo moja. Ila la
msingi ni muhurumie Jelini. Usimuweke katikati ya haiba ya mahusiano ya
aina hiyo ambayo nyinyi mnayo. Unamuumiza bila sababu.” “Nampenda Jelini,
James.” “Lakini wewe si mwanaume kama wanaume wengine Colins! Hilo likubali.”
“Unanitusi James!?” “Mimi nakwambia ukweli si kukutusi. Wewe unajenga
familia yako na ya baba yako. Mimi nimemuoa Jema, tujenge kwetu.
Sijui kama unanielewa?” Colins kimya.
“Mimi kwa sababu ni
mtu wako nakufahamu, nakuelewa. Lakini mtu mwingine anaweza kukushangaa kabisa.
Unasimamiaje mahusiano ya wazazi wako, kama yako!? Utajenga lini kwako!? Lakini
kumbe ni mfumo mliokubaliana, na unaupenda. Ndio maana hata kujenga,
umejenga pembeni ya wazazi na likawa sawa hata kwa Love. Kwamba mngeoana
nyinyi, mnakaa ndani ya mji wa baba yako, maisha yanaendelea kama kawaida,
tofauti na sisi wengine.”
“Japokuwa mimi ni
mtoto wa kwanza kwetu. Na mzee anamali nyingi huko kwake, mimi sijajenga kwenye
mali zake. Nimekuja kuanza huku Dar. Mke nimempelekea mimi. Hata mama yangu
mzazi hana mamlaka juu ya Jema, ila mimi. Na kwetu ndivyo tulivyo, haina shida,
na tunaishi hivyo kama nyinyi mlivyokubaliana kwenu kuishi hivyo. Sijui kama
unanielewa?” Kimya.
“Na aina ya familia
zilizobarikiwa kama hizo zenu, ni chache sana Colins. Wewe ni shahidi. Wengi
hawajabahatisha mlicho nacho nyinyi. Ukaribu wa familia kwa kiasi hicho!
Binafsi sijawahi ona. Sasa kumsogeza mtu kama Jelini ambaye hajakulia
kwenye hayo mazingira ni kumuumiza bila sababu. Na mimi kama mtu wako wa
karibu, kwa heshima kabisa, nakusihi usimfanyie hivyo. Si sawa. Ishi
maisha uliyochagua. Ukipokea faida zake na hasara zake, lakini usimtake Jelini
aingie katikati hapo, halafu yeye akaishia kuwa muhanga. Hapana Colins.
Ni hilo tu.” Colins akapokea hiyo dozi kama ilivyo, akaimeza na kutulia kimya,
siku ya kazi ikaanza.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Kila Pande
Penzi Limechanganyikana Na Pesa.
~ Love Anajirudi Kwa Colins Kwa Kisingizio Cha Kuokoa Mali Za Wazazi.
~ Belinda Anamgeuka Shoga Yake Wa Muda
Mrefu, Akitaka Penzi La Victor Sababu Ya Pesa. Na Anadai Yalishakuwepo
Mahusiano Kati Yao Kabla Ya Vai. Haki Zote Ni Zake, Maana Vai Amemfahamu Victor Kupitia Yeye. Wameapa Kumkomesha Vai Aliyepo Hotelini Akikoleza Mahusiano Yaliyokwisha Mnogea Victor.
~ Bale Anamtaka Vai Aliyekwisha Toa Ahadi Ya Muendelezo Wa Penzi Kwa Victor.
~ Colins King’ang’anizi Akiwa Anajenga Kwa Baba Yake, Kwake Kunavunjika. Mshika Mawili, Moja Limemponyoka. Katikati Ya
Mahusiano Hayo Ya Kifamilia, Na Penzi, Anacheza Vipi Karata Zake Apate ROHO
INAPENDA? Jelini.
Nani Kakumbuka Shuka Kumekuchwa?
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment