“Unajisikiaje
Jelini?” Akabaki akimtizama huyo mrembo. Mzuri sana wa sura. Midomo ya rangi
kama Colins, akahisi ni dada yake. “Usiogope, hapa ni nyumbani kwa…” Akajaribu
kufikiria amueleze vipi. “Si unamfahamu Colins anafanya kazi na shemeji yako?”
Jelini akatingisha kichwa kukubali, na kujaribu kufuta yale machozi kwa haraka
ili asijue kama alikuwa akilia. “Basi hapa ni kwao na mimi ni mdogo wake,
naitwa Connie. Unajisikiaje kichwa?” Hakujibu ila kuendelea kujifuta machozi
yaliyokataa kukauka maana kumbukumbu ziliendelea kumletea sauti ya
kulalama kwa Koku akishugulikiwa ipasavyo na Zenda, kisha kana kwamba
anakomolewa, ikarudia sauti ya Zenda mwenyewe akiwa anapiga bao.
“Tafadhali usilie,
unajiumiza.” Akatingisha kichwa kukubali akijitahidi kufuta machozi yaliyokuwa
yakiendelea kutoka. Akashangaa huyo Connie anakaa pembeni yake, anamkumbatia
huku akimbembeleza kama mtoto, kisha kuanza kumfuta machozi kwa upendo.
Akamwangalia. “Nakutolea taulo ili ukaoge halafu ule. Utajisikia vizuri. Sawa?”
Akakubali kwa kichwa huku na mshangao wa kukumbatiwa na kubembelezwa kitoto.
Hapohapo chumbani
kulikuwa na choo, akaingia kuoga. Haikuwa nyumba ya ajabu ila pasafi halafu
patulivu sana. Huyo Connie mwenyewe jinsi anavyoongea ni kama ananong’ona kama
mama yake. Mzuri wa kuvutia haswa.
Wakati yupo bafuni,
Connie akamtumia ujumbe Colins na kumwambia kama Jelini ameamka ila analia. ‘Nijulishe akitoka kuoga.’ ‘Poa.’ Akamjibu kaka yake
na kwenda kwa mama yao pia kama kumpisha avae. Jelini akapata faragha ya kulia
kwa uhuru huko bafuni. Kilio kikaanza tena huku akiogaa mpaka akatoka. Akakuta
gauni kama tenite hapo kitandani. Connie alikuwa mwembamba haswa, Jelini
alikuwa na mwili japo alishaanza kutoa unene wa pombe alizokuwa akinywa na
kwenda kulala. Ila alikuwa na mwili mkubwa kuliko Connie halafu mfupi kwake.
Ukweli huyo Connie alikuwa mzuri sana. Urefu wakuvutia kama ambaye umshauri
agombee taji la warembo wa dunia.
Akamaliza kuvaa
akarudi kujiegemeza kitandani akijitahidi kutulia hapo ugenini. Mlango
ukafunguliwa, akaingia Connie na mama yake. “Usilie Jelini mwanangu. Unazidi
kujiumiza.” Akazungumza huyo mama kwa upendo, akakaa hapo kitandani pembeni
yake. “Halafu hujapaka mwili lotion. Nipe lotion.” Akashangaa huyo mama anaanza
kumpaka hiyo lotion miguuni. “Makubwa tena
haya!” Akajisemea Jelini nafsini mwake ikishangaa hiyo familia
inavyopenda kushikashika na kubembeleza, ndipo akamuelewa vizuri Colins.
Mara na Colins naye
akagonga na kuingia. “Vipi Jelini?” Walikuwa kama mapacha watatu hapo ndani.
Mama huyo ndio karithisha wanae hiyo
midomo. Wamemfanana na wamepoa wote kama maji ya mtungini. Jelini akajiinamia
tu. Akamvuta mkono taratibu huyo mama akaendelea kumpaka lotion.
“Mama CJ?” Sauti ya kibaba
ikasikika ikiita. “Nipo huku.” Akaitika huyo mama. “Sasa unaniachaje hivihivi bwana?
Umeniambia unarudi, hurudi!” “Nipo chumbani kwa Connie, nipo na mgeni. Njoo
nikuone kabla hujaondoka.” Jelini akasikia mlango anafunguliwa. Akaingia mtu,
ila akashindwa kumuangalia.
“Umependeza dad!”
Connie akaenda kumkumbatia, na busu baba yake. “Asante sweetheart. Vipi, si
nitakukuta?” “Narudi chuo usiku, kwa hiyo utanikuta.” “Sasa huyo badala ya
kuendelea kukaa hapa chumbani, hamieni na mgeni mezani ale.” “Sawa. Ndio
unataka kuondoka?” “Njoo uniage bwana! Hata hujaniombea!” “Wewe umeingiwa hofu
baba CJ, unataka kila saa nikuombee jambo hilohilo! Utafanikiwa tu, na Mungu
yupo na wewe.” Akaonge huyo mama akisimama kutoka hapo kitandani alipokuwa
amekaa akimpaka lotion Jelini.
“Mimi nina imani na
wewe dad. Utafanikisha tu huo upasuaji na huyo mama atatoka salama.” “Nashukuru
Colins.” Akasikia busu jingine. “Asante dad. Uniambie jinsi itakavyokwenda.”
Connie akamuachia baba yake maana alikuwa amemkumbatia. “Nitafanya hivyo.”
Wakatoka baba na mama yao. Jelini mpaka machozi yakakauka kwa hiyo familia
jinsi ilivyo. Ina amani, huwezi leta matatizo yako. Ila akajua huyo baba ni
daktari mpasuaji.
Pumu Imepata Mkohozi.
Taratibu Jelini
akajilaza na kugeukia ukutani. Colins akamfanyia ishara dada yake, akatoka.
Akaenda kuchukua taulo dogo, akaweka maji ya baridi akarudi nalo na kukaa
pembeni yake ila upande wa juu. “Lala chali.” Jelini akalia tena kidogo,
akasikia akimsaidia kugeuka. Na yeye akaanza kumfuta machozi kisha akamuwekea
kile kitaulo kichwani.
“Nisikilize Jelini.
Japokuwa sijui nini kimekuumiza, lakini hapo ulipo, mimi nimepita. Unasikia
maumivu ya kutoka ndani ya moyo kabisa. Hujui imekuaje! Hujui ni kwa nini!
Unatafuta kosa lako, halafu unajihisi umefanya kwa upande wako, hakuna
ulichokosea, lakini imetokea kilichotokea. Moyo hauamini kama
kweli imetokea, ila kumbukumbu zinakuhakikishia ni kweli imetokea.
Uchungu unazidi, unatamani isiwe imekutokea wewe. Si
kweli?” Jelini akashangaa sana amejuaje anachopitia ila hakujibu.
“Basi na mimi nilipita
hapo. Lakini nataka kukuhakikishia, it gets better. Ruhusu moyo upokee
matokeo. Ukifanya hivyo kwa haraka, hutajichelewesha. Utajikuta unavuka
hapo kwenye denial/kukataa kilichotokea, kwa haraka. Na utafikia
pia kwa haraka swali la ‘nini chakufanya’. Kisha kuishi na maamuzi yako bila kuyumba.
Ukichelewa kwenye kukubaliana na kilichotokea, ukabaki hapo kwenye denial
kwa muda mrefu, jua niliyokwambia mwanzo yatakutesa sana, tena kwa muda
mrefu. Mpaka kuja kukubali, utakuja kujikuta chaguzi ambazo ungefanya au nafasi
ambazo ulikuwa nazo mwanzoni kufikiria chakufanya, umezipunguza au zimeisha
sababu umechukua muda mrefu sana kwenye denial. Kukataa matokea.” Colins
akaendelea kuzungumza naye taratibu akimbembeleza.
“Natamani na mimi
ningekuwa si mmoja wa watu waliokwisha kukuumiza, pengine ungeamini
hayo. Lakini Jelini, uaminifu wangu kwenye mahusiano ndio umeniponza na kukuumiza
wewe usiye na hatia. Na pia sikutaka kukuingiza kwenye matatizo. Yule
msichana niliyekuwa naye kwenye mahusiano, alikuwa mkali sana, na hasira
zikimpanda, hanaga mipaka na hawezi kujizuia. Ni bora vile nilivyokuita mimi
tukazungumza pembeni, yeye asingeweza. Angekuzungumzisha vibaya, tena
hadharani, mbele ya watu. Najua ingekuwa vibaya zaidi. Ndio maana niliona
nikuwahi mimi kabla hajakuona ukinisogelea. Alikuwa hawezi kuona yeyote
karibu yangu. Hata Connie hakuwa akimtaka awasiliane na mimi, nikiwa naye.”
Jelini akashangaa sana. Japokuwa alikuwa amefunga macho lakini alikuwa anasikia
kila kitu.
“Inamaana
yule mchumba naye amemuacha mwanaume aliyekuwa mwaminifu kwake kwa kiasi kile!
Kwa nini mapenzi yanakuwa hivi jamani? Hawa binadamu wanataka nini wafanyiwe
ili watulie na kuwa waaminifu?” Jelini akawaza, akamuona machozi
yanamtoka. Alikumbuka jinsi alivyojitoa kwa Zenda na kuwa mwaminifu kwake
akimfanyia kila kitu, leo anamsaliti!
“Mara
ngapi amekuwa akifanya hivyo bila mimi kujua?” Akalia sana akijiona
mjinga, akidhani amempa penzi lote hawezi kutamani la wengine, kumbe hakuna
kitu! Akalia sana kwa kunung’unika akijidharau zaidi kila maneno ya Koku yalivyo
endelea na yenyewe kujirudia akilini mwake. Colins akaendelea kumfuta machozi
taratibu asijue ni mengi yanaendelea kwenye kichwa cha mwanadada huyo.
“Usilie Jelini. Usizidi
kujiadhibu. Hakuna gumu ambalo halina mlango wa kutokea,
labda ukatae tu mwenyewe kutoka. Hata kama sasahivi uchungu unakuonyesha
umefika mwisho, kataa. Upo mwanga mbeleni. Usiogope ukijiuliza itakuje.
Kwa kuwa huna jibu ya itakuaje mpaka uanze kutembea leo. Kila siku itajijibu
yenyewe. Umenielewa?” Jelini akatingisha kichwa kukubali. “Basi naomba nyamaza
kabisa kulia ili kichwa na chenyewe kitulie. Unaendelea kujiadhibu wewe
mwenyewe. Usikubali kujiadhibu. Watu wengine huna uwezo wa kuwafanya
wasikuumize, ila wewe unalo jukumu kwako. Usikubali kujitesa.” Akamfuta machozi
vizuri.
“Nikuletee kitu
kidogo ule?” Akatigisha kichwa kukataa. “Unataka kupumzika?” Akaendelea
kumuuliza kwa upendo huku akimpapasa taratibu kwa kutumia vidole vyake
akipitisha juu ya mkono wake mpaka chini kama anayemkuna ila kwa vidole. Na
hiyo sauti ya Colins, halafu ya kubembeleza, Jelini alijisikia faraja ya
kipekee. Halafu ni Colins sasa! Akaanza kusikia kupoa.
“Niambie nini unataka
Jelini?” Hapo anamuuliza na kumfuta machozi kwa mkono mwingine na kurekebisha
taulo alilomuwekea kichwani. Jelini akafungua macho na kumwangalia maana muda
wote hakuwa akimtizama. Macho yakagongana. Colins alikuwa mzuri sana wa sura.
Kitu kikatembea moyoni kwa Jelini na kushindwa kuelewa katikati ya uchungu
alio nao moyoni, hiyo ni hisia gani!
Akafunga macho.
Akahisi anamvuta mkono na kuubusu. Akashangaa nafsini kwake, nakutoelewa. Ila
akakumbuka hata dada yake na mama yake wapo hivyohivyo, watu wakushikashika
na kubusu. Hakufungua macho tena. Akamsikia akisimama. Akatamani amwambie asiondoke,
ila akamuacha tu. Akatoa lile taulo. Akaenda kulisuuza tena, na kurudi. Safari
hii alikaa, akamfuta machoni, usoni taratibu kisha akarudi tena kuliosha na kurudi.
“Nikiliweka kichwani
lina msaada wowote?” Akamuuliza kwa upendo, Jelini akatingisha kichwa kukubali.
“Afadhali.” Akalirudishia kichwani, akarudi kukaa pembeni yake. Akamshika mkono
vizuri, kwa upendo. Akaubusu tena, akabaki ameushikilia na mwingine akimpapasa,
hapohapo Jelini akapotelea usingizini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alikuja kuamshwa na
Jema. “Vipi kichwa?” “Mama yuko wapi?” Ndio likawa swali lake la kwanza bila
kumjibu dada yake. “Unakumbuka leo ndio ilikuwa ampeleke bibi KCMC kwa vipimo?”
Akaanza kulia tena. “Mama anakuja kesho, Jelini. Ametutuma mimi na James. Ndio
maana tumewahi kuja. Usilie. Twende ukapumzike nyumbani.” “Sasa kwa nini nyinyi ndio hamkumpeleka bibi hospitali,
yeye akaja?” “Wewe unamjua bibi, Jelini. Hakuna anayemuwezea isipokuwa
mama. Swala la hospitali kila mtu ameshindwa isipokuwa mama. Ndio maana kila
mtu amemuachia yeye. Mimi na James tusingemuweza bibi, na safari hii pia
asingekwenda hospitalini. Mama anakuja kesho, usilie. Twende.”
“Vipi kichwa Jelini?”
Akasikia sauti ya James. Ndio akajua hapo chumbani hawapo wao wawili.
Akapandisha mabega juu kukataa. “Kinauma?” James akajisogeza, akazidi kulia.
“Mimi nashauri umpe simu azungumze na mama kama alivyosema mama mwenyewe.”
James akamwambia Jema. Jema akamtumia ujumbe mama yake kwanza, kisha akaona
mama yake anapiga hapohapo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mama anataka
kuzungumza na wewe.” Jema akamkabidhi simu. Jelini akazidi kulia. “Kichwa kinauma sana?” Mama yake akamuuliza, akimjua
Jelini. “Kila kitu kinauma mama. Mbona huji sasa?”
Wakamsikia akimjibu mama yao. “Nakuja kesho Jelini,
mama angu. Bila hivyo bibi asingetibiwa. Naomba nenda kwa kina Jema. Mimi
nakuja kukuchukua kesho. Kunywa dawa ya maumivu na usingizi, ulale mpaka
nitakapokuja mwenyewe. Umesikia?” Akamrudishia simu Jema, akilia. “Ni mimi mama.” Jema akamuwahi maana bado alikuwa
akimbembeleza Jelini.
“Naomba
mumpe dawa ya maumivu na usingizi. Huyo hawezi kunyamaza mpaka nije mimi
mwenyewe na kichwa hicho bado. Kesho mapema sana nitakuwa huko.” “Mimi nashauri
utulie mama. Jelini atakuwa sawa. Tukifika nyumbani, atapata utulivu. Atakuwa
sawa.” “Sawa. Lakini mwambie kila kitu kikienda sawa, kesho nitakuwa huko.”
“Sawa.”
Wakakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mama anakuja kesho
Jelini. Naomba utulie. Twende.” Akatoka hapo kitandani akilia. “Acha mimi
nimsaidie.” Colins anatoa wazo na kusogea, ikabidi Jema ampishe maana
alikuwa amesimama hapo mbele ya kitanda alicholala huyo bidada na tumbo lake.
Akaanza kumfuta machozi kama mtoto. Jema akamwangalia mumewe. James akamuona
ila akanyamaza tu. “Twende Jelini. Kila kitu kitakuwa sawa. Usilie.” Akaongea
naye kwa kumbembeleza. Wakawa bado hawajaelewa.
“Mnisubirie
nikachukue kibegi changu.” James akahisi labda mkoba wake anaowekea laptop
zake. Maana wao watu wa electronics, basi kuzurula na aina hiyo ya mikoba ni
jambo la kawaida sana. Lakini sasa anakwenda nao wapi na inawahusu nini wao
wanaotaka kuondoka na mtu wao!
“Sitakawia.” Colins
akaweka msisitizo. “Kwamba tunaondoka wote!?” James akamuuliza kwa mshangao
kidogo. “Ndiyo.” Colins akajibu na kutaka kutoka. Akawa kama amekumbuka kitu
akiwa ameshafungua mlango. “Hivi si una mataulo yakutosha nyumbani kwako? Maana
mimi huwa sipendi kurudia taulo.” Hayo anamuuliza Jema. “Subiri kwanza Colins!
Kwani unataka kwenda kulala kabisa!?” “Kwani wewe si uliniambia mnavyumba
vyakutosha tu pale? Au ulipata wageni!?” Yaani na yeye akawa kama anamshangaa
James! Na hayo anaongea mlango upo wazi, nusu ya kiwiliwili kipo nje. Na
anaongea kwa sauti tu.
“Vyumba vipo.” “Basi mnisubiri kwenye gari,
sitakawia. Sitaki Jelini aendelee kulia hivi. Daktari amesema kichwa
kitazidi kumuua.” “Naomba tuzungumze kwanza Colins.” James akatoka naye nje ya
mlango.
“Vipi!?” Colins
akamuuliza akimshangaa James kama anayemchelewesha. Jema na Jelini ndani
wanasikiliza. “Wewe si uliniambia mzee Kasa alikufuata kukukataza usiwe karibu
na Jelini, lasivyo atakupiga risasi?” Jelini akashituka sana kusikia
hivyo. “Mimi mwenyewe nina mpango wa kumfuata na risasi. Maana ni kwa
nini Jelini alie hivi? Inamaana yeye anahusika na hicho kilio cha Jelini.”
James akashituka na kushangaa sana. “Colins!?” “Subiri kwanza James! Mbona kama
hutaki kufikiria? Wewe na Jema hamkuwepo hapa mjini. Na mama yao hayupo. Wakumuumiza
Jelini kiasi hiki ni nani kama siye yeye aliyebaki hapa mjini?” Colins akauliza
kwa ukali kabisa.
“Colins, mimi
nashauri utulie, usubiri kwanza.” “Nilifanya hivyo kwa kuwa alinihakikishia
atamuenzi Jelini, ndipo na mimi nikamwambia nitakaa naye mbali kama na
yeye atasimamia ahadi yake. Sasa siwezi mimi nikawa mwaminifu
kwenye makubaliano yetu, wakati yeye ameshindwa! Hata kidogo.” Colins
akaendelea akisikika na hasira.
“Kama hawezi
kumfanya Jelini kuwa na furaha, akae pembeni. Asitake kunichanganya na kunibabaisha!
Na hakuna anayemuogopa ila heshima tu. Akivunja heshima, hataheshimiwa.” Jelini
akashangaa mpaka akatoa macho na kumwangalia Jema. “Mimi nakushauri utulie
kwanza Colins.” “Hivi wewe James, upo upande gani lakini!?” “Unajua nipo upande
wako Colins!” James akamjibu akisikika amechoka kabisa, na mshangao juu,
“Basi nionyeshe
kwa vitendo kama kweli upo upande wangu, mimi kama mtu wako. Tena wakaribu
SANA.” “Ndio nakushauri
Colins! Nashauri usubiri kwanza tujue kwa hakika ni nini kinaendelea, ndipo
ujue jinsi ya kuchukua hatua ukiwa umejipanga.” “Kwa hiyo unaona mimi
kumtuliza Jelini sasahivi, asiendelee kuumia ninafanya haraka? Kwamba nimuache
tu aumizwe huko, halafu mimi eti nisubirie tu! Nasubiria nini na yeye
ameumia leo? Halafu kama hatataka kusema kilichotokea huko? Ninyamaze
tu, nasubiria?” Colins anaongea na James kana kwamba anahusika na huyo
Jelini zaidi yake yeye James. Kwamba jambo limemfika yeye zaidi kuliko
mwingine yeyote yule. Kama nani! Hakuna ajuae. Halafu kalivalia njuga na
kulibebea bango mpaka James akaishiwa hoja.
“Nisubiri.” “Sasa
unahamia kwangu kwa ajili ya nini Colins!?” “Si ndipo atakapokuwepo Jelini!? Au
mnampeleka wapi? Maana alikuwa ametulia hapa. Mama na Connie wanampa huduma
nzuri za kidaktari, analala vizuri. Wewe umekuja kumchukua!” Ikawa tena lawama.
James akachoka kabisa. “Hivi huyu Colins anakumbuka kama mimi ni shemeji
yake Jelini, na ndiye niliyempigia simu kumuomba msaada kwa ajili ya huyu
Jelini, tena kwa muda tu?” James akawaza akimtizama alivyoshupalia jambo.
“Hapa alikuwa ametulia
kabisa! Tena mmemkuta amelala, mmemuamsha!” James akachoka kabisa. “Mama yake
ametutuma tuje tumchukue, Colins. Leo atakuwa kwangu mpaka kesho atakapokuja
kumchukua yeye mwenyewe.” “Mimi najua jinsi ya kumtuliza. Nataka
atulie. Au wewe unaona sawa aendelee kulia huku unajua fika ametoka kushonwa
kichwa?” Akauliza kwa ukali. “Hapana Colins! Unajua wote tupo upande mmoja.”
“Aisee huonyeshi kabisa kama upo upande wangu James!” Mpaka Jema akashangazwa
huko ndani.
“Sawa Colins. Acha
mimi nikuache na maamuzi yako. Maana nakujua wewe unapoamua jambo lako.”
“Basi nisubiri nakuja. Tuondoke wote.” “Si uje na gari yako Colins?” “Kwamba
mimi ndio niondoke hapa na Jelini na gari yangu, tuwafuate hata baadaye?” Na
yeye akamfanyia James makusudi. Akijua James hawezi kukubali. “Naona
wazo lako la kukusubiria sio baya.” James mwenyewe akasalimu amri. “Basi nitatuma
dereva aniletee gari yangu usiku au kesho asubuhi. Sitachelewa.” Colins
akaondoka na kumuacha James hoi.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Ukishika, Shikamana.
Itakuaje?
0 Comments:
Post a Comment