“Colins huyu ni mtoto
wangu. Anaitwa Jeremy.” Jelini akamtambulisha akidhani Colins hamfahamu.
“Nimefurahi kukuona tena Jeremy.” “Tena!?” Jelini akauliza kwa mshangao.
“Siku ya harusi ulimtangaza kuwa ni mtoto wako.” Jelini akaanza kuingiwa hofu,
hakuwa akikumbuka. Ila kwa alivyosimuliwa maajabu aliyofanya, kumbe mpaka kina
Colins walisikia! Akamtizama na kukwepesha macho kwa aibu.
“Siku ile ulivyokuwa
ukinigawa, ulinitangaza pale mbele za watu wote.” Mwanae ikabidi kumkumbusha. Jelini
akaumia sana. “Samahani Jeremy. Nilizidisha pombe,
hata sikujua kama nilifanya mambo ya ajabu kiasi hicho! Unajua mimi sitaki
kukugawa hata iweje utabaki na mimi pamoja na bibi. Wewe ni mtoto mzuri sana
Jeremy, na nakupenda.” Mwanae akamuegemea tu na kunyamaza. Jelini akazidi
kuumia. Wengine kimya.
“Jeremy wewe ni mtoto
mzuri sana. Na unafanana sana na mama yako.” Colins akamsifia akimchungulia
pale alipokuwa amejilaza. “Asante.” Akashukuru na kupoa. “Acha kulia Jelini.
Kichwa kilitulia kwa muda mrefu, usifanye kikaanza tena. Una kitu unataka
kuchukua chumbani kabla hujaondoka?” Akafikiria akakumbuka ana vitu vyake vichache
alivyokuwa akizunguka navyo nyumba hadi nyumba kutokea Moshi, kwa Zenda,
hotelini, kwa kina Colins mpaka hapo.
“Kaa vizuri nakuja
sasahivi tuondoke ukapumzike.” Akamwambia mwanae ili atoke pale alipomuegemea.
Akakaa vizuri. Jelini akanyanyuka kuelekea chumbani. “Nakushukuru Colins kuwa
naye tokea sisi tuko Moshi.” “Karibu mama, japo sisi ni familia.” Akajibu
Colins kiungwana. “Sasa sijui itakuaje maana pale kwetu sisi tuna vyumba viwili,
cha tatu ni ndio kimemaliziwa kujengwa upya kwa ndani. Kitupu kabisa. Jelini
alitaka vyumba vyote kujengewe vyoo na kufanyiwa ukarabati. Kwa hiyo hicho
kilichobaki cha tatu ndio cha mwisho kutengenezwa ambacho ni cha Jeremy. Tumebakiwa
na viwili tu. Changu ambacho natumia na huyu kaka, na hicho cha Jelini.” James
akamtizama Colins kama anayemwambia umeshikwa pabaya!
“Hakuna shida kabisa.
Naona hata yeye ameanza kutulia. Nitakuja tukae mpaka usiku ndipo nirudi
nyumbani. Ila nilitaka kuwakaribisha nyumbani kesho. Tunafunga mwaka kwa
tafrija ndogo tu, ila tukiwa na marafiki wa karibu. Zipo familia kadhaa huwa
tunakutana. Ni marafiki wa wazazi tangia sisi ni wadogo sana. Tunapeana zamu
kila sherehe. Hii ya mwaka mpya itakuwa nyumbani kwetu. Tunapata muda wakumshukuru
Mungu pamoja, kisha kula na kunywa tukisubiria mwaka mpya. Inakua nzuri
kwakweli. Ningependa na nyinyi muwepo.”
“Mama yako
ameniambia. Lakini nikamwambia inategemeana na hali ya Jelini. Kichwa kikiwa
sawa, tutakuja.” “James na Jema, je?” “Kama kuna nyama choma mimi na mke wangu
hatuna neno. Au unasemaje Jema?” “Na mimi mama Colins amenipigia leo
kunikaribisha. Wala nisiwe muongo, nilikubali haraka maana aliniambia
kunakuwa na vyakula vingi na sambusa.” Wakaanza kucheka.
“Hivi nilisahau tu
kumwambia James. Ila kwa kuwa hatukuwa na ratiba ingine, na alisema kutakuwa na
maombi, wala sikuona shida.” “Basi maadamu Jema ameshakubali, sisi tutakuwepo
Colins.” “Basi nashukuru.” Jelini akatoka na kimkoba chake. Kilionekana kizuri
na cha thamani pamoja na pochi. “Mimi nipo tayari mama. Jema na shem,
nawashukuru kunivumilia na kuwa na mimi.” “Wala usijali Jelini shemeji
yangu. Naamini kila kitu kitakuwa sawa.” “Na mimi naamini hivyo shem. Muwe na
jioni njema.” “Acha mimi niwatoe.” “Wewe tulia hapo. Unatutoa wapi na jua kali
hili?” Jema akaanza kucheka. “Mama Jema hutaki kukarimiwa?” “Utaniangukia bure
na hilo jua hapo nje. Wewe kaa, nitakupigia baadaye.” Colins alishaingia ndani
kukusanya vyake na yeye. Akatoka.
“Naomba niwafuate
nyuma nikiwa na Jelini, na Jeremy.” James akatingisha kichwa. “Sasa wewe James
unashida gani?” “Sijawahi kukupatia mwenzio Colins! Hivi kwa nini ukipanga
jambo lako kichwani, na kulipitisha, nilazima libakie hivyohivyo? Huna aibu
wewe hata kwa wageni?” “Mama Jema ni mama yangu. Sasa aibu ya nini? Halafu ujue
bado sikuelewi upande ulipo wewe James!” “Basi bwana. Lakini mimi nisingefanya
hivyo.” Colins akacheka na kumgeukia mama Jema. “Yaani tunakua tukiendesha
nyuma yenu tu.” Akaongeza ushawishi. Mama Jema akacheka akiwa ameshapewa
taarifa zake na Jema pamoja na mama yake huyo Colins, jinsi alivyomganda
Jelini.
Akamtizama Jelini.
Jelini alikuwa ameshika mwanae mkono wanakaribia mlango. “Asante Colins.”
Akajibu hivyo wakajua amekubali. Akawahi mlangoni kumfungulia mlango, James na
Jema wakicheka. “Tunashukuru kwa kutuhifadhi, jamani. Mama mwenye nyumba wetu?”
“Wewe muda na wakati wowote, karibu Colins. Milango ipo wazi.” Jema akajibu. “Nashukuru
sana.” Wakatoka hapo na kumuacha James na mkewe. Kikao kikahamia nyumbani kwa
mama Jema.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Njiani Jelini alikuwa
kimya akiogopa hata kumuongelesha au kumwangalia Colins. Na Colins alijua.
Macho chini muda wote akimbembeleza mwanae kiti cha nyuma. “Utakuwa sawa,
Jelini. Usiogope.” Akajaribu kumrushia neno la faraja akimwangalia kupitia kioo
cha katikati ya gari. Lakini Jelini akashindwa kujibu, akabaki ameinama
nakushindwa hata kujibu. Akaona amuache tu. Safari ya kwenda Tegeta nyumbani
kwao ikaendelea mpaka wakafika.
Akamsaidia kumbeba
Jeremy alikuwa amelala. Akamuingiza ndani, bibi yake akamwambia amlaze kwenye
kochi, atamuingiza ndani baada ya kuingiza mizigo. Jelini akaelekea chumbani
kwake kubadili nguo. Akakaa huko kwa muda mpaka aliposikia kumetulia, akajua
Colins amekaa peke yake sebuleni. Akatoka. Akaenda kukaa kochi la pembeni
kabisa.
Ukweli nyumbani kwa
kina Jelini kulibadilika. Na anavyopenda vitu vizuri! Palivutia. Aliweka
marumaru nzuri sana. Makochi ya hadhi, na meza pia. Hiyo tv, kama ya ukumbi wa
sinema. Kubwa. Wakapapangilia vizuri hapo na sehemu ya kulia chakula na meza
pamoja na viti vyake vya thamani sana. Pakapoa vizuri. Yote hiyo pesa ya Kasa.
Akachukua rimoti
akawasha tv. “Unataka kuangalia nini nikuwekee?” Akamuuliza akionyesha kujali lakini
bado akishindwa kumtizama. “Nataka ukae karibu yangu Jelini. Huko mbali!”
Jelini akajifikiria akiwa ameinama. “Au unataka nikupe nafasi, niondoke.”
Akapandisha mabega kukataa akiwa ameinama. “Basi naomba tukae wote.” Na sauti
ya Colins ilivyo nzuri, nzito na yakubembeleza, Jelini akahamia kwenye kochi
alipokuwa amekaa, akamsogelea na kumuegemea. Alifurahi Colins! Akapitisha mkono
kwa juu. Jelini akajivuta vizuri, akawa kama amemlalia ubavuni. Wakatulia.
Mama Jema kutoka
hapo, akachoka kabisa. “Sasa nyinyi wawili, hamli?” “Tumekula mchana kwa
kuchelewa. Eti Jelini, unataka kula nini?” “Hivyo ulivyomshika huyo, atalala
sasahivi na hatakumbuka kula. Mimi namjua Jelini jinsi anavyopenda mikono. Yupo
hivyo tokea mtoto. Ukimuweka chini tu, kilio. Ndio maana nilikuwa nikimfunga
mgongoni masaa yote ili nifanye kazi. Basi unadeki humu ndani na yeye umemfunga
mgongoni mpaka mwisho. Lasivyo kazi haziendi. Na ndio yupo hivyohivyo.” Colins
akacheka na kumwangalia vile alivyotulia. Na alitulia kweli, kama paka.
“Jelini, chakula?”
Akakataa. “Mbona mimi sishangai. Sasa sisi tulikula wakati tupo njiani. Kaka
ameshiba ndio maana usingizi mwingi. Natoka mara moja kuangalia mambo yangu,
nitarudi.” “Basi mimi siondoki mpaka urudi.” Mama Jema akacheka. “Haya Colins.”
Wakasikia gari, wakajua ameondoka maana Devi alipoacha tu gari hapo na kuingiza
vitu ndani, kazi yake kwa siku hiyo ikawa imeisha. Mama Jema akamlipa kwa
kumuendesha. Akaondoka.
Kwa Zenda.
Alipokuwa akitoka
hapo, Mzee Kasa akampigia kuwa afike nyumbani. Kwa haraka akatoka hapo Tegeta
mpaka Mikochini nyumbani kwa mzee. “Mlisafiri salama?” Hilo ndilo likawa swali
la kwanza. “Ndiyo.” Akajibu Devi. “Ulifanikiwa kumuona Jelini?” “Ndiyo. Lakini
nafikiri ni mgonjwa. Binafsi hakuniongelesha kabisa. Ila uso na macho vilikuwa
vimevimba na vyekundu sana. Na nilimsikia mama yake akipiga simu huku tukiwa
njiani akiulizia hali yake kutoka kwa dada yake. Nafikiri ni mgonjwa.” Mzee
akatulia kimya kwa muda.
“Ila nimewarudisha
wote nyumbani kwao.” “Kemi ulimwambia mngerudi lini?” Likawa swali la mtego,
Devi asijue. “Kama tulivyokuwa tumepanga na Jelini. Kuwafuata baada ya mwaka
mpya. Tarehe moja. Maana Jelini alisema niwapeleke, kisha niwaache.
Wangesherehekea sikukuu ya krismas na mwaka mpya. Akataka niwafuate na
kuwarudisha huku tarehe moja ya mwezi wa kwanza.” “Kwa hiyo na Kemi ndivyo
ulivyomwambia hivyohivyo?” Mzee akataka uhakika. “Ndiyo.” Devi akajibu asijue
ametegwa na kutegeka vibaya sana.
Mzee alikuwa
akimsubiri kwa hamu ili kujua wanae na mkewe wamejuaje kwa undani juu ya
Jelini? Alipo kwa wakati huo mpaka kuweka mipango ya Koku kuja kulala kwake!
Akafikiria kwa muda, akajua lazima tu atakuwa Devi. Ndipo akatumia akili ya
haraka jinsi ya kumtoa ukweli.
Sasa hili swali linalofuata
ndilo lililomfaya Devi ajue si shari. “Na nini kingine walikuuliza juu ya
Jelini?” Devi akatulia. “Nakuuliza, na sitataka kujirudia.” “Hakuna kitu
kingine.” Devi akashindwa kuwa muongo mzuri kwani tayari alishakuwa na hofu. “Nilazima
nijue ukweli. Na kwa kuwa nilazima, basi ujue utaniambia tu. Aidha itakua hapa
au polisi.” Devi akazidi kuingiwa hofu. Akashitukia wanaume wawili
wanawasogelea hapo barazani. Kama waliokuwa wamejificha na kusimama nyuma yake
kwa karibu sana. Devi akatishika sana.
“Nitarudia kwa
manufaa yako. Swali, ni mambo gani uliyokuwa ukiwaambia juu ya Jelini?” Devi
akameza mate na kuwatizama hao wanaume nyuma yake. Kwamba hakuna jinsi
akakimbia hapo na kubaki salama. “Kiukweli dada Kemi alitaka kujua habari zake,
Jelini. Anakaa wapi na anaishije hapa. Aliuliza kwa uzuri tu. Na mimi
nikamwambia. Na nilimwambia mambo mazuri tu kuwa, unaonekana umempenda sana
Jelini. Kwa jinsi mnavyoishi naye. Hata ile kutoka kuja kumpokea nje nikimleta.
Na vile unavyomjali hata kwao.” “Kivipi?” Zenda akataka kujua zaidi.
“Kwanza ni yeye
mwenyewe dada Kemi alitaka kujua kama unamjengea nyumba mahali. Ndio
nikamwambia sijui. Ila ni kama unajenga kwao upya. Kuanzia nje mpaka ndani,
umepabadilisha. Umemwaga mafundi kama mchwa wakishambulia nyumba yao kuijenga
kisasa. Kwamba hata paa ya nyumba ulibadilisha na kuweka vigae na madirisha.
Kwamba ilibidi wahame pale kwa muda kupisha ujenzi.” “Yoote hayo unayatoa
kwangu na kuyahamisha pasipo wahusu!?” Devi kimya.
“Sasa nakupeleka
ndani, walipo hao wenzako kwa kuwasaidia kuweka njama za kutaka kunidhuru
mimi. Wewe umewasaidia kuwapa habari zangu na kuhatarisha maisha yangu. Kitu
kilichosababisha kumuumiza Jelini. Mchukueni.” Mzee akaingia ndani, Devi
asiamini. Akaanza kuomba msamaha. Mzee akafunga mlango. Wale askari kanzu
wakaondoka na Devi.
Huyo mzee akawa amefunga
wanae wote wawili, mume wa Kemi, Koku na huyo Devi. Anawakwa hasira utafikiri
alishikiwa bastola kulala na Koku mpaka kufumaniwa. Alijawa chuki akitaka
waumie kama anavyoumia yeye. Wamemtenga na Jelini! “Hakika watalipa.”
Akaapa kila wakati alipokumbuka makubaliano yake na Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwamba kifo cha mahusiano
yao, ni pale mmoja wao atakapolala na mtu mwingine. Hilo
walihakikishiana ni kosa ambalo hawataruhusu mjadala. Kwamba siku mmoja
wao atakapokuwa kitandani kimapenzi na mtu mwingine, ndio amehitimisha mapenzi yao.
Kingine kinachomliza Jelini,
ni maumivu ya kuchaguliwa Koku, na kuachwa yeye. Akakumbuka sarakasi
zote alizozifanya kwa huyo mzee, akijua ndio amemfunga, amemdhibiti hawezi
kwenda kwa mwingine, amempa kila kitu mwanaume atakacho, halafu kuja
kumfumania, sio katikati ya tendo, akiwa mzee anashangilia goli, kwamba yuko aliyefanikiwa
na yeye kumfikisha kileleni!
Halafu ni Koku
aliyemuapia amemuacha, hana sababu ya kurudi kwake tena! Jelini alijisikia kufedheheka
sana. Ujanja wote ukamuisha zaidi kwa Jema na kwa ndugu alioanza kuingiwa hofu
wakijua ameachwa sababu ya mwanamke mwingine! Kwamba ni mjuaji asiyejua!
Akasikia aibu hata kabla hajachekwa. Akajitengenezea visa vyake vya
kudharaulika, vikazidi kumuumiza yeye mwenyewe.
Na Mzee naye kinachomuumiza alijua kabisa, no
point of return. Ndio mwisho wake na Jelini kitu alichokuwa amehakikishiwa
na Jelini kuwa naye mpaka kifo. Jelini aliishi hicho kiapo na Zenda kana kwamba
ni mke wa ndoa, akifungia macho vishawishi vyote, akimuhakikishia ametulia. Na
mzee alimuona jinsi alivyotulia, maana alimchunguza na kumbana atakavyo, Jelini
hakuingia mtegoni. Hakujua kama Zenda ndio angekuwa chanzo chakuvunjika
mahusiano yao, japo haWAkuwa wamefikiria muendelezo wao. Yaani asubuhi
ya fumanizi ndio Koku akawafungua wote akili na kumfanya mzee afikirie
zaidi.
Yupo na binti mdogo
hata hajafikisha miaka 25. Kwamba angetaka kuwa na watoto. Je, angekuwa tayari
hapo alipofika kimaisha nakuanza kubadili diaper kwa kachanga kake na Jelini?
Je, angempa ndoa huyo Jelini kwamba waanze kuishi humo ndani asubuhi mpaka
asubuhi, akijulikana Jelini ni mkewe? Kwamba maisha yake yabadilike yaongezeke
mtu? Sio penzi la kuiba la weekend tu. Ni mpaka kifo! Koku akawapigia kengele
asubuhi hiyo ya fumanizi, ndio wakaamka na kukutana na ukweli wa maisha.
Jelini akabaki akiwaza kwake. Na mzee kivyake huku akitoa adhabu kali kwa kila aliyemuhisi.
Swala la kuhamisha maneno kutoka
nyumba moja kwenda kwingine, likamponza Devi, tayari akabambikiziwa kosa la
kusaidia kutaka kuua.
~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment