Jema akagonga na
kuingia na dawa. “Nimemletea dawa za kichwa.” Colins akapokea na kushukuru.
“Nashauri ukapumzike Jema. Akitaka kitu mimi hapa kwako si mgeni.” “Basi
ukizidiwa, uje kunigongea chumbani kwangu. Na James naye yupo karibu kuja.”
“Wewe nenda kapumzike.” Akamchungulia Jelini pale alipolala. “Jaribu kutulia
ili na kichwa kitulie. Usikubali kuendelea kuteswa. Kuna mambo unaweza
usiwe na amri nayo kwenye maisha, ila mengine unayo. Usikubali kujiumiza
mwenyewe. Tulia kabisa ukijikumbusha unawajibika na maumivu ya kichwa chako.
Yakupasa utulie ili kichwa kipoe. Mama anakuja kesho.” “Asante Jema. Nitalala.”
“Hayo ndio maneno. Haya usiku mwema.” Akawaaga na kutoka.
Akampa dawa, akarudi
kujilaza kwenye mto. Colins akavuta mto mwingine juu yake akawa kama
anamchungulia kwa chini alipolala. Akaanza kumchezea masikio taratibu. Huku
Jelini akizipata pumzi zake sawia. Akaanza kujisikia raha. Anachezewa na Colins!
“Asante kuwa na mimi Colins.” “Karibu. Kuna njia unaweza kutumia kupunguza
kelele ya ulichokisikia.” Jelini akanyanyua uso kwa haraka kama aliyeambiwa
kuna tiba ya uchungu wake, macho yakagongana. Akahamisha vidole kwenye nyusi.
Mwili mzima wa Jelini ukawa kama umepigwa shoti kukutanisha macho yao.
Akakwepesha.
“Kila ukisikia hiyo
sauti, unaweza kuhamisha mawazo hapo. Au ukaangalia movie mpaka kwa muda fulani,
hadi makali yake yapungue. Au nitakufundisha game, uwe unacheza. Itakuondolea
mawazo huko.” Jelini akatingisha kichwa kukubali. “Unataka niweke movie?
Nitaweka laptop hapo mbele yako, huna haja yakukaa.” Akafikiria kuwekwa hiyo
movie inamaana hatashikwa tena. Jelini mpenda mikono. Kubembelezwa.
Akilinganisha na kuangalia movie! Akasita. “Ni nzuri. Itakufanya ulale.”
Akaweka ushawishi asijue shida ya huyo Jelini ni hiyo mikono yake iendelee
kuwepo kwenye mwili wake. Ila mwishoe akakubali. “Sawa.”
Akatoka hapo na
kuchukua laptop. Akawasha na kuingia nayo kitandani. Akaiweka mbele yake.
“Unaona?” “Unaondoka?” “Unataka niondoke?” Yakawa maswali matatu ambayo
hayajajibiwa. “Ni sawa tukibaki wote?” Likaongezeka la nne kutoka kwa Jelini,
kwa sauti ya kubembeleza. “Kwamba nilale hapa!” Colins akawaza kwa
haraka, akihisi bahati ya mtende inataka kumuangukia, lakini akiogopa asije
akawa amejichanganya, Jelini hakumaanisha hivyo. “Kama hutajali lakini.”
Akaongeza taratibu. “Basi tutakuwa wote usiku wa leo. Sitakuacha. Ukisikia
usingizi, ulale.” Akajisogeza karibu yake, Colins akajua anataka mshike.
Akafurahi moyoni.
Alichokifanya Colins
ni kurudisha mto juu yake, akalala juu kidogo ya mto alio lalia Jelini, laptop
mbele yao. Akajiegemeza kidogo pembeni yake. Uwepo wa Colins ukajaa hapo kwenye
hisia za Jelini, akaanza kutulia nafsini. Kwa mbali akaanza kuhisi ndevu zake
pembeni ya kichwa karibu na shavu. Jelini akajisogeza karibu zaidi, akaendelea
kumpapasa. Hakujua movie ilifikia wapi, ila akalala kama katoto kachanga
akipapaswa na Colins.
Uthamani wa Ulicho Nacho.
Huku kwa Jema akabaki
amejilaza akiwaza anakopita mdogo wake. Akajifananisha na alikopita. Kwa hakika
akamshukuru Mungu kumtumia James. “Inamaana ningekaa na ile fedheha mpaka
sasa! Asante Mungu wangu.” Akajisikia kumpenda James sana. Mara mlango
ukafunguliwa. “Pole mpenzi wangu.” “Hujalala tu!?” “Nilikuwa nikikuwaza wewe.”
“Kwema?” James akamsogelea pale kitandani.
“Niambie kwanza huko jinsi
ulivyopakuta.” “Hapana bwana Jema. Wewe ndio muhimu kuliko kila kitu. Niambie.”
James akasisitiza. “Mimi nipo sawa, ila namuhurumia Jelini, kwa kuwa hapo
alipo, mimi nilikuwepo. Wengine wanaweza wasielewe, lakini mimi nahisi ana roho
kama yangu. Alijifunga pasipofungika, ameishia kuumia rohoni, wengine
wakimshangaa anacholilia. Mimi nilikuwa hapo, James. Japokuwa yanaweza yasiwe
mahusiano mazuri ya kifahari kama Jelini alipokuwa, lakini niliumia sana
mpaka ulipokuja wewe, na kunipenda kwa ukweli. Nakushukuru
James.” James akainama na kumbusu kidogo tu mdomoni.
“Jema wewe unapendeka
bwana! Mtulivu mno. Mimi ndio natakiwa kukushukuru. Huna makuu mpenzi wangu. Unanivumilia
na ratiba zangu ngumu, mpaka huwa nakuhurumia.” “Sivyo ninavyojisikia mimi.
Mwenzio najiona nipo kivulini. Unanitunza vizuri sana James. Hakuna unachojua
nahitaji usinipe! Tena bila hata kuomba! Unanifikiria mpaka huwa naishiwa
uhitaji! Najua haya ni maisha tu, tutakuja kutulia. Niambie huko umepakutaje?”
“Vizuri aisee. Sikutegemea. Naona sikukuu hizi zimekuja na baraka kwetu. Kila
kitu kipo sawa. Acha nikaoge nije tulale.” Jema akaanza kuomba akimshukuru
Mungu wakati mumewe akioga.
Alipotoka tu,
akamuwahi taulo. James akacheka. “Kweli hizi shukurani nzuri. Leo napata double
dozi!” “Utulie sasa ushukuruwe kwa kumpenda Jema.” Jemas akaanza kucheka mara
akatulia kadiri utamu ulivyokuwa ukikolea. Tamu yake ilikuwa ikinyonywa vizuri
tena ikichuliwa taratibuuu. Jema na tumbo lake akajituma usiku huo mpaka James
akafurahi. Wakalala.
Asubuhi.
Jelini akahisi mtu
akimpapasa taratibu. Akaendelea kutulia akiwa anatoka usingizini, mwishoe
akajua sio ndoto akafungua macho na kukuta Colins akimwangalia. Akacheka kwa
aibu na kuficha uso. Ndio akawa amejificha chini ya kifua chake. Akamsikia
akicheka. “Ulilala vizuri, nikawa nasikia raha kukuangalia. Jelini wewe ni
mzuri hata usingizini!” Jelini akacheka chini ya kifua chake alikojificha.
“Sasa mbona wewe hulali?” Jelini akamuuliza akijaribu kujitoa. Ila alitoka
usingizini akajikuta wamelala wakiangaliana.
“Acha nikujibu kwa
huu wimbo. Nataka uusikilize kwa makini.” Jelini akacheka taratibu. “Nachukua
simu nikuwekee.” “Basi na mimi acha nitumie choo ndio nije kusikiliza majibu
yangu.” Angalau Jelini aliamka asubuhi hiyo akicheka sio kama jana yake.
Akajisahau kuwa amelala na nguo ya kulalia. Akatoka hapo kitandani nguo
inaonyesha ndani akili isimkumbushe. Mwili wa ndani unaonekana kwa wazi kabisa.
Colins akamuona na kukwepesha macho.
Akaenda kutumia choo
na kusafisha kinywa hapohapo bafuni, chumbani. James alijenga hiyo nyumba kila
chumba na choo chake. Akajiweka sawa, ndipo akagundua yupo uchi kabisa.
Akahamaki alipojitizama kwenye kioo. Akavuta taulo na kujifunga sasa. Kuanzia
kwenye matiti mpaka magotini nje ya hilo gauni la kulalia. Ndipo akatoka.
Colins alipomuona amejifunga vile na aibu kidogo, akajua amegundua alikuwa
uchi. Akatoa chandarua na kukifunga vizuri, akakakaa kitandani na kujifunika
tena na shuka.
“Njoo nikwambie kitu
Colins.” Colins akarukia kitanda. “Nimepata wimbo wenyewe.” “Asante kuwa na
mimi kipindi hiki. Nilikuhitaji. Najua unaweza usinielewe, lakini moyo
wangu ulikuwa na maumivu makali sana.” “Nina maswali mawili, lakini nitakuuliza
baadaye. Nataka usikilize kwanza wimbo wangu wa kwa nini sikuwa nimelala
nakuangalia.” Jelini akacheka akisubiria.
“Unaitwa, ‘I don’t
want to miss a thing.’ Mpaka hapo Jelini mpenda Club, akicheza na kuimba
usiku kuchwa na pombe, akawa ameshaujua. Alicheka sana na kujificha. “Bwana
Colins!” “Mimi sitaki kupitwa Jelini. Hata ukiwa umelala nataka niwepo,
nisipitwe na chochote chako.” Akamuwekea nakumfanya Jelini acheke sana huku
akisikiliza. Ulikuwa na maneno mazuri sana. Ile tu mwanzo ulisema,
‘Anataka kuwa macho asilale, ili tu kumsikia anavyohema akiwa
usingizini. Amuangalie hata vile anavyotabasamu akiwa usingizini, mbali huko
ndotoni. Kwamba yeye hana shida maisha yake yote yabakie vilevile akiwa
anamtizama yeye tu alivyokuwa amelala. Kwamba huo muda anao tumia hapo na yeye,
ni muda anao uthamini sana. Akasema, hataki kufunga macho yake, hataki kulala,
kwa sababu atamisi, na yeye hataki kupitwa
na chochote chake.’
Jelini alicheka sana akisikiliza hayo maneno. “Endelea
kusikiliza. Maana kila neno hapo ni jibu lako.” “Mimi nasikiliza Colins.”
Yalikuwa maneno mazuri sana. Jelini akajisikia faraja. Akatoa macho kwenye simu
na kumtizama, akakuta akimwangalia akitabasamu. Hodi ikawatoa kwenye huo
wakati. James na Jema.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Angalau tunafurahi
kumsikia Jelini akicheka. Unajisikiaje Shem?” “Vizuri na samahanini kuwaingiza
kwenye wasiwasi. Nilikuwa natamani tu ule wakati. Kulia ili nitoe uchungu
moyoni.” “Bora kama umepata nafuu. Sasa mpigie simu mama Jema, atulie.” Jema
akaingilia. “Acha nimalizie wimbo ameniwekea Colins.” “Mama anawasiwasi Jelini!”
“Nataka aje Jema. Namtaka mama.” “Anakuja.” Jema akatafuta mahali
akakaa. “Haya weka huo wimbo tuusikilize.” James akamwangalia Colins na
kutingisha kichwa. Colins akacheka na kuweka.
Wakasikiliza mpaka mwisho.
“Kwa hiyo wewe leo hujalala ulikuwa ukimwangalia tu Jelini?” “Swali lako James,
lipo kama husadiki vile!” “Wewe jibu swali.” “Naomba Jelini mwenyewe anijibie.”
Kila mtu alikuwa akicheka. “Eti Jelini?” Colins akataka amtetee. “Mimi
nimemkuta macho akiniangalia, ndio nikamuuliza, akanimbia majibu yangu yote
yapo hapo kwenye huo wimbo.” “Enyi wenye imani haba. Umeamini sasa?” James akatingisha
kichwa kwa masikitiko.
“Sasa mjiandae
twendeni tukapate kifungua kinywa kizuriiii. Au unasemaje mke ya James?” Colins
akaongeza. “Nikipata mtori na sambusa mimi ndio nitafurahi.” “Basi twendeni
Break Point. Acha nikaoge chapu, nakuja.” “Hayo ndio maneno.” Colins, James na
Jema wakatoka. Jelini akabaki amekaa kitandani akijifikiria.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mara mlango ukagongwa
tena, Colins akaingia na kumkuta Jelini amejiinamia magotini kwake. “Naomba
twende Jelini. Utajisikia vizuri.” “Sijisikii. Naomba nyinyi muende tu.” “Mimi
nafanya hii kwa ajili yako. Nataka uweke mawazo kwengine mbali na kuruhusu hayo
mawazo yako kurudi kuchungulia pale pachungu na kuendelea kujiumiza.
Ukijiweka kwenye mengi na wengi, itakusaidia. Usikae umejifungia, ukisononeka
mwenyewe. Tafadhali twende.” “Nashukuru Colins. Basi acha na mimi nijiandae.”
Baada ya muda wote
wakajikuta kwenye gari ya James wakitafuta njia kufikia Break Point kutoka hapo
Salasala.
Njiani Jelini
akampigia mama yake. “Sijakutupa mama yangu.” “Najua
mama. Sema nilikuwa nimekasirika sana. Ndio nikawa nakutaka wewe.” “Pole. Vipi
sasa?” “Kichwa kimetulia kabisa. Najisikia vizuri. Usiwe na wasiwasi. Vipi
Jeremy?” “Yupo sawa, amelala. Tupo njiani. Tumeondoka usiku usiku ili
kukuwahi.” Jelini akanyamaza. “Tutafika mapema tu.
Naona Devi amekazana kweli!” “Naomba mwambie awe mwangalifu. Asiendeshe haraka
sana. Mimi nataka kukuona nyumbani sio hospitalini.” “Yupo makini. Vipi Jema?”
“Njaa inamuuma. Anataka sambusa.” Wakacheka.
“Ungeweza,
ungeenda kumtafutia mwenzio.” “Hapa tupo njiani kwenda kuzisaka.” “Sasa mnunue
nyingi. Zibakie na za baadaye.” “Ngoja nikupe umsalimie.” Jelini akampa dada
yake. “Mjukuu anataka sambusa.” “Wewe sema unataka
sambusa bwana! Mjukuu wangu amezijulia wapi sambusa? Acha kumsingizia.”
Jema alicheka sana. “Mama wewe! Si yeye ndio
amesababisha nipatwe hamu?” Angalau kukawa na kucheka. Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jelini alikuwa
ametulia wakati wapo mezani wakisubira chakula. Kila mtu alimuona alivyokuwa
amepotelea mawazoni. Ikawa ni bora vile kuliko kulia. Viliendelea vicheko,
lakini yeye alikuwa kimya mpaka chakula kilipokuja. Hakuna aliyemlazimisha,
lakini alikula vizuri tu, akatulia mpaka wote wakamaliza kula na kurudi
nyumbani kwa Jema kwa makubaliano ya kuangalia movie pamoja. Hao wawili
walikuwa na mapumziko mpaka tarehe 5, Jema alikuwa akirudi kazini tarehe 3.
Kulikopewa Nafasi Ya Pili.
Usiku uliopita Vai ni
kama alikesha kwa ajili ya kusoma, japo alisoma tena na Bale. Huo mtihani wa Anatomy
ulikuwa saa mbili na nusu. Akiwa anajiandaa ujumbe ukaingia. ‘Usiogope.’ Akashangaa furaha imemjaa moyoni. Akaamua
kumpigia. “Nashukuru kunikumbuka asubuhi hii. Ila
naogopa Bale! Mpaka nahisi sipo tayari.” “Ni kawaida. Lasivyo usingekuwa
mtihani. Ila kumbuka jinsi tulivyojiandaa. Wewe ingia ukijiambia wana maswali
ambayo wewe unayo majibu yake.” Vai akaanza kucheka taratibu.
“Nakuhakikishia
ukiingia na huo mtazamo, utajisikia kutulia kabisa. Utajihisi upo mbele ya
mgonjwa, aliyekuja kwako, anahitaji huduma yako na wewe unawajibika kumsaidia.
Fanya hivyohivyo kwenye mtihani. Itakufanya utulie na kufikiria jinsi yakujibu
maswali yao. Kwa kuwa ulijiandaa, hujazembea, na mimi nimekuombea. Amini
utafanya vizuri.” “Nashukuru Bale. Asante. Angalau sasahivi hofu imepungua.”
“Nataka iishe Vai. Wewe ni nesi mzuri sana. Watu watanufaika na mtu kama wewe.
Usikubali hofu ya mitihani ikafanya ukashindwa kufikia watu wenye uhitaji.”
“Basi sasahivi ndio nimetulia zaidi.” Wakazungumza kidogo wakakata.
Kweli ikawa kama
amezungumza na nafsi ya Vai. Akaingia kwenye mtihani akiwa ametulia haswa. Kila
swali alilolikabili, alitulia, akafikiria na kufanya kwa kadiri ya uwezo wake
mpaka akamaliza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati anatoka ili
arudi bwenini simu yake ikaanza kuita. Akacheka alipoona ni Bale. “Bale.” Akapokea kwa furaha. “Njoo.”
Vai akashangaa na kusimama. “Unataka nije kwako
sasahivi!?” “Mimi nipo hapa. Nakuona.” Vai akaanza kumtafuta akicheka.
Akamuelekeza mpaka akamfikia. “Mbona kama umejificha hapa nyuma!?” “Niliona
unatoka na wenzio kwenye mtihani, sikutaka kukuabisha, kuonekana na mlemavu.”
“Bale!” Vai akaumia sana. Akasikia uchungu kutoka moyoni.
“Vipi mtihanai?” Vai akashindwa kujibu.
Akainama kabisa nakushindwa hata kumuangalia. “Vai?” Akabaki kimya ameinama.
“Najishuku Vai. Haya ni maisha mapya ambayo sijui jinsi ya kuishi nayo. Ila
kama nimekosea, samahani. Nimekuandalia kifungua kinywa. Najua hujalala. Nataka
ukila, ulale ndio tuendelee na mipango yetu. Au umegairi?” “Hapana. Ila
ungenipigia tu simu, nikaja kuliko kuhangaika na daladala kuja mpaka huku
kunifuata! Halafu tena tunahangaika kurudi tena!? Mimi ningekuja tu. Ila
asante.” “Karibu.” Wakatulia kidogo.
“Acha nikatoe hizi
sare za shule, nakuja tuondoke. Na naomba ukae pale Bale wakati ukinisubiri.
Usijifiche. Mimi sikufichi. Kila niliye naye karibu hapa chuoni, anakujua. Na
nikiwa kwako huwa namuaga Belinda. Yule msichana tuliyekuwa naye siku ile
ulipoanguka. Belinda anajua kama tumekua marafiki. Mimi sikufichi, na sitaki ujifiche
ukiwa na mimi. Kwa sababu wewe si mlemavu, ni Bale. Rafiki yangu mimi.” Vai
akaondoka kisha akarudi.
“Usirudie tena
kujificha ukiwa na mimi.” “Nimeelewa Vai.” “Na usirudie tena kujitambua kama wewe ni mlemavu. Wewe ni
Bale. Ni zaidi ya mguu mmoja au miwili. Hiyo ni kauli ya mtu…” Akasita. Kisha
akaendelea tena. “Tafadhali usirudie tena Bale.” “Nimeelewa Vai.” “Hapana.
Nahisi hujaelewa.” “Basi niseme samahani. Sitarudia tena. Umeridhika?” Vai
akaondoka.
Baada ya muda akarudi
Vai ambaye ana nguo za kinyumbani, ila amependeza. Alitoa kofia ya unesi na
sare. Akachana nywele zake vizuri, na kujiongezea hereni, mkufu na cheni ya
mkononi. Alivaa sendozi tu. Vai ni mzuri. Akapendeza. Bale akamuona anakuja,
akasimama pale alipomuelekeza amsubirie.
“Umependeza Vai.” “Umeniumiza
Bale.” “Hata nilivyoomba msamaha havijasaidia!?” “Nimeumia kuona hivyo ndivyo
unavyojiona Bale.” “Nilikwambia nini wakati nakuomba uwe karibu yangu?” Vai
akatulia. “Nilikuomba uwe unanikumbusha Vai. Taratibu na mimi nitajifunza kujipokea.
Nivumilie tafadhali.” “Basi yameisha. Ila nimefurahi umenipikia. Nina njaa na
usingizi.” “Basi utaenda kula kisha nitakupisha chumbani ulale.” “Mimi hata
kwenye makochi nitalala tu.” Vai akashangaa wanaelekea upande yaliopo magari.
“Mbona unataka
tuzunguke na huku ndio kwenye njia fupi mpaka kwenye daladala?” “Nimekuja na usafiri.”
Vai akawa kama hajaelewa. “Twende.” Vai alikuwa na mikoba miwili, akijua jioni
wanatoka kama walivyokuwa wamekubaliana. “Naomba nikupokee. Na ukikataa
utanifanya nijisikie vibaya.” Vai akacheka na kumkabidhi mkoba mmoja. Bale
akatoa gongo na kuweka ule mkoba begani,
kisha akachukua gongo lake ambalo alikuwa ameegemeza tu pembeni yake Vai
akimwangalia.
Belinda akaonekana
anakuja kwa haraka. “Utaanguka bure!” Vai akamuwahi shoga yake “Felix amekuja
muda, nilikuwa sijui. Simu niliifungia kwenye kabati. Nimekuta jumbe kibao na
simu zake.” “Wewe ulikuwa ukipiga mdomo na kina Hawa.” Belinda akacheka kama
mazuri. “Kama vile ulivyonikuta. Habari sina. Bwana mwanaume atakuwa kanuna
huyo!” “Na hapa napo umeweka kituo, unataka uanze mdomo tena, mwenzio
anakusubiri garini.” Belinda akaondoka akicheka, hana mbavu.
Akafika karibu na
gari fulani, akageuka. “Nisamehe Bale, sijakusalimia. Maneno mengi.” “Usijali.
Wewe wahi tu.” “Mzima lakini?” “Namshukuru Mungu.” “Basi wewe tutaongea vizuri
wakati mwingine, kukiwa na amani. Maana leo nishalitibua.” Bale akacheka tu,
akaendelea kwenye hiyo gari na kufungua, kisha akageuka tena. “Vai,
tuwasogeze?” Belinda akauliza. Vai akamtizama Bale. “Nimekwambia nimekuja na usafiri.”
“Sikuwa nimeelewa!” Akamgeukia Belinda. “Asante. Nyinyi endeleeni tu. Wakati
mwingine.” “Sasa jua lote hili mtadema mpaka wapi, na mtafika lini?”
Bale akaumia sana. Vai akasimama kabisa akimshangaa Belinda.
“Samahani Vai,
sikukusudia. Nimeropoka tu shoga yangu. Nisamehe kipenzi. Sikuwa na nia mbaya.
Wewe unanijua.” Bale akacheka tu na kuongoza njia, kweli akidema mpaka
alipoegesha gari lake. Mpaka Vai mwenyewe akashangaa. “Kwamba huu usafiri
ndio amesema amekuja nao!?” Vai akashangaa nafsini mwake. Bale akafungua
kwa rimoti, Vai akasogea karibu. “Twende.” “Kwamba huu ndio usafiri ulilokuja
nao wewe!” Vai akahamaki haswa. “Ndiyo.” “Nani dereva sasa!?” “Mimi. Twende.”
Vai akaanza kucheka, asijue alivyomfariji. Maana alijua angeogopa kuendeshwa na
yeye mwenye mguu mmoja.
Akapanda kwa haraka.
“Bale naye! Sasa si ungesema tokea mwanzo kama umekuja na gari!” Bale akaanza
kucheka. “Nilikwambia Vai.” “Wewe umesema umekuja na usafiri. Sasa na wewe huu
ni usafiri au gari?” Bale akazidi kucheka. “Vai!” “Acha utani Bale bwana! Kuna
utani mwingine sio mzuri.” Vai akawa amechangamka kweli.
“Mama umefurahia
gari! La shemeji yangu ujue?” “Wewe twende tufurahie baraka za leo. Kesho
tutapambana nayo.” “Huogopi kuwa sitaweza kuendesha?” “Sasa ungekuwa umefikaje
hapa, nikianza kuogopa sasahivi kama si kutaka kujinyima raha tu? Na usianze
kuniwekea mashaka. Mimi namuamini dereva wangu.” Bale akapata ujasiri
huyo, hofu yote na yeye ikamuisha. Wakaondoka.
“Mbona hukuniambia
kama mwenzangu siku hizi wewe sio mpanda daladala mwenzangu?” “Vai, hii gari
nimeazimwa mama. Acha kufurahia kupita kiasi.” Vai akazidi kucheka. “Kwamba
kuna siku utapokonywa, tunarudia hali yetu?” “Ndiyo.” “Lakini na sisi tutakuwa
tumefaidi bwana. Na mwenyewe pia si mchayo. Umekuja kunifuata best yako na gari!
Na mimi nioshe mjini.” “Kwani na wewe huna kina Felix?” Bale akamchokoza. “Ungejua
stori ya Felix, ungechoka. Bora nijibakie hivihivi tu.”
“Ni nini tena?” “Ni
walewale tu. Acha mimi nistaafu. Nishike moja. Labda shule itakubali.” “Kwamba
Felix si mchumba mzuri?” “Mume wa mtu na ana watoto wake.” Bale
akashangaa sana. “Na Belinda anajua?” “Anajua na anaye mpenzi wake huko kwao,
wanampango wa kuja kuona kabisa. Huyu Felix anamtunza hapa mjini.
Ninachokwambia ni kwamba, wanachumba kabisa. Ndipo wanapoishi. Felex akiaga
kwake anasafiri kikazi, ujue Belinda yupo likizo, ndio wanakwenda huko. Kumuona
hapa Felix, ujue mkewe anajua yupo kazini. Mpaka jioni. Anarudi kwake, Belinda
chuo au ndio atabaki hukohuko mpaka kesho yake. Ndio siri ya unadhifu wake
Belinda. Pesa yote aliyo nayo ni kutoka kwa Felix. Maana Felix anayo pesa
haswa.” Bale akapoa kabisa akiendelea kuendesha.
“Nashukuru kunijali
Bale.” Vai akavunja ukimya baada ya kuendesha kimya kwa muda. “Hamna kitu
nakufanyia Vai! Mimi sina kitu.” “Acha kusema hivyo bwana Bale! Utafananisha
wakati tunaokuwa nao na pesa?” Bale akatulia. “Kuwa mkweli Bale. Tumefahamiana
siku chache tu, lakini muda tunaokuwa nao tukiwa pamoja, utafananisha na
mafanikio ya pesa?” “Mimi mwenyewe sijawahi pata huo wakati kwa muda mrefu sana.”
“Sasa kwa nini unataka kufananisha na pesa? Mimi mwenzio sijawahi kupikiwa na
mwanaume.” Bale akacheka.
“Kweli Bale. Eti
mwanaume anipikie na aje anifuate nikale! Na hangaika yangu yote maishani na
wanaume, sijawahi Bale.” “Basi Vai.” “Naomba acha kufikiria tusicho nacho,
tufurahie tulivyo navyo.” Bale akajua Mungu amemuamulia kwa aina
ya watu anao mkutanisha naye.
Vai alionekena mtoto
wa mjini, mpenda kujirusha, lakini akamshangaza sana Bale kwa kadiri
alivyoendelea kumfahamu. Bale akatulia kimya. Maana mwanamke wa kwanza kumpenda
na kumthamini hapa duniani ambaye ni mama yake, hakuwahi kumsikia ameridhika na
kitu ila kulilia maendeleo kila wakati. Alitaka zaidi na zaidi. Hata katikati
ya biashara mpya walizokuwa wakijaribisha nyumbani kwao, basi mama yake
hakuwahi kuridhika ila kutaka zaidi na zaidi. Ikamuingia Bale. Naye akawa
kijana wakutaka zaidi. Akipata, anataka tena. Ikajengeka tabia ya kutoangalia
alicho nacho ila ambacho hana. Akatulia kimya hapo garini akiendesha.
Walifika anapoishi
Bale, mpaka akamshangaza Vai. “Sasa wewe utakuwa uliamka saa ngapi na kupika
vyote hivi?” “Nataka ufurahie Vai.” “Kwa kweli nimefurahi. Na nilivyo na njaa, pamoja
na usingizi! Tule nikalale. Ila kesho tunaanza kusoma tena.” “Usijali. Kula
huku unaniambia mambo yalivyo kwenda kwenye mtihani.” “Mimi nahisi nilizidisha
kujiamini.” Bale akaanza kucheka akimwangalia.
“Usinicheke, ni
makosa yako wewe mwenyewe. Yaani nilitulia mpaka mwenyewe nikajishitukia.”
“Jinsi ulivyojiamini?” “Usifanye mchezo.” “Sasa katika kujiamini huko, majibu
ulikumbuka lakini?” Vai akapoa. “Sasa nesi wangu wewe vipi tena!? Mbona
unaniangusha?” “Yale majibu mimi naanza kuyatilia mashaka bwana. Mbona kama
nilikuwa nikiandika sana!” Bale akazidi kucheka hana mbavu.
~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment