“Mimi nilikuwa
nimelewa!” “Sikukwambia wewe uache pombe hazijawahi kukupenda ukanibishia na
kusema mbona mimi nakunywa! Sasa ndio ujue kichwa chako kilivyo kibovu,
ukaongea mengi wee, mpaka mtoto akaanza kulia, ndio Jema akamwambia yeye
atamchukua, ila wakiwa safarini atazungumza vizuri na mumewe wapange. Ndio
kamjibu leo asubuhi. Ujue jinsi mwenzio alivyoumia.” “Mimi nilikuwa nimelewa
mama! Sijamaanisha.” “Basi ushamwaga mchele kwenye kuku wengi. Na unamjua Jema
hapendi mambo ya vigeugeu. Ushamgawa mtoto hadharani, yeye na mumewe wamesema
watamchukua na kumsomesha. Ndio uwe huru sasa, endelea na kuzurura kama kuku wa
kienyeji. Halafu sasa nikusikie unabadili mawazo, wakati mimi nataka huyu
asomeshwe shule za maana, na wewe hali yako kama hivyo. Kazi huna, una kazi ya
kulewa tu na kumangamanga.”
“Ila mimi sijasema
simtaki mtoto wangu.” “Jana ulisema.” Mwanae akaweka msisitizo. “Si nilikuwa
nimelewa! Sasa mtachukuliaje kama simtaki?” “Ulisema mwenyewe. Sasa nikuone
unamgeuka Jema.” “Mimi nataka niishi na mwanangu.” “Unaishi naye wapi na wewe kwanza
huwa hulali hapa. Pili kazi huna, kazi yako pombe na kuvaa vizuri? Utaweza
kumsomesha shule za maana huyu?” Hapo akapoa. “Nakuuliza wewe.” “Nitatafuta
kazi.” “Basi ukipata hiyo kazi. Ukaniletea huo mkataba wa hiyo kazi, na
ukalipwa, ukaniletea ada yake huyu, ndio nikusikie unaongea unachokiongea
sasahivi. Lasivyo usitake kunifanya mimi mjinga. Wewe ukatae shule.
Mtoto atake shule, eti umkwamishe hapa kwa starehe zako zisizoisha!” Mama yake
akamjia juu.
“Lakini mimi namtaka
mtoto wangu. Sitaki mtu amchukue.” “Wewe mwenyewe hushindi hapa. Kutwa upo
baa.” “Mbona nimebadilika siku hizi siendi tena, hata nikitoka narudi kwa
wakati.” “Wewe unajua mwanao alilala wapi jana mpaka kumkuta hapa hivi leo?”
“Si ulikuwa naye wewe!” “Ujue wewe mtoto unawazimu Jelini wewe! Unashindana na
mimi wakati wewe akili huna! Mwenzio nilizaa na nikalea. Nilikuwa nakunywa, na
wanangu wanapo pakulala na wanakula. Hamjawahi kushinda njaa. Tena kwa jasho
langu. Niliwasomesha mpaka wenyewe mmekataa shule. Wewe unaniiga, huna
hata kibanda! Mwanao hujui hata anachosoma hapo ni nini!” “Nimebadilika.” “Jana
ulilala wapi?” Kimya.
“Jelini?” “Jana
nililewa sana, lakini kuanzia leo naacha pombe. Naanza kumfuatilia mwanangu.
Sitaki mtu amchukue mtoto wangu. Mimi ndio maana hata nikiondoka hapa, narudi
kwakuwa najua yeye mwanangu yupo. Mkimchukua nitakuwa sina sababu yakurudi hapa.
Hata kama mimi ni mama mbaya, lakini nampenda mwanangu na nimesema
nitabadilika.” Hapo hata mama yake
akanyamaza.
“Nilikosea jana
kukugawa, Jeremy. Nimekosa. Na nishajua pombe inanifanya sifikiriii, sinywi
tena. Na nishaachana na Doro, nitakuwa nalala nyumbani. Hata kama nikiwa
natoka, nitakuwa nikiwaambia. Lakini msimgawe mwanangu.” “Na shule? Maana
sitaki apate elimu ya kuunganisha. Maadamu nimempata mwenye hela na yupo tayari
kumsomesha, nataka asome. Sasa labda unipe mpango mwingine.” “Ndani ya
huo mwezi nitakuwa nishapata jibu. Lakini usimgawe mwanangu. Hata kama ni
Kayumba, atasoma tu.” “Hapo hapana Jelini. Hatasoma Kayumba, kama kuna uwezo.”
“Basi nipe huo mwezi.” “Na nikiona tabia zako za ulevi bado zipo halafu
hubadiliki, Jema akija kumchukua, ujue nampa.” “Sawa. Na samahani Jeremy. Jana
nililewa. Lakini mimi sikugawi.” Mwanae akanyamaza tu. “Hata mtoto mwenyewe
hakuamini.” Akamwangalia mwanae na kuingia ndani akilalamika.
“Msimgawe mwanangu
kama mzigo. Mimi bado namtaka mwanangu. Pombe ndio zinanifanya vibaya.” “Kwani
unanyweshwa?” “Si ndio nimesema naacha sasa! Mbona hamniungi mkono?” “Labda kwa
sababu kila siku unasema jambo halafu unageuka.” “Haya, mwanao huyo, umemsikia.
Hata yeye amechoka.” “Mimi nataka kusoma. Nataka kusoma sana ili nije
kukusaidia na wewe baadaye.” Wakamsikia akilia ndani. “Soma mwaya Jeremy labda
kweli utamsaidia huyo.” Akalia wee, mwishowe kimya.
“Kashalala hivyo.
Akiamka hapo safari ya baa.” “Sijalala, nawaza. Na wala
baa mimi siendi tena. Labda..” Mama yake akaanza kucheka nje baada ya
kusikia, ‘labda’. Jelini akaona anyamaze tu maana alishaahidi sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akabaki akijitafakari
hapo kitandani mpaka akaanza kuingiwa hofu. Mara ngapi amekuwa akilewa na
kuamkia asipopajua! Nini anafanya akiwa amelewa bila kichwa chake kutunza
kumbukumbu! Akaogopa sana kila alipokuwa akikumbuka na maneno ya Zenda. Akaamua
kujiangalia afya yake. “Wasijekuwa wanakuwa wakinifanyia mambo mabaya
wakinipa pombe zao za bure.” Akafikiria bia za bure anazopewagwa baa,
lakini akiwa na akili zake anawakataa. “Je nikiwa sijitambui!” Hofu
ikamuingia zaidi. Akakumbuka Zenda alimwambia huwa anakuaga na kipimo cha
UKIMWI.
Usitukane Mamba, Bado Hujavuka Mto.
Akaoga haraka na
kubadili nguo. Akampigia Zenda. Ikaita sana, wakati inakaribia kukatika
akapokea. “Uliniambia una kipimo cha kupima UKIMWI.
Naomba nije nipime.” “Wewe ni mtu wa ajabu sana Jelini! Umenikatia simu kitu
ambacho hakuna mwanadamu anaweza kunifanyia hivyo na kunikatalia kwa jeuri kwa
kiasi hicho. Wewe kwa nini unakuwa mtu wa kupenda kutumia watu tu?”
Jelini hakutegemea! Kutoka kwenye kubembelezwa mpaka kukaripiwa! “Sasa kwa kuwa umeshindwa kuniamini na unanidharau, na mimi
SITAKI. Nenda kaangalie afya yako hospitalini ambako utakuwa salama nao, sio
mimi.” Simu ikakatwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Hilo wazo ulilokuwa
nalo naunga mkono, na usibadili mawazo. Nenda hospitalini ukapimwe ujijue. Unanisikia
Jelini?” “Naenda mama.” “Usikatishwe tamaa. Na achana na huyo Doro. Ndiye
anayekurudisha nyuma kila siku. Siku mbili tatu ulizomkatalia kwenda kwake,
ukatulia hapa nyumbani, ukawa mtu. Jana umekutana naye tu, akili zikawapaa,
mmelewa na kuondoka na mwanaume hata msiyemjua. Hujui anagonjwa gani! Hujui
kama alitumia kinga au la. Kama kweli unataka kuanza upya, nakuunga mkono,
nenda kapime ujijue.” “Sasa kwa nini unasikiliza nikizungumza na simu zangu?” “Uliyeongea
naye huko sijamsikia. Ila wewe tuliyekuwepo wote hapa, hukufanya siri. Wote
tumesikia. Na nakupongeza Jelini mwanangu.” Akamtia moyo ili asije gairi.
“Sasa kama nimeathirika?” Jelini akauliza kwa
wasiwasi. “Ndio utaanza kuishi kama muathirika, na kutumia madawa. Ila ujue
ndio Jema kajipatia mtoto. Sitakubali umkwamishe Jeremy kwa shida wala raha
zako. Ukienda kukutwa na gonjwa huko, jua na mtoto huna.” “Sasa mbona naogopa?”
“Mwana kulitafuta.” Mama yake akamjibu yeye akiwa chumbani, mama yake sebuleni
na Jeremy anasoma mezani.
“Kwa nini sasa
unaniambia hivyo?” Akaanza kulalamika. “Wewe ni mara ngapi umeniona mimi silali
humu ndani?” Kimya. “Hata siku moja. Kama sipo hapa mjini nipo kwa mama yangu
kijijini nakwenda na Jeremy kwa kuwa sikuamini naye, unaweza ukaondoka na
kumuacha hapa. Lakini je, bia sinywi?” Kimya. “Nakunywa na kurudi nyumbani na
akili zangu timamu, au nakuja kunywa hapa nikimuona Jeremy, au hata nikitoka
naenda kumuacha kwa bibi zake, nawahi kumchukua, na kurudi naye nyumbani.
Lakini wewe kichwa chako hakifikirii. Kinakwenda kutafuta pombe, basi.”
“Nabadilika. Na…” “Wewe usiongee sana. Anza hatua ya kwanza uliyoamua, na ili
pia tukuamini, urudi hapa na majibu. Sio ukutane na bia za bure huko, unywe na
kwenda kulipa fadhila huko usiku kuchwa.” Jelini akazidi kuogopa akishindwa
kujibu kama kweli analalaga kwa wanaume au la. Akatoka.
Mbio Za Sakafuni, Sasa Ukingoni.
Huku kwa Joshua na
Geb wakaegesha magari yao nje ya hiyo nyumba waliyoelekezwa na kuingia ndani.
“Kwamba ndio hakuna hata milango na madirisha!” Akashangaa Joshua kwa kuumia.
“Nafikiri ndivyo alivyomaanisha yule mlinzi akipaita gofu.” Geb akajibu
wakiingia ndani. Harufu mbaya sana ikawafanya wasimame hapo mlangoni
wakaangaliana. Kulikuwa kunanuka kama kulioza kundi la panya.
“Bale?” Akaita
Joshua. Akaita tena na tena, kimya. Wakaona waingie tu. Ndani kulikuwa kuchafu
mno. Wakaanza kuingia kila chumba wakimuita. Wakasikia mtu akikohoa chumba
kingine. Wakaingia na kumkuta mtu amelala juu ya maboksi tu na mengine
amefunika miguu. Joshua akahisi atakuwa yeye tu. “Bale?” Akamuita tena kwa
kumuhurumia sana, hakujibu. “Acha nipigie simu gari ya hospitali, waje
wamchukue. Wao wataweza kujua jinsi ya kumtoa hapo nakumuweka ndani ya gari kwa
usalama huku wakimpa huduma ya kwanza bila kumdhuru zaidi.” Geb akatoka baada
ya kutoa hilo wazo. Joshua akaenda kumshika. Alikuwa anachemka joto, anagugumia
kwa sauti ya mbali, kama mwenye maumivu makali sana. Akamtizama mguu
kuhakikisha aliyoambiwa. Akawa ameufunika na boksi, unatisha hata hautizamiki.
Joshua akajikuta
akilia sana. Alilia, mpaka Geb akarudi ndani. “Tafadhali jikaze Joshua. Gari ya
hospitali inakuja.” Geb akajaribu kumtuliza lakini hata yeye alijua hali ni
mbaya. Bale aliotwa nywele kama msitu kichwani na mandevu. Chafu. Amekonda
kupita kiasi. Ananuka, kuwepo karibu yake ni mpaka uwe ulimfahamu baba yake, na
unaishi na dada yake kama mke, na ni rafiki wa Joshua ambaye anakubeba kipindi
cha shida yako. Geb akatulia.
Ndani ya nusu saa,
gari ya wagonjwa ikawasili wakamtoa Bale pale sakafuni, lakini hata wenyewe
walikuwa wakilalamika hali mbaya. Alikuwa akitoa harufu mbaya sana kama
aliyeoza. Wakachana maguo aliyokuwa amevaa, wakamfunika shuka la hospitali
wakati mmoja akimtafuta mishika ya kumuwekea maji. Wakahangaika naye, baada ya
dakika 15 nyingine ndipo wakamtoa hapo akiwa na maji kwenye mishipa, safari ya
hospitalini ikaanza. Joshua na Geb wakifuata gari ya wagonjwa nyuma
wakikimbilia hospitalini. “Wewe ni Mungu, na badala
yako hakuna mwingine.” Hilo akalirudia Joshua bila kuchoka mpaka
wanafika hospitalini.
Kulikosifiwa Mgema!
Jelini anafika
hospitalini, na Bale naye anafikishwa hospitalini ila kila mmoja kwa shida
yake. Hofu iliyokuwa imemkamata Jelini, ilizidishwa na vile alivyokumbuka hali
ya Doro, alipogundulika anagonjwa la zinaa kali, huku ana vijidudu vya UKIMWI.
Kilio chake na maneno yake akihuzunika kuwa maisha yake ndio yamefika mwisho,
vyote vikawa vikijirudia kichwani kwa Jelini anatetemeka kama ameshikwa baridi.
Hapo amekaa akisubiria zamu yake, maneno yote ya hofu ya Doro yakawa yakijirudia
kichwani mwake, ndipo akaelewa hofu ya Doro. Hofu ikamzidia, akashindwa kujituliza
kabisa.
Akatamani kama
angekuwa na yeye na mtu kama vile yeye alivyofanyika faraja kwa Doro. Angalau
awe naye hapo, aongee chochote, lakini akajikuta hana mtu. Jema yupo fungate.
Mama yake anasubiria majibu nyumbani. Gafla akakumbuka ahadi ya Zenda. Utayari
wa kuwa naye karibu kwenye mabadiliko yake. Akaumia jinsi alivyomuudhi.
Akaongezeka mwingine tena aliyemuumiza, mbali na Jeremy, akawa na huyo Zenda.
Akaamua kumtumia ujumbe. ‘Mwenzako mimi ni mtu mbaya,
Zenda. Ninamkosea kila mtu. Ila naomba msamaha. Nilikosa adabu.’ Akatuma
huo ujumbe. Baada ya dakika 5 akaona simu ya Zenda inaingia. “Nimekuudhi sana?” “Ndiyo.” Zenda akamjibu. “Nisamehe. Nilikukosea sana. Ila mwenzio nimechukua ushauri
wako. Nipo hospitalini.” Zenda akacheka maana alimwambia tu kwa hasira. “Wapi?” Akamuelekeza. “Nakuja
tuwe wote.” Jelini akajishangaa anaanza kulia. Wema aliomtendea Doro,
ukawa haujaoza. Na yeye akapata mtu. Akajisikia kulia kwani alikuwa ameingiwa
hofu na mpweke. “Usilie nakuja.” “Asante.” Safari hii akamuacha yeye ndio akakata
simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hata haikuchukua muda
mrefu sana, Zenda akawasili hapo hospitalini. Alipomuona akimsogelea akasimama.
“Nimefurahi umekuja Zenda. Mwenzio naogopa sana.” “Njoo tukae hapa na uniambie
nini kinakuogopesha.” Wakaenda kukaa sehemu wakijitenga na watu. “Nini
kinakuogopesha?” “Mimi najua watu wanao ambukiza watu kwa makusudi kama
kulipiza kisasi.” “Kama Doro?” Jelini akashituka sana. “Mimi sijamtaja mtu jina!”
“Niliunganisha mazungumzo yetu na vile nilivyokusikia ukimwambia asubuhi ulipogundua
amelala na Kevin.” “Kumbe kule nje mlikuwa mkisikia!?” “Sikuwa nimeelewa mpaka
tulipokuwa wote garini. Nitataka kujua ni kwa nini anafanya hivyo. Ila nataka
kujua ni kwa nini wewe una hofu.”
“Nimejifikiria na
kujiuliza, usiku kama ule wa jana kuamkia leo, kwenye maisha yangu imetokea
mara ngapi maana huwa sikumbuki! Na je, huwa nikiwa nimelewa, nani ananichukua
na nini kinatokea nikiwa sijitambui! Maana inaonekana nafanya mambo ya ajabu
sana. Kwa mfano jana nasikia nilimgawa mtoto wangu
hadharani. Nimefika leo ananiaga, hata sijui kilichoendelea!” “Usilie.” “Mimi niache nilie tu. Nasikia uchungu. Nilimgawa mwanangu
eti na kusema simtaki! Yaani Jema akiwa katikati ya fungate ndio anamfikiria
mwanangu na kumtumia ujumbe kuwa wamekubaliana na mumewe watamchukua wamtunze
wao, halafu mimi sina habari! Namwambia mama ni pombe tu, sijamaanisha, ameniambia
nikirudi na vipimo sijaathirika, ada yake, na mabadiliko ndio hatamgawa
mwanangu. Kwa kuwa yeye anataka Jeremy asome sana.” “Sasa nisikilize
Jelini. Hiki unachokifanya nakiunga mkono sana.” Akamfuta na machozi kama
katoto kadogo.
“Kujua afya yako ni
jambo la msingi. Na kingine ambacho lazima kujua, unaweza kurekebisha kuanzia
hapa tulipokaa, kwenda mbele. Nyuma huwezi tena. Kama ulishaharibu,
umeharibu. Lakini kuanzia sasa, unaweza kubadili. Kujutia, na kujilaumu,
nikupoteza muda na haitakusaidia wewe wala Jeremy. Tukitoka hapa tutazungumza
zaidi maana na mimi nina maswali mengi. Tulia, pima, kisha tukitoka hapa, tutapata
muda.” “Asante Zenda.” Akaendelea kumfuta
machozi kwa upendo, Jelini akafurahia kupendwa vile.
“Kumbe kweli kupendeza ni kawaida yako!” Akamfanya
Jelini acheke sana. “Kwa hiyo hata hapa nimependeza?” “Sana tu.” Wakacheka na
kutulia. Akajisogeza vizuri kwa Zenda, akapitisha mkono kwapani kwake, akamvuta
kwake karibu na kumuegemea. Zenda akacheka akili ya Jelini. Hapo anafanya hana
hata wazo la pili kufikiria macho ya watu au hata kama huyo Zenda amemruhusu!
Yeye amejisikia kumsogeza kwake akafanya na kujituliza vizuri utafikiri
anamfahamu huyo Zenda kwa miaka mingi. “Ukitulia hivi unakua mtoto mzuri!”
Jelini akacheka taratibu akifikiria huku amekumbatia mkono wa Zenda kuanzia
chini ya bega.
“Nitabadilika. Ila
nina hofu sana.” “Kwani wakati mwingine huwa unaamkia wapi?” “Kwa dada Doro.
Ila najiuliza kabla ya hapo nakua wapi na huwa nafanya nini! Maana tunakua katikati
ya kundi la watu wengi. Mimi na dada Doro tu ndio wanawake, wengine wote
wanaume.” “Kati ya hao kuna ambao ulishakuwa nao kwenye mahusiano?” “Kwa akili
zangu hizi, hapana Zenda. Ni wale wanaume malaya wakulala na yeyote,
tena wala si kwenye nyumba za kulala wageni kitu ambacho ndio kinanitia hofu.
Wanamalizanaga nao hapohapo baa! Sasa mimi nilishawakatalia tokea mwanzo, tena
niliwaambia wao ni wachafu hata kwa kuvaa kondomu mimi siwataki. Na
usifikiri ni wanaume wa hovyo! Watu na hadhi zao kabisa. Wana mahela, kwa hiyo
tupo kama washikaji tu kupeana kampani. Ila sasa ndio nimeingiwa hofu.”
Zenda akamshika mkono
vizuri akipishanisha vidole kama kumtuliza. “Aisee naogopa Zenda, naogopa sana.
Maana ni wale wanaosema sio sabuni kwamba itaishia baa, nakushindwa kufikisha
nyumbani kwa wake zao. Wachafu wakulipia hata kunyonywa tu, halafu wanarudi kwa
wake zao. Malaya wanawajua kama wanazo pesa na wanataka huduma. Sasa sijui aisee!”
Zenda akabaki kimya akiwaza binti kama huyo anaishi vipi maisha kama hayo!
Akaminya mkono taratibu kama kumtaka atulie. Wakatulia mpaka ilipofika zamu
yake, akatolewa damu na kusubiria majibu.
“Utafanyaje juu ya
Kevin?” Akacheka na kumgeukia. “Kwa hiyo sio Kasa tena narudishiwa jina langu?”
“Hapana bwana! Wewe utabaki kuwa Zenda. Mbona zuri tu! Au hujalipenda?” “Jinsi
unavyolitamka linavutia. Sijawahi kupewa nickname.” Wakacheka. “Kevin
ameshapima. Na nimemwambia nitamtaka na vipimo vya hospitalini mpaka magonjwa
ya zinaa.” Jelini akashangaa sana. “Kwa nini?! Si anasema alitumia kinga?”
“Kumdhalilisha zaidi. Nakumfanya azidi kuongeza umakini.” Jelini akifikiria
akimtafakari Kasa, Kevin vile alivyo jeuri. “Asipokubali kupima?” “Hathubutu
kwa kuwa hataki kukabiliana na madhara ya kutotii.” Jelini akawa hajaelewa.
“Kevin ni jeuri wa
kurithi kwa mama yake, lakini anapenda starehe ambazo pesa yangu ndio
inamsaidia kuishi anavyoishi kwenye jamii. Kama isingekuwa ni pesa yangu, nina uhakika
asingekuwa akinitafuta kabisa hata kwa salamu, sababu ya upendo kwa mama yake.
Sasa kwa kuwa anaishi kwenye nyumba zangu na kutumia pesa zangu atakavyo
akijiaminisha yeye ndio mrithi, nikifa kila kitu kitabaki kuwa chake, inabidi
aendelee kujinyenyekeza tu kwangu. Lakini si kwa mapenzi kwangu au kupenda
kwake. Yeye ni miongoni mwa wengi wanaonifuata sababu ya nilicho nacho ili
kujinufaisha. Kwa hiyo hana jinsi. Lazima atafanya kila ninachomuagiza.” Kidogo
Jelini akamuhurumia, akamvuta mkono zaidi na kujiegemeza, akabaki kimya
akitafakari.
Akaitwa kuchukua
majibu yake, ikawa hajaathirika. Alifurahi Jelini, nakujikuta akilia tu.
Akatoka hapo hajui aendapo ila machozi tu akiendelea kuongoza njia. “Sasa
unaenda wapi?” Ikabidi Zenda asimame na kumuuliza. “Nimefurahi
sana Zenda, siamini! Acha tu niende.” “Wapi?” Ndipo akasimama na
kujikuta yupo nje sehemu yakuegeshea magari. Akaangalia kulia na kushoto,
akaanza kucheka. “Muone!” “Nimefurahi! Nimefurahi
sana. Nilikuwa nimeingiwa hofu. Nikajua nitakufa nimuache mwanangu.”
“Hilo ni onyo, Mungu amekupa, kisha na nafasi ya pili Jelini. Usibwete, tumia
vizuri.” “Nabadilika. Na sasahivi nitaongeza umakini zaidi.” “Twende basi
tukale chakula kizuri, kusherehekea.” “Sasahivi nakubali. Tutakwenda wapi?”
“Wewe unataka nini?” Akamwangalia na kucheka.
“Umewaza nini huko kichwani
kwako kilichokufurahisha?” “Natamani tukae kama tulivyokaa pale hospitalini.
Ilinituliza.” Zenda akacheka taratibu akimwangalia, Jelini akaona aibu. Zenda
alibeba uzuri wa Kirwanda. Mrefu amenyooka kama raisi wao Kagame. Halafu akapewa
rangi nyeupe pee iliyomvutia Jelini mpenda wanaume weupe. Bila kutongozwa
akajikuta anaanza kuvutiwa naye. Halafu akajaliwa unadhifu wa pesa. Akajua kuuvalisha
mwili wake vizuri. Alivutia, jinsi alivyokuwa akimwangalia hapo Jelini,
mwenyewe akalainika. “Nilikuona vile ulivyokuwa ukitetemeka.” “Lakini si uliona
nilitulia?” Akamuuliza kwa upendo kama si yeye aliyemkatia simu. “Nilikuona.”
“Kuna hali fulani hivi, mwenzio nilijisikia. Nataka nijaribu tena, nione kama
nitatulia ili nifikirie na kuweza kujua chakufanya.” “Na chakula?” Jelini
akabaki akifikiria. “Twende tukale kwanza halafu tutapata muda wa kutulia.” Akakubali.
Akatafuta sehemu
nzuri, ya hadhi yake yeye, tulivu, wakaingia humo. “Nataka kukaa pembeni yako.”
“Nataka ukae mbele yangu, nile nikiwa nakuangalia.” Jelini akacheka na kukaa
mbele yake. Zenda akaagiza juisi ya embe akiomba iwekwe ndimu ila akaomba starter
kwanza. Supu ya mbogamboga. Jelini na yeye akasema aletewe kama Zenda. “Wewe
huwa unaongea ukila?” Akacheka na kumuuliza. “Ulitaka kuongea nini?” “Kwa mtu
ambaye hajasoma kabisa, anaweza kufanya kitu gani cha kumuingizia pesa?” Zenda
akakunja uso akifikiria.
Kisha akamuuliza. “Ukisema
hajasoma, unamaanisha hajui hata kusoma na kuandika?” “Anajua hivyo bwana! Sasa
wewe unafikiri kuna mtu wa namna hiyo?” Akacheka akiendelea kufikiria. “Kwanza
nitataka kujua ni kwa nini hajasoma. Uwezo au mazingira ya shule hayakuwa
rafiki au hapendi tu shule! Ikiwa ni moja wapo ya sababu hizo mbili za mwanzo,
huyu mtu ni rahisi kumshauri. Lakini kama ni mvivu tu wa shule, hataki ile
shida ya shule, kuamka asubuhi na ile kuweka jitihada, inamaana huyu mtu hata
akipewa kazi au biashara ataharibu tu kwa kuwa hana ile inayohitajika
kufanikisha jambo gumu. Sasa sijui kama unanielewa?” Jelini akanyamaza kabisa.
“Mbona tena kimya?”
“Wewe unaongea kisomi sana bwana.” Akalalamika. “Nakwambia ukweli wa maisha
Jelini na wala hapo hakuna usomi. Labda uniulize swali katika nilichozungumza
ambacho hujaelewa.” Kimya. “Hicho unachokificha ndilo jibu lako lilipo.” “Sasa
si ujibu tu! Kwamba kwa mtu ambaye hajasoma sana, ila anajua kusoma na
kuandika, anaweza kufanya nini kuingiza pesa?” “Japokuwa unakwepa ukweli wa
kwanza, labda niulize huyo mtu anapenda nini?” “Labda hajui.” Akabaki
akimwangalia kwa mshangao.
“Basi labda niseme
hajafikiria.” “Kwa sababu si wote waliofanikiwa kwenye biashara, wamesoma sana.
Na pia hakuna uzee kwenye elimu. Hata mtu kama mimi nikiamua naweza kurudi
shule na nikasomea kitu fulani na nikafanikiwa kabisa.” Hapo Jelini akakwama.
Arudi shule! Hakutaka kabisa. Akapoa, na yeye akamuacha. Kwa chakula Zenda
akataka kiazi ulaya kilichookwa na Crub. Jelini akatoa macho. “Nzuri sana. Ila
wewe unaweza kuagiza na samaki au kuku wa kuchoma. Nitakuonjesha crub. Ukipenda
siku nyingine ndio uagize.” Akaona wazo zuri, akaagiza hicho kiazi ila na
samaki wakuchoma. Wakatulia mpaka chakula kikaletwa.
“Mbona vyako
vinaonekana vizuri?” “Acha nikuonjeshe uone ladha. Unaweza kupenda.” Akamuona
anatumia kisu na uma kutoa nyama ndani ya huyo crub kisha akamlisha. “Nzuri!” Akapenda.
Akamuona anamuita muhudumu. Akamuagiza crub kama wake. “Usiingie garama Zenda!
Acha mimi nile tu samaki, siku nyingine ndio nitaagiza.” “Usijali.” Wakaendelea
kula. “Nipe uma wako nikuonjeshe samaki. Ana ladha nzuri sana.” “Kwani uma wako
una nini?” “Nimetia mdomoni tayari, Zenda!” “Hamna neno.” Jelini akasita.
“Sitaki kukulisha uchafu wangu.” “Wewe si mchafu. Nipe tu.” Ikamgusa sana
Jelini. Kwamba hamuonei kinyaa! Akamkatia. “Hiyo ni kubwa sana.” “Utafurahia.
Fungua mdomo.” Akamuwekea na kubaki akimwangalia ili asikie anasema nini juu ya
huyo samaki aliyemuwekea mdomoni.
“Umependa?”
“Ulivyonilisha, ndiyo. Ila hawa samaki wa hapa nawafahamu.” Jelini alicheka
sana. “Zenda!” “Nisingekuleta sehemu ambayo wanavyakula vya kubabaisha. Huwa
nakula hapa karibu kila siku. Napenda vyakula vyao.” Jelini akatulia akimtafakari
huyo Zenda. Na Zenda naye kimya akimtafakari mtoto mzuri Jelini. Wakala mpaka
wakamaliza.
“Bado unataka kuwa
karibu na mimi au umeshatosheka?” “Tena kidogo tu halafu ndio niwahi madukani
nikaangalie vitabu vya watoto. Jeremy anapenda kusoma vitabu.” “Vya aina gani?”
Hapo akatulia. “Jelini!?” “Sijui.” “Kwamba hujui mtoto anapenda kusoma vitabu
vya namna gani?!” “Naomba usinishangae Zenda.” “Labda niulize sasa wewe
ungeenda kumnunulia vitabu gani?” “Nilikuwa sijalifikiria hilo. Ila naweza
kumpigia simu nikamuuliza.” Zenda akabaki kimya akifikiria.
“Cha kwanza mnunulie
tu kama surprise. Hata ukikosea, lakini atajua unamfikiria. Halafu kuanzia hapo
tafadhali onyesha unajali Jelini.” “Nitabadilika.” Wakatoka hapo. “Kama una
mambo mengi yakufanya nisikucheleweshe Zenda. Mungu atatujalia tutapata muda
wakati mwingine.” “Usijali. Twende tukakae sehemu ndipo tuagane.” “Wapi?” “Hofu
na mimi imeisha?” Jelini akacheka akimwangalia kwa aibu kidogo, maana Zenda
alimtizama kiume. “Eti Jelini?” “Wewe nimeanza kukuamini.” “Kwa hiyo hutaogopa
ukijikuta sehemu tuko peke yetu?” “Hapana Zenda. Sitaogopa. Nakuamini.” “Kama
ndio hivyo twende.” Akampeleke mpaka ufukweni. Hapakuwa mbali sana na walipopata
chakula. Ila hawakuingia kwenye hoteli. Pembeni tu ya barabara ila upande wa baharini.
Akatafuta sehemu nzuri, akaegesha gari.
“Si unataka kukaa
karibu yangu?” Akatingisha kichwa kukubali akitabasamu. “Basi tukae hapo nyuma
kwa muda mfupi, ukiridhika na kuniruhusu, tutaondoka.” “Sawa.” Wakahamia kiti
cha nyuma. Jelini akajisogeza karibu kabisa, akamnyanyua mkono akajiingiza
chini ya kwapa kabisa, Zenda ametulia tu akimwacha ajiweke sawa ila akimsaidia kufanya
anachomulekeza kwa vitendo. Akajipanga hapo pembeni ya kifua chake, akapandisha
miguu juu, akatulia. Akajua ameridhika na alivyokaa. Akamuwekea mkono juu,
akambusu kichwani pale alipojiegemeza kwake. Wakatulia kabisa lakini akamfanya
Jelini ajisikie kitu cha tofauti.
Akili Za Mungu Zisizochunguzika.
Huku kwa Bale,
hospitalini alifikishwa mapokezi, hata daktari akawaambia anahitajika chumba
cha upasuaji akatwe sehemu ya chini ya mguu ambako kulishaoza. “Atahimili
upasuaji kweli! Yupo dhaifu mno.” Joshua akauliza kwa wasiwasi asijefia chumba
cha upasuaji. “Hatapewa dawa ya usingizi kabisa. Itabidi apate ganzi tu ya mguu
ili kuweza kukisafisha hicho kidonda na kutoa nyama zilizooza. Ila kwa jinsi
ninavyokiangalia, itabidi akatwe tena kidogo.” Joshua akaumia sana.
“Joshua, nadhani kwa
sasa huna chaguzi ila kukubali ahudumiwe kwa haraka. Bale anahitaji msaada wa
haraka.” Ikabidi Geb amuongeleshe maana ni kama alipoa hivi, akikumbuka maisha
ya hao watu jinsi alivyowakuta kwao Kiluvya. Familia ya maana tu, yeye akiona
imebarikiwa hata nakutamani na yeye angekuwa ametokea hapo. Bale akiwa na nguvu
zake. Amemaliza shahada yake ya kwanza, akiwa na kiu ya maendeleo! Akajikuta akimalizia
mawazoni, “Malon!” Akaumia sana.
“Ila mjue kwa hapa na
hizo huduma zote kama mtaridhia, itawagarimu sana. Labda mumpeleke kwenye
hospitali za serikali.” Daktari akawatahadharisha. “Hapana. Pesa isiwe tatizo.
Maadamu yupo hapa, tafadhali msaidie tu.” Joshua akaridhia. Bale akaingizwa
chumba cha upasuaji akabaki Joshua na Geb.
“Nashukuru Geb,
lakini nashauri wewe rudi nyumbani angalau ukapumzike. Itoshe kwa leo. Kukitokea
chochote nitakujulisha.” “Unauhakika Joshua?” “Huna unachokifanya hapa, na kama
ulivyosikia, inaweza kuchukua muda mrefu. Wewe nenda tu kwa familia yako. Wasirudi
na wewe haupo. Acha madogo wamalizie weekend na wewe. Sisi tutawasiliana tu.”
Geb akaondoka, akamuacha hapo Joshua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akamkumbuka mkewe,
akampigia. “Ulifanikiwa?” “Nilimpata. Lakini hali yake
si nzuri. Ni mgonjwa sana. Sasa hivi yupo chumba cha upasuaji, ndio namsubiria
atoke.” “Pole Joshua. Bado upo na Geb?” “Nimemruhusu akapumzike. Maana inaweza chukua
muda mrefu.” “Basi mtume dereva aje anichukue nije tukae wote.” “Una uhakika?”
“Kabisa Joshua. Ulivyojitoa hivyo! Acha na mimi nitembee kwenye imani yako.
Nitajificha mpaka lini?” “Na utakuwa na mimi. Huna haja yakuogopa.” Naya
akacheka akianza kujiandaa.
Baada ya muda akawa
ameshafika kwa mumewe wakimsubiria Bale nje ya chumba cha upasuji. Naya akaona
aulize. “Joshua? Ni kwa nini unafanya yote haya, tena kwenye hospitali kama hii
ya garama!?” “Sijui ni kwa nini mimi, Naya! Maana Mungu angeweza kumtumia
yeyote kufanya hili, ila naona amenituma mimi nifanye. Ameweka mzigo moyoni
mwangu, siwezi kukwepa. Halafu ni vile humkumbuki baba yako Naya. Yule mzee
aliwapenda kupita nafsi yake. Angefanya chochote kwa ajili yenu. Sisahau jinsi
alivyojitoa mpaka nafsi yake kwa kumtafuta huyuhuyu Bale. Alikubali hata
kuuwawa ilimradi tu, ampate huyu Bale. Sasa wewe jiulize, huyu Mungu aweke huo
mzigo kwa mtu kama baba yako na kwangu pia, kwa mtu mmoja tu!” Tayari akaanza
kuhamasika mwenyewe.
“Yaani huyu Mungu
mwenye enzi yote, anasimamisha ratiba zangu mimi! Mpaka kula siwezi kwa
ajili ya Bale tu ambaye kwa kibinadamu ni mkosaji sana. Hastahili.
Lakini nashangazwa na huyu Mungu Naya! Amekubali yangu yasimame kabisa, ili kufanya
alichokifanya kwa Bale! Mimi sijui anakusudi gani naye, ndio maana nimekubali
kutii, ili na mimi nishuhudie kwa macho. Maana Mungu anapoamua kufanya jambo
lake! Hajui kupunja na hanaga mipaka. Anaweza kuinua hata mawe, ila akatuchagua
sisi. Naomba sisi tutii tu Naya.” Akaendelea.
“Sauli alilitesa sana
kanisa la Mungu. Akiwaua wana wa Mungu waliompokea Yesu kama Kristo. Akafanya
hivyo kwa muda mpaka Yesu mwenyewe alipoingilia kati akiwa tena njiani kwenda
Dameski kungamiza zaidi wana wa Mungu. Hakustahili, lakini ona aliyoyafanya
baada ya kukubali na kutubu. Leo tunasoma bibilia na inatusaidia wengi wetu kwa
sababu asilimia kubwa aliyeandika ni huyu muuaji Sauli aliyebadilika
akawa chombo na msaada wa kanisa.”
“Mungu ana mambo
yake, Naya! Mimi mpaka huwa naogopaga kumuuliza kwa nini, nabaki kusubiria
mwisho wa kazi zake. Kwa hiyo na wewe nakushauri fungua tu moyo, utaona tu
mkono wa Mungu. Kibinadamu ni ngumu sana, lakini mwache Mungu afanye yake.
Atasawazisha kwa namna yake mwenyewe.” “Nimeelewa Joshua.” Naya akatulia kabisa
akiwa amefunguliwa moyo, na yeye akitaka kumsaidia Bale.
Alichukua muda mrefu
tu chumba cha upasuaji, lakini akatoka. Angalau harufu mbaya iliisha kabisa.
Ila akaambiwa ilibidi kukatwa mpaka karibu kabisa na goti. “Mpaka mfupa mkubwa
ulikuwa umeoza. Lakini kwa alivyosafishwa. Na akiendelea na matibabu kitakauka
haraka.” “Aliweza hata kufungua macho?” “Yupo macho, ila nafikiri ni mdhaifu
tu.” “Nashukuru sana kwa huduma yako. Na wauguzi waliomsaidia pia.” “Karibu.”
Akapelekwa wodini ambako kwenye hospitali hiyo hulazwa watu wawili. First class
ya garama zaidi ndio mtu mmoja.
Bale akawekwa sehemu
yake, akaunganishiwa kila kitu akabakishwa na mirija ya mkojo, akabaki
amejilaza. “Pole Bale.” Naya akamsogelea karibu akijaribu kumuongelesha.
“Asante. Akajibu akiwa amefunga macho.” “Unasikia njaa?” Naya akaendelea
kumuuliza, Joshua akimsikiliza tu. Bale akakubali. “Ataletewa chakula muda si
mrefu, na baada ya muda ataongezewa sindani ya maumivu. Atakuwa tu sawa.”
Muuguzi aliyekuwa akimalizia kumuweka sawa akawaambia.
Wakakaa hapo
wametulia mpaka chakula kikaletwa. Joshua akaanza kumlisha taratibu, akala
chote, akamaliza. “Vipi, umetosheka?” Akaomba maji. Akamnywesha na kumfuta,
akamrudishia alale vizuri. Kwa mara ya kwanza roho ya huruma ikamuingia Naya.
Damu nzito kuliko maji. Japokuwa hakuwa akimkumbuka tokea maisha ya nyumbani
kwao ila ukatili kwake, bado akamuhurumia sana. “Tumuombee kabla hatujaondoka.”
Naya akatoa wazo.
“Bale!” Joshua
akamgusa. Akafungua macho. “Ni sawa tukiomba hapa kwa ajili yako?” Akakubali na
kurudi kufunga macho. Joshua akamvuta mkewe pale karibu maana alikuwa
akichungulia kwa mbali kidogo. Bale aliyemfanyia ukati alipomteka na huyu ni
watu wawili tofauti. Huyu alitisha kwa manywele na ndevu. Amekonda kabaki
mifupa. Geb akaanza kuomba rehema kwa ajili yake. Akatubu mbele za Mungu na
akikumbusha kazi ya msalaba ni kwa wakosaji, akamuombea rehema Bale. Joshua
aliomba kwa uchungu sana akiugua, akimsihi Mungu amguse tena Bale.
Wakati wakiomba,
akafungua macho akamuona Naya, akaanza kulia akiita mama. Alilia sana Bale. “Naumwa mama! Nimechoka, nimekosa, sijui nifanye nini!”
Akalia kwa uchungu akizungumza na Naya kama mama yake. Joshua akakumbuka
kusikia Naya anafanana sana na mama yao. Akajua madawa yamemzidi Bale, anahisi
Naya ni mama yake. Aliongea mengi akimwambia Naya kama mama yake mpaka muuguzi
akaingia nakumkuta anaongea mambo mengi mpaka mtiririko wa maneno ukapotea
akawa kama mwehu. Anaongea kila kitu mvurugiko mpaka mengine wakawa hawaelewi.
Naya akawa akilia kwa hofu. Akaitwa daktari kwa haraka maana alikuwa
akihangaika, Joshua amemshika ili asije kujitonesha. Akamuongezea sindano, ndipo
akapotelea usingizini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hujafa, Hujaumbika! Hakuna Umbali mwanadamu anaweza kumkimbia Mungu.
Na,
Pombe si Chai.
Ipi Historia ya Doro Naye?
Itakuaje Kwa Bale?
0 Comments:
Post a Comment