“Mimi ninapopita
kwenye nyakati ambazo zinanifanya nisijue chakufanya. Nafsi na akili yangu
ikiwa imegota. Zaidi nikiwa nimesababisha hilo jambo na sijui jinsi ya kujitoa.
Huwa najikumbusha huu wimbo, aliuimba mwimbaji mmoja, mtu mzima sasa. Anaitwa Don
Moen. Ameuimba huu wimbo katika mafunuo ya ajabu sana. Anasema, ‘God will
make a way’. Sikilizeni tu na mruhusu haya maneno yawaingie, kisha
nitawaambia kitu.” Wakatulia.
Joshua alianza kupiga
hicho kinanda bila kuimba kwa muda tu, mpaka wakaanza kutulia. Alipoanza kuimba
sasa,
‘God will
make a way, Where there seems to be no way, He works in ways, we cannot see, He
will make a way for me. He will be my guide, Hold me closely to His side, With
love and strength for each new day,He will make a way, He will make a way.
Kuwa, ‘Mungu atafanya njia, pasipo onekana na njia. Hufanya njia zisizoonekana
au kueleweka kwa uelewa wetu. Atafanya njia kwa ajili yangu. Yeye atakuwa
kiongozi wangu akinishika karibu yake, kwa upendo na nguvu kila siku,
atatengeneza njia. Naye atakuwa baba yangu, ataniweka upande wake. Kwa upendo
na nguvu zake kila siku, atanitengenezea njia.’ Yaani mpaka hapo
anamalizia kibwagizo tu, akaona sebule nzima imeanza kujiegemeza kwenye makochi
vizuri, ile hali ya hofu ikaanza kupungua kwao. Ukweli Joshua alijua kuimba. Na
akichanganya na hisia, lazima utatulia tu. Akaimba na beti zake zote. Taratibu tu
akiwaangalia mmoja baada ya mwingine mpaka akamaliza.
“Hapo vipi?” Kidogo
wakatabasamu. “Eti Nanaa?” Akainama. “Basi akili ikishaelewa si kwa nguvu zangu
ila yupo mwenye nguvu ya kufanya makubwa zaidi ya nifikiriavyo, basi huwa sina
jinsi zaidi ya kumpa utukufu na heshima. Namuinulia mikono yangu
kulisifu jina lake. Namtambua kama yeye ni mkuu. Nautendaji wake
wa ajabu, natambua uwepo wake kwa kumwambia, ‘Wewe ni Mkuu. Unatenda maajabu,
hakuna kama weweee. Hakuna kama wewe.’ Joshua akaanzia hapo katikati ya wimbo ndipo
akaja mwanzo. Jinsi alivyoimba, wakajikuta wote machozi yakiwatoka, mikono juu
wakilisifu jina lake kwa kuabudu wakisema, ‘Twakupa utukufu, na heshima,
twainua mikono yetu, kulisifu jina lako!’ Wakarudia hapo. Waliimba hapo mpaka machozi.
Joshua alipiga kinanda akiimba huo wimbo bila kuchoka mpaka Geb kuja kumaliza,
na yeye yupo magotini. Kila mtu amefunguka. Joshua akamsogelea mkewe, akamshika
mikono yote miwili, akaanza kumshukuru Mungu. Wote wakamuombea baraka na afya
nje kwenye hiyo safari ya kubeba huyo mtoto.
Joshua akatamka
baraka kwa James na Jema pia. Akawaombea vizuri tu na kumaliza. “Mimi
nimemkosea anko James, anko. Mimi ni mtoto mbaya?” Magesa akaanza baada ya
kusikia akiombewa anko James. “Kitendo chakutambua umekosa tu, tayari wewe ni
mtoto mnyenyekevu. Lakini umejua ulipokosea?” “Sijamsalimia anti, nikaanza
kumuuliza maswali.” “Hayo ni makosa mawili, lakini jingine ni jinsi
ulivyomtambua anti. Ulimtambua isivyo sahihi ndio maana anko alikasirika. Mke wake
anaitwa Jema. Wewe utamuitaje?” “Anti
Jema.” Akajibu.
“Ewaah! Yeye ni anti
Jema.” “Halafu mimi ndiye nilikosa Magesa. Anti hakuwa
na shida yakuingia chumbani kwangu. Mimi niliongea maneno mabaya kwake na
kumuumiza.” “Pole mami. Usilie. Mimi nitamuomba msamaha anti. Mimi sipendi
kumuudhi anko wangu. Najua ananipenda.” “Hapo utakuwa umefanya jambo zuri sana.
Lakini wakuanza kumuomba msamaha ni anti Jema. Na mimi nitakupa simu yangu
umpigie. Ila acha nikapige simu moja hapo nje, nikirudi ndipo uzungumze na anti
Jema.” “Asante anko.” Joshua akasimama na kumbusu Magesa. “Hakika umenifanya
nikupende zaidi Magesa. Sikujua kama ndio unahekima hivyo! Wewe utavuta wengi. Na
Mungu hupenda wanyenyekevu. Uendelee hivyohivyo.” “Asante.”
“Jamani, kuna simu lazima
niipige sasahivi bila kuzembea. Kisha nitarudi tule, ndipo muondoke, baada ya
Magesa kuzungumza na anti wake. Wote wakaitika. “Nisindikize hapo barazani
Naya.” Naya akamfuata nyuma. “Wakati tukiimba, nimepata ujumbe wa Bale. Sijui ni
kwa nini, lakini hauwezi kusubiri. Lazima nizungumze naye sasahivi. Wewe unaweza
kunisubiria ndani tu.” Bila ya kuongeza neno, Naya akaondoka. Joshua akamuacha
tu.
Nafasi Ya Pili.
Akampigia simu Bale
zaidi ya mara mbili akawa hapokei. Mara ya tatu akapokea. “Kwema?” Joshua akaanza, ila akajua alikuwa akilia. “Mungu hajamalizana na wewe Bale. Na upo na deni kubwa sana
ambalo mimi sijui jinsi utakavyofanya kulilipa, lakini nilazima kulilipa kabla
hujaondoka hapa duniani.” Joshua akaendelea taratibu tu. “Baba yako alikuwa mtumishi aliyekuwa akitumika kanisani. Kwa
jinsi nilivyosikia siku ya mazishi yake, walimtegemea kwenye upande wa maombezi,
zaidi kutoa mapepo. Wengi walikuwa wakijilaumu kutotambua uwepo wake wakati wa
uhai wake, lakini karibu wote walikuwa wakilia na kuulizana ni nani ataziba
pengo lake.” Bale alilia sana.
“Zayoni
amekufa na mimba changa. Ndoto nyingi sana ambazo alikuwa akitizamia kuzitimiza
hapo baadaye. Ndoto zote hizo ziliungua
moto. Ndio Mungu amenituma kukwambia, HAJAMALIZANA na wewe. Hilo ndilo
amenituma kukwambia. Mengine ni mimi tu kwa kufikiria kwangu. Utafanyaje, sijui
ila naweza kufikiria kwa makubwa Mungu aliyoniamini nayo, hakuniacha peke
yangu. Alinipa Roho Mtakatifu akawa msaidizi, ambaye ukweli ni msaada
wangu mkubwa sana. Yeye atakufundisha, kukuongoza katika kweli yote mpaka
utashangaa jinsi atakavyotenda na kugeuza hiyo hali unayojisikia sasahivi kuwa
baraka kama usipokata tamaa na kurudi nyuma.”
“Unakumbuka
Paulo alilitenda vibaya sana kanisa? Akiwaua mchana na usiku mpaka akaja
kukutana naye? Leo tunafurahia ukuu wa Mungu kwa aliyoyafanya Paulo. Huna jinsi
ya kubadilisha nyuma, lakini Mungu wako amenituma kwako usiku wa leo kuwa, bado
anayo nafasi yako kwenye ufalme wake. Na kwa jinsi nilivyomfahamu huyu Mungu,
si mwanadamu hata aseme uongo. Kwa hiyo kilichobaki ni wewe kuutafuta ufalme
wake, mengine yote atayafanya yeye mwenyewe. Usiku mwema.” “Asante sana Joshua.” Wakakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi ndani kwa
Magesa. “Upo tayari kuzungumza na anti?” “Asije akaharibu zaidi, Joshua!” Mama
G akaingiwa na wasiwasi. “Hapana. Mimi nimeheshimu wazo lake. Magesa anaakili
na anahekima. Mwache Mungu amtumie hata kwenye hili.” Geb kimya akijiangalizia
tu. Joshua akapiga, Jema alipoona simu ya bosi wake akapokea kwa haraka. “Samahani Jema. Nina mtu ameomba rasmi. Yeye mwenyewe anataka
kuzungumza na wewe. Hajatumwa na mtu. Ni akili zake mwenyewe ila hana simu. Tafadhali
naomba msikilize tu.” “Sawa.” Jema akakubali. Joshua akampa Magesa simu.
“Mimi
naitwa Magesa. Nimekukosea anti, nisamehe.” Ikamgusa kila mtu. “Nimejua makosa yangu. Kwanza sijakusalimia. Halafu nimekutambua
vibaya. Wewe ni anti wangu. Na mimi nakupenda. Ila nimekua mtoto mbaya. Nisamehe
anti. Nitakuwa nikikusalimia kabla sijaongea chochote. Halafu mama yangu ameniambia
yeye ndio alikosea. Alikwambia maneno mabaya. Hutaki kuingia chumbani kwake. Yeye
ndio amekosea. Halafu na mimi sikutakiwa kusema hivyo anti. Nisamehe.” “Kumbe
Magesa wewe ndio mtoto mzuri hivyo!?” “Hata anko Joshua amesema hivyohivyo.”
Ikabidi wote wacheke.
“Ujue anti
mimi sipendi kukuudhi?” “Sikujua Magesa!” “Basi mimi hata bibi anasema nina
upendo mwingi. Hata wewe nakupenda. Ujue anko James ni anko wangu, na huwa
nacheza naye?” “Ameniambia.” Jema akajibu akicheka. “Basi na
wewe ni anti wangu. Na ninakupenda anti Jema.” “Asante kwa upendo Magesa. Kweli
wewe mtoto mzuri. Yaani mpaka sasahivi hapa, nasikia kupendwa sanaaa.” Acha
Magesa aanze kucheka. Kila mtu akaanza kucheka.
“Umefurahi?”
Jema akamuuliza akicheka. “Sana. Wewe utakuwa rafiki yangu kama anti Naya. Wenzio sisi ni
marafiki. Kabla hajanisahau nilikuwa kila mara nampigia simu simu nakumpa stori.
Halafu tukawa tunaimba wote. Akanisahau nikawa namuombea kila siku anikumbuke. Ujue
nilikuwa nikimwambia nini Mungu?” Mama G akaguna na kutingisha kichwa. Wakacheka.
“Hata bibi
alikuwa akisikia nilivyokuwa nikimwambia Mungu. Si ndio bibi?” “Wewe
zungumza na simu Magesa bwana!” “Lakini si nilikuwa
nikimwambia Mungu asaidie anti Naya anikumbuke, turudi kuwa marafiki, halafu tuimbe
wote? Au bibi wewe umesahau? Si kweli dad?” “Hiyo simu kwa Jema ni ya
familia nzima!” Akaongeza bibi yake. “Ni kweli Magesa ulikuwa ukimuombea anti
Naya.” “Asante dad. Umesikia anti?” “Nimesikia Magesa.”
“Basi leo ananikumbuka. Na wewe kwa kuwa utakuwa rafiki
yangu, nitakuwa nikikuombea, na usinisahau. Nitakuwa nikikupigia simu na wewe
halafu tunaongea. Au wewe hutaki kuongea sana kama Liv, kichwa kitakuuma?”
Wakazidi kucheka. Liv na Jimmy wakimwangalia tu Magesa ndugu yao. Wakati wote yeye ndio yupo matatizoni na hakomi.
“Mimi
nikiongea sana kichwa hakiumi.” “Basi kumbe ndio maana sisi ni marafiki. Nakupenda
anti.” “Na mimi nakupenda Magesa. Nimefurahi umenipigia hii simu. Nahisi nitalala
vizuriii.”
Akacheka Magesa kwa furaha zote. “Na mimi nimefurahi umenisamehe.”
“Haya. Usiku mwema.” “Asante na wewe anti Jema, bibi harusi mzuri.” Wakacheka
sana. “We Magesa, harusi iliisha bwana.” Akapokea
James. “Sasa hakuna bibi harusi mwingine anko. Mpaka
akija bibi harusi mwingine, ndio anti hawi tena.” Walicheka sana. “Wewe hukuona anti alivyopendeza na gauni lake kama malaika?”
“Niliona Magesa.” James akajibu akicheka. “Mimi
nilipenda mpaka nikawaambia marafiki zangu shule, anti yangu alivaa gauni kama
malaika! Kwa hiyo abakie tu bibi harusi.” “Sawa Magesa. Ila ujue umenifurahisha
sana kumuomba anti msamaha.” “Asante anko. Usiku mwema.” Akaaga kwa heshima, wakakata kila mtu akahema.
“Joshua, hakika
nakushukuru mwanangu.” “Ni Mungu, mama. Mimi huwa namjua anaposhuka mahali. Inaweza
kuchukua muda kama hutachukua hatua. Kama hivi kama tungemkataza Magesa
asizungumze na Jema, hii amani aliyoweka usiku huu, tusingeipata, kwa kujizuia
sisi wenyewe. Ila Mungu anatenda mama. Anatenda kwa ajabu sana. Tuhamieni mezani.”
Vikaanza vicheko. Angalau usiku huo ukaisha kwa amani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku hiyo ijumaa saa
sita mchana, chakushangaza dunia, mzee akawa amemaliza juma. Akamuita Kemi
msaidizi wake, ofisini kwake. “Kama kuna jambo lolote tafadhali tuzungumze
sasahivi. Natoka, na sitarudi hapa wala sitataka simu za kiofisi mpaka
jumatatu.” “Unasafiri!?” Mwanae akamuuliza akishangaa maana kama ingekuwa
safari ya kiofisi yeye angejua, na kama ni ya kifamilia au binafsi, yeye
kipenzi cha dad angejua. “Umesikia nilichokwambia?” Mzee akauliza kimamlaka
kweli, mpaka akamshangaza Kemi. “Sidhani kama kipo. Naona kila kitu kipo sawa.”
“Basi ni hilo tu.” Kwamba Kemi aondoke ofisini kwake. “Unasafiri?” Ikabidi Kemi
aulize. Jinsi baba yake alivyomtizama, akaona atoke tu, japo hakuzoea.
Penzi kikohozi.
Penzi kikohozi, Zenda
akawa hawezi kukaa bila Jelini. Anataka kumuona na kumshika au kushikwa naye
kila wakati. Weekend yao walipanga wainze ijumaa mchana. Jelini akafurahi kama
amepewa alumasi. “Nilijua utalalamika!” “Kuwa na wewe? Hata
kidogo.” Zenda akacheka akiwa amempigia asubuhi hiyo akimuomba weekend
hiyo awe naye. Mama Jema alishaanzishiwa mchakato wa biashara ya uhakika,
mjukuu anasoma shule ya maana, nyumba inakarabatiwa kuanzia ndani mpaka nje,
hakuwa na shida. Akamsubiri mwanae mpaka akatoka shule. Alirudishwa saa nane
mchana. Akamuaga. “Nasafiri, lakini nitarudi jumatatu, mapema sana. Si
utamsaidia bibi?” Mtoto huyo hakuwa na makuu, akamuaga mama yake, dereva akaja
kumfuata, akaondoka kwenda kwa Zenda.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kama kawaida yake
akatoka kumpokea. “Nilikuwa nakusubiria kwa hamu!” Jelini akacheka akimsaidia
kushuka garini. “Nakuandalia chakula kizuri sana. Utakipenda tu.” Devi ambaye
ni dereva akatoa begi la Jelini, mzee akalipokea. “Twende ukanifundishe na mimi
siku nyingine nikupikie.” Devi akawa anasikiliza tu kwa kujiiba. Alipofunga tu
mlango, akaondoka. Jelini na Zenda ndani. Yakaanza mabusu. “Nitaunguza.” Akamuachia
Jelini akiwa na begi lake mkononi. Akapeleka begi chumbani, wakahamia jikoni.
Akaandaa meza very
romantic. Mishumaa mizuri akaweka na wine, Jelini akimwangalia tu. “Ujue hii ni
kwa ajili yako, wewe tu Jelini. Mimi huwa siachi kazi zangu eti kumpikia
mwanamke!” Jelini akacheka sana. “Jelini anapendwa?” “Sana.” Akajibu Zenda
kwa uhakika kabisa. Jelini hana mbavu. Basi ijumaa hiyo ikawa nzuri tulivu
haswa.
Jumamosi.
Mazoezi ya Zenda
asubuhi hiyo ya jumamosi yakaishia kwa Jelini. Basi wakashitua hapo kwa muda
wakutosha tu, ndipo kifungua kinywa. Na Jelini hakuwa mvivu kwenye mapenzi,
halafu sasa akakutana na Zenda hana papara, mtulivu na hakomeshei. Mapenzi ya
ustarabu, si kuumizana mpaka kumchubua, na kushindwa raundi ya pili.
Mida ya saa tano
wakatoka kwenda kuogelea. Jelini kwenye nguo ya kuogelea, Zenda alijuta. Yeye
mwenyewe yakamshinda. “Bwana Zenda!” “Hakika tuondoke tu. Mimi siwezi hivyo.
Mimi mwenyewe mwenye mali tu, nalemewa. Hayo macho ya wanaume wengine je?” “Sasa
yanakuhusu nini wewe? Waache tu, sisi tuendelee na yetu.” “Yaani wale vyangu
kwa macho! Hapana aisee. Tunaondoka. Usitake kuniua mimi kwa pressure.” Wakaondoka
hapo kurudi nyumbani.
Walipofika tu
akamdaka. Kweli hali ya Zenda ilikuwa mbaya kwa kumuona Jelini nusu uchi huko
walipokwenda kuogelea. Mapenzi yakaanza mpaka hamu zake zikapungua. “Jelini
wewe ni mzuri aisee. Mtoto mtamu, huchoshi!” “Upunguze na wivu Zenda jamani!
Hutaibiwa.” “Na ibakie hivyohivyo.” Akajibu hivyo na kuendelea kumpapasa matiti
taratibu mpaka wakapitiwa usingizi. Usiku wakatoka kwa chakula cha usiku na kwenda
kuangalia movie wakiwa na hali ya furaha.
Usiku wa jumamosi
wakati wanalala, Zenda akaweka ombi kama la mwanae. “Kesho ni siku ya
jumapili. Nilazima niende kanisani. Tutaongozana?” Jelini akaanza kucheka.
“Nini?” “Mwenzio huwa siendi kanisani.” “Utakuwa na mimi.” “Na Kasa akiniona
nipo na wewe je? Au hamsali kanisa moja?” “Hee! Inamuhusu nini yeye!?” Jelini
akashangaa sana.
“Kwamba wewe huna
shida kuonekana na wanao ukiwa na mimi!?” “Ndio nauliza, kwani inawahusu nini
wao!” “Zenda wewe! Ujue nilimkataa Kasa!” “Ukanikubali mimi. Sasa shida ipo
wapi!? Kwani kila wanawake anaotongoza wanamkubali?” Kisha akajirudi. “Labda
nirekebishe. Maana najua wanawake wanampendea pesa, lakini kwako imekua
tofauti. Japokuwa ulijua anayo pesa, lakini ukamkataa yeye na kunipenda mimi!
Sioni tatizo lilipo.” “Hudhani kama watashangaa mimi kutoka na wewe?” “Watakuwa
sawa tu. Usijali.” Akajibu kirahisi kabisa. Jelini akacheka na kutulia.
“Labda wewe ndio uniambie hutaki kuonekana na mimi.” “Mimi unanijua Zenda. Sina wakujificha kwake. Halafu mimi nakupenda. Mwenzio nasikia raha kuwa na wewe popote pale. Nilikuwa nikihofia tu wanao.” “Kama ni hivyo, usijali.” Jelini akatulia kutaka kujua hiyo picha Zenda ataichezaje hiyo kesho mbele ya mwanae! Lakini akafurahi sana. Kwamba hamfichi! “Unacheka nini?” Zenda alimuona akitabasamu mawazoni. “Sikujua kama huna shida ya kuonekana na mimi hadharani hata kwa wanaokuhusu kwa karibu! Nimefurahi hunifichi.” “Wewe sitaweza kukuficha. Nakupenda sana Jelini.” “Nimefurahi.” Zenda akacheka akimwangalia pale kitandani.
Jumapili.
Zenda akamuamsha
asubuhi ajiandae. Jelini akajitengeneza mpaka akaridhika amependeza. Lakini
kila akifikiria Kasa Kevin, kiroho kikazi kumdunda. Zenda akamwambia watoke.
Kwenye gari kimya, kila mtu akiwaza lake. Kwanza ilikuwa asubuhi sana, Jelini
hajazoea kuamka mida hiyo. Akajituliza kitini kimya mpaka kanisani.
Kevin alipomuona
Jelini pale kanisani akawa hajaelewa. Akajongea karibu yao, akiwa na huyo Kemi
kipenzi cha dad na vijana wake wawili. “Huyu anaitwa Jelini. Jelini huyu ni
Kemi, dada yake Kevin na hao wawili ni watoto wa Kemi.” “Nimefurahi…” “Wewe si
umesema huwa huendi kanisani, wewe!?” Kabla Jelini hajamalizia, Kevin
akamuuliza hilo swali kwa mshangao sana. “Mimi hapa nimemfuata Zenda.”
“Zenda!?” Kevin akauliza akizidi kushangazwa na Jelini aliyejibu bila woga
usoni lakini moyoni mapigo mbio. Zenda alikuwa akisalimiana na wajukuu zake,
lugha moja, kingereza. Lakini alisikia swali la kijana wake kwa Jelini. Kemi
alibaki akimwangalia tu hakutaka hata kumsalimia.
“Twende Jelini.” Akamshika mkono wakatangulia
ndani, Kemi na Kevin wakabaki wamepigwa na butwaa. Watoto wa Kemi wakamfuata
babu yao. Misa kwa lugha ya kingereza ikaendelea mpaka mwisho, Jelini
akifuatisha bila kukosea mpaka mwisho na kumshangaza Zenda.
Wakatoka wakasogea
pembeni kama kusalimiana zaidi. Wale watoto wakawa wanamuuliza kitu Jelini kwa
kingereza. “Mimi nazungumza kiswahili. Kwani nyinyi hamjui kuzungumza kiswali?”
Zenda akawa anacheka moyoni. “Kwani wewe hujasoma?” Kemi akamuuliza kwa
kumdharau. “Hee! Kwani kusoma ndio kuzungumza kingereza!? Na wewe kwani
hujasoma? Maana hapo unazungumza kiswahili!” Jelini akauliza bila wasiwasi wala
hofu. Zenda akajua wamepata kiboko yao.
“We Jelini? Kwani
umeachana na Colins?” Jelini akashangaa sana, asijue Kasa anamfanyia makusudi
mbele za baba yake. “Kwani wewe unamjua huyu?” “Mimi hapa naitwa Jelini sio huyu.”
Jelini akamwambia Kemi. “Sana tu. Maana huyu mtoto alikuwa akinitaka sana mimi,
lakini nikaja kugundua anatoka na jamaa tunayefanya naye kazi pale ofisini.
Nikamkataa, nikaweka ukaribu na rafiki yake. Kila mtu mbona anamjua tu huyu
mtoto. Mtoto wa baa tu. Muulize Zilo atakwambia. Kila mwanaume pale mtaani kwao
kashampitia huyu. Shida yake pesa.” Jelini alishangaa kitu kimemkaba kooni nakushindwa
hata kujibu, akabaki akimtizama Kasa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nini kitaendelea kwa WOTE?
0 Comments:
Post a Comment