“Viliwekwa wapi?” Akajikaza na kuuliza. “Inavyosemekana, kwa kuwa hawakujua chakufanya nayo, walizika hapohapo kwenye shamba lake.” Joshua akaumia sana. “Nashukuru kwa tarifa. Basi hiyo tutaongezea tutakapokwenda kuwaona wazazi wake. Tafadhali nitumie hiyo orodha ya mali zake mapema. Na sehemu sahihi walipomzikia, ili ndugu zake wafahamu.” Wakawekana sawa, wakaagana. Joshua akabaki akifikiria.
Akufaae Kwa Dhiki.
Mara simu yake ikiwa
bado mkoni ikaanza kuita na kumtoa mawazoni. Akaingalia na kuipokea kwa haraka.
“Huwezi amini, nilikuwa nikikufikiria sasahivi! Yaani
simu bado ipo mkononi nilitaka kukupigia.” “Kwema?” Geb akamuuliza. “Nimepata taarifa juu ya mali za Malon, na walipozika mifupa
yake.” “Daah!” Geb akasikika akisikitika. “Lakini
bora tutakapoenda kwao, tukiwa na hizo taarifa. Si faraja, lakini angalau
watajua jinsi ya kutunza kumbukumbu yake.” “Sijui kwa nini nimeumia, Geb!”
“Hakuna jinsi ya kujifaraji kwenye lililompata hata kama alitukosea
sana. Bado alikuwa kijana, na ni roho ambayo sina uhakika kama Mungu alijishindia.
Itakuwa imepotea hivihivi!” “Nafikiri hilo ndilo linaloniuma zaidi. Alikuwa
akifanikiwa vizuri sana kwenye mambo mengine yote, lakini shetani aliamua kukamata
roho yake. Sijui bwana! Mimi naona tulimalize hili, niachane naye kwa amani.”
Geb akabaki kimya akifikiria.
“Nafikiria
jumamosi nikitoka kazini, ndio twende Moro, nyumbani kwao. Unaonaje?” “Mimi
sina neno. Nipo tu. Wasiwasi wangu ni Naya ambaye ni muongoza msafara na hali
yake. Unafikiri sasahivi ni wakati muafaka kufanya hivyo?” “Nimeshazungumza
naye na nimemuweka sawa. Hana neno. Yeye ndiye aliyekuwa akisimamia hata
ukarabati wa ile nyumba ya Malon ya Kunduchi. Amefanya kwa moyo tu ili wazazi
wake wanufaike. Anasema japokuwa Malon alikuwa mbaya sana kwa wengine, lakini kwao
alikuwa akitegemewa sana. Ni kama yeye ndiye aliyewainua kwao wote.”
“Daah!”
Geb akabaki kuhuzunika. Wakakubaliana aina ya watu wa kwenda nao huko kwa kina
Malon. Mpaka Polisi waliokuwa wakifahamu utekaji nyara wake, wakawaomba
kuongozana nao wasije kufika kule, wakageuziwa wao kibao.
Kuliko Mwagika Maji.
Akampigia simu na
Bale kumueleza walipofikia. “Nikikwambia najutia kila
kitu, unaweza kuniamini Joshua?” “Mimi ni mtu wa mwisho kabisa kuwa na wasiwasi
naye, Bale. Nilikwambia tokea mwanzo na sitaacha kukukumbusha. Wamuhimu
sana ni Mungu. Kaa sawa na Mungu, utabaki salama.” “Lakini natamani kukusikia
unaniamini Joshua!” “Itakusaidia nini Bale? Maana hata nikikuamini au nisipo kuamini,
Mungu wako yupo na wewe. Anakutafuta wewe mchana na usiku. Inamaana wewe
ukikaa sawa na Mungu, hata mimi nikikupinga, haitasaidia. Tafadhali
naomba hilo ukumbuke Bale. Katika kila unachofanya na kuwaza
kuanzia sasa, jiulize swali unalohangaika kuniuliza mimi, kama je, Mungu yupo
sawa juu ya hilo? Hilo ndilo la msingi. Utashangaa sana jinsi atakavyoweka
mambo mengine sawa. Tafuta kwanza ufamle wake na haki yake,” “Mengine yote
mtazidishiwa.” Akamalizia Bale mwenyewe.
“Umemaliza.”
“Ila nina hofu sana. Sijui ndugu zake watanifanya nini wakijua kama…” Akasita. “Umemuua ndugu waliyekuwa wakimtegemea sana?” Joshua
akamalizia, Bale akabaki kimya. Safari hii akashangaa Bale hajajitetea kabisa
akitoa sababu ya kumuua Malon kama alivyoua familia yake na kumlinda
naye na Naya. Akapoa kabisa bila kujitetea. Joshua akajua ameanza kubadilika.
“Nalo hilo
ni moja ya jambo nililotaka kukwambia maana lilitushangaza hata mimi na Geb.
Sijamuhonga mtu wala Geb hajapindisha mambo, alichofanya alitumia askari
walewale tuliowatuma mwanzo kukutafuta ulipokuwa umejificha kwa Malon, kwenda
kuchukua taarifa kamili juu ya Malon huko Mbeya. Maana ilikuwa ngumu mimi na
Geb kuamini kama kweli uliua. Ndipo wakarudi na ripoti kutoka kwa polisi
wenzao ambao na wao walichukua ushahidi kutoka kwa wanakijiji pale na mmoja wa
mfanyakazi wa Malon aliyeenda kuripoti juu ya uharibifu aliokuta kwenye mji wa
Malon.”
Bale akashituka sana akikumbuka jinsi alivyoweka mipango yake ya mauaji akimtoa
Mbaki pale ili amchome moto Malon. Akajua kwa hakika ni Mbaki ndiye
aliyezungumza na Polisi. Je, hakumtaja? Akabaki akiwaza kwa hofu kubwa na ndipo
akakumbuka Joshua anazungumzia hilo akarudisha akili hapo kwa haraka ili kutaka
kujua Mbaki alisema nini!
“Mmoja wa
wafanyakazi wake anayesemekana alikuwa akiishi hapo alisema walikuwa na tatizo
la shoti ya umeme kwa muda mrefu hata Malon alikuwa akijua na kujipanga
kutafuta fundi wazuri kufanya wiring upya kwenye hilo eneo. Kwa hiyo akasema
anahisi walipata shoti mbaya na kuunguza eneo zima mpaka kifo cha Malon. Kwa
hiyo hiyo ndio taarifa waliyoikuta huko, na ndiyo wanasema watakwenda kuwasomea
wazazi wa Malon.”
“Sasa mimi
sijui Mungu wako amefanyaje! Maana wale polisi wamesema wataeleza hata sababu
ya kujua kifo chake ni juu ya uhalifu alioufanya. Alikuwa akitafutwa na polisi
kwa kosa la kuteka nyara mke wa mtu, ndipo wakakutana na taarifa za kifo chake.
Kwa hiyo hayo mengine, mimi sijui. Ninachokwenda kufanya ni kuhitimisha
maswala ya Malon. Nina uhakika mama yake anayo haki yakujua kilichompata kijana
wake. Atakuwa kwenye mateso akitafuta kujua alipo mwanae.” Bale kimya.
“Kilicho
kikubwa japo si faraja, ni angala nimepata mpaka ushahidi wa mifupa yake ilipo.
Acha nikamalizane nao. Niwakabidhishe mali zake zote, na baadhi ya mifupa yake.
Nimtoe kwenye maisha yetu kabisa.” “Nashukuru Joshua. Asante hata kukarabati
nyumba ile ya Kunduchi. Nilipita pale, kwakweli umefanya kazi kubwa.” “Ni Naya
huyo. Alitaka kuiweka kwenye muonekano ambao hata ndugu zake wataipokea nakuona
ni kitu cha thamani si pagala kama ilivyokuwa.” “Basi nifikishie shukurani
zangu kwa Naya.” “Hapana Bale. Nilikwambia mimi sitakuwa katikati yako na Naya.
Muombe Mungu aingilie kati mahusiano yetu. Ayaponye, siku moja uje umshukuru
mwenyewe.” “Nimeelewa Joshua.”
“Vipi mguu
lakini?”
Joshua akabadili mazungumzo. “Nilianguka vibaya,
nikatua kwenye kovu lenyewe, nikajiumiza tena. Hapa nipo kwenye kutibu tena kidonda.”
“Aisee pole sana Bale. Pole. Kwa nini hukuniambia!?” “Ahaaa! Naona kama ni
adhabu ambayo nastahili kuipata. Acha tu niteseke mpaka Mungu mwenyewe aweke
kikomo. Pengine amekusudia nisirudi kuja kutembea tena.” “Huo ni uongo wa shetani na usikubali. Mungu sio kama
sisi wanadamu. Hayupo kwenye kukuadhibu. Yeye mwenyewe analipa garama ya kuwa
na mahusiano na sisi. Yaani kabla wewe hujataka kuwa na mahusiano naye, yeye
anabisha hodi akisubiri ufungue mlango, aingie.” “Unajua ilikuwa ndio nakwenda
kujaribisha mguu siku nilipoanguka?” Joshua akamuhurumia sana.
“Aisee pole
sana Bale. Usikate tamaa. Uguza kidonda ukijua ni ajali kama ajali nyingine tu.
Mungu wako yupo na wewe. Nina uhakika anakuwazia mema zaidi ya akili zetu
zinavyoweza kufikiria. Utapata mguu na utarudi kutembea kama zamani. Vuta
subira.” “Nakushukuru Joshua. Asante sana.” “Aisee usinyamaze Bale. Ukiwa na
shida yeyote ile, usiache kusema.” “Hivi unavyonisaidia inatosha Joshua. Una
mambo mengi sana, sitaki na mimi niwe ajenda ingine.”
“Ni kweli,
mambo ni mengi. Lakini familia kwanza. Wewe ni familia. Usiugue peke yako.” Ikamfariji sana
Bale. “Nashukuru kujali.” “Anytime. Uwe na wakati
mzuri. Nitakujulisha kilichoendelea kwa kina Malon, tutakaporudi.” “Sawa.”
Wakaagana.
Uchungu Wa Mwana, Aujuae Mzazi.
Siku ya jumamosi
Joshua ni kama alichungulia tu kazini na kumuachia maagizo yote Jema. Dhamana
aliyokuwa amepewa Jema na Joshua, ikawa ni kama akizungumza Jema, basi ujue ni kama
mdomo na sikio la Kumu. Aliheshimika sana Jema.
Mida ya saa tano asubuhi
msafara wa Morogoro nyumbani kwa kina Malon ukaanza wakisindikizwa na hao
askari waliokuwa wamebeba taarifa za kifo cha Malon. Naya akiongoza njia.
Akisindikizwa na familia ya Geb. Nikimaanisha mama G, Nanaa na Joshua. Wote
walikuwa kwenye gari moja, kama kawaida, Geb ndiye dereva. Wanawake hao walikaa
kiti cha nyuma maongezi yakiendelea mpaka mji kasoro bahari.
Mama yake Malon
alipomuona tu Naya na umati wa watu, akaanza kulia. Wakashangaa maana hawakuwa
hata wamezungumza kitu. Walikaribishwa tu sebuleni, wakaambiwa anakwenda
kuamshwa ndipo akatoka na kuwakuta, akaanza kulia kwa uchungu sana. Akalia kwa
muda, kisha akatulia kidogo. “Nilikuwa naumwa Naya
mwanangu. Najua unamjua Malon. Kwa vyovyote alivyokuwa, hata akiwa anaishiwa
mpaka mwisho, basi hataacha mawasiliano na mimi. Hiki kimya cha muda mrefu,
nilijua kabisa hayupo kwenye dunia niliyopo mimi. Nilijua kwa hakika. Ila
sikujua watanifikiaje kuniambia.”
“Pole mama. Ningewahi
kuja kukwambia lakini na mimi aliniteka nyara, mara tu baada ya kumzika
baba. Akanifungia mahali na kunitesa sana. Alikuwa akinipiga kama mnyama
mpaka nikapoteza fahamu kabisa. Sikuwa nikijua mimi ni nani na wala nilitokea
wapi. Nilipoteza kumbukumbu kabisa. Na hawa ni moja ya polisi waliokuwa
wakinitafuta.” “Na kumtafuta na yeye mwenyewe Malon. Tulijua alipo ndipo
atakapokuwepo Naya. Maana alishatoa vitisho vya kuja kumdhuru Naya.” Akaongeza
mmoja wa wale polisi waliokuwa kwenye msafara. Wakazidi kulia. Zaidi mama yake.
“Hatuna nia ya
kuwaumiza zaidi ila ninataka kuwaambia sababu ya kutowafikia kwa haraka. Ni
mimi tu ndiye niliyekuwa nikipafahamu hapa na sikuwa nikijitambua kwa muda
wote. Nilikuwa kwenye matibabu na yeye akitafutwa mpaka taarifa zake
zilipopatikana. Wakawa hawajui jinsi ya kuwafikia kuwapa taarifa za kifo chake.
Lakini hawa ni polisi walio na taarifa zake kamili. Naomba uwasikilize.”
“Naya
mama, najua mwisho wako na Malon haukuwa mzuri. Lakini naomba umsamehe na ujue
katika wote, wewe alikupenda sana. Sema tu alikuwa ameshaharibika. Mtu
asiyejua jinsi ya kuishi na watu au hata kutunza upendo wa kweli. Ila Malon alikupenda
sana Naya.” “Sana.
Hakuna anayemjua Malon asijue wewe ndiye uliyekuwa kipenzi chake. Katika yote,
na wote. Naona nyinyi wawili. Wewe na mama yake ndio mlifanikiwa
kupendwa na Malon. Ni hivyo tu kama alivyosema mama yake, Malon aliharibika
zamani sana. Hakujua jinsi yakuishi katikati..” Mzee
Seduki akaongeza na kukwama. Wakamuona ameinama kwa simanzi mkewe akazidi kulia
kwa uchungu sana.
“Naya,
naomba umsamehe mwanangu.” “Mimi nimesamehe mama. Wala huna haja yakupiga magoti. Na
hata nimemsaidia kukarabati ile nyumba yake ya Kunduchi. Kwa sasa ni nzuri
kabisa inaweza kukalika.” “Nashukuru kama
umemsamehe.” Huyo mama alikaribia kupiga magoti akimuombea msamaha
mwanae, Naya akamuwahi.
“Mtakuwa na muda
niwaite ndugu zake?” Baba yake Malon akauliza. “Maana wote tulikuwa na msiba
usio na uhakika. Hapajawahi tokea ukimya mrefu kati ya Malon na mama yake.
Labda awe mgonjwa ndio hatataka kumwambia mama yake. Lakini kama yupo hai, na
hana uwezo. Basi ni bora akaibe, apate pesa yakumpigia simu mama yake.
Wote tulijua amekufa ila hatukujua jinsi ya kupata uhakika.” Wakaona wasubiri
tu.
Wakaitana ndugu,
baada ya masaa mawili nyumba ikawa imejaa ndugu. Na wao wakawa waungwana.
Hawakusema mengi mabaya ila juu ya kifo chake na kukabidhi waraka wa mali zake zote
na sehemu zilipo. Joshua akawapa funguo za nyumba ya Kunduchi. “Tafadhali
msidharau ile nyumba na eneo lilipo. Nipazuri sana. Nyumba inaweza kuwa ni ya
kawaida, lakini wazazi wangu, Malon amewaachia kitu cha thamani sana. Msiwe na
haraka kupauza. Na hakikisheni mnapata pesa nzuri sana endapo mtapauza. Ipo
sehemu nzuri sana.” Geb akawatajia kiasi cha pesa baada ya kumsikia Joshua anawaambia
hivyo juu ya hiyo nyumba. “Msiuze chini ya hapo.” Geb akaongeza msisitizo na
kuwashangaza zaidi.
“Jamani tunashukuru
kwa uaminifu wenu. Maana hata msingesema, sisi tusingejua.” Kaka yake mkubwa
Malon akashukuru wakati wengine wakiendelea kulia. Wakamshukuru Naya kuleta
msiba wa Malon nyumbani, ila wakasema watakwenda kuomba kibali ili wakafukue
kule alikozikwa, aje azikiwe nyumbani kwao.
Wakaondoka na
kuwaacha wakilia msiba. Ila na wao wakatoa rambirambi yao ya maana tu. Ni Geb
na Joshua. Pesa ipo! Wakapata nguvu ya
kuanzisha msiba ramsi. Wao wakaondoka kurudi Dar, wakawaacha na msiba kana
kwamba ndio umetokea. Huo ukawa mwisho wa Malon kwenye maisha ya Joshua.
Anarudi Dar akijisikia amani kwamba hana mpinzani tena kwenye ndoa yake.
Anahangaikia Maisha Yetu.
Wakiwa wametulia
njiani, simu ya Jema ikaingia kwa Joshua. “Kwema?”
Akamsikia akishangilia. “Usiniambie imepita?” “Imepita
Kumu, bosi wangu. Yaani sasahivi ndio nimekata simu. Walinipigia kunijulisha
sisi ndio tumeshinda.” “Yeess!” Joshua akashangilia. “Jiandae Bonus ya mwaka huu. Utafurahi. Asante sana Jema. You
are the Best.” Jema akasikika akipiga kelele. Kumu amesema! Akajua
pesa haitakuwa ndogo. Kumu akakata simu akicheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Huyu Mungu ni wa
ajabu aisee! Yaani amenituma kufanya haya yote tokea mwanzo nikiwa na mambo
mengi kweli. Nikakubali tu kutii lakini sikutaka kabisa muingiliano kipindi
hiki nilichokuwa na mimba yangu. Akili ilikuwa kwenye mambo mengine
kabisa. Nahangaika nisije haribu mimba, huku moyoni nasukumwa lazima
kukamilisha hili. Simu za yule jamaa kule Mbeya naye akiuliza vitu hata
visivyo maana zikawa hazikomi mpaka vikaoni!” Wakacheka.
“Kweli tena.
Unamwambia jambo asubuhi, mchana anapiga simu kuuliza jambo hilohilo mpaka
nikaona hatakamilisha! Sasa nikawa namwambia Mungu, kwani lazima iwe sasahivi?
Nikawa nampa mipango yangu sasa. Kwamba nikimaliza hili aliloniamini nalo tokea zamani, yaani kazi ya ajira aliyonipa,
basi nitafanya hili. Lakini wapi! Na nilikuwa na sababu zote, tena nzuri
tu, za kugairi. Kumbe mimi nahangaika na Yake, yeye anahangaika na
yangu!”
“Hongera Joshua
mwanangu. Japokuwa haikuwa kwa wakati wako, lakini umemtoa yule mama kwenye
kusubiri kwa uchungu. Maana angeendelea kulia msiba bila kikomo na
pengine angekufa asijue ukweli juu ya mwanae. Umefanya jambo zuri, kufanya yote
haya.” “Mpaka kurudisha na mali zake!” “Kabisa Geb. Si ungeachana naye tu kwa
mabaya aliyokufanyia? Ndio maana Mungu amekulipa. “Asante mama.” Wengine
nao wakampongeza.
“Kwani ni nini tena
Joshua?” Naya akamuuliza. “Mama Kumu!” Naya akaanza kucheka kama wengine jinsi
Joshua alivyomuita kwa hisia na kumgeukia kabisa. “Niambie Joshua mume wangu.
Ehe?” “Acha mama! Yule simba wa kabila la Yuda, amenguruma tena. Coca
watamsimulia Mungu wa Kumu mpaka wachoke.” Akaongea kwa ushindi kisha akageuka
na kuanza kuabudu kwa kuimba taratibu. Nanaa akamwangalia Naya, wakacheka. “Hapo
kafurahi kupitiliza!” Akamnong’oneza. Wakacheka, Naya akampokea kuimba.
Waliimba hao mpaka wanafika Dar.
Adui Wa Mtu Ni Wa Nyumbani Kwake.
Akiwa ofisini kwake
akapokea ujumbe kutoka kwa Kemi akimkaribisha nyumbani kwake. ‘Kwa mara nyingine tena, tutakuwa wote kama familia. Na Kevin
pia safari hii amesema hatakwenda kwa mama, atakuwa na sisi kama kuniunga
mkono. Tafadhali naomba usikose, dad. Pengine mume wangu akiona tupo pamoja na
yeye atarudisha moyo kwenye familia. Sipendi hivi wanangu wanavyokuwa katikati
ya ndoa kama yetu. Nimekusudia kurekebisha kwa garama yeyote. Tafadhali na wewe
niunge mkono.’ Kemi akatuma huo ujumbe akiweka na uzito wa ulazima wa kukutana,
akimtumia mumewe kama chambo akijua lazima mzee ataingia mtegoni tu ili
kunusuru ndoa ya mwanae.
‘Bila
shaka.’
Mzee akarudisha majibu. Kemi alipopata tu hayo majibu, simu kati ya mama na
wana zikaanza kutembea wakipongezana kwamba wamefanikiwa kumtia ndege mjanja tunduni.
Maana baba yao akisema jambo si mtu wa kigeugeu. Ikabaki kazi ya kumpanga Koku
tu.
Ilikuwa ni kawaida
yao kukutana nyumba moja na kubadilishana zawadi za krismas na kula na kunywa
pamoja. Huo utaratibu ukafa mara baada ya ndoa ya Kemi ilipoanza matatizo.
Ikawa wakikutana basi ni kesi zao wao tu, mpaka Zenda na Kevi wakaanza kutoa
udhuru. Kevin akaanza kwenda kusherehekea sikukuu za krisimas kwa mama yake na Zenda
kivyake. Sasa baada ya miaka zaidi ya mitatu kupita ndio Kemi akalianzisha
tena. Lakini si kwa ajili ya ndoa hata kidogo. Nia ni kumtoa Jelini kwenye
maisha yao.
Kila Mtu na Mtuye.
Tarehe 24 ya mwezi wa
12 siku moja kabla ya siku ya krisimasi, wakiwa wamekaa tu ndugu hao wanakunywa
na kula wakijiandaa na sikukuu hapo kwa mama yao, James akaingia majira ya saa
tano asubuhi. Jema alikuwa amejilaza tu kochini anabembelezwa na kibaridi cha
jiji la Kilimanjaro, mama zake wakiongea na kucheka wakati Jelini na Mode
wakitoa vitimbwi vya wanaume wa jiji.
Hakuamini kumuona
mumewe pale, tena mida ile. Akaanza kulia kwa furaha. “Jema naye!” “Mimi aliniambia hataweza kusafiri, sababu ya majukumu
mengi.” Jema akamjibu mdogo wake akifuta machozi ya furaha. “Usilie sasa!
Mimi nimekufanyia surprise wewe na mtoto, nataka mfurahi.” “Nimefurahi James! Nimefurahi sana, ila siamini kama
umenifuata mpaka huku kijijini! Sikutegemea!” Wakacheka.
“Karibu James
mwanangu.” “Asante mama. Nimekaa Dar, akili ikawa hainipi, nyumba haikaliki.
Chumba ndio kikawa kikubwa. Kila nikiingia chumbani nakumbuka Jema wangu
hayupo! Nikashindwa kulala. Juzi nikalala kwenye makochi.” “James!” “Kweli
mama. Nasikia upweke, halafu huruma kwake. Nikajiambia hizi pesa
zinatafutwa na hazijawahi kutoshea. Nikamfikiria Jema wangu, nikamuhurumia
na huyo mtoto aliyebeba na hawezi kumtua mchana wala usiku, mpaka Mungu
aamue kumtoa kwa wakati wake! Nikajaribu kulala havilaliki.”
“Saa sita usiku
nikampigia simu mama kumtaarifu nakuja huku kama kuna maagizo ya nyumbani basi
anipe. Wakaniambia Vai anamitihani baada ya sikukuu, hataki kuondoka chuoni.
Anasoma, anaogopa kufeli. Viola akaomba nije nae na mwanae waje kumsalimia na
wao baba. Nikaenda kuwachukua usiku huohuo na kuanza safari kumfuata mke wangu.”
“Shem anampenda
Jema!” Jelini akaongea kwa kuwatamania. “Sana. Nampenda Jema wangu. Hana makuu.
Huna utakachomwambia akabisha, ndio maana nimemuonea huruma, nikasema acha nije
nilee naye kidogo. Angalau kumpokea huyo mtoto kwa kumsaidia hata anitume tu,
apumzike.” Jema alifurahi sana.
“Ila sasa hapa sisi
tunaondoka. Jema anatakiwa kwenye mji wake. Baba amesema nije nimfuate
nimrudishe kwake. Tusikae huku.” “Jamani!” “Kweli. Ndio nimekuja hivyo na hata
kina Viola wanamsubiria.” “Mlikula mahari ya watu, muache kigugumizi hapo. Jema
anaenda kwao.” Mode akawakazia hukumu. Wakaanza kucheka. Ila Jelini na mama
yake wakasikitika sana. Walitaka wabakie pamoja hivyohivyo watatu mpaka
wanarudi Dar.
“Kesho basi
mkishatosheka hapa, mje na kule mjini tumalizie sikukuu pamoja.” James
akawakaribisha. Na kwa kuwa wanagari, wakaona sio wazo baya kujumuika nao. Jema
akasaidiwa kufungasha vya kwake, akaondoka na mumewe.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Jema amebahatika
sana aisee. Mwanaume mzuri, anapesa halafu anampenda kweli!” “Kabisa dada.”
Mode akadakia na kuongeza. “Wanaume wengine huu ndio ungekuwa wakati wao
wakufanya umalaya huko mjini kwa kuwa mke hayupo.” Wakamfanya Jelini aanze
kujifikiria. Ataishia wapi na yeye kwenye maisha! Akapoa, kimya akitafakari
mahusiano yake na Zenda. Anakila kitu, lakini Zenda si mume. Anayofanya James
kwa Jema, si garama ya pesa au mali, lakini akajua Zenda hawezi kuyafanya.
Kwanza kwa nafasi yake kwenye maisha na umri. Japokuwa ameonyesha kumpenda
sana, lakini hajawahi kuzungumzia hata kwa kuropoka swala la kuja kuishi pamoja
kama mke na mume au mtoto!
“Kwa hiyo Mode,
umeamini sio wanaume wote malaya?” “Nahisi ni huyo James tu. Wengine wote zipu
wazi.” Wakaendelea kuzungumza wakisifia ndoa ya Jema, Jelini kimya akijifikiria.
Mwishoe akajionya. “Lakini siwezi kupata kila kitu kwenye maisha.”
Akajiambia akijitia moyo. “Zenda ananipenda sana. Na kwake nina uhakika wa
kuwa peke yangu, sio kama malaya wengine. Acha nijitulize nisianze kuwaza makuu
ya kutunyima raha.” Akaendelea kujionya, ila tayari shauku ya kupata alichopewa
Jema na James ikawa imeshamuingia. Akapoa. Hilo nalo akakubali kulizika ili
atulie kwa Zenda.
Sikukuu!
Ikawa kweli ni siku
iliyo Kuu kwa wengi. Wengine kukumbuka ya siku ya kuzaliwa kwake
Yesu. Wengine wakisherehekea kuwa pamoja kama familia. Hakuna kazi wala shule.
Kila mmoja siku hiyo ikawa na umuhimu wake, kivyake, siku KUU. Ila kwa kina
Kasa ikawa ni siku ya mtego wao kufanikiwa. Roho mkononi. Jambo
lisiharibike, mzee anaswe.
Hiyo siku ikawa
imewadia Kemi akiwa ameandaa tafrija ya kitajiri haswa nyumbani kwake, kutokana
na hadhi yao. Baada ya misa wanayohudhuria ya kingereza kuisha, wote wakaelekea
nyumbani kwa Kemi wakiwa wanasubiriwa kutumikiwa kitajiri haswa. Kuanzia
matayarisho ya hapo kwake, meza ya chakula, wahudumia meza, wagawa vinywaji,
walikuwa wachache lakini wataalamu ambao wapo nadhifu mpaka tai kuendana na
madhari ya hapo. Ungefika hapo, ungedhani wahudumu na wao ni waalikwa. Safi.
Mume wa Kemi anafanya
kazi kwenye ofisi moja wapo ya Kasa kama kiongozi huko Shinyanga kwenye kampuni
ya madini. Analipwa mamilioni mengi mno na baba mkwe wake. Kitendo cha Kemi
kufukuzwa kazi, wala hakikutingisha uchumi wa familia, bali kiburi kilikuwa
kikimsumbua. Iweje yeye mwenye baba asiwe na kazi halafu mumewe ndio abakie
kazini akiheshimika na baba yake! Kosa ni Jelini.
Na hata Noah, mumewe Kemi
siku hiyo alikuwepo mjini kusherehekea sikukuu hiyo japo hawakuwa kwenye
maelewano na mkewe. Ni kama walibakia ndoa jina sababu ya watoto tu. Mzee
anafika hapo hana hili wala lile asijue shuguli nzima inamuhusu yeye. Hata Noah
mwenyewe hakuwa akijua mipango yao iliyojaa hila. Alikuwa kwake akijua safari
hiyo wanakutana tena kama ndugu, na yeye akiwa ameambiwa yake na Kemi akidanganywa
ili aje jijini kwa sikukuu, kumbe na yeye ni chambo tu ya kumuingiza baba mkwe
nyavuni.
Karibia na muda wa
chakula, maharage yakatiwa nazi, tena tui la kwanza. Kiungo kisichoongopa
kwenye pishi la maharage. Koku akaingia hapo, akiwa amependeza haswa. Kemi
akamchagamkia haswa akijua mambo yamekolea. Lakini chakushangaza hata kumuumiza
Koku mwenyewe ni mzee Kasa. Hata hakuonyesha kuna utofauti. Alinyanyua macho
baada ya kusikia kelele za Kemi akimchangamkia kisha kurudisha macho yake
kwenye simu na kuendelea kuchati na Jelini huko alipo, kana kwamba hamjui
kabisa Koku!
Mara kadhaa walimuona
akicheka na kutingisha kichwa akisoma jumbe kwenye simu yake, kisha anajibu.
Akawa busy na simu yake, kana kwamba hayupo pale kabisa kitu ambacho si cha
kawaida kwao. Wakazidi kukereka.
Ila mpania maji, lazima
ayanywe. Koku hakutaka kuonekana ameshindwa kirahisi kwa kiasi hicho. Kwanza
anajiamini vilivyo. Kwa sifa zote ya mazingira yao, yeye yupo juu sana. Halafu
eti leo aonekane amepuuzwa mbele ya macho ya watu wote! Hata kidogo. Akaamua
amsogelee. Akamsalimia kwa karibu kabisa ili kumtoa macho kwenye simu, naye Zenda
akawa muungwana, akamjibu na kurudisha macho kwenye simu yake.
“Sikujua kama upo mjini! Umekua kimya kweli!”
“Nipo.” Kwa mara nyingine tena, Kasa akawa muungwana, akatoa macho kwenye simu yake
aliyokuwa bado ameishikilia mkononi, na kumtizama akimjibu. “Nani anakuficha?” Koku akaendelea.
“Maisha tu.” Akajibu Zenda wazi akiashiria hataki kuendeleza naye yale
mazungumzo. Na kuweka msisitizo ili aelewe anamuingilia kwenye
anachofanya, akasimama kabisa. “Nitarudi baada ya muda mfupi.” Akaongea hivyo
na kutoka nje kabisa na kuwaacha hapo ndani hoi.
Kwa kuwa mume wa Kemi
hakuwa akijua kinachoendelea. Ilikuwa siri ya Kemi, Kevi, mama yao na huyo Koku
ambaye alisimuliwa yote juu ya Jelini. Akiwa anawajua wote hao watatu, kwanza hawapatani,
na yeye siku hiyo hakutaka maneno mengi nao, Noah akawa mtizamaji bila
kuchangia chochote, akaendelea kunywa zake pombe pombe kali. Akitaka baada ya
hapo awe amelewa vyakutosha, alale bila hata malumbano na Kemi. Akishinda hapo
kesho yake na vijana wake, siku inayofuata ananyanyua majeshi, anarudi
zake Shinyanga, kimya. Maisha yake yakaendelee huko kwa amani, akifanya yake
kwa uhuru wote.
Aliachwa Koku amesimama hapo kama amevuliwa
nguo hadharani. Dharau ya hali ya juu. Wazi alionyesha amemsogelea kumsalimia,
eti anamjibu kifupi na kuondoka kabisa! Koku akazidi kuumia na wivu kuzidi
kumsumbua maana aliambiwa na Kemi kuwa Jelini ni kama amehamia hapo nyumbani
kwa mzee. Mwanzoni Koku mwenyewe hakuamini kabisa. Maana yeye alikuwa akiitwa na
mzee anapojisikia hamu, tena mara moja moja. Yeye akiwa na shida naye
basi anamwambia, anaandaa mazingira, wanakutana na kufanya yao, kila mtu
anaondoka. Sasa kuja kusikia eti kwa Jelini mpaka anauguzwa! Hilo likamsumbua
sana ila akajikaza siku hiyo mbele ya Kemi alipomtafuta kumpanga rasmi kwa siku
hiyo, mpaka hapo alipohisi kudhalilika sana ndio akawa kama amemtibua na
kuamini alichokisema Kemi. Kuwa, LAZIMA waungane kumtoa Jelini. Ameshakuwa tishio
kwao. Morari na hasira vikampanda Koku.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Je, Ndio Wasomi Hao Wa Mjini Wamemshindwa Zenda?
Usikose Mikasa Ya Mpania Maji.
0 Comments:
Post a Comment