Maisha yakaendelea
Jelini akawa akiishi hapo huku akirudi nyumbani kwao kumtembelea mama yake na
mtoto. Zenda akienda kazini alfajiri, anaamka naye. Jelini anarudi nyumbani,
yeye kazini. Anapata muda na mwanae. Saa nane mtoto akirudi. Anakuwepo naye.
Zenda akitoka kazini, anakwenda kwa Zenda ndio mpaka kesho yake.
Taratibu maisha hayo
yakaendelea. Mapenzi mazito kati ya Zenda na Jelini, amani kati yao. Jelini
akamjulia Zenda, hampi sababu. Akajitenga na wanaume, akawa akichunga sana
nafsi yake hataki vishawishi na mwanaume yeyote yule kwani alijiambia Zenda
anampa kila anachokitaka. Na kweli, ungefika nyumbani kwa mama Jema, ungejua
wamefanikiwa. Mama wa kichaga alikuwa akimiliki kadi ya benki ya Jelini ambayo
Zenda anamwaga mihela humo, kama hana akili nzuri. Na yeye akajiweka akijua
kuna leo na kesho. Akaanza kujijenga kibiashara kwa kutumia pesa hiyohiyo ya
Jelini.
Jelini aligoma kabisa
kujenga awe na kwake. Alisema Jeremy amemzoea sana mama yake, hawezi kuwatenga.
Huna utakalomwambia Jelini akakubali kuhusu kuhama kwao japo uwezo amekua nao.
Basi huyo mama akaona isiwe shida. Akili kwenye biashara na kuimarisha nyumba
yake. Zenda alishawachimbia kisima cha maji, nyumba ikabadilishwa ikawekwa
madirisha ya vioo na vyuma vizuri sana. Vyumba vitatu vikafungwa AC, kiyoyozi
cha haja, starehe ya Jelini. Kupenda kulala patam. Chumba chake ndio ni kama
alikijenga upya. Pakawa pa hali ya juu kuliko hata chumbani kwa mama yake
asiyetaka makuu.
Marumaru za hali ya
juu mpaka nje kwenye ngazi. Kwa mara ya kwanza kukajengwa vitofali mpaka kwenye
geti ambalo na lenyewe lilibadilishwa sababu ya uzio wa aina yake uliojengwa
hapo. Usingekutana na vumbi kwenye huo uwanja, maana palipokuwa pameachwa bila
ujenzi, basi maua ya haja. Hapo mama
Jema akamuongezea kazi kijana wake wa bustanini. Kukawa safi. Nyumba ikawa ya tofauti
kabisa. Kufumba na kufumbua mama Jema maisha yakambadilikia.
Maombi yake ya pesa ipotee
njia yakatimia. Pesa ya Zenda ikakutana na ndoto za mama Jema alizokuwa akiwaza
kwa muda mrefu sana, lakini pesa ikawa tatizo. Kulea kuanzia Jema mpaka Jeremy!
Kidogo anachopata ni kwa wanae na mjukuu. Mtaji mkubwa, ikawa ni shida kupatikana.
Anadunduliza mchana na usiku, kibubu hakijai. Ndio sasa Jelini akamfuta machozi
kwa aina yake. Kadi akamkabidhi. Haulizi matumizi wala salio. Shoping anakwenda
na Zenda. Anafanya kukusanya anachotaka huko madukani. Mama yake akapelekwa shule
kabisa ya kujifunza udereva. Alivyo mpambanaji, haikuchukua muda, mama Jema akaingia
mtaani bila shida.
Yule mama Jema ambaye
Jelini alikuwa akimtania wakati mwingine amegombana na sidiria, sababu anaweza
akachomoka kwake na haraka, asivae sidiria. Basi Jelini akimuona hana mbavu. Utamsikia,
“Leo mama Jema mgomvi wako sidiria. Mshagombana!” Atacheka na kuondoka
hivyohivyo, hajali. Hapo kurudi ni baadaye na chakula. Sasa shilingi imepinduka.
Anaendesha Range. Mafuta yanawekwa bila kufikiria, Jema ndiye aliyekuwa
na kazi ya kuzunguka naye kumnunulia mavazi na vitu vya kumfaa maana Jelini
hana muda, analea penzi.
Mama Jema mchaga wa
mjini. Akili ya maendeleo alikuja nayo mjini, shida hazikuwahi kumfanya akasahau
ndoto zake. Alizitunza tu akisubiria pesa ipotee njia, iende kwake. Sasa
ikapotea njia. Bila kuchelewa, akajaa vizuri sana kwenye ulimwengu wake. Ungemuona,
ungekubali uzazi mzuri. Mambo hayakukawia maana ndoto zilishakuwepo, ila
uwezo ndio ilikuwa shida. Sasa ndio uwezo ukatoa zile ndoto kwenye uhalisia,
mimba haikuchukua muda kuzaliwa, watu wakashuhudia kwa macho.
Alipoona mambo ya biashara
ya mama yake yanachanganya, Jelini akajiunga naye kumsaidia. Mtoto akienda
shule, anatoka na mama yake kuwahi kwenye biashara. Mama ndiye akawa muendesha
mambo, akapata mtu wa uhakika wa kumtuma. Ikawa rahisi kwao kwa sababu Jelini
si mbishi hata. Kila akitumwa na mama yake anafanya japo pesa ni zake
kitu kilichomshangaza hata Jema na kushangaa huo moyo wake kila akisimuliwa na
mama yao juu ya Jelini.
Yaani yeye akawa kama
haadahiki na pesa kabisa wala hazimpeleki mbio. Hilo hata Zenda
aliliona. Huna mali utakayomtisha nayo na kumzuzua. Yeye neno lake ni sitaki
kukosa raha. Anataka kupendwa na kubembelezwa. Mwenyewe anasemaga mama Jema
hajawahi kumchoka yeye wala mwanae. Aliwatunza wote tokea wanatua hapa duniani
bila kulalamika wala kunung’unika.
Na Zenda hapo akaona
apoe. Akiwa na Jelini hawana mazungumzo mazito. Yeye Jelini anataka stori na
akae mikononi. Wacheke mpaka machozi. Hana habari na nyumba za Zenda wala mali
zake. Wakitoka kwenda mahali, utasikia vicheko vyao wakati wote. Jelini akizungumza
ujinga wake, Zenda akimsikiliza na kucheka mpaka akamfanya Zenda mfikiria
mazito wakati wote, wakati mwingine kuchukua likizo ya kufikiria magumu na
kuanza kufikiria kama Jelini. Machache yakuwafurahisha. Upendo ukatawala kati
yao, mimba ya Jema na Naya ikiendelea kukua.
Mtu Heteleza Asipotarajia.
Ilikuwa siku ya
jumatano, siku yake Bale ya mazoezi kama kawaida lakini safari hii akiwa na
tumaini jipya. Alihamishiwa kitengo cha MOI mahususi Joshua akitaka apate mguu
wa bandia, arudi kutembea kama zamani. Kwa hiyo mazoezi yakahamishiwa hapo, ili
kuhakikisha anapata mazoezi ya kutosha, kidonda kikauke kabisa, ajaribishwe
mguu. Siku hiyo Bale akashushwa na dereva, akashukuru na kuanza kutembea na
magongo yake ili kuingia ndani.
Bahati yake mbaya,
akajikwaa vibaya sana, alianguka na kutonesha mguu uleule ambao alikuwa
akifanyiwa mazoezi. Pakaanza kutoa damu. Aliumia roho! Akapandwa na hasira
nakushindwa kusimama akabaki amekaa hapo chini akiangalia ule mguu. Nesi mmoja mwanafunzi
akamkimbilia ili kutaka kumsaidia. Bale alikataa kwa hasira sana mpaka
akamsukuma, watu wachache wa pembeni walioona akianguka wakiwatizama. Yule nesi
akamtizama pale chini, akaona ajishushe. Akamsaidia kuokota magongo yake,
akamkabidhi. Bale akayapokea na kuyatupa mbali zaidi kwa hasira na kuzidi
kushangaza watu.
“Achana naye, Vai. Twende
zetu. Yeye si anajidai jeuri. Mwache.” Mwenzie yule nesi mwanafunzi akamwambia
kwa kukereka. Huyo Vai akabaki akimwangalia Bale pale chini alipokaa. Hapakuwa kwenye
udongo. Ni sementi ya barabarani, nje ya jengo la MOI. Kwamba ni kavu ndio
maana ikamkwangua mguu pale ulipotua tu aridhini.
Bale akajifuta machozi
na kuanza kusota yeye mwenyewe kufuata magongo. Kutambaa anashindwa, kwasababu
mguu ulikuwa ukitoa damu na hakutaka kuutonesha zaidi. Akawa anasota na matako,
mguu ule uliokatika, na kutoa damu amening’iniza juu. Kila alipokuwa akisogea,
machozi yalizidi kumtoka. Akasota mpaka akafikia gongo moja, jingine ikawa
ngumu. “Si wewe unajidai mjuaji? Sasa utakaa hapo juani mpaka ukome. Twende zetu
Vai.” Vai akabaki akimtizama. “Acha ujinga Vai na huruma zako za ajabu ajabu. Twende
zetu. Unamuhurumia nini? Yeye si hataki msaada? Mwache.” Vai akabaki akimtizama
Bale na gongo moja akijaribu kusimama, nakushindwa.
Jua la saa sita
mchana kali. Yupo chini, matako pia yakaanza kuungua. “Unahangaika naye wanini
huyo!? Mimi nakuacha.” Mwenzie akaondoka. Vai akaenda kumuokotea gongo la pili
akamuwekea pembeni yake bila kumkabidhi. Akalivuta. Ikaanza kazi ya kusimama
kutoka chini alipokuwa amekaa. Vai akamuona anaungua.
“Ninajua jinsi ya
kukusaidia mpaka ukaweza kusimama bila kujitonesha huo mguu zaidi. Nitasimama upande
ambao umeumia mguu.” “Sema ambao sina mguu.”
Bale akaongea kwa hasira. “Halafu wewe utatumia nguvu zako zote kwa mguu huo
mwingine. Ni sawa?” Kimya.
Vai akaenda kuinama
pale, akampa mabega. “Pitisha mkono unishike kwa nguvu zote, ukitumia mguu huo
mwingine kusimama, ili usiendelee kujiumiza.” Vai akainama akijua amemuelewa. “Nipe
hilo gongo moja nikushikie upande huu, ukiwa wima nitakukabidhi. Akamuelekeza kitaalamu
mpaka Bale akaweza kusimama. Akamkabidhi gongo lake.
“Asante.” “Karibu. Unaelekea wapi?”
Akajifuta machozi na kujaribu kufikiria na kuangalia alipo. “Nina mazoezi. Kwanza naona haina maana tena. Bora
nijiachie tu. Maana hata kama nikupewa mguu, inamaana siwezi tena mpaka kidonda
kipone tena.” “Mimi ni mwanafunzi tu. Leo nimepangiwa na
mwenzangu hapo kliniki. Nashauri twende wakakuangalie, bila ya kuishia njiani. Wao
ndio wataalamu wanajua zaidi.” “Unafikiri huu mguu
nilizaliwa hivi ndio nikaumia jana kwamba sijui ninachozungumzia? Najua maana wanashindwa
kunipa mguu wa bandia mpaka nipone. Najua kwamba siwezi kuvalishwa mguu wa
bandia mpaka nipone kabisa.” Bale akajieleza kwa jazba. “Na unategemea
kupona vipi endapo ukiondoka sasahivi na jeraha hilo jipya?” Vai akamuuliza
taratibu tu.
“Unajua unaweza
kusababisha madhara makubwa zaidi endapo hapo ulipoumia sasahivi hapata tibiwa?
Na kabla hujasema unazo dawa za kwenda kutumia nyumbani, nashauri usirudie
njiani sababu ya hasira. Wapo wataalamu wanaweza kukushauri vizuri. Ingia ndani,
ukawaonyeshe ulipojitonesha, wao ndio wakuruhusu. Usiishie hapa.” Bale
akakubali. Akaanza kuchechemea akiingia ndani. Kisha akageuka na kumtizama Vai.
“Nilishakushukuru.” Vai akacheka na kuondoka kwa haraka kama anayewahi sehemu.
Bale akaingia ndani,
akaenda kujiandikisha, akapewa namba. Ni hospitali ya taifa. Watu ni wengi,
yeye akapewa namba 67. Akatafuta mahali, akakaa akisubiria zamu yake. Alikaa hapo
mpaka kidonda kikakata damu. Ilipofika saa saba na nusu akamuona Vai
anamsogelea. “Vipi?” “Nimepata namba 67.” “Lakini wanaona wagonjwa kwa haraka
na wahudumu wapo wengi.” “Nimeona foleni inasogea. Namba 43 ameshaitwa.” Vai
akaangalia kulia na kushoto, kisha akapata kama wazo.
“Naweza kukusafisha
kidonda wakati ukisubiri. Kitakupunguzia nzi.” Bale alikuwa akishindana na nzi
hapo kwenye mguu wake. “Na hata ukimuona mtu mwingine, ni sisi pia ndio itabidi
kukusafisha. Kwa hiyo nikupunguza muda wa baadaye. Nikisafishe tu. Sitakifunga mpaka
daktari akione.” Bale alishakuwa amechoka kukaa hapo. Akashukuru. Akamuongoza njia
bila yakumsaidia wakafika kwenye hicho chumba. Hapakuwa na mtu. Akamuonyesha sehemu
ya kukaa. Bale akajitahidi mpaka akakaa.
Vai akachukua vivaa
na kukaa mbele yake, akaanza kumsafisha Bale akimuangalia. “Hujaumia vibaya
sana. Hapatakawia kupona. Upo kwenye antibotic zozote?” “Nilishamaliza ndio
maana nilichukia. Nilikuwa nimebakisha kidogo tu, nipewe mguu. Tena hapo ni kwa kuwalazimisha sana nikiwaambia
mbona kama mguu wenyewe umepona ila wananikawiza tu! Ndio hatimae kwenye
kliniki yangu iliyopita wakaniambia leo nikirudi naweza kuanza kujaribu mguu
ili nione utakao nifaa. Sasa hii anguka ya leo, ndio inamaana inabidi tena kusubiri!
Mpaka najiona nina mkosi unaokataa kuisha!” “Eti mimi nimekuja kugundua,
wakati mwingine kusubiri sio jambo baya.” Vai aliongea kawaida tu
akiendelea kumsafisha, lakini ujumbe aliopata Bale moyoni ukawa mzito sana. Ukamkumbusha
makosa yake yote aliyofanya mpaka kumfikisha kwenye ulemavu huo. Akapoa kabisa.
“Usinielewe vibaya,
ukasema naongea hivi kwa sababu nina miguu yote! Naongea hivi kwa sababu maisha
yamenifundisha kwa vitendo juu ya haraka nilizofanya nikiwa mdogo….” “Wewe
bado ni mdogo Vai.” “Muonekano usikudanganye. Ndani ya huu muonekano, nimeishi
maisha ya kama mwanamke aliyemaliza miaka hata 60 hapa duniani. Na sikuachwa
salama kwenye haraka zangu. Najuta na kutamani kama ningesubiri mambo mengi,
pengine leo nisingekuwa hapa, wala nisingekuwa hivi.” “Ulitaka
kuwa nani?” Bale akamuuliza, akajicheka.
“Nilitaka kuwa daktari.”
“Lakini upo upande huohuo. Haupo mbali sana.” “Nesi si daktari. Na kwa akili
nilizokuwa nazo, na uwezo wa baba yangu aliokuwa nao wakati ule, kama si
haraka, nina uhakika ningekuwa daktari. Lakini nipo hapa, kwa haraka zangu.” “Ulisema
usingekuwa hivi. Ungekuwa vipi?” Bale akachomekea swali la pili kwa haraka.
Vai akafikiria jinsi
ya kumueleza bila ya kutoa undani wake kwa mtu asiyemfahamu, akashindwa. Akamwangalia
Bale, akamuona ametulia akisubiria jibu. “Pengine niseme hivi, katika hii miili
Mungu aliyotupa dhamana nayo hapa duniani, kuna viungo amewapa wanadamu
uwezo wa kuvitafutia mbadala, kama huu mguu wako. Ni kiasi cha muda tu. Kidonda
kikipona, unauhakika wa kurudi kutembea kama mwanadamu mwingine yeyote yule na
watu wasijue endapo utavaa suruali na usiamue kumwambia mtu kama una kiungo cha
bandia mwilini mwako. Ukaishi kawaida, nikimaanisha uwezo wa kutenda kama mtu
mwingine yeyote yule.” Bale akabaki akimsikiliza kwa makini.
“Lakini katika hii
miili, kuna viungo Mungu aliviumba, bado hajampa akili mwanadamu ya
kuvitafutia mbadala. Ukikiharibu alichokupa yeye, ujue ndio basi
tena. Unacho mara moja tu. Kikiondoka ndio ujue ni kilema chako cha
maisha mpaka unarudi kwa muumba wako.” Hapo akamchanganya Bale, nakumfanya
atulie afikirie ni kiungo gani hicho kisicho na tiba mbadala!
“Jicho?” Akajiuliza na
kumtizama Vai. Alikuwa na macho mazuri yanawaka kama mwili wake. Vai akacheka
kidogo akijua amemuacha akifikiria. Ila akaendelea. “Kwa hiyo Bale, ukiambiwa subiri,
nakushauri subiri. Waliotangulia, wametangulia tu. Aliyesomea mambo ya
mifupa, anajua ni kwa nini anakushauri alichokushauri. Inamaana aliweka nidhamu
darasani. Akasomea hilo jambo ndipo akaaminiwa na kupewa dhamana na bodi
ya watu wenye uzoefu wa hicho kitu, kukutana na mtu kama wewe mwenye shida kama
hiyo. Chochote watakacho kushauri, fuata ukijua aliweka nidhamu chuoni,
tena kwa miaka mingi tu, akijifunza mchana na usiku jinsi ya kusaidia
watu wenye hiyo shida. Kazi yako wewe ni kuongeza tu umakini ili hivi ulivyoanguka
leo, usianguke tena. Halafu jua unalo tumaini, Bale. Mungu wako amekupendelea.
Analo suluhisho la tatizo lako, hapahapa duniani, tena hapahapa MOI. Ni muda
tu. SUBIRI.” Bale alipoa sana. Huo ujumbe ukabeba maana nyingine kabisa kwake, Vai
asijue. Akatulia.
Vai akamsafisha mpaka
akamaliza, Bale yupo mbali wala hajui anachofanyiwa tena. Vai akasafisha pale mpaka
akamaliza bado Bale amepotelea mawazoni. Akamsogelea. “Nashauri urudi pale
ukasubirie namba yako ili usije ukaitwa, wakakuruka.” Bale akamtizama vizuri akiwa
ametuliza mawazo ndipo akaweza kumuona vizuri zaidi. Vai alikuwa mweupe haswa, tena
wakung’aa. Hana kipele wala kovu aliloweza kuliona. Hiyo rangi yake ikamkaa
yeye vizuri na kumfanya avutie machoni. Hata hapo amevaa sare ya unesi
alivutia. Bale akabaki kama ameduaa kana kwamba ndio anamuona kwa mara ya
kwanza. “Huyu kiumbe atakuwa amekosa nini hicho kisicho na tiba wala mbadala!”
Bale akajiuliza akimtizama nakushindwa kuelewa kabisa.
Vai akacheka na
kumuuliza. “Vipi?” “Nashukuru sana Vai. Asante kwa kila kitu na samahani
nilikuwa mkali kwako bila sababu.” “Usijali.” Bale akasimama akijishuku. Maana Vai
aliyemsaidia si msichana hovyo. Mrembo haswa lakini akajishusha kwake yeye
mlemavu! Akatamani kama angekuwa amekutana naye wakati mwingine, tena akiwa si
mlemavu na iwe ni zile enzi zake akiwa na pesa alizokuwa akizikusanya kipindi
cha Maloni. Angalau angepata ujasiri wa kuzungumza chochote mbele yake. Lakini ujasiri
ukamuishia kabisa.
Akachechemea mpaka
mlangoni kisha akageuka. Akataka kama kumuuliza kitu, akakumbuka ni mlemavu,
hana mguu na hapo alipo anatunzwa na Joshua. Na vile alivyomuona Vai alivyo! Akasita,
Vai akimtizama tu. Akagairi na kutoka bila ya kuongeza neno.
Pesa Imepotea Njia.
Ungemuona mama Jema,
ungejua amefanikiwa. Halii shida akikopa hata kwa ndugu zake. Anazungumzia
mamilioni ya pesa na biashara zakueleweka. Mpaka wanakaribia kufunga mwaka
mambo yao yanazidi kuwaendea sawa tu, ikawa kama Mungu amewaamulia wao. Kituo
cha mafuta kikawa kipo sehemu nzuri, kinakaribia kukamilika kianze kazi
yakuingiza pesa. Mama Jema akiwa anakisubiri, akaendelea kuwekeza nguvu kwenye duka
lake hilo kubwa alilokuwa akiuza vipodozi, vitu vya harusi ambavyo alikuwa
akinunua nakujua watu wangehitaji. Upande mwingine vitu vya wanawake. Pochi na
viatu. Kukubwa na kukawekwa kwa hali ya juu. Ungefurahia kuwepo hapo.
Maisha yakawa yakiendelea,
pesa ya biashara inaingia na Zenda naye bado anamwaga pesa kama anayemlipa
Jelini mshahara kila wakati wala si mwezi. Jelini akatulia haswa, yeye ni Zenda
tu, hataki shida na mtu. Kila anachojua kitamuudhi Zenda, anakwepa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wachaga hawa wanawake
na wao kila krismasi lazima waende migombani kwa mama yao. Lazima. Basi
kama kawaida yake mama Jema akaanza kujiandaa kwa safari. Jeremy akafunga shule
akijua anaenda kwa bibi. Na yeye anamuita bibi kama mama yake. Safari hii
wanakwenda na gari ya Jelini. Renji. Wakafungasha vitu vyakutosha. Jelini akaenda
kuagana na Zenda, wakapeana penzi kwa muda, wakiagana kuwa krismasi na mwaka
mpya Jelini atakuwa migombani na yeye Zenda atakuwa na familia yake mpaka mwaka
uanze. Yalikuwa mapumziko ya siku chache tu, lakini ikawa huzuni kana kwamba ni
mwaka! Walikuwa wakiondoka tarehe 23 na kurudi tarehe moja. Mama Jema akaacha
biashara zao vizuri, safari ya Moshi ikaanza wakiwa na Jema na tumbo lake.
Mchaga James alisema kwake
yeye huo muda ambao hayupo kazini ndio wakati wa kuwekeza kwenye biashara, Jema
akaona aongozane na mama yao. Gari ya Jelini kubwa haswa, Jema akakaa kiti cha
mbele ajinyooshe mgongo, Jelini mwenye gari nyuma na mwanae kama gari si yake.
Mama yao pia alikaa kiti cha nyuma na kina Jelini, Zenda alimwambia Devi yeye
ndiye awaendeshe kwa sababu ni safari ndefu, kisha kurudi kuwachukua huo mwezi
wa kwanza tarehe 2. Safari ikaendelea stori njia nzima wakicheka tu, Jelini
asijue mipango mibaya anayopangiwa.
Usiombe Vita Na Akufahamuye.
Halafu yeye ajipange kimashambulizi
dhidi yako, huku akikuchekea huna habari. Sasa Zenda yeye mwenyewe ndiye
aliyejiweka busy na Jelini, wala si kwamba Jelini alimbana. Lakini wanae
wakaona ni kama Jelini ndio sababu. Na Kemi bado hakuwa amerudishwa kazini,
hicho kikawa kinamuuma hata mama yao huko alipokuwa. Alikuwa akiumia
haswa. Swala la kuumizwa kwake Jelini halikuwa likizungumziwa ila kufukuzwa
kwake Kemi kikatili ndio ukawa msiba kati yao na mama yao.
Zenda huwa na
wanawake, lakini bado wakawa wakinufaika na pesa yake. Sasa kuona safari hii eti
amekuja mtoto mdogo anayesababisha wasitafune pesa ya Zenda watakavyo! Eti ndiye
ameshika masikio ya dad! Hasira yote ikawa kwa Jelini. Yeye ndio akawa sababu.
Hapatikaniki kwa simu
wala jumbe. Hana muda na familia wala wajukuu ambao huwapenda sana. Hapakaliki
kazini wala kwa wanae. Mbaya zaidi Kemi! Kipenzi cha dad, kila mtu analijua
hilo! Ukitaka kitu kwa haraka kutoka kwa Zenda, basi mtume Kemi, utakipata kwa
haraka tu. Lakini eti Kemi amepokonywa mpaka hati ya kusafiria na haruhusiwi kufika
karibu ya mali za dad! Hilo likawa chumvi kwenye chai. Huna kiungo
ukatia ikafaa kunyweka tena.
Watoto hao na mama yao
wakaona ni wakati muafaka wa kutoa mwiba kidoleni kabla
hakijazidi kutunga usaha na kuozesha kidole zaidi. Wafute kabisa
kumbukumbu za Jelini kwenye familia ya Kasa wala asiwahi kurudi tena. Wakafikiria
kumtafutia Zenda mwanamke mwingine watakayeendana na wao. Na safari hii
walazimishie ndoa kabisa ili mzee abaki kuwa upande wao, kosa jelini
lisiwahi kujirudia tena.
Sasa nani wakumuweka kwa
baba yao na wao wabakie ndio wanufaikaji! Yaani asiwe mwanamke mwenye shida au uchu wa
pesa! Atakayeingia na matatizo yake halafu pesa ya baba yao ndio ianze kumkarabati
mpaka afae! Huyo hawakumtaka. Wakabaki wakikuna vichwa na huo ndio ukawa
mtihani. Maana walishapita wengi tu hapo kwa baba yao, ila hawakudumu. Nani!?
Simu kati ya mama na
wanae, watatu hao zikaendelea wakipanga mipango mizito ya kimapinduzi.
Kila wanayemtaja kumuweka kwenye maisha ya baba yao wakawa wakimtoa kasoro, ila
mwishoe kura ikamuangukia Koku. Koku ndiye msichana wake huyo wa booty call.
Wamekuwa kwenye hayo mahusiano ya kupeana penzi tu, bila kujifunga kwenye
mkataba wowote ule, kwa muda mrefu tu, wote wanamjua.
Koku mtumzima, amefanikiwa
kiuchumi haswa. Kwa kumwangalia tu utajua hataki ujinga kwenye maisha, na
hakuwahi kuolewa wala hakuwahi kutaka swala la kuwa na watoto. Ila juhudi kwenye kutimiza ndoto
zake nzito. Darasani alikaa mpaka vitabu vikaitika, ‘abee’! Kazi nzuri aliyounganishiwa
na huyohuyo Zenda ikawa ikimuingizia mamilioni ya pesa ambayo yanafanya wanaume
wamkimbie. Kiburi kipo kwa kumwangalia tu. Mwanamke wa mipango, hana shida
ndogondogo kama kina Jelini mpaka kukarabatiwa nyumba! Anaishi kwenye hekalu la
kujenga yeye mwenyewe na juhudi zake alizoweka kwenye maisha.
Wote walimfahamu na
hakuwahi kuwa tishio kwenye mali za baba
yao kwani kwa hakika Koku alikuwa tajiri, hali zikiendana nao. Ila yupo busy
sana. “Huyohuyo atatufaa. Kwanza Koku ni mtumzima
sana. Umri umekwenda, hana hata uwezo wa kushika mimba tena. Kwa hiyo hawezi
kuzaa na Kasa.” Mama yao akaongeza kwa kuridhia kwa Koku na wote wakaafiki
kuwa watabaki wao tu wawili ndio watoto wa Kasa na warithi pekee
maana hicho hata mama yao alikilinda.
“Sasa jinsi
ya kuwaunganisha tena Koku na dad ndio shuguli.” Kevin akawaza kwa sauti wakiwa bado
kwenye simu. “Na hapo ndipo pakuwa makini sana. Maana
mnamjua Kasa. Anawaza kwa kunusa mbali sana. Kosa dogo tu. Kujichanganya kwa
aina yeyote ile, hata kuropoka neno moja tu, mjue tayari amewakamata. Na akihisi
tu, mjue ndio tumepoteza nafasi nzima, na hatakaa akatusamehe daima. Sisi
tutabakia kwenye upande wa watizamaji timu iliyofungwa uwanja wa nyumbani.”
Mama akaweka msisitizo na kufanya wanae wazidi kufikiria wakijua wanacheza na
baba yao, kichwa yake inafanya kazi kwa haraka sana tena vizuri mno.
“Hakika
tufikirieni kwa makini. Hata mimi sitaki kosa jingine litokee tena. Tulikaachia
haka katoto, kakaingia kwenye maisha ya dad kama utani tu, ona kalichonitenda!
Amenisingizia mimi nataka kumuua na kunifukuzisha kazi! Hakika lazima atoke na
yeye kwenye maisha ya dad.” Kemi akaongea kwa kuumia sana. “Kwanza
atafilisi mali zote. Hakajasoma, ni wale wanawake malaya wanao danga tu.
Anachohitaji ni kujinufaisha yeye tu.” Akaongeza Kevin kwa jazba.
“Kama bado
hatujachelewa!”
Akaongeza mama yao kwa wasiwasi kuwa pengine Jelini alishaanza kuhamisha mali
za Kasa. “Nimechunguza kwa makini sana mpaka kwa kumuuliza
kijanja yule wakili wake, bado. Dad hajamfanyia chochote kikubwa. Devi anasema
ni marekebisho tu ya hapo nyumbani kwao. Lakini sasa mjue muda unavyozidi kwenda,
atazidi kumuingia dad akilini, ndipo ataanza kuchota mali. Before we know,
yeye ndio atakuwa mama Kasa, wote tunaishi kwa rehema za Jelini.” “Hakika
tusiruhusu.” Mama akaongeza kwa jazba wasijue mzee anawajua vizuri sana na
anaakili, ndio maana kila alichompa Jelini, alimtumia Godwin, ambaye ni mwanasheria
wasiyemjua kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kila alichompa
Jelini, alihakikisha kipo kwa jina lake Jelini Kundi. ‘Kundi’ ukoo wa
mama Jema. Wanae wote walichukua huo ubini wake. Watoto wasiojulikana baba zao.
Siri ya mama Jema peke yake. Mali zote za Jelini zikawa hazina hata dalili
kwamba zimetoka kwa Kasa na akamuapisha Godwin. Tena kwa maandishi kuwa
siku atakayotoa hiyo siri, atamshitaki kisheria. Kwamba asijewahi kuzungumzia
chochote, na yeyote, kile kinachoendelea kati yake na Jelini isipokuwa na
Jelini mwenyewe na yeye mwenyewe mzee Kasa. Godwin akakubali ikawa yeye ndiye
anayeweka kila kitu kwa maandishi na kufuatilia mambo kisheria kuhakikisha
hakuna wakuja kumpokonya chochote Jelini hata kama itatokea mzee mwenyewe
hayupo duniani. Na akatunza hayo mambo ikawa ni kati yao tu, wao watatu. Hakuna
mawasiliano hata ya barua pepe, akijua wanae wanaakili, wanaweza kufuatilia
email yake wakajua mazungumzo kati yake na Godwin juu ya Jelini. Kikubwa wakawa
wakizungumza kwa kuonana sehemu mbali na kazini na nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati wao wakiendelea
kuweka mipango yao wakiwa wamejawa jazba, mzee Kasa alishakuwa amejipanga
kivyake kumlinda Jelini, asijue anajilinda upande ambao watu wa nyumbani
kwake wanajipanga upande mwingine wakilinda huo upande anao udhibiti
yeye, kwa wakati huo. Mali.
Wakaendelea kujipanga
kwa makini, ila kwa haraka wakijua huo ndio wakati muafaka wa kufanya yao maana
anayembana baba yao, hayupo mjini. Walishampigia simu Devi na Devi
kuwahakikishia mzee yupo peke yake, kwani yeye ndiye aliyetumwa kupeleka
familia ya Jelini na Jelini mwenyewe Moshi. Hasira zikazidi zaidi. Na
Devi ndiye aliyekuwa akiwapa kinachoendelea kwenye maisha ya baba yao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usiwahi Kuwa Adui Na Anayekufahamu Kwa Undani. Wanapiga Wanapojua
Patauma.
Nini Kitaendelea? Watafanikiwa Kwenye Penzi Zito La Zenda Na Jelini?
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment