Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 11. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 11.

Akalia hapo na kujiona mjinga. Anamlilia nani? Pombe alikunywa mwenyewe! Akajitahidi mpaka akaweza kukaa. Akagundua alilala na nguo zake vilevile. Kwa haraka sana akaangalia chupi. Akajikuta amevaa chupi. Akaanza kujichunguza kama alibakwa. Akaridhika hajabakwa. Akahema kwa nguvu kwa kupata aghueni. Akaamua kujikaza ili kutoka kwenye hicho chumba. Akakutana na sebule nzuri sana, tena ya kisasa. Safi, ila hakuna mtu. Makochi ya hali ya juu, dhahabu safi. Akajua yupo kwenye nyumba ya mtu sio nyumba ya kulala wageni. Ila akazidi kushangaa na kuingiwa na hofu zaidi. “Kwa nani na nilifikaje hapa!?” Akajiuliza asipate jibu maana bado akili iliishia akiwa ukumbini, hakumbuki tena.

Akajaribu kusogea mlangoni ili ajaribu kutoka, milingo ilikuwa imefungwa na hapakuwa na funguo kama alizozoe kwao. Akashangaa sana. Akaenda dirishani ili kuangalia nje pengine atapatambua. Akaona mtu nje kwa kupitia kioo cha dirisha akiwa anasogea mlangoni. Akanyanyua pazia vizuri  kwa haraka huku akijitokeza.

Yalikuwa madirisha mazuri sana. Juu mpaka chini sakafuni. Akampungia mkono kwa nguvu kama amwangalie. Alikuwa mwanaume msafi sana, aliyevalia ramsi. Mtu mzima si kijana mdogo. Akamuona Jelini. Akasogelea upande wa dirisha. Jelini hakuwahi kumuona kabla na akashindwa kumtambua. Wakabaki wakiangaliana.

“Unataka kuingia humu ndani?” Jelini akamuuliza. Akamuonyeshea ishara yakukubali, ila akamwambia asifungue. Hapo akamchanganya Jelini. “Kwa nini sasa!?” Jelini akamuuliza akimshangaa kwamba anataka aingie lakini asimfungulie! “Alam.” Akamwambia hivyo, Jelini akawa hamuelewi. Kila alivyokuwa akitaka kuondoka akamfungulie, alimkataza. “Hutaki kuingia!?” Ikabidi amuonyeshee simu yake na kumwambia na yeye akachukue simu yake. Akaelewa na kukimbilia chumba alichoamkia kujaribu kuangalia kama alifikishwa hapo na vitu vyake!

Akaangalia pale kitandani hapakuwa na pochi. Chumba kilikuwa kikubwa na makochi, makabati yanayofanana na hicho kitanda. Meza nzuri sana za muuondo nadhifu. Jelini akashangaa sana. Huyo tajiri hivyo alimtoa wapi kwenye harusi ya dada yake! Chumba chenyewe chaweza kuwa nyumba na thamani ya familia nzima. Akarudisha mawazo kwa yanayomuhusu. Kwa harakaharaka hakuona chochote kinachomuhusu ila kumepangwa nadhifu, takataka yake angeona tu. Akataka kukata tamaa, akaamua kuzunguka kitanda na kutafuta hata chini ya uvungu, ndipo akakutana na viatu vyake alivyovaa harusini pamoja na pochi yake, akaiokota na kutoka nayo kwa haraka akimuwahi aliyemuona nje amsaidie kujua hapo ni wapi na kama hayupo salama, basi amuokoe.

Akamkuta bado amesimama palepale nje upande wa dirisha. Akachukua simu. Akamwambia aandike namba yake ya simu kwenye simu yake kisha amuonyeshe. Jelini kwa kusoma midomo yake akaelewa. Akaandika namba yake upande wa ujumbe kisha akamgeuzia simu. Akamuona anachukua namba na kumpigia. Akapokea.

“Cha kwanza kabla ya salamu, hii nyumba inalindwa na mitambo. Ukishika kitasa kabla hujatoa alam, itapiga kelele sana. Na askari watajaa hapa.” Jelini akashituka sana na kurudisha kichwa ndani kuingalia tena hiyo nyumba. Akaona kweli inastahili kulindwa hivyo. “Sasa nenda karibu na mlango wa nyuma kuna kiboksi chenye namba, bonyeza…” “Subiri kwanza. Mwenzio mimi hapa mgeni, hata sijui nilipo. Nahisi nililewa sana nikabebwa na mtu, nimeamka hapa peke yangu hata sijui nilipo. Wewe ni nani?” “Kasa.” Akajibu na kumfanya Jelini achanganyikiwe. Akamchungulia vizuri hakuridhika.

“Wewe muongo. Kasa ni mweusi, wewe mweupe. Au wewe ni jambazi!” Akamuona anacheka. “Usicheke bwana! Sasa wewe ni nani?” “Mimi pia ni Kasa.” Jelini akamchungulia tena vizuri akajaribu kumfananisha na Kasa anayemjua yeye, akili yake ikakataa kuwaweka hata kwenye ukoo mmoja. “Mama yako wewe mzazi huwa anakuita nani?” Hilo swali lilimfanya huyo Kasa azidi kucheka. “Kwani wewe unaitwa nani?” “Mimi hapa naitwa Jelini. Haya niambie na wewe jina lako nani? Na usinidanganye. Maana mimi sijakudanganya.” “Kweli naitwa Kasa.” “Sasa kwa nini na wewe uitwe Kasa!?” Jelini akauliza, lakini hapohapo akili ikaanza kufanya kazi kidogo na kushituka sana.

“Kwamba hapa ni nyumbani kwa Kasa!?” “Ndiyo.” Jelini akashituka sana akamuona ametoa macho na kufunga mdomo. “Mimi sinywi tena pombe. Sasa nilifikaje hapa!?” Akamuuliza huyo Kasa wa nje ambaye na yeye ndio amefika hapo. “Sijui Jelini, kwani Kasa hayupo humo ndani?” “Hata sijui! Mimi nahisi jana nilizidisha pombe, akanileta hapa kwake. Sasa wewe kwa nini na wewe uitwe Kasa bwana!?” Ikawa kama tena anamlaumu huyo Kasa anayemtizama nje ya dirisha. “Katafute sehemu ya kutoa alam, unifungulie ndio nikujibu maswali yako. Ukifika huko anza kwa kubonyeza *2345#. Umeelewa?” “Vikipiga kelele?” “Usipokosea, hakutakuwa na kelele.” “Basi sikosei.” Jelini akaanza kuzunguka nyumba mpaka akapata kicho kiboksi chenye namba. Akabonyeza, bado akiwa kwenye simu naye. “Ewaaa! Sasa unaweza kufungua mlango wowote ule.”

Akaanza kufungua akimuelekeza kwani hapakuwa na funguo ila nobs tu. Akamuelekeza mpaka akamaliza wa mwisho. “Wewe unafanya nini hapa?” Jelini akamuhoji bila hofu kama pale ni kwake. “Nimetoka kanisani, sijamuona Kevin, ndio nimekuja kumuangalia.” “Unanichanganya. Kwani Kevin ni nani tena!?” “Anayeishi hapa.” Jelini akatulia akimwangalia. “Kwani wewe unafanya nini hapa?” Ikabidi na yeye amuulize. “Nilikwambia hata sijui wenyeji wangu ni kina nani na nilifikaje hapa. Mimi jana nilikuwa kwenye harusi ya Jema, nimeshangaa nimeamkia hapa.” “Unamfahamu Kevin Kasa?” “Kasa namfahamu. Sasa na wewe kwa nini uanze kuniambia unaitwa Kasa!?” “Kasa unayemfahamu wewe, jina lake analoitwa na mama yake mzazi ni Kevin.” Jelini akaanza kucheka vile alivyojibu kwa kumuigilizia.

Akacheka hapo akimwangalia kwa tabasamu akikishangaa hicho kiumbe mbele yake. Akavutiwa hata vile alivyo. Hapo ndio ameamka hata hajaosha uso, hana viatu, lakini alivutia mno. Akabaki akimwangalia mpaka akamaliza yaliyokuwa yakimchekesha.  “Sasa na wewe mama yako mzazi anakuita nani?” Jelini akaendelea kumuhoji na cheko kubwa, kashasahau yake. “Alexender.” “Jina lako zuri. Ila ningekuwa mimi ningejiita Zenda.” Akacheka akitingisha kichwa akimtafakari Jelini kwa kuvutiwa naye.

“Au wewe hujalipenda?” Akamuuliza kama padre aliyekwisha mbatiza. “Sijawahi kuitwa hivyo, ni kama unanibatiza upya!” “Usijali. Utazoea tu. Haya, Zenda Kasa, hapa unafanya nini?” “Dad!?” Akatoka Kasa akiwa ameshituka sana. Jelini akajishika mdomo kwa mshituko. “Wewe kumbe ndio baba yake Kasa huyu!? Kwamba wewe ndio mzee Kasa?!” Jelini akashituka sana na kuendelea bila kusubiri jibu. “Sasa mbona hujaniambia kama wewe ndio mzee Kasa? Samahani sana. Mimi bora tu niondoke jamani!” Mzee Kasa akabaki akimwangalia Kasa na Jelini.

“I can explain.” Akamsikia Kevin Kasa akizungumza na baba yake lugha nyingine ila kwa hofu ya ajabu sana akiomba ajitetee. “Sijaja kanisani kwa kuwa ni kama unavyoona, nilipata wageni, tuliokuwa nao kwenye harusi mpaka karibu kunakucha. Nilijaribu kuwapa lift ili kuwarudisha makwao, lakini wakaishia kulala kwenye gari, ikabidi kuwaleta tu hapa kwenye nafasi kubwa. Mungu nishahidi, sidanganyi. Sipo hapa kufanya umalaya.” Jelini akashangaa vile jeuri Kasa alivyoingiwa hofu kwa huyo mzee ila akamfanya afikirie kwa haraka.

“Samahani Kasa. Ukisema wageni, unamaanisha nipo na nani humu ndani?”  Hilo swali la Jelini likazidi kumuogopesha Kasa akawa kama aliropoka, hakukusudia kusema hivyo kwa huyo baba yake. Alipoona hajibiwi, Jelini akaingia ndani kumtafuta huyo mwenzie. Akamtafuta huyo wa pili kwenye chumba alichokuwa amelala yeye mpaka chooni, akamkosa, akatoka. “Sasa mbona kwenye chumba nilichoamka mimi hamna mtu mwingine?” “Kwa sababu huyo wa pili atakuwa chumba alicholala yeye huyu.” Mzee Kasa akajibu na kumfanya Jelini akunje uso. Pakapita ukimya wa muda. Akafikiria, akili zake asizopenda kuzichosha zikakosa jibu na yeye akaona asijichoshe.

Akaona aage tu. “Mimi naomba niondoke jamani. Kasa wewe, asante kwa msaada wa kunifishisha hapa. Nachukua vitu vyangu naondoka.” Jelini akarudi ndani. Wakati anaingia ndani tu, uso kwa uso na Doro. “Dada Doro! Yaani umelala na Kasa!?” Akashituka kwa sauti ya juu sana mpaka wa nje wakasikia. “Acha kupayuka wewe.” “Lakini si vizuri dada! Huyu bado kijana mdogo sana!” “Kwani wengine tukoje!? Wewe Vipi Jelini!?” “Mimi nimesema tu dada yangu. Kasa ni mtu mzuri sana, usimfanyie hivyo.” “Kwani mimi nilikuwa mtu mbaya!? Wewe vipi?” “Mimi naondoka, lakini shauri yako.” Jelini akaingia chumba alichoamkia, akachukua viatu vyake akatoka hajavaa viatu, pochi na simu mkononi.

“Kwa nini unataka kujiangamiza kizembe wewe!? Unataka nini kitokee kwako ili utulie?” Jelini akasikia Mzee Kasa akimgombesha kijana wake kama mtoto mdogo. “Ulikumbuka kumpima?” Kimya. “Na usinidanganye?” Mzee Kasa akampiga mkwara. “Nilitumia kinga.” Akamsikia Kasa akijibu kwa hofu ya kujitetea. Jelini akatoka kwa kunyata kama asionekane, wakati ni mchana kweupe, wote wapo nje mwangani. Wakawa wakimwangalia vile anavyoondoka bila hata viatu miguuni. Akatembea mpaka kufikia geti dogo kabisa la pembeni, mlinzi mwenye sare akamfungulia, akatoka akinyata vilevile.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwanza hakujua alipo wala anapokwenda ila akakusudia kutoka hapo. Akiwa anatembea gari ikasimama pembeni yake. “Ingia nikusogeze.” Jelini akamwangalia, alikuwa mzee Kasa. “Kwanza samahani. Mimi sikujua kama wewe baba yake Kasa.” “Ndio maana ukaniita jambazi?” Jelini akakumbuka na kuanza kucheka. “Sasa wewe baba gani mweupe pee, halafu mtoto wako mweusi kabisaaa!” “Kwa hiyo wewe baba yako ni mweupe?” “Wenzio sisi hatunaga baba.” Kasa akakunja uso. “Ila umenifanya sasa nichanganyikiwe. Maana mimi nilikuwa nikidhani pengine nitakuwa nikifanana na baba yangu! Sasa kumbe unaweza kuwa usifanane na watoto wako!” Mawazo hayo yanaendelea kichwani kwake pembeni ya gari ya mzee huyo yeye hana habari ya muda wala wazo la pili. “Kevin amefanana na mama yake.” Ikabidi amjibu, Jelini akamwangalia na kumuuliza. “Mama yake ambaye yupo ulaya?” Mzee Kasa akacheka akitingisha kichwa akimtizama Jelini.

“Nijibu sasa!” “Ndiyo.” “Mmmh!” Akaendelea kuwaza taratibu kama aliyechanganywa zaidi. “Sasa mbona mimi sifanani na mama yangu? Ila Jema anafanana rangi na mama. Mimi nipo tofauti!” Akawa anawaza hapo nje ya gari ya mzee Kasa, mzee Kasa akimwangalia. “Lifti.” Akamkumbusha. “Mimi mwenzio huwa sitaki misaada. Watu wengine wanakusaidia jambo, halafu wanakuja kukudai kitu kingine kabisa! Sasa unajiuliza, huyu mtu kakupa bia moja tu anadai, akikupa gari itakuaje!” Ikabidi mzee Kasa acheke.

“Kweli tena! Mimi bora tu nitembee sitaki msaada wako. Kwanza sikujui, zaidi ya kukusikia tu.” “Umesikia nini juu yangu?” Ikabidi amuulize akicheka. “Eti wewe una mahela mengiii, ndio maana mtoto wako anaringa na ana kiburi. Halafu kwenu nyinyi mnadharau. Hata mtoto wako wa kike naye eti yupo kama Kasa. Uongo?” “Si ni ndugu? Lazima wafanane.” “Ndio wanafanana mpaka majivuno! Lakini wanasema eti wewe ndio unawapa wanao mahela mengi. Akuu! Mimi sitaki.” Jelini akakataa akibetua mabega yake.

“Sasa unaogopa nini kitatokea kwenye kukupa lifti?” “Ukinitamani je?” Mzee Kasa akacheka, akacheka sana. “Wewe cheka tu.” “Sasa umeshajiuliza kama ukitokea wewe ndio ukanitamani mimi, itakuaje?” Jelini alicheka mpaka akakaa chini kabisa. “Unajichafua bwana, simama.” “Unavyojiamini Zenda! Mimi nikutake wewe!?” “Nakutahadharisha tu.” Jelini akasimama akicheka. “Mimi wala sitakutaka.” “Unauhakika?” “Kabisa. Asilimia zote.” “Na ikitokea unanitaka, utafanyaje?” Akamfanya Jelini afikirie, kisha akamwangalia, akakuta mzee Kasa akimtizama.

Akacheka na kupandisha mabega akikataa. “Akuuu!” “Sawa Jelini. Ila hii nyumba ipo mbali na usafiri. Hujavaa viatu, jua limeshakua kali. Utaungua miguu na utachomwa na jua sana. Mimi nitakusogeza unapotaka, na nakuahidi sitakudai.” “Wanasemaga hivyohivyo.” Jelini akajilalamisha hapo kwenye dirisha alipokuwa amekaa huyo dereva akimtizama kiumbe hicho kigeni kwake, ila kweli kinavutia. “Nakuahidi sitakudai. Twende.” Akakubali na kuzunguka kuingia garini.

“Wewe kweli una mahela. Humu ndani pananukia vizuri, halafu gari yako safi kama wewe mwenyewe! Unawaka utafikiri umepaka sijui mafuta ya maji, sijui! Ngozi yako safii. Mimi mpaka napata shida kukaa humu kwenye gari yako bwana! Bora nishuke tu nijitembelee.” “Usijali. Upo sawa tu. Unaishi wapi Jelini?” “Naishi na mama yangu, na mtoto wangu.” “Baba mtoto wako yuko wapi?” Akanyamaza kabisa na maneno yote yakamuisha. Na yeye akawa muungwana, akanyamaza wakitoka hapo.

Akavunja ukimya kwa swali. “Ungependa nikusogeze mpaka nyumbani, au nikushushe sehemu na nikutafutie usafiri wa kukufikisha nyumbani?” Akapandisha mabega kukataa. Akamuacha  hajaelewa. Ila akaendesha, akiwa ametulia hapo kitini, kimya kabisa. Hamuongeleshi tena wala hamwangalii. Kama aliyemnunia. “Jana ulikuwa kwenye harusi ya nani?” Akamjaribisha. “Jema ameolewa. Amependeza huyo! Kila saa mume wake anambusu tu! James anampenda sana Jema. Hata mama amesema.” Akakumbuka kitu. “Halafu akamnunulia gauni zuri hilo! Kwanza sio kumnunulia. Ilibidi watengeneze. Ungemuona Jema, ungemtamani.” “Mimi sina tamaa na visivyo vyangu.” Jelini akamwangalia akiwa amekunja uso. “Sasa sio kihivyo na wewe! Kwamba ungesema amependeza! Zenda naye!” Akacheka kidogo vile alivyoongea. “Ila hata wewe unaonekana ulipendeza sana.” “Mimi kawaida yangu.” Mzee Kasa akaanza kucheka. “Sijisifii. Ila mimi mwenzio napenda kupendeza.” “Sawa Jelini. Nionyeshe basi picha za jana.” Akawaza na kuonekana kukosa jibu.

“Haki naacha pombe! Sinywi tena.” “Kwa nini?” “Yaani nahisi kitu kibaya sana kilitokea jana na sikumbuki. Niliishia niki…” Akawa hakumbuki kabisa. “Na sijui niliingiaje kwenye gari ya Kasa, Kevin! Bwana wewe unataka kunichanganya. Acha yeye abakie Kasa, wewe Zenda. Sawa?” “Sawa.” Akakubali akicheka. “Kwani wewe hukukubaliana na Kasa baada ya shuguli muende nyumbani kwake?” Jelini akashituka sana. “Akuuu! Mimi mwenzio sina mambo hayo. Siku hizi kuna magonjwa. Na watu wanaambukiza wenzao makusudi tu kulipiza kisasi. Nimekoma. Sitaki kabisaa.” Mzee Kasa akacheka na kufikiria kwa haraka akawa kama amekumbuka kitu.

“Wewe umemfahamia wapi Doro?” “Baa! Ila mengine sikwambii, ni siri yetu.” “Wewe na Doro?” “Ndiyo. Doro rafiki yangu sana japo mkubwa kwangu. Yupo karibu na mimi kuliko hata Jema, dada yangu kabisa.” Ndipo sasa akajua huyo Jema anayetajwa ni dada mtu. Akauliza swali jingine. “Kwa hiyo Doro ndiye mpenzi wa Kasa?” “Hapo sasa mimi sijui! Ila mimi nilidhani Kasa hana mtu maana ni kama alitaka ukaribu na mimi. Mimi nikamwambia tokea mwanzo, hataniweza. Kasa mstaarabu sana, mimi mwenzio sio mstaarabu. Halafu kama mkali hivi! Mimi napenda kuongea na tucheke. Kwa hiyo tokea mwanzo nilimwambia waziwazi mimi sitaki. Ila..” Akawa kama amekumbuka kitu.

“Ujue kuna siku nilimkuta nyumbani kwa dada Doro! Ila sikuuliza kwa kuwa hatukuwa kwenye maelewano mazuri na dada Doro, alikuwa ameniambia ukweli lakini kwa matusi makali. Ndio nikaondokaga kwake nikiwa nimeumia. Baadaye ndio akanibembeleza nirudi kwake niwe naenda kulala, mimi nikamwambia sitarudi tena nyumbani kwake. Nitakuwa nalala kwetu, ila nimemsamehe. Aliniumiza sana, hasa nikikumbuka jinsi mimi nilivyomsaidia! Ndio nikawa nimerudi kwetu, kwa mama Jema. Akaja kwetu na kunipigia simu kila saa eti ananikaribisha nyumbani kwake kwa chakula. Nikaona asije dhani sijamsamehe, ndio nikaenda kwake, na ndipo kwa mara nyingine tena ndio nikakutana na Kasa nyumbani kwake.” Mzee Kasa akawa akimsikiliza tu na kununa kukaisha, amechangamka anaongea na kujibu yote ila akamgundua hataki kabisa kusema maswala ya baba mtoto wake.

“Mara ya kwanza kukutana na Kasa ilikuwa wapi?” Akaendelea kumuhoji taratibu. “Anafanya kazi na shem, aliyemuoa Jema. Kwa hiyo nilikutana naye nyumbani kwa shem, siku aliyomchumbia Jema. Alifanya kama kitafrija. Wafanyakazi wenzie na marafiki wakahudhuria na mimi nikaenda ndio nikakutana na Kasa.” “Ooooh! Hapo sasa nimeelewa. Na Doro naye anafanya kazi hukohuko?” “Hapana. Mimi hata sijui amekutana wapi na mtu kama Kasa, maana dada Doro mtu wa baa kama mimi tu, japo mwenzangu yeye amesoma na anakazi nzuri sana. Ila mshinda baa kama mimi tu.”

“Nilifikiri umesema unaacha pombe! Maana ukiendelea kushinda baa lazima utapata vishawishi.” “Lakini kweli! Ila washikaji zangu je? Stori za baa hazina wasomi wala wasio soma. Wenye nazo wala wasio nazo!” “Lakini zinakufanya unajisahau Jelini! Leo umeamkia nyumbani kwa Kasa. Hajakugusa. Iweje siku nyingine uje uamkie kwengine, kwa mtu mwenye gonjwa baya, akakubaka na kukuachia ugonjwa? Huoni kama ni hatari kwako?” Hapo akaogopa maana hayo maneno yalimuingia mpaka kwenye mifupa. Akapoa kabisa. “Mimi naungana na ushauri wako wa kuacha pombe, Jelini. Sidhani kama ni rafiki kwako.” Akanyamaza.

“Ungependa nikupeleke mpaka nyumbani?” Akamwangalia. “Umenikasirikia?” “Hapana. Najifikiria tu.” “Tafadhali ujifikirie zaidi, Jelini. Wewe ni binti mzuri sana. Nitakuja kusikitika sana nikija kusikia kitu kibaya kimekupata.” “Kweli utasikitika au umeongea tu?” “Namaanisha! Unajua kwa nini nimekua mkali kwa Kasa kama unavyomuita wewe?” “Sijui.” “Bado ni mdogo na ahadi nzuri mbeleni kwenye maisha. Kwa nini anataka kujiua mapema? Hilo namsisitiza bila kuchoka na ndio maana nilipomkosa tu kanisani, nilijua kuna kitu hakipo sawa. Kevin si mlevi wa kushindwa kujielewa, kwamba amezidisha pombe akashindwa kuamka kwenda kwenye ibada! Hapana. Akikosa kanisani najua si pombe hata kidogo. Usicheze na maisha Jelini, hayana spea!” Hapo akamgusa Jelini. “Basi wewe baba mzuri. Natamani na mimi ningekuwa na baba yangu pengine..…” Akasita. “Hujachelewa kubadilika Jelini. Unaweza kubadili kila kitu na ukawa sawa.” “Nashukuru kunishauri japo hunifahamu. Nitajitahidi.” “Naomba kujua maendeleo ya hizo jitihada zako, Jelini.” Akamshangaza sana na kumfanya kama asielewe tena.

“Kwamba niwe najua kinachoendelea kwako.” Akaongea kwa kubembeleza mpaka akamlainisha Jelini cha maneno. “Sasa utajuaje!?” Akauliza taratibu. Safari hii akaonekana mtulivu kama siye yeye. “Kama ukiniruhusu, nitakuwa nikikupigia kujua maendeleo yako.” “Kweli Zenda!?” “Kabisa.” “Mmmh! Unanidanganya bwana! Mimi nimeambiwa wewe ni tajiri sana. Na mtu tajiri anakuwa na mambo mengi ya kufanya, utakuja kunikumbuka mimi kweli?” “Najua umezoea kudanganywa. Mimi nikikwambia nitafanya jambo, ujue nitafanya. Nina watoto wawili tu. Na ndio utaongezeka na wewe. Haitakuwa shida.”

 “Mbona sasa hujamtaja mkeo? Mama Kasa.” “Kama unamaanisha mama yake Kevin, yeye alishaolewa na anayo familia yake huko alipokwambia Kevin alikwenda.” Jelini akashangaa sana. “Sio mke wako tena?!” “Hapana. Tulishaachana zamani sana. Nafikiri ni zaidi ya miaka 20 sasa.” “Na hukuoa tena!?” Akacheka. “Unamaswali wewe?” “Mimi nataka kujua bwana! Niambie.” “Hapana sikuoa, japo nilishakuwa na mahusiano baada yake.” Jelini akanyamaza kama anayefikiria kitu.

“Ungependa nikurudishe nyumbani?” “Sidhani kama itakuwa jambo zuri. Watadhani wewe ndiye uliyenichukua jana. Halafu mimi mama yangu anaongea kama hivi mimi, ila yeye mkali sana. Atakwambia maneno mabaya. Nashukuru kwa kunisadia, ila nishushe popote ambako unajua naweza kupata usafiri wa kunifikisha nyumbani.” “Umewaza vizuri.” Akaendelea kuendesha.

Akawa kama amekumbuka tena kitu, akamgeukia. “Sasa kwa nini wewe ni mweupe hivyo!?” Mzee Kasa alicheka na kucheka sana. “Jelini!” “Umenishangaza na kunifanya nichanganyikiwe! Sasa unawezaje kuwa na watoto weusi ukiwa na rangi hiyo?” “Mama yao au upande wa mama yao wana damu kali sana. Hata Kemi amefanana sana na mama yake, kama alijizaa.” “Na Kasa naye?” “Ukija kumuona mjomba wake, ndio utaelewa ni kwa nini nakwambia upande wa mama zao wanadamu kali. Yupo kama hivyo Kevin. Na huko alikoolewa aliolewa na mzungu, hao watoto ukiwaona, utawafananisha na Kemi. Wote ni wa kike. Wamefanana na Kemi, huwezi kuuliza kama ni ndugu.” Jelini akatulia kabisa mpaka akamfikisha karibu na taksii.

“Nakushukuru Zenda. Nitajitahidi kuacha pombe. Hata hivyo huwa nakunywa kama kujificha tu au kutojifikiria. Wakati mwingine huwa najichukia sana. Pombe inanisaidia kujisahau.” “Ni nini kinakuudhi kwako?” “Ni siri, siwezi kukwambia.” “Ila nilazima tuje kukizungumza. Lazima itakuja kukusaidia tu. Ukiendelea kukificha, ujue ndio kitakuumiza zaidi. Nenda ukapumzike. Lakini naomba nikulipie taksii.” “Akuuu! Mimi sitaki. Ninazo hela zangu.” Akashuka haraka garini na kumuacha Kasa akicheka huku akimtafakari.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akampigia simu hapohapo. “Unijulishe utakapofika salama.” “Sio itakuwa usumbufu tena?” “Hata kidogo.” “Wewe usiwe na wasiwasi, nitafika tu salama.” “Nataka kujua Jelini.” Akacheka. “Asante kujali. Basi nitakujulisha.” Wakajikuta wakicheka. “Umepata usafiri sasa?” “Napanda pikipiki.” “Acha Jelini bwana! Tafadhali chukua taksii, nitalipa.” “Mwenzio ndio usafiri wangu.” “Unafurahia kukumbatia hao wanaume huko barabarani?” Jelini alicheka mpaka machozi.

“We Zenda!” “Ndicho unachoking’ang’ania! Sasa kwa nini unakataa usafiri wa heshima?” “Sio wote tuna pesa kama wewe Zenda!” “Sasa mimi mwenye pesa ndio nakwambia nikulipie, hutaki. Unataka nini Jelini?” “Basi nachukua taksii, na nitajilipia.” “Usikate simu.” “Huniamini kama nitachukua taksii?” “Nataka uhakika kuwa amekufikisha salama.” “Unavyojali!” “Na mimi ni kawaida yangu kama wewe kupendeza.” Jelini alicheka sana. “Kumbe ulikuwa ukinisikiliza!” “Sana tu. Ila sikusikii ndani ya gari.” “Dakika moja.” “Na usikate.” “Nimeelewa. Hata mimi napenda kujaliwa.” Akamfanya acheke.

Akamsubiria mpaka akapanda kwenye gari wakawa wanaendelea kuzungumza. “Sasa leo jumapili, unafanya nini baada ya kutoka kanisani mbali ya kumfuatilia Kasa?” “Leo napumzika tu nyumbani. Kusoma magazeti na vitabu.” “Hujisikii mpweke?” “Nafikiri nimeshazoea au nimekubaliana na hiyo hali. Hata hivyo ukweli nina mambo mengi, hujakosea. Na wewe?” “Naenda kutulia zangu nyumbani, kimya.” “Humtafuti Doro?” “Zenda wewe kumbe unafutialia mambo hivyo! Mwenzio sikujua hata kama unanisikiliza!” Jelini akashangazwa maaana alishajijua ni muongeaji sana, ni ngumu mtu kumtilia maanani. Kwanza hajazoea mtu kumtilia maanani.

“Mimi nilijua hunielewi!” “Nilikuwa nikikusikiliza sana na nilikuelewa kuwa ndiye kampani yako huko baa!” “Sasa hivi ukute yupo na Kasa. Na pia naona nimuache kwa muda.” “Lakini kama isingekuwa kumuacha kwa muda ungefanyaje?” “Ndio kampani yangu, mwenzio. Tungeenda zetu baa. Tukakaa mpaka usiku sana. Akinikaribisha kwake, naenda kulala kwake.” Akamshangaza sana, ila akaona hilo aliache kwa muda.

“Kama ndio hivyo, basi karibu kwa chakula cha usiku. Tule wote halafu urudi nyumbani mapema tu.” Akanyamaza. “Unaogopa?” “Mmmh!” “Kwamba nitakudai?” “Mimi sijui bwana! Ila sema wewe haupo kama Kasa. Angalau wewe tunaweza kucheka. Mwanao yule yupo serious sana bwana mpaka anatisha!” “Kuna ulichomnyima ndio maana.” Jelini alicheka sana. “Zenda wewe!” “Kumbe unafikiri angekununia hivihivi!” “Ila mimi sikusema neno baya.” “Hilo zuri kwako, baya kwake. Sasa tutakula wote?” “Nakuonea aibu.” Alimfanya akacheka sana.

“Kutoka kuniita mimi jambazi mpaka kunionea aibu!” Jelini akaanza kucheka na yeye. “Sasa, saa zile si nilikuwa sijui kama wewe ndio Kasa mwenyewe! Sasahivi nishajua, nakuonea aibu.” “Usijali, nitakuziba macho.” Akacheka wee. “Kwa hiyo utakuja?” “Mimi sitoki na kila mtu bwana. Mpaka nikujue vizuri, ndio nitakubali.” “Sasa utanijuaje na hutaki kuja tule wote!” Akamsikia kimya. “Jelini?” “Unataka kwenda kula wapi?” “Popote utakapochagua wewe, isiwe tu baa.” Akaanza kucheka tena. “Au nikusaidie kuchagua mimi?” “Mimi nasita bwana. Nipe muda Zenda.” “Nitaheshimu hilo japo nimehuzunika!” “Kweli?” “Sasa kwa nini unahofu na mimi?” “Sikujui Zenda.” “Nakupa ruhusa ya kuniuliza swali moja litakalokutoa hofu.” “Unaniahidi hutanidanganya?” “Nitakwambia ukweli hata kama utakuwa mchungu.” Jelini akaridhika.

“Wewe umesema hujaoa. Sasa unafanya mapenzi na nani na unajikinga vipi?” “Hayo ni maswali mawili Jelini. Nilikwambia moja. Mengine nitakujibu taratibu. Sasahivi chagua moja.” Akatulia akifikiria. “Ukinijibu yote ndio nitafurahi.” Akacheka akifikiria. “Sawa. Binafsi ni mchaguzi sana linapofika swala la wanawake, haswa baada ya kuvunjika ndoa yangu. Nipo makini sana na wanawake. Na kwa kuwa sitafuti kuoa, nahakikisha namvulia nguo mwanamke atakayekuwa amenivutia haswa.” “Haaa!” Jelini akashituka sana hakutegemea. “Wewe si umetaka kujua wewe? Tulia sasa nikujibu.” Akamsikia akicheka.

“Swala la kinga, ni lazima. Lakini kabla sijaanza kufanya mapenzi na mwanamke ambaye itanilazimu kutumia kinga, lakini pia lazima kumpima. Ninacho kipimo kinachotoa majibu hapohapo. Umeridhika?” “Nina swali jingine.” “Hapana Jelini. Kama unanikatalia niambie tu. Nimekujibu zaidi ya tulivyokubaliana.” “Basi nakukatalia. Sitaki.” “Sawa. Lakini bado ningependa kujua kama utafika salama.” “Nitakujulisha kwa ujumbe. Kwaheri.” Akamkatia na simu. Alishangaa Kasa, hakutegemea! Ameshazoea kutetemekewa. Leo Jelini aliyemkuta akitembea peku, hana hata usafiri wa baisikeli anamkatia simu! Kikampata kilichompata mwanae. Akabaki ametoa macho.

Zimwi Likujualo.

Jumapili hiyo ikawa njema kwa wengi waliotoka harusini kwa James na Jema, lakini ikawa tofauti kwa Joshua. Alishindwa hata kupata kifungua kinywa. Hajui pakumpata Bale, na yeye kikampata kilichompata baba Naya. Hajui aeleze vipi hata mkewe akamuelewa. Kwa Naya yeye Bale ni mtu hatari sana. Hakumbuki hata mahusiano naye zaidi ya kumpiga sana kikatili akiwa analia ugonjwa. Akatulia kimya anaogopa asije akapatikanika huyo Bale, akijua ndio mwanzo wa kumrudisha kwa Malon.

“Njoo ukae hapa Naya mpenzi wangu.” Naya akajisogeza maana alikuwa akimwangalia kwa kijiiba. “Naomba unisaidie, kukumbuka nyumba ya Malon hapa Dar.” “Sikumbuki.” “Hapana Naya. Umejibu haraka sana. Tena umejibu kwa woga ukiwa hutaki hao watu maishani.” “Naogopa sana Joshua.” “Mimi nakuhakikishia, utakuwa sawa. Usiogope. Sawa?” Akatulia. “Kuna kitu si sawa kwa Bale na sijui jinsi ya kueleza. Siwezi kula wala kulala. Tafadhali nisaidie.” Akamuhurumia mumewe. “Niahidi tena kuwa utalinda Joshua. Wasije nichukua.” “Mungu atanisaidia mpenzi wangu. Sitazembea tena. Si umeona nipo makini na wewe?” Akajirudi maana Joshua alikuwa akimlinda mpaka kwa wengine ikawa kero. Akamuona ameridhika.

“Kuna mahali nilisoma. Niliandika zamani wakati nikiuza vitu vya Malon ili kumtoa jela. Niliandika mali zake zote na mahali zilipo. Ya hapa Dar niliiandika ipo maeneo ya Kunduchi, na nikaandika kuwa sikuiuza. Pengine inaweza kuwa ndiyo.” “Nakushukuru mke wangu. Umeandika wapi?” Naya akanyanyuka kwenda kuleta hicho kijitabu chake cha kumbukumbu. Akamkabidhi.

Wakati akisoma, simu ya Joshua ikaita, alikuwa Geb, akapokea. “Vipi GM?” “Safi. Nakucheki tu. Kila kitu kipo sawa? Maana jana tuliagana ukiwa sivyo ndivyo.” “Kuna hali napitia, sina jinsi yakumueleza mtu akanielewa.” “Nijaribishe mimi.” Akaongea Geb akionyesha kujali. “Kuna kitu hakipo sawa kwa Bale. Sijui ni nini kwa hakika! Ila nashindwa hata kula aisee.” “Unajua alipo twende tukamuangalie?” “Wewe si una wageni?” “Man na familia yake wameshaondoka. Nipo tu hapa peke yangu, mama na Nanaa wametoka na watoto kwenda kwenye birthday ya mtoto wa binamu yake Nanaa. Mimi nikaona nipumzike tu. Kwa hiyo, am all yours.” Geb akaonyesha utayari wa kutumiwa na Joshua atakavyo. “Aisee nitashukuru sana. Nilikuwa sijui jinsi ya kumpata, lakini kuna kijitabu hapa nasoma. Aliandika Naya zamani. Naomba tukaanzie hapo. Ni Kunduchi.” Akaanza kumsomea vile Naya alivyokuwa ameandika. “Naona kama hayo maelezo yanajitosheleza! Tunaweza kugonga nyumba mbili tatu, lakini nina uhakika hatuta kwama. Tukutane huko basi.” Wawili hao wakakubalina.

Hujafa, Hujaumbika.

Baada ya kama lisaa wakajikuta wapo Kunduchi. Wakakisoma tena kile kijitabu cha Naya cha kumbukumbu, wakaamua kuanza maeneo ya kuzunguka karibu kabisa na bahari. Walipoenda nyumba ya pili tu, mlinzi akaonekana alishawahi kulinda hapo kwa Malon kwa kupitia kampuni yao na anamfahamu Bale vilivyo. “Ila ile nyumba imegeuka gofu aisee. Inavyosemekana mwenye nyumba alimuacha kijana mmoja pale, yule mtoto bangi halafu alianza kwa jeuri, dharau kwa sisi wote tuliokuwa tukimlindia pale. Nafikiri alipoanza kuishiwa pesa, akaanza kuuza vitu vya ndani. Mbaya zaidi akawa analeta wateja palepale wanaingia ndani anawaonyesha vitu vya kuwauzia. Sisi tukamshitaki kwa uongozi wetu kwa sababu tulimwambia kwa vizuri tu kuwa, anaita wezi yeye mwenyewe, akawa jeuri.”

“Ndio akapewa onyo lakini ujue hapo kila mtu akawa anapajua pale mpaka ndani. Sisi tunavyohisi wenzie walewale waliokuwa wakimsaidia kutafuta wateja, walimgeuka. Wakamzidi mahesabu. Wamemuibia kila kitu. Nikisema kila kitu, kwamba walihamisha nyumba mpaka kitanda. Akawa ameishiwa kabisa, anashindwa kulipa pesa ya ulinzi, ndipo kampuni ikasitisha mkataba. Na sisi tukaondolewa pale tukapewa malindo sehemu nyingine wakati kampuni ikimshitaki awalipe pesa yao. Nilikuwa nikimuona anapita na magongo yake hapa maana magari yaliharibika yote, akaja kuyauza.”

“Bale na magongo!?” Joshua akawa kama haamini. “Yaani alikuwa akipita hapa unamuona akichechemea, anaongea peke yake kama kasharukwa na akili vile. Nafikiri bangi imemzidi. Ila sijamuona siku mbili hizi. Sasa sijui.” “Unasema huyo kijana unayemzungumzia wewe anachechemea!?” Joshua akaanza kuingiwa na wasiwasi pengine si Bale. Bale wanaomjua wao ni mzima. Hana ulemavu wowote. “Mimi wakati nikilinda pale, ni kama alijiumiza huo mguu. Akawa hataki kwenda hospitalini, akisema atapona tu. Ndio mwenzangu akamuona na kusema ule mguu utakuja kuoza tu, yeye hajui sababu ya bangi, maana ulivilia ukawa mbaya kweli. Nafikiri alikaa nao ukamzidia. Nafikiri sijui bangi ilishindikana kutuliza au aliishiwa akawa hana hata pesa ya bangi! Hatujui ila alishindwa kuvumilia. Anavyosema alikuja kwenda hospitalini wakamwambia amechelewa. Umeoza mpaka mifupa. Ndio wakamkata katikati. Wala si muda mrefu maana hata donda lenyewe halijapona. Utamuona tu akipita amelifunga na linaonekana linamvujia.” Joshua aliumia sana.

“Na nyinyi mnamdai nini? Kwake sio mbali kabisa. Ukipita nyumba mbili mbele, yake ipo ndani kidogo maana imekaribia baharini zaidi. Kila anayekwenda kwake ni kumdai ila naona wanashindwa na hali yake. Sio mbali kabisa.” Akawaonyesha. Joshua na Geb wakashukuru, na kurudi kwenye magari yao na kuongozana kwenye hiyo nyumba wakiwa na wasiwasi sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Nini kitaendelea kwa Jelini. Usipitwe na aliyoyafanya ukumbini akiwa hajitambui kwa pombe.

v    Zenda kimempata kitu kama mwanae. Jelini!

v    Joshua naye kimempata kitu kama baba Naya.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment