~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda
akagonga mama yake. “Jema mama, naomba ukanifungulie mlango wa gari dada
amuwekee mataulo. Akioga na kutumia taulo mara moja, hawezi kurudia tena.” “Ila
na mimi ninayo mataulo mengi tu yakutosha mama yangu.” “Wewe wala usijali. Acha
nikuwekee tu na haya. Akiyatumia, anajua jinsi ya kuyaweka vizuri mpaka yaje
kufuliwa hapa na mashine. Nisikupe kazi zaidi. Na jioni dereva akimletea gari
yake, nitampa na chakula awaletee wote mle. Ili upumzike na safari, usihangaike
kupika.” Jema akacheka.
“Mbona huu ugeni
mzuri! Na chakula!” Wakacheka. “Ila usingehangaika mama yangu. Tungekuwa tu
sawa.” “Sitaki huu ugeni uwasumbue. Mimi namjua Colins.” Wakacheka tena.
“Ila atatusaidia kutupa taarifa kujua Jelini anaendeleaje. Mkitaka ushauri wa
kidaktari Connie au mimi nitawashauri.” Mama Colins akaongea akicheka
akionekana alisikia mazungumzo yake na James. “Yupo hivyo kama baba yake. Mumvumilie.
Najua James ameshamzoea. Ila Jema, itabidi umvumilie tu.” “Wala usijali mama
yangu.” Connie naye akaingia.
“Jelini, chukua namba
yangu. Ili muda na wakati wowote ukijisikia sivyo, unipigie, nikushauri.” “Kwani
wewe Connie ni daktari pia?” Jema akamuuliza. “Ila ndio nipo intern.
Namalizia.” “Hongera Connie.” “Asante. Nafuata nyayo za dad.” “Kwamba unataka
kuja kuwa surgueny pia!? Sio muda mrefu sana!?” Akacheka vile Jema
alivyouliza kwa kushangaa. “Napenda mwenzio, anti. Naona wala sio muda mrefu.
Nafurahia kila hatua.” Akamgeukia Jelini. “Utakuwa sawa Jelini. Sisi wote tupo
kwa ajili yako. Na ukisikia upweke tu. Muda na wakati wowote, nipigie mimi hata
mama. Ila mama ndio zaidi. Mzuri sana kwenye kusikiliza. Usiumie peke yako.
Umesikia?” Jelini akajifuta machozi na kutingisha kichwa kukubali. Jema
akashangaa anamkumbatia na kumbusu. “Kila kitu kitakua sawa.” Akambembeleza
taratibu.
“James.” Wakasikia
sauti ya Colins. “Bado gari imefungwa, tunashindwa kuweka mizigo!” James
akatingisha kichwa nakutoka. Wakacheka. “Nitampigia simu na mama Jema kumwambia
juu ya Colins.” “Wala usiwe na wasiwasi mama. Huyo Colins pale kwetu
tumeshamzoea ila kulala tu.” Wakacheka tena. “Acha nimuandae tu. Maana kesho
habari inaweza kuja kuwa kama hii hii ya leo huko kwa mama Jema.” Baada ya hapo
wakatoka hapo kuelekea nyumbani kwa Jema na James.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Abiria wao, Jelini na
Colins wamekaa nyuma. “Niambie nini kinauma sasa hivi.” Wakamsikia Colins
akimuuliza kwa sauti yake nzuri, tulivu ila kwa chini. Jelini akajifuta machozi
na kujishika moyo, kumuashiria maumivu yanatoka moyoni. Mbele hawakuona. “Pole
Jelini. Lakini nakuhakikishia, it gets better. Sasahivi kwa kuwa
umeumia, unaweza usiniamini. Lakini it gets better. Promise.”
Jelini akatingisha kichwa kukubali kisha akajiegemeza kitini akiangalia nje.
James akaendelea kuendesha kurudi kwao. Hapohapo Jema akapitiwa na usingizi.
Kimya.
Uzuri kilikuwa
kipindi cha sikukuu, hapakuwa na foleni sana, haikuchukua muda mrefu, kutoka
nyumbani kwa kina Colins, Mbezi Tangi bovu mpaka kwa James Salasala. “Twende
ukalale ndani, Jema. Chakula kikiwa tayari nitakuamsha.” James akamwamsha mkewe
kwa upendo. “Twende. Na usibebe kitu. Mimi nitakubebea mpaka pochi.” “Asante.
Mgongo unauma! Naona sababu ya safari.” “Pole. Basi nenda kajilaze. Nakuja.”
“Nisaidie kubeba nini?” Colins akauliza. “Wewe mwenyewe una mizigo yako humu!” James
akamjibu, Colins akaanza kucheka. James akamwangalia na kuanza kuingiza
masanduku yao maana na wao ndio walikuwa wametoka safari hata kwao hawakuwa
wamefika. “Twende ukapumzike Jelini.” Akatoka garini na kumfuata dada yake
nyuma mpaka kwenye chumba ambacho angelala.
Mara Colins akaingia
bila hodi. “Wewe nipe mashuka, mimi nitatandika.” “Kumbe bora umekuja maana
nina usingizi, nataka nikajilaze. Nakutolea kila kitu na mashuka ya chumbani
kwako, kisha naenda kulala.” Jema alichofanya ni kutoa mashuka na mataulo,
akaenda kujilaza na kuwaacha hapo. Jelini amekaa kiti cha hapo chumbani
amejiinamia.
Colins&Jelini.
Akamtandikia vizuri
na kumwangalia. Bado Jelini alikuwa amejiinamia hapo kitini. Akaenda
kuchuchumaa mbele yake na kumshika magoti akimchungulia pale alipoinama.
“Niambie unataka nini Jelini.” Jelini akamwangalia na kupandisha mabega
kukataa. Mawazo yalikuwa mbali. Akitafakari maneno ya Koku, yalimtesa sana
Jelini. Akaanza kujidharau na kujiona mjinga. Aibu, akijiuliza alikuwa
akifikiria nini kitaendelea kati yake na Zenda! Akashindwa kupata jibu. “Ila
sikutegemea mwisho wa namna hii! Zenda!” Akashindwa kukubali, ila sauti ya
Zenda akipiga bao chumbani kwake ikamuhakikishia, si mawazo.
“Nakukera, unataka
niondoke?” Colins akauliza lakini akiomba Mungu asifukuzwe. Jelini akatingisha
kichwa kukataa. Colins akafurahi sana. “Nifanye nini ili utulie?” Akatingisha
kichwa kukataa. Kwamba hakuna chakufanya. Vile Colins alivyo mzuri na sauti
yake, vilikuwa vikimtuliza Jelini nakushindwa kujielewa. Japokuwa alikuwa na
uchungu wakusalitiwa, lakini alishindwa kumfukuza Colins. Kule kumbembeleza,
kulimpa hisia ambazo hakuwa akijielewa. Zenda alikuwa mawazoni. Sasa hichi
kinachompata kwa Colins ni nini tena! Hakujua kwa wakati huo. Ila hakutaka
aondoke.
“Basi njoo
nikubembeleze ulale.” Akili zilikuwa zikikataa kabisa, na japokuwa hakuwa akijua
anabembelezwaje, lakini moyo ulikubali. Akabaki ameinama vilevile. Akasimama
pale alipokuwa amechuchumaa, akamshika mkono, na kumvuta taratibu ishara ya
asimame. Akajishauri, lakini akasimama, akamuongoza kitandani. Jelini akapanda
na kujilaza ubavu akiangalia ukutani. “Kichwa bado kinauma?” Akamuuliza kwa
kumbembeleza. Hiyo sauti ya Colins yenyewe tu, inatuliza.
“Naomba zungumza na
mimi Jelini. Tafadhali.” “Sisikii kuzungumza Colins. Nataka kunyamaza tu peke
yangu.” “Basi nakubembeleza kimya kimya. Ila naomba usilie, ulale.” Akatingisha
kichwa kukubali.
“Nigeukie Jelini.
Usinipe mgongo.” Jelini alishangazwa moyoni, nakushindwa kuelewa. “Hivi
sijasema kama nataka kulala?!” Akawaza mawazoni. “Nakukera?” Akauliza kwa
upendo kama mtoto mkiwa. Jelini akamuhurumia vile anavyojitoa kwake, akajirudi.
“Hapana Colins. Ila nimejawa fedheha!”
Akamjibu na kumgeukia. Akamfuta machozi. “Kwa nini?” “Sijui
Colins! Ila nimejidharau sana, nakujiona mimi mjinga! Nimekua ndege mjanja.
Lakini nimebanwa kijinga sana. Ndio maana nina maumivu. Nisamehe kama nakua
mbaya kwako. Lakini hunikeri. Nakushukuru kwa ukarimu wako, hata kuwa hapa na
mimi.” Akamvuta mkono na kuubusu kwa muda mrefu akiwa amefunga macho
kama anayesikilizia hisia fulani, nzuri hivi, asijue na Jelini naye anapata
faraja.
Kisha akafungua macho
na kumuangalia. Akakuta Jelini akitoa machozi. Akamfuta. “Asante Colins. Ila sitaki ubakie hapa na mimi. Sitaki
tukwame wote. Mimi nitakuwa sawa. Nahitaji tu muda kujiweka sawa mawazoni. Wewe
rudi nyumbani uendelee na mambo yako.” “Mimi nataka kuwa hapa na wewe
Jelini. Tafadhali usinifukuze. Niache tubaki wote. Nakuomba.” “Sitaki tukwame wote.” “Kuna usemi unasema, wawili
ni bora kuliko mmoja. Maana mmoja akianguka, mwenzie anamuokota. Naomba nafasi
ya kuwepo tu.” Sauti ya kubembelezana hapo, ungejua tu hakuna
anayefukuzwa.
“Na nikwambie ukweli
Jelini?” Jelini akamwangalia akijitahidi kufuta machozi. “Sijisikii kukwama
hapa. Nikijiuliza sehemu sahihi ya mimi kuwepo muda huu, najikuta najiambia ni
hapa tu, ulipo wewe. Mimi nataka kukaa hapa ulipo.” Jelini akatingisha
kichwa kukubali. Akamlaza mkono juu ya mapaja yake akaanza kumpapasa taratibu
huku mkono mwingine ukimpapa kichwa na kuweka nywele sawa. Kisha kuchezea
vinyweleo. Jelini alikuwa akisisimkwa mpaka akajishangaa. Faraja aliyokuwa
akijisikia! Halafu ni Colins! Hakuna mchana wala usiku ukamwangalia akawa
havutii! Roho ya Jelini ikaanza kutulia na kupitiwa usingizi hapohapo.
Kule Kuliko Ungua Mpini.
Mzee akiwa bado anawakwa
moyoni akaweka mipango kuhakikisha na Koku anafungiwa alipo Kemi ili ajue
ukweli. Hapo pesa yake ilikuwa ikitembea kwa hasira asijue amwadhibu nani na
kwa umbali gani. Kila dakika iliyokuwa ikizidi kupotea bila Jelini, ndivyo
chuki ilivyozidi kumpanda. Akataka kuwakomoa vilivyo, ili wapate maumivu aliyo
nayo moyoni.
Koku anaingia
alipokuwa amefungwa Kemi, Kemi akashituka sana. “Kama wewe siye uliyetuchoma
kwa baba, yeye amejuaje!?” “Yaani wewe ulifikiri mimi ndiye niliyewageuka!?”
Koku naye akauliza kwa kushangazwa sana. “Kabisa. Nilijua ulikolezwa, ukaishia
kuropoka kama mjinga.” “Jiangalie Kemi! Baba yako hana uwezo huo.” “Uwezo upi? Wakukulala
au kukuhonga mpaka kufikisha hapo ulipo?” Wote wakiwa na hasira wakaanza
kutukanana, sasa Koku ikawa zaidi. Anamtukana Kemi na baba yake.
Ugomvi. “Kama kweli
hana uwezo huo mbona hatujakuona ukiolewa na kijana akakukaza kweli, umebaki ukimng’ang’ania
tu yeye?” “Kama utakumbuka vizuri ni wewe mwenyewe ndiye uliyenitafuta, na
kutaka niwasaidie kumtoa Jelini kwenye maisha ya baba yenu. Wala mimi sikuwa na
mpango naye tena, mtu mzima hovyo, anaye tetemesha na kijitoto kisichojua
chochote! Siwezi kuwa na mwanaume dhaifu, mjinga kiasi hichi. Kasa niliyemjua
mimi enzi hizo alikuwa mwanaume kweli, ukiwa naye unajisikia upo na mtu! Sio wa
sasahivi, upuuzi mtupu”
“Kama mpuuzi, mbona
yamekushinda umeishia hapa?” “Kwanza kwa taarifa yako nipo hapa kwa sababu
nimefanya kazi yangu vizuri. Wewe ndiye uliyeshindwa kufanya upande wako mpaka tumekamatwa.”
“Sijashindwa chochote. Mambo yalikuwa sawa, ndio maana nashindwa kuelewa baba ameshitushwa
na nini mpaka kujua yote haya!? Ni nini kilichomfanya ajue kama na wewe
ulifanya kwako kama tulivyokwambia?” “Acha maswali ya kijinga kama vile humfahamu
baba yako. Swala la Kasa kufikiria ndio unalijua leo baada ya kuishia lupango? Wewe
ndio mjinga kama kale katoto. Na sitakuficha kama nilivyomwambia Kasa na
Jelini. Wote nyinyi ni wajinga. Hamuwezi kufikiria. Kale katoto kanajiliza
mbele ya Kasa akijidai kamemfumania Kasa, yeye kama nani? Alitegemea ataolewa
na Kasa, malaya anayeng’ang’ania wanaume tu! Eti na Kasa naye anatetemeshwa! Kwa
lipi mno!? Malaya wa Tegeta yule!” Jazba likampanda zaidi akaanza kuropoka
hapo, wasijue wanarikodiwa na askari magereza aliyekuwa zamu.
“Usiniambie na hayo
uliropoka pale mbele baba, sababu ya wivu wako!?” “Wivu wa nini mimi? Kama
ningekuwa namtaka zee lile si ningekuwa naye? Sina shida na babu. Na
yeye analijua hilo ndio maana alivyompata Jelini, ameng’ang’ania akijua
ameshaisha soko. Nguvu yenyewe yakumuweka mwanamke kitandani hana. Anahangaika
kitandani kama mpumbavu wa mwisho! Yule mtoto anamlia tu pesa yake, anamtapeli.
Mzee amechanganyikiwa mpaka amempa sehemu ya kuweka nguo! Yaani Kasa anampa
sehemu ya closet yake mtoto mchafu kama yule wakati mimi hataki hata niache mswaki
wangu pale!” Hapo akaonyesha chuki yake kwa waziwazi. Akaropokwa zaidi, mtaka
hataki. Anajikoroga na kujichanganya.
“Nilikuwa nakusubiri
nijue ulipojichanganya ni wapi. Yaani hasira yote hiyo, mpaka kuropoka kwa
baba, na kusababisha wote tuingie matatizoni, ni kwa sababu uliona nguo za
Jelini kwenye closet ya dad!?” “Sina shida.” “Shida unayo, maana ndicho
kilichokufanya uropoke na wote kuishia hapa. Wewe mbinafsi na mjinga
wa mwisho. Jumba lote ulilonalo lile bado unalalamikia sehemu ndogo aliyopewa
Jelini kuweka nguo zake?!”
“Acha kelele na fikiria
Kemi kama mtu mzima. Swala si sehemu ya kuwekea nguo. Kufanya hivyo kwa Kasa,
ni zaidi ya hivyo na wewe unajua. Na kwa taarifa yako si sehemu tu. Ni
kama nusu ya chumba cha kuwekea nguo za Kasa, amempa Jelini wakati mimi
nikiacha tu hata mswaki ananiambia nisipochukua, anatupa! Hataki kitu
cha mtu yeyote yule, kibakie kwenye nyumba yake, kichukue sura ya mtu
mwingine mle ndani kwake, isipokuwa yake yeye mwenyewe Kasa. Leo, Kasa
anayethamini mavazi, na wote tunamjua, anayo mpaka sehemu maalumu yakuwekea saa
zake za mkononi, eti ajibane, halafu ampe Jelini sehemu ya kile chumba
kinacholindwa na kamera! Kweli Kemi?”
“Halafu badala
unishukuru nimemtoa yule mtoto kwenye maisha yake, unanitukana! Unafikiri bila
hivyo wote nyinyi na mama yenu mngeishia wapi kama sipakavu? Maana
mwisho wa Kasa ungekuwa ni kumpa mali zote yule mtoto na nyinyi kuambulia
patupu?”
“Sasa, sasahivi hapa
hizo mali zinatusaidia nini, tukiwa wote tumekwama hapa na shutuma za kutaka mumuua?
Kwa ujinga wako, bila kutumia akili, kuwazidi mahesabu, kufanya mambo kama tulivyopanga,
umeharibu, wote tupo ndani kwa kosa la kukusudia kuua. Tunatoka lini
na kunufaika na hizo mali, kama si ujinga huo unaozungumza ukijitetea kama mtoto
mdogo? Tukushukuru kutufikisha hapa, wewe kubwa jinga uliyezidiwa
wivu kwa mwanaume uliyejua fika hakutaki!”
“Nishakwambia sina
shida na baba yenu, acha kuniita mimi mjinga. Nilisha…” “Wewe ni mjinga tu Koku
hata ukikataa. Ulijua fika hutakaa ukawa kwenye maisha yake, hakutaki kwa
maisha marefu. Ni kukutumia tu, sasa kwa nini kupatwa wivu na jazba kwa
Jelini tuliyekwisha kuweka mipango ya kumtoa ili asifike mbali?” “Kwa taarifa
yako alishafika mbali. Shukuru mimi niliyefanikiwa kumtoa. Na usifikiri Kasa
alikuwa akinitumia peke yake, hata na mimi nilikuwa nikimtumia. Mimi si
mjinga.” “Huna lolote mpuuzi tu wewe. Unapoteza malengo katikati mipango mizuri
tuliyoweka sababu ya kukutana na mtoto aliyekuzidi mahesabu! Na sisi
tulikwambia kabisa na tukakuonya! Kama si ujinga huo ni nini? Hata kukataa hapo
ni ujinga zaidi.” Hapo akazidi kumuudhi Koku.
“Wewe ndiye mjinga wa
mwisho Kemi, usiyeweza kufikiria na kutafuta mtu wa kumlaumu badala yakujilaumu
mwenyewe. Wewe kwa akili zako hukujua madhara ya kumgeuka Kasa?” “Kama sio wivu wako wa kijinga, mipango yetu yenye
akili ilikuwa ikienda vizuri tu, mpaka wewe ulipoingiza mapenzi kazini.” “Mimi
sitaki ujinga. Kasa hawezi kunichezea.” “Sio hutaki ujinga, ni hutaki
kushindwa. Umeona umeshindwa na mtoto mdogo ambaye hana hata shule kichwani,
lakini baba amesalimu amri kwake, amempa anachokataa kukupa wewe,
ndio wivu huo.”
“Nani amekwambia mimi
nina shida na Kasa? Kashanitimizia yangu, nimeridhika, nikatulia kwangu. Nyinyi
na mama yenu ndio hamtosheki naona mpaka mpate roho ya Kasa ndio
mtatulia. Kutwa mpo mfukoni kwake mkichota pesa yake bila kuchoka,
huku mkilinda isije kwenda kwa mwingine isipokuwa nyinyi watatu tu. Tena
mpaka na mumeo chupi anategemea kwa Kasa. Ndio maana wote mmeishia hapa, wala sio
mimi. Mchawi wako kamtafute kwenye kioo, na mama yenu asiyetosheka na
pesa ya mwanaume aliyesema hamtaki, akaolewa uzunguni akidhani ni
bora, ila chakushangaza kutwa macho yake yapo kwenye mifuko ya Kasa.” Hapo
akakanyaga pabaya zaidi. Kemi akamrukia wakaanza kupigana, wafungwa wengine
wakiwaangalia nakushangilia, mwishoe wakaja kuamuliwa na askari magereza, na
kutenganishwa wakiwa wameshachukuliwa ukiri wao wote.
Kuliko Baki Shoka.
Yakiwa yanawarudia wenyewe,
yeye Jelini alilala akibembelezwa, akalala asijue alipo mpaka jioni kabisa,
akashituka na kujikuta peke yake kitandani. Akatulia tu akijitafakari na
kurudia maneno ya Koku. Ukweli juu ya utofauti wake na Zenda, ukaanza
kuingia akilini. Akavuta pumzi kwa nguvu na kujituliza hapo kitandani.
Akatamani kulia, akakumbuka tena Koku akimuuliza anacholilia. Akajisuta
ila kuumia rohoni. “Hata kama asingenioa, lakini nilikuwa nikifurahia
kampani yake! Tulikuwa tunakuwa na wakati mzuri!” Jelini
akazidi kuumia asijue alitegwa na kutegeka vizuri sana. Japokuwa waliishia lupango,
lakini lengo lilitimia kwa hakika. Walifanikiwa kuuchafua moyo wa Jelini
vilivyo.
Sauti ya Zenda
katikati ya penzi akisikika kumfurahia Koku, ikamrudia Jelini akilini na kufanikiwa
kumtoa machozi aliyojionya asilie tena. Akijiambia hana sababu ya kulilia
kisichowahi kuwa chake. Ni Koku! Alishamsikia alikuwepo kwenye maisha yake, ila
“Amenidanganya
kwa kipindi chote hicho! Ameshindwa kabisa kumuacha mpenzi wake!” Alishazoea
kutesa wanaume wanao mpapatikia, sio kuteswa. Jelini akazidi kuumia. “Ananidanganya kumbe anamaisha yanayoendelea bila mimi
kujua! Nimekua mjinga kiasi gani jamani! Haya yameendelea kwa muda gani?” Jelini
akakumbuka siku ambazo hakuwa akilala nyumbani kwa Kasa, bila Kasa kumuita, akajithibitishia
ndio muda Kasa alikuwa akiendelea na yake, kwenye kitanda hichohicho alichokuwa
akipiga sarakasi zote za mapenzi akidhani anamkoleza. Jelini akazidi kulia kwa fedheha
akidhani alikuwa kila kitu kwa Kasa. Sauti ile ile aliyokuwa akihitimisha
kwake, ndiyo aliyoisikia akihitimisha kwa Koku. Hapakuwa na mlio wa tofauti
kwamba yeye alikuwa akifanya cha ajabu saaaana. Mwisho ni uleule.
Kumbe Kasa alishaacha
wote kwa ajili yake, siku hiyo ilikuwa siku ya kufa nyani. Zenda
akatelezea pabaya, akaangukia pua. Wenye uchu na pesa zake walimfanyia mipango,
na shetani hakuwa na usingizi, hajachoka, na hana kwingine pakwenda, alikuwa
upande huohuo, akawafanikishia kiurahisi. Akiwa anaaga zilipendwa wake,
na Jelini akatokea bila kutarajia, na kuachwa na kumbukumbu mbaya sana moyoni.
Jelini akazidi kulia
kwa uchungu na hofu ya kuambukizwa maradhi. Mzee si mla pipi kwenye ganda.
Anapiga kavukavu. Hofu ikazidi. “Ataniua,
nimuache mwanangu!” Ukawa ni ukweli wake anaotaka kuupitisha mayoni,
lakini mchungu mpaka machozi yakawa yakimmwagika peke yake hapo kitandani. Giza
la nje lilishaingia ndani. Akageukia mwanga wa taa iliyokuwa imewashwa nje,
mwanga wake umefanikiwa kupenya ndani. Akalia mpaka ikabidi atulie maana
maumivu ya kichwa nayo hayakukawia kumkumbusha kilema alichokipata alipokuwa
kwenye maisha ya huyo mzee.
Akatulia kabisa mpaka
akili zikamkumbusha faraja anayopata kutoka kwa Colins. “Mhh! Hiki
ninachojisikia kwa Colins nacho ni nini tena!?” Akawaza na kujishangaa.
Anaposhikwa na Colins, anapatwa hisia za ajabu, hajawahi kujisikia hivyo kabla.
“Mwili mzima unakuwa kama umepigwa shoti ya umeme!” Akawaza na kusikia
mlango ukifunguliwa taratibu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni nini Kitaendelea? Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment