“Sasa usimalize Jema bwana! Huyu baba atakuja hapa, akute
Jelini hajala hata moja wewe umemaliza.” “Wala sio mimi, mjukuu wako huyo!”
Jema akaendelea kula. “Mbona jasho litanitoka! Mpaka huyo mtoto azaliwe!” Jema
akazidi kucheka. “Kwanza Jelini mwenyewe anashindwa hata kufungua macho. Sijui
wamempa nini! Maneno yote kwisha.” Wakaanza kumcheka vile alivyokuwa amelala.
“Kungwi wako yule.” “Mbona nilimshukuru! Haki ningetia aibu
mama. Nilikuwa sina moja! Kwanza hata sikuwa nikiwaza.” “Sasa ulitegemea nini?”
“Nilijiambia nitajua mbele ya safiri huko kwenye ndoa.” Wakaanza kucheka.
“Jema!” “Nilivyokuwa busy vile! Ningeanza kuwaza saa ngapi kukata kiuno,
mama yangu? Kwanza sikuwa hata na wakumkatikia.” Wakazidi kucheka, Jelini
kalala hana habari.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mara mlango ukagongwa na kuingia, alikuwa Zenda. “Sijui
nimechelewa?” “Hata kidogo. Hapa tulikuwa tukizungumza tu. Jema alikuja
kunipokea mpaka usiku ukija.” “Sasa na Jeremy?” “Nimemwambia bibi yake mwingine
akae naye mpaka nifike mwenyewe.” Akaonekana kama hajaridhika. “Jelini hatakuwa
na wasiwasi na hilo kweli? Ni kama hamuamini mtu mwingine na Jeremy isipokuwa
wewe!” “Wala hujakosea. Ila nakwenda.” Hapo akaonekana kuridhika.
“Nina zawadi zake hizi, unaweza kumwambia zinatoka kwa mama
yake. Aliniambia Jeremy anapenda vitabu.” “Sana. Na asante.” “Karibu.
Wameniambia Jelini amekuwa akilala siku nzima, ameweza kuzungumza naye kweli?”
“Hapana. Hata Jema naye ametoka kuwauliza sasahivi juu ya kulala kwake. Lakini
wanasema kwa siku tatu za mwanzo, ni bora hivyo kuliko maumivu.”
“Mimi na mjukuu wa mama Jema tunashukuru kwa chokleti.”
“Jema wewe mtoto! Ni za mgonjwa bwana!” “Sasa Jelini mwenyewe hazili mama, na
mjukuu wako anataka! Tufanyaje?” “Umenyimwa aibu wewe! Si ulisema hutaki
kunenepa wewe, utakuwa ukila matunda tu?” “Mama naye! Unamuhesabia chakula
mpaka mjukuu!” “Mbona mpaka azaliwe huyo mimi nitakoma! Nitaleta kesho hizo
chokoleti.” “Wewe mama unazijua!?” Wakaanza kuchekana wenyewe, Zenda
akiwasikiliza.
“Nitaziulizia pale dukani.” “Kwamba Mangi auze chokleti kama
hizi?” “Lazima atakua nazo bwana!” “Mmmh!” Jema akaguna akiendelea kula. “Sasa
kama huna uhakika na upatikanaji wake, mbona unaendelea kula bwana Jema?
Ridhika bwana!” “Wewe si umesema utaenda kuzinunua kwa Mangi kesho uje nazo?”
“Kwa ule ugunaji wako, nahisi kama sitazipata!” “Wala hujakosea. Hizi zakizungu
mama yangu, ndio maana mjukuu wako hataki kuacha kula.” Mpaka Zenda akacheka.
“Wewe na mwanao muwe na kiasi bwana! Halafu acha nimbebee na
Jeremy.” Mpaka Jema akacheka. “Hapo sasa ndio tunatia aibu mama Jema bwana!
Unataka wajukuu wote wale!?” “Kidogo tu.” “Msiwe na wasiwasi. Nitaagiza
nyingine.” Zenda akaingilia. “Basi agiza nyingi ili na sisi pia tupate.” “Jema
wewe mtoto umenyimwa aibu, wewe!” “Ni mjukuu wako huyo wala si mimi. Mimi na
chokleti wapi na wapi mama yangu?”
“Usihangaike mwaya. Hawa nitawanunulia za kwa Mangi.” “Sasa
mama wewe unataka kuharibu. Nishakwambia Mangi hana chokleti. Wewe acha sisi
tuletewe chokleti za kizungu. Achana na chokleti zile za mtaani, zinaganda
kwenye meno kama uchafu!” “Haya, simama hapo twende Jema. Unakazi ya kula tu.
Twende unisogeze.” “Twende mama Jema. Nikamsalimie na kaka.” “Wewe kwako
hupiki?” “James harudi sasahivi nyumbani. Leo mpaka saa tano usiku.
Kashanipitia mchana, tukaenda kula, ujue kuja kumuona ni usiku mwingi.” “James
muhangaikaji!” “Sana. Mpaka namuhurumia. Ana mambo mengi na yote yanamtaka yeye!”
“Sasa unafanyaje?” “Tangu namfahamu ndio yupo hivyohivyo.
Akitoka kazini anahamia kwenye biashara. Yupo barabarani mpaka saa sita usiku.
Nilijua naolewa na nani mama yangu. Namsindikiza kwa simu, nikichoka nalala.”
“Bora.” “Basi twende ukale kwangu.” “Wewe mama Jema unataka kuniharibia ndoa
wewe! Nikila kwako, kwangu sitapika, James atarudi nyumbani asikute chakula,
akutane na mke aliyeshiba, amelala hana habari. Wewe acha nikasalimie, niwahi
kwangu nikapike. Au unataka ukapikie kwangu halafu wewe na kaka mkishashiba
ndio muende kwenu?” “Wewe unataka kunivurugia ratiba yake yule. Nataka awahi
kulala, asubuhi shule. Kapike kwako acha uvivu.” Jema akaanza kucheka.
“Ulijuaje? Nilitaka ukifika unipikie na cha kesho.” Wakaanza kucheka
wakikusanya vitu vyao ili watoke, Zenda akiwasikiliza.
Alikuwa amesimama kwenye kitanda anamwangalia Jelini.
“Jelini! Jelini!” Wakamsikia akimuita kwa sauti ya chini taratibu. “Fungua basi
macho hata unione!” Jema na mama yake wakakonyezana. “Jelini!” Akamuita tena.
“Zenda!” Akaitika taratibu. “Umeona maua niliyokuletea?” “Nilikuwa nimelala.
Kichwa kizito!” “Pole. Jaribu kufungua macho kidogo. Niangalie.” Akajitahidi.
“Unaumia?” “Upande huu. Ndio maana nafunga macho.” “Pole sana. Unataka
kumsalimia Jeremy kidogo ili umtoe wasiwasi?” Akafikiria. “Nataka uamke
nijaribishe kukulisha kidogo. Wamenipigia simu na kuniambia hauli.” “Nasikia
usingizi.” “Jitahidi. Simu hii nimeweka chaji, mpigie mtoto. Pengine ukimsikia
utachangamka.” Akakubali. “Basi nanyanyua kitanda kidogo.” Akabonyeza kitanda
kikaanza kunyanyuka, akawa kama anakaa.
“Pole Jelini.” “Jema! Nilikusikia nikahisi naota. Mama Jema
yuko wapi?” “Nipo hapa. Vipi?” “Sasa Jeremy!?” Akawa kama amekumbuka. “Hivi
ndio nilikuwa naondoka. Nilimwambia mama yako mkubwa amsubirie pale nyumbani,
aende naye kwake, nitamfuata. Nimezungumza kama lisaa limepita, yupo sawa tu.”
“Mamkubwa anamjulia.” Akaonekana kuridhika. “Nimechoka, natamani kulala tu.”
“Jikaze ule, Jelini. Utadhoofu!” Jema akasisitiza, Zenda akadakia. “Nakulisha
kidogo tu, halafu nakuacha ulale. Au hupendi chakula chao?” Akamuuliza kwa
kumbembeleza, akajaribu kufikiria. “Hata sijui ladha yake!” “Hajala huyo.
Alikula kidogo sana, akapotelea usingizini.” “Niambie unahamu ya kula nini?”
Zenda akamuuliza, wakamuona anaanza kulia. “Nataka
tu kulala, Zenda. Nimechoka!” “Basi usilie, utajitonesha. Nifungulie tu
mdomo, mimi nitakuwekea chakula mdomoni. Na sitakuongelesha. Sawa?” Akanyamaza.
“Nyinyi nendeni tu. Atakuwa sawa. Na kama atashindwa kula,
nitawaomba waongeze dripu ya glucose ili asidhoofu, mpaka tena kesho pengine
tumjaribishe tena chakula.” Wakazungumza tena wakaweka mipango ya mama Jema
kuleta uji asubuhi wakataka kuondoka lakini Zenda akawawahi. “Gari ya Jelini
ipo tu ofisini haina kazi. Kwa nini usiitumie ikusaidie wewe na Jeremy?” “Mimi
sijui kuendesha magari.” Akajibu mama Jema bila shida. “Nayaonaga tu humo
barabarani na kupewa lifti, sijui hata wanawekaga wapi funguo. Nisije kufa nikaacha
wanangu bure!” “Basi nitatuma dereva asubuhi aje akuchukue.” “Hapo utanisaidia.
Nashukuru.” “Bila shaka.” Wakaondoka.
Upendo, Husitiri Wingi Wa Dhambi.
Wakati yupo njiani na
mama yake wakiongea yao, simu yake ikaanza kuita, akapokea alikuwa Magesa. Jema
akaanza kucheka. “Mimi Magesa.” “Hujambo Magesa?”
“Sijambo. Na mdogo wangu hajambo? Mimi kaka mzuri. Nataka kujua hali ya mdogo
wangu. Halafu jumamosi nimuombe bibi anilete, nimletee zawadi zake, halafu
nimsalimie. Sitaki akija kuzaliwa awe hanijui kama mimi ndio kaka mkubwa.”
Jema alicheka sana.
“Mimi
nimekupenda kaka mkubwa. Kumbe na wajibu wako unaujua?” “Ila sasa sijui mtoto
anapenda nini! Nimekwambia bibi ndio dereva wangu siku ya jumamosi?” “Uliniambia.
Sasa ameshakubali?” “Mimi hawezi kunikatalia.” “Ujue Magesa mimi nina mipango yangu
lazima uniombe?” Akamsikia Mama G akiongea pembeni. “Tunaanza mipango yako
kwanza. Nakusindikiza. Ikikamilika, na mimi unanisindikiza kwa mtoto. Mama
angekua haendi kazini, ningemuomba yeye. Lakini wewe unakua hauna kazi nyingi
siku za jumamosi, kwa hiyo tunaweza kwenda.” “Unapenda kunipanga wewe!” Jema
anacheka hana mbavu.
“Ujue mimi nikiwa
mkubwa na gari yangu, nitakuwa nikikusindikiza bibi?” “Na ulikumbuke hilo. Sio
uje uniruke, ujidai umesahau jinsi nilivyokuwa nikikusindikiza kwenye yako.”
“Mimi siwezi kusahau bibi.” “Sasa uulize muda mzuri wa kwenda na wapi. Sio
ifike siku yenyewe, hatujui sehemu ya kupeleka vitu vya mtoto.” “Anti Jema upo?” Akarudi kwenye simu.
“Nipo
Magesa, nilikuwa nakusubiri uweke sawa mipango ya usafiri.” “Bibi atanileta.
Ila anataka kujua muda gani mzuri na wapi. Halafu mimi nataka kujua mdogo wangu
anataka nini?” “Anapenda kula huyo!” Magesa akaanza kucheka. “Hata mimi napenda sana kula. Kila saa nasikia njaa.”
Jema akaanza kucheka na kusikia upande wa pili wakicheka. Akajua na wazazi wake
wanasikiliza.
“Basi si
bora nikupikie kabisa, ili ukija unakula chakula kingi?” “Kama ni kingi nakuja
na mami wangu pamoja na Jimmy.” “Umeanza kualika watu nyumbani kwa watu Magesa bwana!” “Ni
kwa anti Jema bibi. Usiwe na wasiwasi.” Hilo likawafurahisha. “Ningekuja na dad wangu na Liv, lakini wao hawapendi kula.” Mpaka Geb
akacheka. “Jimmy yeye anasumbua kidogo, lakini mami
akimlisha, anaweza kula kidogo halafu basi kingine namalizia mimi.”
Wakazidi kucheka.
“Kama ndio
hivyo basi itabidi nipike kingi zaidi ili mkiondoka wote muwe mmeshiba. Lakini
sio jumamosi hii. Sasahivi nina mgonjwa hospitalini, sipo nyumbani mpaka kama
mida hii.” “Pole anti. Nani anaumwa?” “Mdogo wangu. Na asante.” “Mimi ningekuwa
siogopi sindano, ningekuja anti. Lakini sipendi hospitalini, halafu naogopa
sana mada..”
Akasikia kimya kama kuna mtu anamuongelesha.
“Sijajua bado mtoto
anataka nini bibi!” “Nakurudishia Magesa, bwana!” “Ila mwambie anti mimi
sijamaliza, usikate.” “Sawa.” “Anti Jema bibi anataka
kuzungumza na wewe. Nimpe simu?” Akajua wameshasikia swala la ugonjwa. “Sawa. Halafu tutazungumzia maswala ya anachopenda mdogo
wako. Maana na yeye nahisi anapenda kula kama wewe.” Magesa akacheka wee
kama mazuri. Akampa simu bibi yake.
“Poleni
Jema.” “Asante. Shikamoo.” “Marahaba. Ni nani mgonjwa?” “Ni mdogo wangu,
anaitwa Jelini.” “Yule alisema yeye kwenu ndio mpole sana ndio maana watu
hawajui kama ni mdogo wako?” Mpaka mama Jema akacheka. “Yaani Jelini!” Mama yake
akatingisha kichwa akicheka maana na yeye Jema aliweka kwenye spika akiongea
huku akiendesha.
“Huyohuyo kiziwanda
wa mama Jema, cha maneno. Alianguka vibaya! Amepasuka lakini mbaya zaidi, pamechimbika.
Juu ya nyusi. Ameshonwa lakini pia amepoteza damu nyingi. Ila anaendelea vizuri
wala msiwe nawasiwasi.” “Ni sawa kuja kumuona?” “Analala tu. Wanampa madawa ya
usingizi, analala tu. Wala msihangaike.” Mama G hakuridhika. “Mbona unataka kuninyima shuguli bwana Jema?” Jema
alicheka sana.
“Nakuhurumia
usumbufu usio na sababu!” “Hayo ndio mambo ya familia yalivyo. Mmoja akiumia ni
wote tunaumia. Si usumbufu. Msiuguze peke yenu.” Hilo likawa faraja. “Haya, tunashukuru. Mida gani nyinyi mnakuwa na nafasi? Maana
mama ndiye anayeshinda naye mpaka jioni nikitoka kazini ndio nakwenda
kumpokea.” “Basi tutapita kama kwenye saa nne ili kumpitishia mama na mgonjwa
kitu cha kula, kisha tutarudi tena jioni.” “Ila Jelini hali. Labda mama.”
Wakazungumza wakijipanga.
“Sasa
Magesa nimwambie aniletee nini? Sitaki kumsumbua.” “Anapenda shuguli kuliko
bibi yake. Hivyo ukimsumbua ndio atafurahi apate chakusimulia. Wewe mtajie kitu
unachopenda kula, tutakuletea tu. Na usijisikie ni lazima kukaribisha wageni
wake wote.” Wakaanza
kucheka. “Hamna neno.” “Wewe ukimuendekeza huyo,
utajikuta unakazi ya kukaribisha ukoo wake mzima.” “Msijali. Nyinyi mjiandae
mje kula kwangu. Ni kweli Geb na Liv wao hawatakula? Naweza kuwapikia kitu
watakachopenda.” “Jiachie tu. Wewe tupikie sisi tunaokula kila kitu. Hawa
hutaweza.” Wakazungumza na kucheka.
“Basi muwe
na usiku mwema.” “Na wewe Jema mwanangu.” “Asante. Msalimie Nanaa na wengineo”
“Tena Nanaa huyu hapa. Bora tu umsalimie mwenyewe.” Nanaa alishituka
nusura akimbie. Pakazuka ukimya hapo, Geb kimya akijiangalizia. “Nampa simu Nanaa.” “Naogopa mama.” Akamsikia Nanaa
akinong’ona. “Msalimie tu. Hana neno.” “Sitaki kumuudhi tena. Naogopa mama.
Naogopa kuharibu zaidi.” “Alikwambia nini Joshua?” Nanaa akapokea simu.
“Halo.” Akaanza Nanaa kwa
sauti ya kutetemeka mpaka mikono ilikuwa ikimtetemeka mpaka mumewe akaumia. “Upo mzima mama ya rafiki yangu kipenzi, kaka mkubwa wa ukoo?”
Angalau wakacheka. “Mwanangu anapenda ukubwa huyo!”
“Lakini bora yake anayependa ukubwa na majukumu yake. Kwa hilo, nimemuheshimu.”
“Basi huyu utamchoka.” “Si rahisi. Huyo anayependa na majukumu! Nishindwe mimi
tu. Hapa naandaa orodha ya vitu anavyotaka mdogo wake.” “Hapo utakuwa
umemfurahisha mwanangu. Na nashukuru mwaya Jema. Asante kwa kila kitu.” “Hata kunifukuza kwako?” “Jema naye? Jambo haliishi!” Angalau
wakacheka.
“Mimi bado
nimenuna bwana!” “Nisamehe Jema. Sina hata jinsi ya kujitetea.” “Ila mimi
nitakwambia kitu Nanaa. Na ninakwambia kwa sababu najua James anakupenda. Hili
jambo linamtesa yeye zaidi maana mimi ukweli hatuna mazoea. Hata tusipokuwa
kwenye mahusiano, hapatakuwa na shida.” “Shida ipo Jema.” “Hapana.
Tumefahamiana ukubwani. Hunijui, sikujui Nanaa. Namaanisha kama isingekuwa
James, ungeweza kuishi bila mimi na ukawa sawa tu, lakini si wewe na James.
Sijui kama unanielewa?”
Nanaa akaanza kulia.
“Maana kama
isingekuwa mimi Jema, basi angekuwa mtu mwingine anaolewa na James. Usingekuwa
na umuhimu wa kunifahamu. Ila nafikiria mahusiano yako na James. Mimi sitaki
nyinyi mkosane kwa sababu yangu. Ila nimekwambia kuna kitu nitakwambia
Nanaa, nitakwambia tu. Hivi nilitaka nikinyamazie, lakini mimi nimekataa
kuwa wifi wa hivyo. Nakataa mahusiano ya kumnyima raha James.” “Ni
nini?” Nanaa
akauliza kwa wasiwasi.
“Sasa,
sasahivi nina mama Jema kwenye gari. Acha nimalizane naye kwenye mizunguko
yake, mimi nitakupigia. Au unawahi kulala?” “Na hivi umenisamehe, nitakusubiri
tu.” “Na wewe si kirahisi hivyo! Mbona unashindwa hata kumuiga Magesa rafiki
yangu?” “Basi na mimi nitaleta zawadi si kwa mtoto, kwako.” “Niandae orodha?”
“Jema naye! Wewe orodha hiyo mpe Magesa. Yangu iwe surprise.” “Basi kwenye
surprise ongeza na matenite.” “Jema wewe mtoto huna aibu?”
Mama yake akashangaa sana, wakaanza kucheka. “Nina
shida sana na matenite ya kimtindo, sio tena magauni makubwa! Hapana. Tulipanga
na Naya twende kuyanunua mazuri yakisasa, yatakayofaa na kazini, ndio Jelini
akaugua. Najiona sina muda tena.” “Basi mimi nitakutafutia.” “Nitashukuru. Nitakupigia
mwaya baadaye.” Wakaagana. Nanaa hakuamini. Alifurahi mpaka mumewe
akafurahi.
“Sasa sijui anataka
kusema nini!?” “Usianze tena kujinyima raha. Naomba tulia na habari njema za
kwanza.” Mumewe akamuwahi. “Ila nimefurahi sana jinsi ulivyozungumza naye.
Kumbe mambo unayajua!” “Sijaamini mama! Nilikuwa naogopa mpaka nikakulaumu
kuniunganisha naye kwa haraka!” Wakaanza kucheka. “Na mimi nilikufanyia
makusudi, maana nilijua hutakaa ukawa tayari kwa hofu.” Angalau kwa mara
nyingine tena wakaanza kucheka Nanaa akisikika amefunguka.
Hospitalini.
Huku hospitalini ilipofika
mida ya saa tatu na nusu akaingia James na Colins wakamkuta baba ya mfanyakazi
mwenzao amekaa hapo na kitabu chake akisoma. Colins alishituka sana. Ni mzee
Kasa! Anamuuguza Jelini!? Hilo likamsumbua kidogo asielewe ndio inakuaje!
“Naona tumekuja muda mbaya!” “Hata yeye amelala siku nzima. Imekua ngumu hata
kuzungumza naye kwa dakika 5.” “Jema ameniambia. Poleni sana aisee.” James
akazidi kumchanganya Colins. “Inakuwa vipi apewe na yeye pole!?” Colins
akajiuliza.
Akamsogelea Jelini.
Akamtizama vile alivyolala na mabandeji kuzunguka kichwa. “Daah!” Akasikika
Colins, Zenda akamtizama. Akamuona anamfunika shuka vizuri, na kubaki
akimwangalia, Zenda naye akabaki akimwangalia Colins. Colins akapotelea
mawazoni akimtizama Jelini asijue Zenda anamtizama kwa makini. Akaingia muuguzi
hapo. “Sasa Colins?” James akamshitua kama waondoke. “Vipi maumivu yake lakini?”
Akauliza Colins akimtizama yule muuguzi. “Yupo kwenye dawa kali za kuzuia
maumivu ndio maana unaona analala sana. Si rahisi kuhisi maumivu.” “Kumbe
afadhali. Daah!” Colins akaongea macho kwa Jelini, ikabidi James amsogelee.
“Mimi naona twende tu.” “Daaah! Anaonekana ameumia sana.” Akaendelea kulalamika
Colins macho kwa mgonjwa. James akaamua kuaga.
Wakawa wanatoka.
“Ningejua mapema, ningekuja!” Ikawa kama anajilaumu, Zenda anamsikiliza tu
wakiwa wanatoka. “Hata ungekuja isingesadia. Jema mwenyewe hajapata naye muda.
Alikuwa amelala siku nzima.” Wakapotelea, lakini kikamsumbua Zenda. Wivu.
Akakumbuka hayo madhara amesababisha mwanae.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakawa kama wote,
mama G, Geb na Nanaa wakisubiria hiyo simu ya Jema. Simu ya Nanaa ikawa
ikiangaliwa kila wakati. Ilipofika mida ya saa nne usiku ujumbe ukaingia. ‘Bado upo macho na unaweza kunisikiliza?’ Hapohapo
Nanaa akaruka hewani. “Nilijua utakuwa umeshalala.
Umenisahau.” “Hapana. Mambo yamekuwa mengi tu. Ningekujulisha.” “Niambie.”
Jema akajiweka sawa.
“Naweza
nisiwe mtu sahihi kukwambia hivi, au ukaona hayanihusu. Lakini nilijiambia
nitakwambia halafu wewe mwenyewe uamue chakufanya. Na naweza nisiwe na jinsi
sahihi ya kukueleza, ila bora usikie tu. Maana naona hakuna jinsi nyingine. Na
utanisamehe kama navuka mipaka.” “Wewe niambie tu.”
“Mimi
sikufahamu Nanaa, ila mwanzo wangu mimi na wewe umekua mbaya sana. Mbaya zaidi
nikazidi kupata habari zako zilizonifanya nithibitishe ulichonifanyia
nilipokuja kwako. Lakini mimi mwenyewe nikajiambia lazima kusamehe kwa ajili
yangu, James na mtoto niliyebeba. Siwezi kuzungumza na Mungu kama wewe ukiwa
katikati yangu na Mungu. Nikaona nikutoe njiani, ili maombi yangu yasizuiliwe.
Hilo nikafaulu. Nikapuuza yote, nikajisikia mwepesi nafsini mwangu, maisha
yakaendelea, lakini nikajisikia jukumu la kuzungumza na wewe.”
“Narudia
tena, mimi sikujui, ila nakufahamu kwa upande ulionifungulia mimi na vile
nilivyokusikia. Sikuhukumu, kwa sababu niliona upande wako mwingine
ukiwa na mtu kama Naya. Nikajiambia si kwamba wewe ni mbaya, ila upo kama
mwanadamu mwingine yeyote yule. Hata mimi si rafiki wa kila mtu, kuna watu
nimeamua kuwa nao karibu, wengine ni salamu tu. Si dhambi maana si lazima
kufuatana nyuma na watu wote, lakini sitaki kuwa na neno na mtu. Hata
kama nikiamua kukuweka pembeni, usiwe mtu wangu wa karibu, basi nahakikisha
tunapokutana mahali, hata kama tupo wawili tu, basi tunaweza kukaa, tukachagua
chakuzungumza, tukacheka na kuachana bila kufuatana nyuma kwa simu wala ujumbe.
Sijui kama unanielewa?” “Nakusikiliza Jema.” Nanaa akataka kusikia zaidi.
“Nimezungumza
hivi kwa ajili ya mahusiano uliyokuwa nayo na mliyo nayo sasahivi wewe na kina
Viola.”
Nanaa alishituka sana. Hakutegemea kabisa kusikia hao watu. “Sikuhukumu kwa kuwa wamenipa historia yenu. Ukweli ni mbaya.
Hata mimi nilishangaa na kuumia kwa niaba yako na wao niliwaambia. Mimi binafsi
sijui kwa nini Mungu aliruhusu upite uliko pita Nanaa. Lakini Mungu alikupa
daraja, ukapita mpaka kufika hapo ulipo. Hukuchagua daraja, aliyekuchagulia
daraja ni Mungu. Sijui kwa undani uliishije, ulikuzwaje mpaka kufika
hapo, lakini kwa walivyoniambia kina Viola, naweza kuhisi ni pachungu. Narudia
tena, sikujui kwa undani lakini acha mimi nikwambie ukweli Nanaa.”
“Wale watu
kukulalamikia, wakisema walikuja mpaka kwako kukuomba msamaha, ukawaacha chini,
ukaenda juu ukiwaambia unawaachia mumeo awasikilize, wewe umechoka
kuwasikiliza. Umewasikiliza sana tokea mtoto. Ukawaacha hata hukuwapa maji ya
kunywa. Hukuja kuwatafuta tena. Na mkikutana hata sehemu mnashindwa
kusalimiana! Hata mlipokuja kwenye shuguli zangu, hamkusalimiana kabisa. Nina
uhakika mlionana. Sijui unasikia jinsi mimi tu ninavyosikika? Ni kama tayari
nakuhumu! Kwa nini? Ni kwa sababu unasikika upande wao, wao wakisema
walikufuata mpaka kwako, lakini ukashindwa kuwapokea, ukiwa wewe ulipokelewa
kwao. Sijui kama unanielewa Nanaa?” “Nakusikiliza.”
“Watu uliokuwa
nao pamoja wanaposema siku hizi Nanaa ameinuliwa sana na Mungu, hawezi
hata kusalimia watu kama sisi. Hawezi kusamehe. Hawezi
kuwa karibu na watu kama sisi ambao tulishindwa shule na maisha. Anakuwa
na matajiri wenzake. Anakaa katikati ya matajiri tu. Hataki hata kutambua kama
tunafahamiana na tulishaishi pamoja! Halafu mbaya, watangulie kusema walikukosea
sana na umeshindwa kusamehe! Sasa hivi ndivyo inavyosikika kwa watu tusiojua
ukweli wa mambo. Kwamba wewe huna shukurani. Na umebadilika. Kwa
mtu kama mimi niliyekuja kwako kwa mara ya kwanza kabisa, ukanikarimu kwa
staili ile. Tena nikiwa nimekuja kuomba mahusiano! Unafikiri inachukua muda
gani kuamini wanachokisema?”
“Haya.
Inawezekana wanadamu tusiwe na maana, usijali. Lakini Nanaa, watu
wakikunung’unikia. Wakilalamika hivyo, je, kwa Mungu aliyeamuru samehe saba
mara sabini akisikia manung’uniko hayo, unafikiri anasikiaje?” Jema akaendelea bila
kusubiri majibu.
“Kwa hakika
mimi nilitaka kuangukia hapo, lakini nikasema hapana. Si lazima mimi nikawa mtu
wako wa karibu, lakini si Ukristo kusikia hili na kulinyamazia. Na wenyewe
wanakuogopa kukusogela sababu wanajua wewe ni kipenzi cha James. Wanamuogopa
James, na wanasema wamekubaliana mpaka na mama yao wakuache kabisa, ufaidi
mafanikio yako kwa uhuru bila kukusonga. Sasa anayeachwa katikati ni James. Na
hili sijazungumza kabisa na James. Hata malalamishi ya dada zake sijamwambia
kabisa kwa kuwa sikutaka kumchanganya James.”
“Naomba
nimalizie kwa kusisitiza Nanaa. Mimi sikufahamu. Sihitaji chochote kutoka kwako
nikimaanisha mahusiano fulani. Ila sitaki tuwe maadui kiasi ya kwamba eti
tukikutana mahali, tushindwe hata kusalimiana! Au tushindwe hata kunywa
chai pamoja! Hapana Nanaa. Mimi nampenda Mungu. Nataka kuishi ukristo. Na kwa
hakika nimeachilia chochote kilichotokea katikati yetu. Nimekuelewa kwa upande
huo. Si kwamba wewe ni mbaya. Hapana. Ila mimi si mtu uliyetaka kuniweka karibu
kama Naya, ndio maana uliweza kunipa maneno makali sana ukiwa hata
hunifahamu na kukataa ukaribu wangu japo nilikuona mkiwa na Naya, mnaitana
mpaka vyumbani! Nilikuona Nanaa na mlikuwa kwenye wakati mzuri tu.”
“Narudia
tena Nanaa. Kwa moyo mweupe kabisa, sina neno na wewe. Sitaki tuwe maadui.
Nataka mahusiano yako na James yaendelee. Ila nimekufikishia yale niliyoyasikia
juu yako. Angalau mimi nimepata neema ya kukufahamu kwa upande mwingine ndio
maana nimepata hata ujasiri wa kukupigia na kukwambia hili. Sio nafasi yangu,
lakini mimi ningekuwa wewe, hivi ndivyo ningefanya.” Jema akaendelea.
“Kwa ubaya
wote uliotendwa ukiwa unakua, jifanye mjinga. Samehe. Watangazie
msamaha. Kisha waache. Hutapungukiwa Nanaa ila itapunguza manung’uniko
masikioni kwa Mungu. Na sio lazima ukawaweka karibu. Fanya kama ulivyofanya
kwangu tu. Hata hivyo wakina Viola wenyewe wapo busy. Mimi mwenyewe hatuna
matatizo nao, lakini hata hatutafutani mara kwa mara. Niliwashawishi mpaka
wakakubali kurudi shule. Wote wawili sasahivi wamejiingiza shuleni, naona
wamekazana kweli. Hawana muda na mtu. Vai analalamika shule yake ya unesi ni ngumu
na Viola naye hivyohivyo. Ni mpaka mimi mwenyewe niwapigie kuwajulia hali au
watatuma ujumbe wa salamu tu. Nakuhakikishia sio watu wa kufuatana nyuma.
Hawana muda.”
“Wewe
jishushe tu, na hata kama ulishasamehe, basi watangazie msamaha wajue
umewasamehe. Na kingine, itawarahishia hata mkiwa mnakutana mahali,
mnasalimiana na kupita kwa amani. Wanakiri walikuwa na utoto mwingi na ujinga.
Viola ameniambia hata mtoto aliyezaa alimpata kutoka kwa mwanaume aliyekuwa
wako. Lakini ona Mungu alichokupa Nanaa. Familia nzuri sana. Yeye amebaki na
hukumu ya kukupokonya mwanaume mpaka leo, wakati pengine wewe hata hukumbuki!
Sasa hudhani ukimtangazia msamaha utamuweka huru? Halafu James alinipa siri ya
mama yake kuwa anapenda sana pesa. Na ukorofi wake wote, pesa huwa inamtuliza.”
Nanaa akacheka
taratibu akimjua mama yake mkubwa. Kwamba James hajakosea.
“Sasa
niambie mtu kama wewe ukamfuata kwa salamu tu na kumshika mkono, itachukua muda
gani kusamehe na kuachana naye kwa amani?” Kimya. “Ni hayo
tu, usiku mwema. Acha nimpigie simu na James nilale, kesho kazini.”
“Kabla
hujakata Jema naomba kukuuliza kitu.” “Uliza tu.” “Kwa mwanzo tulioanza mimi na
wewe, unafikiri kweli hatuwezi kujenga mahusiano mengine ya ukaribu kama hivyo
wewe na Naya?” “Mahusiano yanajengwa Nanaa, si kupangwa. Nilichokifanya kwa
Naya ndicho nilikifanya kwako. Nikitambua wewe ni mdogo wa James, na Naya ni
mke wa Joshua ambaye ni zaidi ya bosi wangu. Kwako likatokea lakutokea, kwa
Naya nikashangaa vimenoga zaidi ya nilivyotarajia! Haitaji kunipigia simu akiwa
na ajenda. Kwangu si kama kwake, lakini anaweza kuja kulala kwenye kochi mpaka
mumewe aje amfuate. Amehamia kwenye saluni yangu ya uswahili na ameipenda. Daktari
anayemuona yeye kwa kliniki, nikajikuta nimependa sifa zake, na mimi
nimejindikisha hapohapo anapofanya kliniki yake. Tunakwenda siku moja kliniki.
Haya, akipikiwa nyumbani kwake kitu anachokipenda, anakibeba, unashitukia
amenitokezea ofisini kwangu na chakula. Tunakula, atakaa hapo mimi nikifanya
yangu mpaka atoke na mumewe jioni. Hatukupanga au hatupangi, lakini tunajikuta
mambo mengi yanaendana sana, bila shida au mipango mizito. Sijui kama
unanielewa?”
“Na Naya
anakupenda Nanaa.”
Hapo akamtuliza. “Anakupenda sana. Anakuzungumza vizuri
sana baada ya kurudiwa na kumbukumbu zake. Na nafikiri hata yeye amechangia
kunipa ujasiri wa kuzungumza haya na wewe baada ya kutambua kutoka kwake wewe
sio mbaya kama inavyosikika. Kwa hiyo kujibu swali lako, sijui. Ila
najua mahusiano huwa hayapangwi kwa simu.” “Nimeelewa na nashukuru kwa
kuzungumza na mimi. Acha nikuache upumzike.” Wakaagana.
Asubuhi, Hospitalini.
Jelini alilala usiku
kuchwa ilibidi kuongezewa tu maji ya glucose ili kumsaidia kumtia nguvu maana
alishindwa kabisa kuamka. Asubuhi alipokuja mama Jema, Zenda akijiandaa kutoka
akaingia Colins. Akawasalimia na kuulizia hali ya mgonjwa. “Ndio nilikuwa
nikiambiwa hapa, alilala usiku, hata hakuamka.” Akajibu mama Jema. “Lakini
hivyo ni afadhali, hatakaa akiugulia maumivu.” “Kwani wewe ni nani?” Ikabidi
mama Jema kuuliza, Zenda akasubiria kusikia huo utambulisho wake, ila kwa kuwa
alishaaga, akajidai anaingia bafuni kuosha mikono ili kuendelea kuwepo hapo na
kusikiliza.
Colins akajibu. “Samahani
nilisahau kujitambulisha. Na pengine umenisahau tu. Mimi naitwa Colins, nafanya
kazi na James.” “Ndio maana sura si ngeni! Nilikuona kwenye shuguli zake na
Jema! Asante kwa kuja kumuona huyu. Alianguka vibaya kweli!” “Aliniambia James.
Tulikuja jana usiku lakini alikuwa amelala.” Colins akasogelea pale kitandani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati anamfunika,
Jelini akafungua macho. Akamtizama kama ambaye haamini. Akashangaa jinsi moyo
wake ulivyosisimkwa kumuona Colins pembeni yake. “Pole Jelini.” Jelini akabaki
akimtizama haamini kama ni yeye! Hisia za ajabu zilizoamka ndani yake zikazidi
kumshangaza Jelini mwenywe! Hakutegemea wala kupanga kujisikia hivyo. Colins
amekwenda kumuona yeye! Akabaki kimya anastaajabu nafsini mwake.
“Unajisikiaje?” Akamuuliza kwa upendo! “Uliniambia nisikusogelee Colins!”
Jelini akasikika kwa sauti ya chini, na Zenda huko bafuni akasikia. Mama Jema
akajiweka sawa.
“Nakumbuka, lakini
nimekuja kukuona.” “Ili iweje? Huna haja ya kuwa hapa.” “Sikukusudia kukuumiza
Jelini! Nilitaka kukuepushia shari.” Colins akamjibu kwa upendo na sauti yake
nzito iliyotulia, na kuzidi kuukoga moyo wa Jelini. “Nilikwambia
hamna shida. Nikaheshimu hilo, ndio maana nilikuacha kabisa. Tafadhali simamia
maamuzi yako, usiwe mtu wa kuyumba.” Jelini akaongea na machozi
yakimtoka. Bila kutarajia, Colins akamfuta kwa upendo, tena taratibu mtoto wa
kiume bila haraka! “Pole Jelini.” Akaongeza Colins kwa sauti iliyojaa upendo na
kutawala chumba kizima, tena huku akiendelea kumfuta machozi taratibu kana kwamba hasikii
alichoambiwa na Jelini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Aluta kontinua…
0 Comments:
Post a Comment