Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 22. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 22.

Sikio Halizidi Kichwa.

Alipofika tu garini akajifungia vizuri akawasha ile video. Kevin aliitengeneza zikaonekana pande zote. Ile aliyopata vizuri akamtumia baba yake. “HAAA!” Zenda alishituka kwa sauti ya juu baada yakuona kitendo alichokifanya mwanae kwa mpenzi wake. Hakuamini. Alijua Kemi anaroho ngumu kama mama yake, lakini si kwa kiasi kile. Akatoa gari kwenda kwake. Akaoga na kula kisha akarudi ofisini. Hakumkuta mtu. Ila akakuta ofisi imesafishwa vizuri hakuna hata dalili kwamba ilimwagika damu pale. Akachukua mkoba wake wa kazi na kuwahi hospitalini akiwahi kumtoa Jema. Alimkuta na yeye amejilaza kwenye kochi. Akamshukuru na kuondoka, akabaki Zenda akifanya kazi za kiofisi pale.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi mida ya saa mbili na nusu akaingia hapo Jema, mama yao na James. Bado Jelini alikuwa amelala. Wakanong’ona wamuache alale. Mama Jema akamruhusu Zenda aondoke, yeye akasema atabaki mpaka mchana mida ya Jeremy kutoka shule. “Jeremy alilala na kuamka salama?” Zenda akauliza kwa kujali. Mama Jema ambaye hajazoea hilo akamwangalia kwa mshangao kidogo. Alishazoea kulea mwenyewe ila akamjibu. “Maswali mengi tu kwa mama yake. Na ni hivyo anaogopa hospitalini, ningemleta.” “Basi itabidi wazungumze jioni ili asizidi kuwa na wasiwasi.” “Naona hilo litakuwa bora.” Zenda akatoka na kina Jema nao wakaondoka kuwahi maofisini. Wakamuacha mama yao hapo.

Donge Limechachuka.

Alikwenda kwake kuoga na kuvaa kiofisi. Alifika ofisini kwa kuchelewa lakini akamuita Afisa mwajiri wake, Gele ambaye ni mwanasheria na Henry kiongozi wa kitengo cha IT. “Jana kulitokea tukio la kutisha hapa. Na mbaya zaidi lilimpata mpenzi wangu.” Hiyo nayo ikawa breaking Newz. “Alikuja nikiwa nimemkaribisha. Yakatokea yakutokea nikiwa nipo kikaoni. Nipo kutafuta ukweli kujua kilichotokea kwa hakika bila kujali aliyesababisha. Kwa sababu, moja kwa moja inagusa kampuni yangu, na mimi ambaye ni mpenzi wake. Sasa basi, nataka tuanze kumuhoji Sesi atuambie kilichotokea kisha Kemi ambaye alijibu askari.” Kila mtu akashituka. Kemi tena! Wakajua kimeshaumana.

    Kemi akafungua mlango baada ya kugonga mara moja. Wote macho mlangoni. “Nimesikia kuna kikao, nafikiri sikupata ujumbe.” “Kwa sababu hukutumiwa ujumbe.” Baba yake akamjibu. Pakazuka ukimya hapo. “Kwamba kuna kikao kinachoendelea hapa bila mimi kuwepo!?” Akauliza Kemi kwa mshangao lakini na cheko la wasiwasi kidogo. Baba yake akajivuta nyuma ya kiti, akakaa wima akimtizama. Kemi akaamua kutoka haraka.

Akanyanyua simu na kumpigia sekretari wake. “Naomba niitie Sesi.” Kisha akarudisha simu. Wakatulia. Sesi akaingia nakusalimia. “Tafadhali naomba ukae.” Akakaa. “Binti uliyempokea jana, na mwishoe akatolewa hapa na kitanda cha hospitalini, anaitwa Jelini. Ni mpenzi wangu.” Hapo akaweka kituo akimtizama Sesi machoni. Hofu aliyokuwa nayo Sesi, iliweza kuanza kuonekana. Mzee akabaki akimtizama. “Ndiyo.” Akaitika Sesi na kumeza mate akijiweka sawa kitini.

    “Nataka kujua ni nini kilitokea mpaka ukapiga kelele kuomba msaada. Na kabla hujaeleza, nataka kukukumbusha Jelini na kilichompata jana kinanihusu mimi moja kwa moja kama mmiliki wa kampuni hii na mtu wangu wa karibu sana.” Kimya Sesi akitetemeka maana Kemi alishamuwahi na kumwambia madhara ya kumchoma na faida za kutomsemea kwa baba yake.

    “Labda mimi niongeze.” Gele, mwanasheria wa kampuni, akaomba ruhusa akimtizama Kasa na kuendelea baada ya kuona hajakatazwa. “Sesi. Huyu binti amepatwa na madhara akiwa ndani ya ofisi zetu. Moja kwa moja sisi tunahusika na chochote kilichompata. Nikimaanisha, akiamua kushitaki hii kampuni, madhara yake si kwa mmiliki tu, hata sisi wote. Ukiongea ukweli, itatusaidia kujua jinsi ya kuzuia madhara yake.”  Jasho likaanza kumtoka Sesi ndani ya ofisi ya mzee iliyojaa upepo baridi uliochujwa. Hajawahi kuitishwa kikao humo tangia anaajiriwa. Leo anahojiwa na watu wazito wa kampuni!

“Sina muda wa kupoteza. Upo tayari kujibu hapa au unataka nikushitaki?” Akaongeza mzee Kasa baada ya ukimya wa Sesi.  Akaanza kutokwa na machozi, akifungua mdomo meno yanagongana. “Usiogope Sesi. Sema tu ukweli.” Mwajiri akamsihi kwa utulivu. “Chochote nitakachozungumza hapa kinabaki hapa au tena ndio kila mtu atajua?” “Itabakia kuwa siri ya uongozi tu maana tupo kwenye kujenga na sikubomoa.” Akamjibu yeye aliyeonekana anamtuliza si kumtisha.

    “Alipotoka tu kwenye lifti, akanifuata mimi moja kwa moja pale mapokezi. Akaniambia anamiahadi na bosi hapa. Nikampigia simu Shamsa, akasema nimwambie asubiri kidogo, umemwambia kuna kitu unamalizia. Mimi nikamkaribisha akae wakati akisubiria. Ndio Kemi akatoka kwenye kikao na kumfuata yeye moja kwa moja, akaanza kama kumfoka. Nikajua wanafahamiana.” “Alimwambia nini?” “Naweza nisikumbuke moja kwa moja maana walikuwa wakizungumza pembeni ya pale mapokezi, pale nilipokuwa nimemkaribisha. Ila nakumbuka kumsikia akimwambia asidhani atakulaghai wewe ili aajiriwe hapa. Yule…” “Anaitwa Jelini. Na acha kulia ili nikuelewe.” Mzee akaweka sawa. Sesi akajifuta machozi na kujaribu kutulia.

    “Nakumbuka kumsikia Jelini akisema, mimi nimekuja kumuona Ze..” “Anaiita Zenda.” “Ewaa! Akasema hivyo hivyo. ‘Nimekuja kumuona Zenda, sijaja kuomba kazi. Na sitaki ugomvi.’ Akasisitiza hivyo lakini Kemi hakunyamaza. Ndio Jelini akasema yeye hataki maneno wala ugomvi. Kwa kuwa hapa sijui alisema kwao au ofisini kwao, ninachokumbuka akasema yeye anaondoka. Wakati anasimama nafikiri alijikwaa kwenye mguu wa Kemi ndio akadondoka. Sasa nafikiri Kemi aliingiwa na hofu akakimbilia ofisini kwake na akasema yeye hakuwepo pale.” “Na wakati yeye ndiye aliyeambia askari kuwa Jelini ameanguka sababu ameshindwa kutembelea viatu virefu!? Alijuaje kama hakuwepo?” Gele akauliza kwa mshangao haswa.

    “Naomba niitiwe Kemi.” Mzee akainua simu na kuagiza. “Naomba Sesi utupishe lakini Kemi akiwa ameingia hapa.” “Kwamba umsubiri mpaka awe anaingia ndio utoke.” Akarekebisha Henry kumfanya aelewe. Akatulia kitini. Wakati Kemi anaingia Sesi akasimama na kutoka.

Kila Kazi Inamalipo Yake.

    Alipokaa tu akaanza Gele. “Jana kulitokea tukio ambalo najua unakumbuka. Naomba niende moja kwa moja kwenye madhara kwa upande wangu mimi kama muhusika wa kampuni.” Akamtizama. “Nakusikiliza.” Akajibu Kemi kwa kiburi. “Kwa upande wa kampuni, tukio limefanyika kwetu, ndani ya ofisi yetu. Kwa haraka sana, bila kipingamizi, yule binti akitushitaki, kampuni itaingia matatizoni kwa uchunguzi zaidi na pia anaweza kulipwa fidia ya mamilioni ya pesa kwa kiasi tutakachoamriwa na mahakama kwa sababu ya madhara atakayothibitisha daktari kuwa ameyapata hapa kwetu, na ikatulazimu kulipa.” “Sitamshangaa.” Akajibu Kemi, baba yake kimya.

    “Ulitoa kwa askari kwa kifupi kilichotokea. Tunataka kujua kwa undani ili kujua ni jinsi gani tutajipanga.” “Mimi niliongea nilichodhani.” “Kemi!” “Sasa unanikazania ukitaka kunisikia nikizungumza nini!?” “Basi rudia ulichosema kwa wale askari.” “Sikumbuki neno kwa neno.” Akajibu Kemi. “Labda mimi nikuulize Kemi, unakumbuka kuwa na mazungumzo yeyote na Jelini mara alipoingia hapa?” Henry akamuuliza taratibu tu. “Nilimsalimia kwa sababu nilishawahi kumuona kabla. Nikaona ananijibu mbovu, ndio nikaachana naye, nikaenda ofisini. Nikatoka niliposikia Sesi akipiga kelele.”

    “Kwa kuwa sina muda wa kupoteza, nakupa nafasi ya mwisho Kemi, useme ukweli. Madhara ya kudanganya zaidi kwangu, tena kwa mwanamke ninaye mpenda, ni mabaya, hutataka kuyapata.” “Yaani baba unamchagua yule mtoto dhidi yangu mimi! Unaitisha…” “Kemi. Hujawahi kuniona nikiwa nimependa na kupendwa kwa dhati bila hila. Sitaruhusu chochote kitokee kati yangu na Jelini. Na kukusaidia tu, mimi ndio mlengwa hapa moja kwa moja. Kwa sababu kwanza Jelini ananihusu mimi. Na mimi ndiye niliyemuita hapa. Hakuwa na mpango wa kuja kabisa hapa. Kingine, hii ni kampuni yangu. Mimi ndiye ninaye athirika moja kwa moja. Sijui kama unanielewa?” Kimya.

    Baba yake akabaki akimtizama. “Inamaana hukumbuki chochote ulichozungumza kwa askari?” Gele akamuuliza tena. “Sikumbuki.” Akajibu kwa jeuri. “Kemi, nakuuliza swali moja na la mwisho kwa kuwa unataka kutukwamisha sisi wote hapa. Unajua chochote kilichompata Jelini jana?” Baba yake akamuuliza kwa sauti ya kumuonya. “Sijui.” “Sasa kwa nini uwahi kujieleza kwa askari kilichompata Jelini wakati kumbe hujui chochote!?” Gele akashangaa sana. “Sasa unashangaa nini? Kila mtu alikuwa amepaniki jana.” “Mpaka kuzungumza kuwa amevaa viatu virefu na hajui kutembelea! Kweli Kemi!?” “Acha upuuzi Gele. Nani anaweza kuchukua usemi kama ule niliozungumza kwenye hali kama ile kuwa ndio kauli ya mwisho! Yule mtoto alitoka kunijibisha vibaya, nikaondoka pale nina hasira naye. Chochote nilichozungumza ni kutokana na hasira na paniki.” Kemi akajibu kwa kujiamini haswa.

    “Henry muwekee rikodi nzima ili kumsaidia na kumkumbusha sisi sio wajinga kama anavyozungumza na sisi.” Mzee akaongea, Henry akachukua rimoti. Hakuna aliyekuwa akijua kama hiyo video ilifufuliwa. Ila tetesi zilishaenea ofisi nzima kuwa, katika mazingira yasiyo kawaida, rikodi ya tukio zima tangia Jelini anafika pale ofisini mpaka kutolewa, haikuwepo.

Mbio Za Sakafuni.

    Kemi alishituka sana kuona kwenye video Jelini anatokea kwenye lifti na kuingia pale mpaka kupokelewa na Sesi, akaonekana Sesi kupiga simu na kumkaribisha akae. Kisha Kemi akajiona ametoka ofisini kwa baba yake na kumfuata Jelini pale alipokaa. Akaonekana anamuongelesha Jelini kwa jazba, Jelini akasimama akawa kama anaondoka, kisha ikaonekana tena kwa kurudia mara tatu, kama iliyotengenezwa makusudi vile alivyomtega mpaka kuanguka, kisha akakimbia. Palizuka ukimya wa gafla kama wamemwagiwa maji ya baridi. Wote walikufa ganzi maana wengine walikuwa hawajaiona hiyo video, kwanza hata hawakujua kama ipo, ila Henry tu.

Madhara.

    “Kwa kuwa umenidanganya hata nilipokupa nafasi ya kurekebisha, Kemi wewe ni hatari. Si kwa Jelini tu. Inamaana kwa mgeni wangu yeyote atakayekuja karibu na biashara zangu, akitaka kufanya kazi na mimi, halafu ikatokea hajaendana na wewe. Wewe ni hatari kwa wafanyakazi wangu na kampuni yangu pia.” Akaendelea mzee Kasa akitizama huyo binti yake.

    “Kuanzia dakika 5 zilizopita, wewe si mfanyakazi wa hii kampuni.” “Haiwezekani dad. Unanifukuza…” “Usiniingilie ninapozungumza Kemi. Unanisikia?” Kimya. “Askari watakusindikiza nje ya jengo hili na pochi yako itakufuata kwenye gari yako.” Kemi alikuwa ametoa macho haamini. “Huruhusiwi kusafiri nje ya nchi mpaka nitakapojua chakufanya na wewe kwa sababu kwa sasa nina mgonjwa hospitalini, na yeye ameomba mtu yeyote asijue kama ulimtega na kuanguka.” Wakashangaa sana.

    “Kabisa. Ndugu zake walipomuuliza ilikuaje, alisema amejikwaa akaanguka. Lakini baadaye kwenye mazungumzo tukiwa tumebaki wenyewe ndipo nikagundua anajua ni nini kilimpata kwa hakika. Na yeye mwenyewe ameomba nisimwambie hata mama yake, tena amesema nisije hata ropoka kwa mtu kwa sababu anajua hiki alichokisema Gele, ndicho atafanya mama yake kwa hakika. Ameniambia yeye anamjua mama yake. Endapo atajua ukweli, itakuwa mbaya sana. Amenisihi nisimwambie mtu.” Pakazuka ukimya.

    “Kwa hiyo Kemi, askari ataongozana na wewe mpaka nyumbani kwako, na utamkabidhi hati yako ya kusafiria. Huruhusiwi kuonekana kwenye jengo lolote lenye kampuni ya Kasa. Huruhusiwi kuwasiliana na wateja wa Kasa hata kwa salamu. Kazi na wateja wote wa kampuni ya Kasa, hawakuhusu tena. Na nakuonya katika hili usinijaribu kwa kuwa hao wateja wote, ni rafiki tuliojenga nao mahusiano tokea wewe ukinyonya. Kunihujumu kwa namna yeyote ile, ukiwauza wateja wangu, ni kosa ambalo litakugarimu zaidi ya hivi. Huruhusiwi kuzungumza kilichotokea hapa ndani jana na yeyote yule, Gele atatafuta jinsi ya kumalizana na vyombo vya usalama. Nataka kujua kama umenisikia na kama umenielewa kwa sababu nikimaliza hapa, utasaini haya makubaliano.” Kemi alikuwa kwenye mshituko, hakutegemea.

    “Kemilembe, umenielewa? Unaswali? Unapingamizi kwa hili? Maana safari hii ukikiuka chochote, ujue kampuni ya Kasa itakufungulia mashitaka. Kwa hiyo nataka kujua kama umenielewa.” “Nimeelewa ila naulizia malipo yangu kwa wateja wa huu mwezi?” “Natumia kulipia matibabu ya madhara uliyosababisha kwa Jelini.” Alimtizama baba yake kwa hasira, akasimama na kutaka kutoka. “Kutosaini karatasi atakazokuandalia Gele, ni KOSA. Na ninauhakika hutaki kunikosea zaidi.” “Utanifanya nini? Kunifukuza kazi tena?” Akamjibu baba yake kwa kiburi na hasira kali. “Ondoka bila kusaini ndipo utapata jibu la swali lako.” Wote wakabaki wakimtizama maana alisimama kama aondoke, lakini wakamuona anarudi.

“Zipo wapi hizo karatasi nizisaini?” Akauliza akimtizama Gele. “Nipe dakika 10 hivi nitakuwa nimekamilisha.” “Na usisubirie hapa tafadhali. Pale alipokuwa amekaa Jelini jana, ndipo unaruhusiwa kukaa mpaka utakapomalizana na Gele. Siku njema.” Wote wakasimama wakijua ndio wamefukuzwa hapo. Wanaume hao waliokuwa wamevalia wote nadhifu sana, wanaojielewa, wakatoka, Kemi akabaki amekaa.

    “Kuna simu za muhimu nataka kupiga.” Baba yake akamwambia akimaanisha na yeye atoke, ampishe. “Naomba nafasi unisikilize dad.” “Unanipotezea muda wangu wakati nilikupa muda wakuzungumza, ukawa jeuri. Acha kutumia muda wangu vibaya wakati mimi nina mgonjwa hospitalini. Umemdhuru vibaya sana yule binti. Najua una roho ngumu, lakini kitendo ulichokifanya nichakinyama Kemi, na mbaya zaidi akiwa hajitambui, eti bado unamsema kwa watu vibaya! Ondoka Kemi, na usinitafute mpaka nitakapokutafuta. Nenda katulie nyumbani pengine itakusaidia hata kuponya ndoa yako.”

    “Kwamba sasahivi mimi ndio mbaya, Noah ndio ameshakuwa mwema sababu ya Jelini?” “Unahangaika na yangu wakati ndoa yako wewe inakushinda! Ninachokwambia ni TOA MACHO YAKO KWANGU, hangaikia maisha yako, wanao na ndoa yako. Haya simama utoke kabla hujaniudhi zaidi. Maana neno jingine litakalokutoka mdomoni kwako bila yakutoka hapa, ni kunikaidi, na sikutanii Kemi. Utaumia zaidi ya hivi.” Akasimama na kutoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Inaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment