“Basi
niombe namba yako, nikuandalie mazingira mazuri, umfikishe hapo. Nyinyi mkifika
muagize chochote mnachotaka, nitalipia. Mengine niachie mimi.” “Kwanini unajihangaisha
na Jelini kaka yangu!? Yule mtoto pasua kichwa.” “Samahani Doro. Mimi ni mkweli
na muwazi. Na pia si mkurupukaji. Huwa napanga mambo yangu. Tafadhali liheshimu
hilo.” Hapo Doro akatishika na kunyamaza.
“Namba?” Kasa
akauliza kwa amri kidogo. Akamtajia. Akamuona anafanya kitu kwenye simu yake.
Baada ya muda mfupi sana ikathibitishwa. Kuangalia ni pesa ndefu mpaka
Doro akamtizama usoni. “Naomba umtumie pesa sasahivi ikiwa bado mapema kwa
ajili ya kununua nguo yake yakuvaa jioni na kama angependa kwenda saluni, ili
asijisikie yupo out of place akifika hapo hotelini.” Hicho nacho
kikamuuma Doro. Yaani ampe na Jelini ile pesa! Alishafurahia kuwa pesa yote ni
yake. “Mchana mwema.” Kasa akatoka kwa kiburi. Kwanza alinukia mafanikio. Msafi
wa kung’aza weusi wake. Juu mpaka chini kiatu safi. Doro akashangaa sana mtu
kama huyo amekutana wapi na mtu kama Jelini! Kikabaki kikimuuma na kumshangaza
akitamani ingekua yeye.
Jelini
hakusoma. Si mstaarabu, mtoto wa mtaani kabisa. Na ni kama yeye ndiye anayemtunza.
Akichoka nguo au akitaka kubadili kabati, basi Jelini alijipatia nguo za maana
tu kutoka kwake maana ni kweli Doro alikuwa akijua kujipangilia, na hakupenda
kurudia nguo mara kwa mara. Leo Kasa anaonyesha msimamo kwake na kuomba heshima
kwenye maamuzi yake. Akapoa.
Tamaa Ikichukua Mimba, Huzaa Dhambi, Na Dhambi Ikisha Kukomaa, Huzaa Mauti.
Akampigia
akiwa na jazba, wivu unamfanya anashindwa kuhema kwa rafiki yake kipenzi
waliyekuwa wameshibana na kubebana kwenye mengi. Jelini alikuwa amelala kitandani
kwa Doro, hana habari. Akaamka na kupokea simu. “Yaani wewe unalala mpaka
sasa hivi!? Wewe utakuwa mtu wa namna gani?” Kidogo Jelini akashangaa. “Kwema dada?
Mbona kama unawaka asubuhi na mapema?” “Kwanza si asubuhi na mapema.
Watu na akili zao sasa hivi wapo kutafuta maisha. Wewe unalala hapo ukipulizwa
na baridi safi kwa sababu mimi naamka asubuhi na mapema kuhangaika kutafuta
pesa. Ingekuwa watu wote tunalala hivyo si wote tungegeuka mafala kama wewe.”
“Hee! Yamekua hayo?” Jelini akashangaa sana. Kwanza
hakutegemea!
“Mimi
nakwambia ukweli.” “Yameanza lini yakuambiana ukweli kwa namna hiyo!?” “Tazizo
lako wewe ni mbishi, na huambiliki. Nakutunza kwangu na kukulisha. Hata pombe
pia ukiishiwa mimi ndio nakunywesha lakini unakuwa na kiburi kwangu?” Jelini
akanyamaza kimya akimsikiliza asimuelewe na kuamini kama yote hayo anayaongea
yeye tena kwake! Hakutaka kumjibu kabisa. Akanyamaza akimsikiliza anavyomtapikia.
Doro mtu
wake sana na hata akiwa na matatizo Jelini ndio faraja na msaada wake. Leo
anamuwakia wakiwa wametoka kunywa naye, na anamjua Jelini vizuri tu. Mvivu na
kazi yake kula, kunywa na kulala. Urembo ndio fani yake. Avae apendeze, basi.
Akaongea mengi akimkumbusha hili na lile, Jelini akimsikiliza mpaka akamkatia
simu. Usingizi wote ukamuisha. “Akufukuzae hakwambii toka. Naona hapa
tushafika mwisho, nihamishe kikao kwa mama Jema.” Akatoka kitandani na
kwenda kuoga. Akajiandaa na kuchukua vitu vyake vyote ambavyo alikuwa akiacha
hapo. Hakuacha hata mswaki. Akatoka kurudi kwao.
Nyumbani ni Nyumbani.
Hakumkuta mama yake
wala mwanae Jeremy. Akajua mama yake yupo kwenye shuguli zake, mwanae shule. Akashukuru
hatapata maswali mengi na mizigo aliyorudi nayo. Akapanga vitu kwa haraka, wakati
anamalizi mama yake akawa anaingia. “Bibi yako anaingia leo.” “Best yangu yule,
hana neno. Nalala naye.” “Hapana Jelini. Analala na Jema. Jema amesema
anakwenda kumpokea na kumleta hapa. Atalala naye. Labda kesho.” “Na mimi nalala
naye leo.” “Unataka fujo zisizo na sababu. Na unamjua bibi yako.” Akaanza kucheka.
Ila akashangaa ni kama hana hata mpango wa kutoka siku hiyo.
Akamuacha tu mpaka
jioni Jema na bibi yake wanaingia hapo na mama zake wadogo na wakubwa nao
wakafika hapo kumsalimia mama yao, Jelini hakutoka. Stori zikaanza wakicheka
kwa hiki na kile, Jelini yupo hata pombe alizoagiza mama yake mkubwa hakunywa,
mama yake akawa akinywa akimwangalia tu bila kumsemesha. Maneno mengi
hayamuishi. Mida ya saa moja James naye akawa amewasili nje. Wakamuona Jema
anakimbilia nje. “Bwana mwanaume anampenda Jema huyo!” Akaongea Jelini. “Hasikii
raha bila kuwa naye. Kamfuata mpaka huku, ilimradi tu awe naye! Na mimi
natafuta wangu.” Mpaka bibi yake akaguna. “Ujue bibi mimi sikuelewi!” Vikaanza
vicheko kila mtu akiongea lake juu ya Jelini.
James akaingia na kumsalimia bibi kichaga.
Bibi alifurahi sana. “Sasa huyu ndiye mwanaume. Hata katikati ya watu tunaongea
yetu.” Akafurahi bibi kila mtu akamuona na lugha akabadili. Uzuri James
anaongea lugha ya kwao vizuri tu. Kikaendelezwa kilugha hapo wakicheka sana. Wakala
pamoja, wakimuangalia jinsi Jema anavyomuhudumia James hapo mpaka akaaga,
wakahamia nje kwenye gari ya James. Walikaa hapo mpaka Jeremy akatoka kumwambia
bibi anakwenda kulala, ndipo James akaondoka, Jema akarudi kwa bibi yake baada
ya kupata busu la usiku mwema.
Kulikoungua Mpini.
Huku kwa
Doro hana habari, alishajiaminisha kwake ni mtakuja kwa Jelini. Jioni baada ya
kazi akiwa anaegesha gari nje ya nyumbani kwake, ujumbe ukaingia. ‘Tafadhali
iwe mapema kidogo kwa kuwa kesho ni siku ya kazi.’
Akamtajia hotel ambayo anataka ampeleke Jelini na kuongeza ujumbe mwingine. ‘Unaweza
kumwambia leo unamtoa kwa chakula kizuri cha usiku ili asishituke mazingira.’ Doro
akasoma na kucheka kwa kushangaa. “Yaani huyu ametuona sisi maeneo kama
haya hatufiki au?” Na yeye akamjibu akiwa ameshamuelewa amewadharau. ‘Na hivi ni
viwanja vyetu sana tu.’ Akamrudishia ujumbe Kasa, lakini hakumjibu tena ila pesa ingine
ikaingia. Asijue mpaka hapo Kasa anamfahamu ndani na nje.
Akashuka
garini na kuingia ndani kwa kiburi akijua Jelini mwenye shida yupo ndani
akimsubiria watoke. Alishamzoea Jelini si muweka kinyongo, kwa hiyo akajua hata
kama asubuhi alikasirika, basi atakua alishapoa, asijue Jelini yupo kwao na
mama zake akimchokoza bibi yao. Hakumkuta sebuleni akiangalia movie kama
kawaida yake. Akajua cha uvivu huyo bado yupo ndani ya mashuka, rimoti mkononi.
Lakini hakuwepo hata chumbani kwake kwani Doro asipoleta mwanaume hapo ndani
basi analala na Jelini. Akiwa na mwanaume, Jelini anarudi kwao.
Kidogo
akashangaa. Akampigia simu akakuta simu haipo hewani. Kuangalia vizuri,
alichukua vitu vyake vyote, hana alichobakiza kwake. Akaingiwa hofu kwa kuwa
pesa ya Kasa amepokea, na anawasubiri hotelini. Akafikiria kwa haraka. Na kwa
kuwa na yeye ni mzuri, tena mzuri haswa, akaanza kujitayarisha yeye mwenyewe
kwa haraka ili asimchelewe Kasa.
Kwa
hakika Doro alipendeza na akajipangilia haswa kwa kiwango cha aina ya hoteli
wanayoenda kukutana na Kasa. Doro mrembo, amesoma na ana exposure.
Anayajua ya uswahilini kula nyama choma baa kwa mkono, na ya uzunguni ya kula
kwa kisu na uma pia anayajulia. Safari za nje ya nchi kikazi zilimfundisha
mengi na kumsafisha fikra zaidi. Kwa hiyo hana shida akikaa katikati ya wenye
nazo na wasio navyo pia.
Kisicho Riziki, Hakiliki.
Akatoka
mapema tu mpaka kwenye hiyo hoteli. Akaingia na kuangaza macho akijua lazima
Kasa angekuwepo huko. Na kweli akamuona kirahisi japo ni kama alijificha ili
kama wanaingi Jelini na Doro, basi Jelini asimuone kwa haraka mpaka baadaye.
Kasa alikuwa akisoma gazeti wakati Doro akimsogelea, akalikunja na kuliweka
pembeni. “Jelini yupo wapi?” Ndio likawa swali la kwanza hata kabla ya salamu.”
Doro akacheka kwa pozi akijua na yeye amependeza, maana ukweli Kasa alijua
kujipangilia. Hapo alipokaa tu, alionekana yupo vizuri.
Doro
akavuta kiti na kukaa mbele yake. “Hamna salamu wala karibu?” “Wewe
tulishaonana mchana. Tupo hapa kwa ajili ya Jelini.” “Jelini ni tapeli. Nimempa
ile hela akaniambia anakwenda kununulia nguo, amepotea na simu amenizimia. Ila
nimeshamzoea. Ni kawaida yake. Akiona pesa anakua kama mwehu! Anatabia ya
udokozi pia.” Kasa akabaki akimsikiliza. “Sasa ujue hivyo alivyoipata hiyo pesa
ya pombe, hutampata tena. Atainywea pombe yote mpaka aishiwe kabisa ndipo
atarudi.” Kasa akatoa simu bila ya kumjibu. Akamuona anaandika ujumbe. Zilo
akapokea ujumbe kutoka kwa Kasa. ‘Nataka kujua kama Jelini
yupo kwenye ile baa uliyoniambia anapenda kuwa hapo akinywa.’ ‘Sekunde Mkuu.’ Kisha
akamuona anairudisha simu mfukoni na kurudisha macho kwake.
“Na wewe
sio mwanaume wa kwanza kutapeliwa na Jelini. Yule mtoto anaishi mjini kwa
utapeli.” Akaongea mengi akimchafua Jelini mpaka akajisahau yupo mazingira ya
uzunguni, analeta uswahili. Kasa kimya akimsikiliza. “Analiza wanaume mjini.”
Akasikia ujumbe umeingia kwenye simu ya Kasa. “Samahani.” Akajua ndio anaambiwa
anyamaze asome ujumbe. ‘Inavyoonekana leo hajafika hapa kabisa hata kwa supu ya asubuhi
ambayo anapata kwenye mida ya saa tano. Nimeulizia mida yake ya jioni,
inavyosemekanika mara nyingi huwa anawahi kidogo jioni kama hatakaa kuanzia
hiyo asubuhi akija kunywa supu. Au kama nikuchelewa, basi ujue atafika na Doro.
Sasa na Doro naye leo hajaonekanika. Haijulikani tena watakuwa wamehamishia
wapi kijiwe kwa leo, maana kila siku lazima wawepo hapa.’ Kasa
akasoma na kuhisi kuna kitu hakipo sawa.
“Mbali na
hapa, maeneo gani mengine huwa unapenda kuwepo?” Kasa akamuuliza kwa haraka
akijua maeneo yake ni ya Jelini. Akajikanya akiwa amefurahi akijua anajaliwa.
Akataja kwingi lakini akagundua alichoongea Zilo ni sahihi. Wanaipenda hiyo baa
na ndiko wanapokuwa muda wote. “Kwa sasa Jelini yupo kwenye mahusiano yeyote?”
Swali jingine ambalo kidogo lilimuuma Doro kwani ni kama walitoka kwa Jelini,
anamrudisha vipi tena kwake!
“Kwani ni
mmoja! Jelini haridhishwi na mwanaume mmoja mpaka utashangaa anataka nini
kwenye maisha. Malaya yule asiyetosheka na moja wala mmoja.” “Kwa hiyo kama
nimekusikiliza sawasawa na kukuelewa ni kama kwa sasa hana mtu.” Kasa akataka
kufupisha. “Hana mtu mmoja.” Doro akamuweka sawa Kasa. “Wapo wengi ndio maana
na wewe nakuokoa.” Akaongea mengi akimsikiliza huku akiokota anayotaka juu ya
Jelini. Akamuona Kasa anaangalia saa yake ya mkononi. Akapoa kidogo. “Nikikaa
kama hivi na Jelini, na yeye unahisi atazungumza nini juu yako?” Hilo swali
likamfanya Doro kupoa kabisa. Kasa akasimama. “Uwe na jioni njema.” Akaondoka
na kumuacha Doro na mshangao kama aliyempiga kibao cha uso.
Doro
akatumia akili ya haraka na yeye akatoka na kumkimbilia Kasa. “Nisikilize
tafadhali usiondoke.” Kasa akasimama, mikono mfukoni. “Jelini si mtu wa kuweka
kisasi. Mimi naweza kukusaidia kumpata.” “Nakusikiliza.” “Pafahamu kwangu. Mimi
nitamuita kwangu. Nitamuomba msamaha. Nitamwambia naalika wageni kwa chakula
cha jioni anisaidie kuandaa na kuwakaribisha. Na wewe utakuwa mmoja ya hao
wageni. Ukija utakutana naye.” Akawa amejichanganya,
hata Kasa hakuwa akijua kama wamegombana, ila akaona aangalie yake. “Lini?”
“Acha niweke mazingira mazuri. Tutawasiliana. Lakini kwanza twende ukapaone
kwangu ili siku nikikukaribisha iwe rahisi.” Kasa akakubalina na hilo wazo.
Wakaongozana mpaka kwake.
Doro
alimkaribisha ndani kwa upendo ili angalau amtege wakiwa ndani, lakini Kasa
akaingia bila kukaa. Katikati ya sebule, amesimama, mikono mfukoni. “Ni kama
kwa maelezo yako, kwa sasa Jelini hana mtu. Nipe jibu la ndiyo au hapana
bila maelezo mengi.” “Hapana. Lakini..” “Tafadhali usichukue muda mrefu
kutekeleza ahadi yako. Ningependa iwe ndani ya hili juma.” Alimkatiza, akaongea
hivyo na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kazi
ikawa jinsi ya kumpata Jelini. Mpaka anaingia kitandani akawa hajampaka kwa
simu na kesho yake ilikuwa siku ya kazi. Alilala akiwa ameumia. Kasa
alimuumiza, akaona ni kama amemdharau yeye. Ameweka uthamani kwa mtu kama
Jelini na si yeye! Lakini akakusudia kuwazidi wote mahesabu. Kasa na Jelini. Na
yeye akaanza kujipanga kivyake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Itaendelea.
0 Comments:
Post a Comment