“Jelini umependeza! Ukiambiwa nakula tu kwa
macho!” “Tena chupi niliyovaa hapa, ni kuitoa tu kwa kidole, kila kitu chako.” Hali ikawa ishakuwa
mbaya. “Kwamba hata sasahivi naweza kupata?” “Wewe tu
na muda wako.” “Acha masihara Jelini!” “Nihivyo upo ofisini na sipafahamu na
wewe ni bosi. Ingekuwa vinginevyo ningekuja kukuinamia mezani. Ukitosheka mimi
nakuacha ufanye kazi.” “Kwamba unaweza kuja hapahapa
ofisini!?” “Ila uache mabao yako ya kelele.” Zenda alicheka sana. “Wewe mtoto mtamu sana bwana!” “Nakuja kukurekebishia
chapuchapu.” “Nakushukuru. Njoo.” Jelini akashangaa ule utayari.
“Sasa huofii macho ya wafanyakazi wako na Kemi?”
“Wapo mjini kwa jasho langu. Waache upuuzi na kuninyima starehe. Njoo Jelini
wangu. Tena naweka mazingira ya lisaa zima nisisumbuliwe.” Akamuelekeza Jelini
akicheka hana mbavu. Ila akampigia simu mama yake, akampa majibu mazuri, mama
yake akaridhika. Akamwambia anakwenda kumuona Zenda, atamtafuta baadaye. Mama
Jema hakuwa na shida. Bora sio kumsaliti Zenda maana huo ndio ulikuwa wasiwasi
wake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ukweli Jelini alipendeza haswa, mwili wake mzima ulitangaza
utajiri wa Zenda, ungependa kumuangalia. Aliacha harufu nzuri kila alipopita mpaka
akafika kwenye jengo zilipo ofisi za Zenda. Askari aliyemkuta chini akamuandikisha
jina lake, na muda alioingia kwenye hicho kitabu cha wageni alichokikuta hapo
mapokezi na kumuelekeza zilipo lifti, akapanda. Yeye mwenyewe akaanza kujiona kipanzi
jinsi madhari ilivyokuwa. Ofisi ilikuwa safi, kila mtu anayo suti na tai,
wanawake ndio utafikiri ni watangaza bidhaa za urembo. Safi kiofisi. Na
hakuwepo mshangaaji hapo anayezagaa hovyo. Akaanza kubabaika. “Inamaana wote
hawa wamesoma!” Akaanza kujishuku na kujihisi hayupo sehemu sahihi. Hayo
mazingira yalimkalia tofauti haswa. Jelini mtoto wa mtaani, hakuwahi kuingia
maofisini! Anatafuta nini?
Akamsogelea sekretari, akajitambulisha kwa jina la Jelini
tu. Akawa na taarifa zake tayari kama aliyekuwa akisubiriwa. Akamwambia asubiri
kidogo tu, mzee anamalizia kikao na viongozi wa hapo. Akakaa na kutulia. Akaona
mlango wenye warembo wawili nje, kama na wao ni masekretari wa hiyo ofisi hapo
ndani, unafunguliwa. Akaanza kutoka mwanaume mtanashati haswa. Alionekana
amejaa mamlaka. Akatoka na Kemi na sura yake ambayo haijuilikani kama amefurahi,
au amekasirika.
Shari Imfuatayo Mtu, Bila kujua.
Alipomuona Jelini akapandwa na kitu rohoni. “Wewe
mtoto unafanya nini hapa?” “Mimi nimemfuata Zenda.” Akajibu Jelini bila hofu. “Hizi
ofisi wanakuja watu wenye elimu zao.” “Mimi sijajakuomba kazi. Nimemfuata
Zenda.” Akarudia Jelini. “Sasa kama unafikiri utamdanganya ili akupe kazi hapa,
ujue utakumbana na mimi na nitakutaka vyeti na ufanye kazi kama kawaida.
Usilete uswahili.” Akamsogelea karibu kabisa akimtisha. “Mbona wewe una mambo
ya ajabu hivyo! Ukoje wewe? Yaani unanikuta tu hapa na kuanza kuniparamia, wewe
vipi!?” “Acha uswahili kwenye maofisi ya watu.” “Mimi sipendi ugomvi na mtu. Na
kwa sababu nimekukuta, acha mimi ndio niondoke.” Jelini akasimama, ile anampita
tu, akamtega na mguu makusudi.
Jelini alinguka vibaya sana, akagonga uso kwenye kona ya
meza ya kioo nzuri sana iliyokuwa mahususi kwa magazeti kwa wageni wao wakiwa
wanasubiria kuingia maofisini.
Kilichoonekana hapo ni damu kuruka kama
bomba, akapiga kelele kidogo, akazima. Sekretari akawa anapiga kelele akiomba
msaada, Kemi akakimbilia ofisini kwake. Kila mtu ndani ya hiyo ofisi mpaka
Zenda wakatoka maofisini kwao kufuata kelele ya sekretari wa mapokezi.
Wakakuta mrembo amelala fudifudi uso kwenye dimbwi la damu
kila mtu akashituka sana. Kwa haraka sana Zenda akakimbilia pale na suti yake
nyeusi na shati jeupee, akamnyanyua huku akiamuru gari ya hospitalini iitwe.
Kumgeuza hivi, uso mzima wa Zenda ukarushiwa damu kutoka
kwenye kipanda uso cha Jelini aliyekuwa amezimia, hajitambui. Shati lake jeupe
ndani likawa damu tupu. Akamfunika pale panapotoa damu kama bomba, kwa kuminya
na mikono yake miwili. “Nataka taulo safi kutoka chooni kwangu.” Akaamuru.
Sekretari akakimbia na kwenda kumletea. Akatoa mkono mmoja na kuweka taulo kwa
zamu. Akafunga kwa nguvu kuzunguka kichwa, damu ikakata, akakaa kabisa pale
chini kwenye damu, na kumuegemeza kichwa chake kifuani kama kufanya kichwa
kusimama kidogo. Kila mtu akabaki akimwangalia jinsi anavyomfanyia huyo binti
tena kwa makini, wasielewe.
Askari walishafika. “Kuna nini?” Askari mmoja wao kama
kiongozi wa ulinzi akahoji. “Nafikiri hajazoea kuvaa viatu virefu,
amejikwaa wakati anatembea, akaanguka na kujigonga kwenye meza. Ameumia usoni.”
Akadakia Kemi kwa haraka akiwa mlangoni mwa ofisi yake. Wote wakamgeukia yeye.
Zenda kimya akijaribu kumshika Jelini vizuri. “Hata Selina alimuona.” Akaongeza
msisitizo kama anayetaka atetewe na huyo Selina ambaye ni sekretari aliyempokea
Jelini na kumwambia asubiri mpaka alipotokea Kemi na kuanza kumbwatukia, ndipo
akaamua kuondoka na kumsababishia yote hayo.
“Gari ya wagonjwa imefikia wapi?” Akauliza Zenda kwa ukali.
“Nahitaji gari ya wagonjwa sasahivi.” Zikaanza simu kila mtu akitafuta msaada,
mzee amelowa damu chapachapa. Baada ya muda lifti ikafunguka na kitanda cha
wagonjwa kikaingia hapo. Wakawapisha mpaka wakafika pale alipokaa Zenda akiwa
amemshikilia Jelini. “Anavuja sana damu. Nikitoa hili taulo nililomfunga
kichwani, damu zitaruka kila mahali. Na amepoteza fahamu.” Wakaweka umakini
kumtoa mikononi kwa Zenda bila kusababisha kupoteza damu zaidi. Wakajaribu
kumuamsha huku wakimuweka sawa. “Anaonekana amepoteza damu nyingi sana kwa
wakati mmoja.” Wakatoka kwa haraka Zenda akifuata nyuma kwa haraka akiwa na mkoba waJelini.
Hakuna Ajuaye Kesho wala baadaye yake.
Jelini alifikishwa hospitalini na kuingizwa chumba cha
upasuaji kwani taarifa zake zilishafika kabla yao kufika kuwa amepasuka sana
kwenye paji la uso. Wakati yupo ndani
chumba cha upasuaji Zenda amekaa akisubiri ndio akili ikamjia, Jelini ni
binti wa mtu na alimwambia alitumwa na mama yake. Akatoa simu ya Jelini ili ampigie
simu mama yake amtaarifu habari za Jelini. Lakini simu yake ikawa imefungwa.
Inafunguliwa kwa macho ya Jelini au namba ya siri. Akakwama maana hakuwahi hata
kumuona mama yake Jelini na hakuwa na namba zake. Ila wazo likamjia ajaribu
namba ya siri. Akazungusha ‘Jeremy’ kwa
kuunganisha herufi, ikakataa. Akashangaa sana. “Sasa kama sio mtoto wake, itakuwa
nini?” Akawaza.
Ndipo wazo likamjia ajaribu ‘Zenda’
huku akijicheka kwa kujidharau. “Aniweke mimi kama namba yake ya siri!” Akajikebehi
huku akiweka ‘Zenda’. Akashangaa imefunguka.
Alishituka mpaka akasimama. “Yaani mimi ndio namba yake ya siri!?” Alijiuliza
kwa mshangao akijisikia kumpenda zaidi Jelini. Akafungua na kutafuta namba.
Alipoona tu mama Jema, akajua ndio mama yake. Akampigia.
“We Jelini?” “Mimi ni Kasa, lakini Jelini ananiita
Zenda.”
Pakazuka ukimya. Alitegemea na kuzoea. Watu wanaomjua yeye, wakimsikia kwenye
simu hupatwa na mshituko. “Nimepiga na taarifa zisizo
nzuri lakini tafadhali usiogope. Jelini ameanguka vibaya sana na amepasuka
akiwa anasubiria kuniona. Sasahivi tupo hapa hospitalini yupo chumba cha
upasuaji, anashonywa. Naweza kukutumia dereva aje kukuchukua kukuleta.” “Yesu!”
Alisikika mama Jema. “Pole sana.” “Ni wapi?” Akamtajia
hospitali waliyokuwepo. “Siwezi kusubiria huo usafiri.
Nakuja.” Simu ikakatwa.
Kwa mara ya kwanza mama Jema akalia kwa hofu kubwa na ya
ajabu ambayo haijawahi kumpata kabla. Watoto wenyewe wawili tu! Akampigia simu
Jema akilia sana. Jema akashituka na kumwambia walikuwa hospitalini na James,
wanakwenda hapo. Baada ya muda mfupi Zenda akashitukia anasimamiwa na hao watu
watatu aliowatisha sana. “Yaani hiyo yote ni damu
ya Jelini jamani!?” Ndipo akajitazama. Ameloa chapachapa. “Sasa yeye atakuwa amebakiwa na damu kweli?” Mama
yake akauliza kwa wasiwasi akiendelea kulia. “Kwani ilikuaje?!” Jema akamuuliza
kwa wasiwasi zaidi.
“Mimi nilikuwa nikimalizia kikao cha mwisho, ndipo
niliposikia kelele sekretari akiomba msaada. Nilitoka kwa kukimbia nikihofia asijekuwa
Jelini maana nilikuwa nikimtegemea. Ndipo nikamkuta ameanguka. Inavyoonekana
aliangukia meza ya kioo iliyompasua sehemu ya kipanda uso. Ila nataka
kuwahakikishia, yupo na wataalamu wazuri sana, kuhakikisha anatoka salama.
Naomba tutulie.” Kimya. Lakini swali la Jema likamfanya Zenda afikirie zaidi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alimpigia sekretari wake na kumuagiza amwambie Sesi msichana
wa mapokezi kuwa anatarajia mgeni. Akifika Jelini, akaribishwe na ataarifiwe yeye
moja kwa moja, wakati akimalizia kikao. Zenda akakumbuka kupokea simu kutoka
kwa Sesi kuwa Jelini amefika. Kidogo akapatwa wasiwasi alipokumbuka maelezo ya
Kemi. Wasiwasi ukamzidia moyoni. Zenda anaakili ya kufikiria sana na ndio
chanzo cha utajiri wake. Maana Kemi alikuwa kama akijitetea japo hakumkuta eneo
la tukio. “Kama hakuwa pale, alijuaje kama Jelini alivaa viatu virefu
vilivyomsababisha kuanguka!” Akawaza Zenda.
“Kwa nini alizungumza vile akitaka na
ushahidi na wa Sesi?”
Akazidi kuwaza kadiri sauti ya Kemi ilivyokuwa ikijirudia kichwani mwake. Hofu ya
isijekuwa binti yake ndiye amesababisha hiyo ajali ikaanza kumnyemelea! Kwanza
tayari amehatarisha maisha ya Jelini. Pili ameshaingiza doa ofisi yake na
kampuni kwa jumla. Mambo yanasambaa. Itajulikana ajali mbaya iliyompata Jelini
ndani ya ofisi yake! Akabaki ameinama kimya lakini mengi yakiendelea kichwani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Pengine ungeenda kutoa hizo nguo na kujisafisha.” Zenda
akamtizama James kama ambaye hajamuelewa. Maana alimtoa katikati ya dimbwi la mawazo.
“Umejaa damu mpaka usoni, mikononi kila mahali. Pengine ungeenda kujisafisha na
kubadili nguo.” Akajiangalia vizuri mpaka mikono ilikuwa imejaa damu. “Siwezi
kuondoka hapa kabla sijamuona Jelini. Hawezi akatoka asinikute mimi hapa.” Wote
wakabaki wakimwangalia. “Basi nashauri angalau ukaoshe uso na mikono. Inatisha
na kuogopesha.” Zenda akasimama kwenda kutafuta choo cha kiume.
Baada ya muda wakamuona anatoka akiwa kweli ameosha uso na
mikono, ila hakurudi pale akawa kama anaelekea nje ya hilo jengo la upasuaji.
Alikwenda kwenye gari kutoa nguo za juu. Koti la suti na shati la ndani
lililokuwa limejaa damu. Huwa nyuma ya gari yake hutembea na nguo za akiba. Akavaa
tu shati jeupe bila tai, akafungua vifungo viwili vya juu, akakunja mikono.
Mzee akabadilika akawa vizuri.
Ujanja Kuwahi!
Akiwa kwenye gari yake akampigia simu kiongozi wa kitengo
cha IT kwenye kampuni yake. “Henry, sitaki uzue wasiwasi
hapo. Lakini nataka uvute kamera zote. Kila kona, unitunzie video kuanzia
Jelini anaingia mlangoni kule chini, anapokelewa na askari pale chini mapokezi,
kuletwa na lifti mpaka juu, na mpaka kufikia vile wote tulivyomkuta sakafuni.
Isikosekane hata sekunde ya yeye alipokuwepo kwenye jengo langu. Na nataka
ufunge chumba kinachohifadhi hizo kumbukumbu.” “Nina
habari mbaya kidogo mzee wangu. Askari walirudi hapa na kutaka kitu kama hicho ulichoniagiza
wewe sasahivi hapa. Wakitaka kuweka kwenye ripoti yao kujua kwa hakika
kilichoendelea wakiwa wameshachukua mazungumzo ya Sesilia. Walipowaleta kwangu
niliwakatalia, kwa kuwa kisheria nilijua nipo sahihi lakini pia nilitaka
tuzungumze na wewe kwanza. Kwa hiyo niliwajibu tu kwa haraka kuwa wewe haupo na
hatuwezi kufanya chochote mpaka utoe idhini.” Zenda kimya akitaka kujua
hiyo habari mbaya, maana mpaka hapo hiyo ni habari njema.
“Walipotoka mimi mwenyewe nikaenda kuangalia kama
ulichosema, nilishangazwa kukuta kamera zote zinafanya kazi, lakini hakuna
rikodi ya huyo msichana kuwepo kwenye hili jengo kabisa.” “Sijaelewa!” Zenda akahamaki
kidogo. “Hakuna kumbukumbu zake kwenye kamera. Yaani
muda yeye anaingia kwenye hili jengo haonekaniki kabisa. Hamna.” “Kwamba
imefutwa!?” “Kwa uzoefu wangu, kuna mtu anayejua nini anafanya, amefuta kabisa.
Ila alichofanya, amerekebisha muda kiasi ya kwamba kama huna uelewa na una
haraka ukiangalia kwa haraka huwezi kujua kama hicho kipengele kimekatwa.”
Zenda akashituka sana.
“Haiwezekani! Nani mjinga wa
kiasi hicho anayeshindwa kufikiria kwamba huyu binti ameonekanika kuanzia
kamera za nje ya jengo, za kampuni ya ulinzi na..” “Si hivyo tu Kiongozi. Hata
hili nimemwambia Gelement, ajiandae kisheria. Nikidhani kama anahusika akitaka
kuwahi kufunika jambo kuokoa kampuni, maana huyu binti ametolewa hapa na
watu wa hospitali, tena na gari la hospitali akionekana wazi amedhurika.”
“Kwamba taarifa ya kilichotokea kwake hazipo tu kwetu zipo mpaka hapa
hospitalini!”
Akaongeza Zenda kwa hasira.
“Lakini nimekuja kugundua si
Gele. Kumbe yeye ni muoga sana wa damu. Ile kumuona vile yule binti, alishituka
sana. Anasema alikuwa akitapika muda wote. Hata kufikiria hilo ilikuwa bado. Kwa
kifupi si yeye kwamba amefanya kwa ajili ya kutunza sifa ya kampuni. Na
aliyefanya anaonekana alifanya haraka, kitaalamu sana, lakini hakufikiria mbali
sababu ya haraka.”
Simu ikakatwa. Lakini kwa akili yake Zenda ilivyo, akawa ameshajua hiyo ni kazi
ya nani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaamua kurudi ndani maana yote hayo
aliyafanya sehemu ya kuegeshea magari. Anarudi ndani akaona Jelini ametolewa
ila mama yake analia sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nani Amefuta Kumbukumbu Za Jelini Akiwa Mjengoni?
Je, Ni Kazi Ya Nani Akisaidiwa Na Nani?
Je, Zenda Atafanikiwa Kupata Uthibitisho Wa Kilichotokea? Maana Kwa
Sasa Ni Maneno Ya Jelini Against Kemi.
Je, Ukweli Na Uthibitisho Vitaendana Kuhakiki Alichosema Jelini Kupingana
Na Alichosema Kemi Tayari Akiweka Ushahidi Wa Sesi?
Zenda Atafanyaje Kabla Na Baada Yakujua Ukweli Juu Ya Binti Yake
Kipenzi?
Jelini Amepatwa Na Nini Akiwa Chumba Cha Upasuaji?
Usikose
Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment