Wakamuona anahema kwa nguvu na
kumgeukia dakatri. “Vipi hali yake?” Akamuuliza. “Alipasuka sehemu kubwa ya juu
ya jicho. Juu ya nyusi.” Akawaonyesha. “Imebidi awekewe damu kwa haraka,
amepoteza damu nyingi sana. Na pia atahitaji damu zaidi.” “Mmepima vizuri hiyo damu mliyomuwekea lakini? Msije kuwa
mmemtibu mwanangu kwa kumpa maradhi mengine.” Mama wa Kichaga akaja juu.
“Damu zote wanazowawekea wagonjwa hapa…” “Acha
kunijibu kuhusu watu wengine. Namzungumzia mtoto wangu mimi na kile mlichompa.
Usinipotezee muda na majibu ya kiustaarabu. Maana baada ya hapa nitakuja
kumpima tena. Sasa ole wako uwe umempa magonjwa kwa damu uliyomuwekea. Hapo
utanijua mimi ni nani. Maana nitarudi hapa na vipimo.” Zenda akamtizama
mama Jema. Akakumbuka Jelini alishamsimulia habari zake. Akanyamaza kimya,
maana aliambiwa mdomo wake huwa hauna kumsitiri mtu tena anapokuwa amekasirika.
"Umenielewa?” Mama akamuhoji daktari
bila kupepesa macho ila kufuta machozi. “Maana huyu amepima na uthibitisho wake
kuwa hana magonjwa hatarishi ninao, nimetunza. Sasa ole wako.” “Damu
aliyopewa ni salama kabisa. Tafadhali usiwe na wasiwasi.” Akajibu kwa utulivu
tu akitaka na yeye huyo mama atulie. “Kichwa
kinauma sana, mama.” Jelini akalalamika akitokwa na machozi. “Pole
Jelini. Pole sana.” Zenda akamgeukia daktari. “Tutamuongezea tukifika wodini.
Naomba akapate sehemu ya kutulia. Kwa sasa hata mwanga unaweza kumuumiza
kichwa.” Wakatoka hapo wakimfuata nyuma, Zenda pembeni amemshika tu mkono.
Jelini akapewa huduma zote na kuachwa
apumzike. “Nashauri aachwe kabisa, apumzike. Huyu binti ameumia kwa hakika
maana mbali na kupasuka, pia amechimbika. Ameshonwa pakubwa na amepoteza damu
nyingi. Anahitaji ukimya kabisa, apumzike. Ataletewa chakula, msihangaike na
swala la chakula. Wanavyakula vizuri sana hapa.” Kimya, daktari na manesi wote
wakatoka akiwa amechomwa dawa ya usingizi. “Mama, usimsahau Jeremy. Ataogopa
akirudi asikukute.” Jelini akaongea amefunga macho. “Sasa na wewe hapa?” “Mimi
nalala. Naomba usimuache. Nenda tu ili asianze kulia peke yake.” “Halafu na
mimi nitakuwepo hapa. Na kama mlivyosikia wanatoa vyakula. Kama asipopenda,
nitaagiza kiletwe chakula kingine.” Zenda akawatuliza.
Jema akamsogelea Jelini. “Pole Jelini
wa mama Jema.” Wakamuona anacheka. “Usianze kunichokoza Jema bwana, mwenzio
naumwa.” “Na unavyoogopa hospitali!” Wakaanza kucheka. “Nilitaka kukimbia
nilipozinduka eti wananiambia wananipeleka hospitali! Wakanishika kwa nguvu,
wakaniambia nikitoka tu pale, damu ndogo iliyobaki itaisha yote mwili. Nikalala
mpaka hapa. Eti nafika kule kwenye chumba walikonishona, yule daktari anaanza
kuniambia watakachonifanyia, nikawaambia wamuite mama Jema, na
asiniambie kitu kingine, mimi naogopa sana. Wasiniguse tena mpaka mama Jema mwenyewe
atakapofika pale. Nikashangaa nimepotelea usingizini.” Wakacheka.
“Watakuwa walikupa dawa ya usingizi.
Pole Jelini mtoto mzuri.” Akacheka taratibu na kufunga macho. Jema akamfunika
vizuri.” “Nini kilitokea Jelini?” Mama yake akauliza. Kidogo Zenda akaingiwa na
wasiwasi. Maana alishajua haikuwa ajali ya kawaida. Akabaki ameshikilia moyo.
“Eti mama yangu?” “Nilijikwaa nikaanguka mama. Halafu nasinzia.” Zenda akahema
kwa nguvu. “Tukiwa hapa huyu hatalala, mama. Tumuache apumzike. Mimi nitarudi
kulala naye jioni.” “Naona mimi ndio nirudi, akili ndio itatulia.” “Bwana mama!
Usimuache Jeremy. Atalala na nani?” “Kweli.” Mama Jema akajirudi. “Au nimpeleke
kwa Mode?” “Sitaki mamdogo akae na mwanangu. Atamsahau tena, amfungie mwanangu
wakati akienda kwenye starehe zake. Nataka wewe ndio ubaki naye. Kwanza kesho
shule na ameshaanza kuzoea. Sitaki akose shule.” “Ni kweli. Basi unipigie usiku
ili nitulie. Umesikia Jema?” “Usiwe na wasiwasi mama. Mimi nitakuwa naye. Ila
acha nikurudishe nyumbani usihangaike na usafiri sasahivi.” Zenda akaona
kujaliwa kwa huyo mama.
Kwanza alionekana ni mama wa kawaida
sana. Lakini alizunguka wanae vizuri kweli. Na jinsi Jelini alivyokuwa
akimzungumzia mama yake kwake, Zenda mwenyewe alitegemea aje akutane na mama
kama Senetor wa Marekani. Lakini! Hapo hakuwa na kipodozi hata kimoja. Nguo alizovaa
za kawaida tu kama aliyekuwa kwenye shuguli zake za kuhaso tu. Hana cha
manukato wala urembo wowote wa hereni wala pete. Hafanani na mwanae hata mmoja.
Ila kwa jinsi alivyosikia sifa zake, na muda mfupi alivyojaa hapo, akiweka
ulinzi kwa wanae, Zenda mpenda vizuri, akapita muonekano wa nje mwenyewe akaongeza
heshima kwake.
“Wewe nenda kazini, mimi nitapata
usafiri hapo nje nitafika tu nyumbani, usiwe na wasiwasi. Usiharibu kazi.” Kisha
akawa kama amekumbuka kitu. “Wewe Jema! Nilipokupigia uliniambia upo hospitali,
kwema?” Jema akaanza kucheka. “Bwana mama ulikuwa unalia mpaka nikaingiwa hofu!
Nikamwambia James, mama Jema analia, leo maji yamemfika shingoni. Si kawaida
yake.” “Niliogopa sana. Maana huyu nilitoka kuzungumza naye muda si mrefu.
Tukaweka mipango mizuri tu. Tena nikamsifia maana nilimtuma usiku, nikashangaa
alfajiri anaamka na kujiandaa kabla ya mwanae, kisha akamuamsha Jeremy na
kumtaarisha akaniambia anampeleka mwenyewe shule, ili waongee njiani. Kisha
anakwenda nilikomtuma usiku. Kuja kupata simu eti yupo chumba cha upasuaji,
nikajua mwanangu amekufa. Ndio alikuwa kama anamuaga Jeremy. Mengi yakapita
kichwani vile alivyokuwa asubuhi, basi mimi moja kwa moja nikajua atakuwa
alikuwa akituaga.” Wakacheka.
“Kwema lakini?” Akashangaa
wanaangaliana na James. “Jema ni mjamzito.” Akajibu James na kumfanya mpaka Jelini
afungue macho. “Hongera Jema.” Jelini akafungua macho. “Asante. Nimefurahi mama!”
“Hongera sana. Basi sisi tukawa tunakusema na Jelini. Mbona Jema asiyependa
unene, haishi kutafuna!” Wakacheka sana. “Nakula mama, halafu sishibi mpaka
tumekubaliana na James niongeze matunda zaidi
maana nitapasuka.” “Hongera sana. Ila usiwe na wasiwasi na mwili sasahivi.”
“Jema na unene huyo, huna utakalomwambia.” Jelini akaongeza. Wakacheka.
“Sasa kwa nini hospitalini?” “Tulikwenda kwa
kliniki tu. Safari hii na mimi nilitaka kuwepo maana mara ya kwanza nilishindwa
kwenda. Akaenda peke yake. Lakini nimefurahi kila kitu kipo sawa. Nimemuona na
mtoto wangu. Mapigo ya moyo ya nguvu.” James akaongea kwa furaha. “Hongereni
sana James.” Jelini akasikia sauti ya Zenda. “Zenda! Kumbe bado upo?!” “Nipo,
siwezi kuondoka na kukuacha hapa.” “Mbona sasa upo kimya? Njoo.” Jelini
akamuita kwa upendo. “Pole sana.” Akajisogeza mpaka pale kitandani. “Acha
kuongea kwa huruma bwana! Mimi nitapona tu. Njoo na unishike mkono.”
Akajisogeza karibu maana alikuwa akihofia ndugu wa Jelini.
“Basi sisi tuende, tutarudi baadaye.”
“Tafadhalini msiwe na wasiwasi. Nitakuwa naye hapa.” Pakazuka ukimya kidogo.
“Kukiwa na chochote nitawajulisha kwa haraka kama nilivyofanya leo. Vinginevyo
msiwe na wasiwasi kabisa. Jelini atakuwa sawa. Na nitahakikisha wanamuangalia
kwa karibu.” “Sawa. Ila usijisikie ni lazima. Mimi naweza kuja wakati wowote
endapo itakulazimu kuondoka.” “Hata kama nikutoka itakuwa kwa muda mfupi, kisha
nitarudi. Asubuhi mama akirudi, mimi nitatoka kidogo na kurudi wakati mama anatoka,
ili tusimuache Jelini peke yake.” Wakakubalina. Wakatoka wakimuacha Jelini
alale.
Uongo Hujitenga Na Ukweli, Ni Muda Tu.
“Pole Jelini wangu.” Jelini akafungua
macho akamuona anaanza kulia. “Naomba usilie mpenzi wangu, utapona.” “Lakini mtoto wako angeniua, tena bila kosa, Zenda!”
Akashituka sana, hakujua kama anajua kilichotokea. “Kemi? Alifanyaje?” Akauliza
kwa shauku akijua ukweli utagundulika sasa. “Alinitega
makusudi kwa mguu. Ndio nikajikwaa. Tena baada ya kuniparamia kwa maneno
mabaya. Nilipoona hanyamazi na pale ni kwao..” “Pale si kwao. Ile ni
kampuni yangu mimi, aliyoikuta hapa duniani. Ehe?” Akaongea kwa jazba.
“Mimi sikutaka ugomvi maana
niliona ananidhalilisha bila sababu. Nikasema niondoke tu. Ndio wakati nampita
maana alinisimamia mbele ya kiti nilichokuwa nimekaribishwa, ndio akanitega kwa
mguu nikaanguka. Ila usimwambie mama. Mama yangu atamfunga au kumlipiza
kisasi kibaya sana kama alichomlipiza aliyekuwa mchumba wa Jema, akamdhulumu
Jema nyumba. Ila Jema hajui kama mama amemlipiza kisasi. Mama hapendi
mtu atuonee. Ndio maana mimi nimemwambia nilijikwaa na kuanguka
tu.”
Mwili mzima wa Zenda ukajawa hofu na hasira. Jambo hilo likija kugundulika,
mwanae yupo matatizoni hata kisheria. Na nishitaka baya sana hata kwa kampuni.
“Samahani sana Jelini.” “Wewe hujakosea Zenda. Usijisikie vibaya.” Akamfuta
machozi kwa tahadhari asimtoneshe. “Hapana. Mimi ndiye niliyekuita bila kuandaa
mazingira mazuri kwako. Najihisi nimehusika. Nisamehe mpenzi wangu.” “Basi ni
busu ndio nitakusamehe. Umeingiwa hofu mpaka nimekuona!” Japokuwa alishahisi
Kemi anahusika, lakini hakujua kama amefanya kwa ukatili wa hali ya juu kwa
kiasi hicho! Akaumia sana. Akainama na kuanza kupata denda taratibu. “Unanuka
damu Zenda!” “Ni zako hizi. Nilishituka Jeilini. Sijawahi ogopa hivi maishani.”
Machozi yakaanza kumtoka.
“Nilitoka ofisini
nikihofia isije kuwa ile kelele ni ya Sesi kuomba msaada kuhusu wewe!
Mbaya nimetoka, nimekukuta umelalia dimbwi la damu! Kukunyanyua, damu zinatoka
kama mvua! Niliogopa sana.” “Pole mpenzi wangu. Itakuwa nilijigonga vibaya. Lakini
usijejisahau ukaropoka hili kwa mama Jema. Hutampenda.” “Nashukuru
kujali.” Jelini akafunga macho, hapohapo akapotelea usingizini.
Ubaya Hauna Kwao.
Alipojiridhisha amelala akatoka
barazani upande wa bahari kwenye hicho chumba alicholazwa Jelini. Moja kwa moja
akajua ni kazi ya Kevin mtu anayejua kucheza na mitandao. Mwanae alisomea
kilekile alichosomea James, lakini yeye alijiongeza zaidi. Kwahiyo Kevina
akishika kompyuta, anaweza kufanya chochote kitokee. Akaanza kwake.
Alimpigia simu ikaita mara moja tu. “Kwa kumsaidia Kemi kufuta ile video, unajua kama umeshiriki
kwenye kusudio la kutaka kuua?” Mzee akatumia akili na kuruka moja kwa moja kwenye tuhuma.
“Kemi hakuniambia ni video ya nini baba. Ila alitaka
nimuelekeze jinsi ya kuitoa kwenye system, na isionekane kama hata ilishawahi
kutokea.” Akawa amethibitisha maneno ya Jelini. Kevin ameshatoa ukiri. “Nilikwambia nini juu ya kufanya jambo bila kuuliza au
kufikiria? Ni mara ngapi unataka nikwambie ili ujifunze?” Mzee
akawaka. “Baba unanionea bure. Kemi alinipigia simu
akisema ni msaada anaoomba wa kiofisi kwa kuwa timu yenu ya IT imekwama na si
mara moja kupata simu za aina hiyo baba yangu. Huwa nawasaidia tu.” “Ulishawahi
kupigiwa simu kuomba alichokuomba leo Kemi?” Kimya.
“Kevin?” Aliita kwa ukali
sana. “Nakusikiliza baba.” “Kwa akili yako ilivyo, hapo
ulipokaa, wewe unafikiri kukata video ya matukio yaliyokuwa yakiendelea
ofisini, hazikuwa sababu za kiusalama kweli, na Kemi asingejihusisha kwa sababu
hausiki, pengine Gele ndio angekupigia?” “Alisikika na haraka baba, nikakosa
muda wa kufikiria.” Simu ikakatwa. Kwa hakika Kevin alijua yupo
matatizoni.
Taka Cha
Mvunguni.
Pesa Ya
Bure Tamu.
Akajua kwa hakika matokea ya
alichokifanya, hatayapenda kabisa. Mbali ya kuwa ni baba yao, lakini pia ni kama
kitega uchumi chao. Lazima kujirudi kwa haraka. Tena kujirudi kwa uhakika. Akafikiria
chakufanya kisha akampigia simu baba yake kwa haraka sana. Haikupokelewa. Akamtumia
ujumbe. ‘Kama ukiidhinisha kuruhusiwa nikaingia kwenye
chumba kinachotunzwa rikodi zote, nina uwezo wakurudisha ile video.’ Zenda
akasoma huo ujumbe na kujibu. ‘Kemi asijue kabisa. Na
ninataka iwe kwenye simu yangu pia.’ ‘Sawa baba. Ila mimi sijashiriki chochote
na ninaweza kwenda baada ya kazi, wafanyakazi wote wakiwa wameshaondoka.’
Hakujibiwa, kwa hiyo akajua ndio ameambiwa aende.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akampigia simu kiongozi wa kitengo cha
IT. Akapokea kwa haraka. “Kevin atakuja baada ya kazi,
kujaribu kupata hiyo video iliyofutwa. Tafadhali mtu yeyote asijue
kinachoendelea. Ibaki kwako tu.” “Sawa. Nitamsubiri mimi mwenyewe.”
Akakata simu na kurudi ndani. Jelini alikuwa amelala, hana habari. Zenda akakaa
hapo akiwaza.
Madaktari walikuwa wakiingia na kutoka wakipokezana hapo
alipolazwa Jelini ilimradi tu, huduma kwa daraja la kwanza chochote
kisiharibike. Akaongezewa tena damu, Jelini akawa amelala tu. Akiwa amepotelea
mawazoni, peke yake ndani ya chumba hicho mwanga hafifu mida ya saa moja na
nusu usiku ujumbe ukaingia. Akachukua simu. Akakuta video.
Wakati anataka kufungua hiyo video aangalie, Jema akaingia.
“Nimekuja kukaa naye kwa muda, ili na wewe ukaoge na kubadili nguo.” “Nashukuru
Jema. Sitakawia kurudi.” “Mimi naweza kukaa hapa mpaka kwenye saa nne. Kwa hiyo
fanya mambo yako taratibu.” “Sawa. Ila anaendelea vizuri. Wamemuongezea damu
ndio inakwenda taratibu.” “Maumivu ya kichwa?” “Hajalalamika tena. Wanajitahidi
yasirudi na nafikiri wanampa dawa kali kidogo ndio maana analala sana. Usiwe na
wasiwasi.” “Nashukuru.” Jema akatafuta sehemu akakaa, macho kwa mdogo wake,
Zenda akatoka kama akimbie.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment