Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 39. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 39.

Jelini akamfuata mpaka kwenye gari yake. Akamtolea simu. “Angalia hii.” Jelini akapokea. “Sio mpya, lakini..” “Nzuri sana na inafanana kidogo na hiyo ninayotaka kuiuza!” “Unaweza kuichukua.” “Siwezi Colins.” Akamrudishia kabisa na kurudi nyuma. Kisha akaondoka kurudi ndani.

Colins akafunga gari na kumfuata chumbani kwake akiwa na hiyo simu. “Sijaelewa!” “Hapana Colins. Mimi huwa sipokei vitu hovyo. Sio mimi na siwezi. Kwanza kwa nini unipe kitu cha thamani kiasi hicho?” “Kwa hiyo akikupa Kasa unapokea, mimi unanidharau, unaona sina uwezo wa kukupa?” Jelini akashituka sana. “Hapana Colins! Mimi sikudharau! Lakini mimi si mtu wakupokea vitu hovyo. Isingekuwa hivyo sasahivi ungekuta nina mavitu mengi sana.” “Ndio nauliza, vyangu vina tofauti gani na ulivyokuwa ukipokea kutoka kwa Kasa? Tena mpaka kumfikia mwanao!” Jelini akakunja uso.

“Unafikiri sijajua kama zile LEGO anazojenga sasahivi Jeremy zimetoka kwa Kasa? Mbona zilipokelewa na zinatumiwa?” Jelini akapoa. “Sikuanza tu kupokea vitu vyake, Colins! Kumbuka ni kama tulikuwa kwenye mahusiano. Au niseme nilidhani nilikuwa kwenye mahusiano naye! Nikaweza kumuamini.” “Kwa hiyo unachotaka kuniambia, ni unamuamini yeye kuliko mtu mwingine yeyote yule hata mimi!? Na umefunga huo mlango ili abakie yeye tu?” “Hapana Colins!” “Ila ni nini?” Jelini akatulia akifikiria.

“Jelini?” “Tafadhali nipe muda Colins. Naomba nichukulie taratibu. Nipo kama nimechanganyikiwa! Nataka kuanza taratibu. Si kwa..” “Kupokea msaada wowote kutoka kwangu?” Jelini akavuta pumzi kwa nguvu. “Njoo ukae hapa.” Akamuonyeshea pembeni yake. Colins akakaa.

“Naomba nikuombe kitu Colins.” Akatulia akimwangalia. “Nipe muda kidogo nianze kujipanga kichwani kwangu kwanza. Kama ungefungua kichwa changu, kama ni mafaili yalikuwa yamepangwa kwenye kabati, basi ungeyakuta yameanguka na kuzagaa kila mahali.” “Na mimi nipo hapa kuhakikisha tunayaokota, na kuyapanga kuanzia mwanzo, bila ya kukosea wala kufanya makosa. Labda uniambie hutaki MIMI niwepo.” “Nataka Colins. Unajua nafurahia uwepo wako.” Akatoa simu na kumkabidhi.

“Tunaanza kwenye swala la mawasiliano kati yetu. Hatuwezi kuanza kupanga au kufanya chochote bila mawasiliano. Mfano leo asubuhi nilitaka kujua uliamkaje, nikashindwa kwa sababu hukuwa na simu. Ushafikiria wakati mwingine tukiwa na jambo la msingi la kuzungumza, tutafanyaje?” “Taratibu Colins! Siwezi kuwa na kila kitu kwa wakati mmoja.” “Basi kwenye swala la mawasiliano tuwe tumemaliza. Na kwa taarifa yako tu, mimi ni mpenzi sana wa simu. Si kwa muonekano au kupambana na toleo jipya, ila kwa kila kitu kipya wanachoongeza kwenye simu. Huwa nanunua kwanza kujifunza na kunufaika na ongezeko jipya la kitekinolojia. Kwa hiyo kwa kifupi, huwa sinaga simu za zamani.” Jelini akaanza kucheka.

“Colins ukikazania jambo wewe!” “Naona unataka kuninyima mawasiliano bila sababu!” “Nashukuru.” “Twende ukale, kisha tukasajili namba mpya.” Akamuona kama anayefikiria. “Ni nini tena!?” “Kuna sehemu nataka kwenda. Utanisindikiza?” “Mbona swala la chakula huzungumzii? Au unataka kupungua zaidi? Maana umepungua sana Jelini.” “Nilikuwa nikilala na pombe mwilini ndio maana. Nafikiri bia ndio zilikuwa zikininenepesha, lakini si kula wala kupanga kupungua. Mimi mlaji. Ila sema sasahivi nina mambo mengi, hamu ya kula imepungua.” “Sasa itabidi ujibidishe. Unatumia dawa, lazima kula, lasivyo utaharibu tumbo kwa kuweka madawa bila chakula. Una hamu ya kula nini?” “Sina. Pengine nikiona mambo yangu yanakwenda vizuri, nitatulia.”

“Sasahivi unataka nini?” “Mimi nina matumizi mabaya sana ya pesa, ndio mama anataka kunisaidia. Ila natamani kuweka vitu vizuri chumbani kwa Jeremy, sina hela. Sasa nataka kuchukua kilichokuwa kitanda changu na makabari yangu ya zamani pamoja na vingine nilivyotoa humu chumbani kwangu na kwa mama, nimuombe fundi kama anaweza kuvibadili kwa muundo nilio nao kichwani. Kisha apake rangi nzuri, aje aniwekee chumbani kwake wakati nikijipanga upya. Ila kwa jinsi nilivyofikiria, na yule fundi alivyo, nahisi atatoa kitu kizuri tu. Twende.” Wakatoka hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~

Ndani ya gari ya Colins, aliweka nyimbo zilizoanza kumtuliza Jelini. Akacheka. “Nini?” “Hayo maneno yake mazuri sana. Wewe ulishawahi kubahatika kuambiwa hivyo?” Colins akacheka na kutulia. “Mbona kama unasita kusema?” “Wewe ulishawahi kuambiwa hivyo?” “Kwa kumaanisha, bila kudanganywa, hapana kwakweli. Kama ingekuwa kuna mtu ananiambia hivyo na hanidanganyi, si ningemng’ang’ania!” Colins alicheka sana.

“Kwamba usingemuachia?” “Sasa utake nini tena hapa duniani?” “Na mimi hivyohivyo, Jelini.” Wakacheka na kutulia kuendelea kusikiliza lakini Jelini hakuwa ameelewa jibu la Colins. Alimaanisha zaidi ya hivyo alivyozungumza na yeye akajua Jelini hajaelewa. Ila akamuacha tu. Akamuona ameweka mkono wake mmoja kwenye moyo kama ameushikilia ila ametulia haswa, macho nje ya kwenye gari kama aliyepotelea mawazoni.

Kuliko Ungua Mpini, Kukabaki Jembe.

Wakati Jelini akiliwazwa na nyimbo, huku kwa kina Kasa mwaka ulianza vibaya sana. Mzee alitumia pesa yake kuhakikisha Koku, Kevini, Kemi na mumewe, hawatoki jela kwa dhamana yeyote. Maana hata aina ya kesi aliyoandikisha, wasingeweza kutolewa dhamana. Walikuwa wakikabiliwa na kesi ya kusudio la kutaka kuua. Mama yao akahangaika huku na kule akiwa mbali, akitaka kuwasaidia nakushindwa. Kwanza aliogopa kurudi nchini kwa ajili ya hilo, akijua Kasa amekasirika haswa, kinaweza kumpa kilichowapata wanae. Lakini hata kwa simu, alijua yeye ni mtu wa mwisho kabisa anaweza kumsikiliza.

Baada ya hangaika ya muda mrefu akigonga mwamba kila mahali, akamtafuta rafiki yake mkubwa Kasa. Ambaye yeye huwa anajua kuzungumza na  kichwa cha Kasa na wakaweza kuelewana. Akamueleza bila kwenda kwa undani ila tu kutupa lawama kwa Kasa kwamba amefunga watoto wake na mume wa Kemi. “Haiwezekani!” “Nakwambia kweli tena. Eti sababu ya mwanamke! Kweli? Tafadhali nisaidie, Mgisha kaka yangu. Watoto wa Kemi ndio wameachwa peke yao. Hivi nimewaita. Ndio wamefika leo.” “Aisee nakwenda kuzungumza naye sasahivi.” Akatoka Mgisha akiwa amepatwa na mshangao haamini.

~~~~~~~~~~~~~~~

Mgisha rafiki wa karibu sana wa hiyo familia. Alisoma na Kasa enzi hizo za chuo kikuu cha Makerere kinavuma mno. Wakawa miongoni mwa watanzania wa mwanzoni wazazi waliomudu kupeleka watoto wao huko. Wamekua karibu tokea hawajaoa.  Kasa akaja kuoa mwanamke anayetokea sehemu moja na Mgisha. Ndio mahusiano yakazidi. Na hata walipoachana, bado wakabaki kuwa marafiki. Na yeye amefanikiwa sana kwenye maisha kama Kasa tu.

~~~~~~~~~~~~~~~

Akatoka na kwenda nyumbani kwa Kasa. Akamkuta. Alishajua kilichompeleka kwake ila akamuacha tu. “Nini kinaendelea Alex?!” “Nina hali mbaya, Vincent. Sina uwezo wa mazungumzo ya kuzungushana. Nenda kwenye kilishokuleta.” “Kwa nini umefunga watoto wote jela?” “Dada yako amekwambia  sababu. Kwa nini kuja kunisanifu?” “Kweli mwanamke ndio anakufanya hivi Alex?!” Kasa akakaa vizuri akiwa amejivuta mbele kabisa ya kochi hata kuegemea aliacha akihisi anachotaka kuzungumza hakitaeleweka.

“Niambie ukweli ila naomba ufikirie kwanza.” Mgisha akatulia akimsikiliza. “Wewe katika maisha yako yote. Ulishawahi kupendwa kwa dhati wewe kama Vincent? Sio kama Vincent Mgisha! Namaanisha mtu akaweza kukutenga na hilo jina lako la Mgisha. Akaweka pesa yako yote pembeni, shule yako, mafanikio yako yote huku akijua wewe ni nani, lakini akakupenda kama wewe Vicent? Hivyohivyo jinsi ulivyo. Na kuwa makini na jibu lako. Maana sisi tunafahamiana tokea vijana wadogo sana, Vincent. Ulikopita, ulikooa, kote mimi napajua. Niambie ukweli.” Kikapita kimya cha muda, Kasa anampa muda wa kufikiri.

Akamuona kama amechanganyikiwa. “Ndio inakuaje!?” Mgisha mwenyewe akakwama. “Basi hilo swali mimi lilikuja kujibiwa kwa vitendo. Yaani unapata mwanamke, huna unachompa kikamshitua nafsi, kama kumpa uwepo wako.” “Haiwezekani!” “Nakwambia hivi, hata ukimpa gari, halimshitui kama kumuweka mikononi. Ukamtuliza. Hajawahi kuniomba hata shilingi na anajua mimi ni KASA. Ndio nakuuliza, ulishawahi kumpata huyo mwanamke Vicent? Tokea tupo Makerere?” Akamsaidia kumfafanulia, na kurudia swali.

“Sasa kule si kila mtu alikuwa akitujua sisi ni kina nani!” “Ewaa! Na hapa nyumbani si tulioa hawa wanawake hivyohivyo kwa majina yetu tu?” Kimya. “Wanawake wote tunao lala nao unafikiri ni kwa nini wanakubali kuwa na sisi, na inachukua muda gani tokea umuweke karibu tu hata kwa kinywaji tu, hajakwambia mahitaji yake yote?” “Kwa kweli kwangu ni wote. Kila anayenisogelea ni pesa. Na hili tulishazungumza Alex. Unajua!”

“Basi kwa mara ya kwanza mimi na umri huu, nilibahatika kupata mtu wa namna hiyo. Binti mdogo tu, lakini Vicent?” “Ehe!” “Mtoto alinipenda mimi kama Alexender. Kwa mara ya kwanza, mwenzio nilionja tulichokuwa tukikitamani. Huna pesa, wala zawadi utampa yule mtoto ikamchanganya kama kuwa naye. Hajui kuomba pesa, ila mimi tu. Yaani nikiwa naye, anajawa na furaha kwa kunishika mimi kama mimi. Huna wakati utafanya naye mapenzi umkute hayupo tayari, kuashiria akili zake zipo kwangu. Nimemchunguza na kumtega, mimi mwenyewe nilikosa sababu! Sikuwahi kumtaka muda na wakati wowote nikamkosa. Alitaka niwe na furaha, mimi kama mimi Alexender, muda wote.”

“Lakini dada yako na watoto wake, wamepanga njama, wakamtumia Koku kuja kuniharibia.” “Haiwezekani!” “Hivi nilikuwa nikimngoja aje hapa nchini, nilipanga nimkamate na yeye, nimuweke jela. Nimuadhibu yeye na watoto wake mpaka wakome. Angalia hii video.” Akamkabidhi simu yake. Akamuonyesha ile video iliyoonyesha Kemi kumtega Jelini mpaka akaanguka na kupasua uso. Mgisha alishituka mpaka akataka kutupa simu.

“Sasa nilimuonya Kemi na kumfukuza kabisa pale ofisini nikijua kwa tabia hiyo anaweza kufanya kwa mwingine na kunisababishia matatizo. Nilimwambia Kemi, huyu mtoto nampenda. Amuache kabisa.” “Hajawashitaki?” “Huwezi amini Vicent. Huyu binti alinionya hata nisiwaambie watu, wasijue hiki alichafanyiwa na Kemi. Hata mama yake mzazi hajamwambia ili nisije ingia matatizoni! Kemi amemuacha huyu binti na kilema au tatizo ambalo itachukua muda mrefu sana na pesa nyingi sana kurudia kama alivyokuwa. Sasa hiyo si mbaya. Mbaya ni hii.” Kasa akajivuta zaidi mbele kama anayemsogelea Mgisha, mgongo hautaki kuegemea.

“Ipi tena?!” “Ulishawahi wewe kufumaniwa? Nikimaanisha sio kukutwa uchi kitandani. Namaanisha kushuhudiwa ukifanya mapenzi, mpaka unamaliza? Kwamba si kufumaniwa, ni kushikwa ugoni, ukifanya mapenzi?” Kimya. “Basi mimi imenikuta Mgisha.” Mpaka Mgisha mwenyewe akapoa.

“Huyu binti akiwa safari. Kina Kemi wakiwa wamejipanga…” Akamsimulia kila kitu, Mgisha akapoa kabisa. “Ndicho kilichonipata mimi.” “Mimi huwa nakwambiaga ukweli Alex. Na hapa nitakwambia. Mimi ningekua wewe, nisingefanya ulichokifanya.” Hapo akataka kumtibua.

    “Nini!?” “Usikasirike maana sisi huwa tunaambiana ukweli mtupu usioweza kuusikia kwa mwingine. Kuanzia asubuhi umeamka pembeni ya Koku, mpaka hapa tulipokaa, ulifanya kila kitu kwa kupaniki huku ukijua fika sisi ni kina nani na laana tuliyobeba.”

“Unakumbuka tulifika mahali mimi na wewe tukajiuliza kama haya mafanikio ni baraka au laana? Unakumbuka?” Kimya. “Hapajawahi kutokea mahusiano kati yetu na yeyote yule, tena tukasema mpaka watoto tuliozaa wenyewe, wanatutafuta sababu ya tulicho nacho si kwa mapenzi. Kweli leo uje ubahatike, halafu uje uniambie ulikuwa ukilipa fadhila! Come on Alex! Si kweli na si kwa Koku ambaye wote tunajua yupo alipo kwa ajili yako! Sikatai anayo akili kichwani, lakini kila kitu chake ni wewe. Na ulishasema, kuja kumuoa yeye ni kurudia kosa. Iweje leo utupe bahati kwa ajili ya mtu kama Koku?” “Ilikuwa ni kumtoa tu hapa!” “Hapo sasa unajitetea, kitu ambacho si kawaida yako. Na usifanye hivyo. Inakufanya uonekane weak. Dhaifu mno. Na sisi hatuko hivyo.” Kasa akapoa kabisa.

    “Baada ya hapo, kila kitu unafanya kwa kupaniki, ukiadhibu watu wote, ila mimi na wewe tunajua ni kwa sababu ya makosa yako Alex. Si wao. Wewe ndio umekosa. Umefumaniwa ukiwa hujalewa! Na Koku si mgeni hapa! Au niambie ni lini ulimpigia simu kumwambia upo kwenye mahusiano, hutaki kuja kumuona tena hapa?” Kasa akapoa kabisa kama si yeye.

    “Koku ni zimwi lako ulilofuga. Na hutaki kumuachia kwa sababu unajua halitakukula mpaka kwisha. Wewe mwenyewe umeshindwa kukata mahusiano yako na Koku ndio maana imekua rahisi kwake hata kumtusi Jelini mbele yako akijua yeye ndiye wakudumu. Angejua wapi umuhimu wa Jelini kwako bila wewe kumtambulisha kwake?” Kimya.

    “Ilichukua muda gani kwa Jelini kujua kama yupo Koku?” Mgisha akamuuliza kwa kumsuta. “Kwa sababu Jelini mwenyewe aliuliza tokea mwanzo! Hakutaka aina ya mahusiano kama niliyokuwa nayo na Koku. Na mimi nilimpenda, sikutaka kumdanganya ndipo nikamtaja Koku lakini si kwa sababu nampenda sana Koku.” “Pengine hukuwa ukilijua hilo. Ndio nakufungua macho Alex. Inawezekana Koku ndio anamaana kubwa kwako kuliko Jelini, ndio maana ulikuwa radhi kumridhisha asiondoke hapa kwako akiwa hana furaha, ukimsahau Jelini. Akili yako inaweza kukuaminisha chochote ungependa kikufurahishe, ila moyo wako upo kwa Koku. Sasa hivi unaadhibu watu wasio na hatia.”    “Unawezaje kusema hivyo Vicent!?” 

    “Wote wanao nufaika na sisi hawataki tufe ili waendelee kujinufaisha na sisi. Mimi nalijua hilo, na wewe unalijua hilo. Hayupo aliye tayari kurithi kwa kuwa tumezaa watoto wasio na uwezo na nidhamu ya kazi kama sisi. Wao wanajua, mimi najua na WEWE unajua. Na wanaakili yakujua, siku tukifa, haitachukua muda mrefu na wao watafilisika. Wote tunajua, ndio maana hakuna anayetaka vifo vyetu ila pesa yetu. Waishi kwenye majumba yetu bure, huku wakibadilisha magari ya kifahari hapa mjini kwa pesa yetu wanayoipata bila shida. Hilo unalijua, wala si siri Alex! Shutuma ulizowapa watoto wako ni hasira ya KOSA lako tu. Lakini najua, unajua, hawana nia ya kukukua. Huna wakumlaumu Alex, kaangalie kwenye kioo.”

    “Kwamba unaona hawastahili adhabu!?” “Wamekosa. Wanastahili adhabu. Lakini si kuwafunga jela. Hapo HAPANA Alex. Na badala ya kupaniki na kukasirika, wewe kubali sisi tuliandikiwa kukosa, ujitulize tu. Bahati kama hizo za kina Jelini si zetu. Ndio maana hata Mungu alipompitisha kwako, umeishia kumuachia madhara tu. Pesa yetu, inalaana. Achana na watoto wasio na hatia.”

    “Acha kusema hivyo!” “Sasa unabisha nini Alex!? Unajichelewesha bure kwenye kukubali huo ukweli ambao wote tunaujua tokea zamani! Na kwa jinsi ninavyokuona sasahivi, utapoteza heshima mjini. Rudisha akili kazini, tengeneza pesa inayokupa heshima. Achana na mapenzi. Lasivyo utakosa vyote.” Mgisha akasimama na kuanza kuondoka.

    Kasa akamuwahi. “Nina mpango wa kumtafuta Jelini. Tena mimi mweyewe.” Mgisha akamgeukia. “Ili umwambie nini?” Akashindwa cha kujibu, wakabaki wakitizamana. “Tafadhali rudisha akili sehemu sahihi Alex. Hutaki uzee wa aibu. Nikimaanisha usio na pesa. Wanawake kama kina Koku, wapo wengi tu. Endelea na maisha yako. Acha kuanzisha maisha ya kupendana ambayo kwanza wote tunajua hatujawahi kuyaishi hata mara moja. Kwa hiyo hatuyajui. Ndio maana hata ulipopata nafasi, umeharibu vibaya sana. Rudisha akili sehemu sahihi Alexender Kasa. Achana na unachotaka kufanya. Na watoe watoto JELA.” Akaondoka na kumuacha amesimama palepale akijifikiria.

~~~~~~~~~~~~~~~

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment