Akapata
uungwaji mkono upande wa mama zake na marafiki zao mpaka akashangazwa. Kazini
nako wakatoa michango ya kila sherehe. Wanawake wakachanga kwenye kitchen party
na sendoff. Jema alijawa hekaheka za kazi na harusi lakini akiwa na furaha
sana. Mama G naye akamwambia Nanaa watulie kabisa ili kumpa nafasi ajiandae kwa
siku yake muhimu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kile kitu
kikawa kinamla Nanaa ndani kwa ndani hawezi kujisaidia. Majuto yakupitiliza.
Akapoa kuliko kawaida ya maneno mengi kama mwanae Magesa. Kuanzia asubuhi mpaka
jioni kimya kama hayupo sehemu, kitu kisicho kawaida. Hakuna faraja aliyopokea
kwa yeyote hata kutoka kwa mumewe. Ikawa kama amekua mgonjwa tena. Kazi zake ofisini
anayefanya ni mumewe. Anadamka asubuhi na mapema kwenda kazini, akimuacha Nanaa
akiwa amelala. Geb akabaki na kazi yakumuhimiza kunywa dawa maana bado Nanaa
alikuwa ni mgonjwa wa moyo wa kunywa dawa kila siku kusaidia moyo wake kufanya
kazi. Hakuna aliyejua jinsi yakusaidia hiyo hali, maana James aliwaambia
kabisa, wawe wanamkumbusha asije akasogea alipo yeye wala Jema. Kwamba hata
Nanaa akiugua, asiambiwe! Hakuna aliyejua chakufanya.
Ijumaa.
Siku ya
ijumaa usiku kuamkia jumamosi siku ya kaka yake kutoa mahari wakiwa sebuleni,
Grace akizungumza na mama yake juu ya ujio wao kesho yake kwenye mahari na
mapokezi, mama G akamuomba aje na watoto angalau awaone, watabakia nyumbani
wakati wao wakienda kwenye shuguli. “Mama bwana! Wewe unataka
kunitia shuguli. Nije na wote hawa! Kwanza ni siku moja tu!” “Kwani unawabeba
mgongoni au unawapakata huko kwenye ndege? Au kutaka kuninyima tu wajukuu?”
“Umeanza mama jamani! Kwanini hukuyasema hayo mapema nikajipanga?” “Ndio
nimefikiria nikaona sio sawa mje bila watoto.” Grace akabaki kimya akifikiria.
“Wewe
niletee hapa, utaenda kulala na mumeo popote utakako.” Akaanza
kucheka. “Ulijuaje?” “Kwani wewe mgeni kwangu?” “Nataka muda na Man bwana,
akiwa nyumbani Giana anamganda hataki kushuka mpaka nachoka kusubiri naishia
kulala mimi sijashikwa!” Mama
yake alicheka sana. “Basi na wewe ulikuwa hivyohivyo! Ukimuona baba yako, ulikuwa hutaki
hata kusogea mpaka upitiwe na usingizi, ndio akuweke yeye mwenyewe kitandani.
Hapo muda unakua umeisha, anarudi kwake, mimi na Geb wangu ndio tunaishia
patupu. Hatujapata naye muda hata kidogo.” “Bwana Giana kazidi mama! Utafikiri
ananifanyia kusudi mimi, Fili na Gian jamani!” Mama G anacheka hana
mbavu.
“Na deko
lake lile Giana, mama mkwe wako, kama namuona!” “Nakwambia huna utakachomwambia
wala kumshawishi, akaelewa! Kwanza inakuwa kama anakua hana masikio tena kwa
mwingine, ni baba yake tu! Fili yeye alishajua, basi Man akiingia tu, yeye na
Gian wanamuwahi mlangoni na kumvuta pembeni, dada mtu akisikia tu sauti ya baba
yao, ni wake. Hapo tena mwanangu yule hataki mtu amuongeleshe baba yake. Yeye
tu na vijidonda hata vya miaka iliyopita, anataka baba yake aviangalie,
avipulize na kumbembeleza kama ndio akatoka kuumia! Sasa nikafurahia hii
safari, nikajiambia nitakuwa na Man peke yangu kuanzia kwenye ndege mpaka hapa
na kurudi! Na wewe unataka kunijazia msafara!” Grace akaendelea
kulalamika.
“Mimi
nitakua nao hapa, wewe utakwenda popote unapotaka na mumeo. Tena mkija asubuhi
mnaniletea hapa, nyinyi ondokeni hata mkitaka tukutane huko kwenye mahari, mimi
sina neno.” “Kama hivyo sawa.” Nanaa akabaki akisikiliza vile huyo mama
anavyojali wanae nakuzidi kuumia yeye kushindwa kumpokea mtu muhimu sana kwenye
maisha ya kaka yake! Watu wanamipango ya kwenda kwenye shuguli muhimu ya James
aliyekana maisha yake kwa ajili yake, yeye anapitwa! Wakaendelea kuzungumza
wakicheka, Nanaa akaona aondoke tu hapo.
Kila Mchuma Janga, Hula na Wakwao.
Akanyuka
kochini taratibu, mumewe akamuona. “Unakwenda wapi?” Wanae wote kila kitu
kikasimama baada ya mama yao kusimama, macho kwake maana alitoka kitandani ili
awe nao hapo sebuleni baada ya kurudi shule na Geb ndiye aliyekwenda kumtoa
kitandani ili watoto wake waridhike. Waanze weekend na furaha wakijua mama yao
yupo sawa. “Narudi kupumzika ndani. Msiwe na wasiwasi.” Akajibu kinyonge
akijaribu kutuliza wanae. “Twende nikusindikize.” Geb akasimama kumfuata maana
alijua wazi mazungumzo ya Grace na mama yake yatamuumiza tu. Grace anakuja Dar
kwa shuguli ya kaka yake ambayo yeye aliyekuwepo hapo mjini hatahudhuria!
Akajua lazima aumie tu.
Ile
anapandisha ngazi ya tatu, akasikia kizunguzungu, giza, Nanaa akaanguka na
kupoteza fahamu. Uzuri Geb alikuwa naye karibu akamdaka na kwa haraka sana
akampigia baba yake simu. “Mlaze chale na mpe CPR haraka, wakati mimi natuma
gari ya hospitali. Mtanikuta hospitalini na madaktari wakimsubiri.” Geb
alishafundishwa jinsi ya kufanya CPR na ilikuwa mafunzo mahususi kwa ajili ya
huyohuyo mkewe. Watoto wake walikuwa wakilia sana kwa hofu. Walijua mama yao ni
mgonjwa, ila kuanguka na kupoteza fahamu na vile baba yao alivyokuwa akimfanyia!
Ikawashitua sana. Walikuwa wakilia kwa hofu sana wakimuita mama yao. Ndipo Geb
akajua hakuna maisha ya wanae hapo bila huyo Nanaa.
Viliendelea
vilio vya watoto, yeye akijaribu kutulia akihesabu kwa makini na kuminya kifua
cha mkewe, kisha kumuwekea hewa safi mdomoni akitumia midomo yake ili kumsaidia
kusambaza damu mwilini kote mpaka kwenye ubongo. Akafanya kivyo mara kadhaa, mpaka
akafungua macho. Baba yake mzazi yupo kwenye simu akimpa maelekezo Geb kitu
chakufanya kumpa huduma ya kwanza mpaka gari ya wagonjwa ilipowasili kumchukua
ikiwa na maelezo kitu gani cha kumsaidia mpaka kumfikisha hospitalini.
Saa nne
usiku Nanaa akawa ameshapewa huduma, yupo kwenye chumba cha hospitalini
amepumzishwa. Baba yake na Geb ndio waliokuwepo hapo kwenye hicho chumba. Geb
akabaki ameinama tu. “Sijaelewa Geb! Kwani Nanaa aliacha kutumia dawa? Mbona
pressure iko mbaya hivi!?” “Anatumia, lakini yupo na msogo wa mawazo
ndio maana pressure haitulii.” “Kwa nini hukuniambia mapema?” Ikawa kama analaumu.
“Nilijua tumeimudu. Mchana nilirudi nyumbani, nikampa dawa na kumpima,
ikaonekana ipo sawa. Niliporudi tena jioni na kumuamsha ili angalau apate muda
na watoto, maana walirudishwa nyumbani kutoka shule mpaka mimi narudi jioni
walikuwa hawajamuona mama yao, kitu kilichowapa wasiwasi. Ndipo nikamuamsha
nakumuomba atoke kidogo tu, wamuone waridhike. Akaniambia anajisikia vizuri
akatoka kitandani na kufuata watoto. Alipotaka kurudi chumbani kupumzika ndipo
akaanguka, uzuri nilikuwa nyuma yeke, ndipo nikamdaka.” Baba yake akafikiria
kisha akawa kama amekumbuka kitu alichosema mwanzo.
“Umesema
ana msongo wa mawazo!?” “Hawapo kwenye maelewano mazuri na James. Hiyo ndiyo
inamsumbua sana Nanaa.” Ikawa kama amemchanganya kabisa. “Unasema James!? Kwa
nini tena!?” “Ni habari yao wenyewe, lakini hicho ndicho kimetibua kila kitu.
Na nafikiri ni kama hajui kitu chakufanya kurudisha mahusiano yao.”
“Haiwezekani! Kwani James anajua kama anaumwa?” Geb akawa ameshamaliza
mazungumzo, na yeye Lubuva alishamjua Geb. Hata hapo alishazungumza sana. Akakumbuka
alimwambia hawapo kwenye maelewano, inamaana James hajaambiwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akamuona
Lubuva anatoka. Akaenda kumpigia simu James. “Unajua kama Nanaa anaumwa?”
“Kwa wewe kunipigia simu, inamaana yupo kwenye mikono salama, na mimi sihitajiki
ndio maana mpaka sasa unaona hata sijaambiwa, wewe umeambiwa.” Akajibu
James na kumshangaza sana Lubuva. “Yameanza lini hayo!?” Lubuva
akashangazwa sana. James aliyemkuta na Nanaa, hawezi kulala kama Nanaa ni
mgonjwa! “Upo na watu sahihi sana, wanaoweza kukujibu maswali yako yote.”
“James! Hivi umenielewa lakini? Nakwambia Nanaa anaumwa, ni mgonjwa, yupo na
hali mbaya sana, anakuhitaji!” “Ndivyo ambavyo ungedhania na
mimi ndivyo nilivyokuwa nikidhania hivyo tokea mwanzo. Lakini sivyo ilivyo na
yeye Nanaa aliliweka hilo wazi mbele ya familia yake. Hanihitaji mimi.
Mliopo hapo ndio watu amewachagua kwenye maisha yake, na ndio amekusudia
kuwaweka karibu. Naamini wewe ni mtu sahihi anayekuhitaji hata sasahivi na
utamsadia. Usiku mwema.” James akaaga na kumuacha Lubuva haamini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi
ndani. “Tafadhali niambie kinachoendelea kati ya James na Nanaa. Hakika
sijaelewa!” “Mimi si mtu sahihi wa kukueleza.
Tafadhali naomba rudisha mawazo kwa Nanaa, nimeacha watoto wangu wameingiwa
hofu, wanalia, hawajui nini kimempata mama yao. Kumtoa Nanaa kwenye ile hali
pale, nafikiri ndilo la msingi.” Ikawa wakati wa Nanaa kula na wakwao, janga
alilochuma. Kila mtu na wasiwasi. “Hawezi kutoka kwenye hiyo hali kama hujatibu
tatizo Geb! Inamaana hiyo hali itarudia tena, hata kama akitoka hapa kesho.”
“Sijui chakufanya Lubuva. Ila najua wewe una jinsi ya kumsaidia Nanaa.
Tafadhali msaidie hata kubadili dawa.” “Unakumbuka nilikwambia dawa anazotumia
ni za kiwango cha mwisho kwenye tatizo lake?” “Basi nipishe mimi niombe.”
Lubuva akatoka, Geb akapiga magoti. Akajaribu kuomba lakini hofu ikawa
imemkamata kwelikweli anashindwa hata kuomba.
Akufaaye Wakati Wa Dhiki,…
Akampigia
simu Joshua. Joshua akapokea kwa haraka maana ilikuwa usiku, si kawaida yao
kupigiana usiku mwingi hivyo. “Kwema kaka!?” Joshua akauliza akisikika
kujali, akiwa kitandani na mkewe. “Nahitaji
unibebe mimi na Nanaa kwenye maombi. Nashindwa kabisa kuomba. Nahisi nimeingiwa
hofu.” “Upo wapi?” “Hospitalini. Mke wangu amelazwa. Alianguka, pressure ipo
juu sana. Mbaya zaidi alianguka mbele ya watoto, alipoteza fahamu kabisa. Kila
nikiomba nasikia vilio vya wanangu, nashindwa kutulia mbele za Mungu. Nisaidie.”
“Nakuja.” Akamuelekeza walipo. “On my way, lakini pia
naanza maombi.” “Asante.” Geb akakata simu nakubaki amepiga magoti hapo pembeni ya kitanda
cha mke wake, kichwa ameegemeza kitandani. Ametulia tu, picha ya wanae wakilia
kwa sauti wakiita ‘mama’ ikaendelea kumtesa. “Mungu
nisaidie, nimekwama.” Hilo ndilo aliloweza kuongea mbele ya Mungu wake, akabaki amepiga
magoti pale mpaka Joshua alipokuja.
Na yeye
akaenda kupiga magoti hapo pembeni yake. Akaanza kuomba bila salamu wala
kumuongelesha Geb. “Najua hata sasa unatusikia Mungu wetu
na Baba yetu.” Ikawa kama mafuta ya petrol kwenye moto. Geb akapata nguvu ya
ajabu. Wanaume hao wawili wakaanza kuomba hapo pembeni ya kitanda alichokuwa amelazwa
Nanaa mpaka Lubuva akaingia na kutoka, wao wanaomba tu. Geb ndio alikuwa
ameinama kabisa mpaka sakafuni kana kwamba yupo kwenye sakafu ya nyumbani kwake
kumbe ni hospitalini. Walinena wakiomba hapo mpaka wakasikia sauti ya
Nanaa akimuita Geb.
Geb akainua kichwa
kwa haraka na kumsogelea akiwa amepiga magoti. “Nimekosa
Geb.” Geb akamshika mkono. “Mimi najua
Nanaa. Najua. Tafadhali anza kwa kujisamehe ili utoke hapo.” “Nimekosa Geb. Nimekosa sana.” Joshua akasimama na kwenda kukaa pembeni kabisa akiomba
taratibu kama kuwapa nafasi. “Naelewa, ila sasahivi huna utakaloweza kubadili
ila kuharibu zaidi. Tafadhali tulia mke wangu ili uje kurekebisha baadaye. Kama
nilivyokwambia, sasahivi James amesimama sehemu ambayo hataki chochote kitokee kitakachomfanya
Jema akabadili mawazo na kushindwa kumuoa. Mpe muda mpaka wamalize mambo
yao yote. Baada ya hapo, Mungu ni mwenye rehema. Atakurehemu tu.” Nanaa
akaendelea kulia.
“Watoto
wanalia nyumbani, wameona jinsi ulivyoanguka. Hali yako inatuathiri sisi wote. Naomba tulia, nakuhakikishia unayo
nafasi kubwa sana ya kuja kurekebisha baadaye. Hawana dawa nyingine ya kukupa.
Ikishindikana hapa ndio basi. Naomba upone Nanaa.” Geb akaanza kulia hapo kama
mtoto mdogo hapo, Joshua akaenda kumtoa hapo akaenda kumkalisha kwenye kochi,
yeye akavuta kiti na kukaa pembeni ya Nanaa.
“Naomba
na mimi unisikilize Nanaa. Sijui kwa undani nini kilitokea, lakini…” “Nimeharibu
vibaya sana Joshua. Sijui chakufanya tena. Nimeharibu mno.” Nanaa
akaongea akisikika amejawa hofu ya ajabu sana. “Basi hapo akili yako inapogota,
ndipo uwezo wa Mungu unapoanzia. Huwa nampenda Mungu, na ndio maana mimi huwa
wakati wote namuita Mungu wa impossibilities. Wa magumu, mazito
yasiyowezekana kwa akili za kibinadamu. Yeye hajawahi kushindwa. Unakumbuka
hata kwenye bibilia Mathayo19:26 Yesu alithibitisha hili?”
“Huyu
Mungu ambaye watu wanayemsoma kwenye bibilia akitenda mambo mazito na magumu,
Nanaa, mimi nimemthibitisha kwa macho haya ya nyama. Yapo unayoyajua na wewe,
ambayo alinitendea na mimi, kama kunirudishia Naya wangu, lakini kwa hakika,
nilishafika hapo ulipo. Akili ilishindwa kujua ninatokaje, kama vile Mfalme
Daudi, na mimi nikasema, ‘Nitainua macho yangu, niitazame milima. Nikajisalimisha kwa Mungu,
nikasema, msaada wangu utatoka kwa Bwana, Muumba wa mbingu na dunia. Hatauacha
mguu wako uteleze Nanaa. Yeye akulindaye hatasinzia, kwa hakika,
yeye akulindaye hatasinzia wala hatalala usingizi.’ Mstari
wa 5 unasema, ‘Bwana anakulinda, Bwana ni uvuli wako Nanaa. Mkono wako wa kuume,
jua halitakudhuru mchana, wala mwezi wakati wa usiku.’ Mstari
wa 7 unakuhakikishia unasema, ‘Bwana atakukinga na madhara YOTE,’ na
ameahidi kwenye mwisho wa huu mstari wa 7, kuwa, ‘Atayalinda maisha yako.’ Mstari
wa mwisho wa 8, kwenye hii Zaburi ya 121, unasema hivi, ‘Bwana
atakulinda wewe Nanaa, unapoingia na unapotoka.’ Halafu si mara moja.
Anamalizia kusema, ‘tangu sasa na hata milele.’ Sijui kama unanisikia?”
Joshua mwenyewe akahamasika.
“Nimekosa
Joshua. Nimemkosea sana kaka. Hata simstahili huyu Mungu.” “Si kwa
Mungu ambaye ni Baba yetu, Nanaa. Yaani huyu Mungu mwenye enzi yooote,
anakuahidi wewe Nanaa, kuwa si kwamba ulinzi wake ni pale ukiwa sawa naye! Yaani
umepatia sana. Hapana. Yaani jicho lake hata sasa linakutizama hapa ulipo.
Anasema, ‘hata milele.’ Huyu Mungu mtakatifu ametoa mwaliko mwingine mzuri sana
kwa sisi wakosaji, anasema hivi kwenye ‘Isaya 1:18 Njoo basi
tuhojiane’. Mungu anakuita wewe Nanaa sio ukiwa unajiona ni mtakatifu.
Hapana. Anakualika kwake vile ulivyo tena akiwa anakutia moyo akijua umekosa
haswa. Anakwambia hivi, ‘Ingawa dhambi zako wewe Nanaa ni nyekundu’, mbaya,
inatisha kwa namna ya kibinadamu. Anakuita na ahadi ambayo hakuna mwanadamu
anaweza kukupa Nanaa ila huyu Mungu wa rehema, anasema hivi, ‘zitakuwa
nyeupe kama theluji. Ingawa ni NYEKUNDU SANA kama damu, zitakuwa nyeupe kama
SUFU.’ Joshua akacheka.
“Eti naye
Yesu, kwenye Mattayo 11:28 Anatualika, anasema, ‘Njooni kwangu, nyinyi nyote
msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.’ Come
on Nanaa! Unataka nini tena? Unataka kipi kingine kutoka kwa huyu Mungu?
Anachohitaji ni usemezane naye kama hivi ulivyoniambia mimi na Geb, kuwa
umekosa sana. Halafu unamkabidhi yeye ule uzito unaousikia moyoni
mwako, that’s it! Halafu anakuhakikishia pumziko! Tena kwa moyo huo wa majuto,
hakika jiachie kwa Mungu uone atakavyoligeuza hata hili linalokutisha jinsi
litakavyofanyika kuwa jema kwako na kwa James mwenyewe. Ataigeuza hii habari
kwa namna ya ajabu sana. Sijui atafanyaje, lakini kwa kuwa YEYE ndiye amesema,
hakika ATAFANYA tu. Nakupa muda uitike wito wake. Mwambie Mungu vile
ulivyotuambia sisi, kisha mwache akusafishe na dhamira yako pia. Utashangaa
sana.” Mpaka hapo neno likafanyika hai ndani ya Nanaa, akaanza kujisikia
kuomba.
“Mimi na
Geb tutakusindikiza patakatifu pa patakatifu, kuomba rehema mbele za kiti cha
rehema. Tutakushika tu mkono tuingie wote, kisha mwachie Mungu uone. You
will never go wrong patakatifu kwa Bwana.” Geb akasimama na yeye
akaenda kumshika mkono upande mwingine. Wakaanza kuomba naye taratibu. Nanaa
akatubu akilia na wenyewe wakiomba vile anavyoomba mpaka akamaliza. Joshua
akambusu shavuni. Akacheka. “Vipi?” “Nashukuru Joshua, nasikia kifua chepesi.”
“That’s what am talking about.” Akaongea kwa furaha sana Joshua.
“Unawajibu mwingine Nanaa, Yesu alimwambia yule kiwete, ‘Inua
godoro lako uende.’ Hapo ulipolala si sehemu sahihi ndio maana wanao na mumeo wanalia
usiku huu. Kataa hayo maradhi yanayosababisha uwepo hapa. Jiambie na ukatae
hiyo hali. Nakutamkia uzima, urudi kulea watoto na mumeo.” “Amina. Na asante
Joshua.” Akamwangalia Geb.
“Asante
sana.” “Anytime Man. Anytime.” Wakacheka. “Acha mimi niwaache naamini
usiku wa leo na nyinyi mtaumalizia nyumbani.” “Naamini hivyo.” “Naomba
kukusikia Nanaa.” “Nimepona dhamira. Ile hali ya mzigo ndani yangu imepungua
kabisa.” “Naomba iishe tafadhali.” “Basi nasema imeisha.” “That’s
what am talking about.” Akarudia Kumu usemi anaoupenda sana akimpongeza. Wakacheka.
“Wewe Geb usinisindikize, ili upate muda wa kushukuru na mkeo. Tutazungumza
baadaye.” Joshua akatoka.
Kwa Mungu Wa Yasiyowezekana Kwa Wanadamu.
Na kweli
Nanaa akaruhusiwa usiku huo wa manane kurudi nyumbani kwa kuwa hakuwa akipewa
matibabu ya tofauti na akaonekana anaendelea vizuri. Akashauriwa akapumzike,
Geb akaondoka na mkewe. Walirudi nyumbani kila mtu amelala. Nanaa akaenda
kumuamsha mama G alikuwa amelala na wajukuu wote kitanda kimoja. “Wote walikuwa
wakilia ndio nikalala nao. Vipi?” “Najisikia vizuri mama.” “Utakufa Nanaa uache
watoto wewe! Fanya mchezo.” “Basi mama.” “Mimi nakwambia na naomba hiyo ‘basi’
umaanishe. Ushakubali kosa, kama mumeo alivyokwambia, muda utarekebisha. Tulia.
Utakufa uache wanao wanaharibikiwa. Ingekuwa wote tunashikilia makosa,
unafikiri hao kina Geb ungewakuta hivyo? Unajifunza kutokana na makosa
unaendelea na maisha. Jukumu lako la kwanza ni hawa watoto. Leo wanao wamelala
wakilia wakiona unatolewa hapa na watu wasiowajua, tena kwenye vitanda vya
wagonjwa, hujitambui! Acha Nanaa. Tulia mama. Mimi nakujua huna roho
mbaya, ni hasira tu. Hutatumia nguvu nyingi kurekebisha, lakini ukiwa hai sio
umekufa.” “Nimeelewa mama. Nimemuachia Mungu, naamini atanisaidia.” “Hayo ndio
maneno.” Geb akaanza kubeba watoto wake mmoja baada ya mwingine kupeleka
vyumbani mwao kulala mpaka akamaliza.
“Twende
tukaoge, ulale.” Geb akarudi kumchukua Nanaa aliyekuwa ameinama pembeni ya
kitanda cha mama G. “Mwili umeisha wote! Hapana Nanaa. Badilika bwana.” “Usiku
mwema mama. Kesho.” Akatoka na mumewe. Wakaoga na kupanda kitandani mumewe
akamvuta karibu na kumkumbatia ili alale. Lakini akamgeukia. “Samahani na pole
kukuogopesha Geb.” Kitu kilimpanda Geb, akaanza kulia. Alilia kama huyo Nanaa ndio
amekufa. Alilia sana na ndipo udhaifu wake kama mwanadamu ukaonekana wazi.
Hakuwa Geb milionea mwenye akili ya ajabu ambayo Mungu alimpendelea. Alilia
sana kwa kwikwi mpaka Nanaa akamuhurumia. Ni kama aliona uhai wa mkewe ukitoka
mbele ya macho yake na wanae kumlilia, akishindwa chakufanya. Akabaki kuwa
Mungu tu.
~~~~~Atafutaye, Hachoki~~~~~~
Huku kwa
Jelini Mama Jema akashangaa inakua mchana, inakua usiku, asubuhi Jelini amejaa
humo ndani hatoki halafu amepoa si kama kawaida yake ya kelele nyingi. Kukawa
kuna kukusanyika hapo kwao kila siku jioni wakija kumuona mama yao, bibi wa
wakina Jema. Basi ndugu hao vikao vyao ni vya pombe. Wanakunywa, wanacheka hapo
wakiongea hili na lile, usiku mwingi wanatawanyika kwenda kulala makwao lakini
si Jelini. Akahisi mwanaume aliyekuwa naye safari hiyo amemtenda. Hakuwa
akizungumza mambo yake hapo ndani, kwa hiyo wakati wote walijua anakuwa kwa
wanaume.
Siku ya
tatu akiwa kazini Doro akapata ujumbe kutoka kwa Kasa wenye alama ya viulizo
viwili. ‘??’. Akaelewa anachomaanisha. ‘Leo nimepanga niwahi kutoka
kazini nimfuate kwao maana hata baa jana hakuja.’ Akarudisha hayo majibu.
Kimya. Asijue swala la kutotokea kwa Jelini baa kwa hizo siku zote Kasa
alishalijua ndio maana alikuwa akiulizia mpango wao wa pili.
Doro
akawahi mapema sana ili kwenda nyumbani kwa kina Jelini. Akamkuta anajiandaa
kutoka yeye na mama yake. “Karibu dada Doro!” Akamkaribisha kwa mshangao,
hakutegemea kumuona pale. “Kwanza umepafahamuje nyumbani kwetu!?” “Nimeulizia
vijana wa pale kijiweni wa bodaboda ndio wamenielekeza mpaka hapa.” “Kwema!?”
Ikabidi Jelini aulize. “Nimekumiss tu.” Jelini akabaki amemtolea macho mama
yake akisikiliza akiwa upande mwingine tu hapo ndani.
“Na
nimekuja kukuomba msamaha mdogo wangu. Nilikukosea. Nahisi nilikuwa na hasira
za kazini nikakumalizia wewe. Naomba usiondoke kwangu. Iwe kama zamani.” Mama
Jema akawa hajaelewa. “Nakumbuka jinsi ulivyoniuguza na kunisaidia wakati watu
wamenisusa. Ukasimama na mimi kama mtu wako ki ukweli. Nisamehe kwa maneno yote
yale.” “Lakini ulichozungumza dada Doro kilikuwa na ukweli. Inawezekana
ulizungumza kwa hasira lakini hata mimi nimejifikiria, nimeona upo sahihi.
Sijakukasirikia, ila tu nimeona nitulie nyumbani, nijifikirie maisha yangu.
Siwezi kubaki nikifurahia mafanikio yako tu wakati mimi sina kitu.” Mama
Jema akakaa kwa mshituko asiamini kama
anayezungumza hivyo ni Jelini.
“Kwa hiyo
uwe na amani tu. Mimi sijakasirika.” “Kwa hiyo tunaondoka wote?” “Nashukuru
dada yangu, lakini hapana. Acha nilale tu hapa kwetu tunakojipepea kwa
magazeti. Tutakuwa tukikutana baa, lakini narudi kulala kwetu.” Mama Jema
akashangaa sana. “Jelini naye! Ile ilikuwa hasira tu!” “Wala usijali. Mwenzio
sijakasirika.” “Twende basi kwa washikaji.” “Hivi hapa umetuwahi kidogo tu.
Tulikuwa tunatoka kwenda kwenye kikao cha kitchen party ya Jema. Na huko mama
mdogo kaniambia kuna bia za kufa mtu. Acha nikanywe bia za bure.” “Sio za bure.
Kuna aliyelipia. Na tuondoke sasahivi maana kikao hakianzi bila mimi.” Mama
Jema akadakia na kusimama. “Mama naye! Sasa si bure kwangu!” “Mbona sasa mimi
sikaribishwi?” “Wewe wala usilalamike. Kama unataka, twende. Huko ni michango
tu.” Ikawa msaada kwao. Wakatumia gari ya Doro kwenda kikaoni.
“Jumamosi
kesho naandaa chakula cha jioni kwa marafiki zangu wa karibu. Utakuja
nyumbani?” “Hapa tunapeleka mambo mengi kwa wakati mmoja. Leo kikao cha Kitchen
Party, kesho siku yake yakulipiwa mahari.” “Jumapili je?” “Tuna kikao kingine
tena cha send off. Nitakuwa na mama kwenye kikao na uchovu wa kesho nitataka
kurudi nyumbani nipumzike.” “Jumamosi ijayo je?” Doro akaendelea kubembeleza.
“Ni kikao cha mwisho cha send off na kitchen party, ndio shuguli zinaanza.
Kitchen party jumatano, send off ijumaa, kisha harusi jumamosi.” “Baada ya
kikao jumamosi si unaweza kuja?” “Itakuwa usiku na mimi nataka kila usiku niwe
kwa mama Jema.” Jelini akaendelea kuweka ngumu. “Sasa hapo Kunduchi na hapa
kwenu kuna umbali gani na wewe Jelini? Nitakurudisha.” “Ukiahidi hivyo sawa.”
Mama Jema kimya akisikiliza na kujaribu kuelewa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kikao
kikawa kimechangamka kwelikweli. Vikajaa vicheko hapo na mipango mizito. Doro
na yeye akatoa mchango wake hapohapo na kuchukua mtandio wake ambao ni sare ya
kuvaa kwenye kitchen party. Wakiwa wamekubaliana rangi ya kuvaa siku hiyo ni
nyeupe na huo mtandio wa gold mzuri sana. Jelini akawa na kazi ya
kunywa. Hakuwa amekunywa bia zaidi ya siku tatu ambazo kwake ni nyingi mno.
“Nashauri umrudishe nyumbani mama. Inatosha.” “Jema naye! Kwani mimi nimelewa? Nimekunywa
kidogo tu!” Jema akamtizama na kurudisha macho kwa mama yake. “Tupe lifti
basi.” “Sasa bibi harusi ndio anaondoka tena!? Mama Jema chukua usafiri hapo
nje bwana ili tubaki na Jema bibi harusi wetu tupige stori” “Mimi nitawarudisha
nyumbani.” Akajitolea Doro. “Si kikao kimeisha?” Jema akauliza. “Ndiyo. Lakini
situkae wote ili tupige stori?” “Wewe mamdogo umelewa na kusahau mwenzio mimi bibi
harusi. Kesho alfajiri na mapema, natakiwa saluni na mama ananitaka saa sita
mchana niwe nimefika kwake. Halafu kuna kitu nataka kuzungumza na mama. Acha
mimi mwenyewe niwashushe kwao nikiwa na kwenda kwangu huku tukizungumza.”
Jema
akasimama na pochi yake. “Haya, Jelini, inua majeshi.” “Usiku mchanga kabisa
huu, lakini naambiwa nikalale kama Jeremy! Jeremy analala saa mbili eti na mimi
nalala muda huohuo! Nakuwa kama mtoto mdogo, wakati ningebaki hapa na kina mama
mkubwa! Si mamdogo atanirudisha!” “Naomba malalamiko yako ukayamalizie ndani ya
gari Jelini. Unanichelewesha.” Jema akamuwekea msisitizo. “Mimi wala sifurahii
kuondoka sasahivi.” Wakamsikia akiendelea kulalamika huku anakwenda kwenye gari
akawaacha wanacheka.
“Mwenyewe
si mbishi kwa..” “Jema tu.” Mama yake akamalizia. “Napo anavitu vyake ambavyo
anakubali kushauriwa na vingine hataki.” Jema akaongeza. “Kama kazi?” Mama yao
mkubwa akauliza, wakacheka. “Hapendi kazi kama kifo!” “Sasa na wewe Jema ndio
tuondoke kabla hajarudi tena.” Wakaaga. “Au abaki mimi nitamrudisha.” Doro
akamtibua mama Jema. “Hivi wewe, mbona umemkazania Jelini hivyo!?” “Ni shoga yangu
na nikutaka kampani tu!” “Kwa nini hutafuti watu wazima wenzio umemkazania
mwanangu na ashakwambia anataka akalale kwao!? Huwa unamuuza?” Mama Jema akawa
mkali kwelikweli mpaka akafanya wengine wawageuzie wao macho na masikio.
“Maana
umemkazania tokea nyumbani nakusikiliza tu. Na yeye amekuwa muungwana kweli
akikwambia kwa yote uliyomtendea amesamehe, ila anataka kuwa kwao. Bado
umemkazania mwanangu! Hivi wewe unajua umri wake yule au unadanganywa na lile
tako na hips?” Jema kimya maana alimjua mama yake akipandisha hasira, matusi
yanatoka kama mvua.
“Umekula
pesa ya watu nini ndio unahaha kutaka ukamuuze mwanangu?” “Hapana mama yangu…”
“Koma. Mimi sio mama yako. Na koma kumpeleka mwanangu huko unakokazania. Kakunwe
wewe, mwache mwanangu. Twende Jema.” Mama zake Jema waliobaki hapo wakinywa
wakaanza kucheka maana walimjua mama Jema. “Na bora hukuendelea kumjibu yule.
Angekuvua nguo hapa kwa matusi.” Wakazidi kucheka na kubadili stori kama hakuna
kilichotokea.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walipoingia
tu kwenye gari Jelini akalalamika mpaka akalala. “Kwani ni nini mama?” Akamsimulia
Jema kuanzia mwanzo Doro anafika kwao mpaka mwisho. “Inamaana ndiko anakolalaga
huko huyu Jelini?” “Sasa sijui kama ni siku zote anakuaga huko au kuna
anakokwendaga! Ila leo kwa mara ya kwanza nimeanza kujilaumu kutomfuatilia kwa
karibu! Ni kama nilimkatia tamaa mapema!” Jema akanyamaza akitafakari
nakushindwa kujua azungumze nini, akihofia kumfikiria tofauti na kuja kujilaumu
baadaye. Wakanyamaza mpaka nyumbani.
“Ulitaka
kuzungumza nini na mimi?” “Wala sina cha kukwambia mama yangu. Nilitaka tu
kutoka pale. Nilishachoka kelele.” Mama Jema akacheka. “Jema na kelele! Sasa
utafanyaje ukipata wakwe wenye fujo?” “Nimegundua wanamuogopa sana James. Mno.
Na wanasema huwa hawaendi kwake.” “Basi umepona.” “Sana. Tena ndio ushuke
nianze kuzungumza na mpenzi wangu.” Mama Jema akacheka.
“Jelini!
We Jelini?” Akamuamsha mdogo wake. “Nimechoka!” “Nenda kalale ndani. Mmefika.” Akaangalia
nje. “Mama yuko wapi?” “Twende, na mwenzio aende kwake akampumzike.” “Asante
Jema. Ila sina hela na ninashida sana.” “Umeanza!” “Sasa mimi nitaishije
jamani!?” “Yaani wewe ukiwa hata usingizini unawaza hela tu! Nipigie kesho mapema
kabla sijaenda saluni.” “Mimi ndio maana nakupenda Jema.” “Shuka bwana acha kunidanganya.”
Mama Jema akacheka na kushuka garini. “Tatizo lake Jema haniamini!” Akafunga
mlango na kuingia ndani na mama yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bado Doro ambaye ameshakula pesa ya Kasa anatakiwa kufanikisha
miahadi ya kumfikisha Jelini kwa Kasa huku mama yake akianza kuweka ngumu, na
Jelini kuwa na msimamo kwenye maamuzi yake. Ni nini kitaendelea?
Maandalizi ya siku ya mahari
yanaendelea. Bado Nanaa nje ya tukio.
Baada ya yote, je, Geb atafanyaje? Uwenyekiti wa harusi ya James,
rafiki wa tokea vijana wadogo kabisa, akaja kuwa shemeji-baba mkwe, bado
atataka?
Grace anakuja jijini kukutana na Danny, akiwa mke wa Man.
Nini kitaendelea siku ya mahari?
Kasa atafanikiwa kwa Jelini?
0 Comments:
Post a Comment