Wakiwa
nyumbani kwa Bale, mwaka ukiwa ndio mpya kabisa. Tarehe moja. Kwani Vai alilala
hapo, akamuuliza swali Bale asijue hakuwa tayari na jibu lake. “Najua mwaka
huwa ukianza, watu wanakuwa wakijiwekea malengo tofauti tofauti. Wewe mwaka huu
una malengo gani?” Bale akafikiria kidogo. Akamuona kama amesita. Vai akacheka.
“Unataka ndege nini?” Bale akacheka akaona aseme tu.
“Ahadi
ya mguu mpya ni jumatano ijayo. Natamani nimalize hilo. Nijaribu tena
kuzungumza na Joshua, nione kama atanisaidia kutafuta kazi. Maisha yaendelee
kama si kuanza.” “Unamaanisha nini?” Akafikiria tena. “Maana mimi nilidhani ni
kama unaishi maisha tayari!” “Ndiyo. Lakini bado ninashauku ya kuanzisha
familia. Mke na watoto angalau wasiopungua watatu kurudisha jina la mzee wangu.
Najihisi ninawajibika. Kuacha hivihivi nitakuwa nimemuua yeye mwenyewe na
kumbukumbu yake yote.” Ikawa kama kengele masikioni kwa Vai.
Akapoa
kabisa. Akakumbuka alivyotolewa kwa Zinda sababu ya kutoshika mimba. Akaanza kuwaza.
Bale akamuona vile alivyopotelea mbali mawazoni hata asijue kama alikuwa
akimsikiliza. Vai akajua historia inajirudia. Ila Bale hajawahi kumtaka
kimapenzi! “Pengine ndio maana hajajisogeza kimapenzi kwangu, akijua siwezi
kuja kumzalia mtoto!” Vai akawaza, nakuanza kuumia.
“Mbona
kama nimekupoteza hapo katikati!?” Kimya. “Vai!?” “Nipo nilikuwa nikikusikiliza.”
“Unanidanganya bwana! Ni nini?” “Hamna kitu. Ila wakati ukizungumza, na mimi
nikawa nikijifikiria. Kwa muda fulani, nilijisahau.” “Juu ya nini tena!?” Akatulia,
ila akamuona jinsi alivyobadilika.
“Tafadhali
niambie Vai.” “Sio kitu cha kigeni. Nilishakwambia. Sema hayo malengo yako yamenikumbusha
uwezo wangu wakutozaa.” Bale akashituka moyoni, alishasahau. “Inamaana
kwangu mimi, kama ni kuja kuolewa, ni kuja kutafuta mwanaume aliyefiwa na
mkewe, tena aliyekwisha kuwa na watoto wakumtoshea, hataki tena mtoto hata
wakuunganisha udugu. Malengo kama hayo yako, hayawezekaniki tena kwangu.” “Kwa
nini unakata tamaa!?”
“Sikukata
tamaa, ila kukubali matokeo. Si kwa bahati mbaya. Ni chaguzi mbovu nilizofanya
zamani.” “Namaanisha ni kwa nini unajikatia tamaa yakutopata watoto tena?” “Kwa
sababu mimi si kama wewe Bale. Mwenzio niliishi na mwanaume unyumba kabisa, na
sikuwahi kushika mimba. Na si kwa mwanaume mmoja tu. Ni kote nilikopita baada
ya kutoa mtoto wa mwisho, ilishindikana. Kwa hiyo si kukata tamaa, ni
kukubali matokeo.” Bale akapoa kama aliyemwagiwa maji.
Tayari
hiyo siku ikabadilika. Kwa mara ya kwanza tokea wafahamiane wakicheka na kuwa pamoja
kwenye kila ghali, utofauti ukatokea katikati yao. Vai akajiona hastahili hata
kuwepo hapo. Baada ya muda akaona aage tu. “Tafadhali usiondoke Vai! Ni nini?” “Sijisikii
vizuri.” “Tokea lini ukijisikia vibaya hapa pamekuwa sehemu ya kukimbia na si
kukimbilia?” “Mpaka lini Bale?” “Sijui! Lakini kumbuka sisi ni mrafiki wa nyakati
zote. Tunazungumza na kubebana katika kila khali. Kweli unataka kuondoka na
mipango yote tuliyokuwa nayo ya jioni!?” “Acha nikatulie chuoni. Mwaka mpya
mwema. Tutawasiliana wakati mwingine.” Ikawa kama utani vile. Vai akaanza
kukusanya vitu vyake, Bale akimtizama. Mwishoe akakumbuka anakopitishwa. Akajirudi.
Akaanza
kumfungashia vyakula wakati akifungasha vitu vyake. Akakusanya mpaka akamaliza.
Akamuaga akiwa tayari na mizigo yake yote mlangoni. “Basi acha nikurudishe
chuo. Usiondoke kama umefukuzwa!” “Nakushukuru.” Akaingiza vitu vyake vyote
kwenye gari, na kuhakikisha haachi kitu hata kimoja. Ndipo akaingia garini na
kutulia, akagundua gari inanukia vyakula. Akajua inamaana amemfungashia
chakula. Ikamgusa Vai, akajikuta roho ikimuuma, asijue chakufanya. Alishapitishwa
kwenye hali yakukataliwa sababu yakutozaa, hakutaka kupita tena hapo. Lakini Bale
hajamfukuza, wala kumtaka mtoto. Hisia zilishajichanganya. Akawa haelewi tena
nafasi yake. Na upendo ukishazidi mahali, ni rahisi kujisahau.
Bale
akaondoa gari. Kimya kikazuka garini. Wakati wanakaribia chuoni, Bale
akamtizama. “Najua umekusudia kutorudi tena kwangu. Naelewa kabisa na nipo
kwenye kukubali kila adhabu Mungu anayonipa.” Vai akamtizama kwa mshangao. “Na
mimi hii hali ya upweke na kukataliwa, nilijitakia. Nilichagua kwa
maamuzi yangu mabaya. Sina wakumlaumu. Ila nataka ujue, nakushukuru kutoka
ndani ya moyo wangu. Umeyabadili maisha yangu kwa kiwango chake. Najua nisingekuwa
hivi nilivyo bila wewe. Ulikubali kupitishwa kwenye maisha yangu ukaweka
mabadiliko.” Vai akatulia.
“Kuna
mtu alinisaidia kwa kuniambia hivi, mimi ni zaidi ya huu mguu uliopotea. Na wewe
upokee hiyo. Wewe ni zaidi ya hicho unachojisikia moyoni mwako na kufikiri huna
uwezo wa kukipata. Na hata kama ukishindwa kupata mtoto, usipotelee kwenye
hilo. Una uwezo wa kuzaa vitu vikubwa zaidi ya mtoto peke yake. Wewe ni mtu
mzuri sana Vai. Umenitoa sehemu mbaya, ukanipa faraja. Unajua kuridhika hata na
vitu vidogo. Umejawa na furaha na utulivu wa aina yake. Unazalisha amani na
utulivu sehemu isiyo na tumaini kabisa.”
“Kwa hiyo kabla hujafikiria kumpa mwanaume mtoto,
jua unauwezo mkuwa sana wa kufanya jengo
likawa nyumba, sehemu ya mtu kukimbilia na akawa salama. Kitu ambacho nimekua,
sijakiona hata kwetu. Wewe unao uwezo huo Vai. Nilikuwa nikizitizamia siku au
muda wa wewe kuwepo pale kwangu kwa shauku sana. Maana ulijua kuweka hali ya
utulivu, furaha wakati wote, na amani. Huna hasira, hujui kunung’unika hata
kwenye ugumu. Kwa hakika naumia unaniacha. Lakini sina jinsi.” Vai
akatulia kimya. Bale akamfikisha chuoni kwao. Akaanza kushusha vitu vyake vyote
akirudisha chumbani kwake mpaka akamaliza, kisha akarudi kumuaga. Akamuhisi alikuwa
akilia peke yake garini japo hakumkuta na machozi.
“Mungu
hana hasira na wewe Bale. Alishakusamehe. Na naamini atakupa mwanamke mzuri tu
maana hata wewe unalipa.” Bale akacheka akimtizama. “Umeanza Vai.” “Kweli. Kwani
uongo? Unalipa Bale. Na unajua kujali sana. Binafsi sijawahi pata mtu
anayenijali kama wewe, mpaka najuta uchafu wangu wa zamani. Natamani kama na mimi
ningekuwa…” Akasita.
“Acha
nikupishe tu, ili uweze kufikia ndoto zako. Tusipotelee kwenye njia
itakayotufanya tushindwe au iwe ngumu zaidi kutoka huko pindi muda wakutakiwa
kutoka ukifika. Mimi nimeshapitishwa hapo zaidi ya mara moja. Ni chungu mno. Na
najua umuhimu wa familia. Ikishafikia muda wa watoto wanahitajika kwenye
familia, kunakosekana amani kabisa. Hata upendo mdogo unakuwa unapotea. Nitapita
hapo na yeyote, ila si wewe. Kwanza sipangi kuendelea kufanya huo mchezo. Nishajua
nilicho nacho na ambacho sina. Sitarudia kujiumiza tena.”
“Jipe
tu muda. Mungu atakupa haja ya moyo wako. Mke mzuri na watoto wazuri. Usirudi kwenye
swala la kama Mungu amekusamehe au la. Anaendelea kukuadhibu au la! Umesamehewa.
Na najua ipo siku utarudi kuiangalia hii siku, utajua nilikuwa nikikutakia
mema. Nataka upate unachotamani. Sitaki kuwa mbinafsi. Na kwa kuwa mimi
naelewa unachokitaka kwa kukiishi, acha tusipoteze muda.” Bale hakujibu kabisa.
Akabaki kimya, mpaka mishipa ya kichwa ikawa imemsimama. “Kwa kheri, Bale.” Vai
akaondoka, Bale akimtizama.
Kwa Colins&Jelini.
Wakatafuta namba mpya
ya Jelini, Colins akawa wa kwanza kuipata. Akajipigia na kuitunza kwenye simu
yake. Wakamtafuta fundi mbao ambaye wanafahamiana kwa muda mrefu tu na ndiye
aliyejengea makabati mapya ya kisasa hapo kwao. Akamuelekeza, wakakubaliana mpaka
rangi, na bei ikawa nzuri tu. Jelini akaridhika.
“Naomba na mimi
unisindikize.” Jelini akakubali bila ya kufikiria. Wakaongozana mpaka sehemu
wanayouza fast food na ice cream. “Mimi huwa nilazima nile kila mlo.
Lasivyo akili huwa haifanyi kazi, hata James anajua. Sipitishi mlo hata mmoja.”
“Pole nilikusahau. Akili haijatulia.” “Bado tu?!” Jelini akanyamaza, wakashuka
garini, wakatafuta sehemu ya kukaa.
“Utakula nini? Na
‘sijisikii’ naomba isiwe jibu, Jelini. Ili kuanza upya unahitaji akili na
nguvu. Usijitese na njaa wakati wenzio maisha yao yanaendelea kama kawaida. Na
si kwamba napuuza kuumizwa kwako, lakini nataka uvuke hapo. Wewe sio wakwanza
kuweka tumaini sehemu isiyo sahihi. Utakuwa sawa tu. Ila unatakiwa kujipanga.”
Jelini akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu, akajisikia vizuri.
Akatulia.
“Nikuagizie nini?” “Kwa sasa sijis..”
Akabadilisha maana alimwambia hilo si jibu. “Naona nitakula jioni nyumbani kwa
Jema. Sasahivi tumbo lipo kama limejaa gesi hivi! Acha litulie. Nahisi nikiweka
kitu humo ndio nitajiumiza zaidi.”
Colins akamtizama na kuondoka pale kwenda kuagiza chakula. Baada ya muda
akamuona anarudi na ice cream. Akakaa pembeni yake wala si mbele. Akabaki akimwangali
tu.
Akaifungua na kuchota na kijiko,
akamnyooshea kama amlishe. “Hiyo ni ice cream yangu au yako?” Akauliza kabla
hajafungua mdomo. “Naomba kula, Jelini!” “Siwezi kushiriki kijiko na wewe
Colins. Nina wasiwasi wakupita kiasi. Mpaka nikajipime tena.” Colins akabaki
akimwangalia. “Kumbuka maisha niliyokuwa nikiishi Colins. Watu kama mzee Kasa
na tabia zao, ndio walikuwa washikaji zangu baa. Nayajua maisha
wanayoishi kwa kuyashuhudia. Ni machafu kuliko nitakavyo kuambia. Ngono au kitu
alichokifanya Kasa, hata nikitokea kwao sasahivi nikawaambia kuwa ndicho kinacho
niliza, watanishangaa sana. Kwakuwa wao ni maisha yao ya kawaida sana.”
“Wake kwa waume hilo si
kosa lakusema wanaachana au kugombana. Ni maisha ya kawaida
sana, na jamii wameyakubali. Ndio maana mimi nilikuwa nikinywa nao, nakuogopa
sana kulala nao. Sikuwahi kukubali kushawishika kwenye hilo. Ni malaya, na
ngono ni starehe ya kawaida kama kunywa soda na kusahau hata aina ya chupa waliyotumia
kunywea. Ni kama kunywa hapohapo na kuagiza ingine. Niliishi nao nikishuhudia
wakifanya ngono kama wanyama.”
“Vyooni
huko baa na kwenye magari yao huku wakijisifu sio sabuni kwamba imeisha,
nakushindwa kupeleka nyumbani. Ikanitia kinyaa cha mapenzi, nikabaki kula na
kunywa nao tu, huku nikishuhudia miongoni mwao wakisambaza vijidudu vya UKIMWI
kwa makusudi.”
“Kwamba
kuna waliokuwa wameathirika miongoni mwao tayari!?” “Kabisa Colins. Na kusambaza
kwa makusudi. Ndio maana japokuwa mimi ni hovyo sana,..” “Wewe si hovyo.”
Colins akamkatiza kwa haraka. “Ninachotaka kusema, kwa udhaifu wowote nilio
nao, linapofika swala la kufanya mapenzi, hapo nimechora mstari. Sina kuzembea.
Maana nimeshuhudia kwa macho madhara yake. Starehe ya dakika 5 inaweza kubadili
maisha yako yote hata mafanikio uliyonayo yakageuka kuwa machungu.”
“Nilijipima
siku nilipoamka kwa Kevin nikiwa sijitambui. Nikiogopa sana inaweza kuwa nakuwa
hivyo halafu japo nawakataa nikiwa sijalewa, nikilewa nikiwa sijitambui pengine
wananifanyia mambo mabaya, sijijui.” “Na nilimsisitiza Kevin asije
akakosea akakugusa kwa namna yeyote ile kimapenzi.” “Nashukuru Colins.
Maana angeweza nifanya chochote na nisijue. Na nilijichunguza nilipoamka,
ukweli hakunifanya kitu. Ila nilikwenda kupima. Sasa safari hii najipa miezi
mitatu, nikapime tena kujihakikisha Kasa ameniacha bila maambukizi
yeyote yale. Tafadhali tusitumie kijiko kimoja. Roho yangu itaniuma sana
na sitajisamehe endapo nitakuja kukuambukiza.”
Colins akapooza haswa akabaki ameduaa.
“Kula
hiyo ice cream isiyeyuke.” “Ndio maana huna raha?” “Kabisa Colins. Naogopa mno.
Na najilaumu kukimbilia kwenye mahusiano na Kasa bila kumchunguza.
Nimejawa hofu, yakujitakia mimi mwenyewe.” “Pole. Ila nadhani yupo makini
kwenye mambo yake. Hawezi akawa anajiachia tu.” Jelini akakumbuka jinsi Kasa
asivyopenda kondumu ndio maana anapima na kila mtu anayefanya naye mapenzi!
Akakumbuka yeye alimpima mara moja tu, hakurudia kumpima tena. “Sasa na huyo
Koku anamaisha yake. Akirudi wanaendelea walipoachia. Nimejiua kwa ujinga wangu
mimi mwenyewe!” Akazidi kuingiwa hofu kila akikumbuka jinsi alivyojiachia
kwa Kasa. Akajua inamaana na kwa Koku ni hivyo hivyo, penzi bila kikomo, wala
kinga. Akazidi kunyongea.
“Niangalie
Jelini.” Ndipo akarudisha akili pale. “Usiogope.” “Siwezi
kujisaidia Colins. Wewe Ukimwi unausikia kwa watu, mimi nimeishi na mtu mwenye
vijidudu vya UKIMWI. Nikaona jinsi anavyoteseka kihisia akiwa wala si mgonjwa.
Ana kila kitu. Nikisema kila kitu, kwake na alivyo peke yake, naweza kusema
amefanikiwa haswa. Lakini amejawa hofu. Hawezi kulala bila pombe kichwani. Na
amejawa uchungu moyoni, ndiye huyo anayesambaza kwa kila anayemsogelea.
Ukimwangalia hivi, huwezi sema anavyo hivyo vijidudu. Mzuri na afya nzuri tu.
Ndio maana nilikuwa nikijihami.”
“Wale watu walikuwa wakisema kuonja sio mbaya. Sasa hebu
fikiria, ni wangapi wameonja kwake, na kupeleka huko wanakokula? Na huko
wanakokula kwa wenza wao nao wanaenda kuonjwa na wengine, na hao wengine
wanapeleka kwengine. Havijamfikia mtu kama Kasa kweli, tena mwenye pesa na
kujua kuhonga vile? Mimi je?” “Acha kujitia hofu zaidi Jelini bwana!” Jelini akajifuta
machozi.
“Sio kujiogopesha. Nakumbuka dereva wake siku moja aliropoka
nakusema huwa analeta wasichana wengine pale kwake, lakini huwa hatoki
kuwapokea kama mimi.”
“Jelini!!” “Kweli Colins. Sasa sasahivi ndio
najiuliza nilijiachia vipi! Na kujiaminisha vipi? Maana nilimuuliza, akasema
atabadilika, tubaki peke yetu.” Colins akavuta pumzi kwa nguvu na
kuzishusha taratibu.”
“Sasa
nisikilize Jelini. Huna njia yakubadilisha nyuma ila kuanzia sasa. Tulia mpaka
muda uliojiwekea ufike, nitakusindikiza kupima.” “Na
kama nimeathirika?” “Hiyo ni kesho. Naomba tuishi leo. Na najua ukiwahi,
unaweza kuanza kutumia dawa na ukaishi vizuri tu. Namfahamu mtu anayeishi na
hivyo vijidudu. Ila yeye nimesikia akisema, ameacha kabisa kujamiiana.
Anazingatia mlo na dawa. Ukimuona hivi, huwezi kujua aisee. Yupo safi, ila
mwenyewe ameamua kujitangaza. Hafichi. Na ana maisha mazuri tu. Naomba utulie.
Sawa?” Jelini akavuta tena pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu Colins
akimsaidia kufuta machozi.
“Naomba
ule hii ice cream. Fungua mdomo mimi nitakuwekea.” Jelini akacheka. “Sio kwamba
ndio nina hali mbaya kiasi hicho bwana! Naweza kula mwenyewe, ila sijisikii.”
Akasimama na kwenda kuchukua chakula. Akarudi na chakula alichoagiza ila mara
mbili yake, na ice cream nyingine mbili na vijiko viwili. Ile ya mwanzoni
akaitupa na kurudi tena pale. “Unataka tukae hapa tule au tukale kwenye gari?”
“Ningependa kwenye gari zaidi.” “Basi twende wakati ukila hiyo ice cream
isiyeyuke tena. Haitakuwa nzuri.” Wakatoka akiwa amebeba vyakula, Jelini
anakula ice cream.
“Kuna
sehemu sio mbali sana na hapa. Patulivu, tunaweza kwenda egesha gari tukala kwa
utulivu.” Colins akakubali, wakatoa gari mpaka hiyo sehemu. Akamkabidhi maji na
chakula. “Sikujua ungependa kinywaji gani, nimekuchukulia maji tu.”
“Nashukuru.” Akapokea, wakaanza kula huku wakisikiliza mziki. “Una nyimbo nzuri
Colins! Zinakufanya unatulia.” “Nimefurahi kama na wewe umependa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Nikuulize
kitu Colins?” Colins akamwangalia. “Juu yako na Love.” “Unataka kujua nini?”
“Ni katika kujifunza tu. Mmekuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa muda gani?
Na mlikuwa na malengo gani?” “Baba yangu na baba yake walikuwa shule pamoja
pale Muhimbili. Kwahiyo na sisi tukakulia pale kwenye magorofa ya Muhimbili.
Tulikuwa pamoja tokea shule ya msingi.
Wazazi wakaamua kujiendeleza shule. Ni marafiki tokea vijana. Tukajikuta tuko
pamoja tena huko ugaibuni. Tukaanza tena shule huko nje ya nchi. Pamoja tena,
wote tukiwa watoto wa kwanza kwenye familia zetu, na kina mama marafiki. Kina
baba walipomaliza, kina mama walipoona elimu ya huko ni nzuri, wao wakabaki na
sisi ili kumaliza shule. Kwa hiyo tukaishi tena nje ya nchi pamoja na kina mama
nao wakaanza masomo ya unesi.”
“Sisi
tulipoanza chuo kwa shahada ya kwanza ndipo tukaamua kujaribisha mahusiano ya
kimapenzi. Wakati tunakaribia kumaliza, kina mama, Connie pamoja na mdogo wake
Love, wakarudi nchini. Nikabaki naye huko. Ilikuwa mbaya sana. Hatujawahi
kupitia wakati mgumu kama huo. Tukajua kabisa, hatutaweza kuja kuona.”
“Kwani mliishi pamoja?” Colins akawa kama anayefikiria jinsi ya kujibu hilo
swali.
“Tulipoachwa
sisi wenyewe tukiwa chuoni, tukajiamulia tuchukue apartment moja yakututosha
sisi. Yalikuwa maisha mabaya sana, lakini ilitusaidia kujua hatima yetu.
Ikawa tena tunabaki kwenye mahusiano sababu ya wazazi. Anyways. Akataka
kufanya kazi kule baada ya kumaliza chuo, mimi nikawa nimeshachoka maisha ya
kule, ndio nikaja kuanza kufanya kazi huku. Ikawa anakuja likizo na kurudi.
Akapata kazi anayofanya sasahivi kwa ahadi ya mshahara mkubwa sana. Na kwa kuwa
alishafanya kazi kule, ilikuwa rahisi kuzungumzia mshahara mkubwa. Ndio akarudi
nchini sasa.”
“Tukajaribu
tena, lakini binafsi nikaona nitapoteza muda wake zaidi. Siwezi kuwa kile
anachotarajia. Hakuna kitu ninamfanyia kikawa sahihi, na nafikiri nilikueleza.
Mapungufu mengi akawa anayalalamikia, na mimi nikachoka. Nikiwa katika hiyo
hali ya kuchoka, nikagundua kumbe na mimi naweza kupendwa zaidi ya
muonekano wangu ambao na mimi nadanganywa na wengi tu, wakivutiwa na
muonekano wangu.” Jelini akainama kwa aibu. Maana kweli Colins alivutia
machoni.
“Nilipoona
nashikilia sehemu ninayoumia, wakati naweza kupendwa na nikatulia, ndipo
nikaona nisiendelee kujipunja. Nikahitimisha. Ila malengo ilikuwa kuwa na
familia kama wazazi wetu. Inamaana kuja kuoana na kuanzisha familia pamoja.”
“Alichukuliaje ulipomwambia unahitimisha?” Jelini akarudia swali akitaka uhakika.
“Alisema sawa, Jelini. Unakumbuka nilishakwambia?” Jelini akatulia akiwa
kama hajaridhika maana amemuona nyumbani kwao.
Akaamua
kuuliza tena. “Kwahiyo sasahivi yupo kama nani?” “Kama mtoto wa nyumbani. Love
ni kama mimi pale kwetu, na mimi ni kama kijana wa nyumbani kwao tu. Tumekua
pamoja na wazazi wetu ni marafi mno.
Jinsi baba zetu walivyosoma pamoja, ndivyo mama zetu wakaja kusoma tena pamoja,
elimu ya utuuzimani. Ila mama yake Love alikuja kujiendeleza zaidi. Mama
akashindwa akitaka kumlea Connie. Hawafanyi kitu bila kuambizana na kila kitu
wanafanya pamoja japo baba sasahivi amehamia kwenye mambo ya moyo. Ila wenyewe wanasema
ni faida yao wote. Wanaongeza utaalamu kwenye kliniki yao.” “Kwamba wana hospitali
yao pamoja!?” “Sio hospitali ni kliniki. Hawalazi. Ni kuona tu wagonjwa.”
“Mmmh! Nyinyi mngeoana tu ndio ingependeza.”
“Kila
mtu alifikiria hivyo. Lakini mwishoe kila mtu akatuchoka. Yaani kutengana kwetu
ikawa tena pumziko kwa kila mtu kwenye familia. Walishatuchoka kwa
mashitaka ya Love. Na mimi nilikuwa sina raha! Nahangaika kama
anayekimbiza upepo! Ikatosha.”
“Swali
la mwisho.” Colins akacheka. “Naona umeniamulia! Haya uliza.” “Kwa maisha
uliyoishi na watu wanaokuzunguka. Hivi kweli wewe utakuja kuoa au kuwa na
mwanamke ambaye sio msomi kweli?” “Kwa haraka, sijui. Maana nilijaribu
na msomi, ikashindikana. Ikaniashiria mapenzi si shule. Si kile
mlichobeba kichwani ila moyoni.” Hapo Jelini akatulia. “Umeridhika?” Jelini
akatingisha kichwa kukubali na tabasamu.
“Ukitoka
hapa unampango wa kwenda wapi?” “Maisha ya kazi yanaanza rasmi kesho, Colins.
Nataka kujiandaa. Kufua na kuweka kila kitu sawa kabla ya jioni sijaenda kwa
Jema. Si na wewe utakuwepo?” “Wewe ulitaka niwepo?” “Mimi nafurahia kampani
yako Colins. Ningependa uwepo. Ila kama una..” “Nitakuwepo. Nishamwambia James
nitakwenda na si nilikwambia hata kina mama waliahidi watapitia?” “Nakumbuka.”
“Basi tutakuwepo wote. Kuna kitu unataka kabla sijakurudisha nyumbani?”
“Hapana. Ila nashukuru kwa chakula. Najisikia vizuri.” “Usiache kula bwana!
Utanyongea. Na punguza hofu. Naamini kila kitu kitakuwa sawa.”
“Najihisi
nimejipokonya tonge mdomoni, Colins.” “Kwa nini?” “Mwenzio zamani nilikuwa hata
siwazi mambo ya kesho. Mambo ya mipango mizito! Hapana. Nifurahi leo, kesho
itajijua yenyewe. Lakini kadiri nilivyokuwa nikimwangalia Jema na James, tamaa
ya kuwa na walichonacho ikanipata. Eti na mimi nikatamani niwe kama Jema na mtu
wangu na familia yangu. Lakini najifikiria kama nimeathirika, hayo yote
ndio basi tena!” “Naomba usifikirie huko. Bakia kwenye hii shauku yako.”
“Siwezi kuepuka Colins. Sitaki nijipandishe mukari halafu nije nijikute siwezi
kuvipata vyote hivyo! Acha nitulie mpaka nijue hatima yangu. Na asante
kunisikiliza. Naona upo sahihi. Nikizungumza hivi na wewe, angalau napunguza
hofu.”
“Basi
muda na wakati wowote unapojisikia kuzungumza na mtu, nipigie. Hata kama ni
usiku, mimi nitakuwa na wewe. Na naomba tena, Jelini. Najua ni ngumu. Lakini
naomba upunguze hofu. Ukianza kujisikia hofu, tafadhali vuta kumbukumbu
kwenye unaloweza kufanya. Au furaha fulani ili kutoa mawazo kwenye hofu. Usikae
kwenye hofu kwa muda mrefu.” “Nitajitahidi. Twende na wewe ukapumzike.”
“Mwenzio hata ukiniambia nikae na wewe mpaka usiku, sitachoka.” “Kweli
Colins?!” “Si nimekwambia nataka kuwepo ulipo?” “Hujachoka kusikiliza
matatizo?” “Nataka matatizo yako nikusaidie kuyabeba. Usiwe peke yako.”
Jelini akamwangalia na kutulia.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akaondoa
gari na kutoka hapo kurudi nyumbani kwa kina Jelini. Akadhani anamshusha
aondoke, akashangaa anaingia naye ndani. “Ndio unajiandaaje kwa kazi?” “Nafua.
Tokea nitoke safari sijafua.” “Unafulia wapi?” “Nje. Ingekua mama hajaninyima
hela, ningeshamuita mtu ninayemlipa anifulie.” Jelini akanong’ona, mama yake
asisikie. “Kwani huwa hufui?” “Sipendi. Ila acha tu nifue.” “Kwetu kuna mashine
ya kufulia. Chukua nguo chafu zote tukafulie kwetu.” “Mwache afue huyo. Hivyo
humsaidii.” Wakamsikia mama Jema akizungumza kutokea chumbani kwake.
Wakanyamaza gafla wakiangaliana.
“Umesikia
we Jelini?” “Kama una nguo chafu nitolee nifue na za Jeremy mara moja.” “Uje
uchukue huku chumbani.” Akaenda akicheka. “Kwani kusaidiwa ni vibaya mama
jamani!?” “Utasaidiwa mpaka lini Jelini, mama yangu? Si umesema unataka kuwa
kama Jema? Ndio anza kwa kuanza kujitegemea. Acha misaada ikukute upo njiani na
umesimama. Unataka kuanza tena maisha mengine, halafu vikiishia katikati uanze
tena kulia?” “Basi mama. Naenda kufua mwenyewe. Nipe hizo nguo zako na za
Jeremy.” Akamtolea nguo, kweli Jelini akatoka nje na nguo zote. Akatafuta
kivuli, akakaa kabisa.
Colins
akamfuata. “Pole.” Akaanza kucheka. “Mwenzio huwa sifuagi. Na sipendi.
Nilikuwa nikiwa na kijihela changu, namuita mtu ananifulia na kunipigia pasi
kabisa. Acha tu nifue. Kwanza hizi sio nyingi. Nitamaliza sasahivi. Wewe nenda
kapumzike.” “Acha nikae hapa. Nikuwekee mziki wakati unafua.” Ikaanza kazi ya
kufua na mziki. Colins anaenda ndani kumuangalia Jeremy, anarudi nje kwa mama
yake mpaka akamaliza.
Baada
ya kuanika, wakahamia chumbani kupanga. Jua kali na uchovu, Colins akajilaza
kitandani na simu yake akibadili nyimbo, Jelini anapanga chumba mpaka
akamaliza. Akaenda kuoga chumbani kwa mama yake, akarudi ameshavaa, Colins bado
yupo amejilaza kitandani kwake, haondoki.
Akajipandisha na yeye kitandani. Colins akajisogeza. “Pole, najua umechoka.” “Nasikia na usingizi.” “Njoo nikubembeleze ulale.” Jelini akaanza kucheka. “Nakuahidi utalala vizuri.” Jelini akageuka kumpa mgongo. Akavuta mto juu ya kichwa chake, akawa kama anamchungulia kwa chini, ila karibu kabisa, Jelini akizipata pumzi zake sawia. Akaanza kumpapasa mkono kwa juu mpaka karibu ya bega. Ile kuguswa tu na Colins, kuwa karibu yake vile, roho ya Jelini ikatulia kabisa. Hapo hapo wote wakapitiwa na usingizi mpaka hodi ya mama Jema ikawatoa usingizini.
Saa moja usiku, nje kumeshakua giza! Kuangalia, wamelala hapo kitandani kwa Jelini wamekumbatiana ila Jelini amempa mgongo vilevile. Colins akambusu karibu na sikio na kumsisimua vilivyo, akatoka akiaga anakwenda nyumbani kwake kuoga, watakutana nyumbani kwa Jema. Jelini naye akawahi kujitayarisha.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Mimi
sielewi Jelini! Sasa huyu kijana amehamia hapa au?” “Mimi sijui ila
namfurahia.” “Jelini wewe mtoto?!” “Mimi hata sijielewi. Lakini nilikuwa
nampenda hata kabla ya Zenda.” “Jelini! Imekua kumpenda tena?” “Si kihivyo mama
jamani! Ila napenda kuwa naye. Ndio wakati ule akasema ana mtu wake na wewe
nilikwambia kabisa.” “Mimi ningeshauri utulie kwanza ujue hitimisho la Zenda.”
“Hitimisho gani tena?! Kwanza si Zenda, ni mzee Kasa.” “Angalau pata muda wa
kujifikiria kabla hujaanzisha kingine.” “Mimi sianzi jambo lolote na Colins.”
“Sasa usikasirike.” “Naona na wewe unataka kumfukuza kama mzee Kasa
alivyomfukuza! Mimi sipendi mtu amfukuze Colins.”
“Kwa
hiyo ulikuwa na Zenda huku mawazo yapo kwa Colins?” “Mimi sijui. Ila naombeni
mumuache Colins. Ananipa moyo na…” “Kukuweka mkononi?” Mama yake akamkatiza kwa
kumalizia kwa swali akimkejeli, akimjua jinsi anavyopenda mikono. “Mimi nataka
kusema yupo na mimi wakati ninaomuhitaji bila kuchoka. Mtu asimfukuze.
Nitafanya kila kitu utakachoniambia ila si Colins.” Jelini akaondoka na
kumuacha mama yake akimtizama.
~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment