Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 9. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 9.

Nani Kaachwa Njia Panda!

Mpaka siku hiyo ya kitchen Party kina Magesa hawakuwa na mualiko wala sare.  Kama kawaida Grace akatua jijini asubuhi ya siku hiyo na familia yake yote, wakakutana na hiyo hali. Man na yeye alikuwa tayari kwa Bag Party jioni yake iliyokuwa imeandaliwa na kina Joshua na Geb. Walipanga kwenda kuifanya kisiwani na maboti yao. Ilikuwa ya watu wa karibu na James. Wakaiandaa kitajiri, wanaume hao na wao wakataka kwenda kumfunda James.

“Sasa itakuaje!? Maana kama ningejua tungekuja hata usiku! Nimeacha shuguli nyingi kweli! Ningepunguza kidogo.” Grace akauliza kwa mshangao na kujuta kuwahi kufika bila taarifa za kutosha. “Hata sijui! Acha nimpigie James.” Mama G akampigia James akiwa katikati ya shuguli. “Nakusumbua James mwanangu, lakini mpaka sasahivi hatuna taarifa za kitchen party.” “Si ni leo?! Au nimeshachanganya madesa!” James akauliza kama ambaye hana uhakika. “Ndiyo, ni leo. Lakini sisi hatujasikia chochote.” “Acha nizungumze na Jema.” “Nashukuru mwanangu. Na Grace ameshafika kwa ajili hiyo.” James akaona kuna uzito, akampigia Jema.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Najua upo busy, lakini nina swali la haraka. Mambo ya mualiko wa kitchen Party, nani anashugulika nayo?” “Ukimaanisha nini?” “Upande wa wanaotaka kuhudhuria.” Jema akafikiria kwa haraka akawa hajaelewa. “Ukimaanisha upande wako?” Jema akauliza. “Ndiyo.” “Ni nani aliyetaka kuhudhuria na hajaalikwa mpaka sasa? Maana nilisema hata ile siku ya kikao cha kwanza nyumbani kwako siku uliyonichumbia, kuwa kina Viola na mama yako watatupa idadi ya watakao taka kuhudhuria, niwape kina mamdogo kisha wawafanyie taratibu. Maana mama zangu ndio wameandaa. Nahisi kila kitu kinakwenda sawa. Na kila kikao kina Viola wamekuwa wakihudhuria vizuri tu na kuchukua sare pia.” “Kina Magesa hawajapata mpaka sasahivi.” Jema akashangaa.

“Kwamba hawana mawasiliano pia na kina Viola na mama James!?” Hapo ndipo akili ikamrudia James. Ni kambi mbili tofauti. Kimya. “Au wao kina Magesa walitakiwa kupewa huduma ya tofauti na waalikwa wengine?” Jema akauliza. Ila ile uliza yake, James akaona itampotezea amani. “Nafikiri watawasiliana nao tu. Wewe usijali. Vipi lakini?” “Sitaki nionekane kama nawanyima shuguli, ikazua maneno mengine. Wakanipa sifa nyingine mbaya zaidi.” “Usijali. Acha mimi nitaliweka sawa hilo. Nataka kujua wewe unaendeleaje. Mbali na kila kitu, mke wangu mimi anaendeleaje?” Kidogo Jema akatulia maana kifua kilishaanza kujaa hasira akikumbuka mara ya mwisho alipokuwa nyumbani kwa Nanaa na jinsi alivyomjia juu.

“Wanakuandaa lakini kwa fungate! Maana mwenzio nipo tayari, jumamosi usiku ni usiku wetu.” Jema akaanza kucheka. “Usiniambie hakuna maandalizi yeyote!” “Ujiandae kula kuku kwa mrija.” James alicheka sana. Hakutegemea kumsikia Jema akiongea hivyo. Alicheka sana. “Jema huyo!” “Utachoka mwenyewe! Mimi nipo tayari.” James alicheka sana na kumfanya Jema atulie zaidi. “Sasa ujue na mimi naendelea kujinoa zadi. Wewe si unapagawishwa na kiss za mdomo tu?” Jema alicheka. Hapo akashindwa, akakata simu akicheka sana. Na James alimfanyia makusudi akijua ataona aibu atakata aendelee na mambo yake. ‘Acha matusi James.’ ‘Nilishakwambia hayaitwi hivyo.’ James akarudisha majibu kwa haraka akijua huko atakua akicheka kwa aibu. ‘Mimi naona tuyaite tu hivyohivyo.’ ‘Unakosea Jema!’ ‘Mimi sina neno. Nayapenda makosa yangu’ James akacheka sana.

Wifi.

Alipoagana na mpenzi wake tu, akampigia Viola wakasalimiana vizuri tu, akaamuuliza. “Kwani kina Magesa wanapelekewa mualiko na nani?” “Na nani wifi yangu? Sisi nyumba za mamilionea hatukaribishwi.” Akajibu Viola na kuendelea. “Nanaa amepandishwa juu sana na Mungu, sisi tena hatufai kwenye maisha yake. Hata hivyo kwake hata sipakumbuki. Tulifika hapo siku moja tu, tena usiku. Tulikwenda kumuomba msamaha kwa mabaya tuliyomtendea wakati tukiishi naye. Tulikuwa na kaka pamoja na mama. Nanaa alipotuona tu tumefika sebuleni kwake, akaaga na kupandisha juu gorofani kwao.” “Haiwezekani Viola!” “Muulize kaka ambaye anampenda sana Nanaa. Atakwambia kama nimeongeza jambo. Tena tukamwambia tumekuja kuomba msamaha, tuzungumze. Akasema tuzungumze na mumewe. Yeye amechoka kutusikiliza sisi. Ashatusikiliza sana tokea anakua. Mungu amempa masikio mengine, yaani huyo mumewe, milionea. Yeye hachoki kusikiliza. Sisi tuongee mpaka tuchoke. Nanaa akapandisha juu tukimtizama hivi. Hata maji ya ukaribisho ya kudanganyishiwa, hatukupewa. Tukaondoka, mimi na Vai tukajiambia tumuache kabisa.” Viola akaendelea taratibu.

“Sasa kama hali zetu sisi unavyozijua. Maeneo tunayoenda, si atakayoenda Nanaa wa siku hizi. Kwa hiyo kwa kifupi, hatujawahi kugongana hata kwa bahati mbaya barabarani, ila tulimuona siku ile alipokuja pale kwenu siku ya mahari. Na hatukutaka kumkera. Maana Nanaa ni roho ya kaka James, na sisi tuliambiana tusimuudhi kaka, atulie aoe kwa amani. Tukajiweka pembeni kabisa. Alikuwa amekaa pale katikati ya wale matajiri pale, tungemfikiaje?” Jema akazidi kushangazwa na Nanaa, kwamba alishindwa hata kusalimia ndugu zake!

“Sasa kujibu swala la mwaliko, sisi hata hatukujua kama wanataka kutusikia au kualikwa na watu kama sisi. Kwanza nahisi wangekataa kualikwa na sisi, labda wewe mwenyewe. Kingine, hatuna namba zake za simu. Hatuwasiliani kwa la kheri wala la shari. Kwa hiyo kwa kifupi, mialiko michache tuliyopewa na mama mdogo wako Mode, mama kawapa mashoga zake, wakamchangia ndio huyo akawapa mama zako pesa. Na nafikiri hicho kikundi chake alichowaalika wamejipanga wenyewe mpaka na zawadi zao. Mengine mimi siyajui wifi yangu. Kaka ndiye yupo karibu na hao watu. Sio sisi.” Jema akachoka kabisa na kuamini Nanaa anao watu wake.

Akakumbuka hata kutomuona siku alipochumbiwa nyumbani kwa James, lakini alimuona kwa Kumu akiwa bega kwa bega na Naya. Akakumbuka siku ya kulipiwa mahari jinsi walivyokuwa wamekaa kivyao, tena kitajiri! Akaumia sana. Akajua anamdharau.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

James akampigia Viola. “Nani anamialiko ya kitchen party?” Akauliza baada ya salamu. “Mama yake mdogo Jema alitupa na vikoi, tukamkabidhi mama. Mama amewapa mashoga zake wanaocheza nao kikoba huku mtaani, na waliokuwa wakifanya nao kazi Moshi. Naona wamejiandaa kweli. Watakwenda kama kikundi.” Viola akajibu kwa heshima tu na kujiweka pembeni maaana alimjua kaka yake na Nanaa. James akakwama, akawa ameachwa njia panda. Inamaana kina Magesa hawajaalikwa. Akamuaga na kukata.

Kila Mchuma Janga, Hula Na Wakwao.

Akatumia akili akampigia simu mama G. “Na mimi nilisahau kabisa, ndio Jema ananikumbusha vile alivyosema siku ile pale nyumbani kuwa kina mama na Viola ndio wangeshugulikia. Kwa hiyo hao ndio waliokuwa wakisaidia maandalizi ya kitchen party pamoja na mama zake Jema. Wamepewa mialiko na nafikiri kwa kuwa hamna mawasiliano nao, hawakujua jinsi ya kuwafikia au hawakujua kama mngetaka kuhudhuria. Nilivyosikia kutoka kwa Viola, ni kama mama amewapa marafiki zake.” “Hakuna shida James mwanangu. Bora kufanikisha hili.” “Unisamehe. Mambo yamekua mengi nikasau kuwa hampo karibu hata na kina mama pia.” Hiyo kauli ikamuumiza mama G.

“Ningefuatilia mwenyewe, ili kuwapa.” “Hakuna shida kabisa. Sisi tunawaombea kufanikiwe.” “Amina.” James akaaga na kukata. Akakumbuka mbali na wadogo zake na mama yake, alimpeleka na Jema pia hapohapo nyumbani kwao, wakamshindwa wao wenyewe. Akaona asijiingize kwenye kuvuna kwao. Bila kutarajia Nanaa akawa amechuma janga, anakula na wakwao. Na James naye hakutaka kurudi kabisa kulizungumzia hilo kwa Jema. Akajua anaweza kumuudhi bure akaharibu shuguli nzima. Akaachana nalo kabisa.

Kitchen Party

Jema alikwenda saluni. Akatengenezwa vizuri sana. Kitchen party ikawa ya kiswahili haswa. Mamdogo akaleta mashangingi ya jiji. Lugha za aibu tupu humo ndani. Kila kiungo kinatamkwa kile kilivyo. “Mwali hafundwi hadharani, ndio maana tumejifungia humu ukumbini, tumfunde mwali wetu. Atakayesikia, na hayamuhusu, ajue kajitafutia.” Basi kazi ikawa ya kukata mauno, Jema anacheka mbavu hana. Kina mama wa kichaga wakakutana na Wazaramo wenye jiji lao. Hawajasomea udaktari lakini kila kiungo mwilini wanakijua na kazi yake. Viuno feni. Mabonge kwa wembamba. Mwanamke nyonga, makalio majaliwa. Ndio ukawa usemi wao usiku huo wakisema usisingizie huna tako kubwa, kinachokatwa ni nyonga si tako. Hakuna tafsida, mambo hadharani.

Kukachezwa taarabu humo na mambo ya chumbani matupu. Ikafika saa ya kusasambua begi. Muandaaji mamdogo Mode. Halafu akakodi msasambuaji kabisa. Anatoa nguo huku akimuonyesha jinsi ya kutumia na mwendo wake. Jamani Jema alikuwa akicheka sana. Na msasambuaji akawa anaonyesha nyingine na staili zake za mapenzi. Jema alikuwa akicheka mpaka kuficha uso. Aibu! Watu wakawa wanashangilia humo ndani kupita kiasi.

“Jema kafurahi!” Jelini akamnong’oneza mama yake. “Namuona anavyocheka mpaka machozi. Ila umemfaa!” “Sitaki dada yangu akaonekane mjinga huko chumbani.” “Kweli umeamua. Na pombe hunywi!” “Wote tukilewa hapa, hakuna atakayeendesha mambo. Naenda kulewa nyumbani baada ya hapa.” Jelini akamsaidia kweli dada yake, akitaka mambo yaende vizuri na wasipoteze zawadi. Akakusanya zawadi zote na kuingiza kwenye gari ya Jema. Akapanga mpaka kiti cha mbele. Kisha akaweka na kwenye gari za mama zake mpaka vikaenea. Akatulia mpaka ikaisha na kumrudisha dada yake nyumbani.

“Nawashukuruni mama zangu. Nimekua na wakati mzuri mno.” Wakaanza stori. “Mamdogo nimefurahi sana. Asante. Na Jelini mdogo wangu, asante sana. Umenijenga mno. Mpaka najisikia wa tofauti!” “Upunguze aibu Jema. Bado unaaibu sana. Utashindwa kumnyonya mumeo kwa uhuru.” “Na wale wanawake pale walikuwa wanasema kabisa. Tamka viungo vya mumeo.” “Mamdogo siwezi. Yale maneno mazito sana kumwambia James eti niingizie…” Akasita nakufanya wote wazidi kucheka mpaka machozi.

“Ila bwana vile vimezidi. Haaah!” Mama Jema naye akakubaliana na Jema. “Basi ndio mjue hao wanaume zenu wa uzunguni ndio wanayafuata kwa malaya wa uswahili. Wewe unafikiri wakifika huko wanaambiwa kwa kizungu?” Mamdogo akafanya wazidi kucheka. “Mimi nawaambia kweli. Sasa wewe mfikirie mumeo ndio kachepuka, halafu kakutana na mwanamke kama yule aliyekuwa akifundisha staili za bafuni, halafu akulinganishe na wewe kama atarudi leo au kesho.” “Mamdogo usiniogopeshe bwana!” “Mimi nakwambia kweli. Na ukweli umeletwa mbele ya macho yako. Kwa hiyo kila unapokua chumbani na mumeo, acha uvivu na kiasi. Jua yapo magumegume kama sisi tunasubiria pande ya pili. Ukishindwa tu, ukajidai kuleta ya kizungu, sijui umechoka, unanunia mchezo, sisi huku mtaani tunakurekebishia mumeo.” Zikaanza stori hapo wakicheka sana.

Bag Party.

Huku kwa wasomi, mamilionea, wakampa shule ya kutosha James. Kuanzia kumuandaa mwanamke, jinsi ya kufanya naye mapenzi, na maisha ya unyumba wakimjadili mwanamke. Kila mmoja akaongea lake kuhusu mwanamke. Mizunguko yao ya hedhi na joto lao. Nini wanapenda, udhaifu wao. Maisha kabla na baada ya watoto. Yakawa mambo mengi kila mmoja akapata muda wakueleza juu ya ndoa yake, James akisikiliza kwa makini. Kukawa na kula na kunywa. Kina Geb, Man, Joshua na Lubuva ambao hawanywi wao wakakubalina kuondoka mapema na James kwa kutumia boti yao. Walimshauri James akapumzike sababu ya send off siku inayofuata.

Kila Kazi Na Malipo Yake.

Wakati wanataka kuondoka, Man akamuita Danny. Nusura Danny akimbilie wito. Akajikwaa kabisa wakati akiwasogelea. Alikuwa Geb na Man, Joshua pembeni kimya. “Nimezungumza sana na Grace. Hayupo tayari kumkutanisha Fili na wewe. Bado Fili anakuogopa sana, na anavyosema haachi kumuuliza kama ipo siku atakuja kumrudisha kwako. Na wakati wote anamsihi mama yake asije akasahu akamrudisha tena kwako. Mimi hilo sikuwa nikijua, kumbe ndicho kinachoendelea kati ya Grace na Fili. Anasema kila akisikia safari ya kuja huku Dar, anamuita mama yake kwa siri na kumkumbusha ahadi yake kuwa alimuahidi hatamrudisha tena kwako.” Danny alilia sana.

“Safari hii nikaamua kumvizia ili kujua kwa hakika anachozungumzia Grace. Juzi usiku wakati nikiwaambia leo tutakuja huku Dar, nikaona wadogo zake wanafurahia, lakini Fili akakosa raha kabisa. Ndipo na mimi nikajilaumu kuona sikuwa nikitilia maanani hiyo hali. Sikuzungumza naye kitu ili kuona atakachofanya. Ila baadaye nikamsikia akimsihi mama yake yeye abaki tu Arusha, atusubirie mpaka turudi. Ikabidi kuzungumza naye. Mbaya zaidi Fili anakumbukumbu ya ajabu sana.”

“Alinisimulia siku aliyomsihi anko wake asiwarudishe kwako, yeye na wadogo zake, anasema tena aliahidi hataongea tena. Atabadilika, lakini anasema walirudishwa, na wewe ukaua wadogo zake huku ukimpiga yeye makofi.” Kitu kilimpanda Geb, maana alikumbuka vile Fili alivyomuomba kwa machozi mpaka akapiga na magoti. Akalia kwa uchungu, mpaka akaondoka hapo kabisa. Yeye alishasahau hiyo siku kabisa, yaani siku hiyo ndio anakumbuka kwa wazi kabisa, hakujua kama ni kumbukumbu aliyotunza Fili.

Walisikia kilio cha Geb akilia kwa sauti ya wazi kabisa akielekea botini, Joshua akamfuata. “Ni nini tena?” James na Lubuva ambao walikuwa wakisubiri botini wakauliza. Geb akaenda kukaa chini kabisa na kuzidi kulia akiwa ameinama. Joshua akakaa pembeni yake bila yakumsemesha kitu.

“Ilibidi kuzungumza na Fili upya.” Man akaendelea. “Na kumuhakikishia hakuna atakayemtoa kwenye maisha yangu isipokuwa kifo. Ilikuwa ngumu kufikia naye muafaka, maana na Grace naye alikumbuka kama hivi alivyokumbuka Geb. Alilia sana na kushindwa kujitetea kwa mwanae. Kwa kifupi, huyu mtoto anakuogopa Danny. Anakuogopa sana. Sasa ni hivi.” Hapo Man akabadilisha na sauti. “Fili atakuwepo kwenye send-off na harusi. Tafadhali nakusihi, hakikisha hakuna mazingira unakutana naye na mpo peke yenu hata chooni. Ulichokifanya kwangu siku ile kunivizia, usikifanye kwa Fili. Sitakuruhusu. Na utanikasirisha sana Danny, kwa kuwa mimi sitamdanganya wala sikusudii kubadili kauli yangu kwake.”

“Fili anakumbukumbu kali sana. Anazungumzia mambo kana kwamba yote yalitokea jana! Nimetumia pesa nyingi sana na muda mwingi sana kumfikisha alipo sasahivi, amepoa, ila hajasahau kabisa. Sitaki turudi huko tena. Naamini umenielewa.” “Nitaliheshimu hilo kabisa. Hata mimi sitaki kumuumiza zaidi. Nilitaka mahusiano tu.” “Bado hayupo tayari na wewe.” Akajibu hivyo Man, nakuondoka.

Send-Off.

Siku ya send-off Kasa hakuwepo kati ya walio alikwa kwenye kuhudhuria, kwa upande wa bwana harusi kwa sababu hakuwa karibu sana na James. Ila alijua kama siku hiyo ingekuwa siku ya send-off. Akamuacha kabisa Jelini, ila akakubaliana na kuwa tokea mwanzo ni kweli Jelini hakumpenda. Maana tokea waachane siku walipokwenda kula ice cream hakukosea hata kumtafuta kwa ujumbe kitu ambacho si kawaida ya wanawake kwa Kasa. Wanampenda sababu yakujua honga yake ya pesa nyingi, akitaka tu sifa. Hilo halikumsumbua kabisa Jelini japo alimuonyesha kwa vitendo ni nini atapata akimkubali. Kilimshangaza sana Kasa kwa msichana kama yeye asiye kitu mbele yake, lakini akabakiwa na ajenda moja tu, kusafisha hadhi yake kwa wenzake wanaofanya nao kazi.

Shuguli ilikuwa nzuri sana. Wakahakikisha Jema anapendeza haswa. Wakala na kunywa kwa furaha. Kama alivyofanya kwenye kitchen party na hapo Jelini alikuwa msimamizi wa shuguli nzima kuhakikisha mambo yanakwenda sawa akisaidiwa na mama yake mdogo.

Alimuona Colins na mchumba wake. Akajua meza aliyokaa. Akahakikisha hakosei kupita hapo hata mara moja. Wakati wa waalikwa kupata chakula, alipomuona yeye na mpenzi wake wanasogelea meza ya vyakula, yeye akiwa anasimamia ugwawaji wa vyakula, alitoka kabisa hapo kama kuwapisha. Colins alimuona akashangaa kinamuuma rohoni kabisa. Akatamani hata kungekuwa na salamu tu, lakini Jelini alimkwepa kabisa. Akatulia na huyo mpenzi wake akisumbuka rohoni mpaka akajishangaa wakati ni yeye mwenyewe alimuomba huyo Jelini akae naye mbali.

 Akahisi hukumu ndani yake. Akasikia maumivu ya ajabu akijutia kuzungumza vile kwake. “Nimemuumiza Jelini.” Akashangaa gafla anajali hisia za Jelini! Akabaki amekaa pembeni ya mpenzi wake, mawazo yapo kwa Jelini muda wote akijionya arudishe mawazo pale, nakushindwa. Akatamani hata achomoke, amfuate nje, arekebishe kwa kusema hili au lile, lakini mpenzi wake alikaba mpaka mwisho hata chooni hakwenda.

Wakati hiyo hali ikiendelea kwa Colins, wengine walikuwa wakifurahia shuguli nzima. Walichekeshwa na maneno mengi ya Msema Chochote, MC kwa utani mwingi akimsifia Jema kwa mumewe kwa maneno ya heshima, lakini utani wa kuvutia. Kila mtu alikuwa akicheka lakini wao, Colins na mpenzi wake walikuwa kimya, kama wapo kwenye vikao vya bunge la Ulaya!

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Natamani leo ndio ingekuwa kesho.” James akamnong’oneza Jema sikioni, wakati wakila. Jema akacheka taratibu. Kumbe hajaelewa kwa hakika anachomaanisha mumewe, yeye akidhani akitamani hizo shuguli ziishe, wapumzike. Maana walifululiza mpaka wao wenyewe wakachoka, kumbe hamaanishi hivyo kabisa na James akajua. Akaona asimuache, afikishe ujumbe wake. Akamnong’oneza tena. “Lile swala letu la matusi.” Jema alishituka mpaka akapaliwa. Akaanza kukohoa, James akampa maji watu wakiwaangalia. “Bwana James!” Jema akalalamika baada ya kutulia na kumfanya James aanze kucheka. Alicheka James mpaka machozi.

“Wala havichekeshi!” “Mimi nilijua nijiandae kula kuku kwa mrija!” “Sasa si kesho!” James akazidi kucheka akimwangalia. “Acha kuniangalia hivyo bwana!” “Mimi nakuhisi wewe unataka vitendo tu, sio maneno. Au nimekosea?” “Na ulikumbuke hilo bwana James! Acha matusi.” “Hayaitwi hivyo Jema mpenzi wangu! Mbona umekazania?” “Naomba usiniambie vinavyoitwa.” James alikuwa akicheka sana. “Leo kiss hutaki?” “Vyakuuliza wala havinogi.” “Unataka nikushitukize?” Jema alicheka sana. “James! Mimi sijakupatia mwenzio.” “Na ibaki hivyohivyo. Sitaki msaidizi.” Jema na James wakabaki wakizungumza wao wawili bila kujali watu wengine mpaka shuguli ikaisha. Ungejua tu, Jema amefurahi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Napo Jelini hakunywa, akamrudisha dada yake nyumbani akiendesha gari yake. “Mwenzenu nimekuza.” Mama Jema akamtania. “Mimi najielewa ila nyinyi ndio hamnielewi.” Jelini akajibu akiendelea kuendesha. “Hilo nakubaliana nalo. Hata pombe hujanywa!” “Hii shuguli ni yetu. Sikutaka kuharibike jambo. Sasa kesho! Nahisi nitaogelea.” “Kwani kuna shida gani ukinywa kiasi au ukaacha kabisa?” “Starehe dada yangu. Kwa nini kupunja nafsi? Unakunywa na kusahau matatizo yote.” Jema akamtizama tu na kumuacha.

Waliofanikiwa, Hawakukata Tamaa.

Wakati anaingia kulala akaona ujumbe umeingia. Akajiweka sawa hapo kitandani huku akichukia kutozima simu yake, akapumzika. Kwani ni kweli alikuwa amechoka na shuguli nzima maana yeye aliianza hiyo shuguli kuanzia asubuhi kwa maandalizi. Kumbe Kasa aliangalia muda wa nchi ya Tanzania na kujua watakuwa wamemaliza shuguli nzima. Ndipo akamtumia ujumbe. ‘Nilisubiri ukaribisho wa sendoff, mpaka nikakata tamaa.’ Jelini akasoma akiwa kitandani akacheka baada ya kuona mtumaji na kurudisha ujumbe. ‘Nilijua hata ningekukaribisha usingekuja Kasa, nilijua haupo nchini.’ Kasa akaamua kumpigia.

“Kwa hiyo kama ningekuwa nchini ningekaribishwa?” “Ningejaribu. Kwema lakini huko?” “Nilikuja kumuona mama kidogo kwa siku chache tu, ninarudi kesho asubuhi kabla ya harusi.” “Basi msalimie mama Kasa.” Kasa akacheka. “Nakudanganya mwaya. Usije ibua maswali bure!” “Hamna shida. Vipi lakini send-off?” “Ilikuwa nzuri sana. Tulikuwa na dada Doro. Hajakwambia?” “Na picha zenu nimeona.” Jelini akacheka sana.

“Dada Doro naye!” “Ulipendeza sana Jelini. Wewe ni mzuri.” Hapo Jelini akacheka sana. “Sema basi, asante.” “Asante, lakini ujue mwenzio nilipania kupendeza.” Kasa akaanza kucheka. “Kweli. Kwa hiyo kuanzia juu mpaka chini nilipania.” “Basi ulijitendea haki.” “Asante mwaya.” Wakacheka kidogo. “Ungependa zawadi gani?” “Lete stori za Ulaya, na mimi nifahamu japo kwa stori na upige picha nyingiiii, nipaone Ulaya bila chenga.” Kasa akacheka. “Kama hilo tu, usijali.” Hawakuendelea sana, wakakata simu lakini Kasa akishangazwa sana na Jelini. “Ameshindwa kuomba hata pafyumu kama wenzake au Doro!” Ikamuwia vigumu pakumuweka kwenye kundi la namna gani! Alifanania kuwa mchunaji, lakini tena sivyo! Mwenzie Doro ameomba pafyumu mbili! Haya, akaonekana kama mwanamke wa kukubali kila mwanaume, lakini tena sivyo! Akabaki akimtafakari Jelini na kuzidi kuvutiwa naye. Akabaki hajui chakufanya.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hatimaye Imebaki Harusi Tu. Usipitwe Na Siku Ya Harusi Ya James Na Jema, Bikra Hawa Ambao Ni Kama Mambo Yao Yanakwenda Kwa Mteremko Yakiwa Na Baraka Zote.

Nini Kitatokea Siku Hiyo?

Ø  James Amepania Usiku Wake Wa Kwanza Na Mwanamke Kitandani. Wote wamepewa mafunzo. Watafanikisha?

Ø  Siku hiyo ya harusi Kasa Anataka Kurudisha Heshima Kwa Rafiki Zake Na Imeshamgarimu Pesa nyingi sana. Sasahivi Hisia Zinaanza Kumchanganya, Japo Doro Ndiye Anayeonekana Kufanikiwa kwenye mipango yake. Kuwa Karibu na Kasa. Amefanikiwa Mawasiliano Ya Karibu Sana Na Kasa Akimtumia Jelini kama chambo huku na yeye akisubiri fainali siku ya harusi. Yaani, anausubiria usiku Wa Harusi kama yeye ndio Jema.

Ø  Colins naye hisia kwa Jelini, mchanganyiko. Sitaki ataka. Kimempata cha rohoni. Atakuwepo harusini na mpenzi wake.

Ø  Danny mwenye hamu na majuto kwa mwanae ataweza kujizuia atakapomuona Fili siku ya harusi.

Usipitwe na harusi ya James&Jema.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment