Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 19. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 19.

Jelini alikasirika sana maana hayo Kevin alikuwa akiyazungumza mbele ya wote mpaka wale watoto! “Twende Jelini.” Jelini akaanza kutokwa na machozi kwa hasira na kushindwa kusogea. “Kwani uongo? Mpigie simu Zilo, atakwambia Kemi. Huyu mtoto anatafuta kwenye hela. Inamaana hapo kashamlia pesa Colins, ndio yupo hapa.” “Mimi siondoki hapa Zenda, mpaka umpigie simu Colins umuulize kama mimi nishakuwa na mahusiano naye.” Jelini akaongea akilia ila wakashangaa ni kama anamuamuru mzee!

“Nipe simu yako.” Baba yake akamuamuru Kevin, akabaki akimwangalia. “Sitarudia mara mbili, Kevin. Na unipe ikiwa haina namba ya siri.” Akatoa na kumkabidhi. “Ipo namba ya Colins humu?” “Huyo atakua nayo.” Ikimaanisha Jelini. “Usinizungushe Kevin. Nataka namba ya Colins.” “Yaani wewe unamsikiliza huyu mtoto malaya tu? Atakuwa anakudanganya.” “Kwanza anaonekana ni msichana wa uswahilini tu. Hamna shule kichwani.” Kemi akaongeza nguvu, baba yao akawatizama wote wawili na kurudisha macho kwa Kevin, kisha akaanza kupekua namba mpaka akaipata namba ya Colins.

Mzee akaenda hewani akiwa kwenye spika wote wanasikia. “Kwema Mkuu?” Sauti nzito, nzuri na tulivu ya kiume ikasikika. Colins akijua anazungumza na Kevin. “Mimi naitwa Kasa, baba yake Kevin.” Colins akashituka akanyamaza. Kimya. “Upo Colins?” “Nipo mzee wangu, shikamoo.” “Marahaba.” Kemi alivyosikia tu hivyo akajua mzee amekasirika, akawapa vijana wake funguo, watangulie garini. Wakabaki wao tu.“Unamfahamu Jelini?” Kidogo pakazuka ukimya. Ila alishazoea. Wengi hufa ngazi wakijua ni yeye ndiye yupo upande wa pili wa simu. “Colins!?” “Najaribu kufikiria. Maana Jelini ninayemfahamu ni mdogo wake Jema, mke wa James ambaye nipo naye ofisi moja. Wanaishi Tegeta. Kama ni huyo, hata Kevy anamfahamu. Kwa haraka ndiye huyo Jelini ninayeweza kumkumbuka. Sasa sijui kama ndiye huyo unayemzungumzia wewe mzee wangu?” “Ndiye huyohuyo.” “Basi James atakuwa na taarifa zake zaidi. Ni mdogo wake Jema. Mimi naweza nisiwe na taarifa zake zakutosha, maana kama sijakosea binafsi nilikutana naye kama mara tatu hivi. Na mara zote ilikuwa ni kwenye shuguli za kufanikisha ndoa yao. Jema na James. Otherwise, naweza nisiwe msaada zaidi. Samahani.” “Haina shida. Nashukuru sana.” Mzee akakata simu.

Wakashangaa anamgeukia Jelini. “Umeridhika?” “Haaa!” Kemi akashindwa kujizuia, akashangaa kwa sauti kabisa. “Mimi sio malaya.” Jelini akaendelea kulia kwa hasira. “Mimi najua. Nimefanya hivi kwa ajili yako wewe, wala si yangu au mwingine yeyote yule kwa sababu wote tunajua, Kevin amedanganya kukuchafua tu, sababu ulimkataa. Na Kemi hayamuhusu kabisa. Nimefanya hili nikitaka wewe uridhike tutoke hapa. Si tunaweza kuondoka sasa?” Mzee akauliza akibembeleza haswa mpaka kushangaza wanae kwa kiasi kikubwa mno. Jelini akatingisha kichwa kukubali. Akamkabidhi Kevin simu yake. “Muwe na jumapili njema.” Wakaondoka na kuwaacha wakishindwa chakuongea.

Kisasi.

Wakati Jelini akibembelezwa na Zenda huko kwake, huku mama Jema anafanya yake. Alishakamilisha upelelezi wake, akahakikishiwa mwanae hana chake tena. Siku hiyo ya jumapili akaenda kumuacha Jeremy nyumbani kwa mama yake mkubwa, safari ya Kigamboni ikaanza ili kwenda kulipiza kisasi. Alitulia njiani akijipanga. “Akatafute mwanamke wa kumzalia mtoto wa kuonea, si wangu.” Akawaza mama Jema kwa jazba.

Alikuwa akijua sehemu mwanae alipokuwa akijenga na mchumba wa zamani. Temu. “Anataka akaishi kwa jasho la mwanangu! Hakika labda niwe nimekufa. Sipo hapa duniani ndipo wawaonee wanangu. Lakini sio nikiwa hai, na nisijue.” Mama akashuka kwenye pantoni, akaingia kwenye daladala mpaka Mji Mwema. Akaanza kutembea. Palikuwa mbali kidogo na makazi ya watu. Kiwanja cha bei nafuu. Jema kwa pesa zake za kuungaunga, akanunua mwishoni, mbali. Kutoka kwenye daladala mpaka hapo ni mwendo wakutosha tu. Mama hakujali. Akachapa mwendo mpaka akafika.

Akakuta kweli imeisha. Lakini ipo kama aliyekuwa akijenga, ameishiwa, kwa hiyo imesimama. “Alifikiri nirahisi. Mshenzi wa tabia.” Akachunguza vizuri, akagundua hakuna mtu anayeishi hapo. Kumeachwa tu. Hakuna madirisha wala milango. Nyumba zipo mbali na hapo kwao. Akaridhika.

Akaenda kutafuta baa, akakaa mpaka giza lilipoingia. Akatoka hapo baa, akajifunika vizuri akaenda kununua mtungi wa gesi. Akarudi kwenye ile nyumba. Kwa kujificha, akaenda kufungulia huo mtungi mpaka akaridhika gesi imesambaa. Akatoa huo mtungi na kwenda kuuacha mbali kidogo na hapo. Akarudi na kumwagia petroli kuanzia ndani akitengeneza kijimfereji mpaka nje ya mpaka wao kwa nyuma.

Aliporidhika yupo peke yake kwenye mji huo ambako hakuna makazi ya watu wengi, nyumba nyingi ndio zinajengwa, giza, akatupia njiti za kiberiti. Moto ukaanza kuwaka ukifuata njia ya petrol mpaka ndani ilipokutana na gesi. Mama Jema akaondoka kwa haraka na kwenda kusimama mbali kabisa akiangalia jinsi ile nyumba inavyoshuka chini. Alishaweka bia zake kichwani, akacheka sana wakati ikishuhudia ile nyumba ikiteketea. “Mshenzi wa tabia. Akamwambie mama yake amzalie mwanamke wa kumuonea. Sio mwanangu.” Aliporidhika hata wakisaidia kuzima moto haitaokoa chochote, akaondoka. “Yeye si mwanaume? Sasa aanze ujenzi na kumaliza. Mjinga wa tabia.” Huyo akarudi zake kumchukua mjukuu wake, roho kwatu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi na mapema sana kabla mwanae hajaamka, Jelini akawa amerudi nyumbani. Mpaka mama yake akashangaa. “Kweli umeamua!” Jelini akacheka. “Ndio umedamka hivi!” “Sitaki mwanangu anione tapeli. Acha nijitahidi mama yangu. Ninapoweza, nisizembee.” “Sasa njoo nikupe mchapo wa jana.” Wawili hao ni mashoga wa kuendana. Chanda na pete. Akili zao sawa, na wanapikika chungu kimoja. Hakuna mwenye raha bila mwenzie. Huna jinsi ukamtenga Jelini na huyo mama yake.

“Haya, umefanya nini tena? Maana mama Jema, huishiwi vimbwanga!” “Ile nyumba aliyokuwa akijenga Jema na yule mshenzi.” Jelini akaanza kucheka asijue mwisho wake. “Yule mchaga mwenzio, ukamuita tapeli mbele yake?” “Basi nimemtenda, hapa roho kwatu.” “Mama Jema! Umeua?” “Nimtoe duniani kirahisi hivi, aringe? Tubanane hapahapa duniani aonje joto la jiwe.” Jelini akajiweka sawa, maana alijua kinachokuja si kidogo.

“Umemfanyaje mama wewe!?” “Nilikwenda jana, nikaitia kibiriti nyumba yote.” Jelini alibaki mdomo wazi, macho kayatoa. “Yeye si mwanaume kweli?” “Mama Jema!” “Basi ndio aanze tena ujenzi, tumuone sasa. Mjinga wa tabia. Mwanaume mzima anataka ajengewe nyumba? Tena na mwanangu mimi! Asinitanie kabisa. Akamwambie mama yake amzalie mwanamke wa kumjengea. Sio mimi. Mimi sijasukuma leba kwa ajili ya kumtumikia yeye.” Jelini akaanza kucheka kama mazuri.

“Tuanze taratibu mama yangu! Sasa hukuogopa kuua?” “Hakika nilihakikisha hafi, ili aanze kule alipotolewa na Jema. Yeye si kidume cha kubadili wanawake? Sasa tumuone.” Jelini hana mbavu kwa cheko. “Na usimwambie Jema, asije akatuombea laana bure!” Jelini akazidi kucheka mpaka machozi. “Mwenyewe amesema amemuachia Mungu.” “Subutu. Anamwachia Mungu ndiye aliyeijenga ile nyumba? Ndiye aliyesukuma leba? Asinitanie mimi.” Jelini hana mbavu, anafuta machozi kama mazuri.

“Basi siku ile unaambiwa muachie Mungu, nikaona umenyamaza mwenyewe kimya, nikajua mpo pamoja. Kumbe!” “Pale nilikuwa nikifuatilia kisheria mwenzio. Nikatafuta wanao elewa mambo hayo, kisheria. Nikauliza maswali yangu yote mpaka nikaridhika kuwa, kisheria, nyumba ni ya Temu. Hatuna jinsi kuja kuipata tena. Kwamba Jema kaula wa chuya. Nikamuhurumia mwanangu jinsi anavyojua kujinyima. Halafu mwanaume mwenyewe alikuwa mshenzi, alimfuata yeye kwa kuwa alimuona mnyonge, hana baba wakuja kumtetea! Akanitizama hali yangu, akanidharau. akijua sina nitakachomfanya, ndio akamchagua mwanangu amuonee! Hakika nilisema sikubali. Hata kama sina mwanaume wa kusema atatetea wanangu, mimi mwenyewe nitapambana nao. Washenzi kabisa.” Hapo akazungumza kwa kuumia, Jelini akamuhurumia. “Pole mama yangu.” “Mbona hapa nishapoa. Na nishamsamehe kabisaa. Na hivi Jema wangu sasa hivi anakula kivulini. Nimemsamehe buree.” Jelini hana mbavu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwenye mida ya saa nne simu yake ikaita. “Zenda!” “Ulirudi kulala?” “Hapana. Nimefurahi nimerudi Jeremy akiwa bado amelala. Ameamka amenikuta namsubiria. Amefurahi huyo! Nimemsaidia kujiandaa na kumsubiri mpaka basi la shule lilipokuja akapanda. Sasa hivi nipo tu.” “Unafanya vizuri.” “Uliamka salama?” “Niliamka na swala la yule mwalimu.” Jelini akashituka sana. “Hapa tunapozungumza, ameshakamatwa, yupo chini ya ulinzi.” “Zenda! Ulimpataje?!” “Niliweka mtu wa kumtafuta maana kumbe alikwenda kusoma. Sasa aliporudi shule akapelekwa wilaya ya Mkuranga kama afisa elimu huko. Ndio wamempata na kumkamata.” “Nilijua umesahau!” “Hata kidogo. Lakini ujue utahitajika polisi. Kwanza kumtambua, pili ambapo ni pagumu kwa ajili ya ushahidi, kumpima Jeremy DNA yake ili kumfananisha na yeye.” “Mmmh! Hapo hapana Zenda.” Jelini akakataa.

“Mwanangu amekua bila mimi. Ndio kama kwa mara ya kwanza naanza naye mahusiano, anaanza kunizoea, halafu nimuanzishie habari nzito hivyo, kisha kesi zakumpeleka mahospitalini na mahakamani! Hapana Zenda. Mimi sitaki kumuingiza Jeremy kwenye hayo mambo.” “Upo sahihi. Nina wazo. Unaweza kumchukua na kwenda naye hospitali ambayo atakutana na daktari ambaye anajua nini chakufanya, halafu wewe unamwambia tu unakwenda kuangalia afya yake.” “Jeremy muoga wa hospitali na sindano kama mimi.” “Hii kesi itachukua muda mrefu sana bila hivyo Jelini wangu. Tafadhali pata muda wa kufikiria kabla hujakataa kila kitu.” “Sawa. Na nitazungumza na mama pia. Ila ujue nimefurahi sana kuweza kunijali kwa kiasi hiki Zenda.” Jelini akaanza kulia.

“Hata mama na Jema hawajui kilichokuwa kikiendelea kwenye maisha yangu. Wanachojua ni umalaya ndio ulinisababisha kushika mimba. Yaani nashindwa hata pakuanzia na mama ili ajue kinachoendelea sasahivi. Nimefurahi hujanipuuza Zenda. Nimefurahi umejali mateso yangu ya nyuma.” “Usilie sasa. Ila ujue na wivu unanisumbu.” Jelini akaanza kucheka. Alitegemea. “Mimi nilijua mapenzi!” “Sipendi mtu ashike vyangu. Tena alikushika bila ridhaa yako! Hakika hatakaa akatoka jela.” “Basi acha nizungumze na mama.” Wakaagana na kukata.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jeline akampigia simu mama yake. “Upo wapi?” “Mtaani. Na hivi umenipa pesa, nataka tufungue duka kama la Mode, lakini hukuhuku Tegeta. Hapa nahangaikia fremu, nishaongea na Mode, amesema kupata vipodozi nisiwe na shida, ilimradi niwe na pesa. Sasa naona mwenzangu akaunti yako haikauki pesa, nimeona bora niiwekeze.” Jelini akashangaa sana. Maana alimuonyesha tu mama yake pesa aliyonayo kwenye akaunti, tayari mama yake amefikiria chakufanya! “Mama wewe unaakili jamani! Mwenzio nilikuwa hata sifikirii!” “Kuna leo na kesho Jelini. Hiyo mipesa inayoingia sasahivi, hujui baadaye itakuaje. Si bora kuyawekeza tusirudie shida. Au hutaki?”

“Wewe ukitaka pesa yeyote ile sema. Utachoka mwenyewe.” “Hapana. Nafanya hii ya vipodozi ila kwa kuwa pesa ipo, nafanya kwa hali ya juu zaidi. Duka kubwa na bidhaa nzuri zaidi. Wakati tukisubiria hicho kituo cha mafuta.” “Wewe endelea mama yangu, lakini kuna jambo ninataka kukwambia. Sikuwahi kukwambia kabla.” “Basi subiri nirudi. Naingia kuzungumza na mtu sasahivi. Tukishawekana sawa, nakuja kukupa hesabu.” “Uwe unaniita mama yangu na mimi unichangamshe!” “Kama unataka hivyo bosi wangu, ndio furaha yangu. Wawili ni wawili tu Jelini mwanangu. Halafu kuna leo na kesho. Hujui…” “Naomba usiniambie habari za kufa kwako.” Akakata simu hapohapo. Hilo Jelini hakutakaga kufikiria kana kwamba walishazungumza na Mungu kuwa mama yake ataishi milele.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akampigia simu Jema. “Njooni kwetu leo kwa chakula cha usiku. Kuna jambo zito nataka kuwaambia nyinyi ndugu zangu.” “Unamaana na James?” “Sasa si ndio mwanaume pekee kwenye familia yetu!” Hilo likamfurahisha sana Jema. “Mimi sina vikwazo. Baada ya kazi nipo huru, James ndio inabidi kumpanga mapema. Ila kwa kuwa umewahi kuniambia mapema, nitamuomba asikose.” Jelini akashukuru na kukata, akaamua kumfuata mama yake aone mwanamke wa kichaga anavyohangaika.

Mama yake akafurahi sana kumuona Jelini anajichanganya na kutaka kujifunza. “Kuna jambo nataka kuwaambia. Wewe, Jema na shem. Nitawaandalia na chakula cha usiku, nimewaomba waje.” “Mbona unanitisha?” Akanyamaza. Wakazunguka na mama yake mpaka wakafanikiwa. Ndipo wakarudi nyumbani kwa matayarisho ya chakula cha jioni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika mida ya saa moja Jema na James wakawa wanaingia. “Mama, nyumba imependeza!” “Asante.” Karibuni ndani. Jema akawa anashangaa kwao. “Hivi tulipanga tuje kuwaona weekend hii. Tumerudi na mambo mengi!” “Wala usijali.” “Jema umependeza!” Jelini akamsifia dada yake. “Nashukuru. Mimi njaa inaniuma. Nakula kama mchwa.” Akasogea mezani. “Njoo James tukae hapahapa tule huku tukizungumza.” Akajikaribisha. “Husubiri kukaribishwa!?” James akashangaa. “Hapa!? Hata kidogo. Njoo bwana James.” “Hapa nyumbani James mwanangu. Njoo tu tuzungumzie hapa. Naona Jema amegoma kusubiri.” Wakahamia mezani.

“Haya Jelini, yang’aze.” Jema akasema macho kwenye vyakula akitayarisha sahani ya mumewe. “Kipindi kile nipo shule, mimi nilikuwa na marafiki wa kiume kama washikaji tu lakini si wapenzi.” Akaanza Jelini nakufanya Jema atulie maana alijua tu anataka kuja kuombwa hela. “Nilipokuwa nakaribia kumaliza, akahamia mwalimu mmoja hivi. Kijana tu. Akawa anatufundisha somo la hesabu. Akaanza kunituma hiki na kile. Wale washikaji zangu wakawa kama wanatania kumwambia yule mwalimu, Jelini sio monita. Ili asizidi kunituma. Akawa anazidi kunituma kisha ananifuata kama ni ofisini na yeye anakuja. Alipoonyesha nia ya mapenzi na mimi nikamjua tokea mwanzo, nikamuonyesha wazi simtaki. Akaanza kuwa mkali na katili kwangu, ananichapa bila kosa, na kunisingizia mambo kwa walimu wengine, nikaanza kuchukiwa na walimu wote pale shuleni.” Wote kimya.

“Akanihamisha siti pale nilipokua nikikaa na wenzangu, akanisingizia nawaigilizia. Akasema kwa walimu wote eti mimi naigilizia. Ikawa shida kila siku mimi nachapwa msitarini. Siku moja akaniita akanimbia yeye ana uwezo wakubadili maisha yangu yakawa mabaya zaidi ya hivyo. Ataua ndugu zangu wote. Hapo ananitisha mimi nishachoka. Akanituma kwake. Ile nimefika tu kwake na yeye akaja. Akanibaka kisha akasema nisithubutu kusema, lasivyo atanidhuru mimi na familia yangu na kusambaza picha ambazo alisema alirikodi kamera inipige wakati nipo kwake.” Mama Jema aliumia sana.

“Basi nikawa na kazi ya kwenda kwake, ananifanya atakacho. Akinituma kwake ili na yeye aje nikikataa, ananionyesha picha zangu za uchi alizonipiga anasema nisipoenda atazisambaza kwa kila mwanafunzi na atanichinja kisha kuja kuchinja ndugu zangu wote. Nikawa naogopa, nafanya kila kitu anachotaka mpaka nikashika mimba ya Jeremy. Nikamwambia. Bwana alinipiga yule kaka, nakumbuka alinigonga, nikapoteza fahamu, nikaja kuzinduka ananimwagia maji. Nilipozinduka tu akanitoa hapo na kunirudisha mpaka hapo karibu na nyumbani akanionya na kuniambia nikija kumtaja, kilichonipata kitawapata familia yangu yote. Yaani mama na Jema. Hapo alishajua sina baba. Basi mimi ndio nikafukuzwa shule. Nipojifungua Jeremy mama alipotaka nirudi shule, ndio maana nilikataa. Nilijua yale mambo yatarudia tena.” Jema alilia sana.

“Nikawa siwezi kulala kwa hofu na uchungu na siwezi kumwambia mtu, naogopa. Siku moja mama alinituma pale baa kumnunulia mamkubwa bia. Alikuwa amekuja hapa ndio nikakutana na dada Doro. Sasa sijui tulizungumza nini, tukaanza kucheka mpaka tukashangaa. Wakati nimepewa na muhudumi hizo bia, maana mimi nilifika nikaka kwenye meza yake wakati nikisubiria hizo bia. Dada Doro akaniambia nirudi tupige stori, amependa kampani yangu. Mimi nikarudisha bia hapa, nikatoka kwenda kwa dada Doro baa. Akaanza kuninunulia bia. Nikamwambia mimi sinywi, bia chungu. Ndio akaniambia yeye anazinywa sababu ya matokeo yake baada ya pale, analala na kusahau matatizo yake yote.”

“Basi nikaanza kunywa na dada Doro. Ikawa inanisaidia sana kulala. Akaanza kuniomba nikalale kwake eti yupo mpweke. Nikakubali kwa haraka. Akaniambia sasa nyumbani utaagaje? Mimi nikamwambia kwetu mimi wananijua malaya, hawana shida na nilipo. Basi maisha yakaendelea kunywa kwa pesa ya dada Doro au Jema kama ananipa. Uzuri dada Doro anakazi inayomlipa sana na anapenda sana kuvaa. Mwenyewe anasema hawezi kurudia nguo zadi ya mara mbili. Basi na mimi ndio mtu wake wa karibu, akawa ananipa mimi nguo zake za zamani. Maisha yakaendelea ila hapo nina hofu na chuki sana ya wanaume kwa kile nilichofanyiwa. Kundi letu pale baa likakua. Wale wanapesa, lakini kila walipokuwa wakinitongoza sitaki kabisa. Sitaki tena.”

“Sasa siku ya jumapili ile baada ya harusi yenu si nikaamkia sehemu nisipopajua! Sijui nilifikaje wala pale ni wapi! Nikaamka chumba kizuri na pasafi. Nikaanza kuangaza macho ikabidi nitoke kutafuta. Jumba zuri kwelikweli. Kuchungulia nje nikakutana na mwanaume msafi sana. Akaniambia nichukue simu tuzungumze mimi nikijua yeye mwizi.” “Kwa nini?” “Nilimkuta na yeye ni kama anachungulia ndani anashindwa kuingia ndio akaja kuniambia sasa kwa simu kuwa hawezi kufungua nyumba inalindwa na mitambo, lazima kutoa sasa alam.”

“Akanielekeza mpaka nikaweza kufungua ndio nikatoka sasa. Ananiuliza mimi ni nani, na mimi namuuliza pale ni kwa nani. Ikabidi kumuelezea mimi nililewa sana.” “Tena sana Jelini, mpaka ukagawa mtoto!” “Nisameheni jamani. Nimeacha pombe. Muulizeni mama. Sijanywa tena na nimemuomba Jeremy msamaha. Sikukusudia.” “Malizia.” “Basi kufupisha habari akatoka Kasa, kumbe alikuwa humohumo ndani ila amelala chumba kingine na dada Doro, na ndipo nilipojua yule niliyekuwa nikizungumza naye muda wote ni baba yake.” “Mzee Kasa!?” James akauliza kwa kuhamaki sana.

“Mimi nilikuwa sijui! Kwanza hawafanani kabisa.” “Hata sisi tulikuwa tukimwambia Kasa unaweza sema ni kaka yake. Yule mzee ni mtu wa Burundi. Anasura kama watu wa huko. Halafu hajafanana kabisa na wanae. Hata huyo Kemi dada yake Kasa, tena bora Kasa, yeye ndio anasura kama mwanaume tena mweusi tii. Halafu baba yao yupo kama shombe!” “Ewaaa! Kumbe shemu wewe unawajua vizuri.” “Malizia Jelini.” Mama yake akataka amalizie. Hapo uchungu umemkamata, kama azae tena.

“Basi mimi nilivyogundua kuwa yule ndio mzee Kasa mwenyewe maana habari zake nilishazisikia kuwa ndio chanzo cha kiburi cha mwanae, kwa kuwa huyo mzee anapesa sana.” “Unapoishia kusema sana, ongeza sana nyingine. Anamigodi ya madini huko Mwadui. Anamakampuni yake makubwa sana hapa nchini. Na Kasa anasema ni kichwa chake mwenyewe. Anaakili sana na nidhamu ya kazi. Hata mwanae wa kike amemwajiri kwenye makampuni yake. Unaambiwa dada anapesa huyo!” “Basi shemu ameshamaliza.”

    “Sasa mimi nikaondoka pale kwa kujinyata maana mzee alikuwa anamfoka mwanae, kulala hovyo na wanawake. Basi wakati nipo njiani natoka kwao kwenda kutafuta usafiri akanikuta akasema anipe lifti. Mimi nikamkatalia nikamwambia sitaki msaada wake asije akanitaka baadaye.” Wote wakashangaa. “Kweli tena. Nikamwambia mimi kwangu watu wanaanzaga kutaka kunisaidia mwishoe wanataka kadhalika. Akacheka sana na kuniambia yeye hatanidai ila pale ni mbali sana na usafiri, ananisogeza. Ndio nikapanda kwenye gari yake.”

    “Akaanza kushangaa nawezaje kuishi maisha kama yale yakulewa vile mpaka kutojitambua! Akazungumza sana na mimi. Basi akaniambia anirudishe nyumbani. Nikamkatalia. Nikamwambia itakuwa picha mbaya kwa mama, atajua nililala kwake. Akashukuru akaona ni kweli. Ila katika mazungumzo yake akaomba niwe nampa maendeleo ya kubadilika kwangu maana nilimwambia nabadilika. Ila kufika hapa nyumbani mwanangu kuniambia na nilimgawa, na wewe utamchukua. Niliumia sana.”

“Mimi jamani nampenda sana mwanangu. Japokuwa sijui kumtunza, lakini ndio sababu hata kama napapenda kwa dada Doro, huwa narudi nyumbani ili tu nimuone. Basi nikakaa nikajifikiria, hivi siku kama ile kuamkia nisipopajua, imetokea mara ngapi! Halafu wale wanaume wote ambao nawakatalia, nikilewa sijitambui, watakuwa wakiniacha kweli! Nikaingiwa hofu. Sasa katika mazungumzo Zenda akasema yeye anacho kipimo.” “Zenda ni nani tena!?” Akawa kashamchanganya Jema.

    “Anaitwa Alexender Kasa, ndio mimi nikambatiza jina la Zenda.” Mama Jema akatingisha kichwa, Jema akashangaa sana. “We Jelini! Huyo baba tajiri!?” “Mimi nilimwambia atanichanganya. Nimeshamzoea mwanae kuwa ni Kasa, nikamwambia yeye nitamuita Zenda. Lakini mwenyewe amependa. Basi kufupisha habari ndio nikakimbilia hospitalini kupima kwa hofu nikidhani watakuwa wakinifanyia mambo mabaya nikiwa nimelewa maana kumbe nikilewa nakuwa kweli sikumbuki si matatizo tu, sikumbuki chochote.” “Na mama alikwambia Jelini.” “Sasa wakati ule nilikuwa sifikirii, Jema.” “Wewe utampoteza. Mwache amalizie.”

    “Siwezi mimi…” “Acha maneno mengiii. Wewe endelea.” Jelini akacheka nakuendelea. “Nilipokuwa hospitalini nikamtumia ujumbe Zenda maana nilimgombesha na kumkatia simu.” “Jelini!” “Wee mwache wee.” Jema akawa haamini. James kimya anataka kujua mwisho wake. “Basi nikamwambia Zenda nipo hospitalini, napima Ukimwi na anisamehe. Akaja kukaa na mimi. Nilikuwa naogopa maana mama alinipa mwezi. Niwe nimepata kazi na kumletea ada ya mtoto lasivyo anakupa wewe mwanangu. Akaniambia na pia kama nimeathirika anakupa wewe mtoto. Sasa mimi hapo nikawa naogopa, sitaki kumpoteza mwanangu. Ndio Zenda akawa ananipa moyo mpaka majibu yakatoka. Tukatoka naye pale kwenda kula, maana mwanzo nilimkatalia. Ila kile kitendo cha kuja kukaa na mimi pale mpaka mwisho, kikanigusa.”

    “Basi katika mazungumzo baadaye ndio nikamuuliza mtu kama mimi naweza kufanya nini maishani. Akanishauri kurudi shule. Mimi nikakataa kabisa. Nikamwambia shule sitaki kabisa. Ndio baadaye akaunganisha mazungumzo yangu akajua naogopa sana shule. Halafu akajua nilizaa nikiwa shuleni. Moja kwa moja akajua nilibakwa, haikuwa hiari yangu. Akaniambia nimsimulie ilivyokuwa. Nikamsimulia kila kitu.”

    “Mimi nikajua amesahau bwana. Leo asubuhi amenipigia simu akaniambia ameshamkamata yule mwalimu, yupo jela.” “HAIWEZEKANI!” Mama Jema na Jema wakahamaki kwa pamoja. “Mimi naamini. Jema, mimi nikikwambia mtu anayo pesa, niamini. Yule mzee anayo  pesa ya kuamuru mambo yatokee, na yakatokea. Mwanae huyo Kevin, anaishi pale kazini, utafikiri ametuajiri sisi wote na mabosi wetu. Kwa dharau ya pesa ya baba yake, sema tu ananidhamu ya kazi.” “Ni baba yake ndio anamlazimisha kazini. Zenda ameniambia amemwambia akifukuzwa pale, ajue na mshahara anaomlipa unakoma.” “Subiri kwanza Jelini. Kwamba Kasa analipwa na baba yake kufanya kazi pale?” “Ndiyo. Mbali na mshahara mnaolipwa nyinyi na mwajiri wenu, kila mwezi Kasa analipwa na baba yake. Na si pesa ndogo. Nyumba zote anazokaa Kasa ni za baba yake.” “Wewe umejuaje?” Swali la Jema likamfanya Mama yao aanze kucheka huku akimwangalia Jelini kama anayemwambia umekamatwa.

    “Sasa unacheka nini mama?” “Wewe Jema kakuuliza swali, jibu. Achana na mimi.” “We Jelini?” “Mimi hapa Zenda mpenzi wangu.” Jema na mumewe wakabaki wametoa macho. “Sasa mnashangaa nini?” “Huyo baba yake Kasa ndio mpenzi wako!?” “Ndiyo, na tunapenda sana. Kamlipia mwanangu ada ya mpaka darasa la saba. Hapo Hopac.” “Haaa! Kwamba Jeremy anasoma hapo!” “Zenda huyo. Anasema pesa ni nyingi lakini elimu nzuri.” “Si nilikwambia yule mzee anapesa? Sasa uamini anayo pesa haswa.” “Sasa hujaona kituo cha mafuta anachomjengea huyu! Hutaamini.” “Acha masihara Jelini!” “Bwana mama unanipoteza nilichowaitia.” Jelini akalalamika.

    “Subiri kwanza Jelini. Kwamba na Kevin anajua?” “Bwana watoto wameumia hao mimi mpaka nikawashangaa! Maana Zenda mwenyewe alitaka niende nao kanisani. Mimi nikamwambia namuogopa Kasa kwa sababu yeye nilimkataa, iweje leo anikute na wewe!” “Kwani mwanae pia alikutaka!?” “Kevin alikutaka?” Jema na mumewe wakafululiza maswali wakiwa bado na mshangao. “Ndiyo. Ila mimi nilimkataa mapema sana. Alianza kunihonga, nikamwambia mimi sipendi mambo yakuhongwa halafu aje anitake baadaye. Mimi sitaki. Bwana aliumia huyo! Sasa sijui hajazoea kuachwa mimi nikamkataa.” “Kasa kwa kupenda ushindani, hapo ni kwa sababu ulisema Colins ndio mchumba.” “Heee! Kwani ni madogo Shem? Acha palepale kanisani anisingizie kwa baba yake na mbele ya huyo Kemi na wanae, eti mimi mwanamke wa Colins. Mimi malaya. Eti nilimtaka, akanikataa.” “Jelini!” Mpaka mama yake akashituka.

    “Kumbe sikukusimulia mama? Bwana mimi nikaanza kulia, kuongea siwezi. Na Kemi yupo kama anashabikia. Ila sasa Zenda ananipenda sana. Akaniambia twende. Mimi nikamwambia siondoki pale mpaka ampigie simu Colins amuulize mbele za wanae. Bwana watoto wanamuogopa Zenda wale! Kama mungu!” “Si ndiye anayewapa kiburi mjini? Nasikia hata mume wa Kemi ameajiriwa na baba yao. Ikawaje?” James akataka aendelee.

“Zenda akachukua simu ya mwanae akampigia simu Colins, Colins akasema yeye ameniona kama mara tatu tu ila wewe ndio unataafa zangu kamili. Alipomaliza akaniuliza kama nimeridhika. Bwana wanae walikereka. Akasema yeye alimpigia simu Colins kwa ajili yangu wala si wanae. Akasema kwa kuwa Kemi hayamuhusu na Kasa anajua ni muongo, analia wivu sababu nilimkataa.” “Jelini wewe mtoto!” “Mimi mwenzenu nampenda Zenda, kufa na kupona. Nampenda haswa.” Wote wakabaki wakimwangalia.

    “Huna haya na baba anayeweza kukuzaa!” “Bora lipi mama yangu. Vijana wenye tamaa na kunibaka, au Zenda anayenipenda mimi na mwanangu? Ananitunza na kunifikiria haswa. Sasa leo ndio alisema ili mashitaka ya yule mwalimu yaende haraka, lazima kumpima Jeremy na yeye DNA. Mimi nikakataa kesi kwa manangu. Sitaki mwanangu asimamishwe mahakamani na yule jambazi. Sitaki apite hapo. Huyu mtoto amelelewa na mama bila shida. Wakianzisha tu kesi na yeye, watamchanganya mwanangu.” “Lakini huyo mshenzi lazima anyongwe. Huyo mzee niwakumshukuru.” Mama Jema akaongea kwa jazba. “Naomba usimuite mpenzi wangu mzee. Anaitwa Zenda, ukitaka wewe muite Kasa.” Jema akaanza kucheka.

    “Usicheke bwana Jema!” “Kwani Jema huyo baba ukimuona utafikiri kaka yake Kasa!” “Jamani mwanaume mzuri yule! Acha nikuonyeshe picha zetu tulikwenda kisiwani na bonge ya boti. Na ni yake. Nzuri ndani ipo kama nyumba!” Akampa simu na kumfungulia. “Haaa!” “Si nilikwambia! Huyo ndiye baba yake Kasa.” “Au kabambikiziwa watoto!” Jema alimfanya mumewe acheke sana. “Sasa hujamuona mwanae wa kike.” “Bora Kevin kuliko dada yake. Halafu maringo sasa!” “Si wanayo pesa!” Akaongeza James.

    “Turudi kwa ya leo. Ndio Zenda akatoa wazo kuwa tumuepushe Jeremy na mahakamani, ila nimpeleke hospitalini kwa daktari ambaye atakuwa amemuandaa. Amfanyie vipimo tu, halafu basi. Jeremy asionekanike mahakamani wala polisi. Mimi nikamwambia mwanangu anaogopa sindano.” “Kwa hiyo huyo Zenda ndiye anayejenga hii nyumba?” “Mwaya Jema!” “Acha nishangae mdogo wangu! Maana sasahivi ndio nikiangalia hapa ndio naona haya mabadiliko hata ya humu ndani!” “Nakwambia ndani ya juma moja, kulichimbwa kisima hapa, maji yanatoka mpaka ndani.” “Mama!” Jema akashangaa. “Mzee anayo pesa si…” “Msimuite mzee. Ni Zenda.” “Haya, baba anayopesa. Wanaingia watu na kutoka mchana kwa alfajiri. Ukiingia hapo jikoni kwetu, hutaamini. Ni kama pametengenezwa upyaa. Kila kitu kipya, mpaka makabati ya ukutani yamejengwa. Friji na majiko vyote vipyaa. Ndani ya juma moja nyumba imechukua sura yake. Sakafu nafikiri waliitandua na kuweka hizi marumaru unazoziona hapa nafikiri ndani ya siku tatu walikuwa wamemaliza. Vyumba ndio vinakarabatiwa mpaka vyoo vinajengwa kila chumba. Uzio wenyewe umejengwa kwa kushambuliwa kama mchwa!” “Mama!” Jema hakuwa akiamini.

    “Nakwambia kila kitu mpaka kiwanja amenunua kwa jina la Jelini, ujenzi ni hivyo kaniachia mimi nikisimamia ndio naamini ni vya Jelini, hamdanganyi. Lakini kila kitu kwa jina lake huyu mtoto.” “Ila huyu Jelini, naamini.” Wakaanza kucheka wakikumbuka mambo ya Jelini aliyokuwa akimfunda Jema na kumuacha James haelewi. “Hongera mwaya Jelini. Umeuchinja.” “Sasa swala la yule mwalimu?” James akataka warudi kwenye lamsingi. “Kwanza nasikia alijiendeleza. Sasa hivi anafanya kazi wilaya ya Mkuranga kama afisa elimu si mwalimu tena.” “Mshenzi kabisa. Yeye maisha yake yanaendelea halafu yako aliyakatiza, mimi nitaenda na Jeremy hospitalini. Mwambie amuandae huyo daktari.” “Mwanangu anaogopa sindano mama.” “Wewe unajua mpaka sasa hivi ameshachomwa sindani ngapi huyu mtoto?” Kimya.

    “Akiumwa unajua huwa anapewa dawa gani?” “Basi mama, ila mimi najua huwa anaogopa sindano.” Jelini akajibu kwa upole maana kweli huyo mtoto amekuzwa na mama yake yeye hana taarifa. “Au nyinyi mnasemaje?” Akataka ushauri wa Jema na mumewe. “Hakika achukuliwe hatua asije umiza watoto wengine.” James akaongeza. “Na Zenda naye amesema hivyohivyo.” “Jema mke wangu mbona unaanza kuninyima raha! Macho hayaondoki kwenye hizo picha!” Jema akashituka, maana alishapotelea kwenye picha, hamalizi! Jelini alicheka sana. “Naona mwenzangu hamalizi!” “Hizi picha nzuri James bwana, wala hakuna kingine.” “Mmmh! Mpaka umenisahahu?” “Siwezi mpenzi wangu.” Akarudisha simu kwa Jelini wakicheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ni nini Kitaendelea?

Watoto wa Kasa ndio wamemkubali Jelini?

Ticha aliyebaka Mali ya Zenda?


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment