Zenda akagundua sauti inatoka hapo nje ya mlango. Aliruka kitandani nusura aanguke, Koku akimtizama. Anatokaje bila nguo! Akaanza kusaka sasa japo pensi tu huku amepaniki kuliko maelezo. Anakimbia humo chumbani mpaka akafanikiwa chakujisitiri chini. Akafungua sasa mlango akitetemeka mpaka Koku akashangaa kumuona KASA anatetemeshwa na mwanadamu! Ikabidi akae vizuri na kuvuta shuka kujisitiri maana alikuwa na yeye kama alivyozaliwa, macho yakimsindikiza Kasa vile anavyo haha.
Kufungua mlango na
kutoka, lahaula, Jelini! Amekaa chini kabisa, uchi zaidi ya mnyama
aliyesitirika na manyoya. Amefukia uso katikati ya mapaja. Analia kwa kwikwi
akijitahidi sauti isitoke, mikono ameziba masikio kama aliyekuwa hataki
kusikia. “Mungu wangu!” Akasikika Zenda. “Mungu wangu Jelini!” Akasikika tena Zenda
kwa mshituko wa ajabu. Mikono kichwani Koku akimtizama pale mlangoni
akichungulia nje kama anayeogopa kutoka kabisa.
Kile kitu kikamkera
Koku na kumpandisha hasira ya ajabu. “Acha utoto Kasa. Unachanganyikiwa
nini hapo kama mtoto mdogo!? Nani alimwambia aje kwenye majumba ya watu asubuhi
asubuhi bila taarifa? Yeye hajui kama una maisha yako? Au yeye ndio alidhani ni
Livingstone kwamba ndio amekugundua hapa duniani!?” “Nyamaza Koku.” “Unapaniki
nini wewe?! Ndio madhara yakutembea na vitoto vidogo visivyo na akili. Havina
mipaka! Ona sasa unafuatwa mpaka chumbani! Si wazimu huo?” Kasa akatoka, Koku
naye akatoka pale kitandani kajifunga shuka tu, ndani mtupu.
Akatoka mlangoni,
akamkuta Jelini kwenye ile hali. Kunyanyuka aondoke hawezi, mwili
umekufa ganzi kabisa. “Acha ujinga wewe mtoto, hebu nyanyuka hapo nenda kwenu.
Wewe ulifikiri Kasa atakuoa?” Koku akamuuliza kwa kumdharau.
“Umenikuta na Kasa, tumetulia kimya. Umeingia hapo siku mbili tatu, tayari
unajiona mmiliki halali! Si ujinga…” Jelini akasikia kibao cha nguvu.
“Unanipiga Kasa wewe sababu ya malaya huyu?” “Ondoka Koku.” Kikasikika
kibao kingine cha nguvu, Jelini akazidi kujificha uso asiwatizame.
Kumbe Koku
alimrudishia Kasa kibao. Na yeye akampiga Kasa. “Usiwahi kunipiga maishani
mwako kote Kasa. Uliniita hapa wewe mwenyewe ukiniomba, tena ukaniambia hujaridhika
kwa muda mrefu, unahamu na mimi. Iweje leo uanze kunipiga? Tena usirudie
tena.” Koku akamfyoza kabisa.
“Kinakuchanganya
kitoto hiki, unakua kama mwehu, kwa kipi mno? Malaya tu huyu wa hapo Tegeta!
Analala na kila mwanaume hata Kevi alimkataa!” Hasira na wivu zikamfanya Koku
atoe siri ambayo alionywa asije akaropoka kwa baba yao hata neno
moja juu ya Jelini. Lakini Koku akaonyesha anataarifa zake zakutosha.
Akaendelea kubwatuka.
“Anajiliza nini hapo kama si uongo tu? Ingekua amekufumania hapo sawa.
Amekukuta nyumbani kwako, ukiendeleza starehe, kama kawaida yetu! Anachojiliza
nini sasa? Acheni kunichanganya.” Koku akarudi chumbani na kuwaacha hapo akiwa
ameharibu haswa. Ameridhika kuwakosanisha haswa. Jelini amepata habari yake
kamili. Kasa alikuwa ameishiwa nguvu, hajui afanye nini. Akaenda kukaa kwenye
kochi la hapohapo, akainama, Jelini akiendelea kulia kwa uchungu kama kafiwa
na mama Jema.
Kimya, Zenda hajui
aseme nini, Koku yeye akioga ndani bila hata wasiwasi. Kazi aliyopewa
kaimaliza, tena kaikamilisha vizuri haswa mpaka mwenyewe akashangaa. Mwishoe
Jelini akajikaza, akajikusanya, akanyanyuka pale, uchi vilevile akarudi sebule
kubwa alikokuwa ameacha nguo zake. Akaanza kuvaa akilia sana. Kamasi na machozi
vikimtoka kama mvua. Zenda akamsogelea ili amshike. Jamani Jelini aliruka, kama
anaye epuka moto, au amepigwa na shoti ya umeme, nusura aanguke
mpaka akamtisha Zenda. Akachukua pochi yake, sidiria alishindwa kuvaa, akaiweka
kwenye pochi, nakutoka. “Nisubiri nikusogeze Jelini. Usi…” Mlango ukafunguliwa,
nakufungwa, Jelini akatoka.
Zenda akamkimbilia
kwa haraka akiwa na pensi nyepesi sana, kifua wazi, bado analia, anatembea hapo
kwenye ua wake mrefu akielekea getini atoke. “Jelini! Jelini! Akakimbia mpaka
mbele yake. Naomba usiondoke. Tafadhali mpenzi wangu.” Jelini akamzunguka na kuendelea
kutafuta geti. Jumba la Zenda kubwa sana. Zenda akakimbilia ndani kuvaa na
kuchukua funguo ili amfuate na gari, akamkuta Koku anavaa taratibu hana haraka.
Hakumsemesha.
Akaanza kuokota nguo
za jana hapo sakafuni, alizokwenda nazo kanisani nakuanza kuvaa kwa haraka ili
kumuwahi Jelini. “Unapaniki nini wewe Zenda?! Mbona hueleweki? Jana unalilia
penzi langu, leo unapaniki na katoto hako ambako hakana mbele wala nyuma? Wewe
muache, atarudi mwenyewe sababu ya pesa. Maisha magumu hivi, unafikiria
kwa mjinga kama yule, atakula nini?” “Katika wote, yeye ni mtu wa
kwanza maishani ambaye anajua ninazo pesa, na hajawahi kuniomba hata
shilingi, ila upendo wa kweli. Kwa hiyo kujibu swali lako la kwa nini na
paniki, basi hicho ndicho kinanipanikisha.”
“Jelini ni watofauti
na nyinyi wote. Nyinyi mmesoma na mnalipwa mishahara yenu, ila mpo na
mimi sababu ya pesa zangu, lakini Jelini amenifuata leo kwa sababu jana kwa akili
zangu nilimlalamikia nipo mpweke, nimemmisi, nina hamu naye.” “Basi ndiyo
hayohayo uliyoniambia na mimi.” “Mimi najijua Koku. Na sijui jana nilinyweshwa
nini, lakini WEWE, siwezi kukulinganisha na Jelini hata nikiwa
usingizini.” Hapo akamuudhi Koku mpaka mwisho.
“Wewe ni mshenzi
Kasa.” “Sikutusi, lakini kilichoniamsha asubuhi hii nikiwa kwenye usingizi
mzito nikidhani ni Jelini ndiye anayecheza na mwili wangu, lakini haikuchukua
hata dakika moja nikashituka nikijua wewe si Jelini. Mwili wangu ukiwa
mikononi kwa yule mtoto, ni hisia ambazo nina uhakika kwa asilimia 100 wewe
hujawahi kuzisikia. Na kwa jinsi ninavyokujua, nina uhakika
utakufa kabla yakupata hizo hisia. Kwa hiyo usiwahi kujifananisha na
Jelini, Koku. Haupo hata robo yake. Siku njema.” Kasa akatoka kisha akarudi.
“Utatamani
lile kofi nililokupiga, usingenirudishia, itoshe vile. Lakini ulinirudishia,
tena mbele ya Jelini!” “Utanifanya nini? Nakuuliza Kasa, utanifanya
nini?” Koku akauliza kwa hasira kali sana. Kasa akamwangalia kwa sekunde
kadhaa, akacheka kwa kumsikitikia, kisha akatoka akiwa amemuumiza sana
Koku. Yaani yeye hayupo hata nusu ya Jelini aliyemdharau kwa kiasi kile! Akaumia
sana akabaki akimfyonza Kasa na kumtusi kwa sauti. Alimsikia, lakini akatoka
kumuwahi Jelini.
Ukweli Mchungu.
Zenda akakumbuka
shuka, kweli kumekuchwa. Akatoka kwa kasi kumkimbilia Jelini, hakumkuta kwenye
uwa wake. Walinzi wakamwambia alishatoka. Akarudi kuchukua gari ili kumfuata
akijua atampata tu kama siku ya kwanza kukutana kwao Jelini alipoamkia
asipopajua, baada ya harusi ya Jema. Kasa aliendesha kama mwehu asimpate
Jelini. Jelini aliyelelewa jijini bila usafiri wa nyumbani, huna utakapomuacha
asifike anakokutaka. Alishapata usafiri na kuomba apelekwe hotelini maana
nyumba walifunga, wakiwa wanaenda kwa bibi. Alirudi bila funguo akijua atakuwa
kwa Zenda mpaka mama yake na Jeremy warudi jijini. Hakuchukua funguo za nyumba.
Uzuri alikuwa na pesa, akachukua chumba kwenye hiyo hoteli, akaingia hapo
nakuzidi kulia.
Kila akikumbuka sauti
ya mapenzi aliyokuwa akiisikia kati ya Zenda na Koku alizidi kulia akigandamiza
mto masikioni kama asisikie tena. Mbaya zaidi dhihaka za Koku ziliingia
mpaka moyoni, akili ikawa na kazi ya kujichotea tu huko moyoni nakurudisha
kwenye kumbukumbu. Akakumbuka mazungumzo ya jana yake kati yake, mama yake
mdogo na mama yake. Akaumia kugundua mama yake alikuwa sahihi, wakati akimtetea
Zenda. Jelini akazidi kuumia, akishindwa kunyamaza kabisa.
Kuliko Ungua Mpini.
Huku nyuma baada ya
kukata tamaa hampati Jelini, akarudi kwake. Hakumkuta Koku. Akakaa akiwaza.
Akili ya mzee ipo kichwani. “Hata kama nilikuwa nimelewa kwa kiasi gani,
maneno aliyosema Koku nilimwambia, si kweli.” Akapinga kabisa mawazoni. “Halafu
sikuwa nimekunywa kiasi chakunifanya nilewe hivyo!” Zenda akaendelea
kuwaza. “Na Koku anaonekana anafahamu habari zangu na Jelini mpaka Kevin!”
Taa kichwani zikawaka. Zenda alijaliwa akili ya kufikiria sana, na wanae walimjua
ndio maana walimuomba Koku asije ropoka jina la Jelini mbele yake. Hasira na
wivu kuona Jelini amethaminiwa kuliko yeye, vikaushinda ubinadamu. Akamwaga
mchele kwenye kuku wengi.
Zenda akasimama kama mshale.
“Walinilevya!” Akashituka sana baada ya akili kukubaliana na hilo. “Sasa
ole wao nikakute madawa mwilini mwangu.” Akatoka kwa haraka kama simba
aliyejeruhiwa kwenda hospitalini kupimwa damu. Hakuwa ameoga wala kusafisha
uso. Alikuwa amepaniki kama mwehu. Damu kutolewa na kupimwa, wakakuta madawa
kwenye damu yake. “Wamemwaga mchele, acha niwamwagie mboga. Wamemtoa Jelini
kwangu, nawatoa na wao kwangu.” Akatoka hapo mpaka polisi.
Mzee akatoa mashitaka
kuwa jana alikuwa nyumbani kwa familia ya Rweza akiwa amekaribishwa chakula,
walimpa madawa. Anahofia maisha yake. Kwamba wanataka kumuua.
Hapo mzee anafungua kesi na wakili wake alishafika hapo, ila akashangazwa sana na
hao watu anaowashitaki. Wanae wote wawili, mume, na Koku! Akawashitaki wote akisema
ndio aliokuwa nao, sasa hajui ni nani alitaka kumdhuru kwa hakika. Kesi
ikatengenezwa, ikawa ni shitaka la kukusudia KUUA. Akatoa vipimo vya
hospitalini, wakajiridhisha.
Mwisho Wa Ubaya, Ni Ubaya.
Usicheze na aliyekutangulia,
halafu mwenye hela aliyetafuta kwa kutumia kichwa chake! Mwisho wake si mzuri. Koku
akiwa nyumbani kwake, akagongewa na polisi, akaambiwa yupo chini ya ulinzi kwa
kusudio lakutaka kuua. Alishituka Koku, akapigwa pingu akatolewa hapo
kwenye jumba lake kama mtuhumiwa kwelikweli na Kasa alitaka
washugulikiwe kama majambazi haswa. Pesa anayo, ashatanguliza kwa watakao
kwenda kukamata wabaya wake, na kweli msomi na tajiri Koku akiwa na harufu
nzuri mwilini, akatupwa nyuma ya gari, akakimbizwa rumande asiamini.
Kemi naye akiwa ameshapongezana
na mama yake pamoja na ndugu yake kuwa wamefanikiwa kumrudisha Koku kwenye
maisha ya baba yao, wasijue Koku alivunja sharti kubwa walilomsisitizia
hata kama awe amelewa vipi, asije onyesha anamfahamu Jelini mbele ya baba yao,
maana mzee ataunganisha matukio, wote watakuwa matatizoni. Na kweli alishindwa
kirahisi sana. Hasira ikawa hasara yao wote.
Akiwa na wanae
wametulia tu nyumbani, mume ametoka kwenda mtaani kwa marafiki zake wa jijini,
Kemi naye akaambiwa ana wageni. Akatoka kwenda kuwasikiliza maana hakutaka mtu
asiyemfahamu ndani kwake. Hapohapo akasomewa shitaka lake, akaulizwa
alipo mumewe, akasema hajui, basi yeye akapigwa pingu, polisi. Hivyohivyo kwa
Kevin.
Noah akiwa baa
akifurahi na marafiki zake kitajiri, wakinywa mapombe ya garama, akapata simu
kutoka kwa vijana wake, wamepaniki kwelikweli. Wakamsimulia. Pombe yote
ikamuisha, akakimbilia polisi ndipo na yeye akakamatwa. Wote wakawekwa
ndani. Mbaya ni msimu wa sikukuu, shitaka ni la kukusudia kutaka kuua.
Hakuna DHAMANA. Hapo ndipo Zenda akaridhika na kurudi nyumbani sasa.
Bahati Ya Mtende.
Takataka Kwako, Hazina Kwa Mwengine.
Inafika jioni Jelini
kichwa kinamuuma hawezi hata kusogea. Ikabidi awashe simu ampigie mama yake. “Nakufa mama.” Mama Jema alishituka kumsikia
mwanae analia. Mama wa kichaga anapenda hao binti zake, kuliko roho yake.
Akaanza kutetemeka. “Upo wapi?” “Kichwa kinauma, nahisi ule mshono unapasuka, mama. Nipo
peke yangu hotelini. Nitakufa mama, niache mwanangu.” Hapohapo akampigia
simu Jema. Amepaniki kwelikweli. “Naomba tulia mama,
ili nielewe.” James akachukua simu. “Kuna nini
mama?” “Sijui. Ila Jelini amenipigia simu, ule mshono wa kichwani unataka
kupasuka na yupo peke yake. Atakufa
mwanangu, mimi ndio nibaki sina kitu. Watoto wenyewe ni wawili tu. Sina..” Mama Jema na yeye kilio, ameshapaniki. Udhaifu wake
kila mtu alimjua, ni hao binti zake. Ni jeuri, roho ngumu yule wakuweza banwa
kidole na mlango, asishituke ila si kilio cha hao binti zake. “Naomba tulia mama yangu. Acha nimpigie mimi simu.”
Akakata kwa mama Jema na kumpigia simu Jelini.
Jelini alipoona simu
ya James akapokea. “Pole Jelini. Nini shida shemeji
yangu.” Jinsi alivyoanza naye, ikamfanya Jelini atulie. “Nipo peke yangu hotelini. Kichwa kinaniuma sana, kinakaribia
kupasuka.” James akafikiria kwa haraka, nani wakumtuma hapo. Maana ndugu
zao wote wapo Moshi. “Nampigia simu mtu, aje akufuate
na kukupeleka hospitalini. Hakikisha hujaloki mlango ili aweze kuingia. Na
kingine, naomba nyamaza kabisa. Usilie hata kidogo ili kichwa kitulie. Sawa?”
Akakubali.
James akabaki
akifikiria mtu wa kumtuma hapo kwa haraka, siku hizo za sikukuu, mtu ambaye
hana mengi yakufanya ni nani? Wazo likamjia ni Colins. Na hivi mama yake
ni muuguzi, akampigia na kumueleza. “Nilikuwa nikitaka
kutafuta mtu wa kunisaidia, amfuate hotelini na kum….” Colins nusura
aruke. “Wewe vipi James!? Nakwenda mwenyewe.”
Uzuri alikuwepo tu kwao, wamekaa wote sebuleni kama familia, wakiangalia movie,
wakila na kunywa. Siku hiyo walikuwa wanapumzika tu baada ya sherehe za
krismasi walizo sherehekea pamoja na familia nyingine nyumbani kwa kina Love
ambaye baba yake ni rafiki wa tokea ujanani na baba yake Colins. Walikesha nyumbani
kwao, walitawanyika kurudi makwao karibia panapambazuka.
Walikwenda kulala
wote ndio wameamka mida hiyo ya jioni, Colins akaenda nyumbani kwa wazazi wake,
nyumba ya pili tu, uzio mmoja, ndio wamekaa hapo wamepumzika, ndio na simu ya
James kuingia. Colins akamuomba mama yake amsindikize, akatoka na mama yake
mbio wakiwahi hotelini. Wakaendesha Colins akiomba Mungu amkute Jelini salama.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika na kuelekea
chumbani moja kwa moja bila hata kuulizia mapokezi wakamkuta amelala chini ya
mto. “Jelini mama!” Jelini akashangaa sauti nzuri sana ya kimama ikimuita.
“Pole sana Jelini.” Akatambua sauti ya Colins, akatoka chini ya mto.
Akajitahidi kufungua macho, akaona kwa shida kama mapacha wamemsimamia ila
akagundua ni mama yake. Akafunga macho nakutamani asingekuwa Colins amemkuta
kwenye hali ile. Akajisikia aibu!
“Samahani
kwa usumbufu.”
Jelini akaongea akijitahidi kugeuka vizuri. “Pole.” Colins akarudia tena akiwa
anamwangalia anavyojiweka sawa pale kitandani. Kugeuka na kumwangalia vizuri! Alikuwa
amevimba uso, macho mekundu kwa kulia mpaka wakashituka. Colins akakimbilia upande
wa bafuni, akachukua taulo na kulilowesha maji ya baridi, akaenda kuanza
kumfuta huku mama yake akimpima pressure. “Pressure siyo mbaya. Nashauri twende
hospitalini ili wamwangalie zaidi.” Colins akamuweka sawa, Jelini akachukua
pochi yake, Colins akaibeba na kumshika mkono kama mtoto mdogo anayemvusha
barabara mpaka kwenye gari. Safari ya hospitalini ikaanza. Mama Colins
akashauri wampeleke kwenye hospitali anayofanyia kazi, ili wamsaidie kwa
haraka.
Ikawa wazo lake lipo
sahihi. Walifika tu na walipomuona mama Colins wakamsaidia kwa haraka.
Wakaangalia kichwa, kila kitu kipo sawa. Daktari akamuuliza Jelini ni nini
kinamfanya alie vile. Akidhani ni kichwa ili akafanyiwe MRI. Jelini akasema
hapana, ila kulia ndio kumesababisha kichwa. Ndipo wakaelewa.
“Sasa nisikilize
Jelini. Huu mshono unawezekana umepona kabisa kwa nje ila ndani kunaweza kukawa
bado. Unapoendelea kulia unafanya mishipa ya kichwa kukakamaa na kusababisha
kichwa kuuma zaidi. Nakupa dawa ya maumivu na ya usingizi ili ulale kabisa. Na
ukiamka, marufuku kulia.” Akakubali kwa kutingisha kichwa huku amefunga macho.
Wakazungumza na mama Colins. Kwa kuwa na yeye ni muuguzi, akaomba aondoke naye,
akapumzike.
Colins tena akamshika
mkono mpaka kwenye gari, ndipo mama Colins akampigia simu mama Jema kumtuliza. “Tafadhali usiwe na wasiwasi. Huyu ameshafika kwetu, atakuwa
sawa tu. Wewe malizia likizo yako, Jelini atakuwa na sisi nyumbani. Wamemchoma
sindano, amelala. Usiwe na wasiwasi kabisa.” Mama huyo ongea yake
yenyewe itakufanya utulie tu. Mama Jema akauliza maswali yake mengi hapo ya
hofu mpaka akaishiwa. Akatulia. “Kesho nampeleka mama
KCMC kila kitu kikienda sawa, nitarudi Dar kesho kutwa. Naomba niangalizie
mpaka nirudi.” “Mama Jema, nimekwambia usiwe na wasiwasi. Huyu Jelini anakwenda
nyumbani. Wewe hata ukikaa huko zaidi ya mwezi, atakuwa sawa tu.” “Nitakufa kwa
ungonjwa wa moyo, mama angu. Acha nirudi tu mwenyewe.” Akacheka taratibu
huyo mama. “Basi kukutuliza, asubuhi akiamka
nitamwambia akupigie ili utulie.” Wakakubaliana na kuagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bahati Haiji Mara Mbili. Anguko La Zenda, Bila Kutarajia Jelini
Mikononi Kwa Colins.
Nini Kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment