Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 7. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 7.

 'Jumamosi ijayo kutakuwa na chakula cha jioni nyumbani kwangu. Saa moja usiku. Jelini atakuwepo lakini ataanzia kwenye kikao cha sendoff ya dada yake ndipo aje. Anaweza kuja kwa kuchelewa, lakini amesema hatakosa.’ Akatuma huo ujumbe. Kasa akasoma na kuamua kutorudisha majibu. Ila Dora akajua amepata ujumbe.

Jumamosi Ya Mahari Ya Jema.

Alfajiri sana wakasikia kengele ya mlangoni. Geb akashituka na kutoka kwa haraka kwenda kufungua akidhania labda ni Grace ameleta watoto na pia kuwahi asije amsha wanae waliokuwa wamelala kwa kuchelewa kwa kumlilia mama yao. “Lakini mbona mapema sana!” Akaingiwa na wasiwasi akiwa anakimbilia chini kwenda kufungua. Akashangazwa kumuona James pale. “Nimekuja kumuona Nanaa.” “Wewe jana ulipopigiwa simu na baba yake ulimjibu nini?” “Acha kunihoji Geb.” “Huo ni usumbufu na kuchanganya watu. Unakua na..” “Haya pisha hapo mlangoni Geb.” “Huyu anasumbua watu mama na kumchanganya mke wangu. Hajulikani kama anamtaka au hamtaki! Anataka kumuua mke wangu halafu mimi na wanangu ndio tupate shida!” “Ndio amekuja kutengeneza na wewe unamzuia! Pisha hapo.”

“Nashukuru, maana nimeshindwa…” “Hapana James. Anachozungumza Geb ni sahihi. Jana Nanaa ametolewa hapa hajitambui, wanae wanalia kwa adhabu ulizompa.” “Naona nimejiadhibu mwenyewe wala si yeye.” “Ungemuua mke wangu James.” “Sasa mbona wewe umekazania lawama bila kushangaa kwa nini mida hii nipo hapa? Kama ningekuwa nimefurahia nilichofanya sasahivi si ningekuwa bado nimelala? Sijalala mimi tokea nakata simu ya baba yake. Sasa nakuja kumuona na wewe unaanza habari zako!?” Wakaanza kubishana wawili hao.

“Wakati nyinyi mkibishana, acha mimi nipigie simu gari ya wagonjwa kabisa ije iwe inasubiri hapo nje ili kuondoka na Nanaa baada ya kumtibua.” “James anataka kuniulia mke wangu mama.” “Sasa akikosa asikemewe? Aliniudhi je?” “Si kwa…” “Acha nikachukue simu.” Mama G akawa anarudi ndani. “Basi mama, mimi nanyamaza. Ila naomba zungumza na James maana…” “Si ndio nimekuja sasa!  Wewe Geb vipi!?” “Mbona..” Mama G akaanza kuondoka tena. “Mimi nanyamaza mama.” “Naona hammalizi!” Wakasikia mlango wa juu unafunguliwa. “Mmemuamsha sasa huyo mgonjwa, mmefurahi?” “Ni James.” Geb akajibu na kukimbilia juu akipanda ngazi, James naye akamfuata kwa nyuma.

“Unaenda wapi sasa!?” “Kumuangalia Nanaa.” “Hapa si hospitali.” Wakaanza tena, mama G akakaa mbele ya kochi linalotizama ngazi akiwaangalia wakianza kulumbana tena. “Nani amekwambia nimesema hapa ni hospitali? Wewe vipi leo?!” “Ondoka James acha kumchanganya mke wangu. Sio unakuja nusunusu, na habari za kumuumiza zaidi. Unataka wanangu wabaki yatima?” “Kwamba na wewe unakufa?” “Acha ujinga.” Nanaa akawachungulia hapo kwenye ngazi,  James akampita Geb na kupandisha ngazi mpaka alipo Nanaa.

“Nilikosa kaka. Ilikuwa ni hasira ya kutokukuona muda mrefu na ukawa hupokei simu zangu. Hasira nikammalizia Jema. Lakini mimi simdharau.” “Yeye hilo hatajua Nanaa kwa kuwa alishakuona na watu wengine. Lakini tuyaache hayo. Unaendeleaje?” “Vizuri. Geb alikuwa akinipima sasahivi ili anipe dawa. Ameniambia sio mbaya. Lakini naomba unisamehe. Sikukusudia kukuvunjia heshima.” “Mimi nataka upone. Hayo mengine tuyaache, yatajijibu kwa wakati. Mahusiano yanajengwa kwa vitendo vya muda mrefu, ila ubaya wake huvunjwa kwa haraka sana kwa neno hata moja tu. Naomba huko tusipazungumzie tena. Tuache tu kama palivyo.” Nanaa akazidi kuumia.

James mwenyewe alionekana anausingizi, hajalala. “Maadamu nimekuona upo salama, acha niende nikapate usingizi hata wa masaa machache ndipo nianze siku.” “Unaonekana umechoka James mwanangu. Ingia chumba cha mwisho kabisa, ulale, huko hutamsikia mtu. Siku ya leo kwako itakua ndefu sana.” “Aisee sitafikiria mara mbili maana nilikuwa nikiendasha huku nasinzia. Acha nilale kidogo.” Akaanza kushuka.

“Pisha Geb, wewe vipi bwana!?” “Sijaridhika James.” “Sasa wewe ulitaka kunisikia nimesema nini wakati aliyeumizwa ni Jema na hayupo hapa?” “Na wewe?” “Mimi nimesema yaishe.” “Kuisha sio kusamehe, acha kutufanya sisi watoto wadogo.” “Haya, Nanaa nimekusamehe kama kweli ulikosa.” “Si alishasema amekosa! Sasa ulitaka kumsi…” “Watoto wote wataamka wawakute mnalumbana hapo.” Mama G akaingilia.

“Anachoshindwa kumsamehe mke wangu ni nini? Kwani Nanaa amemuua Jema?” “Sasa kwa nini unalazimishia mambo yaende unavyotaka wewe?” “Wewe mwenyewe unatesema James mwanangu ndio maana hujalala, na asubuhi hii upo hapa. Adhabu uliyompa Nanaa inakutesa wewe mwenyewe na Nanaa pia. Wewe ulidhani ingekuwa rahisi. Nanaa huyo ni mtoto kwako kama mama uliyemzaa kwa uchungu. Huna jinsi ukamuadhibu roho yako ikatulia. Samehe ili na wewe leo siku yako iishe kwa amani na furaha.” “Aisee ni kweli. Mimi mwenyewe nataseka. Ila sina jinsi yakurudisha mambo kama zamani. Ameongezeka Jema, na sitaki kumchanganya.” “Kwani nani amekwambia Nanaa anataka kuwaingilia? Wewe umsamehe, nyinyi endeleeni. Hatawaingilia.” “Basi yaishe Nanaa. Acha undugu ubakie kwetu tu. Huko kwa Jema, muda utajibu.” Geb akampisha.

James akacheka na kutingisha kichwa. “Wewe ni mkorofi Geb.” “Huwezi kuua mke wangu aisee.” “Sasa kwa nini unalazimishia mambo?” “Wewe nenda kalale.” Geb akampisha na kupandisha ngazi kurudi juu, James akimwangalia. “Umenielewa Nanaa?” “Nimeelewa kaka, na nashukuru. Ila natamani kama ningepewa nafasi ingine nirekebishe hata kwa Jema.” “Wewe achana kabisa na Jema. Mwache tu. Nenda kapumzike acha na mimi nikalale kidogo, nisije nikashindwa kwenda ukweni leo.” “Chumba kisafi na mashuka tumebadili hata siku tatu hazijaisha” “Hamna neno. Nashukuru mama G.” James akapitiliza mpaka chumbani, akajitupa kitandani na suruali yake ila alitoa viatu na shati. Nyumba ikapoa.

“Haya, na wewe nenda kalale. Wanao wakiamka tu, watakuja hapohapo kitandani kwako.” “Nashukuru mama.” “Mungu anajibu Nanaa. Ungekufa bure kumbe Mungu wako bado anakutengenezea njia. Na hata na la Jema, najua linakuuma, lakini jipe muda. Kila kitu kitakuwa sawa tu.” “Amina mama. Hata sasa angalau nina tumaini.” “Acha kulia sasa Nanaa! Utaanza kuumwa tena. Tulia mpenzi wangu.” Mama G akaanza kucheka akisimama. “Sasa na wewe unapigania msamaha kwa nguvu?” Akamuuliza Geb akienda chumbani kwake. “Vyakubembeleza vimeshindikana. Anataka kuniulia mke, mimi?” Mama G akazidi kucheka. “Naona leo na maneno yamekutoka!” “Asinitanie kabisa James.” Wakarudi kulala.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika saa sita James haamki akaenda kumgongea. “Wewe vipi? Hulipi tena mahari?” James akashituka kutoka usingizini. “Nilikuwa nimechoka! Kwani sasahivi ni saa ngapi?” “Saa sita. Toka uende saluni, usitucheleweshe.” James akatoka hapo kwa haraka. “Vipi Nanaa?” “Naona yupo vizuri. Magesa anamuongelesha huko juu.” “Utaniagia basi. Acha niwahi. Tutawasiliana kabla ya muda wa kwenda Tegeta.” “Nije na Nanaa?” “Acha kunichanganya sasahivi Geb. Kwani wewe nilikukaribisha? Mbona ulikuja kwa nguvu?” “Sasa msianze tena huko koridoni. James nenda wahi saluni.” “Anataka kunichanganya mimi!” “Nakuchanganya kivipi wakati wewe mwenyewe ndio misamaha yako haieleweki? Unasamehe nusunu…” “Geb Magesa nakuonya wewe mtoto!” Kimya.

“Haya, James pita hapo kimyakimya. Kula au ondoka nenda saluni.” “Mimi njaa inaniuma mama G. Labda nibebe kitu.” “Geb usiongee neno. James pitiliza jikoni, chukua unachoweza, uondoke, usitucheleweshe kwenye shuguli ya jioni.” Akacheka wakati akimpita Geb kwa kumsukuma kidogo kwani bado alikuwa amesimama katikati ya mlango.

“Grace ameshafika?” “Jeshi lake liko huko juu na Nanaa. Fujo yote ipo huko juu.” “Na yeye mwenyewe?” “Wapo hotelini na mumewe, tutakutana nao jioni.” “Na mimi uniombee ndoa yangu isichuje mama.” “Wewe pia unalo jukumu James mwanangu. Usibadilike na kumzoea mwenzio. Hao wawili wanakua kama wameoana jana. Kila wakipata mwanya, wanautumia kwa ajili yao. Watoto hawajawahi kuwatenga.” “Sema kuwatenga sana. Maana haiwi kama zamani kabla watoto hawajaja. Ila sema na wenyewe wanafanya juhudi za makusudi kutoua mahusiano yao. Kama wewe mwenyewe ulivyosema asubuhi, mahusiano hujengwa. Ukizembea tu, rahisi kuparanganya matofali yote uliyoyajenga.” Akaongeza Geb.

“Halafu uache mazoea kwa mtoto wa watu. Hata baada ya ndoa, ishi naye kama unatongoza. Hili hata Joshua atakwambia ndicho kinachofanya ndoa zetu kubaki changa japo zina muda mrefu.” “Sasa usikae bwana James!” Mama G akamkatisha. “Geb anaongea!” James akaongea kwa mshangao. Wakacheka. “Acha nisikilize mama.” “Hapana. Tutakuandalia bag party, hao wote watakuja kuzungumza na wewe. Hata Man atakuja. Chukua chakula uondoke, leo tusije haribu ukweni.” James akaingia jikoni akicheka. Akatoka na vyakula wima wima.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

James alipotoka tu, Geb akamgeukia mama yake. “Naomba nenda na Nanaa saluni. Akatengenezwe kwa shuguli jioni. Itamsaidia kuchangamka. Mimi nitabaki na watoto.” “Geb umekazania!” “Niliingiwa na hofu ambayo sijui niisimuliaje! Unajua ni kama niliona uhai wa Nanaa ukitoka mbele ya macho yangu hivihivi! Halafu wanangu wanalia, siwezi kuwasaidia kwa lolote! Hakika niliogopa mama! Nikashindwa hata kuomba, ikabidi kumpigia simu Joshua, akaja kunisaidai.” “Haiwezekani Geb! Usiku ule!?” “Acha mama yangu. Sijawahi kuogopa maishani kama jana. Nilikuwa nikitetemeka kama nimeingiwa baridi. Nikawa najiuliza nitafanya nini na watoto wote hawa bila Nanaa!”

“Lakini mbona hukuonyesha! Japokuwa wanao walikuwa wakipiga mayoe, lakini nilishangaa vile ulivyokuwa umetulia na kuendelea kufanya CPR bila kukosea mpaka akaamka!” “Pale sijui Mungu aliniwezesha vipi kuhesabu na kumpa hewa safi bila kukosea! Sijui aisee!” Wakaendelea kuzungumza yeye na mama yake huku wakisikiliza kelele za watoto juu. “Hiyo fujo huko juu huyo Nanaa atapumzika kweli?” “Mwenyewe anataka hiyo kelele, ndio anasema anajisikia vizuri.”

Mahari Ya Jema.

Iliposika saa 10 jioni upande wa James wote walikuwa wamekusanyika sehemu waliyokubaliana wakutane kabla ya kufika kwa kina Jema. Hapakuwa mbali sana na nyumbani kwa kina Jema. “James ulivyopendeza! Kama siku ya harusi!” “Nimepania Grace.” Wakacheka. “Asanteni sana kwa kuja.” “Hongera sana aisee!” Wakapeana mkono. Geb akasogea karibuya Grace na James, na Danny naye alikuwa awasogelee pale, alipomuona tu  Geb amefika hapo, akabadili njia, akarudi kwenye gari. Geb alimuona akanyamaza tu. Grace hakuwa amemuona, Man alikuwa akizungumza na simu, alipomaliza naye akaungana nao, stori zikaanza hapo wakimpongeza James.

Wakajipanga hapo ndipo msafara wa kwa kina Jema ukaanza. Walipokelewa vizuri sana walikuwa wakisubiriwa wao tu kwani ndugu wa Jema wote walikuwepo hapo tokea asubuhi. Jelini akafurahi sana kumuona Colins. “Mchumba umekuja?” “Na mimi nipo Jelini. Mzima?” “Mimi mzima, eti nimefurahi kukuona!” Akili za Jelini akazungumza mbele za watu wote huku akicheka. “Na mimi nipo Jelini.” Wakaanza kumchokoza. “Akuu! Mimi nimemuona mchumba Colins tu. Wengine wala sijawaona.” “Bwana Jelini ni umependeza!” “Basi mwenzio ni kawaida yangu. Huwa sijui kutisha.” Kila mtu akacheka, James akamgeukia. “Mimi sijasema neno baya Shem.” “Basi kamsaidie Jema.” “Jema mwenzio kasema nisinywe bia hata moja. Niangalie jambo lisiharibike huku. Wote mle na kunywa. Ila nisiongee.” Kila mtu akacheka.

“Ila unaongea.” Danny akamchokoza. “Nimemsalimia Colins tu mimi. Sijaongea jambo baya. Eti shem?” “Basi hakikisha kweli watu wana vinywaji.” “Jema ameshamuambukiza! Mimi nakua mtu wa kufukuzwa tu. Sijaongea jambo baya hata moja!” “Jelini!” James akawa kama anamsisitiza. “Basi mimi naenda ila namuhudumia Colins mchumba wangu. Sitaki ahangaike. Akitaka chochote, namletea. Sitaki apate shida.” “Sasa na sisi Jelini?” “Akuu! Mimi nyie sio jukumu langu. Kuna watu watawahudumia, ila mimi nimeambiwa niwasimamie kuhakikisha kuna vinywaji tu.” “Kwa hiyo watamuhudumia na Colins?” “Yeye mchumba namuhudumia mimi.” Wakataka kuendelea kumuongelesha, James akamuita. “Naenda kuleta vinywaji.” Akaondoka hapo. “Mahari inayofuata ni mimi kwa Jelini.” Wakaanza kubishana hapo kama watoto. “Jelini anamtaka Colins tu. Haya nyamazeni.” Danny akawanyamazisha watu wazima hao na pesa zao, wengine wanacheka.

Nanaa alikuwa amekaa katikati ya mumewe na mama G. Halafu Grace katikati ya Geb na mumewe. Kimya kama kawaida yao. Joshua alikuwepo ila Naya alikuwa ndani na Jema. Alimleta hapo mapema kidogo akawa chumbani na Jema. Joshua akasimama. “Unaenda kumuangalia nini?” James akamchokoza. “Wasije mtoa mlango wa nyuma.” “Jema amesema jicho lake haliondoki kwake mzee! Huamini?” “Acha na mimi nikaridhishe macho yangu.” Joshua akaondoka na kufanya wacheke. Geb akamuona mkewe ametulia kwa kupoa, akamtingisha kwa kumsukuma kidogo na kumvuta mkono akaushika. Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu, nakutulia.

Wakaanza kugawiwa vinywaji kwa vile walivyotaka huku meza ya chakula ikiendelea kuandaliwa. James mwenyewe alichangia pesa ya kutosha tu kwenye hiyo shuguli kumsaidia Jema kujiandaa. Kwa hiyo kukawa na vinywaji vyakutosha kwa vile James na Danny walivyojua marafiki zao. Ilikuwa ni kata mti, panda mti.

Baada ya shuguli kuanza, James akalipa mahari akiwa na baba zake, mama yake pia. Wakapeleka mambo kimila. Na hivi bibi alikuwepo, ikawa nzuri na heshima ya kipekee. Walipokabidhiana mahari, na James kupewa Jema ndipo akatoka naye. Ukweli walipendeza sana. James alivaa shati rangi sawa na gauni alilovaa Jema. Akatengenezwa saluni vizuri haswa. Kwa hakika Jema alipendeza. Ungemuona jinsi alivyokaa na James, ungejua wanapendana na wamekusudia kukamilisha swala la kuishi pamoja.

Majuto, Mjukuu.

Shuguli ikaendelea watu wakila na kunywa kwa furaha. Lakini akili na mawazo ya Danny ni jinsi ya kumfikia Man. Macho yake na akili zake vilikuwa kwake wakati wote akimuwinda angalau ajitenge na kina Magesa azungumze naye. Akashindwa kufuatilia tukio zima wala hakula kwa uhuru, macho kwa Man wakati wote.

Karibu na mwisho kabisa, akamuona Man ametoa simu mfukoni. Akaiangalia, akamuona anamuonyesha Grace, akamuona Grace ameingalia simu ya mumewe, akambusu midomoni, akasimama na kuondoka pale. Moja kwa moja akajua anakwenda kuzungumza na huyo aliyempigia simu. Akampa kama nusu dakika, na yeye akasimama kumfuata. Akamuona amezunguka mbali kidogo na pale kama anayekwepa kelele za kwenye sherehe, akafuata kwa tahadhari, akajibanza kwenye kona akimsubiria amalize mazungumzo yake asiingilie.

Alipomaliza wakati anarudi kundini, Danny akajitokeza kwa haraka mbele yake mpaka akamshitua. “Kwema kaka!?” “Samahani nimekushitua. Lakini mimi naitwa Danny.” Man akasimama vizuri akimtizama. “Sitaki kukuudhi mkuu. Nilikuwa nataka tu ujue nakuheshimu na nakushukuru sana kwa kile unachokifanya kwa Grace na Fili.” “Ukweli haijalishi kile unachojisikia juu yangu, mke wangu na watoto wetu. Kwa kuwa Grace ni mke wangu na Fili ni mtoto wangu. Sidhani kama huwa unavizia watu na familia zao kuwaambia haya unayoniambia sasahivi!” Man akajibu akiwa ametulia tu.

“Sifanyi hivyo kwa wengine kwa sababu sijawahi kuwasababishia wengine madhara kama niliyomsababishia Grace na Fili.” “Sema kwa wengine hujasababisha madhara ya moja kwa moja. Ila madhara uliyosababisha kwa watu ni makubwa sana, Danny. Ukisema ni kwa Grace na Fili tu, unakosea.” “Najua nimekosa sana. Inawezekana nimeshindwa kuliweka hili sawa kwako, tena sasahivi, lakini upo sahihi. Najua kwa hakika nimekosa.” Man akashangaa anapiga magoti.

“Vipi wewe!?” “Tafadhali naomba kujua hali ya Fili. Tafadhali sana Man. Hata uniambie tu kwa mdomo na kama Mungu atakupa rehema kwangu, basi ningeshukuru kama ungenionyesha picha yak…” Geb akafika hapo wasijue alitokea wapi. Akasimama na mikono mfukoni akimtizama Danny. Man alimuona jinsi Danny alivyoingiwa hofu na kupaniki. “Nazungumza naye kwa uzuri tu, Geb.” Danny akaanza kutetemeka mpaka midomo, akisikika kujitetea kwa hofu ya ajabu. Ukweli iliumiza kuangalia.

Lakini akajikaza na kuendelea. Akamgeukia tena Man. “Na wewe una watoto Man. Tafadhali naomba tu kujua hali ya Fili ni hilo tu.” Akawa anaongea huku anafikicha mikono mbele akitetemeka, na bado alikuwa magotini. “Mimi ni yatima Man. Ndugu wa damu niliyebaki naye hapa duniani ni Fili tu. Nilikosa sana. Ninachotaka kujua ni hali yake tu. Na ndio maana nakuuliza wewe kwa heshima, wala si Grace.” Danny alikuwa mnyenyekevu, usingeweza dhani ni yule Danny aliyekuwa amejawa kiburi.

Man akamtizama Geb. Geb kimya, macho kwa Danny. Man na yeye akarudisha macho kwa Danny, akakumbuka na yeye alishapitishwa hapo anakopita Danny sasahivi ila yeye alikuwa jela, hana wakumlilia wala kumpigia magoti. Kipindi alipofungwa na mke wake wa kwanza na kumtenga na mtoto aliyemlea kwa mikono yake mwenyewe kama yaya. Liam. Uchungu ukamuingia.

“Fili ni mzima. Juu ya kukuonyesha picha yake ni mpaka nizungumze na mke wangu. Grace akikubali, ndipo nitakuonyesha. Na haitakuwa leo kwa sababu wewe ni mtu wa mwisho ninayetaka kukutaja kwake leo, haswa akiwa mapumzikoni. Nitazungumza naye wakati mwingine, akiridhia, utapata picha ya Fili.” “Nashukuru sana Man. Asante sana. Na naomba uniombee msamaha kwa Grace na Fili.” “Kwa hakika sitafanya hivyo.” Man akageuka na kuondoka, Geb naye akamfuata nyuma wakiwa wamemuacha Danny amepiga magoti.

“Nitaipataje hiyo picha yake, endapo mama yake atakubali?” Akapaza sauti kwa nguvu ikisikika yakutetemeka. “Utaipata.” Man akajibu akiwa anaondoka wala hakugeuka ndipo Danny akajikung’uta na kusimama. Akajihisi uchungu wa ajabu, mwanaume akalia. Akazunguka nyuma kabisa ya nyumba, akaridhika yupo peke yake, akalia sana. Akakumbuka jinsi alivyokuwa na amri kwenye familia yake. Kwa Grace na wanae! Heshima aliyoipata kwa ajili tu ya kummiliki Grace! Danny akalia sana akiombolezea tena wanae. Na kila alipokuwa akifiria Man ndiye anayemmiliki Grace, mwanamke ambaye hakuwa akitaka hata kuhisi mwanaume mwingine yupo karibu yake, alilia sana. Tena kwa kwikwi, asijue chakufanya.

Kumbe Geb alishamfikiria muda mrefu sana. Kabla hajafika hapo, alishajiweka kwenye nafasi ya Danny kwa kutumia aina ya akili yake. Akajiuliza mengi jinsi ya kumfanya Grace atoke hapo kwenye hiyo shuguli akiwa hajasababishiwa maumivu mengine na Danny. Akaweka kila njia akizijadili kichwani mwake. Akajua kwa hakika hata kama Danny ni mwehu kiasi gani, asingethubutu kumsogelea Grace kwa kuwa itakuwa ni kama anaweka kidole jichoni kwake yeye Geb. “Hathubutu!” Akajiridhisha Geb. Akajua atakaye mfuata ni Man tu. Hakumwambia mtu, ila akabaki akimfuatilia na yeye huyo Man zaidi kama vile alivyokuwa akifanya Danny. Sasa alipoona Man ametoka tu, akampa muda kidogo na kuangalia alipokaa Danny. Alipomkosa tu ndipo akawafuata. Danny alilia sana kukumbuka shuka kumekuchwa.

Kisicho Ridhiki, Hakiliki.

Ukweli Jelini alimuhudumia vizuri sana Colins tena bila maneno mengi akiwa hajalewa kabisa. Mpaka chakula alimletea alipokuwa amekaa. Akamkarimu kwa heshima kitu ambacho si kawaida ya Jelini. Na tena alifanya kwa moyo wa furaha mpaka yeye mwenyewe akajishangaa. Kwa mara ya kwanza maishani akajisikia kitu cha tofauti kwa huyo Colins.

Wakati wanaondoka Colins akamuomba wazungumze. Jelini akacheka akijua anataka kumshukuru, ila ikawa tofauti. “Nashukuru kwa huduma nzuri sana.” Jelini akacheka kwa furaha akijua hata yeye ameona jinsi alivyomuenzi. “Lakini naomba kukwambia jambo na niombe usinichukulie vibaya kama mwanaume asiye na shukurani au sijielewi.” Jelini akaanza kupoa.

“Nina mchumba wangu. Na siku ya send off pamoja na harusi, Mungu akipenda na yeye atakuwepo. Hiki ulichokifanya hapa ni kitu kizuri sana na ninashukuru. Lakini yeye hatakifurahia akiona unanitamka mbele ya watu, na kunihudumia hivi. Italeta matatizo.” Jelini alijisikia vibaya, akashindwa kabisa kumuangalia. Ikawa kama amempiga kibao cha uso mbele ya umati. “Ndio maana nilitangulia kuomba msamaha, Jelini.” Akamuona vile alivyomuumiza. “Samahani. Sikuwa nimekusudia ku…” Akasita. Kisha akarekebisha. “Hapana. Sitaomba msamaha kwa nilichokifanya kwako, kwa kuwa utaniibia furaha yote niliyokuwa nayo Colins. Nilifanya kwako kwa moyo na sijui ni kwa nini! Kwa sababu hakuna mtu nimewahi kumfanyia hivyo! Najihisi sijakosa, ila nimefanya kwa mtu asiye sahihi. Sitarudia tena. Uwe na amani kabisa kufika kwenye hizo tafrija zote ambazo na mimi nitakuwepo, nakuahidi sitakusogelea wewe na mpenzi wako.” Jelini alizungumza kama mtu anayejielewa, kisha akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alimuacha Colins amezubaa hapo. Akataka kuumia pengine hakutakiwa kusema hivyo kwake, lakini alishazoea kutongozwa na wanawake, kitu kinachowakosesha amani kati yake na mwanamke wake na kuzua ugomvi kwa wivu wa kupitiliza. Colins alijaliwa sura ya kike. Alikuwa na uzuri wa namna yake wakuvutia wanawake. Rangi yake nyeupe hata gizani ungejua ni mweupe. Halafu akapewa umbile la kiume, na urefu wa kumtoshea kupendeza kwa kila aina ya vazi la kiume analoweka mwilini. Alichokifanya Jelini kwake si kigeni hata kidogo. Anafanyiwa na mabinti chungumzima na wamama watu wazima pia huwa wanamtongoza. “Ni wale wale tu, hamna jipaya.” Akajitia moyo na kuondoka kabisa hapo kwenye tafrija.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jelini akaenda kutafuta sehemu zilipokuwepo bia, akaanza kunywa. Jema akamfuata baada ya kuagana  na James. “Asante kunisadia Jelini mdogo wangu. Wageni wameridhika na kila kitu. “Bora yako wewe hata umeona nimefanya jambo zuri.” “Sasa sio kwa sababu umeona bia, ndio unywe mpaka ujisahau Jelini. Kuwa na kiasi.” “Sitoki hapa wala siendi popote. Sasa nikilewa nyumbani pia ni vibaya jamani!?” “Basi. Mimi nakwambia kwa faida yako. Weka nyingine unywe kesho.” “Mimi nataka kulewa leo. Na sitoki. Nikilewa mama ataniweka kitandani.” “Wewe unywe kwa starehe zako, halafu shida nipate mimi!” “Basi niacheni hapahapa labda mwanangu atanisitiri.” Akajibu kwa hasira wasijue ameumizwa haswa. Wao wakamchukulia ni tabia yake.

“Sasa wewe Jema unaenda wapi tena?” “Nimeshakubaliana na mama baada ya kitchen party ndio nihamie hapa. Kwa sasa kakubali nirudi kwangu. Haya sema jingine mama mdogo.” “Eti dada! Huyu si ashakua mwali?” “Kazi zake huko ofisini utamfanyia wewe?” Kama kawaida yake akajibu mbovu. “Sasa mwali si anawekwa ndani?” “Umesikia huyu mmakonde?” Wakaanza kucheka. “Mwenzenu muajiriwa. Likizo naanza jumatano ijayo. Mama wa kichaga, kaniambia nitulie kazini. Huyo hapo ndugu yenu, hangaikeni naye.” “Wewe nenda zako. Kilichobaki hapa ni sisi kunywa na kelele, na wewe huyawezi. Nenda.” “Mimi ndio maana nampenda mama Jema. Ananijua mwanae.” Jema akaondoka haraka sana kabla hawajaanza kulewa.

Raha ya Penzi, Kupendwa.

Akaingia tu kwenye gari simu kwa James. “Mwenzio naolewa.” James alicheka sana. “Unampenda mchumba wako?” “Hilo swali la pili na wewe! La kwanza ulitakiwa kusema unaolewa na nani?” James akazidi kucheka. “Samahani Jema. Unaolewa na nani?” “Bwana mpenzi wangu ni mzuri, hujawahi ona maisha! Bwana kaka ananipenda huyo! Na leo kanilipia mahari. Sema sijafurahi sana.” “Kwa nini tena?” “Anajua kukiss huyo, ila leo hata haja nikiss.” Jema akawa analalamika kwa deko. “Labda mazingira hayakuwa rafiki. Si wazazi walikuwepo?” James akamuuliza. “Kwa hiyo anawaogopa wazazi!?” “Mimi nafikiri ni kuwaheshima tu. Asifikishe wazazi mbali kihisia.” Jema akacheka na kuongeza. “Mmh! Basi nimetoka patupuuu! Nilikuwa nammezea mate! Nikatamani hata anikisi kidogo tu, lakini wapi! Na alivyokuwa amependeza!” “Kwa hiyo siku haijakamilika?” “Labda kwa mama mkwe wake maana amekua tajiri gafla. Amelipwa mahari na kupewa zawadi juu! Huna utakalomwambia mama Jema, asimsifie mkwewe.” James alicheka sana.

“Lakini si bibi harusi?” Akauliza akicheka. “Bibi harusi katoka kinyonge. Na anakwenda kulala kwake kinyongeee.” Akajilalamisha. “Pole sana. Pengine na yeye alikuwa akikutamani, ila anajikaza tu. Anajiambia huyu, atanikoma kwenye fungate.” Jema alicheka mpaka akakata simu.

Alipofika kwake, akakuta James anamsubiria nje ya mlango. Jema alifurahi na kushindwa kusubiria waingie ndani. Akaacha kila kitu kwenye gari akamkimbilia James. “Nimekuja kukamilisha siku yako.” Jema akakimbilia midomoni. Alimbusu James kama aliyekuwa na kiu ya miaka. “Nakujibu swali lako la kwanza, mimi nampenda mchumba wangu. Sana.” Jema akajibu akiwa amekumbatiwa vilivyo. James akarudi midomoni, kiss zikaendelea.

Taka Cha Mvunguni.

Ikaendelea kazi ya kumbembeleza Jelini kwa jumbe ili kumfanya awe upande wake lakini ni kama akashindwa. Jelini alipigiwa kengele ambayo alijua anatakiwa kuamka lakini ikawa akibishana nayo maaana hakuwa tayari kuamka upande anaotakiwa, ili kubadili maisha yake. Colins alimfanya ajidharau sana, maana kwa ukweli Jelini alikuwa na umbile la mtoto wa kike la kiafrika. Anavutia kwa kumtizama, na yeye alijua. Kuanzia kichwa mpaka unyayo hata akitembea bila viatu utamuangalia tu. Kuja kuambiwa vile na Colins, ikamshusha sana. Alishazoea kutetemekewa na wanaume kama tu Colins alivyozoea kutetemekewa na wanawake. Wote hawajui kukataliwa. Ile ikamuuma sana mpaka akajishanga inakuje mtu kama Colins amsumbue kichwa wakati anahangaisha wanaume wa maana zaidi yake!

Doro akazidi kutapatapa. Anamtaka Jelini kumridhisha Kasa na kumvuta Kasa karibu yake, lakini Jelini naye ameamua kutulia kwao tu. “Mbona hata baa huji sasa?” “Mwezio baa nafuata bia za bure. Sasa kama mama Jema ananipa bia za bure bila masimango si bora nitulie kwetu!” Jelini akamjibu na cheko. “Kwa hiyo bado hujanisamehe?” “Kwani ulikosea? Ni kweli japo unauma.” “Kwa hiyo?” “Kwahiyo nini na mimi ndio nakupunguzia shuguli! Acha nikae kwetu. Ila jumamosi nitakuja kwako kama nilivyokuahidi. Wala usiwe na shuguli yakunipigia simu kila wakati. Matusi yako yamesamehewa.” Alimjua Jelini hawezi hasira za muda mrefu, wakacheka na kuagana asijue jinsi Doro anavyomchafua kwa kila mwanaume anayemtaka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

v Safari ya kuoa kwa James inakwenda vizuri si kwa vipingamizi kama kwa Joshua na Geb watu wake wakaribu. Amefanikiwa kupendwa ukweni. Kitajiri kipi kwa maharusi hawa wote bikra, na James anatizamia sana fungate?

v Bado Doro hajafanikisha yake. Lengo lake ni nini? Maana si kumuunganisha Jelini na Kasa.

v Kwa mara ya kwanza, Colins amekuwa umiza kichwa kwa Jelini. Kulikoni hapo?

v Bale?

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment