Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 17. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 17.

Mapenzi na pesa vikaendelea kwa kasi zote. Zenda akawa kama amechanganyikiwa na huyo Jelini. Kila anachompa anaona kidogo. Ofisini hata mwanae akamuona amebadilika. Si wakukaa mpaka mwisho kama zamani. Mchana anaweza akatoka, asirudi tena mpaka kesho yake. Na ujue simu hatapokea. Na Jelini naye asipokuwa naye, simu zake zote video kumuhakikishia haibiwi. Zenda akawa kama mwehu kwa huyo mtoto. Gari alishampa, lakini likabaki kwake mafundi wakiendelea kujenga kwao  kuimarisha ulinzi. Na pesa ya biashara akawa ameshaidhinisha. Na ni yeye mwenyewe ndiye aliyeona wanunue eneo wajenge kuliko kukodi, wala si Jelini akiwa na mama yake. Wao walifikiria biashara ya kawaida tu kwenye frame ya kukodi, iishe. “Huu uuzaji wa kupima mafuta kwa vijiko, utachelewa kufanikiwa.” Zenda mwenyewe akajiongeza.

Ndipo akamnunulia hiyo sehemu sio mbali na Tegeta, tena barabarani akiwa amehamisha watu kwa kuwalipa pesa nyingi tu wampishe Jelini hapo. Mama Jema alishangaa kupita kiasi. Hakuwa akiamini. Na hakusubiri, akaanza kumjengea hicho kituo cha mafuta. “Jelini! Huyu baba wewe unamfanyaje!?” “Nampenda mama. Nampenda sana Zenda. Na usifikiri namuomba, ni yeye mwenyewe na huyo mshauri wake. Sasa sijui huyo mshauri anajua ni vyake au la! Maana naona mawazo mapya kila siku tena makubwa ya pesa nyingi sana. Hapa amesema anataka kuweka kama mgahawa, kwamba watu wakija kuweka mafuta kwenye magari, wakutane na huduma ya chakula.” “MmmH! Na vyote vipo kwa jina lako!?” “Nilikuonyesha karatasi zote mama yangu. Kila kitu ameweka kwa jina langu. Na anasema hataki ijulikane kama yeye anahusika. Nikahisi labda anakwepa wanae.” “Pengine hataki waje kukupokonya.” “Labda.” Mama Jema gafla akawa tajiri, yeye ndio muongoza mambo nyuma ya pazia, Jelini busy na Zenda kitu kilichomfurahisha zaidi Zenda kuona japokuwa anamsaidia, lakini mapenzi bado yapo vilevile.

Kila Kosa, Lina Garama Ya Kulipia.

Kwa Umbali Gani! Muda Gani! Ni Rehema Za Mungu.

Bale alikaa hospitalini kwa majuma manne akipatiwa matibabu ya hali ya juu. Dada yake huyohuyo ndiye aliyekuwa na kazi ya kumuuguza maana Joshua alikuwa akienda kazini. Basi alikuwa akimtuma dereva awe naye mpaka wodini alipolazwa Bale na shariti kuwa jicho lake limuone Naya mpaka anapomrudisha nyumbani. Basi Naya akawa akienda na vyakula anavyopika mpishi wao, anakaa naye, kisha anaondoka mpaka Bale akapona kabisa na kurudisha akili zake timamu na kuweza kumtambua Naya, japo Naya hakuwa akimkumbuka bado ila mtu aliyekuwa katili sana kwake.

Siku ya mwisho anaruhusiwa, ilibidi Joshua mwenyewe atoke kazini, kuwepo ili kulipa hayo mamilioni ya pesa anayodaiwa mgonjwa wake. Akaomba kuzungumza na hao ndugu wawili. “Haijalishi alichokifanya Malon kwenye maisha yake na yenu, lakini mali zake zote, kama yeye hayupo basi ni haki ya wazazi wake.” Akaanza Joshua. “Bale, chochote ulichonacho cha Malon, nitakitaka kwa maandishi, ili wakabidhiwe wazazi wake kihalali.” “Nimeishiwa kila kitu ilibaki ile nyumba tu ambayo ni kama pagala.” “Ile nyumba inathamani sana kwa pale tu ilipo. Bado ndugu wana haki nayo. Je, hayo mashamba yake huko?” “Tokea nilipomchoma moto, sijarudi tena kule.” Naya akashituka sana. Akamwangalia Joshua.

“Naomba usiogope Naya. Tutazungumza.” “Huyu Bale amemchoma moto Malon?!” “Najuta Naya.” “Bale wewe ni mkatili sana! Unaweza kuua mtu?!” Bale akaanza kulia sana. “Ni bangi.” “Hapana. Mimi nahisi ni zaidi ya bangi Bale. Bangi haimpelekei mtu kuua moja kwa moja. Ila labda kumsaidia mtu kutekeleza azma yake. Inamaana ulikusudia kumuua tokea mwanzo!” Naya akawa akizungumza naye, asijue si Malon tu alimchoma moto, hata ndugu zake. Bale alilia sana kwa hofu, maana Naya alimbadilikia kabisa akisikika si Naya asiye na akili iliyochanganyikana. Anajua anachozungumzia.

“Bado nitataka kujua huko mlipokuwa na Malon, alimiliki nini ili kuwafikishia wazazi wake taarifa kamili. Kifo chake na mali zake.” “Kwamba utaenda kunishitaki Joshua!” “Hapo nitakuachia wewe na Mungu wako Bale. Ila sisi tunawajibika kujulisha ndugu zake juu ya kifo chake. Hawawezi kuendelea kuishi hivi bila kujua kijana wao alipo. Halafu mali zake zote, ni HAKI yao. Kwa hiyo, bado nitataka kujua mashamba yake yalipo na mali zake zote.” Naya akatoka nje kabisa hakutaka hata kuendelea kukaa pale.

Joshua akamfuata. “Bale ameokoka.” Joshua akaongea naye taratibu. “Kwani hakuwa amekoka kabla?” Hapo kidogo akakwama. “Unajua japokuwa sikumbuki sana, lakini nakumbuka kusoma kuwa tulikuwa tukiimba naye kwaya kanisani. Inamaana huyu mtu akikasirika anakuwa mbaya Joshua! Mimi alinifanyia vile. Na rafiki ambaye aliniteka kunipeleka kwake, kumbe alimchoma moto! Wewe huogopi ni nini atakufanya siku utakapomuudhi?” “Ninachotaka kufanya akitoka hapa akaishi sehemu niliyokwisha mwandalia ya kuishi. Akiendelea na mazoezi hapa, akarudi kutembea baada ya kupata mguu wa bandia, nimtafutie kazi itakayoweza kumuingizia kipato, na kuachia hapo. Tuone Mungu anatupa naye mahusiano ya nana gani.” Naya akawa kama amekumbuka kitu. Akarudi ndani na kumuacha Joshua amesimama palepale.

“Naomba uniambie ukweli na usinidanganye.” Bale akamwangalia. “Wewe umesema ndiye uliyemchoma moto Malon. Je, baba?” Joshua alishituka sana aliposikia hivyo. Hakujua kama akili ya Naya kwa wakati huo, kama ingeweza kuunganisha matukio kwa namna hiyo. “We Bale? Na usidanganye.” Naya akawa mkali kabisa mpaka kumshangaza Joshua.

“Malon alinishauri vibaya.” Naya akawa hajaelewa. “Usiniambie maneno mengi. Baba na ndugu zetu wengine nilisikia waliungua na moto vibaya sana mpaka kifo. Nani anahusika?” Ikabidi Joshua arudi ndani. “Malon aliniambia tuwashe moto kuunguza tu gala kama kuwakumbusha walipotoka, kumbe yeye alikusudia kuua kabisa. Ndio moto ukaenda mpaka kwenye nyumba na kuwaua baba, Zayoni, bi…” Naya akasikia kizunguzungu cha gafla, akaanguka na kupoteza fahamu. Aligonga kichwa vibaya sana.

Hapana Marefu Yasiyokuwa Na Ncha.

Joshua alishituka, akapiga kelele maana damu zilianza kutoka kichwani alipojigonga. Manesi wakajaa hapo ndani, Naya akatolewa hapo hajitambui na kupelekwa sehemu kupewa huduma ya kwanza. Akazinduka akajikuta amelazwa akashituka sana. “Joshua?” Hilo ndilo la kwanza alilosema. Akaanza kulia sana kama anayejiokoa. “Mimi ni mke wa Joshua, si mke wa Malon. Ameniteka nyara. Naombeni mumpigie simu mume wangu atawahakikishia.” Akili ya Naya ikarudi akiwa mafichoni kabisa. Joshua alikuwa nje ya hicho chumba alichoombwa asubiri wamsadie mkewe, akafurahi maana alishaambiwa hilo na daktari kwamba akili inaweza kurudia ilipopotelea.

“Amenipiga ndio nimezimia. Ananificha kwake, hataki nitoke. Lazima mume wangu atakuwa akinitafuta sana. Naombeni msiruhusu anisogelee.” Yeye akadhania kile kipigo cha mara ya mwisho, alizidiwa na Malon akamkimbiza hospitalini asijue hata Malon hakujali. Aliendelea kumfungia, na ni muda mrefu sana ulishapita. Joshua akaingia kwa haraka.

“Naombeni mnipishe mimi nitamtuliza. Na msimshike kwa nguvu, mtamuumiza.” “Anaruka!” Wauguzi wote wakaongea kwa pamoja wakiwa bado wamemshikilia. “Akiniona mimi, atatulia. Mwachieni.” Mmoja akampisha, Naya alikuwa akilia sana. “Naya, fungua macho niangalie. Mimi ni Joshua. Nipo hapa.” “Malon amenifungia kwake Joshua.” “Najua. Na sasahivi upo salama na mimi. Sitakuacha tena. Sawa?” “Nishike wewe Joshua. Naogopa sana. Alikuwa akinipiga sana. Halafu ananibaka kwa nguvu, kikatili kama mnyama kwa sababu nilikubali kuolewa na wewe.” Joshua akaumia sana. Naya alikuwa akilia kwa sauti ya hofu, anatetemeka mpaka jasho linamtoka. “Nisaidie Joshua.” “Naombeni mnipishe nimtulize. Akili yake ndio inarudi leo. Lasivyo anaweza akajidhuru vibaya akidhani anajiokoa.” Wakampisha.

 Joshua akamnyanyua pale alipokuwa amelala, na kumkumbatia vizuri. “Upo nyumbani Naya. Na upo na mimi salama. Usiogope.” Naya akaendelea kulia, Joshua akimuhakikishia yupo salama na alisharudi nyumbani muda mrefu. Akatulia na kumwangalia Joshua kama asiyeelewa. “Ulisharudi nyumbani mpenzi wangu, ila ulipoteza kumbukumbu. Ulikuwa na uvimbe kwenye ubongo, ukawa ukitumia dawa. Lakini uvimbe ndio ulisababisha kupoteza fahamu. Ila sikujua uliipataje?” “Malon alinipiga teke nikajigonga na kupoteza fahamu. Alikuwa akinipiga sana kila nilipokuwa nikikutaja. Na Bale hakujali kabisa. Aliniacha naye.” “Basi naomba utulie Naya. Upo salama. Na upo na mimi. Sawa?” “Alikuwa akinibaka kikatili sana. Nilikuwa nikilia nikikuita kila wakati nikimsihi Mungu uisikie sauti yangu. Lakini hukuja Joshua. Niliendelea kuteseka peke yangu.” Naya akaendelea kulia, akilalamika na kumuumiza sana Joshua. “Pole Naya wangu. Pole sana.” “Nipime UKIMWI na mimba, Joshua. Malon alikuwa malaya sana.” “Ulishapimwa kila kitu.” “Hapana Joshua. Nataka unipime tena, nione. Mimi naogopa.” Ikabidi Joshua aombe vipimo vyote kwa Naya, ili kumridhisha tu. Akambembeleza akimfariji. Na vile alivyokuwa ameshituka, kuumia vibaya kichwani na dawa alizopewa, akapitiwa na usingizi na kulala.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alipohakikisha amelala kabisa ndipo Joshua akatoka kwenda kumalizia malipo ya Bale na kuomba dereva amchukue na kumpeleka kwenye kinyumba alichokuwa amemkodia. Na mpishi wake ndiye aliyemsaidia kumnunulia kila kitu alichomwambia Joshua kingehitajika kwa mtu kuanza maisha. Na Joshua hakumpunja. Akamnunulia vitu vya thamani tupu. Kuanzia chumbani, sebuleni mpaka jikoni.

Bale anashushwa kwenye hiyo nyumba na magongo yake, akaingia na kukutana na sehemu nzuri ya hadhi ya aina yake. Kama hoteli mpaka kitanda kimetandikwa. Patulivu, kajumba kadogo tu, ambacho kinajitegemea. Aliona jumba kubwa pembeni yake, akajua mwenye nyumba anaishi hapo. Akakaa. “Mlo wa kwanza upo tayari mezani, vitu vingine vipo kwenye friji na makabatini. Namba zangu zipo kwenye hii simu, pamoja na za Joshua.” Akamkabidhi simu mpya. “Ukiwa na tatizo lolote usisite kunipigia mimi au Joshua. Ratiba zako za mazoezi mkuu amesema atampa Pelo ili msikose. Kuna swali?” “Nashukuru sana. Asante.” “Swali?” Akasisitiza. “Kwa sasa sina. Nashukuru. Akamfundisha jinsi ya kufunga na kufungua milango yote, akaondoka na kumuacha hapo.

Bale alipobaki peke yake ndipo  akaweza kufikiria. Akaanza kulia kwa uchungu sana, hajui chakufanya. Picha aliyoondoka nayo hospitalini ni ya lawama kutoka kwa dada yake, na kuanguka kwake vibaya sana. Akapiga magoti hapohapo sebuleni, na kuanza kulia. “Nitaua wangapi hapa duniani Mungu wangu! Tafadhali nirehemu.” Bale akalia mbele za Mungu na kushindwa kusimama. Alilia akitubu tena na tena kana kwamba Mungu anatatizo la kusikia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Huku kwa Naya majibu yakatoka na kuogopesha hata daktari aliyehusika naye maana walisikia Naya alikuwa akibakwa huko alipotekwa. Akarudi kwenye sehemu aliyokuwa amepumzishwa. Joshua akanyanyua uso kumtizama, akamuona na uso uliojawa wasiwasi. Akasimama. “Ni nini!?” “Nina majibu ya mkeo.” “Kuna nini?” “Kila kitu kipo salama, ila amekutwa ni mjamzito.” “What?!” Joshua akamuuliza kwa kuhamaki mpaka akamtia wasiwasi zaidi yule daktari. “Kitanda hakizai haramu ndugu yangu.” “Hapana!” “Halafu si kwamba alijitakia ni jambo ambalo….” Daktari akataka kuendeleza ushawishi akimuhurumia Naya.

“Hapana, wewe huelewi. Huyo mtoto mimi nilikuwa nikimsubiria lakini sikujua ni kwa namna gani au nianze kuomba vipi maana ni kama nilijifunga mimi mwenyewe kwa maneno ya kinywa changu mbele za Mungu, nikitaka kuzaa baada ya miaka miwili baada ya ndoa. Mke wangu alivyorudi nikatamani sana ashike mimba ila nikajiona nitakuwa mbinafsi kwa kuwa bado hakuwa na kumbukumbu. Hatukuwahi kutumia kinga ila akawa hashiki mimba, nikajua mimba haishiki kwa ukiri wangu. Na sikuwahi kumwambia mke wangu wala Mungu. Nikawa najua nimejifunga kwa maneno ya kinywa changu mwenyewe, nikaamua kusubiri tu mpaka muda niliosema mwenyewe ufike, ndipo nizungumze na Mungu wangu tena. Maana aliporudi huyu alipimwa kila kitu hakukutwa na lolote, na hakuwa na kinga na hashiki mimba. Kwa hiyo huu ni wakati wa Mungu. Nimefurahi sana.”

Daktari akashangaa Joshua anapiga magoti palepale pembeni ya mkewe, akasema. “Wewe ni Mungu. Na badala yako, hakuna mwingine.” Acha aanze kububujika mpaka daktari akaondoka! Kwa muonekano wa Joshua, usingedhani hata anahabari na Mungu. Lakini ni mwanaume anayejua kuomba, na si kuomba yale maombi ya kiustarabu! Ni yale maombi ya kupiga magoti popote linapofika swala la Mungu wake. Alilia mbele za Mungu kwa shukurani. Akashukuru hata katika lililompata mkewe, shetani alitaka kuligeuza kuwa baya, lakini akamshukuru Mungu kuwa, ameligeuza kuwa jema. Japokuwa alianguka vibaya na kujiumiza, lakini amerudisha akili ya mkewe, tena akiwa anaiihitaji kwa ajili yake na mtoto wao. Akambariki mkewe na mtoto aliyembeba. Akabariki siku atakayozaliwa. Joshua aliomba mpaka akatosheka. Akakaa akifuta machozi na furaha tele.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hapohapo akampigia simu Geb, mtu wake wa karibu. “Niambie kaka.” Geb akapokea kwa haraka akiwa ofisini mida hiyo ya mchana. “Yule Mungu asiyekawia wala kuwahi, ametutokelezea na sisi LEO.” Geb akacheka. “Ameleta nini?” “Kumbukumbu za Naya.” “Waw!” Geb akahamasika. “Hapana Geb. Hajaishia hapo.” Geb akacheka na kuuliza. “Na nini tena?” “Ametubarikia mtoto. Naya ni mjamzito.” Geb alifurahi sana. “Yupo wapi nimpe hongera?” Ikabidi amsimulie kilichompata mkewe. “Lile baya shetani alitaka limpate mke wangu, Mungu wangu ameliwahi na kuligeuza kufanyika kuwa jema. Wamempa dawa, amepumzika.” “Aisee poleni sana. Tunakuja na Naya.” “Hapana Geb. Msiache kazi kwa ajili ya hili. Naya atakuwa sawa tu, na ninajua watamruhusu leo. Labda mje nyumbani jioni mkiwa na nafasi” “Kama ni hivyo basi tutakuja nyumbani jioni.” “Hapo sawa.” Wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni alipoamka, Naya akawa anajisikia vizuri hata akaamka akiwa na nguvu. “Njoo unishike Joshua.” Joshua akasimama. “Usiogope Naya.” “Nasikia kuumia Joshua! Naumia sana. Bale amenitenda ubaya wa kupita kiasi. Na si mimi tu, ameua familia yetu! Kwa ajili ya nini!?” Naya ndio kumbukumbu ikawa imemjia vizuri. “Yaani sasahivi nakumbuka kila kitu jinsi ilivyokuwa. Unajua nilikuwa nimekwenda saluni. Tena nilikuwa narudi nyumbani. Wakati nikifungua mlango, nikashitukia Bale tuliyekuwa tukimtafuta kwa udi na uvumba, eti amenisimamia nyuma yangu! Nikashangaa sana. Maana Bale aliyekuwa akitafutwa tukidhani yupo matatizoni, hakuwa yule niliyemuona pale! Alikuwa na hali nzuri tu!” Akamsimulia Joshua akilia kwa uchungu sana.

“Naomba utulie Naya.” “Hapana Joshua. Bale alinitendea vibaya tena akiwa anajua fika, simtaki Malon! Kweli ananitoa kwenye ndoa na kunipeleka kwa mwendawazimu yule na kunitelekeza! Hakika Mungu aingilie kati, Joshua. Hujui ni kiasi gani niliteseka kule.” “Naweza kuhisi, maana ulirudi ukiwa umevilia damu, mwili mzima Naya. Ulikuwa ukitisha sana. Pole mpenzi wangu.” Akaendelea kumbembeleza.

“Nina habari ingine.” Akamfuta na machozi. “Mungu ametubarikia mtoto.” Naya akashituka moyoni ila akajaribu kutulia. “Umenielewa?” “Kwani miaka miwili tayari tokea tuoane?” Naya akauliza kwa wasiwasi. Akajua ni kweli anakumbuka kila kitu. “Bado kidogo, ila naona ni wakati wa Bwana.” Akamuona ametulia akijifikiria. “Nimefurahi Naya.” “Sio unaniona mzembe?” “Hata kidogo. Uliporudi tu nilikuwa nikitamani ushike mimba, lakini nikaona si sawa kwako na hali uliyokuwa nayo. Naona Mungu amenihurumia japo nilikuwa nimejifunga kwa maneno ya kinywa changu mwenyewe. Nimefurahi sana Naya. Naomba ufurahie na mimi.” “Mimi napenda sana watoto Joshua, ila wewe ndio ulisema tusubiri. Isingekuwa hivyo, binafsi ningetaka kuzaa mara tu baaada ya ndoa.”

“Nilikuja kujutia sana baadaye, nikajihisi nimekuwa mbinafsi. Halafu nikawa kama nimejipunja mimi mwenyewe kufurahia baraka za Mungu mapema. Kwa sababu tungeweza kuwa na ndoa nzuri tu, na bado tukawa na nafasi ya mtoto. Lakini nikashindwa jinsi ya kujirudi. Nisamehe mpenzi wangu. Hata hili tulitakiwa kuweka mwanya wa majadiliano, kuamua kwa pamoja si kama mimi nilivyofanya, kama kupitisha sheria tu!” Yakaanza mabusu hapo wakimfurahia huyo mtoto. Jioni wakaruhusiwa kurudi nyumbani.

Tamu & Chungu.

Ikawa ni mchanganyiko wa hisia jioni hiyo. Habari njema za mtoto aliyekuwa akitamani hata kabla hajaanzana na Malon, halafu akawa amemkumbuka baba Naya. Kwamba huyo mtoto hatakuja kukutana na baba Naya! Akasikia kuumia sana. “Kwamba hata nikiamua kwenda Kiluvya sasahivi, si kwamba sitamkuta tu baba Naya na Zayon, lakini pia hatuna tena kwetu!” Akabaki amejituliza pale kitini mumewe akiendesha lakini alimuona yupo mbali. Akamuona anajishika tumbo kama anayetafuta kitu humo tumboni. Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu, akatulia. “Utakuwa mama mzuri sana Naya.” Akajaribu kumrudisha kwenye wakati huo. Naya akamwangalia na kuvuta tena pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu akijaribu kutulia.

Akagundua msiba ulishaisha muda mrefu tu, na kila mtu alishaendelea na maisha yake. Yeye anarudi na kumbukumbu ambazo watu walishazisahau! Inamaana hawezi kulia tena msiba. Na nani? Akazidi kuumia kimyakimya na kushindwa kujieleza kwa Joshua mumewe ambaye alishaonekana kuridhika na uyatima wao. Hakuwahi kumuonyesha kama wanapungukiwa na kitu, wao wapo yatima na Mungu ni baba yao. Basi. Akaona na yeye asije anzisha jambo jingine tena. Akatulia kimya mpaka wakafika.

“Acha nikukaribishe tena nyumbani.” Ndipo akaangalia vizuri na kugundua mpaka walifika ndani kwamba hata geti lilipokuwa likifunguliwa, hakuwa akijua. Naya akamtizama akijitahidi kutoa tabasamu. “Maana vile ulivyorudi ukiwa huna kumbukumbu. Sihesabu. Sasahivi umerudi nakukaribisha wewe na mtoto.” Naya akacheka taratibu na Joshua alilitambua hilo akakusudia kumchukulia taratibu.

Akashuka na kuzunguka upande wake, Naya akisubiri kwani alishazoea mumewe kumfungulia mlango. Ila safari hii alimfungulia mlango na kumbeba. Naya akacheka, akamdaka midomo hapohapo nje. Akaanza kupata kisi ndipo wakaingia ndani akiwa amembeba mpaka ndani. “Acha nipandishe ngani mwenyewe nisikuchoshe Joshua.” Naya akaongea akiwa bado mikononi kwa mumewe. Joshua akang’ang’ana mpaka juu kabisa chumbani. Akamuweka kitandani. “Unakumbuka ahadi uliyoniahidi siku walipokuja kukuteka?” Hapo ndipo akili ya Naya ikakumbusha deni alilomwambia Joshua.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwamba angemlipa siku ile akitoka kazini kabla hajatekwa. Alikuwa akiomboleza msiba wa baba yake, kwa hiyo Joshua hakuwa akipata kitu, ndipo akatoa ahadi kwamba, akirudi usiku huo atampa penzi lakukata na shoka, hakuna kulala. Joshua akiwa anatizamia usiku huo kwa hamu, akijitahidi kumaliza kazi kwa haraka, ndipo akapata ujumbe kutoka kwenye simu ya Naya, eti ameamua kumuacha! Haikuwa imeingia akilini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Ahadi ni deni, mama.” Naya akacheka. “Na mimi nimekusudia kulipa deni langu.” Basi penzi likaanza taratibu na kunogeshwa na furaha ya mtoto. Kukawa na utulivu wa namna yake. Hisia mchanganyiko. Wakafanya yao na kubaki wamejilaza hapo kitandani wakipanga yao taratibu. Mtoto huyo apewe chumba kipi ndani ya hilo jumba. Kama atakuwa ni wa kike au wa kiume. Angalau Naya akapata kitu cha kufikiria na kucheka wakijaribu kumfikiria huyo mtoto atafanana na nani.

Walishakaribisha watu wao wa karibu wafike jioni hiyo kwa chakula, kumshukuru Mungu wa Joshua ambaye huwa hatakagi kumkawiza sifa zake. Siku hiyo akawaomba hao watu wao, watenge muda, wale na kufanya ibada fupi kumshukuru Mungu. Mpishi akawa anaandaa chakula cha familia tatu.

Maji Yalishamwagika.

Ilipofika majira ya 12:30 hivi, James na Jema wakawa wameshafika na sheko, wanandoa hao wapya, furaha. Ndoa si ndoano. Bado wapo fungate. Wametoka kupeana kisi la haja ndipo wakashuka garini, wenyeji wao wakisubiria mlangoni. “Kwahiyo Naya sasahivi unakumbuka kila kitu?” “Kila kitu, Jema. Na nakumbuka nikiwa na Joshua, kukuandikia kadi ya shukurani kwa kujitoa kwa kiasi kikubwa kwenye shuguli yetu nzima.” “Niliipata. Hongera na karibu tena duniani. Mungu ameona utoke mafichoni.” “Joshua naye ameniambia hivyohivyo.” Wakakaribishwa ndani.

Hata hawajakaa sana, jeshi la Magesa wakaingia wakiongozwa na Magesa mwenyewe. Joshua na mkewe wakasimama kwenda kuwafungulia mlango, Jema na mume wake wakabaki kimya sebuleni. Wakasikia sauti ya Magesa. “Kwa hiyo sasahivi anti umekumbuka kama mimi nilikuwa rafiki yako?” “Wewe salimia kwanza Magesa, bwana! Wewe vipi baba mzazi?” “Samahani bibi. Nilikuwa nimefurahi mpaka nikasahau kuwasalimia. Shikamoo anko na anti.” Wakaitika. “Kwahiyo unanikumbuka sasahivi?” “Akikazana jambo huyo!” “Nimekumbuka Magesa. Tena tulikuwa tukiimba wote.” Akafurahi sana.

Wakati wazazi wake na ndugu zake wanaingia hapo, yeye akapitiliza sebuleni ndipo akawakuta Jema na James. “Wewe ni anti bibi harusi unayetaka kuingia mpaka chumbani kwa mami wangu?” Magesa akauliza swali lililozua ukimya mpaka kwa waliokuwa wakiingia hapo. Jema alishituka, moyo ukawa kama kumeanguka chuma sakafuni, akabaki kimya. “Mami wako ndiye atakuwa na majibu mazuri. Nenda kamuulize yeye.” Wakasikia James akijibu, ila si Jema. “Kwahiyo..” “Hata hilo swali unalotaka kumuuliza sasahivi, na jingine litakalokujia baada ya hilo. Iwe leo au kesho, juu ya anti na kule nyumbani kwenu, mami wako anayo majibu yake mazuri sana. Muulize yeye.” James akaendelea.

“Na usijewahi kumuuliza tena anti. Yaani siku ile nyumbani kwenu, na leo, iwe mwanzo na mwisho, kumvamia anti kwa maswali juu ya nyumbani kwenu. Usiwahi kurudia tena kumuhoji juu ya maswali ya nyumbani kwenu, au chumbani kwa mami wako, kwa kuwa anti hana uhitaji wowote huko nyumbani kwenu wala chumbani kwa mami wako. Kwa hiyo acha kumvamia kwa maswali juu ya kwenu. Umenielewa Magesa?” Hapo wakasikia sauti ya amri na ukali kutoka kwa James. “Ndiyo anko.” Magesa akasikika akijibu kwa utulivu kama ambaye ametishika.

“Na siku nyingine. Hata kama unafuraha au haraka ya kiasi gani, unapokuta watu wazima sehemu, unasalimia kwanza kama alivyokwambia bibi. Huanzi kwa kuparamia watu wazima kwa maswali, bila salamu. Umeelewa?” “Ndiyo anko.” “Haya, nenda kakae pale, umsubirie mami wako, uje umuulize maswali ya ‘anti bibi harusi aliyetaka kuingia mpaka chumbani kwake’.” Wakajua disco ishaingia mmasai wa uchi.

“Twende mke wangu.” Akamshika mkono Jema, akasimama. Wakawa wanatoka na wale waliokuwa wakiingia hapo wamesimama wameduaa. “Mama G, shikamoo.” “Shikamoo.” Jema naye akapenyeza salamu yake. “Marahaba. Mnaendeleaje?” “Sisi ni wazima kabisaa. Tunamshukuru Mungu.” Akajibu James na kuunganisha. “Jamani sisi tuliwatangulia, acha tuwapishe na nyinyi.” Akaongea James, Nanaa ameinama pembeni ya mumewe. “Lakini tuliandaa chakula cha pamoja kisha ibada ya shukurani James! Mngesubiri kidogo tu, hatutachukua muda mrefu nikijua kesho ni siku ya kazi na shule.” “Basi wenzetu watatuwakilisha kwenye fellowship na swallowship. Acha sisi tuwapishe. Twende Jema.” Akamvuta mkono mkewe na kutoka.

Joshua na Naya wakawafuata. “Tungekaa kidogo Jema!” Naya akaongea kwa kubembeleza akisikika kunyongea tayari. Maana wawili hao walishageuka mashoga tokea harusi ya Jema. Kupigiana simu na kuchati kwa hili na lile likawa jambo la kawaida. Wakajenga ukaribu kuliko Naya na Nanaa, ambaye bado hakuwa akimkumbuka kama walikuwa marafiki. Na kwao hakuwahi kurudi tena tokea siku Malon alipokwenda kwao na kumchukua wao wakiwa ndani, na mumewe kumuokoa mikononi kwa Malon siku ya birthday ya Magesa na Liv.

“Acha tu tukapumzike Naya. Tutakuja wakati mwingine tena. Ilimradi sisi tumeshakuona, na tumepata habari njema tupu, acha itoshe kwa leo.” Naya akanyongea. “Usiku mwema.” James akamalizia na kuondoka na mkewe bila nyongeza. Joshua akawawahi. “Nashukuru kwa kuja jamani.” “Asante sana.” Wakajibu na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kibao kimegeuka kwelikweli. Wakati akitetewa na kulindwa yeye, hakujua madhara yake kwa wengine. Leo anashuhudia ulinzi uleule aliokuwa akipewa yeye, ndio anaupata Jema. Jema aliondoka pale, nusu aombe kuolewa tena na James. Maana kwanza moyo wake haukuwa tayari kuwepo pale chumba kimoja na kina Magesa. Na hata hawakuwa wameyamaliza, ndipo Magesa naye akauliza akiwa hana hila ya kumuumiza mtu, ila kutumia kumbukumbu zake vizuri, kwa haiba yake ya uchangamfu, akili ya kitoto, akaweka petrol kwenye makaa ya moto, yaliyokuwa yamefunikwa na majivu tu. Hata lile jema alilokuwa amekusudia Joshua usiku huo, likaingia doa. Wakabaki yeye na mkewe wakisindikiza gari kwa macho. Kimya wakila janga alilochuma Nanaa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

-       Nini kitaendelea?

-       Jelini na Falia ya Kasa na Zenda mwenyewe?

-       Mahusiano ya James na undugu wa muda mrefu aliotengeneza na Joshua pamoja na Geb? Baraka za wanawake walioongezeka kwenye maisha yao zimeshaanza kuwatenga. Wanaponyaje mahusiano yao au ndio mnara wa Babeli Umevunjwa? 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment