Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 41. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 41.

Akajitengeneza vizuri kama kawaida yake, akapendeza. Na mwanae akawa tayari wakaondoka kuelekea kwa Jema, Jelini ametulia kimya akiendesha. “Hivi tukirudi ujue hatutakuwa na gari.” “Sawa. Mimi sina neno mama. Mbona tulikuwa tukiishi bila gari na tulikuwa sawa tu?” Mama yake akashangaa sana nafsini mwake. Jelini ndiye mwenye pesa yote, lakini hajajiweka kama mmiliki na wala hajaomba mama yake amrudishie kadi zake! Mama Jema akawa kama ndio anaanza kumsoma Jelini. Hawakuwahi kuwa na mahusiano ya namna hiyo, ya kifedha.

Akaendesha ametulia mpaka kwa Jema. Wakakuta rafiki baadhi wa James walishafika na vinywaji vyao na nyama zao. Wameshaanza kula vitu vyao wakati Jema akiwaandalia cha hapo kwake. Wakaanza kumchokoza Jelini. Colins hakuwepo. “Mimi mwenzenu siku hizi nishakuwa mtu mzima, sitaki uchokozi na mtu.” “Jelini mtoto mzuri, njoo tutete yetu huku tunakata kinywaji taratibu.” “Akuu! Mimi sitaki. Nataka kutulia zangu na pombe nishaacha zamani sana. Mimi nikilewa, naanza kugawa mwanangu wakati mimi nampenda mwanangu.” Wakazidi kucheka wakimzuia asimfuate mama yake huko alipopotelea jikoni kwa Jema, ili abaki pale sebuleni alipowakuta wazidi kumchokoza.

“Ila ujue Jelini mimi nitakua baba mzuri sana wa mwanao?” “Akuu! Sitaki.” “Mwacheni Jelini.” Akaingia Colins na huo mkwara, wote wakageukia mlangoni. “Mzee upo?” “Nipo.” Wakasalimiana kwa kupeana mikono wakigonga.

“Wewe ndio umemtoa Kevin, nini?” Wakamuuliza Colins. “Kumtoa wapi tena!?” “Kwamba wewe hujui kuwa Kasa mwaka mpya alikuwa rumande?” “Kwa kosa gani!?” “Nasikia mzee wao ndiye aliyewaweka jela wote, mpaka dada yake na mumewe.” Kila mtu akawa anataka kusikia, Jelini mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi. “Na ndio maana akampigia Mdosi akamuwekee dhamana kwa kuwa hakuwa na mtu wa kumtoa.” Mwingine akadakia.

“Basi Mdosi atakuwa ndiye aliyemtoa ila si mimi.” Colins akajibu akiwa anakaa. “Mdosi kamchinjia baharini! Unafikiri sisi tulijuaje?” “Mdosi kamtema. Alikuwa anasema yeye si ananyodo kama mtoto wa kike, basi akatafute matajiri wenzie wamtoe. Akamwambia hana hiyo pesa yakumuwekea dhamana atoke.” “Acha masihara!” Danny akadakia.

“Kumbe? Yeye si anasemaga sisi wote tunashida, yeye yupo pale ili kutoka kitandani tu? Ndio Mdosi akamwambia, hali yake kama anavyoijua. Pesa hana.” “Na kamfanyia kusudi tu.” “Kwani siri? Amesema ingekuwa mtu mwingine, hata benki angekopa ili amuwekee dhamana. Amesema amemfanyia hivyo ili atie akili ajue pesa si kila kitu, ila utu.” Wakaanza kumsema Kevin na familia yake, wakawa wameshampoteza Jelini.

“Matajiri wana mambo! Sasa mzee aliwafunga kwa sababu gani?” “Itakuwa walitaka kumzidi tu mzee mahesabu, akawakamata ndio akaamua kuwatia akili kuwaonyesha yeye ndiye anayewaweka mjini. Wasijisahau.” “Nasikia mzee wao mkorofi!” “Unaambiwa ni kama Hitler. Katili hacheki na kima.” Mazungumzo juu ya hiyo familia yakaendelea, Jelini kimya.

Jema na mama yake walikuwa jikoni. Mama Jema alishamchukulia Jeremy hizo nyama walizoleta rafiki wa James, na sahani yake akapitiliza naye jikoni na kumuwekea ili ale. Jelini akanyanyuka taratibu na kutaka kuondoka, Colins akamuwahi. “Nisubiri.”

~~~~~~~~~~~~~~~

Akamshika mkono na kumtoa nje baraza la pembeni kabisa wala si mbele wala nyuma. Hapo James aliweka kwa kujenga bustani ndogo tu. Muundo mzuri ndipo kunapoangaliana na hilo baraza. Unaweza kujificha hapo na kufanya yako mtu asikusumbue. Akafunga tv kubwa tu, nzuri. Ndipo marafiki zake huwenda kuangalia mpira kwenye hilo baraza bila kumkera Jema hata akiwa na wageni wake. Watapiga kelele huko na kubishana mpaka wachoke. Napo James alipafunika uzio wa wavu pia. Na makochi ya kukaa hapo mazuri tu na meza zake, kama kwa kina Magesa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wawili hao wakakaa hapo. “Nisikilize Jelini. Hii familia na mambo yao, hayakuhusu hata kidogo, wasikuumize kichwa. Unanielewa?” Jelini akabaki ametulia. “Umepita kwenye maisha yao, umetoka, mengine waachie wenyewe. Usijiumize kichwa kabisa. Huusiki tena.” Jelini akavuta pumzi kwa nguvu na kuanza kuzishusha taratibu kama kusafisha kifua. “Wasikuharibie usiku wa leo, wala usiwape mwanya wa kukutesa zaidi.” “Umependeza Colins! Na unanukia vizuri kama kawaida yako.” Colins akaanza kucheka.

“Kweli tena. Umeacha harufu pale kwenye mto wangu. Wakati natandika nikapata hiyo harufu yako.” “Na wewe umependeza Jelini. Nataka ufurahi usiwe na huzuni.” “Sasahivi inapungua. Nilitaka kujipanikisha bila sababu!” “Hawakuhusu tena. Hata ukiwasikia, wasikuumize kichwa. Sawa?” Jelini akakubali kwa kichwa.

“Basi turudi ndani.” “Mimi naenda kuwasaidia kina Jema, wewe nenda kwa wenzio.” “Sasa tutapata muda wetu saa ngapi!?” Colins akawa kama analalamika. “Wakati wakula.” Colins akafikiria, akawa kama hajaridhika. “Usikae sana jikoni. Ukichelewa nakufuata.” Jelini akacheka. “Au hutaki nikufuate.” “Mimi nataka wewe unifuate kila mahali.” Colins alicheka sana. “Sikukeri?” “Hata kidogo. Ndio nafurahi. Napata faraja. Nikiwa na wewe na ukiniongelesha, natulia.” Hawakufanikiwa kutoka hapo.

 Wakabaki hapohapo barazani wanaongeleshana hawamalizi. Colins amekaa nyuma yake, anaongelea shingoni kwake, akimchungulia kwa mbele, amemuegemea bega. Mara waangalie simu ya Colins wakipekua hiki na kile na Jelini ndiye aliyekuwa ameishika.

Hawakukumbuka kula wala kinywaji. Wakawa kama wamepotea kwenye kusanyiko. Wamebaki wao wawili tu, upande wa barazani. Wakati wenzao wanakula na kunywa ndani. Danny akawakumbuka, akaanza kuwasaka bila kumwambia mtu. James akamuona na yeye akamfuata, wakawakuta wamekaa vile. Danny akakunja uso. Colins hata hakushituka ila kumuuliza. “Vipi, umeniita sana nini?” “Hata ningekuita, ungeitika kweli?” Danny akamuuliza, James na Colins hawana mbavu.

Jelini akataka kusogea ili wasikae vile mbele yao, akashindwa maana hivyo Colins alivyokuwa amemuegemea! Wengine wote wakawafuata maana hilo baraza si geni kwao. Wakawakuta vile. Zikaanza fujo. “Colins hatimaye kachukua jimbo.” “Alibana weee, yamemshinda.” “Jelini namba tasa. Inagawanyika kwa moja tu, na yenyewe.” Akaongeza mwingine wao, wote vicheko. “Kwa hiyo Jelini hagawanyiki kwa mbili?” “Ushaona mwingine kama Jelini?” Akajibu na kuongeza fujo wakicheka kishabiki. “Hata wachoraji hawajaweza kumchora mtu kama Jelini. Yupo peke yake dunia nzima.” “Basi kweli Jelini namba tasa.” “Nilisema mimi.” “Sasa, sasahivi Jelini umefurahi?” “Mimi nishasema sitaki uchokozi, nishakuwa mtu mzima.” Wakazidi kucheka.

“Jelini mtoto mzuri mimi nina swali.” “Sitaki.” “Sasa mbona hata swali langu hujalisikia!?” “Kashasema hataki. Muache. Nyinyi kaeni hapa, acheni majungu.” Colins akaingilia. Kikao kikahamia hapo kula na kunywa hapohapo. Stori zikaendelea, Jelini katulia kimya hapo kwa Colins mpaka wazazi wa Colins walipofika.

~~~~~~~~~~~~~~~

Colins akasikia sauti zao akamwambia Jelini amsindikize. James akafuata nyuma. “Tumeleta sambuza za wajukuu, wala hatukai. Baba CJ kesho kazini, alfajiri. Hata huko tulipokuwa tuliomba udhuru.” “Nashukuru sanaaa.” James akashukuru yeye. Wakazungumza kidogo, wao wakaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Na mimi kesho naanza kazi, Jema.” “Mama ameniambia. Naona umekazana!” “Nataka hela. Na sasahivi nimejiambia sitaki tena kukuomba. Mchana mama alivyonikatalia hela, nusu nikutumie ujumbe nikuombe wewe, lakini nikajisuta. Acha na mimi nifanye kama wewe Jema. Naamini nitafanikiwa.” “Halafu ni kwa muda tu, Jelini. Mwanzo mgumu. Mambo yakikaa sawa mbona utapumzika?” “Mmmh! Nimeona matajiri jinsi wanavyofanya kazi mama yangu. Hawana kupumzika kama mimi. Acha tu nibadilike.” Wakazungumza kidogo, Colins akasema atamsindikiza kurudi nyumbani, awahi kulala. Gari walishakubaliana kuliacha hapo. Jema alisema yeye atamrudisha mama yake na Jeremy. Hao wawili wakaondoka na kufurahia kuwa peke yao.

~~~~~~~~~~~~~~~

Wakahamisha kikao nyumbani kwa mama Jema. Wawili tu, hamna gasia ya watu. Wakajizungusha kwa hili na lile wakitafuta sababu ya Jelini kuwa mikononi kwa Colins, wakakosa. Jelini anahangaika ili tu ajikute amekumbatiwa tena, akashindwa kujirudisha, akaenda kukaa kochi la pembeni mbali na alipokuwa amekaa Colins.

“Njoo nikuonyeshe kitu.” Akahamia kwenye kochi alilokuwa amekaa ila pembeni. Wote hawakuridhika. Colins uzalendo ukamshinda. “Mimi hivi najihisi mpweke! Nataka uwe hapa na mimi.” Jelini akacheka na kujisogeza karibu kabisa. Akarudi kukumbatiwa, ndio wote roho kwatu. Jelini anasikia raha uso wa Colins kwenye shingo yake huku akizungumza naye. Colins anasikia raha kumkumbatia vile kwa karibu. Ukabaki ulimwengu mzima peke yao wakibembelezana kwa hili na lile. Wakati mwingine wanatulia tu wakisikiliza mziki kwenye simu ya Colins.

Walikaa hapo mpaka James akawarudisha Jeremy na mama Jema. Hakuingia ndani ila alijua bado Colins yupo. Walipolikuta gari lake pale nje wakaangaliana na mama Jema na kucheka. Mama Jema akaishia kutingisha kichwa na kushuka garini. “Usiku mwema Jeremy.” Akawaaga na kurudi kwa mkewe. Ilashakuwa saa saba usiku. Naye mama Jema hakutaka kukaa hapo. Akawasalimia na kupitiliza kulala na mjukuu wake. Alishaambiwa Colins kituo cha polisi, aachwe kabisa, asifukuzwe hapo ndani. Na yeye hakutaka mengi, akamuacha.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Bosi wangu amerudi, acha na mimi nikalale. Maana mama anapenda mambo ya kudamka. Sitaki kesho aniache.” “Kwa hiyo utakuwa ukifanya kuanzia muda gani.” “Mama ameniambia nikifungua kuanzia saa mbili kamili, na nikaweza kukaa mpaka saa mbili usiku sio mbaya. Ili na wale wanaotoka makazini, kama wanataka kununua vipodozi baada ya kazi wanikute. Ila amesema usiku atakuwa anakuja kunipokea ili na mimi nipate muda na mtoto.” Colins akasikiliza, na kubaki akifikiria.

“Mbona kama kuna kitu unataka kusema?” “Sitaki kukukatisha tamaa, ila ujue ni ngumu. Si rahisi kama inavyosikika. Najua nia ipo, ila tafadhali Jelini, unapokumbana na uhalisia, ukachoka, nakuomba, usije tafuta mbadala. Niambie.” “Kama wasiwasi wako ni kwamba naweza kurudi kutafuta msaada kwa mwanaume mwingine…” “Kasa.” Ikabidi Colins awe muwazi kabisa.

 “Mimi sirudi tena kwa Kasa, Colins. Bora nimuombe Jema hela kuliko kuuza utu wangu. Hapana Colins. Mimi sipo hivyo.” “Niahidi mimi nitakuwa wa kwanza kuniambia kama mambo yamekuwa magumu sana na unahitaji msaada.” “Na wewe usikimbilie kunihurumia. Fanya kama mama. Nataka nijenge tabia ingine zaidi ya hii ya uvivu. Mwenzio sijasoma na wala sina mpango wa kurudi shule. Sasa na biashara pia nishindwe! Sitaki kuwa tegemezi daima. Kama hivi vitu vya chumbani kwa mwanangu vinaninyima raha! Sasa nataka kupambana mimi mwenyewe mpaka nimnunulie, au nikomboe vile nilivyoanza mchakato kwa fundi. Kwa hiyo nitie moyo. Kama hivyo wewe unavyoamka kila siku asubuhi na kwenda kazini mpaka jioni, na mimi nataka huo uwezo. Nishalala sana.” “Sawa. Mimi nitakuwepo kukutia moyo.” Ahadi hiyo akatoa na busu la shingoni upande wa masikio.

Jelini alisisimkwa nusura amgeuzie mdomo, lakini hakutaka kufanya chochote na Colins. Hata busu la mdomo, mpaka akapime kwanza. Akajishika pale alipombusu. “Asante Colins.” Akashukuru akiwa ameinama bila kumuangalia maana alijua akimwangalia tu, uzalendo utawashinda. Na Colins alijua. Akasimama hapo nyuma alipokuwa amekaa. Jelini akabaki amekaa na kuinama. “Nitakuona kesho.” “Si unakwenda kazini?” “Hapana. Tunarudi tarehe 5. Nitakuona kesho.” Colins akatoka kurudi kwao.

Siku Inayofuata.

Alfajiri mida ya saa 12:30 Colins akarudi hapo na kumshangaza sana mama Jema wakati akimfungulia mlango. “Sasa wewe utakuwa umelala kweli!?” Mama Jema akamuuliza. “Nimekuja kukumbuka sijamuuliza Jelini hilo duka analokwenda kufanya kazi litakuwa wapi. Nataka kuwa naye siku ya kwanza.” Mama Jema akabaki akimtizama. “Kama hutajali lakini.” Akajirudi. “Kwamba na wewe ukauze duka la vipodozi!?” “Si ndiko atakapokuwa Jelini? Au sikuwa nimemuelewa?” Mama Jema akaona amuache tu. Jelini akatoka akionekana bado alikuwa amelala.

“Karibu Colins.” “Nimewahi sana. Samahani kwa kuwasumbua mkiwa mmelala.” “Usijali. Njoo unisubiri wakati najitayarisha. Tutatoka kwenye saa mbili na nusu. Nilisahau kukwambia muda.” Akaenda kumshika mkono kabisa. Mama Jema akajirudia chumbani kwake. “Nimejisikia vibaya nimewaamsha!” “Basi mimi nimefurahi kukuona.” Colins akaanza kucheka, mama Jema akiwasikiliza.

“Njoo usinzie kitandani kwangu wakati mimi najitayarisha.” Ikawa kama amepewa ulimwengu wote. Akavua viatu haraka na kwenda kujitupa kitandani kwa Jelini wakicheka.

“Leo mimi ndio nakubembeleza ulale.” “Wewe hurudi kulala?” “Nataka kujiandaa. Ikiwepo kutengeneza kifungua kinywa. Lala hapa.” Akamuonyeshea kwenye mto. “Bila hata kukugusa!?” Jelini akaanza kuona aibu.

“Bila kukugusa sitalala bwana!” “Nitakubembeleza utalala tu.” Colins akabaki kama anayejishauri, kwamba hajaridhika. “Njoo, utalala. Huwa namfanyia hivyo Jeremy analala haraka.” “Mimi sitaki unibembeleze kama Jeremy.” Jelini akacheka na kujifunika uso. Akamuhisi anamlalia mapajani. “Hivi ndio najisikia vizuri, angalau nimekulalia.” Jelini akaanza kumpapasa taratibu.

“Sasa ukilala nikikuweka kwenye mto si utaamka?” Akajigeuza chali na kumwangalia. “Lakini nitakuwa nimekuwa karibu na wewe.” Jelini akacheka na kuanza kumuweka sawa nyusi kama ambusu, ila ikawa kama aliyekumbuka kitu akarudi haraka pembezoni mwa nywele na masikio. Akamchezea, akamuona anajigeuza kurudi kulala ubavu. Wakatulia kwa muda.

“Njoo ujilaze pembeni yangu.” Jelini bila ya kufikiria, akajilaza akimpa mgongo. Akamuwekea mkono, Jelini akaukumbatia vizuri kwa mbele akimchezea vinyweleo vya mkono taratibu huku akipata sawia pumzi za Colins kitu alichopenda maana na hapo alijiiegemeza uso karibu sana na yeye. Ile harufu na uwepo wa Colins, hapohapo wote wakalala.

~~~~~~~~~~~~~~~

Walikuja kuamka saa tano asubuhi, wasiamini. “Nimekuponza.” Colins akamwambia. “Hata hivyo tulilala muda mbaya. Usijali. Acha nioge, nimtafute mama. Maana najua mida hii atakuwa ashafanya mengi sana.” Jelini akaoga, akagundua mwanae yupo chumbani kwake. Akamfuata. “Bibi amesema vyakula vipo kwenye friji. Alipika kingi jana kwa anti, amebeba.” “Wewe umeshakula?” “Nakaribia cha mchana. Bibi ameniwekea kwenye sahani kabisa, amesema nikisikia njaa, nipashe tu.” Jelini akatoka na kumuacha huyo Jeremy  maana alionekana ametingwa na hataki kuingiliwa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akaonelea kumpigia simu mama yake “Nilipitiwa na usingizi.” “Na mimi nilijua tu. Nikaona nikuache.” “Nikufuate wapi?” “Sio sasahivi. Mimi nishahama upande wa pili. Huko tena nishatoka. Kwani Colins anaanza kazi lini?” Jelini akaanza kucheka. “Mama naye?” “Wewe niambie tu.” “Tarehe 5.” “Basi naona na wewe ajira yako ianze siku hiyohiyo, usinidanganye na kunipotezea muda wangu. Kwaheri.” Jelini akabaki akicheka asiamini.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Akarudi chumbani alikomuacha Colins. “Umefukuzwa kazi?” Akamdaka mlangoni na swali. “Mama ameniambia nianze kazi, wewe ukianza kazi.” Colins akacheka sana. “Sio jambo zuri bwana!” “Tunahitaji muda Jelini. Mwenzio sipati likizo kila mara. Acha tutumie hizi siku zilizobaki vizuri. Unataka tufanye nini? Twende wapi? Chochote unachotaka.” “Siwezi kutoka, Jeremy yupo busy na ujenzi wake.” Colins akazidi kucheka. “Basi usiku mama akirudi, sisi tutoke twende dinner halafu movie, au unasemaje?” Jelini akatulia.

“Mbona unasita tena? Itakusaidia kuchangamka na kupata muda pamoja.” Jelini akafikiria jinsi ya kumueleza, akasita. “Pengine niwe nilikuelewa vibaya. Ni kama nilielewa unafurahia muda na mimi!” “Ni kweli Colins. Natamani hata usiondoke.” “Sasa shida ni nini!?” “Nimekumbuka vitu vyangu nilivyoacha kule.” Akamuelewa kuwa alivyoacha kwa mzee. “Kwa hiyo unataka kwenda kuvifuata kwanza ndio tutoke!?” Wivu tayari. “Hapana. Kwanza nahisi hapa ninavyo vitu vyangu vingine. Nitakuwa sawa.” Colins akaonekana bado analo jambo.

“Unataka tutoke saa ngapi?” Akawa kama anamtoa huko alipokwama. “Inamaana unampango wa kuja kurudi kwake, kufuata tena vitu vyako?” “Si lazima.” “Jelini?” “Yaani ndio nimekumbuka sasahivi baada ya kusema tutoke. Lakini sio hata kitu nakipigia mahesabu.” “Kwani ni kama ulihamia huko?” “Kwa sehemu. Zaidi siku za weekend. Ila naomba usirudi huko. Turudi kwenye mipango yetu.” “Itasaidia nini kama mimi sirudi huko kimawazo lakini kumbe mwenzangu una safari itakayokulazimu kurudi kwake? Tena chumbani!” “Colins wewe unafika mbali sana ambako mimi huko wala sipo!” “Tafadhali kabla ya kurudi kwa yule mzee unishirikishe Jelini.” “Sawa.” Hapo tena akaharibu maana aliitika bila ya kufikiria, ilimradi yaishe.

“Kwamba tayari kuna mpango wa kurudi!?” “Colins wewe unawasiwasi wa bure tu! Kwanza hata sikuwa na mawazo ya huko. Tafadhali tutumie hizi siku mbili vizuri, sio tena kumuwaza na yeye. Utaninyima raha. Nataka tubaki mimi na wewe tu.” Hapo akatulia.

“Naomba uniamini, Colins. Mimi si kigeugeu.” “Lakini mlikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi, Jelini! Haitachukua nguvu nyingi kukurudisha mlipokuwa. Ndio maana napatwa wasiwasi.” “Niambie unataka nifanye nini ili uamini ninachokwambia?” “Sijui Jelini. Hata sielewi tena.” Jelini akaenda kukaa kabisa pale pembeni yake.

“Sina mpango wa kwenda kwake. Na ikitokea nakwenda, nitakujulisha. Tena tunaweza hata kwenda wote.” “Sitaki kwenda kwake.” Hapo na ubishi akauweka. “Mimi naona nimwambie amtume dereva aniletee ili yaishe.” “Jelini! Kwamba mrudishe tena mawasiliano mpaka kupanga tena mipango!?” Hapo Jelini tena akakwama.

“Basi nishauri wewe kitu chakufanya.” “Kwani ni vitu vya thamani sana?” “Sana Colins.” “Kwamba kupita hivi vyote hapa!?” “Sitakudanganya. Nimeacha kule vitu vya thamani sana. Mpaka dhahabu zangu zipo kule. Tena dhahabu nyingi tu. Nguo za jioni ndio nyingi, tena za thamani na viatu. Mimi napenda sana kupendeza Colins. Kwa hiyo nikiwa napesa kwenye kuvaa, sijipunji.” Colins akachoka kabisa, akasimama pale.

“Sasa unaenda wapi!?” “Nahisi kuchanganyikiwa tu. Bora nitoke kwanza.” “Njoo Colins. Usichanganyikiwe. Sitakuumiza. Hiyo ndio ahadi yangu ya kwanza, japo sijui tutaishia wapi. Na nina ujasiri wa kusema hivyo. Ipo siku nitakupa sababu. Kabla wewe hujaumia, ujue mimi nitakuwa nimeumia zaidi. Hakuna mali, itanifanya nikukosee. Ni bora nipoteze kila kitu, mimi na wewe tubaki salama.” Hapo akaupata moyo wa Colins. Akatulia kabisa na kurudi kukaa.

“Mimi sina pesa kama za yule mzee, Jelini. Sina uwezo wakusema eti nitakununulia mavitu ya thamani. Sina huo uwezo mkubwa kiasi kama chake.” “Kama ningekuwa na shida na pesa, ningeanza kulala na mwanae ndio nikaja yeye. Sikutegemei uwe yeye, na najua wewe si yeye. Na ujue kabisa, haupo kwenye mashindano naye.” “Una uhakika?” “Asilimia 100.” Akatulia.

Jelini akajipenyeza mwilini mwake mpaka akafanikiwa kuingia katikati ya mikono yake akajilaza kifuani kabisa. Na yeye akamkumbatia. “Umeniamini?” Jelini akamuuliza kwa kumbembeleza. “Sitaki kukupoteza Jelini.” Jelini alishituka, akamwangalia. “Unamaanisha Colins!?” “Sina sababu ya kukudanganya. Najua umetoka kuumizwa. Ndio maana naona nikupe muda utulie, ili angalau akili yako hata ije kunifikiria na mimi, kwamba nikikwambia kitu, uweze kunielewa na kuniamini. Sasa tena kusikia bado kuna mambo yakuwahusu nyinyi wawili tena! Nafasi yangu itakuja kufika lini?”

Ikamgusa kweli Jelini. “Nikikwambia nafasi yako haijawahi kupotea, utaamini?” Colins akakunja uso wa wasiwasi. “Sijaelewa Jelini!” “Nitakuja kukueleza vizuri nikiwa nimetulia, Colins. Lakini amini sitarajii kukuumiza na wala usiwe na wasiwasi naye. Mimi nakupa uhakika.” Colins akatulia. “Twende ukale kwanza.” Kazi ya kufuatana hapo ndani ikaanza. Kila mahali wapo pamoja. Wakikaa, ni kukumbatiana kwa huba haswa mpaka ilipofika jioni Colins akatoka kujiandaa kutoka na Jelini kwa chakula cha usiku wakiwa wamehamasika haswa kuja kupata tena muda wa pamoja na mipango ya kutumia hizo siku mbili ipasavyo, kabla yakurudi kazini.

Mtoto wa Jelini hanaga shida. Yeye bora ale. Muda wote alikuwa chumbani kwake akifanya yake. Jelini akaoga na kuanza kazi ya kujiandaa.

Machozi Ya Samaki.

Colins anafika kwao, mlinzi akamuwahi getini. “Mama anakuita ndani.” Colins akakunja uso. “Amesema ukija tu, nikwambie uende moja kwa moja.” Mlinzi akaongeza msisitizo. Colins ikabidi atoe simu yake. Haikuwa hata hewani na hakujua ni wakati gani ilijizima. Akasogeza gari mpaka nyumba ya wazazi. Akashuka kwa haraka kama akimbie ili asipoteze muda hapo, arudi kwa Jelini kwa wakati.

Akawakuta baba yake na mama yake hapo sebuleni. Akasalimia amesimama. “Kwa nini unamtia mama yako wasiwasi!?” “Simu ilikuwa imezima baba. Sijajua. Kwema?” Akauliza akimwangalia mama yake. “Mbona wimawima hata hukai?” “Nina haraka mama!” “Kwamba huna hata dakika 10?” “Zote hizo!?” Colins akahamaki kama ameambiwa mwaka mzima.

“Kaa chini Colins.” Mzee akaweka msisitizo wa amri. Akakaa akilalamika. “Mimi nina haraka.” “Unakwenda wapi?” “Kwani kuna nini?!” “Love anaumwa. Amelazwa.” Colins akatulia akimsikiliza mama yake kwa macho ya ‘kwa hiyo?’. “Umesikia Colins?” “Nakusikiliza.” “Kwamba hutaki kujua anachoumwa?!” “Sasa hata nikijua itanisaidia nini mama jamani? Mimi nina haraka.” “Colins! Nakwambia mwenzio amelazwa, hata kutaka kujua kulikoni!?” “Love sio mwenzangu mama. Naomba rekebisha huo usemi.” “Ujue yupo serious sisi tulikuwa huko karibu siku nzima, hata wazazi wake wanawasiwasi!” “Basi labda niseme hivi. Mniambie alipolazwa, nitakwenda kumuona.” “Afadhali hivyo.” Colins akasimama.

“Sasa mbona hata hujajua alipolazwa halafu unaondoka?” “Amelazwa wapi?” Colins akauliza na kushangaza wazazi wake, wakabaki wakimwangalia. “Au nitawapigia simu wakati nikienda. Sasahivi nina haraka.” “Colins, hebu subiri kwanza.” Baba yake akamuwahi kabla hajaondoka.

“Yule binti anakupenda sana. Leo alikuwa akiugulia maumivu huku akikutaja! Kwa kukiri kwake kwa baba yake, mimi nikisikia amemwambia baba yake anajuta na kama angepata nafasi ingine na wewe, atafanya tofauti. Sasa si bora umfikirie?” “Mimi simtaki tena.” Colins akajibu bila hata kufikiria mara mbili.

“Si wewe ulisema Love ndiye mke wako?” “Dad!” “Wewe mwenyewe uliniambia. Na ukasema utafanya kila uwezalo, kumfanya awe na furaha.” “Basi kama mama hakukwambia, nilishindwa. Na sitaki tena.” Hapo anajibu akionekana wazi anataka kuondoka.

“Coli..” “Mbona kama unanilazimisha?! Nimesema SIMTAKI. Simtaki tena. Wewe hujui nilikopita na Love.” “Najua na usisahau wakati wote kwenye safari yenu na mimi nilihusika. Niambie ni jipya lipi ambalo limetokea upya.” “Nilikwambia nimechoka.” “Kwa sababu ulikuwa ukijitahidi peke yako. Sasahivi yupo tayari kubadilika. Na sasahivi ni mgonjwa. Anatuhitaji sisi kama familia. Jioni hii tunakwenda wote kama familia. Haijawahi kutokea tukatengana. Sasa sitaki wewe ndio uanze kuvunja umoja wetu. Tunakwenda wote hospitalini. Na Connie pia nimemwambia aache kila kitu. Tunakwenda kuungana na familia ya Simba kwenye kipindi hichi kigumu.” Mzee akaweka amri, akasimama na kuondoka.

“Lakini hivyo sio sawa mama. Mimi ni mtu mzima, nina uhuru wangu wa kujiamulia mambo yangu. Kwa nini hunitetei, umenyamaza tu kimya!?” “Kwa sababu katika hili yupo sahihi Colins. Hatujawahi kuishi hivyo maisha yetu yote. Familia zetu zimekua zikilia pamoja na kufurahi pamoja. Leo Love ilikuwa ni kama tumpoteze! Halafu wewe huonekani kujali ndio maana baba yako amekasirika.” “Kwani anaumwa na nini?” “Hilo swali lilitakiwa liwe la kwanza, Colins! Lakini wewe ulionekana kupuuza.” Colins akarudi kukaa.

“Nisikilize mama. Nampenda Jelini, sijawahi penda kwa namna hii.” “Mimi sijakukataza lakini…” “Subiri mama. Nipo kwenye kipindi cha kuupata moyo wake, kipindi hiki. Nikizembea tu, nitampoteza. Nilishampoteza mara ya kwanza, sitaki kumpoteza tena. Na kingine, sasahivi ananihitaji sana. Nimemuahidi kumtoa kwa chakula cha usiku. Namwambia nini? Eti nimeshindwa kutoka naye sababu Love ni mgonjwa? Na ukumbuke Jelini anayajua mahusiano yangu na Love!” “Leo unakwenda kumuona Love kama mmoja wa familia, si kama mpenzi! Ndio maana hata yeye alipokuwa mgonjwa, kila kitu kilisimama, tukamkimbilia hotelini alipokuwa na kumpeleka hospitali.” “Mama!” Colins akalalamika kwa kushangaa yanavyomrudi.

“Ni kipimo hichohicho tunampimia na Love. Familia yetu hatubagui. Labda wewe leo ndio uniambie, unaweza vipi kwenda kupumzika nje, halafu familia ya Simba inalia ugonjwa wa binti yao.” “Kwani anaumwa nini?” “Apendex ilipasuka akiwa kazini.” Colins akachoka kabisa.

“Sio jambo dogo Colins! Halafu katikati ya hiyo hali, analia akisema anakufa akiwa amepoteza mtu muhimu sana kwake, ambaye ni wewe. Watu wote wamesikia. Halafu usitokee! Kweli Colins mwanangu!?” “Basi mama.” “Huko kutoka na Jelini unaweza kutoka siku nyingine yeyote, lakini leo umepatwa na tatizo la kifamilia! Kweli Jelini atashindwa kuelewa hilo?” “Basi acha nikazungumze naye.” Akasimama.

 “Lakini mimi simtaki tena Love, mama. Na nilishakwambia. Huo ukurasa nimeshafunga. Tafadhali jaribu kuzungumza na baba. Mahusiano yabaki kuwa ni ya kifamilia tu.” “Baba yako hajalazimisha umuoe.” “Lakini ndivyo anavyotaka. Na wote tunajua. Mimi simtaki Love kama mke wangu. Mimi nimeishi naye, najua ninachozungumzia.”

“Kwa hiyo umeshamwambia Jelini kama unampenda?” “Siwezi mama yangu. Jelini yupo kipindi kigumu. Nataka kwanza angalau nimuonyeshe mimi nipo, na nimwaminifu ndipo nianzishe jingine. Kumbuka jinsi nilivyomuumiza mwanzo. Nahitaji muda zaidi. Sasa mambo kama haya yakitokea ndio atazidi kuniona mimi ni mbambaishaji.” “Huu si ubabaishaji. Ndio ukubwa na unaonekana ni mtu wa familia.”

“Au niende nikazungumze naye ana kwa ana.” “Hapana Colins. Najua hutarudi.” “Nitarudi mama.” “Ukiondoka hapa, iwe safari ya hospitalini Colins, na si vinginevyo. Umenisikia?” Wakasikia sauti ya mzee kutoka ndani.

Colins akanyanyuka kwa hasira na kutoka hapo. “COLINS?” Mzee akafoka kwa sauti. “SIONDOKI. Nakwenda kupiga simu.” Na yeye akajibu kwa hasira. “Taratibu ml..” Kabla mama yake hajamaliza, wakasikia mlango umebamizwa kwa nguvu kwa hasira. Mama yake alitegemea ndio maana alikuwa akimuwahi lakini akawa amechelewa.

Kisicho Riziki.

Colins akampigia simu Jelini. “Ukiniona jinsi nilivyopendeza hutaamini kama ni mimi! Mama mwenyewe amenikubali.” Colins akafunga macho kwa kuumia. Kimya. Jelini akadhani aliwahi kuongea kabla hajapokea. “Colins?” Akaita huku akiangalia simu yake. “Nipo Jelini.” “Nilifikiri naongea peke yangu!” “Nimekusikia. Ila nina habari si nzuri.” “Ni nini tena!?” Jelini akapatwa na wasiwasi. “Tumepatwa na mgonjwa. Inabidi twende hospitalini kama familia.” Jelini akashituka sana.

“Poleni sana! Nani mgonjwa na ni nini tatizo?” “Apendex ya Love ilipasuka alipokuwa kazini. Ndio amefanyiwa upasuaji.”

~~~~~~~~~~~~~~~~

Katikati ya mipango yao, nalo hilo limejitokeza. Ilikuwa Kasa, sasahivi ni Love anayeonekana ni kama hakwepeki, tena amebeba baraka za wazazi!

 Nini kitaendelea?

Usikose muendelezo…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment