“Nilifikiri jana
tulikubaliana kufunga na kukaribisha mwaka pamoja! Imekuaje tena?!” “Mpenzi
wako alikuja Colins. Na wewe uliniambia hutaki nikusogelee ukiwa na mpenzi
wako.” Akammaliza nguvu zote Colins. “Ni wakati ule nilipokuwa kwenye mahusiano
naye, Jelini!” “Sasa mimi ningejuaje, Colins? Ilinibidi kuwapisha.” Colins
akapoa na kubaki ameinama kama anayepiga mahesabu fulani akitaka kuzungumza
jambo na kuona si wakati wake.
“Nikuulize kitu
Colins?” “Juu ya nini?” “Siku ile ya harusi ya Jema na James. Nililewa sana.
Sikujua uchafu niliofanya. Kila mtu ananiambia kwa vile nilivyomuathiri.
Natamani kujua picha nzima.” “Itakusaidia nini?” “Nataka kujua, ili hata
nikisikia tena, nijue jinsi ya kukabiliana nayo. Au hata kuomba msamaha
kwa wale ambao niliwafanyia ubaya. Jeremy nilimuomba msamaha. Sijui wengine.”
“Hayo yanatokea wapi tena, leo!?” Akauliza kisha akawa kama amegutushwa na
kitu.
“Ni nini Love
amekwambia!?” “Hakuna mtu ananiambia kikamilifu. Naambiwa kwa kifupi tu. Na
nimesikia wewe ulihusika kwa sehemu.” Colins akafikiria akiwa ameinama kisha
akamwangalia. “Unajua ni nani alikuweka kwenye gari ya Kasa?” “Sijui Colins!
Nilikuwa sijitambui kabisa.” “Kwa hiyo hata maneno uliyoniambia usiku
ule, hukumaanisha Jelini!?” Jelini akashangaa maana Colins aliuliza kwa kuumia
haswa.
“Kwani niliongea
nini!?” Akanyamaza na kuinama kama aliyevunjika moyo kabisa. “Nisamehe Colins,
nilizidisha pombe, sikuwa hata nikijitambua. Nilisema nini?” “Haijalishi tena,
Jelini. Basi, tuyaache tu. Lakini mimi ndiye niliyekuingiza kwenye gari ya Kasa
na kumuomba asije akakugusa kwa namna yeyote ile. Akusaidie ulale mpaka
uamke.” “Nashukuru Colins. Na kama kuna baya nililifanya, naomba unisamehe.
Naona pombe hazijawahi kunipenda. Nimeacha kabisa.” Akamwangalia na kurudi
kuinama. Jelini akamuona vile alivyobadilika.
“Mbona kama
nimekuumiza Colins!? Nilifanya nini?” “Hapana Jelini. Acha muda utajibu kila
kitu.” “Nikikuomba msamaha itasaidia? Maana siku ile nilikosea watu wengi
sana.” “Mimi hukunikosea. Usijali.” Wakatulia. Jelini hajui aseme nini na nini
kimemleta. Akawa kama aliyepoteza dira
tayari. Akabaki ameinamia magoti. “Nikupe kinywaji gani?” Akanyanyua uso na
kumwangalia. Macho mekundu.
Jelini akamsogelea
pale alipokuwa amekaa. “Colins wewe ni mtu wa mwisho kabisa nataka kukuumiza.
Tafadhali niambie ni nini nimekosea.” “Hujakosa Jelini. Hujakosa kabisa.”
Akamvuta mkono, akamshika kwa upendo. “Sasa kwa nini umebadilika?” “Kwa sababu
kuna maneno uliniambia usiku ule, nikayaweka moyoni nikijua umemaanisha Jelini!
Sasa kuja kujua hata hukujua ni nini uliongea, ndio imeniuma.” Jelini
akaumia sana.
“Naomba uniambie ni
nini nilisema.” “Itasaidia nini Jelini? Acha muda uje ujibu.” Jelini akaanza
kulia. “Hujaniudhi, Jelini. Ila nimetamani ingekuwa kweli.” Akanyanyuka kabisa
pale na kutaka kuondoka, Colins akamdaka mkono na kumvuta kumrudisha akae. Akakaa
na kumvutia kwake, wakakaa wamekumbatiana. Jelini amemlalia. Akamkumbatia kwa
mikono yote miwili na Jelini naye akapitisha mkono mmoja nyuma akaukutanisha na
wa juu, akawa amemkumbatia na yeye. Akaegemeza kichwa kifuani. Wakakaa hivyo
kwa muda, Jelini mpenda mikono, akatulia haswa.
“Nilihitimisha
mahusiano na Love, ndio maana nilikwambia uwe na mimi leo, nikijua yeye
angekuwepo na wewe ungekuwepo. Sasa hivi hukuna mipaka.” Jelini akatulia.
“Umenisikia?” Kimya. “Mimi nafungwa na maneno yangu Jelini. Nathamini ahadi
zangu. Ndio maana nipo makini na kila ninachosema maana najua kitanifunga.
Nikikwambia wewe ndiyo, ujue nitabaki kwako hata kama utanifanyia
vituko, mpaka tubadili makubaliano yetu. Sijui kuahidi hivi na kuishi vingine.
Ndio udhaifu wangu huo. Kwa hiyo nilikuwa kwenye mahusiano na Love, na yeye
alikuwa na wivu sana, ilibidi kufuata kila sharti lake ili tu tuwe na amani
kwenye mahusiano yetu, lakini pia tulishindwa. Haikusaidia mpaka
tukahitimisha.”
Jelini kimya kifuani.
“Kwa hiyo kuanzia sasa, ukiniona naye ni kwa kuwa ni kama tumekua pamoja
na familia zetu ni marafiki wa kama wazazi walinyweshana damu zao au kuwekeana
viapo vya mahusiano mpaka kifo. Ila kwa sasa hayupo kama mpenzi wangu. Kwa hiyo
uwepo wake pale leo, si kama mpenzi wangu, ila rafiki wa familia. Umeelewa?”
Jelini akatingisha kichwa kukubali.
“Naomba tukamalizie
na kukaribisha mwaka na familia.” Jelini hakutegemea. “Yaani kwa YOTE hayo niliyokufanyia,
bado tu unataka niwepo karibu na wewe!?” “Bado nataka uwe karibu na
mimi, Jelini. Kama ulivyoniambia siku ile nilipokwambia nina mpenzi wangu, na
asingefurahia kukuona ukinikarimu. Unakumbuka jibu ulilonipa baada ya
kubadili ulichotaka kuniambia?” Kimya. “Ulitaka kuniomba msamaha.” Jelini
akatulia akijaribu kuvuta kumbukumbu.
“Lakini ukapingana na
hilo lakutaka kuomba msamaha. Tena ukasema, ‘Samahani. Sikuwa nimekusudia ku…’ Ukasita.
Kisha ukarekebisha. Ukasema, ‘Hapana. Sitaomba msamaha kwa nilichokifanya kwako, kwa
kuwa utaniibia furaha yote niliyokuwa nayo Colins. Nilifanya kwako kwa moyo na
sijui ni kwa nini! Kwa sababu hakuna mtu nimewahi kumfanyia hivyo! Najihisi
sijakosa, ila nimefanya kwa mtu asiye sahihi. Sitarudia tena. Uwe na amani
kabisa kufika kwenye hizo tafrija zote ambazo na mimi nitakuwepo, nakuahidi
sitakusogelea wewe na mpenzi wako.’ Colins akanukuhu neno kwa
neno mpaka akamshangaza Jelini.
“Colins!”
“Uliniachia hukumu! Nikabaki nikiyarudia hayo maneno kila wakati na kuzidi
kuumia. Halafu ni kama
uliniachia mimi ile hali. Sijui kwa nini, lakini na mimi napata faraja kuwa
karibu na wewe, Jelini. Labda uniambie kama kuna kizuizi.” Jelini akajivuta na
kukaa vizuri. Akajua kuna jambo anataka kumwambia.
“Kwa sasa sina
Colins. Nimeamua kuachana na Kasa.” “Una uhakika? Maana yule mzee anayo pesa,
Jelini. Hutakuja kubadilika baadaye?” “Mimi sikuwa naye sababu ya pesa.
Nilidhani…” Akasita. “Labda nibadilishe. Nilimuumba mtu wangu kichwani,
nikidhani yeye anaweza kuwa huyo mtu, kumbe hawezi.” “Ni mtu gani
ulimuumba ukitaka awe yeye?” “Natamani kile Jema amempa James, na mimi
nikipate.” Colins akakunja uso.
“Najua nataka
makubwa. Lakini kama James amempata Jema, naamini na mimi nitampata tu mtu
wangu.” “Sijaelewa Jelini. Jema yukoje na kwa nini isiwe Jema ndio amempata
James?” “Mimi simjui James kwa undani. Ila nimeishi na Jema, namjua. Ni
mwaminifu sana. Ametulia mno. Na yeye yupo kama hivyo ulivyosema wewe upo.
Akimkubalia mtu, hata kama huyo mtu ni mbaya, anajua kujifunga kwenye
mahusiano. Na mimi nataka mtu wangu Colins. Siamini kama eti wanaume
wote ni malaya. Kwamba eti WOTE hawawezi kutulia na mwanamke mmoja! Mimi
naamini wapo waaminifu.”
“Basi hata James yupo
hivyo. Ila yeye amekwenda umbali mrefu zaidi. Jema ndio mwanamke wake wa kwanza
na amemuoa. Hana tamaa za wanawake kabisa. Mimi ni mtu wangu wakaribu
sana. Ananijua ndani na nje, hivyohivyo na mimi namfahamu James. Tupo ofisi
moja. Mimi na yeye tu.”
“Si umeona sasa? Kama
yupo mwanaume kama James, inamaana na mimi naweza kupata wangu. Nasubiri
Colins. Mimi sina tamaa na pesa. Hata wanaume niliokuwa nikinywa nao, wanapesa
kama hivyo Kasa tu. Lakini kwa tabia zao, sikuwahi kuwakubali. Sitaki kuja kufa
na maradhi, na pesa nimeacha benki. Zitamsaidia nini mwanangu au mama
yangu?” Colins akacheka akimtizama.
“Usinicheke bwana!”
“Mimi nimefurahi kukusikia ukisema hivyo Jelini. Maana nilijua unalilia pesa za
Kasa.” Jelini akampiga na mto. Colins akakwepa akicheka. “Kweli tena. Yule mzee
anayo pesa haswa. Binafsi nisingekuhukumu.” “Mimi nalia kujidanganya
kirahisi Colins. Nilitulia bila mwanaume kwa muda mrefu sana, nikijiambia
nasubiria mwanaume wangu. Nilipojaribu kwako ukanifukuza vibaya vile, kisha
akaja Kasa akinionyesha ni mtu mtulivu, nikapata faraja, nikamkubali.”
“Nilikuwa kwenye
mahusiano Jelini!” “Na mimi nilielewa. Ila niliumia Colins. Sijawahi kukataliwa
vibaya vile. Au niseme sijawahi kumkarimu mtu vile. Wewe ukawa wa kwanza na
ndio ukani..” Akanyamaza macho chini. “Ila niliomba msamaha, Jelini! Na sikuwa
na jinsi nyingine.” “Nilielewa Colins. Hamna shida.” Wakatulia kidogo.
“Utafanyaje?”
Akavunja tena ukimya. “Maisha lazima yaendelee Colins. Mimi ni mama. Sina jinsi
ya kubweteka tena. Nilimtelekeza mwanangu kwa muda mrefu sana nikijificha
kwenye pombe. Na hata jana nashukuru kunitia moyo nisirudie tena pombe. Lakini
ukweli mwenzio ilikuwa ikinisaidia sana. Nilikuwa nikijisahau. Nazika
maumivu yangu yote, nalala vizuri.” “Lakini ukiamka unakutana na matatizo yako
yapo vilevile, hujatatua hata moja! Si ndio?” “Sasa hivi nimebadilika. Mama
amenisaidia. Tunajipanga kuendelea sio kurudi nyuma. Nitatulia kabisa.”
“Nikuulize Jelini?”
“Juu ya nini?” “Usikasirike lakini.” “Niulize tu, pengine itanisaidia kufikiria
zaidi.” “Ulikuwa na malengo gani na yule mzee?” Jelini akatulia kidogo.
“Nikimaanisha hivi, ni malengo yapi yamevunjika uliyokuwa nayo na yule
mzee?” “Nikwambie ukweli Colins?” “Hilo ndio litanifurahisha.” “Kinachoniliza si
kuvunjika kwa malengo fulani. Maana hayakuwepo. Ila ile hali ya utulivu
niliyoipata nikijiaminisha nimepata mtu wangu. Ile hisia ya kuwa na mimi
napendwa na kuthaminiwa.” Akaendelea.
“Kasa si mnyama au
mkorofi sana kama wengi wanavyomuogopa. Tulikuwa kwenye wakati mzuri sana,
ndio maana niliweka matamanio yangu yote pembeni, nikakana nafsi ili nitulie
naye. Na ilikuwa nikiwa naye, kweli huwa napata wakati mzuri sana. Kucheka
kusiko isha na kufanya kutulia mpaka nafsini kwangu. Nilichopambana nacho kwake
hapo majuzi, hakikuwahi hata kupita akili, kwa jinsi alivyoniaminisha
ametulia na mimi.” “Ulimfumania?” Jelini akainama maana lilikuwa swali la moja
kwa moja.
“Umeniambia
utaniambia ukweli, Jelini.” Akajicheka taratibu kwa kujidharau. “Nilikuwa
nikitamani kukimbia Colins, ili baadaye aje hata anidanganye halafu
yaishe. Lakini miguu ilikufa ganzi. Nikashindwa hata kusogea, nikabaki nje ya
mlango nikisikiliza wanavyofanya mapenzi ndani.” “Haiwezekani Jelini!” “Kabisa
Colins. Sijui nini kilinipata. Kila nilivyokuwa nikitamani kuondoka,
nilishindwa. Nilibaki pale nikisikiliza mmoja baada ya mwingine wakipiga bao.
Yaani kilio changu ndio kiliwatoa kitandani. Na matusi ya mwanamke wake ndiyo
yalinisaidia kupata nguvu na kuondoka pale.”
“Alikutusi mbele yake
tena!?” “Hapana. Nirekebishe. Aliniambia ukweli ulionifanya nipate nguvu
ya kuondoka pale. Jamani yule mwanamke aliongea Colins, mpaka mimi ndio nikapatwa
aibu. Maana ukweli si kwamba niliwafumania. Ni mwanamke wake wa muda
mrefu tu, lakini aliniambia alimuacha kwa ajili yangu ili tubaki wawili
tu, kwa kuwa mimi mwanzoni kabisa nilimwambia sitaweza mahusiano ya watu wengi.
Sitaki kuja kufa na maradhi nikamuacha mwanangu. Heri wao waendelee.
Ndipo akanisihi sana nitulie, akiniahidi hatarudi kulala tena na yule mwanamke.
Tutabaki wawili tu.”
“Na wewe uliamini!?” “Ukweli niliamini,
Colins. Wala nisikuzungushe kujitetea. Ila kwa nini niliamini, maana wala si
kwamba alitumia mbinu nzito sana kuniaminisha, hapana. Maneno yake tu, nikaamini.
Ndio ujue sikuwa nikifikiria sawasawa. Na sijui nini kilinipelekea nijione mimi
ndio bora zaidi ya mwanamke wake, aliyekuwa naye kwa miaka yote hiyo! Mimi
sijui. Lakini kwa jinsi ya ajabu sana, hakika nilimuamini Kasa.” Colins akabaki
akimtizama.
“Sasa kujibu swali
lako, tulikuwa tukiendelea bila makubaliano yeyote.” “Ungeendelea hivyo mpaka
lini?” “Hata sijui Colins! Kuna mambo yanatokea ndio yanafanya mtu afikirie.
Kwa mfano yule mwanamke wake alikuwa akinihoji ukweli mtupu, kwamba mimi
nilitegemea nini kutoka kwa mwanaume kama Kasa? Kwamba kwa vile alivyo, je
nilitegemea aje anioe? Aje aanze kuzaa na mimi tena?” “Ambayo hayo ni maswali
ya msingi sana, Jelini!” Colins akaongeza kwa makini ila msisitizo.
“Basi mwenzio sikuwa
hata na mawazo hayo, zaidi ya kustarehe tu. Ila nahisi sasa hivi imenifanya
nifikirie zaidi. Ila kwa hakika, sikuwa nimempendea pesa. Alinijia
kwangu akiwa mshauri mzuri sana. Alinisaidia kufikiria zaidi maishani kuliko
kushinda baa na kwenda mziki usiku kuchwa. Akanivutia kwa mengi, akawa rafiki
tunayepigiana simu muda na wakati wowote tukiongea na kucheka. Nimepoteza
rafiki Colins. Kwa vyovyote alivyo, Kasa alikuwa rafiki ambaye tulikuwa
kwenye mahusiano mazuri sana, ndio maana nimeumia.”
“Pole Jelini. Swali
jingine. Akikurudia, akaomba msamaha na ahadi ya ndoa na mtoto, au watoto,
utafanyaje?” Jelini akainama akifikiria. “Hapo ujue kuna uhakika wa pesa.”
Jelini akacheka kwa masikitiko. “Mimi si mlevi wa pesa, Colins. Sina tamaa ya
pesa. Kama ningekuwa hivyo, sasahivi ungenikuta silii. Na wala Kasa mwenyewe
asingenipata. Nilikuwa na kunywa na wenye pesa zao, Colins! Pesa isiyo na
mawazo. Ila tabia ni kama hizi za Kasa, tena wanasema kabisa, si sabuni kwamba
itaisha. Kwa maana nyingine Kasa ni walewale tu. Fikiria kama nisingemfumania.
Nilikuwa safarini, si ningerudi nisijue kilichoendeleaa huku nyuma?” “Kweli.”
“Sasa kwa nini awe
yeye si wanaume wengine? Kasa hana cha ajabu na wanaume niliokuwa nikiwakataa.
Ila yeye alifanikiwa kunionyesha ni mwaminifu sana, na mimi nitabaki peke
yangu kwake kitu ambacho nafikiri alijua ndio shauku yangu, akatumia huo
udhaifu wangu.”
“Hiyo shauku bado
haijaisha?” “Maadamu James amefanikiwa kumpata Jema, naamini na mimi nitapata
tu, Colins. Sitakata tamaa. Najua nitapata mwanaume wa peke yangu, japo
nikisema hivyo watu wanaona kama naomba kitu ambacho hakiwezekani.
Lakini najua kinawezekana. Si wanaume wote ni malaya au hawatosheki. Ni bado tu
sijakutana na mtu wangu. Na ninajua ni muda tu. Sikati tamaa.” Colins
akatulia nakuonekana amepotelea kwenye anachowaza, kisichotoka mdomoni kama
mimba ambayo haijatimiza muda wake wakuzaliwa.
“Na mimi nikuulize
Colins?” Akaonekana amemtoa mawazoni, akamtizama. “Nipo kwenye kujifunza
na kurekebisha makosa. Nataka kujua kwa mtu kama wewe ulivyokuwa kwenye
mapenzi na Love. Msichana mzuri tu. Na anaonekana amesoma sio kama kina sie. Na
kwa jinsi nilivyomsikia Connie akimtambua, anayo kazi nzuri, nikimaanisha
yakueleweka. Halafu ametoka kwenye familia inayofanana na yenu. Nikimaanisha
lazima mtakuwa mkiendana kimaadili. Kingine kwa jinsi nilivyokushuhudia wewe,
unaonekana ulikuwa ukimpenda SANA, na kulinda chochote kisitokee kati
yenu ili usimuudhi mpenzi wako. Sasa ni sababu gani imewafanya watu kama nyinyi, msitishe mahusiano
kama hayo?” Colins akafikiria na kutaka kuzungumza kitu akitaka kurekebisha
kauli ya Jelini kwenye uulizaji wake swali, akasita.
Akafikiria tena,
akaona endelee tu si kukanusha. “Labda niseme hivi, niliishiwa.
Nikimaanisha, sikuwa na kitu kingine tena chakutoa tukaweza kuwa na
furaha na amani. Nilifanya kila kitu, na bado haikuwahi kutosha.
Ukifanya hiki, atahitaji kingine lakini pia kile ulichomfanyia kinakuwa
hakijatosha au hakikukamilika kwa usahihi. Tuliendelea hivyo kwa muda mrefu
sana, mwishoe nikaanza kuhisi napotea. Yaani mimi mwenyewe nikaanza
kujidharau nikijihisi labda nina matatizo, maana hapakuwahi kuja kutokea
ukamilifu kutoka kwangu!” Akaendelea.
“Sikuwahi kumfanya
mwenye furaha. Na kila nilipojaribu kufanya kitu, basi ujue kutakuwa
kunakukosea tu kiasi ya kwamba hata jambo zuri na la garama, wakati wote
linageuka kama si ugomvi, basi kununa. Nikaona si sawa kwake wala
kwangu, pengine anaweza pata mwanaume ambaye anaweza kumfurahisha. Nisimzibie.
Nikamuomba tuhitimishe tu.” “Alilichukuliaje?” “Alisema sawa tu.” Jelini
akabaki akimwangalia kwa mshangao, Colins akacheka na kutulia.
“Mimi hapo ndio huwa
nachoka Colins. Hawa wanadamu wanatakaga nini jamani!? Maana unajikuta umetoa
mpaka utu wako kumpa ili tu kumridhisha, lakini bado!” “Huwa
tunazungumzia sana hili na James. Lakini kila wakati tunaishia kuambiana hivi,
kuna kubweteka unapopata kitu kizuri. Na ikitokea unampata mnyenyekevu,
ndio kabisaa. Ipo hali hata ya kudharau mbali na kubweteka. Unajua si
yupo tu. Kwa hiyo unakua hujali. Ndio maana James ananiambiaga, kwa mkewe,
anafanya juhudi za makusudi. Maana kwanza mkewe ni mpole sana.” “Sana.
Jema mpole jamani! Na hataki ugomvi. Chochote anachojua kitaleta kutokuwa na
amani, bora anyamaze.” Akaongeza Jelini.
“Basi na mumewe
anasemaga hivyohivyo. Anasema ni rahisi sana kumsahau Jema. Anasema
akikumbuka kitu cha kumfanyia mkewe, hata kama yupo busy, anakiwekea alam ili
baadaye akumbuke.” “Ndio maana! Yaani mimi na mama huwa tunawasema,
hatuwamalizi! Bwana James anampenda Jema, na kumjali mpaka wivu! Ndio maana na
mimi nimepatwa hamu Colins. Mimi nilikuwa sifikirii swala la ndoa. Ila baada ya
kuwaona wale, nimetamani.” Simu ya Colins ikaanza kuita mfukoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaitoa na
kuiangalia. “Mama!” Ndio akili ikamrudia anahitajika kurudi nyumbani. “Naomba
turudi wote nyumbani.” “Naomba tu uende Colins. Nimeingiwa aibu pale, sijui
hata nikirudi nawatizamaje wale watu, zaidi mama yako na Connie. Maana
Love aliongea uchafu niliofanya nilipokuwa nimelewa, siku ya harusi! Na mbaya
zaidi kumbe alishampa habari zangu dada yako ila Connie hakujua kama ni mimi.
Halafu aibu ingine ni kilio nilichoshindwa kujizuia hata pale kwenu, sababu ya
yule mzee. Lazima watakuwa wananiona mimi ni hovyo sana. Na kwa ina ya
wageni wenu, na familia yenu, mimi pale hapatanifaa. Ninachotaka
kukwambia ni SIWEZI kurudi tena kwenu, Colins. Nikushukuru kwa kila
kitu, naomba wewe ukaendelee tu na wageni wenu.”
“Uliposema umebadilika,
ulikuwa ukimaanisha pombe tu au tabia kwa ujumla?” Jelini akashituka moyoni.
Ila akajikaza. “Najitahidi Colins.” “Kufanya nini?” “Kubadili maisha yangu kwa
jumla.” “Basi ujue ni pamoja na kusimamia maneno yako mwenyewe, na kuna usemi
unasema, own your own mistakes. Unanielewa Jelini?” Jelini akatulia.
“Mwaka huu umeniahidi
kumaliza na mimi na kuanza mwaka mpya pamoja. Gafla unanibadilikia! Halafu
unakimbia makosa yako mwenyewe! Ili nani arekebishe?” “Siwezi kubadilisha nyuma
Colins!” “Ila unaweza kubadili kuanzia hapa. Au unataka kuanza ‘kesho’ ambayo
haijawahigi kufika kwa yeyote?” “Mbona nilishaanza!” “Kwenye nini na nani? Au
wengine hatuna maana, ni rahisi kupuunzwa tu?” Jelini akashituka sana.
“Nakuthamini Colins
na wewe unajua!” “Najuaje?” “Mbele ya wenzio nilikuweka kipaumbele Colins!
Unafikiri huwa najali hivyo kila mtu?” “Kwa hiyo ilikuwa ni kwa mara moja,
basi?” Jelini akakwama. “Nilikuomba ramsi tuwe wote leo. Ukakubali.
Gafla unanibadilikia!?” Kabla Jelini hajajibu ujumbe kwenye simu ya Colins
ukaingia.
‘Pokea simu
yangu Colins mwanangu. Unanipa wakati mgumu.’ Aliposoma tu, hapohapo akampigia mama
yake kwa haraka. “Samahani mama. Lakini naombeni nyinyi
muendelee tu.” “Kweli Colins mwanangu? Tunaalika watu kwenye mji wetu, halafu
unakimbia? Sidhani kama ni sawa. Nikatalie kitu kingine lakini si hicho.” “Sio
kwamba nakukatalia mama, lakini..” Akasita.
“Ni juu ya
Jelini?”
Mama yake akamuuliza. “Nataka kuwa naye, mama!” “Kwa
nini usirudi naye tu?” Colins akanyamaza kama anayefikiria. “Colins?” “Nakuja mama. Usihuzunike. Nakuja.” “Sawa, lakini
ujue sijala nakusubiri.” Pakazidi kuwa pagumu. Ameshindwa kumtoa mama
yake barabarani kwa ahadi ambayo hata hakuwa amemaanisha. Hakuwa na mpango wa
kuondoka hapo na kumuacha Jelini usiku ule hata kidogo. Akihisi ndio nafasi
pekee ya kujisogeza karibu ya mrembo huyo aliyepo majonzini, akitaka yeye ndio
aweke historia moyoni kwa Jelini. “Colins?” Mama
yake akaita akitaka kujua kama amemsikia na kumuelewa kuwa hatakula
mpaka yeye arudi nyumbani. Colins akakumbuka bado mama yake yupo masikioni.
Nani zaidi?
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Colins akabaki njia pamba. Mama masikioni, mrembo mbele yake.
Anakwenda, au anabaki? Mwaka anamaliza na mama au Jelini? Akabaki hajui
chakuzungumza tena.
~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment