“Naomba niangalie.
Kaa vizuri.” Akajishauri kama ambaye alikaa pazuri hataki kutoka. Zenda
akatulia tu akimsubiria. Mwishoe akajitoa hapo alipokuwa amemlalia. “Niambie
nini unafikiria kufanya.” “Sasa kama ni shule si nitahitajika kusoma, kulipa na ada! Hapo nitamsaidiaje
mtoto tena?” “Una elimu gani?” Akanyamaza. “Lazima unijibu.” “Niliishia kidato
cha pili, ndio nikashika mimba, sikurudi tena shule.” “Kwa nini?” Akapandisha
mabega juu kukataa. “Lazima unijibu Jelini.” “Ni siri.” “Sasa nitakushaurije?” Akanyamaza.
“Niambie.” Akamsihi kwa kumbembeleza, akaanza kulia.
Moyo Wa Mtu, Msitu.
“Ni mwalimu ndiye
aliyekuwa akikuchezea mpaka kukupa mimba?” Akatingisha kichwa kukubali.
“Ulimwambia mama?” “Aliniambia nikisema atanichinja
mimi na familia yangu yote. Mimi nahisi ni mvuta bangi yule.” “Mlikuwa
mkikutana wapi?” “Alikuwa akinituma kwake halafu
ananifuata baada ya shule. Inaniuma Zenda, halafu eti nilivyoshika mimba akanipiga,
akaniambia mimi ni mjinga. Najiachia mpaka nashika mimba hovyo. Akaendelea
kunipiga eti ananiambia nimtaje aliyenipa mimba maana si yake na wala nisiwahi
kumtaja popote. Nikimtaja atanichinja kama kuku. Hapo alikuwa amenipiga kupita
nitakavyokwambia, halafu akanifukuza kwake. Nilikuwa siwezi kulala mpaka
nilivyojua kuwa pombe ni dawa. Kuwa ukilewa kabisa unakuwa hukumbuki tena.”
Hapo akaelewa kwa nini anashinda baa.
“Pole sana Jelini.
Sasa Doro ulijuana naye vipi?” “Baa tu. Na yeye
alikuwa na matatizo yake, tukakutana wote pombe zinatusaidia kulala, ndio
tukawa tunaongozana. Tukishakunywa, tunaenda kwake kulala.” Jelini
akaendelea. “Ila baadaye yeye akasema yeye
hatakubali lazima alipe kisasi, ndio akaanza.” “Naomba usinifiche.
Niambie.” “Ndio akaanza kulala na watu makusudi ili kuwaambukiza huo ugonjwa. Sijui
alikutana na mtu mwenye gonjwa la zinaa kali, akamuambukiza huko kwenye kulipa
kwake kisasi, lakini aliumwa. Aliumwa sana. Sasa hapo ukumbuke anavyo hivyo
vijidudu, hana kinga ya mwili, halafu akapata huo ugonjwa wa zinaa! Zenda! Yule
dada aliumwa. Nilimuuguza mpaka mimi mwenyewe niliingiwa hofu nikadhani
atakufa. Anavuja usaha tu, unanuka! Lakini akaja kupona.”
“Sasa eti amepona
badala atulie, akaapa hataacha kulipiza kisasi. Ataendelea tu kuusambaza na
wengine wapate kama yeye. Ndio mimi nikaingiwa hofu kabisa ya kulala na
wanaume.” “Ni kwa nini sasa analipiza kisasi?” “Ila usimwambie mtu. Wewe
nimekuamini.” “Sitamwambia mtu.”
“Dada Doro alikuwa
mlokole kama Jema. Kwa anavyodai yeye alikuwa mwaminifu sana mpaka akapata huyo
mchumba ambaye walikaribia ndoa kabisa. Anasema alikuwa amejitunza. Wakati
wanakaribia ndoa anasema siku moja huyo mchumba wake akamwambia yeye amezidiwa,
amsaidie. Anasema akamuhurumia maana alimbembeleza sana, halafu hakuona shida
kwa kuwa alijua atakuja kuwa mumewe. Wakaanza taratibu mpaka ikafanyika mazoea
wakawa kama wana ndoa.”
“Maisha yakaendelea
lakini akaanza kuona anambadilikia. Hata swala la ndoa nalo anaendelea kulipiga
teke kwa sababu zisizoisha. Ikabidi sasa kuanza kumfanyia uchunguzi, ndipo akaja kugundua kumbe huyo mwanaume
alishakuwa na mke kabisa, alioa. Mkewe akaja kufa na mtoto kwa ugonjwa mbaya.”
“UKIMWI.” Akaweka sawa. “Ndiyo. Na mbali ya hilo akaja kugundua kuwa ni tapeli tu
na mengi aliyokuwa amemwambia alikuwa akimdanganya. Ndio ikabidi aende akapime
kujithibitisha. Bahati yake mbaya, akakutwa ameshaathirika. Ndio hasira hizo
kwa wanaume wote na kuwalipiza kisasi. Bila bia kichwani, hawezi lala.”
“Kabla huyo mwalimu
hajakuharibu akili, ulitamani kuwa nani maishani?” “Nesi. Nitibu watu wagonjwa.
Mtu akija hospitalini anaumwa sana, basi nambembeleza na kumpa dawa.” Zenda
akacheka. “Si unajua bado unaweza kuwa nesi?” “Sitaki kusoma tena. Kila
mwanaume akiniona ananitaka tu kimapenzi. Halafu wakishajua nipo chini yao,
wanatumia nguvu. Sitaki.” “Haitakuwa kama mwanzo Jelini. Naomba fikiria
kabla hujakataa.” “Mimi sitaki kusoma. Sitaki kurudi tena shule.” “Unataka nini?”
“Kitu kitakachoniingizia pesa ya kumtunza mtoto wangu na mimi.” “Sasa ofisi
gani itakuajiri na wewe huna vyeti? Ndio utaishia kupata kazi ya kuwagawia
mabosi chai, unarudia mtindo uleule.” Jelini akacheka sana.
“Acha dharau bwana!”
“Nakwambia ukweli.” “Basi nifanye biashara.” “Biashara gani?” Akabaki akiwaza,
hata hajui watu wanafanyaje biashara wakati amezungukwa na mama zake wote
wafanyabiashara. Akakwama kabisa. “Jipe muda wakufikiria halafu utaniambia.”
“Nimefurahia kukaa hapa na wewe.” Zenda akacheka. Akavuta mkono wa Zenda kwa
upendo, mwenyewe akimwangalia tu, kisha akaushika vizuri. “Asante kuwa na
mimi.” “Karibu. Na mimi nimefurahi umeongea na mimi lakini huyo mwalimu lazima
akamatwe ili asichezee watoto wengine.” “Mimi sitaki kesi.” “Unafikiri wewe
ulipoondoka, aliacha hiyo tabia yake?” “Sidhani. Aisee ni mkatili yule kaka!
Anakufanya mchezo mbaya kama vile wewe ni mnyama. Na akimaliza anakufukuza kama
mbwa!”
“Nitumie jina lake,
shule uliyokutana naye, nitamfuatilia tu. Ila uwe tayari kujitetea wewe na kwa
niaba ya wengine wanaopitishwa hapo.” “Acha kwanza nitulie kwenye maisha Zenda.
Kesi zitanichanganya, watanichukulia mtoto wangu.” Hapo anaongea, anachezea
vidole vya Zenda. Anavipanga hivi na vile.
“Nakupa kazi.” Jelini
akamwangalia kwa mshangao akidhani anataka kumuajiri. “Kesho nenda katafute
shule nzuri sana ya mtoto. Usiogope bei. Kisha unijulishe. Mimi nitamlipia
mpaka amalize darasa la saba.” Jelini alibaki akimwangalia. “Umenielewa?”
Kimya. “Acha kufa ganzi bwana! Niambie kama umeelewa?” Akaanza kulia. Safari
hii akajirudisha kifuani kabisa na kumkumbatia akililia kifuani kwake. Usicheze
na Jelini.
“Nilijua ungefurahi!”
Akajiliza hapo mpaka akatulia akimbembeleza mgongoni. Wakatulia kwa muda,
Jelini hata hatikisiki, kamkumbatia, kimya. “Tutachelewa kitabu cha mtoto.” “Asante Zenda. Asante sana.” “Basi kesho ufanyie
kazi. Uliza kila kitu, mpaka usafiri, nguo, na michango mingine. Ikiwezekana
tukikutana tena, unijie na fomu zote.” “Kesho si siku ya kazi, nina uhakika
unakuwa busy.” “Jioni itakuwa muda mzuri.” “Saa
ngapi ili nisikusumbue na simu.” “Nitakupigia. Ila kama kuna swali,
usisite kunipigia kuniuliza. Ila isiwe pesa ya ada. Hiyo nimekupa ruhusa,
ilimradi iwe shule nzuri. Kiasi cha ada kisikuogopeshe.” “Mimi napenda vitu vizuri.” “Najua.” Kisha
akamsaidia na kumfuta machozi vizuri.
“Tuondoke hapa.” Zenda
akashauri. Akajitoa hapo kifuani, wakahamia viti vya mbele. Akamuona Jelini
ametulia. Akamuacha tu mpaka akamfikisha sehemu, akamsaidia kununua vitabu
viwili vya mtoto wa miaka 8, akamsogeza mpaka karibu na usafiri. “Si umeshasema
unaniamini?” Akamuuliza baada ya kuweka gari pembeni. “Wewe nakuamini.” “Basi
naomba safari hii mimi nikulipie usafiri na wa kesho wakati ukitafuta shule.”
“Nashukuru sana Zenda. Asante.” “Karibu.”
Hakujua anamuagaje.
Anampa mkono au! Akajifikiria Zenda na yeye ametulia tu akimchukulia taratibu.
Akamuona anachukua vitu vyake. “Ukalale salama, Zenda.”Akamwambia kwa upendo. “Na
wewe.”Akashuka akiwa haamini. “Akija kubadilika kesho!” Akaanza kuingiwa
na wasiwasi. “Nisije kumtafutia mwanangu shule halafu apotee!” Akawaza
Jelini akielekea kwenye taksii. Akaona hilo asimwambie hata mama yake, asije
akaendelea kuonekana muongo.
Moyo Umependa.
Wakati akimsindikiza
kwa macho, hapohapo akampigia simu Zilo.
Zilo alipoona tu simu ya Mzee Kasa mwenyewe, akapokea kwa haraka sana. “Unamfahamu Jelini, anaishi Tegeta?” “Yule binti ambaye Kevin
alitaka nimfuatilie?” Mzee Kasa akafikiria kwa haraka akajua atakua ni
yeye tu. “Uliambiwa nini juu yake?” “Ila mimi
nilimwambia ukweli kwa vile nilivyopata taarifa zake. Kama kuna jingine, basi
nitakuwa nilidanganywa, au Kevin mwenyewe hakuwa amenielewa.” Ikawa ni
kama anajitetea.
“Wewe
ulimwambia nini?” “Huyu binti ni wa Tegeta. Ana mtoto alizaa nasikia akiwa
shule. Maskani yake ni baa akiwa na msichana mwingine anaitwa Doro yeye ndio
kama anayemnywesha.” “Ana mwanaume gani?” Mzee akaendelea kuhoji. “Kwa nilivyopeleleza, anakunywa na huyo Doro na ndiye
anayeondoka naye kila siku kama hatarudi kwao. Inavyoonekana japo Jelini
mwenyewe hajajua, ni kama huyu Doro anamchukulia wanaume. Yule muhudumu wa pale
baa wanayopenda kunywa, nilivyozungumza naye alisema kwa jinsi
walivyomchunguza, ni kwamba kila mwanaume anayemsogelea Jelini, Doro anajitahidi
kumuwahi yeye na kuishia kuwa naye. Wanavyodhani ni kama Doro anamuweka Jelini
karibu ili kujinufaisha naye kwa wanaume watakaokuwa wakimtongoza. Maana mtoto
mwenyewe si mchezo! Mimi mwenyewe nilipomuona huyo Jelini, nikasalimu amri na
nikamuelewa Kevin kwa nini ahangaike na mwanamke wa aina hii.” Zilo
akaendelea, mzee akaweka umakini.
“Kwa hiyo
huyo Doro anamuweka karibu na kuwa naye kila siku hapo baa. Japo wanakunywa
kama kundi. Wapo wanaume wengine mpaka wazee tu na nyadhifa zile za juu haswa
hata ukiona, utawashangaa, ndio wanakuwa nao hapo. Nilipotaka kujua ni yupi kati
yao anatoka naye au alishawahi kutoka naye, sijapata uhakika kwa ukweli.” Hapo akamshitua
tena. “Unamaanisha zipo fununu yupo na mtu!?”
Wivu tayari.
“Hapo ni
kama tena pana utata. Ukitaka kujua ni yupi kati yao kwa hakika, inakuwa kama
hakuna uhakika tena. Ila ni wale wasichana walioshindikana makwao. Mtoto wa baa
asubuhi mpaka usiku. Sio msichana wa maadili wa kama hadhi ya Kevi. Na hilo
hata Kevin mwenyewe sikumficha.” Zilo anaongea, asijue mzee anajiulizia
mwenyewe sio mkwe tena.
Kukumbatiwa na binti
mdogo kama Jelini, kachezewa vidole, na akapewa jina jipya! Hali ikawa
imeshatibuka ndani ya mzee. Akili imevurugwa. Akawa anamtaka Jelini haswa.
Akaona aachane na Zilo. Anataka kumchanganya tu. Akamshukuru na kukata simu.
Kisha akamrushia pesa kitu anachokipenda
sana Zilo. Pesa itoke kwa mzee mwenyewe. Habani.
Penzi Kikohozi.
Akaanzwa na tamaa.
Wivu, hataki mtu amsogelee tena Jelini. Akatamani kumpigia, akaona awe
mstaarabu, ajikaze kiume asije onekana amepagawa kama wanaume wengine aliozoea
kuwaona Jelini jinsi wanavyotapatapa. Akaanza kutuma pesa bila kufikiria asijue
anatuma kwa Jelini ambaye hajazoea kuhongwa. Akatuma zaidi ya mara tatu huku
akihisi ni chache. Mwishoe akajiambia atulie.
Jelini kuona pesa zinaingia mfululizo
akampigia. “Zenda, nahisi unabonyeza sehemu, pesa
zinajituma kwangu!” “Nataka zikusaidie.” “Hii pesa ni nyingi sana Zenda!”
“Usijali. Utanipigia kunijulisha kama umefika nyumbani salama?” “Safari hii
nitafanya hivyo Zenda. Ila nimeshakuwa na hamu na wewe.” Zenda akacheka
taratibu na kutulia akijikaza kiume asije onekana fala kwa Jelini aliyezoea
kubabaikiwa.
“Nimefurahia
muda na wewe Zenda.”
Akaweka msisitizo kwa upendo. “Na mimi pia. Tutatafuta
muda mzuri zaidi. Ila naomba ukumbuke ahadi zako Jelini.” “Nitabadilika Zenda.”
“Hapana. Niambie umebadilika. Jelini niliyemkuta leo asubuhi, asirudi
tena. Ukijihisi upweke, nipigie. Na achana na Doro
kabisa. Tutalipa kisasi kihalali, si kwa kuuza miili.” Jelini akajisikia
vibaya. “Sitarudia tena Zenda. Nakuahidi.” “Nashukuru.”
Hapo akajisikia vizuri haswa. Bila kutarajia Jelini akajikuta anajitia
kitanzi yeye mwenyewe kwa mzee.
“Ila sasa
hivi napitia hapo baa kuchukua kuku wakupeleka nyumbani.” Hapo akamtibua
kabisa. “Jelini! Kwa nini hukusema wakati tunakula ili
wafungiwe na wao?” Zenda hapo akalalamika na kujisahau kabisa kana
kwamba yeye ameshakuwa mmiliki halali. “Sitakaa Zenda.
Nakuahidi sitakaa.” “Hayo mazingira ukirudi haitachukua muda kukuridisha nyuma.
Tafadhali usiende Jelini. Utaninyima usingizi na kunifanya nishindwe kufikiria
kabisa.” Akajikuta anasalimu amri. Wivu umemlemea. “Basi Zenda.” “Sio kwamba sikuamini! Ila hakuna sababu
yakujitia vishawishini. Tafadhali mtume mtu akakununulie.” “Naona nitafanya
hivyo.” Wakatulia.
“Sitakwenda
Zenda. Acha nirudi tu nyumbani, nitampigia mtu wa pikipiki akafuate chakula.” Yale aliyomwambia
mwanae kuwa yeye hayataki, mtu kutawala maisha na ratiba zake. Kumpangia wapi
awepo, akajikuta anayakubali kwa baba mtu bila kujijua. Tayari akajihisi
anawajibika na furaha ya Zenda. “Hilo ni wazo zuri. Upo
kwenye taksii tayari?” “Tayari, hapa napita baa
ilikuwa niingia lakini naelekea nyumbani. Sisimami tena. Na wewe umeshafika
nyumbani?” “Bado. Nimekutana na foleni kidogo.” “Pole. Basi nitakupigia tena
baadaye. Acha nimtume mtu akachukue chakula.” “Usinisahau kama asubuhi.”
“Sitakusahau Zenda. Nitakupigia.” Wakaagana. Zenda akitamani ageuke
upepo amfuate awe naye. Gafla akawa anajihisi anaibiwa.
Nyumbani.
Akafika kwao akamkuta
mama yake na Jeremy wamekaa sebuleni kimya, macho kwenye luninga yao ya kawaida
tu. “Nimepima na cheti hiki hapa.” Mama yake akaanza kucheka. “Sasa unacheka
nini? Kama nimeathirika je?” “Mbona wewe nakujua! Ungekuwa ukilia, ningekufuata
hukohuko hospitalini. Sasa tulia Jelini.” “Nimekoma mama. Ujue kwa nini nilienda
kupima?” Mama yake akabaki akimwnagalia. “Mwenzio nilikuwa nikienda kulala kwa
dada Doro wala si kwa wanaume. Ana nyumba nzuri yule dada, sasa napenda
chumbani kwake usiku anawasha A/C unalala usingizi mzurii.” “Tafuta vyako, acha
kutaka vya watu.” “Nimesema nimebadilika.” Akaendelea kusimulia.
“Sasa ile kuamka leo
nisipopajua, na mkasema nilimgawa Jeremy, nikasema usijekuta nikiwa nimelewa
huko, wananifanyia mambo mabaya. Ndio nikaona nipime.” Mama yake akamwangalia
na kunyamaza.
“Nimekuletea zawadi
ya vitabu Jeremy.” Akaongea kwa kujikomba kwa mwanae. Akamuona amefurahi sana
mpaka akatoka pembeni ya bibi yake na kumsogelea. “Vitabu gani?” Akavitoa
kwenye pochi na kumkabidhi. “Au sio aina ya vitabu unavyosoma?” “Sasa hivi
nasoma chochote tu nitakachokipata. Asante.” “Unisamehe jana nilikugawa. Wewe
ni mtoto mzuri Jeremy. Mimi ndio mama mbaya. Lakini nimebadilika. Na naacha
pombe kwa ajili yako. Umesikia?” “Utakuwa ukirudi kulala hapa?” “Sasa hivi
sifanyi kama zamani nita…” “Wewe mjibu mtoto, acha maneno mengi.” “Namuelezea!”
“Hapana Jelini. Wewe jibu maswali yake aridhike.” “Nataka kusema hata kama
nikutoka nitakua naaga na kuwaambia ninapokwenda na kurudi.” “Hapo sawa.”
Akatulia.
“Nimeagiza chakula,
wanaleta. Nimekuagizia na bia mbili, mama. Na wewe fanta yako, wataleta.” “Na
wewe?” Mwanae akamtega. “Mimi sitakunywa.” Jeremy akafurahi, mama yake
akacheka. “Makubwa! Lakini nashukuru.” Jelini akacheka na kujituliza. Mama yake
akamuona amepoa. Macho kwenye tv tu. Kisha akamuona kama amekumbuka kitu, akatuma
ujumbe. ‘Nilifika nyumbani. Nipo nimekaa tu.’ ‘Nataka
kukusikia Jelini. Ukipata nafasi unipigie.’ Akacheka akisoma ujumbe wa
Zenda. ‘Unalala saa ngapi?’ ‘Huwa nawahi kulala kwa
sababu naamka mapema sana.’ ‘Kwa nini?’ ‘Nitakujibu tukizungumza.’ ‘Sawa.’
Akajibu na kutulia. Kimya.
Kweli chakula
kikaletwa na bia mbili tu, na fanta moja ya mwanae. “Wewe huli?” “Nilishakula
na rafiki yangu tulipotoka kupima.” “Anaitwa nani?” “Mama jamani! Mimi sitaki
kusema uongo. Nimebadilika. Acha kunichimba.” “Si umtaje tu jina?” “Anaitwa
Zenda.” Mama yake akashangaa hilo jina. “Wa wapi?” “Usiendelee mama bwana! Ila
ujue ni mtu mzuri, yeye ananiongoza vizuri.” “Bora.” Akasema tu hivyo na
kuendelea kula. Wakamuona anasimama. “Naenda kuzungumza na simu, nitarudi.”
“Zenda huyo?” Akamchokaza, Jelini akacheka sana. “Mama Jema!” “Au kuna mwingine
tena, Zenda anaibiwa?” “Sijaona wakumuibia Zenda, mimi.” Mama yake alicheka
sana, Jelini akakimbilia nje.
Moyo Haujafundishwa Kupenda, Umependa.
“Nakuwahi
kabla hujalala.” “Nisingelala mpaka nikusikie.” “Kweli Zenda?” “Kabisa. Hapa
nimebakiwa na harufu yako kifuani mwangu.” Jelini akacheka kwa kudeka. “Kujibu swali lako lile uliloniuliza. Nimeshajizoesha kuamka
alfajiri na mapema tokea kijana mdogo sana. Kichwa changu kinafanya kazi vizuri
mwanzoni mwa siku. Nikishafanya mazoezi asubuhi, naanza kazi. Kwa hiyo na
kulala pia huwa najitahidi kulala mapema ili angalau kuupa mwili masaa angalau
nane yakupumzika.” “Ndio maana unaonekana kama kaka yake Kevin.” Zenda
alicheka sana.
“Kweli! Una
mwili mzuri sana.” “Mazoezi na kula sahihi. Na pia namshukuru Mungu, sina
magonjwa yanayokuja na uzee. Kwa hiyo mwili haujapatwa shuruba nyingi.”
“Hongera. Kwa hiyo unajiandaa kulala?” “Nimeshakusikia hivi, na najua upo
sehemu salama, naingia kulala sasa.” “Asante kujali.” “Tutazungumza zaidi
kesho.” “Usiku mwema.” “Na wewe Jelini.” Wakakata simu, kwa mara ya kwanza
Jelini akasikia upendo wa ajabu sana ndani ya moyo wake. Akasahau hata swala la
umri.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi ndani na kutulia. Hata wao hawakuwa wamemzoea Jelini huyu. Akakaa hapo mpaka wakakubaliana kwenda kulala. Alilala akimtafakari Zenda na kutamani kukuche amuone tena. Gafla alichokisema Zenda kikatimia. Yeye ndio akaanza kumpenda. Akakumbuka na kujicheka mwenyewe hapo kitandani, gizani, asijue kwa Zenda ndio zaidi. Alimpenda huyo Jelini kuliko alivyopenda kwa… Akabaki akiwaza mwenyewe kitandani. Akasita kila alipojaribu kuvuta aina hizo za hisia kama alishazipata kabla. “Aisee sidhani!” Akajipinga mwenyewe akiwa hapo kitandani kwake. “Jelini ni wa tofauti aisee!” Akawaza Zenda huko upande wa pili. Yeye anawaza kwake, na Jelini akabaki akiwaza vyake huku akiogopa asije kuwa tofauti kesho yake. Akabaki akiwaza mpaka akapitiwa na usingizi mawazoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nini Kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment