Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 36. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 36.

 Mama Jema anarudi nyumbani mida ya saa tatu usiku, akawakuta palepale kwenye kochi. “Nimekuja na chakula. Naombeni muhamie mezani.” Akaongea hivyo na kuendelea na yake. Colins akamchungulia Jelini pale alipokuwa amemlalia. Alikuwa ametulia kimya, alidhani amelala kumbe macho kwenye luninga, kimya. “Nikuletee hapa?” Akamuuliza kwa kumbembeleza akimpapasa taratibu. “Hapana. Acha nikalale tu. Sijisikii kula. Bado nimeshiba sana.” Colins akaendelea kumpapasa hapo kwa muda kisha akamchungulia tena.

“Natamani kukuona tena kesho, Jelini.” Jelini akabaki ametulia. “Utakuja nyumbani na mama pamoja na Jeremy?” Kimya. “Inakua nzuri sana. Watu wanakula na kunywa usiku kuchwa.” “Mimi niliacha pombe.” “Najua.” Jelini akashangaa sana mpaka akamwangalia. “Wewe si mgeni kwangu Jelini.” Jelini akabaki akimwangalia kwa mshangao kisha kujirudisha kumuegemea, na Colins naye akarudisha mikono hapo mwilini mwake akiendelea kumpapasa.

“Mimi huwa sinywi pombe. Au nisema kwetu hakuna anayekunywa pombe, ila baba yeye huwa anakunywa kidogo, tena mara moja moja sana, lakini kila mtu huwa anatizamia hiyo siku. Inakua nzuri sana. Najua unapenda mziki. Kunakuwa na mziki pia.” Jelini akashangazwa naye zaidi. “Amejuaje habari zangu huyu! Na mbona hajakinahiwa, bado yupo tu!?” Jelini akajiuliza nafsini mwake.

“Eti Jelini? Utakuja?” Jelini akavuta pumzi kwa nguvu na kujaribu kuzishusha taratibu. Kimya. Colins akisubiria jibu. “Natamani kukaa tu ndani.” “Haitakusaidia.” “Ni kwa muda tu, nikijipanga kuanza upya.” “Unafikiri mimi ninakuzonga?” “Hapana Colins. Ila natamani kujitafuta nafsi yangu kwanza. Kama ulivyosema, sitakiwi kurudi nyuma ila kuendelea. Nipo na wakati mgumu sana. Nataka kujifunza jinsi ya kukabiliana na changamoto zangu, bila pombe. Mimi kama Jelini.” “Na mimi nakuahidi kuwa na wewe Jelini. Sitaki uwe peke yako. Unapoona nakuzonga, niambie tu. Nitaondoka. Ukitaka ushauri, uwe na mtu wa kuzungumza naye. MIMI. Hata ukisikia upweke, nataka niwe mtu baki mbali ya mama yako, unayeweza kumpigia simu muda na wakati wowote na kuzungumza naye. Nataka tu kuwepo.” “Nashukuru Colins.” Hapo Jelini anashukuru, amemlalia ubavuni, mkono ameulaza kifuani kwa Colins, ameegemeza kichwa chake.

Akamchungulia tena maana alikuwa ameinamisha kichwa amelala. “Kwa hiyo kesho utakuja nyumbani?” “Nikiamka nikiwa sina maumivu ya kichwa, nitakuja na kina mama. Ila kama sitakuwa nikijisikia vizuri, mama na Jeremy wataniwakilisha.” Colins akanyamaza akiwa hajaridhika. Jelini akahisi, akanyanyua uso kumwangalia. “Nataka kuwa na wewe kesho, Jelini!” Akaongea kwa kumbembeleza na kumkumbatia kabisa kwa mikono yote miwili.

“Nataka kufunga huu mwaka, na kuanza mwaka mwingine nikiwa na wewe. Tafadhali Jelini.” Hivyo alivyokuwa akizungumza na kumshika, Jelini akalainika mwenyewe. “Basi nitajitahidi kufika.” “Hapo sawa. Na mimi nitakuja kukuangalia mida ya saa nne asubuhi. Si ni sawa?” “Nitashukuru.” Jinsi alivyomwangalia, Jelini akarudisha kichwa kifuani kwake kujiegemeza maana mwili wote ulishakuwa kama umepigwa shoti ya umeme, mapigo ya moyo tofauti. Ni Colins!

Wakatulia hapo kama dakika 15 mbele, mama Jema akatoka tena chumbani. “Kweli nyinyi hamtakula kabisa!?” “Jelini akienda tu kulala, na mimi naondoka mama. Nitarudi tena kesho.” Jelini akajitoa kwake na kukaa. “Nashukuru Colins. Wewe uwe na usiku mwema.” “Asante.” Akasimama, Jelini akamsindikiza mpaka mlangoni, akaondoka.

Nafasi Ya Mama.

“Njoo chumbani mama.” Mama yake akamfuata baada ya kufunga milango yote. Akamkuta amekaa kitandani kwake. “Ulimfumania na nani?” Hilo ndio likawa swali la kwanza, na la moja kwa moja. Jelini akaanza kulia. “Sikukwambia mimi wanaume wa hapa mjini ni malaya, hawajiwezi na zipu? Wewe ulikubalije kumpa moyo wako?” “Aliniambia anaacha wanawake wote, anabakia na mimi tu.” Mama yake akaguna. “Mimi nilimuamini mama.” “Ulimuaminije Jelini mwanangu wewe?! Gumegume la mjini, lenye pesa zake, halitosheki kuzimu wala peponi!” “Sijui nifanyaje! Roho inaniuma, halafu aibu!”

“Pole mama yangu. Ndio dunia inakukaribisha kwenye uhalisia. Huyo si ndio mwanaume wako wa kwanza kukubali kuwa naye kwenye mahusiano?” “Na nilijua ndio angebakia wa mwisho.” “Jelini mama yangu wewe! Kweli ulijua angekuoa na kukupa watoto mtu kama yule!? Aanze kulea vichanga?” “Mimi sijui kwa nini mama, nilijihakikishia nimefika na kumaliza. Ndio maana nikatulia. Sikuwa hata nikifikiria huko mbele.” “Mmmh!” Akaguna mama Jema.

“Ilikuwa mbaya mama! Nilikuwa natamani nikimbie nisiwe nimemfumania ili baadaye aje anidanganye tu, nimsamehe tuendelee, lakini miguu ikawa mizito. Siwezi hata kuondoka, wakati yeye yupo ndani na mwanamke wake wakifanya mapenzi, mpaka wanamaliza, mimi nimeganda tu, siwezi kusogea. Nasikia kila kitu ndani, nikitaka kuondoka, siwezi. Nikawa kama nimeganda, mpaka wakatoka na kunikuta hapo nje. Bwana mwanamke alinitukana yule.” “Jelini!”

“Acha mama. Kuondoka siwezi, kujibu siwezi, maana ni mwanamke wake wa muda mrefu aliyeniambia amemuacha kwa ajili yangu.” “Sasa Zenda akasemaje!?” “Usimuite Zenda. Anaitwa mzee Kasa. Yule hawezi kuwa Zenda. Zenda ni mwanaume niliyejiumbia kichwani nakutamani awe yeye. Hana uwezo wakuwa Zenda.” Jelini akazidi kulia.

“Pole mama yangu. Sasa akasemaje?” “Ni kama aliishiwa nguvu maana wote tulimkamata kwenye uongo wake. Yule mwanamke ananiuliza nalia nini kama nimemfumania Kasa, wakati wao walikuwa wakiendelea na yao kama kawaida? Akaniuliza maswali magumu mama, halafu kweli tupu!” “Maswali gani?”

“Maswali kama haya uliyoniuliza wewe. Ila sasa mbele ya Kasa mwenyewe. Kwamba mimi nilitegemea nini? Kwamba nitaolewa na kuja kuwa mama mwenye ile nyumba? Kwamba Kasa angekuja kuzaa na mimi? Na mengine mengi ambayo ni kweli mama. Ikanifanya nianze kujifikiria na kujidharau! Hivi nilikuwa nikifikiria nini muda wote huo!” Jelini akazidi kulia kwa uchungu sana.

“Nisikilize Jelini. Mimi najua wewe unapenda kupendwa, na kudekezwa. Ndivyo ulivyoumbwa. Yule mzee alikuonyesha upendo mkubwa, wewe ukapokea na kujifunga kwake. Huna kosa. Na usijilaumu kwa sababu wewe sio mjinga. Uliamini kutokana na alichokwambia. Na uzuri ni hukuharibu wewe, ni yeye ndio amekuwa sio mwaminifu. Huna utakapojilaumu. Ulifanya kwa kadiri ya uwezo wako, yeye ndio ameshindwa. Na hilo limenifurahisha kuona unauwezo wa kutulia. Usijiadhibu hata kidogo.”

“Natamani kuwa na mtu wangu mama! Kwani haiwezekani tena?” “Si huyo James anaye Jema? Nini kikushinde wewe?” Mama Jema akamuuliza na kuendelea. “Sio dunia yote imeharibika. Kama James amepata mtu kama Jema, kwa nini wewe usipate wako? Wala huombi na kutamani la ajabu.” “Au Jema amempata James?” Tayari Jelini alishaanza kumuelewa James, akajikuta safari hii yupo upande wake.

 “Kwa nilipofika sasahivi, na kuelewa watu na jinsi mwanadamu anavyoweza kubeba sura mbilimbili, acha niwe kama wewe ulivyokuwa mwanzoni. Kuongelea kwenye uhakika. Ulikuwa sahihi siku ile. Huwezi kumsemea mtu. Kwa sasa nina uhakika na Jema kwa kuwa nimemzaa, na kuishi naye kiumbe chenye maadili. Kama yupo mtu kama Jema, inamaana wapo wengine. Na wewe utapata tu. Tulia mama yangu. Wala huna haja yakulia.”

“Nimeamua kuachana naye kabisa.” Jelini akaongea kwa unyonge ila kwa wasiwasi kidogo. “Kabisa. Hee! Achana naye.” Jelini hakutegemea kusikia hivyo kutoka kwa mama yake. “Huna neno wewe!? Maana biashara hazijakaa vizuri na tunategemea pesa yake.” Akazidi kuumia. “Kumbe ndicho kinachokuliza!?” “Nakuhurumia mama yangu. Naona umeweka juhudi, zitaishia katikati tutarudi kuwa watu duni kwenye familia yenu. Tunarudi kuwa chini kwa ndugu zako na kurudi kukopakopa tena kwa dada zako kama zamani.” Mama Jema akashangaa sana.

“Zitanisaidia nini mimi hizo biashara zote halafu aje akuue na maukimwi? Pesa yote hiyo itanifaa nini, nikikupoteza Jelini, mama yangu? Hapana aisee.” “Kweli mama?” “Oooh kabisa. Mimi mbona hawa wanaume wenye pesa nipo nao hapa mjini miaka yote? Nawajua na nimeishi nikilea wanangu bila wao! Hamjawahi kulala njaa mpaka mmekua. Leo kiwe kimebadilika kipi? Si uongo pesa ilituletea unafuu mkubwa sana, lakini sio kifo. Hata kidogo. Yaani akulize hivi kila mara sababu ya pesa! Si nitamchoma kisu afe.” Jelini akaanza kutulia.

“Yaani hilo wala lisikutie wasiwasi. Wewe sio kitega uchumi changu Jelini mwanangu. Hujawahi na haitakaa kutokea. Nilimpokea sababu niliona anakuongoza vizuri. Lakini sijamzalia mtoto wa kuja kumuua. Hapo hapana aisee. Ataniona mbaya. Mwache aondoke na pesa yake, atuache alivyotukuta. Tulikuwa tukicheka hapa siku nzima bila pesa yake. Hatukupungua. Wewe tulia, tuanze kujipanga kwa tulicho nacho. Najua pesa ya kufungua kituo cha mafuta hatutaweza, lakini uzuri pesa yote ulikuwa ukiniachia mimi, na mimi sijaichezea, mbona tutajipanga tu na tutafanikiwa? Ilimradi sasa na wewe ubadilike.”

“Unamaanisha nini?” “Kwa tulicho nacho, tunaweza kufanya kitu kama tukisaidiana. Yale maisha ya kulala na kujitengeneza kwa mapesa mengi, inabidi ubadilike tuweke nguvu kwenye uzalishaji.” “Sawa.” Mama Jema akashangaa kidogo maana hakutegemea. “Ujue ni kuhaso haswa. Tunabadili gia angani. Hakuna kulala wala kuomboleza. Badala ya kufanya tulichopanga mwanzoni tuta..” “Unayo pesa yote. Na wewe ndio mwenye akili ya biashara. Panga, uwe unanituma kile unachotaka kufanya.” “Kama ukinipa uhuru wa kupangia pesa yote, haina shida.”

“Wewe endelea tu, mama. Mimi nakuamini sana wewe. Mimi najijua nilivyo mbaya na pesa. Nikiishika tu hiyo pesa, yote itaisha kwa matumizi yasiyo maana. Nafanya kama sinayo kabisa hiyo hela. Na wewe fanya kama yako kabisa, ili tusirudi kuwa ombaomba. Nataka usipate tena shida na mwangangu.” Hilo likamfurahisha sana mama Jema. “Basi usijali. Maadamu duka limeanza kuchanganya, pale tulipotaka kuuza mafuta tutaweka kitu cha kutuingizia tu pesa ila kwa uwezo wetu si wa Kasa tena. Acha kesho nitoke nianze kuulizia. Tutakuwa sawa tu, wala usijali. Tulicho nacho tutakizalisha, na sisi tutafanikiwa tu. Mbona wao wanaweza, kwa nini sisi tushindwe?” “Yule baba ananidhamu ya kazi mama! Anaamka saa 10 alfajiri. Saa moja na nusu alishakalia kiti chake ofisini. Mchapakazi bila kuchoka.” “Sasa hayo ndio yakuiga.” Wakazungumza na mwanae, angalau Jelini akatulia, na kulala.

Asubuhi.

Mida ya saa nne asubuhi mwanae akaingia hapo chumbani kwake. “Bibi amesema ukiamka unywe dawa kabla kichwa hakijaanza kuuma tena.” “Yeye ameshaondoka?” “Muda tu.” “Umekula?” “Tayari, na nishaosha sahani na kikombe cha maziwa.” “Jeremy wewe ni mtoto mzuri!” Akacheka na kumsogelea mama yake pale kitandani akaanza kuongea, stori nyingi, Jelini akicheka akimsikiliza. Wakasikia hodi. Jeremy akakimbilia mlangoni alikuwa Colins. Akarudi kumwambia mama yake.

Jelini akajiweka sawa ndipo akatoka. “Afadhali nimepokelewa na tabasamu.” “Jeremy alikuwa akinipa story za bibi huko migombani, walikotoka. Karibu Colins.” “Asante.” Akakaa. “Nipo kwenye maandalizi ya jioni, nyumbani, lakini nikaona nije kukuangalia kwanza kuhakikisha upo sawa, ili nipate uhakika wa uwepo wako jioni.” “Tutakuja Colins. Nashukuru. Kuna msaada wowote pengine mngetaka kutoka kwetu?” “Uwepo wenu tu. Kila kitu kipo sawa.” Colins alikaa kidogo na kuondoka.

Nyumbani Kwa Kina Colins.

Mida ya saa mbili usiku wakatoka wakiwa wamependeza tu, Jelini ametulia. Alikuwa akiendesha yeye mpaka nyumbani kwa kina Colins. Colins akatoka nje kabisa kuwapokea na kusaidia kuegesha gari sehemu nzuri ndipo wakaingia ndani. Wakakuta viti vimepangwa vizuri na watu wamekaa nje upande wa bustanini, akawasindikiza mpaka sehemu walipokuwa wamekaa Jema, James, na Connie akizungumza nao kama kuwapa kampani. “Nimefurahi kukuona Jelini. Hivi nimekaa hapa kufukuza watu ili mkija, mpate sehemu ya kukaa pamoja.” “Asante Connie. Na mimi nimefurahi kukuona tena, na asante kunikarimu nilipokuwa hapa.” “Basi mwenzio nikajua ungenipigia!” Connie akaongea kwa kulalamika, wakacheka.

“Kwa sasa sina simu Connie. Nikitulia nitatafuta namba, na wewe utakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuwapa namba yangu.” “Kama hivyo sawa.” Colins akawaletea vinywaji na kuwaambia anakwenda kumalizia kazi ya mbuzi waliyekuwa wakimuandaa wanaume huko nyuma ya nyumba yao, akiwepo baba yao. “Nitarudi, sitakawia.” Hayo anaongea macho kwa Jelini. Jelini akatingisha kichwa kukubali. “Na hicho kiti hapo pembeni yako Jelini, mtu asikalie wala kisichukuliwe. Ni changu.” James akatingisha kichwa kama mwenye masikitiko, wakacheka. “Nina wasiwasi sana na upande uliopo James.” Akaongea hivyo Colins na kuondoka na kuwaacha wakiendelea kucheka. Akasogea mama yao.

“Karibuni. Nimefurahi mmekuja.” Jeremy akasalimia kwa haraka. Akaitika mama Colins na kumwangalia na cheko kama mwanae Connie. “Huyo ni mtoto wangu mama.” “Ndio unakijana mzuri hivyo? Unaitwa nani?” “Jeremy.” Akajibu akicheka.  “Nimefurahi kukufahamu Jeremy. Uwe unawaambia wakulete na kwa bibi wa Mbezi. Sawa?” “Sawa.” Jeremy akakubali akicheka.

“Naona wageni wengine walitutangulia.” Mama Jema akamchokoza Jema. “Mimi niliwahi sambusa kama ahadi ya mama Colins.” “Nakuona una kazi ya kutafuna tu, hata  maneno hayatoki! Umebakiza kweli?” Wakaanza kucheka. “Za James amempa mwanae.” “Sasa mpaka huyo mtoto azaliwe, si zitaharibika kweli!” Mama Jema akazidi kumchokoza. “Nishamsaidia kumlisha mwanae.” Wakazidi kucheka. “Mpaka mjukuu wangu azaliwe, atasingiziwa mengi!” “Muulize James kama sijamlisha mwanae.” “Wewe kuwa na kiasi bwana Jema.” Wakazidi kucheka.

“Zipo nyingi mama Jema. Hizo nilimfichia Jema na mjukuu.” “Bora. Maana na zangu pia zingechukuliwa ili alishwe mjukuu.” “Hizo zako tunamuwekea ale kesho.” Jema akajibu bila wasiwasi huku akiendelea kutafuna, nakufanya wazidi kucheka.

Pombe Sio Chai.

Ikasogelea familia ingine. “Mpaka aibu jamani!” “Wala usijali mama Simba. Ujumbe wako nilishapata tokea mchana. Mimi mwenyewe nimewaambia nimekuwakilisha. Kazi zako zote nimekufanyia mimi na Connie.” “Mbona nishatumiwa taarifa zako. Nakushukuru.” Wakacheka. “Leo tulikuwa na wagonjwa wengi, wote tulitaka kumalizana nao kabla ya mwaka kuisha. Nimemaliza muda si mrefu. Nimekimbilia nyumbani ndio nikamwambia Love tuje.” “Shikamoo mama CJ.” “Marahaba Love. Umependeza!” “Asante. Vipi Connie?” “Mimi nipo. Kazini leo hukwenda? Maana uso unaonekana umetulia!” “Ninamapumziko niliyoyatumia ipasavyo. Yupo wapi Colins?” “Nyuma, na wazee.” Connie akamjibu Love.

“Huyu ni mama Jema. Yule ndio Jema na mumewe anafanya kazi na Colins.” “Nilikuwepo kwenye harusi yao. Mambo? Naona na ndoa imeshajibu.” “Mapema sana.” Akawahi James. Wakacheka.

“Na huyu hapa ni mdogo wake Jema, anaitwa Jelini.” Jelini kugeuka na kumwangalia ili amsalimie baada ya utambulisho wa mama CJ, ni yule mpenzi wa Colins. “Hee! Namfahamu sana. Huyu si ndiye aliyekuwa amelewa siku ile anatangaza kugawa mtoto?” Love akahamaki haswa, tena kwa kupaniki, wengine kimya

“We Connie! Huyu ndiye yule niliyekupa habari zake mpaka nikakwambia pombe si chai! Mpaka akawa anamlilia Colins kule nje! Eti wale wenzie ndio wakaja kumuita Colins ndani, eti akamtulize nje ili wamtoe pale ukumbini kabisa. Colins naye alivyo, eti akaenda. Nikamfuta na kumpiga marufu. Nikamwambia nisimuone naye tena. Pombe kazinywa kwa starehe zake, asituharibie siku. Ndiye huyu msichana.” Ikawa kama kapatwa na jazba. Anaongea kwa kupaniki, Jelini hana habari na yote hayo.

“Basi ndio ujue raha ya pombe. Unainywa mpaka inakukolea. Kesho yake huna unalokumbuka, unaacha watu wakikukumbuka, halafu wewe huwakumbuki.” Akajibu mama Jema. Jema akajua tayari kashanunua ugomvi, na hapo pataharibika vibaya sana kama yeye hataishia mshindi akimsadia mwanae. Huna utakapomuonea mtoto wa mama Jema mbele yake, akubali. Hajiwezi, hasaidiki. Bora yeye mwenyewe ndio ashugulike na wanae sio mwingine. Hapo hatanyamaza hata iwe mbele ya nani. Haoni shida kuharibu hata hapo uzunguni kwa wasomi, kisha kuondoka na wanae.

“Maana wewe umebaki na kumbukumbu ya Jelini, yeye kastarehe, hata hakukumbuki. Unabaki ukihaha wewe.” “Sio kwamba nahaha.” “Unahaha sana, ndio maana unaeleza habari zake humalizi wala kutosheki. Ulisha mtafuta Connie kumwambia kwa starehe zisizokuhusu. Na ndio maana hata siku ile aliitwa Colins sio wewe. Lakini pia bado unahaha na kumbukumbu ya Jelini.” Jema alishamsimulia James juu ya mama yao. Hata yeye akajua mama Jema kashachemka katikati ya wamama hao wasomi. Ila aliambiwa akiwa kwenye hiyo hali, asiingiliwe mpaka atulie mwenyewe, lasivyo nikuharibu zaidi. Basi James na yeye kimya kama Jema.

“Sasa hii meza itanywewa pombe. Ili kukupunguzia shuguli, hapa ondoka, tupishe tuanze starehe zetu. Lasivyo, vuta kiti na wewe ujiongeze.” “Mimi sinywi pombe.” Love akajibu kibishi ila kama kudharau unywaji wa pombe. “Basi hapa hapatakufaa. Ongoza njia, tupishe.” Huyo Love, na mama yake wakaondoka. Jema akahema kwa nguvu, maana alijua dakika moja mbele ya hayo mazungumzo kama yangeendelea, na Love kumjibu vibaya mama yake, pasingekalika hapo, na yeye alikuwa akisubiria nyama choma.

“Samahanini jamani.” Akaongea hivyo mama Colins na yeye kuondoka. “Jamani samahanini sana.” Connie naye akaongeza. “Jelini naomba usikasirike. Ndivyo Love alivyo. Muwazi sana, na huwa anaongea chochote hajui kuchuja mambo.” “Usijali Connie. Siku ile nilizidisha pombe. Wala sikujua kama nilifanya mambo ya ajabu kiasi hicho!” Jelini akaongea kinyonge. “Wala usijali. Acha nikawaonyeshe meza yao. Maana baba yake Love alishatangulia hapa muda mrefu sana tokea mchana, wanasaidiana na dad kutengeneza mbuzi huko nyuma. Alitaka wakija wakae kwenye ile meza yao kule.” “Hamna shida, Connie mwanangu. Wewe endelea kukarimu wageni.” Mama Jema akajibu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jelini akainama pale kwa muda, akijifikiria. Mengi yalikuwa yakiendelea kichwani bila majibu. “Hawa watu kweli wamejiandaa kukesha hapa!” James akavunja ukimya. “Mama Colins ameniambia nikichoka, kitanda kinanisubiri.” “Maana wewe hapa huondoki?” Mama Jema akamuuliza Jema. “Si ndio tumekubaliana tunafunga mwaka na kufungua mwingine hapahapa? Nishafika mimi.” “Unapenda kula kwa watu wewe!” Kidogo wakaanza kucheka. “Mimi nimekaribishwa, mama Jema. Kosa langu kuitikia wito?” “Wewe una mengi bwana.” “Acha nikachungulie huko nyuma, wanaume walipo, nione kama kuna chakusaidia.” “Bora.” Akamjibu mkewe, James akaondoka.

Maji Shingoni.

Jelini akafungua pochi, akatoa funguo na kumkabidhi mama yake. “Vipi?” “Acha nikapumzike mama. Sijisikii vizuri” “Jelini bwana!” “Wewe na Jeremy bakini na Jema. Acha nikatulie mama yangu. Nikijisikia vizuri nitarudi tufunge mwaka pamoja. Nawaachia gari.” “Sasa utarudije nyumbani!?” “Kweli mimi ndio wakuniuliza jinsi yakufika nyumbani kweli!? Wala usiwe na wasiwasi. Mapema hivi, nitafika tu.” Akanyanyuka na kuondoka. Akamuacha Jema na mama yake hapo kimya, wakiwaza yao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda akarudi Connie, akakaa. “Jelini yuko wapi?” “Ameenda kupumzika nyumbani. Amesema akijisikia vizuri, atarudi.” “Angepumzika hata chumbani kwangu! Asingeondoka.” Connie akaongea kwa kulalamika kidogo. “Atakuwa sawa tu.” Akajibu mama Jema. Wakatulia. Baada ya muda akarudi James na nyama kwenye sahani. “Nyama za mwanangu, aonje.” “Mmmh!” Mama Jema akaguna, Connie hana mbavu.

“Sasa mama wewe unaguna nini, wakati James kamletea mwanae?” “Mama Colins huyo ndio kanituma nyama za wajukuu. Tena amesema wale wote wawili na Jeremy.” “Sasa Jema uwe na kiasi, na Jeremy apate.” “Kwani mimi nina neno. Umesikia ni kuonja tu. Njoo mwaya Jeremy mwanangu ule na mdogo wako.” Jeremy hana mbavu kama Connie.

“Wewe bibi huli?” Jeremy akamuuliza bibi yake kwa kumjali. “Acha mimi nisubirie za wote. Kula baba.” “Sasa Colins yupo wapi?” Connie akamuuliza James. “Ameenda kuoga atoe jasho. Alikuwa akinuka moshi.” James akakaa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda Colins akafika hapo. “Jelini yuko wapi?” Akauliza kabla hajakaa. Kimya kwa muda. “Connie!?” Akamgeukia dada yake. “Mimi mwenyewe sijamkuta. Wameniambia amekwenda kumpumzika.” “Chumbani kwako?” Colins akazidi kumuhoji dada yake kama aelekee chumbani kwa dada yake. “Kwao.” Bila kuongeza kitu akaondoka. “Sasa unaenda wapi?” “Kuchukua funguo za gari, namfuata.” Wote wakabaki wanashangaa.

Wakati anaondoka. “Colins?” Akaitwa na mama yake alipokuwa amekaa na kina mama Love na wanawake wengine. “Nakuja mama!” Akajibu kama anayecheleweshwa. “Wapi, mbona mbiombio? Njoo usalimie bwana, wewe vipi?” “Nakuja mama! Namfuata kwanza Jelini. Narudi sasahivi.” Akaondoka kurudi ndani. Akachukua funguo za gari, akawa anatoka. Wakamuona anapita kwa haraka na baba yake akatokea pembeni ya nyumba akamuona. “Colins?” Akasimama. “Njoo usaidie ku..” “Nitarudi muda sio mrefu. Mtume mtu mwingine.” “Wewe unakwenda wapi bwana? Wakati tunataka tuanze kula, watu walikuwa wakisubiria nyama tu. Ishakuwa tayari na wewe ndio..” “Nitarudi dad. Nyinyi endeleeni tu.” Akajibu hivyo, wakamuona anaondoka kama anayekimbia. Akamuacha baba yao ameduaa kama ambaye hajaelewa.

Mkewe akasimama kumfuata. “Umemtuma wapi huyu!? Mbona mbio mbio!” “Wewe muache. Unataka usaidiwe nini?” “Nyama imeshakamilika. Inatakiwa kuletwa huku. Nilitaka awasaidie kina mzee Simba kuleta huku.” “Wewe nenda kaoge, nitakamilisha hili.” Mzee akaingia ndani, mama Colins akazunguka nyuma kwenye hiyo nyama. Jeremy, Jema, mama Jema na Connie wakijiangalizia. “Acha nikamsaidie mama. Nakuja.” James akasimama na kumfuata mama Colins.

 “Wewe Connie, kakae na wenzio acha kujitenga. Sisi hapa tumeshafika. Kafurahie na wenzio.” “Nyinyi ni wageni wetu anti Jema. Sitaki mjisikie wapweke.” “Wala usitujali sisi. Tukiwa na shida tutakuita.” “Kweli anti?” “Sasa hapa utaongea nini na mama Jema?” Wakacheka. “Wewe kakaae na wenzio Connie. Sisi hapa tupo sawa.” “Basi nitakuwa nikija kuwaangalia kila mara, ili msipungukiwe.” “Hayo ndio maneno.” Akaondoka akicheka akielekea lilipokuwa kundi la wasichana wenzie, akiwepo Love.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Huyu Colins alimkataa Jelini, akafukuzwa na mzee Kasa, AMERUDI akionyesha kumfahamu Jelini kwa undani mpaka kumtisha Jelini mwenyewe.

Nia nini?

Umbali gani yu radhi kwenda na Jelini mwenye mengi?

Mze Kasa? Waliopo Gerezani?

Usikose muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment