Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 28. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 28.

Chakula kikawa tayari mzee hajarudi, anacheka na Jelini nje baraza jingine kabisa mbali kabisa na hapo kama asiyetaka usumbufu. Anacheka kwa sauti ya juu kwa furaha zote. “Sasa sio unirudie na mchaga huko!” “Umenipa wazo.” “Acha kutaka kuniua Jelini!” Jelini akazidi kucheka. “Ukirudi ujiandae kukesha. Nishaona mali zangu, hapa hali mbaya.” “Sikukukataza kuchungulia wewe?” “Wala sijuti! Nimeona hivyo, hamu ya kusubiria imeongezeka.” Wakaendelea kuzungumza mpaka akaja kuitwa na mtoto mdogo wa Kemi kuwa chakula tayari. “Hey grandpa, lunch is served.” Mtoto akamwambia. “Right behind you.” Dogo alivyojibiwa hivyo kuwa yupo nyuma yake, yeye akaondoka zake.

Wakabaki kumsubiria. Hawawezi kula bila mzee mwenyewe kuwepo mezani. Kiti chake maalumu kikabaki kikimsubiria, kila mtu yupo meza ya chakula, wanamsubiria yeye akiagana na Jelini. Wakabembelezana kwenye simu mpaka akaamsha tamaa kwa Jelini pia, ndipo mzee akarudi ndani akakuta wote wakimsubiria. Alivyo jeuri wala hakujali. Akakaa wafanyakazi wakaanza kuwahudumia hapo mezani, Zenda akawa mtulivu haswa, akili na mawazo kwenye mwili wa Jelini aliouona muda mfupi kabla hajarudi kukaa hapo mezani. Wivu na wasiwasi kwa vijana wa kichaga, waliorudi migombani kuhiji, wasije mzidi mahesabu.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Huku kwa kina Jelini, Mode akawa anacheka nje hana mbavu maana alijua anachokifanya Jelini chumbani. Alivyotoka tu, akamuwahi. “Karidhika?” “Wapi! Ndio nimeharibu kabisa. Anatia huruma, analalamika eti anateseka. Anatamani niwepo pale alipokuwepo sasahivi.” “Baba lina mihela ya kununua jiji, sasa kwa nini usilishikie mimba kulibana moja kwa moja?” Mama Jema alishituka sana alivyosikia hivyo karibia kuruka. “Mode koma wewe! Koma kama ulivyokoma ziwa la mama yako. KOMA.” “Basi dada.” “Nakwambia koma. Koma kabisa.” “Basi dada yangu.” Mama Jema alikuwa amewaka kama moto wa dizeli. “Unamtia ujinga huyo, atazalia matajiri wangapi mjini? Kama yeye anania ya kweli na Jelini si angetangaza ndoa ndio nikajua ana..” “Mama, umekasirika. Unaanza kum..” “Usinitanie Jelini wewe! Unafikiri mimi mjinga? Yeye hana mke. Kama kweli anakupenda si angekuoa?” “Zenda ananipenda mama.” Jelini akajibu kwa upole.

“Kama anakupenda mbona haalalishi? Anasubiri nini mtu mzima na ashakamilisha kila kitu kwenye maisha yake? Anakazi ya kusema hawezi kulala au kuishi bila wewe, mbona hakuoi kama kweli?” Mama Jema akabadilika, Jelini asiamini. “Usinione nimenyamaza, ukajiachia hovyo. Na Mode koma kumshauri mwanangu ujinga.” “Nimeomba msamaha dada, jamani!” “Unataka kumuharibu kichwa mwanangu, akakwame kwenye ulezi wakati mwanaume anaendelea kuhangaika na wanawake wengine?” “Zenda sio malaya, mama.” Jelini akamtetea kwa upole.

“Kwa hiyo unataka ufuate ushauri wa Mode, kwenda kujishikisha mimba kwa mtu asiyeonekana na nia na wewe yakudumu? Amekuona dogodogo mzuri, ndio anakuwinda. Sasa jidanganye ushike mimba uone kama hajaendelea na wanawake zake wengine.” “Zenda anania na mimi, mama. Hana wanawake wengine tena. Amewaacha wote kwa ajili yangu. Ananipenda mimi kwa dhati na ndio maana halali na mwanamke mwingine yeyote yule tokea aanzane na mimi. Hilo nina uhakika nalo kwa asilimia zote. Hanidanganyi. Zenda yupo na mimi tu. Ndio maana hata iweje atanisubiri mimi au atanipigia simu niwe naye. Kama angekuwa na wanawake wengine, kwa nini angekuwa akiniita tu mimi? Si wakati mwingine angejidai hata amesafiri ili awe nao?” “Wewe amini unachotaka kuamini, lakini hutambembea mimba mpaka awe mumeo kihalali. Usinitanie mimi.”

“James anampenda Jema, roho yake. Mbona asimpe mimba ndio akamuoa? Tena hakumgusa mpaka alipokabidhiwa kihalali. Leo unataka kunibebea mimba zisizoeleweka mimi?” “Ila mimi sijasema kama nataka kumbebea mimba. Ni mamdogo ndio akasema.” “Sasa Jelini usinirudishie mimi mpira tena! Kwangu alishaondoka. Unataka kumrudisha tena, azidi kuniwakia!” “Alieanzisha huo ujinga ni nani kama si wewe? Koma Mode.” “Nimekoma dada yangu. Naomba yaishe. Nikuongezee bia ingine?” “Sitaki.” Dada yao akaanza kucheka.

“Sasa dada na wewe unacheka nini badala ya kunitetea?” “We koma! Unataka mama Jema anigeukie mimi? Wewe umelikoroga, linywe.” “Unataka ku..” “Mama, naomba yaishe. Mimi sishiki tena mimba mpaka ndoa, kama Jema. Kwanza kizazi chenyewe umekifunga mama yangu. Hiyo mimba inaingiaje?” “Kwani hakifunguki? Ushauri huo wakijinga ukiupokea si unaweza kwenda kutoa hicho kitanzi ili ushike mimba? Na hivi unavyojisifia anakupenda! Sasa kitakachokushinda kujiachia ni nini?” “Mimi sitatoa kitanzi, wala sitaki ushauri wa mamdogo.” Mama mkubwa mbavu hana, Mode kimya. Mama Jema akafyonza kwa hasira na kunyanyuka. “Nikusindikize dada yangu?” Mode akamchokoza. “Sitaki.” Jelini na mama mkubwa mbavu hawana.

Kupigwa na Akujuaye.

Wakala na kunywa, Zenda asijue anapigwa wanapojua patauma kweli. Inafika mida ya saa moja, mzee amelewa hawezi hata kunyanyua mguu. Koku akajitolea kumrudisha nyumbani kwake, kwa gari yake. Likawa si jambo baya kwa Zenda. Cheko limemjaa hana habari ya kadhalika. Akamfikisha nyumbani mpaka chumbani. Koku mwenyeji pale. Anajua kila kitu, kila sehemu. Akamfikisha mzee chumbani akamtoa na nguo. Akamchombeza kimapenzi, na hivi alishaanzishiwa na Jelini mpaka kumuona vya undani akimtaka amuonyeshe hiki na kile na Jelini naye akawa hana hiana. Akaenda mpaka chumbani, akatoa nguo zote akawa na kazi ya kumgeuzia Zenda atakavyo. Hapo Koku anamchombeza, hakuchukua muda, mzee akagawa penzi kisha kuzima asijue kama Koku alilala pembeni yake uchi kama alivyozaliwa na mama yake mzazi.

Baada ya.

Huku kwa Jelini yeye alilala kwa shida akimuhurumia Zenda aliyeachana naye akiwa na majonzi ya upweke. Akaamka naye mawazoni akiwaza muda watakao tengana. Akajua kweli Zenda yupo sahihi, ni muda mrefu sana. Akakumbuka sononeko lake akilalamika kuwa yeye hawezi kuishi bila Jelini, na maneno mengi yaliyomuingia Jelini na kuona anahitajika sana na Zenda. Na picha za uchi alizokuwa akimtumia na mwishoe kwenda kujitoa nguo zote akimuonyesha kwenye video hiki na kile mwilini mwake, Zenda akimwambia anahali mbaya, anamtamani, zikaamsha hisia na kwake pia, asijue mwenzie alishakatwa kiu zake na amelala na zilipendwa wake.

Akabaki akikumbuka wakati mzuri anaokuwa nao akiwa na Zenda. Jinsi anavyomsifia kwa kila kitu. Jelini akabaki kitandani akiwaza na kushindwa kuvumilia kumuacha Zenda kwa muda wote huo. Eti mpaka na mwaka mpya awe mbali naye! Moyo ukakataa.

Akakumbuka vile Jema alivyofuatwa na mumewe kwa surprise akapata wazo na yeye la kwenda kumsuprise Zenda ili ainue furaha ndani yake kama James alivyoinua furaha ya Jema. Akahangaika kupiga simu huku na kule mpaka akapata nafasi ya ndege inayotoka KIA alfajiri sana kumfikisha Bongo kwa mpenzi Zenda. Akakodi taksii kutoka migombani kwa bibi yake mpaka KIA, hakutaka kumsumbua mtu. Ila akaacha ujumbe kwa mama yake na Jema kuwa amepata dharula, anatangulia Dar kumbe si dharula, anataka aka msuprise Zenda.

Ndege Mjanja.

Huku kwa Zenda yeye akawa kweli amenaswa kwenye tundu bovu. Kila alipojitahidi kuamka, kichwa kizito, akarudi kulala na Koku naye aliweka mziki mzuri wa usingizi, na chumba akaweka mwanga mzuri anaopenda Zenda kutumia akilala siku asizoenda kazini. Koku alijua, na yeye mwenyeji pale anajua kila kona ya hiyo nyumba. Na mwenyewe Zenda anaweka alamu. Kwamba muda wake wa kuamka ukifika, mziki na mwanga wa usingizi vinabadilika, madirisha yanaanza kujifungua kuruhusu mwanga wa nje kuingia ndani. Kwa hiyo hata kama yupo usingizini, basi ataamka tu kwa sauti ya madirisha kujifungua na mwanga kuingia mpaka kitandani. Hata kama si mwanga wa nje, basi anayo mitambo yake italeta mwanga mzuri tu, kama wa jua, kumfanya aamke. Sasa Koku alitoa yote hiyo, kila Zenda akifungua macho akiona giza, anajua muda wakuamka bado, basi anarudi kulala.

Maisha!

Bale aliamka siku ya pili akabaki akijifikiria na kukumbuka mbali sana. Akasikia kulia kwa uchungu sana. Siku ya jana ilipita kama siku nyingine zote, wakati haikuwa hivyo mwanzo. Akakumbuka maisha aliyokuwa akiyadharau nyumbani kwao, lakini siku kama ya jana, ya krismasi walivyokuwa wakiisherekea nyumbani kwao. Hapakuwa na makuu sana, lakini lazima wangekuwa pamoja. Na yeye angepika, wakasifia chakula chake kisha kukaa na kuanza kuchokozana na Naya. Bale akalia sana.

Akamkumbuka mdogo wake. Mtoto aliyekuwa hana hatia. Mpole sana Zayoni. Hana ugomvi na yeyote! Akaumia sana kuona amemtoa duniani kwa hasira tu. Akajiangalia alipo na alichonacho, akazidi kulia. Akatamani yale maisha aliyoyaona ni ya kifukara aliyomudu kuwapa baba yao, wakati yeye na mama yake wakiyalalamikia bila kuyaishi, akatamani hata yangerudi kwa siku moja, siku kama ya jana yake, akayaishi. Lakini ameishia peke yake! Akiwa na kila kitu anachotaka, mpaka usafiri ni kiasi cha kuita tu, dereva wa Joshua anakuja kumpeleka atakako, lakini ameishia kuwa peke yake. Kijinyumba cha kifahari na thamani nzuri haswa ndani, lakini hana mtu!

Akawaza na kujifikiria akabaki akilia sana. Mara simu ya Joshua ikaingia. Akashituka sana mpaka akakaa na kupokea. “Ulikuwa na sikukuu nzuri?” Bale akajikuta analia sana. Joshua akanyamaza tu. “Nimekumbuka sana familia yangu Joshua. Najuta. Natamani siku zirudi nyuma angalau nirudi kuyaishi yale maisha. Lakini nipo mpweke sana.” “Hiyo hali unaweza kuibadili Bale. Usikae ukajifungia peke yako. Kama mguu hauna maumivu, toka. Nenda katembee au hata nenda mazoezini. Unayo pesa yakutosha tu. Jiandikishe gym, kwa muda wako nenda kafanye mazoezi ambayo unajua ni salama kwako.”

“Rudi kanisani. Tumia kipaji chako. Yapo makanisa mengi sana yanatafuta watu wenye kipaji kama chako. Weka akili zako huko kuliko nyuma. Huna utakalobadili nyuma, ila unaweza kutengeza maisha mengine na ukajipatia watu.” Joshua akaendelea taratibu tu.

“Nakumbuka na wewe ulikuwepo nilipowapa historia ya maisha yangu. Bale, mimi nilibakishwa peke yangu kwenye hii dunia. Sikuwa na mtu, ndugu wote walinikataa. Lakini huyu Mungu!” Joshua akatulia kwanza. “Aisee Mungu yupo Bale. Naye ni halisi. Nikikwambia ni baba wa yatima, si yatima mmoja. Ni WOTE. Mkubali. Mpe jukumu la kuwa Baba yako, uone atakavyobadilisha historia yako. Si kwamba utasahau! Mimi sijawahi kumsahau mama yangu. Lakini hata katika huo wakati ananitumiaga faraja aisee.”

“Huyu Mungu aliyejitamblisha kwangu na nikamkubali, amenipa vingi vya thamani mpaka namshangaa. Mimi Joshua, amenipa mwanamke kama Naya! Huyu Mungu ambaye ni Baba yangu amenipa familia ya kina Magesa wamekuwa ndugu ambao ni zaidi ya ndugu wa damu! Amenipa Geb ambaye sijui nikwambie nini Bale! Amefungamanisha mioyo yetu, lake ni langu, langu ni lake. Sina jinsi nikawa kwenye shida na yeye asiwepo na mimi. Iwe mchana, iwe usiku, hakuna mipaka kwetu. Tunabebana kwa hali zote mpaka magotini. Lakini haya ungeniambia kipindi nahangaika kutafuta malazi, chakula na KUKUBALIKA na watu, nisingeamini. Lakini nilipita, na amenibariki tena. Au zaidi. Ila nikiwa ndani yake, NIKISUBIRI.” Hapo akaweka msisitizo.

“Hakuna mzuri wa kusubiri. Lakini ahadi zake ni kweli na amina. Nabii Isaya Anasema, wale wamngojeao Bwana, watavikwa nguvu mpya.” Akamsikia akicheka kwa kuhamasika. “Yaani hizo nguvu mpya utakazovikwa, zina ahadi ya kupaa juu kwa mbawa kama Tai! Acha tusome wote Bale. Unayo bibilia?” “Nilinunua mpya, lakini nashindwa kusoma kabisa Joshua! Naona kama…” Bale akasita.

“Basi leo iwe mara ya kwanza. Chukua, kisha fungua kitabu cha Isaya 40 anzia mstari wa 29 soma kwa sauti mpaka 31.” “Nisubirie kidogo nikaitafute.” “Bila shaka. Huu ni muda wako.” Bale akatoka kitandani kwenda kuifuata upande wa sebuleni. Akakaa hapo hapo kwenye kochi na kuanza kufungua, Joshua akimsubiria.

“Nitasoma.” “Anzia mstari wa 29 tafadhali.” Joshua akaongeza. “Inasema, 29. Huwapa nguvu waliolegea na huongeza nguvu za wadhaifu. 30. Hata vijana huchoka na kulegea, nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka, 31. Bali wale wamtumainio Bwana atafanya upya nguvu zao. Watapaa juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio wala hawatachoka, watatembea kwa miguu wala hawatazimia.” Akamaliza kusoma na kutulia kabisa akabaki akifuta machozi. “Hivi umesikia lakini Bale?” Joshua akauliza akicheka kwa hamasa.

“Yaani huyu mwenye enzi yote, anayo ahadi kwako asubuhi ya leo, kukupa wewe nguvu, endapo tu kama utamtegemea. Mpaka vijana na wote unaodhania wewe wanaweza wasichoke, basi upo wakati wanaweza wakachoka lakini kama wewe ukiweka tumaini lako kwake, anaahadi ya kukupa nguvu. Na si nguvu za ugali? Hapana. Zinazidi. Kwamba wewe utapaa juu kwa mbawa kama tai. Kwamba hata ukikimbia hutachoka. Ukitembea pia hutazimia! Akupe nini huyu Mungu zaidi ya hivyo?” “Kweli hamna.” Bale mwenyewe akakubali.

“Basi anza upya Bale. Kila ukisikia kuchoka, soma hili andiko. Na MSUBIRIE yeye Mungu. Lakini ukiwa unafanya anachokuagiza. Anza kwa kuishi hayahaya maisha uliyo nayo SASA. Acha kujihurumia. Mabadiliko yote yatakutana na wewe njiani. Iwe mguu mpya au chochote Mungu atakachotaka kukupa, basi kije kukutana na wewe ukiwa umeshaanza. Yaani upo njiani. Sio umekaa ndani.”

“Wewe ni zaidi ya huo mguu. Usikwame hapo Bale. Uwe na mguu wa pili au la, wewe ni zaidi ya hivyo. Unavipaji vingi sana. RUDI kanisani, endelea kutumika. Utaona jinsi hata akili yako inavyoanza kufikiria mengine zaidi ya ulivyo na ulichofanya. Maana wewe na shetani bado mpo sehemu ambayo Mungu alishakutoa huko na akaondoka huko muda mrefu sana. Usikubali kukaa huko akili zako zinapokurudisha. Songa mbele.” “Nashukuru Joshua. Nitatafuta kanisa.” “Na gym. Anza mazoezi. Itakusaidia kutokaa ndani muda mrefu na kujihurumia.” Akamtia moyo na kuagana naye.

Chachu Ndogo, Huchachua Donge Zima

Lile neno likainua ari mpya ndani ya Bale. Na Joshua akawa ameweka wazo aliloona akalifanyie kazi bila kuchelewa. Akapata kifungua kinywa, akatoka na magongo yake wala hakutaka kuita dereva. Kwa mara ya kwanza akaamua aanze kuishi vile alivyo bila aibu au utofauti. Akatembea kwa magongo yake kwa makini mpaka kituo cha daladala. Akasubiri daladala mpaka ikafika na kupanda. Japokuwa hakupata nafasi ya kukaa, lakini akajisikia kana kwamba amefanya jambo fulani la ushindi mkubwa. Huo nao ukawa mwanzo mwingine aliojipongeza.

Safari ikawa ni kwenda kutafuta gym. Bale mtoto wa jiji, alishauza bangi kila mtaa wa jiji, alijua ni wapi aende pakumfaa. Safari ikawa mpaka Sinza. Akaingia kwenye moja ya gym aliyoona ni karibu na barabarani. Alikuta watu wachache. Akazungumza na mtu wa mapokezi, akakamilisha taratibu zote, pesa ipo, haina shida. Akaweka mambo sawa, akaingia sehemu ya mazoezi. Akaanza mazoezi kama anayofanyiwa hospitalini, lakini akajiongeza kwa umakini asije jiumiza. Akafanya ya chini, akaja juu sasa. Hapo alifanya mazoezi ya kifua na mkono mpaka kifua kikafunguka na mwili ukasalimu amri.

Alitoka hapo ameloa chapachapa. Akaona apande tena daladala kurudi kwake asiite usafiri ili tu kujichanganya na watu.

Mwenda Bure Si Sawa Na Mkaa Bure.

Wakati anatembea kuelekea kituoni akasikia mtu akimuita jina lake lakini kama ambaye hana uhakika vizuri. Akasimama na kugeuka kwa tahadhari. Akacheka alipomuona Vai.

“Nilihisi tu utakuwa ni wewe. Una urefu wako wa tofauti. Ila nikahofia nisije kujichanganya. Unafanya nini huku?” Bale akacheka. “Nilikuwa gym, ndio narudi nyumbani. Nafuata daladala.” “Unauhakika!? Huogopi kusukumwa na kujiumiza tena?” “Sasa wewe nesi gani unanitisha!” Vai akaanza kucheka.

“Mimi sitaki uanguke tena bwana! Vipi lakini?” “Safi tu. Mbona upo huku na sikukuu hizi?” “Nipo chuo. Nimegoma kuondoka. Ila nimetoka kwa msusi wangu. Alijaza sana kipindi cha sikukuu. Kila mtu anataka apendeze siku ya sikukuu. Sasa kwa kuwa mimi sikuwa na pakwenda, tukakubaliana ajiingizie pesa kwanza. Pakitulia, mimi ndio iwe zamu yangu.” “Sasa kwa nini hujasheherekea sikukuu kama wengine?” “Kuna professal anajidai hana kitu chakufanya ila kutuhenyesha. Amesema tarahe 28 mwezi huu wenye sikuu nzuri tupu na tarehe 2 mwezi wa kwanza, anatoa mitihani. Sasa mimi kichwa changu ni chakusoma tena, na tena. Halafu kurudia TENA.” Bale akawa anacheka.

“Nikajua nikienda tu kula sikukuu, nitarudi sina kitu kichwani, ndio mwanzo wakurudia mwaka ambao sina tena maishani.” “Nakumbuka hayo maisha.” “Wewe ulisoma wapi?” “Hapo chuo kikuu cha Mlimani. Hayo uliyosema ni kawaida sana tu. Sasa ushasoma TENA?” Akarudia kumuigilizia ‘TENA’ yake ya mwisho. “Niringe! Nipo kwenye ‘tena’.” Bale akacheka akimwangalia.

“Umependeza sana Vai.” “Wewe mwenyewe umependeza. Umenyoa vizuri! Vikaendana na sura yako. Nikataka kukusifia, nikajionya. Ila asante. Huwa nampenda huyu dada, anajulia bichwa langu.” Bale akabaki akimwangalia na kucheka. Vai alionekana mzungumzaji. “Acha mimi nikatafute chakula, nile ndio nirudi chuoni. Nimefurahi kukuona Bale. Na swala la mazoezi ni zuri sana, ila kuwa makini bwana.” “Umechoka kuniokota?” “Niwepo sasa! Nisipokuwepo na unavyojua kukataa kwa ukali vile!” Bale akacheka sana.

“Wewe kuwa makini. Mchana mwema. Nisikuweke juani muda mrefu.” “Unaenda kutafutia chakula wapi?” “Mtaani tu.” “Basi twende ukale kwangu. Nilipika chakula kingi sana jana. Cha kisherehesherehe. Nikaishia kukiweka kwenye friji na kushindwa kula kabisa.” “Kwa nini tena!? Au mapishi mabaya?” Bale akacheka tu na kubaki akifikiria.

“Sitapigwa huko au kuunguzwa na maji ya moto?” Akamtoa mawazoni na hayo maswali. “Usiogope. Nipo peke yangu, halafu naishi nyumba inayojitegemea. Karibu.” Vai akafikiria na kuona haina shida. “Ila tuchukue bajaji bwana! Mimi njaa inauma sana. Daladala itatuzungusha sana.” “Basi tujiongeze kabisa, tuchukue taksii ili tusiharibu nywele zako.” Vai akacheka sana. Hapo wakakubaliana. Wakasimamisha usafiri, wakapanda. Bale akamuelekeza dereva. Ilikuwa si mbali. Mwenye taksii akapita njia za mtaani, wakafika.

    Vai akashangaa sana madhari anayoishi Bale. “Pazuri!” “Asante. Karibu ukae wakati nakuandalia sahani yako.” “Wewe huli?” “Wakati unakula, naenda kuoga kutoa jasho.” “Sasa si unielekeze nipashe wakati ukioga?” “Sawa kama hutajali. Nilidhani mgeni siku ya kwanza.” “Lakini kweli. Samahani kwa haraka.” Vai akaona aibu na kujisikia vibaya.

“Hapana. Si kwa nia mbaya. Mtu mwingine angeogopa hata kusogea. Ila kama wewe huna shida, endelea tu. Kila kitu kipo kwenye friji. Upande wa jiko ule pale. Hakuna kilichojificha.” “Acha tu nikusubirie Bale. Nimejisikia vibaya! Nimejiona nina kiherehere.” Bale akacheka sana. “Acha hizo bwana Vai! Wewe endelea tu.” “Mmmh! Acha tu nikusubiri.” Akajirudisha kabisa kwenye kochi na kupoa, Bale akamtizama na kuelekea jikoni. Akatoa kila kitu na kuweka juu ya meza.

    “Njoo nikuelekeze jinsi ya kupasha.” Vai akanyanyuka taratibu kama aliyeishiwa ujasiri. “Mimi napenda sana kupika, na mazingira ya jikoni huwa napenda kuyapangilia. Hutapata shida kupata chochote unachotaka. Mabakuli ya kupashia yapo kwenye kabati hili. Vyakupakulia vuta droo ile pale. Sahani hapa, vijiko kwenye droo hii. Chagua chakula chochote unachotaka. Weka kwenye sahani, weka kwenye microwave, funika na mfuniko upo ndani ya microwave ili isichafue microwave. Vinywaji vipo kwenye friji. Chukua utakacho, kula. Jisikie huru, kama upo nyumbani. Mimi nitarudi muda si mrefu.” Bale akaondoka na kumuacha Vai amesimama hapo.

    Alichofanya Vai ni kupasha vyakula sahani mbili. Akaandaa meza na kubaki akimsubiria Bale. Akatoka akionekana msafi. “Sijajua unataka kunywa nini. Mimi nimependa hii juisi ya embe. Hii glasi ya pili.” “Basi acha na mimi nichukue hiyohiyo.” “Sasa si unitume mimi?” “Usijali. Wewe kaa tu.” Bale alishazoea kujitumikia hapo ndani. Alishaona sahani mbili, akajua amemuandalia na yeye. Akarudi na jagi zima.

    “Nashukuru kuniandalia na mimi sahani yangu.” “Nimeweka tu hata sikujua ungependa kula nini! Ila nikajiambia maadamu ulipika mwenyewe, hutakuwa na shida ya kula chochote.” “Nashukuru.” Wakakaa hapo mezani, na kuanza kula taratibu. Vai akashangaa ubora wa kile chakula.

    “Nilijiambia muonekano unaweza kuwa tofauti na ladha. Kumbe ladha imepita hata muonekano! Hutawahi kula chakula changu, Bale.” Bale akacheka sana. “Hujui kupika?” “Labda kuchemsha.” Bale akazidi kucheka, akamkumbuka Naya.

    “Dada yangu naye alikuwa hajui kupika kabisa, halafu hapendi. Lakini nilikuja kuona alifundishwa na mama, mpaka akaweza kutoa chakula kama hiki. Mama yetu yeye alikuwa akijua kupika sana. Halafu pia alikuwa mwalimu.” “Kumbe unafamilia! Sasa kwa nini hukuwa nao jana?” “Niliua familia yangu, Vai.” Vai akamwangalia na kutulia akifikiria. Akajikaza kuuliza. “Unamaanisha nini kuua?” “Kwa kuwachoma moto.” “Ndio maana ulisema unahisi unamkosi unao kataa kuondoka?” “Mbona hujashituka!?” “Kwa sababu na mimi niliua sana Bale. Najua kukosa. Najua adhabu ya kuua. Najua.” Wote wakabaki kimya kama waliorudi kwenye enzi zao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ipi Historia Ya Vai?

Nini Kitatokea? Jelini Yupo Njiani Kwenda Kum Surprise Zenda Aliyekuwa Bado Amelala Na Zilipendwa Wake. Koku Atafanikiwa Kuondoka Kabla Jelini Hajafika?

Nani Atakuwa Suprized?

Usikose Muendelezo. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment