~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakawaona wanaingia.
“Kazi ipo!” Akaongea mama Jema, na kumfanya Jema acheke akiwaangalia.
Wakawasogelea. “Hizo nguvu unazozitumia ungeziweka kule kwenye kupambania
maslahi yetu, sasahivi tungekuwa tukilipwa mishahara ya kutisha sana hapa
mjini.” Colins akacheka akikaa. Hapohapo akaitwa na mama yake. Akasogelea sikio
la Jelini aliyekuwa amekaa pembeni yake. “Hapa nilipokuacha, usiondoke mpaka
mimi mwenyewe nikurudishe nilikokutoa. Sawa?” Hayo maelezo anayotoa kwa
kunong’ona sikioni kwa Jelini, mwili mzima unamsisimka. “Asiwepo wa kukutoa
hapo kwenye hicho kiti, ila mimi mwenyewe. Na nitakuwa nikikuangalia
popote nilipo.” Akacheka taratibu na kutingisha kichwa akikubali.
Ndipo akasimama
alipopata tabasamu kutoka kwa Jelini. “Hicho kiti pembeni ya Jelini kisikaliwe
na yeyote, James.” James akatingisha kichwa kwa masikitiko, yeye akaondoka kwa
haraka kuelekea alipokuwepo mama yake. Wakamuona amepewa kazi anaingia na
kutoka akimnong’oneza mama yake hili na lile kisha kutumwa tena. Jelini kimya ametulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Ukawa usiku mtulivu,
watu walijua kusherehekea hapo kwa vile wanavyojuana. Ukweli ilipendeza sana na
kuvutia. Shuguli zilipomuishia Colins baada ya watu kula na kubaki wakinywa tu
huku wakiongeza nyama kwa nafasi, Colins akarudi kukaa pembeni ya Jelini aliyekuwa
amempakata mwanae. “Acha nikamlaze.” Akampokea, akaenda kumlaza yeye, na kurudi
kukaa pembeni yake. Akamuwekea mkono juu, akamvutia kwake. Jelini akajisogeza
mpaka ubavuni, wakatulia.
“Umeshiba?”
Akamnong’oneza sikioni. Jelini akatingisha kichwa akimtizama, macho
yakagongana. Na vile walivyokuwa wamekaa karibu, moyo wake ukajawa furaha ya
ajabu, akarudi kujiegemeza ubavuni. Mambo yakaendelea wao wakiwa watizamaji
wakicheka tu.
Baba yake alipochukua
kipaza sauti watu wakaanza kushangilia sana. Kina Jema wakawa hawajaelewa. “Kwa
nini wanashangilia.” James akauliza. “Pombe ishaingia kichwani, basi anataka
kumuimbia mkewe. Ndio kazi yake, wote wanamjua. Huwa wanasubiri akifurahi, aanze
kuimba. Baba ana sauti nzuri sana. Tulieni msikilize.” Miluzi ikaendelea kwa
wasomi hao kama vijana. Wanaume wote waliokuwa hapo, marafiki wa baba yao ni
madaktari wanaojuana miaka mingi.
“Huu ni maalumu kwa
mke wangu. Muache kelele asikilize.” Wakazidi kushangilia wakitaka zilipendwa,
mama CJ cheko limemjaa. “Nothing’s Gonna Change my love for you.” Wote
wakaongea kwa pamoja, wakishabikia kwamba ndio wimbo wanataka aimbe.
Wakashabikia mpaka akakubali kuimba huo. Wakamuwekea mlio tu bila maneno.
Akaanza huyo mzee kwa sauti yake nzito kama Colins, mpaka vinyweleo vikasimama,
maana alianza vizuri sana na hisia zote. Jelini mwenyewe akajitoa ubavuni na
kukakaa wima akabaki akisikiliza.
Aliimba huyo baba CJ
mpaka akamaliza, watu wote wakasimama. “Kumbe ndio maana!” James mwenyewe
akaafiki na kuanza kupiga makofi. Akainama kama anayepokea shukurani za watu
akarudi kumbusu mkewe, mziki ukawekwa, wakaingia hapo na wazee wengine
ikachezwa twist ya nguvu wakicheka sana mpaka wakamaliza mwaka. Ila mama CJ
akataka wote watulie, waombe kwa muda wakiwa wanapokea mwaka mpya. Pakatulia
haswa. Wakaomba kwa kumshukuru Mungu wakiukaribisha mwaka mpya na baraka zake
zote, ndipo wakaagana.
Mwaka Mpya.
James akaondoka na
mkewe. Mama Jema na mtoto wakatangulia na gari ya Jelini aliyokuwa amepewa na
aliyekuwa Zenda, akabaki Jelini na Colins. Jelini akasaidia kazi kidogo hapo,
vingine wakakubaliana watamalizia kesho yake. Wakatoka Jelini na Colins mpaka nyumbani
kwao. Wakaishia ndani ya ua, maana Colins alienda kumfungulia mlango,
aliposhuka, akamvutia tena pembeni. Wakabaki wamesimama nje ya gari, Jelini
amekumbatiwa vizuri, amejilaza kifuani wanazungumza yao taratibu.
“Kesho tunakwenda
wapi?” Akauliza Colins akimchungulia pale alipojilaza. “Mwenzio nabadili
maisha. Naanza kufanya kazi. Sijui mama atakua ameamua nifanye nini! Amesema
kesho ataniambia na kunipangia majukumu. Na nimemuahidi nitafanya. Nataka na
yeye aone mabadiliko. Nimecheza sana.” “Kwani ulikuwa ukifanya nini kabla?”
“Kulala.” Colins akacheka na kutulia.
“Mimi mwenzio
sijasoma Colins, na sipendi shule wala kufanya kazi. Kuwajibika, au
kujishugulisha nimekubali kubadilika. Ila kusoma, sitaki kabisa.” “Si
lazima kusoma.” Jelini alishangaa, hakutegemea akamwangalia. “Nakwambia ukweli.
Kama kunaunachotaka kufanya kinahitaji kuongeza ujuzi, hapo huna jinsi. Lakini
si usome tu kwa sababu kila mtu amesoma! Hapana. Ila lazima kujishugulisha. Na
nini, ndio swali la kujiuliza. Je, hicho kitu kinahitaji elimu? Ndipo
itakulazimu urudi shule. Ila kama hakihitaji elimu, sasa kwa nini ukasome?”
Hapo Jelini akatulia.
“Naomba unipigie mimi
simu, mara tu utakapoamka nakujua siku yako itakwendaje.” “Sina simu Colins.”
“Simu yako imekwenda wapi?” “Nimeifunga kabisa na sitaki kuiwasha.” “Sababu ya
mzee Kasa?” Jelini akatulia. “Naomba tafuta namba ingine ili tuwe tukiwasiliana.”
“Naona nitafanya hivyo kesho, kisha nitakupigia.” “Ni sawa nikiweka mpango wa
kwenda kuogelea na Jeremy?” Jelini akaanza kucheka akifikiria.
“Wenzio sisi hatujui
kuogelea. Kwanza hata hatuendagi bichi. Nilikwenda na Kasa nafikiri mara mbili
au tatu tu, napo hiyo siku tuliyopanga kuogelea hata hatukukaa sana,
tukaondoka.” “Kwa nini?” “Wivu. Anawivu sana ndio maana sikutegemea kwa msimamo
ule, eti mimi ndio nije kumfumania! Ila kujibu swali lako alisema yale
mavazi ya kuogelea siwezi kuvaa mbele za watu na kuwaacha waendelee kunitamani.
Tukaondoka.” Colins akacheka akimfikiria vile Jelini alivyo, halafu awe na vazi
la ufukweni, yaani kinguo tu chakuogelea! Hapo hata yeye akamuelewa Kasa.
“Unafikiri Jeremy
atapenda?” “Mwanangu hanaga neno. Bora ashibe.” “Basi nitaenda kumnunulia vifaa
vya kuogelea. Ukiniambia muda ambao mpo free, nitakuja kuwachukua.” “Nashukuru
kwa kujitoa muda wako na kuwa radhi kuonekana na mimi pamoja na Jeremy. Imenifariji
kuona humtengi.” “Alivyo mtoto mzuri vile! Hafichiki wala kutengeka.” Jelini
akacheka na kuinama akifikiria.
“Nimefurahi
tumemaliza wote mwaka na kuuanza mwaka mwingine pamoja.” “Kwanini sasa
unafurahia kuwa na mtu kama mimi, Colins!?” “Sijui unamaanisha nini
ukisema ‘kuwa na mtu kama mimi’! Lakini nahisi na mimi nimepatwa na ile
hali kama uliyosema wewe uliipata kwangu. Hujui ni kwa nini lakini unafurahia
kutoka moyoni ile kunihudumia mimi. Basi na mimi nafurahia kuwa na wewe.”
Jelini akamwangalia na kutulia.
“Naomba tujiwekee
malengo Jelini?” “Malengo gani!?” Jelini akauliza taratibu akimwangalia ila kwa
mshangao kidogo. “Tujipe muda tujue ni nini kinaendelea ndani yetu. Ila.” Hapo
akatulia. “Ila nini?” “Ikitokea unaanza mahusiano na mwanaume mwingine au ukiwa
unataka kurudiana na mzee Kasa, niombe mimi niwe mtu wa kwanza kujua.” “Sawa.”
Akakubali kwa haraka bila shida. “Na mimi itakuwa hivyohivyo. Ikitokea naanzana
na mwanamke mwingine, nitakwambia.” Hapo pakawa pagumu kidogo. Akamwangalia na
kunyamaza bila yakujibu.
“Kapumzike, tutaongea
kesho.” “Asante, usiku mwema.” Wakaangaliana na kucheka kama hawajui waaganaje.
Jelini akaondoka. Akamsubiria mpaka akafungua mlango akaingia ndio na yeye
akaondoka.
Mambo Mapya.
Jelini akiwa amelala
mama yake akamgongea na kuingia. Akatoa chandarua na kukaa kitandani kabisa.
“Shikamoo mama.” “Marahaba. Sasa unakumbuka nilikwambia tunabadili gia angani?”
Jelini akakaa sawa. “Nipange mama yangu.” “Kwa utayari huo, tunaanza na pesa
tuliyo nayo. Ni nyingi tu. Tunaendeleza duka letu vilevile na vitu vya kisasa,
na kule ni kama kumekamilika kabisa ila walitaka makubwa tu, ila sisi kwasasa
tunafanya tunachoweza ili tusije tumia pesa yote ikaisha.” “Kwa hiyo mimi
ulitaka nifanye kazi gani?” “Dukani tumepata watu wazuri na wanapawezea. Ni
kuwafuatilia, zaidi pesa ili wasiingiwe tamaa wakaanza wizi au kubweteka.
Halafu tuhamishe nguvu pia kwenye kuuza mitungi ya gesi, majiko, Luku na..”
“Mama wewe una mambo mengi! Pesa itatosha kweli? Si tuanze na vichache kwanza!”
“Pesa tulionayo si chache!” “Hata sijui ni kiasi gani.” “Ni..” Akamtajia na
kumshangaza sana Jelini.
“Mama wewe! Kwani
yule mzee alikuwa akiweka pesa kila siku!? Mbona nyingi hivyo!” “Si Zenda
tena!?” “Akuu! Hana uwezo wa kuwa Zenda hata kidogo. Achana naye.” “Hutajuta?”
“Mwenzio nimekuwa na tamaa ya alichopata Jema, mama. Kwake kumetulia!
Mwanaume anampenda! Na mimi nataka mama. Hizi pesa na mabwana wasio wako
havina raha. Starehe tu, ambazo si za kudumu! Mmmh! Sitaki tena. Vinaishia
kukuumizwa tu. Mimi sitaki tena.”
“Kwa hivi
nilivyokuona, sasahivi najua unaweza Jelini. Eti mimi nilikuwa na wasiwasi na
wewe kuliko hata huyo Kasa. Lakini ikawa tofauti!” “Ujue mama mimi sio malaya
kabisa. Kwamba nataka kuvulia kila mwanaume nguo! Kwanza nina kinyaa mama. Na
yeye ndicho alichoniumiza nacho. Nafikiria jinsi alivyonichanganya na malaya
zake! Hapa nasubiri miezi mitatu ipite nikapime tena Ukimwi, nitulie kabisa.”
“Bora.” Mara simu ya mama Jema ikaanza kuita.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Nani mbona umekunja
uso?” “Hata sijui.” Akapokea. “Mimi ni Colins, nipo
hapa getini. Naomba uwaambie wanifungulie. Si naweza kuingia?” “Karibu Colins, nakuja.” Jelini akaruka kitandani
kukimbilia bafuni baada ya kusikia ni Colins, tena yupo getini! “Kazi ipo.”
Mama Jema akaonge akitoka. Wakati akivaa akamsikia akizungumza na Jeremy.
Akimuuliza maswala ya shule na kutaka kujua kama anapenda kuogelea. “Mimi sijui
kuogelea.” Akamsikia Jeremy akimjibu. “Ungependa kujifunza?” Hakusikia mwanae
akijibu. “Unaogopa?” “Sijui!” Akajibu kama ambaye hana uhakika.
“Mimi najua sana
kuogelea, na ninapenda. Tunaweza kuingia wote kwenye maji. Nitahakikisha
hauzami.” Kimya. “Na tutakuwa na mama.” “Na yeye atakuwepo kwenye maji?” “Sijui
kama atapenda. Lakini pia sio lazima ikawa leo Jeremy. Kama leo hujisikii
kuogelea, tunaweza kufanya wakati mwingine.” “Basi tufanye wakati mwingine.”
Jelini akashangaa sana huko alipokuwa chumbani. Hakutegemea kama mwanae
angekataa. Bibi yake huko jikoni kimya akisikiliza.
“Unataka nikuitie
mama au bibi?” Akamsikia Jeremy akimuuliza kama yeye anataka kuondoka. “Wewe
unaondoka?” “Nataka kurudi chumbani. Kuna kitu changu nafanya.” “Ni nini
unafanya?” Jelini akamsikia mwanae akianza kucheka kama anayesita kusema.
“Ni nini?” Akamsikia
Colins akimuuliza. “Nataka nisimwambie mtu mpaka nifanikiwe kwanza.” Colins
akacheka. “Unatengeneza?” “Ndiyo. Lakini…” Halafu akasita. “Pengine naweza
kukusaidia.” “Kwanza sina uhakika. Nilipewa zawadi na mama. Bibi aliniletea
kwenye mfuko. Nilipofungua, nikakutana na vitu pamoja na kijitabu kidogo
chenye picha mbalimbali. Kwa jinsi nilivyosoma, ni kama ni maelekezo ya kuweza
kujenga zile picha kwa vile vitu vidogovidogo vilivyopo hapo. Ndio
nasoma na kujenga.” “Jeremy wewe unaakili sana. Sasa umefikia wapi?” Akacheka
kama anayesita.
“Sina uhakika sana.”
“Usisite. Wewe niambie tu.” “Kwa jinsi nilivyoona, na kuanza kujenga ni kama
treni na reli. Nimefanikiwa kutengeneza reli. Nahisi nimefanya ndefu sana.
Sitaki kubomoa, nahisi labda nikijenga na treni, pengine itakua kubwa itahitaji
hiyo reli ndefu. Sasa kwa kuwa sijawahi kuona hata mara moja, ndio najaribisha.
Nifanye mpaka nione mwisho bila kubomoa reli kwanza.” Jelini mwenyewe
akashangaa ni nani amempa hiyo zawadi maana na yeye mwenyewe ndio anasikia.
“Mimi mwenyewe
nimeshaanza kuvutiwa. Naomba nikaangalie. Sitakuingilia.” “Najengea chumbani
kwangu, bado bibi hajanirudishia kitanda, kulikuwa kunajengwa. Hamna hata
sehemu ya kukaa. Mimi najengea chini tu sakafuni, halafu usiku nalala na bibi.”
“Na mimi nitakaa sakafuni.” “Kweli!?” Akauliza akicheka na mshangao juu.
“Kabisa.” Colins akajibu. “Ila usiwe na wasiwasi. Nipasafi, bibi alisafisha
vizuri tu, ila bado hakujarudishiwa vitu vyangu. Twende nikakuonyeshe.” Jelini
akatamani kutoka kwa haraka, ila akaona awape muda kidogo.
“Natengeneza kwa
kuangalia picha.” “Na hivyo ndivyo anavyotakiwa.” Wakawasikia wakizungumza
wakielekea kwenye chumba ambacho ni cha Jeremy. Na hicho mama yake
alikibadilisha vizuri sana. Sakafu ilibadilishwa ikawekwa ya marumaru
inayofanana na chumbani kwake na bibi yake. Akamvutia choo ili apate cha kwake
peke yake. Madirisha yalishajengwa na kuwekwa vioo vizuri na makabati ya
ukutani akawa ameshajengea. Akafunga feni na A/c ndogo tu. Akawa anataka
kumnunulia kitanda kipya, meza na kiti chake cha kusomea, na meza yenye kioo
kwa ajili ya kuweka vitu vyake vakutumia baada ya kuoga.
Wakaingia huko,
mlango ukafungwa, kimya. Jelini akatoka kwenda kwa mama yake. “Ni zawaidi gani
hiyo!?” “Alinipa Zenda ulipokuwa umelazwa, akaniambia nimpe, nimwambie inatoka
kwako. Nilikuwa na mambo mengi wala sikutilia maanani. Nikamkabidhi mfuko mzima
bila hata kuangalia, nikaendelea na yangu. Kumbe mwenzangu ukimya wote huo
anakua ndani anajenga treni!” Jelini akutulia akifikiria.
“Ila Jeremy
nimemsifu! Akifanya jambo lake hataki kuyumbishwa! Kakataa kuogelea ili
amalizie mambo yake!” “Mimi mwenyewe kanishangaza! Sikutegemea kama angekataa
kwenda kuogelea! Nilijua angefurahi kweli!” “Lakini mwache. Usimuingilie.
Mwache mpaka awe tayari.” Jelini akatoka kwenda na yeye kuangalia.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akawakuta wamekaa
chini kabisa sakafuni, wakamwangalia alipoingia, akaenda na yeye kukaa hapo
akiangalia. “Umejenga vizuri Jeremy!” “Najaribu mama. Nataka itokee kama kwenye
hii picha. Nina uhakika picha zote hizi unazoziona hapa, zinatokana na hivi
vipande hapa. Nikifanikiwa kuviunganisha kwa usahihi, vitatokea kama kwenye hii
picha.” “Unafanya vizuri. Mimi sitakusumbua.” Akarudisha akili kwenye hivyo
vijipande vingi vimekusanywa kwenye boksi kubwa tu vya kutoshea. Jelini
mwenyewe akachoka. Kwamba akusanye pale mpaka vitokee treni! Akapotelea
mawazoni.
Colins akamgusa.
“Ulilala salama?” Akamuuliza Colins, lakini Colins akamfanyia ishara aache
kuongea. Jelini akacheka na kumtizama Jeremy. “Tutafukuzwa hapa.” “Nikusaidie
Jeremy?” “Muache mtoto bwana!” Jelini akaanza kucheka. “Nilikuwa namchokoza
aniangalie.” Jeremy akamwangalia. “Umekula?” “Nishakula.” “Haya Jelini toka
huko. Mimi nakujua wewe kunyamaza hutaweza.” Mama yake akaingilia. Wote mpaka
Jeremy wakacheka.
“Wala hujakosea.
Maana nilitaka kumuuliza tena, atamaliza saa ngapi ili…” “Haya toka.” Mama yake
akamfukuza tena. Jelini akacheka akisimama. “Ukimaliza njoo mwaya tupige
stori.” “Muache bwana, Jelini.” Colins naye akaingilia. “Hata hivyo sitamaliza
sasa hivi. Ni vingi.” “Jeremy naye!” “Haya toka huko.” Mama yake akamsisitiza.
Jelini akawa anatoka.
“Basi Colins wewe
njoo hata tusalimiane, ndio uje uombe kusaidia.” “Ulijuaje?” “Nimeona jinsi
ulivyokaa hapo kama upewe na wewe ujenge!” “Inanikumbusha utoto wangu sana.
Nilikuwa nikijenga LEGO kama hivi, mpaka za roboti. Nilikuwa na meza chumbani
kwangu, najaza. Na ndio ilikuwa zawadi ukinipa, tunapatana. Ikajenga
ufahamu mkubwa sana kwangu mpaka nikaingia kwenye darasa la Engineering la
watoto shuleni.” “Kumbe ndio maana James anakusifia unajua sana kompyuta?”
Akacheka na kurudisha macho kwa Jeremy.
“Komputa nimeanza
kuchezea tokea mtoto sana. Kwa hiyo hichi anachokifanya Jeremy ni kitu kizuri
sana. Baadaye atajua ni vitu gani anapenda, basi ndio kumnunulia aina hiyo ya
LEGO.” “Basi wenzio na mama hata hatujui jina lake.” Wakacheka. Jelini akatoka
na kumuacha Colins bado akiangalia kama aliyekumbuka mbali.
“Kama unataka kujenga, njoo tujenge wote.” “Nitakupunja.
Mimi napenda sana LEGO. Itanichukua muda mfupi sana kujenga hiyo reli nzima na
kumaliza.” “Kweli!?” “Kabisa. Nilikuwa nikijifungia kama wewe hivi. Sitaki kutoka
mpaka mama alikuwa akinilazimisha kula. Ndio ilikuwa furaha yangu. Nikazoea
mpaka nikawa nafanya za watu wakubwa nikiwa bado mdogo sana.” Jeremy akavutiwa
na Colins.
“Kwa hiyo na mimi
nifanyaje ili niweze?” “Hivyo unavyofanya ndio sahihi kabisa. Lazima kujua ni
nini unajenga, ndio uanze. Tena naona wewe utajua mapema na kuwa mfanisi sana.
Umeanza vizuri. Endelea hivyohivyo. Na huwa haiitaji haraka.” “Sasa mbona wewe umesema
unaweza kujenga haraka?” “Kwa sababu nimefanya hicho unachokifanya sasahivi kwa
zaidi ya miaka yako wewe.” Jeremy akacheka.
“Kwamba nina uzoefu
na akili imeshaozea kujenga. Sasahivi najenga vitu vya kweli. Hata ukinipa
tatizo kubwa kiasi gani juu ya mitandao, kompyuta, macho yakishaona tu, akili
inajua kwa haraka sana kitu gani chakufanya. Nimefurahi kuona na wewe
unapenda.”
“Kwa hiyo nikiwa
mkubwa nitakuwa nikifanya kazi kama yako?” “Si lazima. Ila ujue unafanya akili
yako iwe na uwezo mkubwa wa kufikiria chochote kile. Kwa juhudi uliyo nayo na
ukiendelea hivyo, ukija kujua unachopenda kufanya ukiwa mkubwa, basi ujue
utakifanya kwa urahisi sana, kwa kuwa akili yako ina uwezo mkubwa wa kufikiria
nakufanya.”
Zipo Tabia Za Waliofanikiwa Sana,
Na Tabia Za Walioshindwa.
Jelini akamfuata mama
yake chumbani kwake. “Nataka nikamilishe chumba cha Jeremy kiwe cha hadhi
nzuri. Mwanangu anajitahidi mama.” Mama Jema akamtizama. “Nataka nikamnunuli
seti nzuri ya kitanda, meza zake, vikabati vizuri vinavyoendana ili aweke
vitabu vyake na vitu vyake, viti vizuri vyakusomea vitakavyoendana na…” “Kwa
pesa ipi?” Mama yake akamkatisha kwa swali, Jelini akapoa. “Wewe unataka kidogo
tulicho nacho tena tuanze kutapanya?” “Ni hivyo tu mama!” “Hapana Jelini.
Tukianza maisha tu yasiyo yetu, ujue hivi karibuni tunarudi kule tulikokuwa.
Sijui kama unanielewa?” Kimya.
“Uhalisia
wangu mimi na wewe nilazima tuukubali na ukumbuke sisi ni kina
nani. Nilikuwa nikitamani pesa ikosee njia, ije nifanye mambo ya maana ili
tutoke pale tulipokuwa. Sasa pesa tuliyonayo unaweza ona nyingi, lakini
isipozalishwa tu, ujue ndani ya muda mfupi sana, tunarudi chini kabisa tukianza
kumuomba Jema pesa na kukopa kila mahali. Au wewe unataka kurudia yale maisha
ya kuomba omba pesa kama zamani?” Akapandisha mabega kukataa.
“Basi naomba akili
ihamie kwenye kuzalisha kuliko matumizi. Ukifanya kazi, ukalipwa, tumia pesa
yako utakavyo, ila si mtaji.” “Basi naomba unikope, nitakulipa.” “Mimi mwenyewe
bado sijaanza kulipwa, kwa kuwa sijaanza kazi.” “Mama!” “Sasa wewe
umeniona nikifanya kazi hapa?” “Si unalile duka pale?” “Lile duka nimeajiri
watu. Pesa yote niliwekeza, na itachukua muda kuja kujiendesha lenyewe ndipo
nipate faida.” “Basi nipe na mimi kazi nianze kuingiza pesa nimnunulie mwanangu
vitu.” “Sasa hiyo ndio akili. Na ujue hapa napo mambo yatabadilika.” “Kama nini
tena!?” Jelini akauliza kwa mshangao.
“Hiki anachokifanya
Jeremy, kuamka asubuhi kwenda shule na kurudi mchana, ndio
itabidi kuwa maisha yako na wewe.” “Mimi nimekubali mama. Nitafanya.”
“Sawa. Na huku kulindwa hapa kama sisi ni maraisi, hiyo garama hatutaweza.” “Na
hili gari sasa!?” “Yaani hili gari ndio tulilipie pesa yakulindwa? Kwanza
hatuna uwezo wa kuendesha hili gari sasahivi. Kiuhalisia, hatuna huo uwezo wa
kuendesha Renji. Lasivyo pesa yote itaishia kwenye mafuta. Nilipanga kumuomba
Jema na mumewe watusaidie kulitunza kwao, sisi turudie maisha yetu ya zamani.
Bajaji na pikipiki. Au hutaweza? Maana hilo gari linakunywa mafuta haswa.”
“Mimi nitaweza mama.” Mpaka mama Jema akashangaa.
“Kweli!?” “Nitaweza
mama.” “Basi hapo utanirahisishia maana nilijua utaanza kulalamika.
Lazima tubadili gia angani. Maisha yamebadilika, tunapinduka nayo. Lasivyo tutakwama
muda si mrefu. Na utajikuta inabidi kufanya mambo usiyoyataka ili
kujiingizia pesa, na huo ndio umalaya ulionithibitishia huna. Sasa
usianze kwa ajili ya maisha ya starehe.” Jelini akapoa.
“Au unataka kurudiana
na Zenda?” Jelini akashituka sana. “Maana yeye ndiye mwenye uwezo wa kukupa
maisha hayo ya anasa.” “Hapana mama! Yeye na wanae watakuja kuniua bure! Sina
sababu ya kurudia maisha ya hatari.”
Akawa kama amemchanganya mama yake. “Kivipi wanae wakuue?” Jelini
aliropoka tu akiwa amekumbuka alilofanyiwa na Kemi na kumdhuru vibaya sana. Kwa
ajili ya kuwa na baba yao ambaye alishaona hastahili madhara makubwa hivyo. Kwa
penzi lipi? Akajiuliza Jelini. Akaona hana sababu ya kuyatupilia mbali maisha
yake kwa kujiweka hatarini kwa mwanaume kama mzee Kasa asiye muaminifu. Kwanza
alishajua hakuna mwisho mwema wowote kati yake na baba yao.
Akafikiria kwa haraka
jinsi ya kumjibu mama yake mlipiza visasi kwa kila anayemuonea mwanae. “Baba
yao asije niua kwa maradhi. Na watoto wake bado hawamuamini yeyote na baba yao.
Nafikiri sababu ya mali. Hawataki mtu awe karibu na baba yao wakihofia mali
zao. Kwa hiyo huko sitarudi mama. Na ninashukuru kunilinda nisirudi. Wewe nipe
kazi nitafanya.” “Umenifurahisha Jelini, ni hivyo hujui. Nilijua utasumbua
kweli.” Jelini akaanza kulia.
“Mimi mwenyewe
sijategemea kama utakubali kubadilika kwa haraka mama. Nilijua utamtaka mzee
Kasa ili azidi…” Jelini akashindwa kuendelea akizidi kulia. “Wewe si
kitega uchumi changu. Nilikuacha naye kwakuwa ulisema unampenda. Kama mapenzi
yameisha, basi! Huna haja yakujitesa. Hee! Kwa kipi mno? Kama yeye
amefanikiwa na sisi tutafanikiwa tu. Tuweke juhudi. Na wala usiogope.
Hii ni shida ya muda tu. Kwanza tusiite shida. Ni mabadiliko ya muda tu.
Tukiweka juhudi na sisi tutarudia maisha ya gari.”
“Eti ninazidi
kumuonea wivu Jema, mama?” “Kwa nini?” “Aliweka juhudi
kwenye mambo yake mpaka akafanikiwa kujinunulia mpaka gari na kuwa na maisha
mazuri tu. Akatulia mpaka akampata mwanaume anayempenda! Ila nasemea ile juhudi
yake tena bila hata wanaume! Ujue mwenzio nilijua Jema alikuwa akihongwa! Sasa
kuja kuolewa bikra! Hakika imenigusa mama.” “Ni juhudi na kujikana
Jelini. Na wala hujachelewa.” Hilo likamtuliza Jelini, akajifuta na machozi
akifikiria.
“Sasa mimi nianze
wapi kazi?” Mama yake akacheka. “Usinicheke bwana!” “Unanifurahisha sana Jelini
wangu. Kwa moyo huo, tutafanikiwa. Sasa kwa kuwa mimi nataka kuanza ile
biashara ingine, nafikiri tugawane. Mimi na wewe tusikae upande mmoja. Wewe
mzuri kwa kuzungumza na watu, nataka tufungue upande wa pili wa lile duka, na
wewe uwepo na wale mabinti pale. Wajue wewe upo pale ili kwanza wasiibe na
wajali wateja. Nitakufundisha mahesabu yake ya biashara nzima. Ili ujue kwa
siku umeuza kiasi gani, faida na matumizi yote ya pale. Sio ngumu. Siku tano tu
utakuwa sawa. Nakuachia pale, mimi nahamisha akili kwingine na yule kijana.
Nakuachia wale mabinti pale dukani muwe wote. Fiona mwepesi halafu hana kiburi kabisa. Mtafanya
mambo kwa urahisi.” “Sawa.” Jelini akakubali bila shida. “Sasa kanywe dawa
kabla kichwa hakijaanza.”
Kwa Colins.
Akatoka na kukuta
Colins ametulia kimya kwenye kochi macho kwenye simu. “Sijui alikuwa
akitusikiliza?” Jelini akawaza akimsogelea. “Vipi kichwa?” “Sio mbaya. Ila
acha nimeze dawa kabla hakijaanza, halafu tupate kifungua kinywa.” “Sasahivi ni
chakula cha mchana Jelini!” “Samahani mipango tuliyoweka jana haijafanikiwa.”
“Usijali. Anachokifanya Jeremy ni kitu kizuri sana.” “Sasa unaondoka?” “Wewe
unataka kufanya nini? Kama unakazi itakayokufanya usiwe huru mimi nikiwepo,
nitaondoka.” “Bosi wangu, mama, amenipa mapumziko ya leo. Kesho kazini.” Colins
akacheka.
“Kwa hiyo nipo tu.
Tukae wote. Au ulitaka kufanya nini?” “Kanywe dawa kwanza halafu ndio tujue
chakufanya. Nikusindikize?” Jelini akawa hajaelwa. “Dawa zipo chumbani!” Colins
akasimama na kumfuata, Jelini akacheka. “Sasa maji yakumezea dawa?” “Acha nichukue
kwenye friji.” Akashangaa anamfuata. Akachukua maji na kurudi naye chumbani,
akajitupa kitandani, Jelini akacheka.
Akashangaa vile
Colins anavyoshangaa kile chumba. Akapoa. Maana ni kweli pesa ya Zenda
ilitumika hapo ndani. Colins akasimama na kwenda mpaka chooni. “Waw!” Akamsikia
akihamaki kwa sauti. “Sijawahi ona sinki la kuogea kama hili! Umelipata wapi?”
“Hata sijui Colins. Tulihama kabisa hapa, tuliporudi ndio nikakuta kila kitu
unachoona.” Colins akabaki amesimama huko bafuni. Akatoka na kubaki kama
ameduaa anayefikiria. Jelini akamuacha tu akijua kinachoendelea huko kichwani.
Anapigia mahesabu pesa ya Kasa iliyomwagwa humo ndani. Akawa anatafuta dawa zake.
Colins akarudi
kujirusha kitandani. “Na mimi James amenialika kwao usiku. Naona na kina mama
pia walialikwa lakini wanamiahadi kwengine. Ila wamesema watapitia tu
kuchungulia kidogo.” “Na sisi tutakwenda kwenye saa 12 jioni.” Akanywa dawa na
kwenda kukaa. Akamuona kama kuna kitu anafikiria. Colins akajivuta na mto mpaka
pale alipokuwa amekaa. Jelini akamshika. Colins alifurahi huyo. “Sasa unacheka
nini?” “Umenishika.” Jelini akacheka sana.
“Colins wewe!”
“Napenda tukiwa wote, Jelini.” “Ila nahisi umekuja muda mbaya kwenye maisha
yangu Colins. Nina mambo mengi, akili haijatulia. Nipo kwenye majuto! Hata
sijui.” “Unajutia nini?” “Naona nimejichelewesha! Jema amezaliwa na mama huyu
huyu. Amekuzwa kama mimi tu. Ila mwenzangu alifanikiwa kumsikiliza mama mapema,
amefanikiwa. Jema anakazi nzuri, sababu ya juhudi niliyokuwa nikimsikia mama
akimkazania. Nakumfundisha jinsi ya kupambana mpaka akafanikiwa.”
“Halafu Jema ametulia
Colins! Mimi sikujua kama ni kwa kiasi kile! Na
mpaka Mungu amempa mwanaume mzuri, anampenda Jema!” “Nisikilize Jelini.
Hujachelewa. Hujachelewa hata kidogo. Hapo ulipo, na kwa akili hiyo, unaweza
kufanya makubwa sana. Uzuri unaye mama wa kukuongoza vizuri, hujachelewa.
Ila ujue si rahisi. Kuna garama ya kulipa na vishawishi vya kushinda.
Popote kwenye malengo kunakua na vishawishi. Unaweza ukachoka katikati
ya safari, ukashawishika.” “Unamaanisha kutafuta
mwanaume wa kunisaidia?” Jelini akauliza.
“Hata hilo.” Colins
akaongeza na kumfuta machozi. “Ni vile hunifahamu
mimi Colins. Na umenikituta nikiwa na mzee Kasa. Sina tamaa na pesa na wala
shida haijawahi kunishawishi kutafuta mwanaume ili anihonge. Sipo hivyo.
Kama ningekuwa hivyo, ningeshakuwa na wanaume zaidi ya mzee Kasa. Kwa kuwa
wanaume kama yeye wala si wageni kwangu. Ninao wengi tu, na nilikuwa nikinywa
nao baa kila siku.” “Uliniambia Jelini.” Jelini mwenyewe akatulia
akijifuta machozi.
“Ninachotaka
kukwambia, nimekua na mzee Kasa nikidhani yupo tofauti. Na kwangu kwakweli
tulikuwa na wakati mzuri wala nisikudanganye. Watu
husema ni mkali sana, lakini mimi alijifunua kwa upande ambao ndio maana nahisi
nitammisi sana.” Hapo Colins akaumia. “Alikuwa akinipigia simu,
tunazungumza na kucheka kwa muda mrefu sana na hatukosi chakuongea. Tukienda
mfano sehemu kutembea, yaani ile sehemu utafikiri tupo peke yetu! Tutacheka
mpaka giza linaingia ndipo tunaondoka. Tulikuwa na wakati mzuri na kwangu hakuishi
na mimi kama mwanaume tajiri au msomi. Alikuwa wakawaida sana. Ikawa rahisi
kuwa naye. Lakini si pesa. Na ninakwambia ukweli, ambao unaweza
usiamini, nilikuwa naye yeye kama Alexender wala si kama milionea
Kasa. Sikuwahi kumuomba pesa hata mara moja ila uaminifu nikihofia asije
akawa na mambo ya kando akaja kuniua, nikamuacha mwanangu. Ni hilo tu, lakini
si pesa.”
“Na si kwake tu. Kwa
wanaume wote wanaonifahamu mimi kwa karibu, wananijua mimi huwa sihadaiki
na pesa.” “Basi mabadiliko yako yatakuwa marahisi Jelini. Usiogope. Hiki
anachokifanya Jeremy, ndio na wewe fanya. Soma ramani na kuanza kujenga tofali
moja hadi jingine. Taratibu, na kwa makini. Usiogope, utafanikiwa tu. Na MIMI
nipo na wewe. Nilikwambia ukitaka ushauri, muda na wakati wowote ule, nipigie.”
“Mwenzio nimefikiria, ila sijamwambia mama.” Akanong’ona.
“Nini?” “Nina simu ya
mahela mengi, sioni sababu. Kuna mtu najua huwa anapenda sana simu na pesa si
tatizo kwake. Nataka nimuuzie, niweke vitu chumbani kwa Jeremy. Halafu mimi
nitanunua simu ya kawaida tu.” “Twende.” “Wapi?” “Nifuate kwenye gari.” Wakatoka
hapo chumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment