Akamsogelea. “Ulilala
vizuri?” Akakubali kwa kutingisha kichwa. “Vipi kichwa?” “Kinauma, Colins.”
Akajibu taratibu. Akamshika kichwani akimpapasa. “Pole sana.” “Nikuulize kitu?”
“Niwashe taa ili tuzungumze vizuri?” Akakubali. Akawasha taa na kwenda kukaa
pembeni ya kitanda.
“Unataka kuniuliza
nini?” “Kwa nini upo hapa na mimi?” “Kwa sababu nataka kuwa hapa na wewe.”
Jelini akamwangalia, akiwa amekunja uso kama ambaye hajaelewa, na kutulia na
yeye Colins akabaki akimwangalia, Jelini akakwepesha macho.
“Uliniambia sikukeri,
Jelini. Au imebadilika, nimekuwa kero?” “Hapana. Wewe sio kero kwangu.
Nilitaka tu kujua.” “Kwa hiyo sasahivi umeshajua?” Colins akamuuliza kwa
kumbembeleza. “Nafikiri. Labda! Hata sijui! Nipo kwenye wakati mgumu Colins!
Sijui chakufikiria. Natamani nitumie njia yangu ya zamani kujituliza, ila naona
nitapotea tena.” “Pombe haitakusaidia Jelini.” Akaongea moja kwa moja kama mtu
anayemfahamu vizuri sana mpaka Jelini mwenyewe akashituka na kuishiwa nguvu. Hakutegemea,
akamwangalia.
“Mabadiliko
uliyoyafanya kwenye maisha yako, kwanza nakupongeza. Pili, usirudi tena nyuma.
Ukiwa na akili hiyohiyo, sasahivi, na changamoto unayopitia, anza kujifikiria
na kuendelea kuanzia hapa. Ukianza na changamoto hii kwa tabia ile ya nyuma,
utaharibu msingi mzima ulioanza kujenga na kuaharibikiwa zaidi kabisa.” “Itakuaje kama msingi wenyewe nilianza na mtu? Nakuwa
kama nakosa dira Colins. Inakuwa kama mtu amekutoa sehemu moja, anakufikisha
sehemu nyingine, halafu anakuacha! Naogopa, nahisi kama kuporomoka.” “Hizo
ni hisia zilizoumizwa ndio zinakuogopesha. Umeshawahi kusikia
usemi kuwa unaweza kumpeleka punda kisimani na asinywe maji?” Anamuuliza huku
akimfuta machozi. Jelini akakubali.
“Basi jua unaweza
kupelekwa hiyo ‘sehemu moja’, na kama hujaamua kukaa hapo, hata kama ni Mungu
mwenyewe ndiye aliyekupeleka, utaondoka tu. Kwa sababu hujaamua. Wewe
umeshafikishwa sehemu, lakini ni wewe Jelini ndio ulikubali kufika, na
sasahivi unalo jukumu la kubaki hapo ulipo na kwenda mbele zaidi. Au ukarudia
maisha yale ya kushinda baa, na kulala klabu. Au kushinda baa ukinywa, na kulewa masaa yote.
Wewe Jelini ndio unao huo uwamuzi na si mtu mwingine yeyote.” Jelini
akamshangaa Colins anavyozungumza habari zake kama anayemfahamu sana!
Akajisikia aibu, na kunyamaza.
“Umenielewa?” “Lakini nilibadilika Colins. Niliacha hayo maisha ya
kushinda baa, na ulevi.” Jelini akajitetea. “Naomba ujisikilize mwenyewe.
Umesema uliacha, na umebadilika. Wewe kama wewe, wala si
mtu mwingine. Sasa usirudi nyuma. Usikubali mwanadamu uliyekutana naye kwa muda
mfupi, akakuchanganya kiasi cha kuharibu maisha yako. Sikatai yapo maumivu.
Lakini ukiwa na akili safi, itakusaidia
kufikiria jinsi ya kuendelea kuanzia hapo. Pole. Lakini hayo maumivu yabebe
ukiwa na akili zako timamu. Na usiyazike kwa kulewa, maana hayatakaa yakaisha.
Kila pombe itakapokuwa ikiisha, akili itakutuma kwenda kuchungulia kule ulikoficha,
kisha kuendelea kunywa zaidi na zaidi. Na ndio maana wanaolewa kwenye matatizo
huwa hawaachi pombe mpaka watatue hilo tatizo. Na nikujichelewesha.
Usikubali kuchelewa hapo. Jambo limeshatokea, kubali matokeo na jua
jinsi yakuendelea kuanzia hapo.” Jelini alishindwa hata kumtizama, akabaki
kimya.
“Nikuletee chakula
ule?” Jelini akakataa. “Kula kidogo.” “Nimejawa
hofu, majuto, uchungu kiasi ya kwamba yote hayo yamejaza tumbo langu. Sina
nafasi ya chakula. Acha tu nilale tu.” “Basi acha nilete movie tuangalie
wote ili upumzishe mawazo. Ni sawa?” Akakubali. Alipotoka tu Jema akaingia.
Jema Kwa Mdogo Wake.
“Vipi mtoto wa mama
Jema?” “Njoo ukae hapa.” Jema akaenda kukaa na tumbo lake. “Hapa nimeshiba
chakula cha mama Colins, nahemea juujuu.” Jelini akamwangalia na kunyamaza.
“Pole Jelini mdogo
wangu. Japokuwa sijui ni nini kimekuumiza, lakini naomba fikiria afya yako.
Kichwa hicho, bado. Utajiumiza bure.” “Nimeanza kukuonea wivu,
Jema! Nakutamania! Maisha yako yana uhakika sasahivi.” Jema akamwangalia na
kucheka kama anayetafakari hilo. “Tutakuja kuzungumza zaidi. Lakini si unajua
chochote nilichonacho na wewe Mungu anaweza kukupa? Ni kutaka kwako tu na kuwa
tayari.” Jelini akaanza kulia.
“Mungu hana
upendeleo mdogo wangu. Ni wewe tu kuwa tayari kulipa garama kwa unachokitaka.
Huwezi kutaka mtoto wa kumzaa, halafu eti hutaki kubeba mimba! Sijui kama
unanielewa? Kila baraka inakuwa na wajibu wake. Ndio maana wengine wanaona shida
kuwajibika, wanatafuta njia fupi. Sasa labda wewe uniambie unataka
upande gani?”
“Una mwanaume
anayekupenda Jema! Anakutetemekea, utafikiri nini sijui! Mimi na mama
tunakusema hatumalizi. Mumeo anakuthamini kupita kiasi! Japokuwa mimi nimefanya
mengi mpaka yale niliyokufundisha na wewe, lakini sijabahatika kupata
mwanaume hata nusu yako Jema!” “Sema hujabahatika bado. Wewe bado mdogo sana,
halafu sasahivi ndio kama unakua Jelini. Ulicheza sana hapo katikati. Kwa hivi
ulivyo sasahivi, halafu ukajua unachokitaka, na kujipa muda,
utapata sana tu. Jipe muda na jiwekee malengo bila kukata tamaa na
kuyumbishwa. Utafika tu.”
“Unakumbuka mimi
nilivyotendwa na Temu?” Jelini akatingisha kichwa kukubali. “Niliingia aibu ya
mwaka, maana mwanaume alijua kunichafua yule! Ni vile nilishindwa
kumwambia mama, nilijua nitamuumiza tu. Nilishindwa hata kwenda kanisani.
Nilikuwa siwezi kula wala kulala. Aibu na fedhea.” “Ulitokaje hapo?” Jelini akauliza.
“Mungu alinisaidia
Jelini. Japokuwa nilikuwa nimeumia, lakini sikuacha kuomba. Na sikukata
tamaa ya kuja kupata mtu wangu. Mwenzio nilikuwa nikijitunza nikijua kabisa,
nitakuwa mke wa mtu fulani. Niliishi kama namtunzia mtu kitu chake.
Sikutaka kujiachia kwa yeyote, wala kwa sababu yeyote ile. Hata walipokuwa
wakinitongoza, wenye pesa na wazuri, kama hapakuwa na ndoa, nilijitenga
bila yakufikiria mara mbili.” Jelini akaumia sana.
“Mimi nitakwambia
ukweli Jelini. Haya maisha ya mama zetu, mimi mwenzio siyapendi.
Niliionya nafsi yangu, ndio maana nilijikana kabisa. Nilimwambia Mungu
anisaidie, nivunje hii tabia za mama zetu, hata watoto na watoto wetu
waje wajue zipo ndoa. Sikutaka watoto wasio julikana baba zao kama sisi.
Binafsi sikutaka kabisa. Na ndio maana sikujichanganya hata katikati ya
majaribu, nilijikumbusha nini nataka. Nikamlilia Mungu mpaka akanipa James
wangu. Mume wangu hana makuu, au mamilioni ya pesa, ila ana upendo wa kweli,
ndicho nilichokuwa nikikitaka. Basi. Kwa hiyo hata wewe hujachelewa. Jiwekee
malengo. Omba Mungu, atakusaidia tu.” Jelini akabaki akilia kwa uchungu.
“Pole sana Jelini,
mdogo wangu. Kama anavyosema Colins, ‘it gets better’. Hapo ulipo,
mwenzio nilipita. Ila sikuwa na mtu, ila peke yangu. Aibu, kusema huwezi, maana
mama alishanionya juu ya Temu, nikashupaza shingo! Halafu kama unavyonijua mimi,
sina msiri wa kumwambia mambo yangu ila Mungu. Hakika niliteseka. Ila
wewe upo na sisi. Tutumie sisi tuliokuwepo karibu yako kujipatia faraja. Halafu
uzuri ni kuwa, na mimi nimepita hapo. Mama Jema yupo na wewe. Usiumie peke
yako. Umesikia?” Akatingisha kichwa kukubali.
“Unataka kula
kidogo?” “Siwezi. Tumbo limejaa gesi. Nahisi na
mshituko pia.” “Nikutengenezee chai hata ya rangi?” Akatingisha kichwa
kukataa. “Toka basi hapo kitandani angalau uangalie tv upoteze mawazo.” “Colins amesema analeta movie tuangalie.” Jelini
akajibu akijaribu kutulia akifuta machozi. “Hiki chumba hakina tv. Labda
akalete ya kule chumbani kwake. Colins?” Akaanza kumuita.
Akafika hapo na
kibegi chake kama aliyekuwa akisubiria aitwe. “Labda uhamishe ile tv ya
chumbani kwako huku.” “Tutatumia laptop yangu. Asante.” “Basi mimi naenda kuoga
nijilaze kitandani wakati nikimsubiria James. Mkitaka kitu, mje kunigongea.”
Jema akawaacha hapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ikawa kama kijihofu
na aibu kimemuingia Jelini! Colins anamfahamu kuliko anavyodhania. Akakumbuka
na maneno ya dada yake juu ya wanaume. Akajihisi vibaya na kujiona mjinga kama
alivyosema Koku. Kwamba anajiliza kwa mwanaume asiye mume wake. “Lakini nilimzoea Zenda!” Jelini akajisemea
nafsini kwake na kuona machozi yakimtoka. Akakumbuka nyakati nzuri alizokuwa
nazo akiwa naye. Vicheko na utulivu. Halafu Zenda alijua kutumia mwili wa
Jelini vilivyo!
“Ndivyo
anavyofanyia wanawake zake wote!” Akaumia sana kuona amepitisha midomo
yake kwenye mashine inayoingia kwa wanawake wengine na yeye akipitiwa! Akajichukia
na kuona kinyaa cha hali ya juu.
Akakumbuka vile
alivyomsikia Zenda akipiga bao akiwa na Koku, hasira na wivu vikamzidia. Akainamia
mto nakuanza kulia akishindwa kujizuia. Akalia akiwa amefunga mdomo na sauti
isisikike, akisikia maumivu makali moyoni. Hakuwa na wakumlaumu hata Zenda
mwenyewe. Koku ni mwanamke wake. “Lakini
aliniambia atamuacha kwa ajili yangu!” Akazidi kunung’unika rohoni.
Akakumbuka alivyokuwa
akikataa watu, akijiambia anasubiri wake wa peke yake, kisha kuangukia
kwa mwanaume aliyemuaminisha hatamsaliti, na kuja kumfumania akipiga bao
kabisa! Jelini alilia sana. Colins akaweka vitu pembeni na kumsogelea pale
alipokita uso wake kwenye mto. Akaanza kupitisha mkono mgongoni taratibu
akitumia kucha. Akamfanyia hivyo kwa muda mpaka akamsikia ametulia. Akatoka
kitandani.
“Unakwenda wapi?” “Nataka kuoga, ndipo nilale.” “Basi acha
nikupishe, nitarudi baadaye.” Colins akatoka. Jelini akapiga magoti pembeni ya
kitanda na kuanza kulia tena kwa uchungu, sauti ya chini, tena kwa uhuru.
Alilia bila ya kunyamaza mpaka kichwa kikaanza kugonga kama kinapasuka. Hapo
akakaa kitandani na kuanza kujituliza na kushindwa.
Ikawa kama bahati,
Jema naye akawa amepigiwa simu na mama yake, anataka kuzungumza naye. Anaingia
na kukutana na Jelini anayelia sana. “Sidhani kama
ataweza kuzungumza mama. Acha atulie tu.” “Nilikwambia mpe dawa ya usingizi
Jema! Atajiumiza huyo, mimi ndio nipate hasara.” “Acha kulalamika mama, bwana!
Alikuwa amelala. Nampa dawa sasahivi atalala tu.” “Najua umechoka Jema
mwanangu, lakini usimsahau huyo. Tafadhali mama yangu. Nakuja mwenyewe kesho.”
“Mama,
unanilaumu bure! Lakini sijamsahau. Naomba utulie, Jelini atakuwa sawa.
Anahitaji tu muda. Hata kama wewe mwenyewe ungekuwepo hapa sasahivi, ingekuwa
hivihivi. Mimi nazungumzia uzoefu. Nimekua hapo alipo Jelini. Anahitaji huu
muda kupokea ukweli. Akisha kubaliana na ukweli, ndipo atatulia.
Hakuna utakachofanya sasahivi akawa sawa, isipokuwa muda ndio utasaidia.
Tulia ili na yeye ataulie.” Kimya. “Nampa dawa, atalala tu.”
“Nashukuru.” Mama Jema akakata simu akisikika kutoridhika kabisa.
“Nataka
nikaoge Jema, ndipo ninywe dawa, nilale.” “Basi vua nguo twende bafuni.”
Akamsaidia mdogo wake mpaka akaoga, na kurudi naye kitandani. Alimpa nguo yake
ya kulalia. Akamfunika shuka vizuri ndipo akamruhusu Colins kuingia. Jema
akatoka, Colins akaingia mpaka ndani ya chandarua na yeye akionekana alishaoga
vizuri tu maana alivaa pajama nzuri za kiume.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kitakachoendelea Katikati Ya Kilio Cha Jelini Usiku Huo Mikononi Kwa
Colins!?
0 Comments:
Post a Comment