Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 14. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 14.

 Asubuhi wakati mama yake ameamka akimwandaa mtoto wake na yeye akaamka. “Nimsaidie nini?” Akawa mgeni kwa mambo aliyotakiwa yeye ndio aulizwe. “Wala hana mambo mengi. Ila kama utanisaidia kumsindikiza mpaka kituoni na kuhakikisha anapanda daladala hilo lingekuwa la msingi.” Akavaa kwa haraka, na kumsaidia mwanae kidogo tu. Jeremy alikuwa mtoto aliyekwisha fundishwa na bibi yake kujitegemea.

Alipokuwa tayari akamsindikiza. “Unatoka shule saa ngapi?” Mwanae akamwangalia akitembea. “Kwani utakuwepo?” “Hata kama hutanikuta nyumbani lakini nitawahi kurudi kabla hujalala. Shuleni wanakuonea?” “Ni Maliki tu ndio anapenda kuchukua vitu vyangu bila kuomba. Ukimkatalia anakupokonya kwa nguvu.” “Ulimwambia mwalimu?” “Anasema nikimsemelea atanipiga.” Akamuhurumia mwanae na kumkumbusha jinsi alivyokuwa akionewa, tena na baba yake huyohuyo Jeremy halafu anamtisha asiseme.

“Ulimwambia bibi?” “Hajauliza.” Jelini akakwama. “Sasa huwa unakula nini shule?” “Bibi ananipa hela.” “Kwa hiyo hapo unayo hela?” “Ndiyo.” “Inatosha?” “Tumepanga na bibi, huwa inatosha mpaka nirudi kula nyumbani.” “Jeremy wewe ni mtoto mzuri sana.” Akanyamaza tu akitembea. “Umenisamehe nilivyokugawa?” Hakujibu akaendelea kutembea. “Bado umekasirika?” “Nimesamehe mama.” “Mimi ni mama mbaya?” “Umesema umebadilika.” “Na naacha pombe kabisa. Halafu ukitaka kitu uwe unaniambia mimi. Na ukirudi uniambie habari za Maliki. Ila leo akijaribu kukupokonya kitu, mkatalie na akikichukua kwa nguvu na wewe kichukue.” “Akinipiga je?” “Na wewe mpige kwa nguvu zaidi yake mpaka kiume, ndipo atakuogopa. Ukimpiga kama yeye, hatakuogopa. Hakikisha unamkatalia kwa ukali. Akikunyang’anya, chukua kwa nguvu zako zote. Na mwambie asirudie tena.” “Nikimpiga anaweza kunipeleka kwa mwalimu.” “Mkifika kwa mwalimu akitaka kukuchapa, kataa mwambie anipigie mimi simu. Kataa kabisa, mwambie mama ameniambia usinichape, kwa kuwa ni haki yangu. Lasivyo wanipigie mimi simu.” Jeremy akacheka.

“Wakinilazimisha kunichapa?” “Ndio kataa kabisa. Halafu lia kwa sauti waambie wampigie mama yako simu. Nitakuja.” Hakuna siku aliyokuwa na furaha kama hiyo. Hata akabadili kutembea kwake. Akaanza stori kwa mama yake. Wote wazungumzaji halafu akafanana na mama yake. Mtoto wa kiume mzuri, ikawa kama Jelini alijizaa. Wakaanza kuongea wakipokezana  maneno, wanacheka mpaka akamfikisha. “Usije acha kupokea simu!” “Siwezi. Na jioni kabla ya kulala nitakuwa nimesharudi kama hutanikuta nyumbani ili unipe stori za Maliki.” Akacheka. Akamsubiria apande kwenye daladala, akarudi nyumbani.

“Sasa hayo yasiwe ya siku moja Jelini. Sio iwe leo tu, kesho haupo hapa. Utamchanganya mwanao. Ona alivyofurahi ulivyomwambia unamsindikiza!” “Nimebadilika mama. Na hata nikiaga natoka, siendi tena baa, kuepuka vishawishi.” “Sawa.” “Mbona itika yako ni kama hauna imani na mimi!?” “Wewe usiwe na wasiwasi na mimi, ila jiangalie tu Jelini. Mwenzio Jema kang’ang’ania kwenye aliloamini mpaka amefanikiwa mwanaume wamaana. Ona thamani aliyowekewa na mumewe. Sasa wewe uzuri wako wote huo unautumia vibaya, wakati ulitakiwa ukunufaishe zaidi.” Akanyamaza na kuingia ndani kuoga. Akajitayarisha vizuri kama mdada anayelipwa mamilioni ya mshahara. Akatoka.

“Kuna mambo nafuatilia. Yakikaa sawa nitakwambia. Ila siende baa na nitawahi kurudi.” “Hayo unayoniambia mimi, uyakumbuke huko kichwani mwako.” “Hivi mimi katika safari zangu zote nilishakuwa nikikuaga au nilikuwa nikiondoka tu?” “Wewe usinikasirikie mimi bure.” Akaondoka bila yakuongeza neno.

Pesa Huongea Popote.

Mtihani ikawa hakuna uhakika wa kipato kuaminisha Utawala wa kila shule za maana alizotaka mwanae ajiunge, kuwa anauwezo wa kulipa ada bila kuchelewa au kushindwa katikati. Kila alipokuwa akienda, akiulizwa elimu yake mwenyewe na kazi anayofanya, wakaishia kumwambia hakuna nafasi. Akaanza kukosa raha. Akazunguka mpaka majira ya saa sita hajafanikiwa.

Akaona simu ya Zenda ikiingia, akapokea. “Uliamka salama?” “Ndiyo. Na wewe?” “Mimi nipo sawa. Siku imeanza na mambo mengi, lakini nilitaka kukwambia kuna shule niliifikiria, nikamtuma sekretari awapigie simu na kuwaomba nafasi ya mtoto mmoja wa miaka 8. Wameomba uende naye ili wakamfanyie usaili wajue wanamuweka kwenye darasa gani. Sasa nashauri uchangamke. Iwe leo. Maana ni shule nzuri na nafasi zake wanabania sana, mpaka ufahamike.”  Alipomtajia shule yenyewe akaumia sana.

“Mimi mbona wameniambia hakuna nafasi hapo!? Nimezunguka kila mahali wananiambia hakuna nafasi!” “Naomba usilie Jelini. Hao watu mbali ya kutoa elimu kwa watoto, ukumbuke pia wanafanya biashara. Wanataka uhakika wa pesa yao kila muda wa kulipwa unapofika. Sasa wakiona huna kitega uchumi cha kueleweka, lazima watakukataa tu.” Jelini akaumia sana. “Sasa naomba utulie. Nakutumia gari, ukamchukue mtoto kwenye hiyo shule aliyopo, umpeleke wakamfanyie usahili. Halafu utaniambia watakachoamua. Ila wanakutegemea hapo.” “Asante Zenda.” “Karibu. Tutazungumza baadaye.” Wakakata simu baada ya kuelekezana na kuelewana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jeremy alifurahi sana mama yake alipompeleka kwenye hiyo shule. “Nitakua nikisoma hapa?” “Ngoja tuwasikilize kwanza.” Ikawa Jeremy hajawahi kusoma shule za kingereza. Hajui kuzungumza kingereza ila anajua kusoma na kuandika. Walipotaka arudie darasa, hapo Jelini akakataa kabisa. Na anavyochukia shule, akakataa mwanae asirudie darasa. “Mimi mwanangu anaakili. Akisoma hapa kwa muda mfupi tu, ataelewa, mpeni nafasi muone. Ila kama ni kurudia, mimi sitaki, naondoka na mwanangu. Mnataka mwanangu azeekee shule!? Hapana kwakweli.” Hapo hakutaka tena kushauriwa wala kumsikiliza mtu.

Akashangaa hawambishii, ndipo akahisi pengine wanafahamiana na Zenda. Wakashauri masomo ya ziada ambayo atapata hapohapo shuleni. Hapo akakubali. Akapewa kila kitu juu ya mtoto. Akazungushwa na kupewa ratiba ya basi. Muda na sehemu itakayopita kumchukua. Jelini akafurahi sana. Akapewa na sare za shule, tayari kuanza kesho yake. Yaani shule ileile aliyoambiwa hakuna nafasi, ikawa kuna nafasi mpaka yakuanza kesho yake! “Wanaosemaga pesa sio kila kitu, waongo.” Akajisemea Jelini wakati akimsikiliza mwanae anavyofurahia. Maneno mengi kwa furaha akimsimulia hata yale waliyokuwa pamoja kama mama yake hakuwepo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akampigia simu Zenda akilia kwa furaha. Zenda akacheka. “Acha nikupigie baadaye. Kutakuwa kumetulia kidogo. Nimebanwa. Ila usilie, nataka ufurahi.” Jelini akakata kwa haraka. Akaenda kutafuta sasa viatu na begi la shule. Akamnunulia mwanae vitu vizuri sana,  tena vya hali ya juu ili tu aendane na hiyo shule. Kuanzia nguo za ndani mpaka viatu na begi. Aliporidhika hata akifika huko hataonekana ni wa hali ya chini ndipo akarudi nyumbani.

 Mama Jema hakuamini. “Kumbe akili yako inafanya kazi! Sasa usinywe tena pombe. Ukiendelea hivyo naona hata kujenga utajenga.” Jelini akacheka sana. Mwanae akaanza kumsimulia bibi yake habari ya shule ya kizungu. “Nakuja kuchukuliwa na gari, bibi.” Akajisifia Jeremy. Hilo likamfurahisha mama Jema zaidi.

Kwa Zenda.

Jelini hakutoka. Akakaa hapo nyumbani mpaka mida ya saa kumi na moja ndipo akaona simu ya Zenda. Akatoka kuzungumza naye. “Ndio unakuwa busy hivyo!?” Akacheka taratibu “Siyo mbaya sana. Vipi siku yako?” “Nilikuwa tu nyumbani, baada ya kuweka sawa mambo ya Jeremy. Amefurahia huyo! Anaanza kesho. Wanakuja kumchukua na gari ya shule.” “Afadhali. Naona na malipo yamekamilika. Ahadi yangu nimemakamilisha. Ada imelipwa mpaka amalize darasa la saba.” “Nashukuru Zenda. Asante sana. Mama amefurahi sana. Na pia nashukuru kwa kunielekeza vizuri.” “Karibu.” Akataka kusema kitu, akasita. Wakatulia.

“Mbona kama kuna kitu unataka kusema, unasita?” “Natamani kukuona Zenda, hata kwa muda mfupi tu! Ila najua upo busy.” “Leo nimeshamaliza siku ya kazi. Natoka ofisini muda si mrefu. Unataka nikutumie dereva akulete nilipo?” “Ningefurahi, angalau nije kukukumbatia kidogo tu.” Zenda akacheka sana. “Sasa kwa nini kidogo?” “Sijui bwana! Lakini unakumbuka jana nilikwambia nilishakuwa na hamu na wewe?” “Basi acha nimtume dereva, na mimi nitoke hapa. Tutaonana nafikiri baada ya lisaa.” “Sawa.” Akarudi ndani kwa furaha.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Nitatoka, kwenda kukutana na Zenda. Sitachelewa sana kurudi. Jioni ndio anakuwa na muda. Kwa hiyo lazima kukutana naye jioni. Mle, msinibakishie. Na Jeremy uwahi kulala, ili kesho uende shule ukiwa hujachoka.” “Lakini huendi baa?” “Hapana Jeremy. Siendi tena baa. Na nitarudi. Hata kama utalala kabla sijarudi, ujue asubuhi nitakusaidia kujiandaa na kukupiga picha na nguo zako mpya.” “Na viatu na begi langu la shule.” Jelini akacheka. “Kabisa. Na ninajua utapendeza sana.” Mwanae akafurahia, akaingia ndani kuoga tena ajiandae.

Baada ya muda mama yake akamfuata. “Lile gari lililowaleta, limerudi  tena. Naona ndio umekuja kuchukuliwa!” Jelini akaanza kucheka. “Sasa utulie. Maana huyu anaonekana ni mwanaume anayejielewa. Mpaka anakusomeshea mtoto!” “Lakini ujue ni mtu mzima.” “Hata kama ni mzee.” “Kweli mama!?” “Sasa bora lipi? Vile ulivyokuwa ukishinda baa, au huyu anayekujali na kukuongoza vizuri? Ameoa?” “Mkewe ameolewa tena huko Ulaya, na mzungu.” “Kwa hiyo hana mwanamke?” “Sijui mama!” “Basi ndio kumbana mpaka ubaki peke yako. Na kumbana kwa kutulia. Tulia mwanangu, fanya anachokwambia. Anaonekana ana uwezo. Shule anayokusomeshea mwanao ni ya mamilioni ya pesa!” “Na anamlipia na masomo ya ziada pia. Nimefurahi mama. Na asante kunihimiza.” “Basi usichelewe huko.” “Nitajitahidi kuwahi kurudi. Ila kama muda wa Jeremy akifika wa kulala sijarudi, usikasirike.” “Siwezi. Maadamu nishajua upo na mtu mwenye akili nzuri, hapo sina ugomvi. Ila mpime kabla ya chochote.” “Sawa. Ila nampenda. Mzuri huyo! Mweupee. Anangaa kwa usafi kama katoka kikaangoni.” Mama yake akacheka. “Nenda usichelewe.”

Kivulini!

Jelini akatoka amependeza haswa. Akamuaga mwanae, akatoka. Gari safi, akaingia na safari ikaanza akipelekwa asipopajua. Akatulia kimya mpaka Mikocheni karibu na kwa Mwinyi. Geti likafunguliwa, akaingia ndani, Bonge la jumba! Zenda akatoka amevaa nyeupe tupu mpaka sendozi. Alipendeza sana na kuvutia. Akamfungulia mlango. “Uliniambia unaniamini, na huna hofu na mimi, si ndiyo?” Akakubali akitingisha kichwa akicheka. “Basi twende ndani. Nimekupikia kitu kizuri.” Akashuka garini. “Umependeza mpaka unavutia, Jelini!” Akazidi kucheka, dereva akaondoka kabisa hapo. “Hapa ni kwako Zenda!?” “Samahani sijakukaribisha vizuri. Karibu sana nyumbani.” “Asante. Pazuri sana kama wewe mwenyewe! Msafi.” Akacheka. “Nashukuru. Twende ndani.” Akaingia amemshika mkono.

“Kaa hapa sebuleni nilete kinywaji, kisha nitakwambia kitu.” “Natamani hata kukukumbatia kidogo Zenda. Nimefurahi mno swala la mtoto.” “Utanikumbatia mpaka uchoke wewe na kuniaga. Muda wote huu mpaka saa mbili, ni wako wewe tu Jelini. Chochote utakachotaka kufanya na mimi, ruksa.” Jelini akaanza kucheka, Zenda akaenda kuchukua vinywaji akaja na juisi zilionekana nzuri sana kwenye glasi. “Hii juisi ni ya nyanya tu, nimetengeneza na kuweka asali kidogo na ndimu kuweka ladha.” “Inavutia! Asante.” Akamuwekea pembeni.

“Sasa kabla hatujaendelea, unakumbuka jana ulipima, mimi sikupima. Acha nipime hapa mbele yako.” “Na kile kipimo chako ulichonikatalia?” Zanda akacheka sana. “Lakini ilinisaidia kujua kuwa wewe ni mtoto mzuri. Ukikosa unajua kujishusha. Nakuja.” Akaondoka hapo, baada ya muda akarudi nacho. Akamuelekeza jinsi ya kupima na matokeo yanakuje ndipo akajipima. Jelini akafurahi alipoona hana maambukizi ya vijidudu vya Ukwimwi.

“Hongera Zenda.” “Nipo makini sana, kwa sababu wazazi wangu walifanikiwa sana wakiwa bado vijana, ila wakafa pia wakiwa bado wanadai kabisa. Ndio nikaishia kumiliki mali zao zote. Nilijiambia sitaki kurudia kosa. Ndio maana nipo sana makini. Na nikiwa na mtu kwenye mahusiano, kosa la kunisaliti hata mara moja tu, halina msamaha.” Jelini akainama na kukalia mikono yake. “Mimi nina wivu mbaya sana Jelini, na nipo makini mno. Siwezi na sitaki kuchanganywa.” Jelini akaishiwa nguvu akabaki ametulia kimya. “Umenisikia na kuelewa?” Akatingishwa kichwa kukubali.

“Nina swali na naomba uwe mkweli kwangu. Hakuna jibu sahihi wala baya kwenye hili swali. Umenielewa?” Jelini akakubali kwa kichwa akiwa amenyongea. “Je, unaye mwanaume ambaye upo naye kwenye mahusiano kwa sasa?” “Hapana, sina.” Zenda akatulia akimwangalia. “Sidanganyi Zenda. Nimebadilika.” “Naomba kukuamini Jelini. Sitaki uniue.” “Siwezi. Hata mimi sitaki kufa nikamuacha mtoto wangu. Mimi sio mtu wa kulala hovyo na wanaume. Kwanza naogopa.” “Na mimi unaniogopa?” “Wewe nakuamini Zenda.” “Nashukuru.” Akachukua glasi yake ya juisi, na kurudisha vifaa ndani. Akarudi akiwa ameshamaliza. Akapitiliza jikoni.

“Njaa imeanza kuuma?” “Bado. Njoo ukae hapa na mimi.” Jelini akamuita kwa upendo, akamsikia anacheka huko jikoni, baada ya muda akatoka. “Napika.” “Nini?” “Naoka vitu vichache tu. Nataka ule vizuri, ushibe.” Jelini akacheka akimwangalia, akaenda kukaa pembeni yake. “Jelini wewe ni mzuri sana. Sana.” Akamvuta vizuri na kujiweka sawa. “Asante Zenda. Na asante tena na tena. Nimefurahi kuliko nitakavyokwambia. Umenisaidia kubaki na mwanangu.” “Ulishashukuru bwana Jelini! Mbona unataka kupoteza muda kwenye jambo moja tu?” “Ile shule ni garama sana. Mama mwenyewe ameshangaa.” “Sasa umemwambia nini?” “Nimekusudia kubadilika, sikutaka kumdanganya. Nimemwambia ukweli kuwa Zenda ndiye anayemsomesha.” Akakunja uso.

“Mama ameelewa na kuona unaniongoza vizuri kuliko wote. Dada Doro nimekua naye lakini hajawahi hata kumjali mtoto wangu kwa chochote kile. Na nilikuwa nikishinda naye baa hanikumbushi hata swala la mtoto. Wewe mama amekufurahia. Anaona utakuwa rafiki mzuri.” “Kama ndio hivyo afadhali.” Akajivuta. Akaelewa anataka kumlalia kama jana yake. Akajiegemeza vizuri kwenye kochi, akajivuta mpaka kifuani. Akapitisha mkono nyuma akaukutanisha na wa mbele, akawa amemkumbatia. Na yeye akaanza kupitisha vidole vyenye kucha ndogo sehemu ya juu tu alipofikia. Jelini akazidi kujivuta kwake, kisha akamwangalia kama anayetaka kumuomba kitu, akasita, na kurudi kuinama. Naye Zenda kimya.

Akaweka mkono mmoja kifuani kwake akaanza kutembeza vidole taratibu. “Unakua na kazi gani ofisini?” “Acha kunirudisha kazini bwana Jelini!” Akalalamika nakumfanya Jelini acheke sana. “Nataka kujua.” “Nafanya mambo mengi sana, nikikwambia utachoka bure, halafu utanitoa hapa, na kuanza kunifanya nianze kufikiria tena mambo ya kazini badala ya kuwa na wewe hapa. Mimi nataka muda na wewe. Huoni mpaka nimekupikia!” “Kwani huwa hupiki?” “Pale tulipokula jana ndio sehemu yangu ya chakula. Mara chache sana kupika na ni kama sipiki, japo najua sana kupika.” “Mimi najua kupika, lakini sipendi kushika moto ili nisiungue.” Zenda akacheka sana. “Wewe mpishi gani unaogopa moto? Twende nikakuonyeshe glovu. Navaa kila ninaposhika sufuria au sinia zakuweka kwenye oven. Siungui.” Wakaelekea jikoni.

“Mmmh! Jiko lenyewe zuri, hapa huwezi kuungua.” Zenda alicheka sana. “Moto ni moto.” “Si kwenye majiko yenu haya! Jiko halina moshi! Hata mimi ningependa kupika. Sasa kule kwetu mpaka uweke mkaa, upepee mpaka ushike, kabla hata hujabandika sufuria, umeshaungua!” Zenda akazidi kucheka. Akamuonyesha vitu vingi vya hapo jikoni Jelini akabaki akishangaa. “Pananukia vizuri! Ndio unapika nini?” “Viazi nimeponda baada ya kuvichemsha kisha nikaweka cheese na kuweka kwenye oven kidogo kufanya cheese yangu iyeyuke. Mboga za majani, na nimekuokea nyama nzuri sana.” “Nikikubusu nitakuwa nimevuka mpaka?” “Mimi nataka uvuke.” Jelini alicheka sana na kujifunika uso, akahisi mikono yake ikimsogele. Akatulia.

Akapitisha taratibu mpaka kiunoni. Akamvutia kwake. “Nasubiria busu langu.” Afungua macho akakuta akimwangalia, akambusu shavuni. “Hapo utavukaje mpaka sasa!?” Zenda akashangaa akilalamika. “Naogopa.” “Usigope, ilimradi unihakikishie hiyo midomo itabaki kwangu tu. Isipite kwengine.” “Na wewe hivyohivyo Zenda. Ukijalala na mwanamke mwingine, ujue umemuua Zenda wangu, na ndio basi tena. Hatutakaa tukarudi kuwa kama hivi. Tafadhali usinisaliti Zenda.” “Mimi nakuahidi.” Akakubali kwa haraka mpaka akamshangaza Jelini.

“Kwani huna mwanamke!?” “Alikuwepo au yupo, lakini!” Akatulia akifikiria. “Sijui nikwambie nini juu yake. Ni On and Off. Yupo kama hayupo, halafu anakiburi na hasira zisizo na maana.” Hapo Jelini akamuachia. “Subiri kwanza.” “Hapana Zenda. Mimi hivyo sitaweza.” “Ni kama tuliachana.” “Zenda!” “Kweli. Sikumbuki hata mara ya mwisho kuwa naye ni lini!” “Jamani Zenda wewe! Kwa hiyo bado yupo kwenye maisha yako?” “Ni kama hayupo.” “Ni kama!?” “Labda niseme hivi, hatujaachana ramsi, lakini hatupo pamoja.” “Basi naomba unitafute utakapokuwa unanafasi yangu.” Jelini akatoka jikoni kurudi sebuleni alipoacha pochi yake.

“Subiri kwanza Jelini! Mbona unaondoka hata hatujawekana sawa? Wewe ndio umenifahamu. Unafikiri nilikuwa nikiishije? Yule alikuwa mtu wangu mfano nikitaka penzi, namtafuta, basi.” “Jamani nyie Zenda!” Jelini akashangaa sana. Lakini Zenda akaanza kucheka kama mazuri. “Si bora nimekwambia ukweli? Sio kwamba tuna mahusiano fulani. Ilikuwa tukisaidiana. Akibanwa, ananitafuta namsaidia na mimi hivyohivyo. Wanaita booty call.”

“Mimi hivyo sitaviweza. Hayo maisha nimeyaona, na ningetaka kuyaishi pengine usingenikuta hapa na shida zangu, Zenda. Nimezungukwa na ahadi nzuri za mali nyingi lakini na wanaume wa namna hiyo wakulala na wanawake bila shida wala kuwaza mara mbili. Ngono kwao ni starehe kama starehe yakunywa pombe. Sasa wewe unaweza sema kwako ni tofauti, unamsaidia yeye tu, kumbe akikukosa wewe kuna mwingine anayemsaidia. Na huyo anayemsaidia naye anaye mtu wake. Huo mzunguko utakwenda mpaka unawafikia watu kama kina dada Doro, kisha kuja kunirudia mimi. Mwenzio mwanangu mdogo. Sitaki kufa nimuache. Hakika hivyo sitaweza Zenda. Samahani sana.” Hapo Jelini akasalimu amri.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Itakuaje? Maana ni kama Zenda amebeba majibu ya shida zote za Jelini, lakini Jelini na shida zake zote, anamisimamo yake anayoelewa yeye na kuisimamia bila kujali jamii inaishije.

Kumbe na uzuri wake wote angeweza kutumia kujinufaisha kimali, ila hapo, ameweka STOP.

ITAKUAJE NA HARUFU YA MEMA IMESHAMIRI?

Inaendelea?

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment